Kwa mwendo huu tutaushinda utandawazi?

Na Boniphace Makene

MIEZI mitatu iliyopita kulikuwa na mjadala mkubwa kupitia vyombo vya habari hapa nchini. Ni wazi kila Mtanzania aufahamuye umuhimu wa elimu aliupatia nafasi mjadala huu kwa kuuchangia kupitia vyombo vya habari ama kuusikiliza tu.

Mjadala huu ambao kiundani unatokana na kuboronga kwa baadhi ya wafanyakazi wa Wizara ya Sayansi Teknolojia na Elimu ya juu uliosababisha idadi ya wanafunzi 603 waliokuwa wamechaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu katika Mwaka wa Masomo 2002/2003 kukosa udhamini wa Serikali. Naita kuboronga kwa Wizara kwani iweje wafute udhamini na baadaye upatikane?

Hadi sasa sifahamu nini hasa kilichowapa udhamini, lakini hiyo ndiyo hali halisi ya Serikali yetu ambayo viongozi wake mara zote wamekuwa wakitoa kipaumbele katika kupitisha mawazo yao huku wakisingizia kuwa ni ya wananchi. Wananchi wamekuwa siku zote kama kivuli cha kuwakinga viongozi kupitisha kile wakitakacho.

Suala hili la wanafunzi 603 halikuanza kama mzaha, lilichukua muda mrefu kujadilika, lakini kama ilivyo kawaida ya wakubwa wetu, mawazo yao ya mwisho yakawa yamepata uthamanisho.

Ni katika uthamanisho huu ambapo Watanzania 603 walijikuta hawana udhamini hadi walipoanza harakati zao binafasi wakihusisha asasi zingine na hatimaye Serikali ikakubali kulegeza msimamo wake.

Sijui hata sasa kuwa Serikali ilipata wapi hizo pesa za kuwasomesha hawa baada ya kuwa suala hilo limezua mjadala na sishawishiki kuamini kama kweli Serikali haikufanya danganya toto. Maelezo kuwa Serikali imekopa toka kwa wafadhili siyaoni kama yana mantiki hapa!

Nasema hivyo licha ya kuwa sitaki kuzikumbusha Wizara na Serikali kwa jumla kukumbuka kuwashirikisha wadau kabla ya kupitisha maamuzi mazito kama hayo. Naamini sana kuwa ni njia hii tu, ambapo maendeleo ya kweli yamepatikana na kila mmoja akabaki kijino nje akifurahia mchango wake katika kufanikisha maendeleo ya jamii yetu.

Wananchi wana haki ya kutoa mchango wao wa mawazo na lazima mchango huo usikilizwe na Serikali yao. Kama hilo halifanyiki, basi Serikali inafanya kazi zake kwa minajili ya watu wachache tu.

Katika suala hilo la udhamini wa wanafunzi, kulitokea hali ya wananchi wa chini kutoshirikishwa kabla ya maamuzi.

Ni wazi kuwa wanafunzi 603 waliumia sana na waliathirika hata kisaikolojia jambo ambalo lisingetokea kama kungekuwa na dhana shirikishi. Ndani ya dhana hii, wananchi wangesema hawana haja na ndege ya Rais ama Rada kwanza kabla ya vijana wao kupata urithi halali wa karne hii ya 21 yaani elimu.

Ni kweli hapa Serikali ilikuwa imeonesha mfano mbovu mithili ya mzazi asiye na hekima ambaye aombwapo chakula na mwanaye, yeye yuko radhi kumpa jiwe atafune. Vijana wetu kweli walikuwa wamepewa mawe watafune na ninaamini mwisho wake wasingekubali kuyatafuna mawe hayo, bali wangeyageuza zana ambazo zingekuwa hatari sana hususan katika kipindi hiki ambacho dunia inapambana dhidi ya ugaidi.

Serikali ilikuwa inapanda mbegu mbaya ya chuki ambayo ingewatafuna viongozi na wananchi kwa jumla; tena kwa kipindi kirefu. Ni wazi kuwa malipo ya mbegu hii yangekuwa na madhara makubwa katika siku za usoni.

Mjadala huu nimeutoa huku ili nifikie hapa katika eneo la Mlimani ambako kuna wasomi wetu tegemezi wa taifa. Katika Chuo Kikuu hiki na chenye hadhi kubwa kumejaa mambo mengi yanayonipa hamasa kuandika leo.

Ni wazi tulipambana wote kuhakikisha kuwa wanafunzi 603 wanapewa udhamini jambo hilo limeshafanyika na hakuna aliyeshinda.

Hapa si Serikali wala wananchi walioibuka kidedea baada ya mjadala huo kukamilika na hata pia wenyewe hao 603 nao hawawezi kutamba kuwa wameishinda Serikali kwani tayari walishaathirika kisaikolojia.

Kizuri ni kwamba Watanzania tumejaliwa hulka ya kusahau matukio ya nyuma jambo linalorahisiha kusameheana. Lakini, tabia hii imesababisha mara nyingi kurudiwa makosa ambayo yangeweza kuepukika kama kweli tungekuwa na tabia ya kuithamini historia ya matukio ndani ya nchi.

Kuna mifano mingi ambayo inathibitisha hoja hii ya Watanzania kusahau kila jambo linalopita.

Kauli za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere nyingi zimebakia nyimbo tu za kuimbwa katika redio na televisheni!

Hakuna tena anayetambua kuwa Mwalimu  aliwahi kutufundisha wanafunzi wake juu ya adha ya ukabila! Hakuna anayefahamu sasa madhara ya ubinafsishaji wa mashirika nyeti kama TANESCO na NBC na tena kumbukumbu hazitupi kabisa juu ya udini unaochukua taswira mpya kila kukicha.

Hapa ni wazi Mwalimu  hakuwa na wanafunzi...kama angekuwa nao basi wangeeneza taaluma yake aliyioiacha. Kamwe wasingekubali kuchana vitabu vyake kwa kusingizia kuwa ni vikuukuu. Dhamira ya usawa na umoja milele haina mwisho.

Tusingekubali kuona tena kivuko cha Kilombero kinatia watu simanzi mara baada ya janga kubwa la meli ya Mv Bukoba. Naamini hatukujifunza chochote kutokana na matukio kadhaa yaliyotokea na kwa mwendo huu safari yetu bado ni ndefu katika kukabiliana na utatuzi wa matatizo ya wananchi wetu.

Nirejee sasa ndani ya mada yangu ili niweze kudondoa namna Mlimani sehemu ya wasomi inavyochangia sasa kukosa wasomi wenye dira. Wasomi wenye uyakinifu wa hoja kutokana na mfumo mbovu wa kuwapika wasomi hao!

Idadi ya wanafunzi ndani ya chuo hicho imekuwa ikiongezeka sana kila mwaka na sasa kuna karibu wanachuo 10,000. Idadi hii ni ndogo kwani Tanzania ni ya mwisho Afrika mashariki ukilinganisha na Kenya na Uganda kwa kuwa na wasomi wengi wa chuo kikuu.

Ni jambo lililo wazi kuwa idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu Kenya na Uganda ni wengi kuliko wa hapa nchini kila mwaka. Mfano mzuri ni wanafunzi wanachukua shahada katika somo la Kiswahili ambalo mhimili wake mkubwa ni Tanzania kwa miaka miwili iliyopita ilikuwa ni katika ya 20 Tanzania kwa 150 Kenya.

Ni wazi idadi yetu ni ndogo hivyo inapaswa kuongezwa ili taifa liendane na utandawazi. Lakini ongezeko hili linapaswa kuangalia upande mwingine wa nyenzo za utoaji wa taaluma sambamba na ongezeko hilo.

Kuongezeka kwa wanafunzi 603 mwaka huu ni mafanikio makubwa kwani idadi hii inatupeleka katika ushindani. Wasiwasi wangu unabaki katika mfumo mzima wa kuwaandaa wanazuoni hawa ili wafanikiwe kupata elimu muafaka katika zama hizi za ushindani.

Niliwahi kufika Chuo Kikuu kishiriki Muhimbili ambapo nilizungumza na baadhi ya wanafunzi na mmoja wao akanieleza juu ya ukosefu wa vifaa katika maabara zao. Mwanafunzi huyo alinifafanulia kuwa hivi sasa darubini moja hutumiwa na wanafunzi si chini ya 10 kwa saa.

Uwiano huu unaonyesha kuwa mwanafunzi anaweza kutumia darubini katika dakika 10 pekee ili atoe mwanya kwa wengine nao kuangalia kazi walizopewa kuzitafiti. Inaumiza zaidi pale wanafunzi hao wanapokuwa katika mitihani kwani inabidi washikane mashati ili kila mmoja apate nafasi ya kuitumia darubini hiyo.

Huu ni ubabaishaji mkubwa kwani kama madaktari wetu wanaandaliwa katika mazingira ya namna hii katu hawawezi kuwa na uwezo wa kumudu hali halisi ya magonjwa yanayowataabisha watanzania kila kukicha. Siamini kama fani hii inaweza kuwa na makanjanja kama zilivyo fani nyingine lakini kama kweli wataalamu wanaandaliwa kwa zana duni punde wahitimupo hawana tofauti na kanjanja yoyote tu!

Ukiingia katika maktaba ya Mlimani utaamini kuwa wanafunzi wa miaka ya sasa wanataabika sana. Si suala la kushangaza kuwaona wanafunzi 700 wakifukuzana kukimbilia kitabu kimoja. Mara nyingine kitabu hicho hakipatikani lakini mwalimu anakuwa anahitaji kazi yake ifanyike tu!

Hali hii imewafanya wanachuo kutokuwa wabunifu kwani kazi ya mtu mmoja inaweza kuandikwa na wanachuo 50 na bado mwalimu akatoa maksi tofauti. Sifahamu kama hao walimu huwa wanapata muda wa kusoma kazi hizo ama wanasahihisha tu bora lengo litimie.

Inawezekana pia kuwa idadi ya wahadhili ni ndogo pia kulingana na namba ya wanafunzi. Iweje kweli mhadhili mmoja awe na wanafunzi 600 halafu apate muda wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wake wanamuelewa na tena apate uwezo wa kuwapa majaribio ili kuamini umakini wa kazi yake?

Hapa lazima patazamwe kimakini kwani panachangia sana kudumaza elimu. Elimu haiwezi kutolewa huku hakuna wataalamu wa kutosha. Kuna kila sababu ya kuwa na wataalamu wengi ili waendane na ongezeko kubwa la wanafunzi chuoni hapo.

 Nafahamu kuwa mbinu hii ya kuongeza idadi ya wanachuo inaweza kusaidia katika kupatikana kwa wataalamu wengi wa siku za usoni. Kama lengo litakuwa ni hili basi kunatakiwa kuwa na mipango madhubuti ya utoaji wa elimu chuoni hapo.

 Ni vigumu kumpata msomi aliyefuzu vizuri toka zuoni hapo kama kweli hakuna vitabu vya kutosha. Tena si kupatikana vitabu tu bali morari wa kusoma vitabu umepotea miongoni mwa wanafunzi wengi Tanzania na chuo Kikuu pia.

Uwezo wa wanafunzi wenyewe kumudu gharama za kununua vitabu ni mdogo mno kulingana na vitabu vya taaluma zao kuwa ghali. Kila mwaka wa masomo serikali hutoa shilingi za Kitanzania 120,000 kwa kila mwanafunzi aliye chini ya udhamini wake kwa ajili ya vifaa vya masomo.

Katika fungu hili vipo vitu vingi atakiwavyo mwanachuo kununua na kamwe hataweza kunua kitabu cha kiada kutokana na bei zake kuwa kubwa. Kiasi hicho cha fedha ni kidogo mno hivyo hakiwezi kuwasaidia wanachuo kwa kiwango kinachotakiwa.

Ongezeko la wanafunzi chuoni hapo limesababisha hata ratiba ya masomo kuanza saa moja asubuhi na kumalizika saa mbili usiku. Si jambo la kushangaza kumuona mwanafunzi akimaliza kipindi saa nne asubuhi na kusubiri kile cha saa moja usiku huku akikabiliwa na kurudi kwake Kajiungeni ama Mbagara ambako ni mbali sana toka chuoni hapo.

Idadi hiyo kubwa imefanya tena tatizo la makazi chuoni hapo ama katika hosteli za wanafunzi zilizo nje ya chuo hicho kubakia pale pale. Wangekuwa pamoja  ingewezekana tu kuwafundisha hata katika muda huo lakini sasa anaumizwa mwanafunzi anayeishi nje ya chuo hicho.

Mwanafunzi huyo huyo atatakiwa kurejea kesho yake saa moja asubuhi ili awahi kipindi cha kwanza hali inayowafanya wengi wakose hata nguvu za kwenda maktaba kujisomea kutokana na usingizi kuwatala. Hakuna  tena raha ya kusoma na masomo yanaonekana adhabu jambo ambalo ni hatari kwa msomaji yoyote kuelewa dhana mpya kiundani kutokana na mazingira hayo magumu.

Bado tatizo la vyumba vya masomo kulingana na idadi ya wanafunzi lililokuwepo miongo mingi liko pale pale. Hakuna uwiano mzuri kati ya idadi ya wanachuo wanaoingia na vyumba vya kusomea. Chumba kinachowatosha wanafunzi 250 sasa kinatumiwa na wanachuo 700 hali ambayo ni hatari si tu katika kuelewa masomo bali hata kiafya.

Nadhani bado tunayo safari ndefu sana katika zama hizi za utandawazi lakini kuna kila sababu ya kuhakikisha tunaboresha maisha ya wataalamu wetu ili tuweze kweli kupata wataalamu bora watakaoweza kupambana katika ushindani ndani ya utandawazi. Pasipo kufanya hivi hatuna pa kwenda kesho kwani hata sasa tumeshaanza kulia.

Ni vigumu sasa kumshindanisha Mtanzania aliyehitimu shahada yake na Mkenya ama Mganda katika usaili. Wenzetu wataweza kujieleza vizuri si tu katika taaluma zao bali pia katika maisha ya kawaida.

Hali hii inatokana na mifumo safi wanayopata katika maandalizi ya elimu ya huko katika nchi zao. Ni wakati nasi tuamke ili kukabiliana na hali hii la sivyo tutajikaanga kwa damu zetu wenyewe.

Uamsho ni Ulokole katika Ukatoliki? (4)

Katika matoleo yaliyotangulia,Askofu Kilainialisema kuwa, kwa bahati mbaya, kwa kuwa walioanza walikuwa Walokole, utakuta mara nyingine katika Uamsho wa Kikatoliki Walokole utakuta pia wamo humo na hata wanajaribu kuleta vitu vyao vya Ulokole humo ndani. Endelea.

Hata hivyo ninafurahi sana nilipowaambia wakarismatiki waeleze wao ni watu gani, wakati tulipoviambia vyama vyote vya kitume kueeleza ni akina nani, wao waliandika hivi:

Lengo: Kueneza Injili, kutangaza Habari Njema ya kwamba Mungu anatupenda na kwamba Yesu Kristo katika maisha yake, kifo na ufufuko, anawawezesha wanadamu wote kupatanishwa na Mungu na kupokea wokovu kwa kushiriki uzima wa milele.”

 Hilo ndilo lengo la kwanza, hivyo unakuta mambo kama haya ya kuponya ni namna tu, ya kusaidia, lengo la pili ni kuwatakasa watu na lengo la tatu ni kutangaza upya mambo ya ulimwengu na hivyo, ndiyo kusema kuwa karama hii ni nzuri kwa sababu hata katika Jimbo tunasema tutegemeze Umoja wa Vyama vya Kitume na kila Chama waeleze vizuri karama za wengine na waeleze vizuri karama zao ili waeleweke.

Kuhusu utaratibu wa Kanisa katoliki kuanza kuhubiri Nje ya kanisa, Askofu Kilaini anasema:

Kwa kweli tunajitahidi kusema kuwa, ibada  kama ibada ya misa, ifanyike kanisani, mwaka huu ibada yao waliifanyia nje, lakini Msimbazi Senta (Dar es Salaam). Ilikuwa ni nje, halafu wakaandamana kwenda Jangwani (Dar es Salaam), sio kwa sababu eti labda ibada haiwezi kufanyika Jangwani, ila kwa sababu tulitaka kusisitiza ule utakatifu wa kanisa.

Na hii ilikuwa ni kwa sababu kwamba tunapokwenda kule Jangwani, tunajikuta kila mtu yupo; mwingine hata anataka Ekaristi, lakini hajui ni nini; kwanza waende waeleze Ekaristi ni kitu gani.

Hata hivyo, wale wanaokuja katika Misa, tukiwapeleka kanisani (Msimbazi), sio kwa sababu hakuna uwezekano wa kufanyia Jangwani na pia, sio eti ni kwa sababu ni Karismatiki tu, ndio wanaopeleka Jangwani kwa sababu hata Baba Mtakatifu alipokuja, Misa Takatifu ilifanyika Jangwani hapohapo.

Pia, ni vizuri kufahamu kuwa kusali nje sio kitu cha Karismatiki tu, ila nao wanaitumia njia hiyo kwa kuwa inakubalika na inatumika kuwaita watu wengine.

Hii ni kawaida maana hata kwenye Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo, tunaposali, tunasali nje kwenye sehemu zilizowazi karibu na watu.

Tunachofanya pale sio Ukarismatiki. Vaticano ya Pili imetoa Misa ndani ya Kanisa kwenda kwa watu. Sio kwamba imeitoa kanisani kuipeleka nje, hapana…. Imeianzisha kanisani na ikitoka kanisani, iendelee nje.

Hivyo, wanachokifanya ni kutimiza hicho hicho tu, cha Vaticano ya Pili, ila wao wanakifanya kwa shamra shamra; wanapaza sauti, kwa nyimbo, kwa kuruka, kwa matangazo, lakini ni kitu hicho hicho cha WALETENI WATU WOTE WAJE KWANGU.

Alipoulizwa mintarafu madai ya baadhi ya Waprotestanti kuwa Wakatoliki sasa wanaiga mtindo wa Waprostenti katika kuhubiri, Askofu Kilaini alisema:

Mimi hilo halinitii wasiwasi hata kama ni kuiga kwa sababu Mtaguso wa Pili wa Vatican unasema HATA KATIKA MAKANISA MENGINE KUNA VITU VIZURI.

Sasa kama kuna kitu kizuri ambacho sisi kwa bahati mbaya tulikuwa tumekisahau kidogo, tukikiweka hakuna ubaya wowote kwa sababu ni kile cha Kanisa lile tulilorithi toka kwa Kristo.

Na vitu hivi havikuanza sasa, vilianza toka zamani. Mtakatifu Fransisco katika Karne ya 13, alianza kwenda na watu wake, akihubiri katika masoko.

Alianza mapema kweli na kwa kwenda kidogo tu, alikuwa na watu 3000 waliokwenda kila mahali; wakisimama kila mahali na kuanza kuhubiri na hao hawakuwa Waprotestanti kwa sababu katika karne ya 13, Waprotestanti walikuwa hawajaja.

Hivyo, kitu hicho sio kipya ila, labda tulikuwa hatujakianza sawasawa na sasa tunakianza kwa namna yetu.

Unajua, katika Ubatizo, tunapakwa mafuta ya Krisma; na unapakwa na Roho Mtakatifu. Unapokuja kwenye Kipaimara, unapakwa tena kama mtu mzima. Kisha unapokuwa Padre, tunakupaka tena kwenye viganja vyako yaani kukuongezea sasa kwamba unatakaswa kwa Roho Mtakatifu.

Unapokuwa Askofu, Wanakupaka Karisma kichwani. Bado ni Roho Mtakatifu Yule yule tunayempata.

Kwa hiyo Roho Mtakatifu tulikuwa naye. Watu walikuwa wakihubiri. Na ndivyo, hata sasa watu ambao sio Wanauamsho, unawakuta katika Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo wakihubiri.

Ukija kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu, wanahubiri; ukienda kwa Neokatekumenato, wanahubiri; ukienda kwa Lejio Maria, wanahubiri; wote hao kila watu wanahubiri kwa namna yao. Hata ukienda WAWATA, wanahubiri sio tu kwa sababu ya dini, hata kwa sababu ya dunia, wanapitia hukohuko; wanahubiri.

Ila sasa cha kujua hapa ni kuwa, Uamsho ni kundi moja wapo; tena dogo tu, linalosisitiza suala hilo na sio kwamba linaleta kitu kipya hapana.

Kwa mfano, sasa mtu anaweza kusema kuwa anakwenda kujiunga na Karismatiki. Wanaweza kumuingiza huko, wakamfanyia Ibada ya Roho Mtakatifu, hapa sio kwamba atapata sakramenti mpya, hapana Roho Mtakatifu ni yule yule isipokuwa yeye sasa anafanya rasmi kwa namna ya pekee kuwa NITAIFANYA IWE KARAMA YANGU, lakini si kwamba hakuwa nayo., anakuwa nayo kama watu wengine

 

Itaendelea.

Unywaji pombe na imani za dini

l Wanaokunywa pombe wana hatia Kibiblia?

l Viongozi wa dini wanaruhusiwa kunywa pombe?

Na Mwandishi Wetu

SUALA la chakula na vinywaji vinavyoruhusiwa Kibiblia, limekuwa likitumika vibaya kwa watu wanaotafsiri vibaya Maandiko Matakatifu. Wengine wanaitumia Biblia kudai kuwa wengine wanakula ama kunywa vyakula na vinywaji vinavyowatia unajisi na vinavyokatazwa na Mungu.

Uwepo wa kinywaji pombe ni moja ya kweli zilizo katika maisha ya mwanadamu hapa duniani. Binadamu wa karne zote na wa kabila mbalimbali wamekuwa wakiitengeneza na kuitumia pombe katika mazingira kadhaa.

Matumizi ya pombe ni kitu kinachohitaji mwongozo na maelekezo ya kimaadili kama zilivyo kweli nyingine za maisha ya binadamu.

Leo hii, tunashuhudia imani za kidini na vikundi vinavyokataa matumizi ya aina yoyote ya pombe.

Baadhi ya vikundi vinajaribu kutumia  kila njia mojawapo ikiwa ni pamoja na Biblia, kuonesha kuwa pombe ni kitu kibaya na imekatazwa na Mungu.

Baadhi ya wafuasi wa vikundi au madhehebu hayo, husema kuwa pombe ni shetani na yeyote anayeionja ni mfuasi wa shetani.

Wengine wamefikia hatua ya kudai kuwa chochote kile kinachohusika na utengenezaji wa pombe, mfano ndizi au ulezi ni shetani na havifai kutumiwa na binadamu.

Katika kijarida cha Jimbo Katoliki la Moshi (News Bulletin of the Diocese of Moshi – Kilimanjaro), Toleo la Mei 2000, Padre Gregory Olomi, alijadili kwa kina suala hili kama linavyozungumzwa katika toleo hili.

Jambo lililo wazi ni kwamba, pamoja na kampeni za watu hao, hawajafanikiwa kuiondoa pombe katika maisha ya watu.

Upo umuhimu wa kuwafundisha watu ukweli kuhusu kinywaji hiki kuliko kushikilia tu kwamba ni kitu kibaya.

Makala hii inalenga katika kujaribu kudhihirisha machache kati ya mengi yanayofundishwa na Biblia kuhusu pombe.

 

POMBE

Pombe ni kinywaji chenye asili ya kilevi (kwa Kiingereza Alcohol). Kutokana na kilevi hicho pombe huitwa pia kileo.

Pombe hutambuliwa kuwa ni kali au isiyo kali kutokana na kiwango cha kilevi kilicho ndani yake.

Kiwango cha kilevi kinachopatikana katika aina fulani ya pombe kinategemea namna pombe hiyo ilivyotengenezwa. Kutokana na kilevi hicho, mtu anapokunywa pombe kupita kiasi, mishipa yake ya fahamu hulegea, mwenyewe kujisikia kuchoka, hushindwa kufikiri na kufanya kazi zake za kawaida na kwa wakati wake, hukosa mpangilio sahihi katika kufikiri na katika utendaji wake. Mara nyingine hopoteza kabisa fahamu.

Historia inaonesha kuwa makabila na mataifa mbalimbali yamekuwa yakitengeneza na kutumia aina mbalimbali za pombe.

Mfano Wachaga hutengeneza ‘Mbege’, Wazaramo ‘Tembo’, na Wahaya ‘rubisi’.

Pombe za mataifa ya kigeni ni pamoja na divai (au mvinyo), Bia, Whisky na hata Brandy.

Kutokana na ukuaji wa teknolojia na mawasiliano rahisi viwanda na utengenezaji, pia matumizi ya pombe hizo za kigeni yameenea katika nchi nyingi duniani.

Bw. Stephen Mmassy wa Tanga, aliwahi kusema katika gazeti moja la Kiswahili litolewalo mara moja kwa juma nchini kuwa, “Pombe sio ulevi. Chakula sio ulafi na ukinywa pombe mno, unazidisha mno kilevi ndani ya mwili, hivyo, unakuwa na ulevi. Pombe inaweza kuwa divai, bia, mnazi na kadhalika”.

Akafafanua ULEVI kuwa ni kula chakula au kutamani kuwa na kitu fulani kupita kiasi.Bw. Mmassy, aliuelezea ulevi kuwa ni hali ya kupotewa na fahamu au kutokuwa katika hali ya akili timamu kutokana na matumizi ya vitu kama dawa za kulevya,  kuvuta bangi na kunywa pombe kupita kiasi.

Kama hivyo ndivyo, Bw. Mmassy akauliza, “Je, kuna mtu mwenye mamlaka ya kukiita chochote alichoumba Mungu kuwa ni najisi?”

Katika Biblia, Maandiko mengi yanabainisha tofauti kati ya pombe au ulevi, lakini makala haya yatatumia Biblia kudhihirisha ukweli wote kuhusu pombe na ulevi.

Agano la Kale:

Tusomapo Maandiko Matakatifu, tunaona wazi jinsi Mungu alivyopendezewa na sadaka ya kinywaji cha divai/ mvinyo, ambapo aliagiza viteketezwe pamoja na vitu vingine, na hivyo kuifanya harufu nzuri yenye kumpendeza (Kut 29:40, Hes 15:7).

Tena Mwenyezi Mungu aliruhusu watu kunywa divai. (Kumb. 14: 23, 26: Wim. 5:1.) Hii ni mistari michache tu kati ya mingi iliyomo katika Biblia. Je. Mungu anaweza kukubali apewe kitu najisi au kitu ambacho ni dhambi kama sadaka ? Je, ni kweli kuwa analaani na hapo hapo anaruhusu ; angeeleweka ?

 

AGANO JIPYA

Tunaona Muujiza wa kwanza alioufanya Yesu Kristo katika Harusi ya Kana, ni kugeuza maji kuwa divai, tena nzuri kuliko iliyokuwa ikitumika (Yn. 2 :10).

Tena Bwana Yesu kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake, alikunywa divai. (Mt. 11 :18-19 ;26 :27-29). aligeuza divai kuwa damu yake !

MILA NA UTAMADUNI

Mmasai anapochomeka mkuki nyumbani kwa mwenzie anaashiria nini?

l Wake wengi, watoto wengi ni sifa

Na Furaha Piniel

 

WAMASAI ni miongoni mwa makabila yaliyo mstari wa mbele katika kulinda na kudumisha mila zao. Ukweli huu unadhihirika wazi kwani wengi wao licha ya kuingia katika miji mikubwa, bado mavazi wanayovaa na namna ya kusuka nywele zao, ni ishara tosha ya kuwatambulisha.

Kabila hili ambalo kwa kiasi kikubwa ni wenyeji wa Mkoa wa Arusha, hutumia mavazi hayo ikiwa ni miongoni mwa nyanja zinazotambulisha utamaduni wa jamii pamoja na chakula, lugha na michezo.

Kabila hili la Wamasai kwa kiasi kikubwa, limeonesha kutobadilika haraka wala kukubali kile kiitwacho KWENDA NA WAKATI kwa kuiga mitindo mbalimbali ya mavazi, michezo na hata chakula.

Makala hii haikusudii kuizuia jamii kwenda na mabadiliko ya sasa, bali inalenga kuihimiza jamii kudumisha tamaduni, mila na desturi zinazoifaa jamii ya sasa.

Ni vema na haki ya kila Mtanzania kula, kuvaa, kwenda, kutoa maoni yao kulingana na nguvu na mwongozo wa Katiba ya nchi ili mradi tu, asivunje sheria.

Msisitizo wa makala hii ni kuiasa jamii kuepuka kuifanya Tanzania kuwa dampo la mavazi, tamaduni na jadi za watu wengine bila kujali kipi kizuri, na kipi kibaya.

Hii nayo haimaanishi kuwa, Tanzania lazima ibakie katika hali ya kutembea kwa miguu zaidi kilomita sitini ili kupata mahitaji ya lazima kama maji, vyakula na vitu vingine, hapana.

Pia, haina maana kuwa Watanzania waendelee kupanga mistari ili kupata sukari, unga, maharagwe dukani, wala eti waendelee kuvaa ngozi na magome kama katika zama zilizopita, wala kutuma barua kwa mkono tena kwa njia ya treni au miguu, hata kidogo.

Lengo la makala haya, ni kuonesha hali halisi ilivyo katika jamii ya Wamasai na namna jamii hiyo inavyotazamwa.

Kwa asili, Wamaasai ni wafugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda. Ufugaji ndio njia yao kuu ya kuendeshea maisha kwa kupata chakula na fedha kwa ajii ya mahitaji mengine.

Watu hao huishi kwa kutegemea mvua kwa ajili ya malisho ya mifugo wao. Ni watu wa kuhama hama kutafuta majani na maji kwa ajili ya mifugo.

Katika kabila hilo, mgawanyo wa kazi huwekwa kulingana na umri wa mtu na jinsia yake.

Kundi muhimu katika jamii ya Kimaasai ni vijana kuanzia umri wa miaka 18 hadi 35, maarufu kama ilmuran (morani) kama wengi walivyozoa kuwaita.

Kundi hili huandaliwa chini ya usimamizi wa kundi la rika lililowatangulia katika tohara na hata pengine kuzaliwa.

Hata hivyo, kunakuwepo na mtiririko maalumu wa kuwaandaa vijana kukabiliana na mambo mbalimbali yanayoweza kutokea katika jamii kama vile janga la moto, ajali, matetemeko ya ardhi, wizi na uvamizi wa aina yeyote.

Morani ni tegemeo muhimu la usalama katika jamii ya Kimasai kama lilivyo jeshi la ulinzi katika nchi yoyote.

Huhakikisha kuwa jamii yao inakuwa salama kwa nyakati zote.

Pia, wanalo jukumu la kuhakikisha kuwa mifugo wanapata majani na maji kwa wakati wote, na ikibidi kuhama kama kuna wasiwasi wa kutokuwepo na mvua.

Morani pia huongeza idadi ya mifugo yao kwa kuchukua mifugo ya watu wengine (makabila) hata ikibidi kwa nguvu.

Mzee Oltwati lo Leng’agile, kutoka Impopo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, alisema hajui kisa hasa cha Wamasai kufanya hivyo, ila aliambiwa na babu yake kuwa vitendo hivyo ni vya jadi.

Aliongeza kuwa babu yake alimwambia kuwa miaka iliyopita, kulitokea njaa kali sana, hakutaja mwaka kwani hajui kusoma wala kuandika isipokuwa yeye anakumbuka alipo hadithiwa na babu yake kuwa ilikuwa ni wakati wa wakoloni aliowataja kwa jina la Ildashi yaani Mjerumani, hivyo mifugo wote ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda walikufa kwa wingi kutokana na ukame na magojwa yaliyojitokeza wakati huo, kitu kilichosababisha watu kula hata mizoga.

Baada ya mvua kunyesha na kupoa kwa ugojwa wa mifugo kukawa na kundi la Maasai wachache waliobakia na kuanza kujiwekea sheria kuwa ng’ombe yeyote na popote alipo, ni ng’ombe wa Mmasai. Hivyo, wakaanza kuwapora watu mifugo.

Aliongeza kuwa tabia hiyo ipo hadi sasa, lakini anadhani kuwa, huenda itapotea baada ya ongezeko la watu wa Serikali kuwa karibu zaidi na makazi yao.

Kwa misingi hiyo ,watu waliohusika na kazi hiyo ni Morani pekee ambao ni kundi la vijana lenye nguvu na amri juu ya nini kifanyike na nini kisifanyike, ingawa wanaheshimu sana uongozi wao na wazee.

Hata hivyo, siku hizi kuna wimbi kubwa la vijana wa Kimasai wanaoingia mijini na wengi huajiriwa kama walinzi katika maduka, gereji na ofisi mbalimbali kwa imani kuwa wengi wao ni waaminifu.

Bw. Ndininiyi Ole Lomayani kutoka Oltrumet wilayani Arumeru katika Mkoa wa Arusha, ni miongoni mwa Morani waliohojiwa na makala haya kuhusu sababu ya vijana Wamasai kuhamia mijini na kuacha  mifugo yao huku wanawake, watoto na  wazee wao wakiendelea kupata shida huko vijijini.

Yeye alianza kusema kuwa kutokana na hali ya hewa kubadilika na nchi kuwa kame na Serikali kumnyima eneo la malisho ya ng’ombe eti ili kuhifadhi mazingira, imekuwa ni vigumu kupata mahitaji kwani afya ya mifugo imedolola na haitoi mazao bora.

Anasema kutokana na kukosa malisho bora, mifugo sasa hawafai kuuza wala kwa kuchinja, na kilichobaki ni kwenda mijini kutafuta kazi ili wapate fedha kwa matumizi yao.

“Kwa sasa hatuna maeneo ya kutosha kwa ajili ya kulisha mifugo yetu. Kuna elimu iliyoanzishwa miaka ya nyuma kuwa lazima mtu awe na mifugo wachache,  lakini wenye manufaa kwake.”

“Unatakiwa kuwa na ng’ombe watatu hadi wanne wa kisasa tena wa maziwa tu. Sasa hao ng’ombe gharama yao ni kubwa kwani ni lazima kuwa na maji zaidi ya lita 40 hadi 70 kwa siku kitu ambacho hakiwezekani kwetu kupata hayo maji kila siku,” alisema.

Akaongeza, “Unatakiwa kuwa na dawa ya kuwapiga mara mbili au tatu kwa wiki na hatuna uwezo huo; bado unatakiwa kuwa na pumba ya kuwapa ili wawe na maziwa mengi na hiyo ni pesa pia.”

Anaendelea kusema, “Sasa unakuta tumeacha hali ya ufugaji wetu ili kufuata maelekezo ya Serikali, lakini tunajikuta tukiachwa njiani bila msaada. Hii ndio hali inayotufanya tuje kutafuta kazi”.

Hata hivyo, alifafanua kuwa pamoja na mabadiliko yaliyotokea baada ya kupewa elimu ya mifugo wachache kwa faida, alisema ni lazima wabadilike kwa kuwa dunia ya sasa sio ile ya jana na mambo yanaendelea kubadilika.

Katika jamii ya Kimaasai, mtoto wa kiume ndiye pekee anayepewa kipaumbele kwa mambo mbambali.

Mtoto wa kike hana nafasi wala cha kurithi kutoka kwenye familia zaidi ya zawadi anayopewa na mama yake au baba yake anapoolewa.

Tohara ni kitu cha lazima katika kabila hilo bila kujali huyu ni mtoto wa kike wala wa kiume. Hatua hiyo huchukuliwa kama ni hatua mojawapo muhimu ya kutoka katika hali ya utoto, kwenda utu zima.

Vijana wanapotahiriwa huandaliwa kwa kupewa vyakula na dawa zaidi kama nyama na damu iliyochanganywa na maziwa (osaroi) kwa imani kuwa, wanawakinga dhidi ya maradhi mbalimbali kama vile tetenas.

Baada ya kutoka jandoni, hupelekwa porini Olpul kwa muda wa miezi mitatu au zaidi kutegemeana na idadi ya mifugo waliowapeleka huko kwa lengo la kuchinjwa.

Olpul ni sehemu maalum inayoandaliwa ndani ya misitu mikubwa (porini) ili kuwaandaa vijana (Ilmuran yaani Morani) hasa kwa kuwapatia dawa na nyama ili kuwa imara.

Hali kadhalika, mtoto wa kike hutahiriwa pindi panakuwepo na tohara kwa vijana wa kiume au hutegemea hali ya mabadiliko ya mwili kwa mtoto wa kike.

Suala la kwamba baadhi ya wanawake hupoteza maisha wanapotahiriwa, Wamaasai wanasema haijawahi kutokea mwammke akafariki kutokana na tohara, bali wao wanaamini kuwa kifo kinaweza kumjia mtu wakati wowote bila kuangalia ni wakati gani.

Kuhusu uongozi, Olaigwanani ndiye kiongozi mkuu katika jamii hiyo.

Kiongozi huyo hupewa rungu nyeusi ambayo ni alama kuwa yeye ni mtu muhimu kwenye jumuiya, na pia huonesha tofauti kati ya viongozi wakuu.

Kazi kubwa ya viongozi hao ni kutoa miongozo na maamuzi yanayoleta utata katika jamii.

Wanawake ni kundi ambalo halina sauti katika jamii hiyo licha ya mchango mkubwa unaotolewa na wanawake katika kuiendeleza jamii yoyote duniani.

Kazi yao kubwa ni kujenga nyumba (manyata) pindi wanapohamia kwenye makazi mapya, kulea watoto, kuteka maji, kukata kuni na kuandaa chakula.

Nyumba za Kimasai ni rahisi kujenga ukizingatia wapo ndani ya pori na hawahitaji misumari wala saluji.

Wanawake hutumia miti kama oleleshua, oltepesi, oloirien na magome ya baadhi ya miti kwa kujengea nyumba zao.

Kinyesi cha ng’ombe hutumika kukandika ukuta na paa mithili ya saruji na hii hutumika kwa kuwa haina gharama wala ugumu wowote katika upatikanaji.

Ndani ya nyumba huwa na vyumba na mpangilio wa vyumba vya kulala (irtwatini), jiko (oltiren), na chumba kidogo kwa ajili ya ndama wadogo na mbuzi wadogo vile vile (alale).

Nyumba hizo hazihitaji kuwa na madirisha wala milango imara, bali huwa na milango ya kufunga na ngozi au pengine kitawib cha mti (Olchoni/ oltim).

Sasa, Morani wanapofika kwenye manyata (mkusanyiko wa nyumba zilizojengwa kwa pamoja katika familia nyingine ya Kimasai) za majirani zao kwa mazungumzo, matembezi au wanapokuwa kwenye mapumziko yao, kuna tabia ya kuweka mkuki nje au kuuchomeka chini.

Miongoni mwa tafsiri zinazochukuliwa na jamii nyingi juu ya suala hili, ni madai kuwa Mmasai mwanaume anapokwenda katika familia ya mwenzake, akachomeka mkuki nje, ni ishara kwa mwanaume mwenye familia kutambua kuwa yupo mwanaume mwingine ndani akiongea kwa faragha na mke wa mwenye nyumba.

Jamii nyingi ya watanzania, inadai kuwa kwa kufanya hivyo, Mmasai huyo ambaye ni mrika wa huyo mwenye mke, kimila huwa amehalalishwa na hawezi kupata swali wala upinzani wowote toka kwa mume wa mwanamke.

Inadaiwa na baadhi ya makabila kuwa, kwa kutambua hilo, Mmasai mwenye mke huwa hana la kuhoji na badala yake, huzurura zurura nje, akisubiri yule aondoke ndani ili naye sasa arejee nyumbani kwake; hakuna swali.

Kuhusu suala hili, Mzee Ndobir Lendulo (55) wa Kijiji cha Emarti, wilaya ya Mondoli anasema; “Sababu kubwa ya kuweka mkuki nje ni kuwa, ni vigumu kuingia ndani na mkuki, na pia inakuwa vigumu wakati wa kutoka nao nje haraka kama kuna dharura”.

 Pamoja na hivyo, alisema kuwa hiyo ni ishara kama zilivyo ishara nyingine, kwamba kuna Morani ndani ya nyumba hiyo, hivyo mkuki huo huwa kivutio kwa Morani wengine kujumuika na kundi la Morani wenzake.

Wanapojikuta wamefanya kundi kubwa kiasi cha kuwaridhisha, kama ilivyo desturi yao huanza kucheza.

Bw. Ndobir alifananisha mkuki na viatu kwenye nyumba za wasomi na Waswahili walioendela kama alivyosema yeye kuwa watu huvua viatu na kuacha nje kitu ambacho kwao ni mwiko.

Naye Morani, Lesikar Lolemoipo (36) kutoka Sikirari anasema ; “Hiyo ni imani mbaya, lakini hakuna haja ya kupingana na mawazo ya watu kwa sababu ni haki yao kuwaza kwa jinsi wanavyofikiri.”

Akaongeza, “Ninavyo fahamu mimi ni kwamba ni kitu cha kawaida tu, wala haina maana hiyowanayosema watu.”

Sasa, tukigeukia upande wa wazee wenyewe, tunakuta kuwa ni kundi ambalo kazi yake kubwa ni kusimamia utekelezaji, kushamili, kutatua migogoro na kutoa miongozo (utawala).

Kuhusu nafasi ya wanawake wazee, Mmoja wa Wazee wa Kimasai anayefanya kazi ya ulinzi katika moja ya gereji zilizopo Ilala, Dar es Salaam, aliyekataa kutajwa gazetini, alisema “Kwa Mmasai, mwanamke ni mtu asiye na nafasi na pia, mwanamke hakui mbele ya wanaume, yeye anakua kwa wanawake wenzake.”

Anasema kinadharia, jamii ya Kimasai, mtoto wa kiume akishatahiriwa, anakuwa mkubwa kuliko mwanamke yeyote.

Watoto ni kundi lisilo na majukumu mengi wala makubwa, mbali ya kuchunga ndama, mbuzi, na kondoo wadogo.

Watoto hawa hufanya kazi hii wakati wakubwa zao wakiwa wamewapeleka mifugo wakubwa kwenye maji na malisho.

Katika kazi hiyo, hakuna ubaguzi wa kijinsia; watoto wote wa kike na wa kiume hufanya kazi hiyo kwa pamoja.

Chakula kikuu cha Wamasai ni nyama, maziwa na damu ya ng’ombe. Kwa sasa baada ya kuenea kwa zana za kilimo hadi vijijini, hununua unga japokuwa ni kwa msimu.

Hivyo, uji ni kiungo kikuu katika nyama. Maziwa hununuliwa debe moja kwa kila mke kwa muda wa mwezi mmoja.

Nyama huliwa ingawa ni kwa nadra sana kutegemea matukio muhimu kama sherehe za jando, unyago, ndoa au uchumba, uzazi au vijana kupelekwa porini (OLPUL).

Zaidi ya ng’ombe kumi hupelekwa na vijana hao na kuchinjwa. Vijana hao hurudi nyumbani na ngozi na pengine na utumbo au mafuta kidogo ili walau kuwadanganya na kuwaridhisha wanawake na watoto ambao ni watafutaji na kiungo muhimu kwenye familia.

Jamii ya Kimasai katika suala la ndoa ni tofauti sana na makabila mengine mengi ya Tanzania.

Kwa Wamasai ndoa yao huanzia utotoni na hii inategemea uhusiano uliopo baina ya pande mbili zinazotaka kuoana.

Malipo ya mahari ni kidogo kwani mtu hulipa ng’ombe saba hadi kumi, ila ni kwa awamu tofauti, ndoa zao ni za kudumu.

Ndoa za Kimasai hudumu muda mrefu kwani mila za Kimasai humtazama kwa macho ya kusuta mwanamke au mwanaume aliyeachika.

Idadi ya wanawake hutegemea uwezo wa mwanaume, anaweza kuwa na wake 15 hadi 20, ili mradi tu awe na mifugo ya kutosha.

Wanawake ni watu wanaopendana sana bila kujali idadi yao kwa mume wao, huwa hawana wivu kama baadhi ya makabila mengine, wengine  wanasema Wamasai wanafuata Agano la Kale.

Kuwa na watoto wengi katika jamii hiyo ni fahari kubwa, Inasadikika kuwa, kila mtoto amekuja duniani akiwa na riziki yake hivyo, utajiri wa mtu hupimwa kwa idadi  ya watoto alionao na mifugo.

Hata hivyo, Wamasai wengi wanaonesha wasiwasi kuwa kwa siku zijazo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, huenda baadhi ya mila zao zikapotea.

Wanasema kuwa kuna miradi mbalimbali  inayoanzishwa vijijini na watu bila kutoa elimu ya kutosha au kuishia njiani na kuwaacha wakiwa wameacha njia  zao rahisi ya maisha.

Wameeleza pia kuwa, kutokana na mbuga za wanyama kukabidhiwa kwa baadhi ya mashirika ya nje, wamepata usumbufu wa kuwalisha mifugo wao kama zamani, hivyo Serikali inapopanga mipango, izingatie namna wanavyoweza kuendesha ufugaji wao.

Mzee Loidini Saiteu wa Kijiji cha Lengijane, Wilaya ya Arumeru, alisema kuwa zamani wao hawakuwa na mipaka katika malisho ya mifugo yao.

Hata hivyo, Wamasai na Watanzania kwa jumla, hawanabudi kuchuja ili kuzibaini mila zenye manufaa ili waziendeleze na zisizo na manufaa kwa jamii, waachane nazo.

Elimu ni urithi muhimu ambao jamii ya Kimasai haina budi kuwapa watoto wake na pia, katika kipindi hiki cha UKIMWI, haina maana kuendelea kuwa na imani kuwa wake wengi ni umaarufu.

UCHAMBUZI WA KITABU

Ushairi na Ulimwengu Ulivyo Sasa

Kitabu: CHUNGU TAMU

Mwandishi: Theobald Mvungi

Mhakiki: Projest M. Christopher

 

Utangulizi: Chungu  Tamu ni ushairi unaozua wasiwsi kwa wanyonyaji, wala rushwa, walanguzi, madikteta, wazembe na wote wanaokifanya chombo kiende mrama. Lakini ushairi huu unaleta matumaini kwa wanyonge, wanaoonewa, wanaonyonywa na wote wa chini. 

Ushairi huu unaibua matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii hasa yale ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

1.        Uongozi mbaya: Katika harakati za ujenzi wa jamii mpya, msanii ameonesha kuwa uongozi mbaya ni kikwazo. Viongozi wanatumia vyeo vyao visivyo na wengine kung’ang’ania madarakani na kujiita life president afanyao Idd Amin, msanii anasema:

“Tulio wengi twajua, hawa wanatudhulumu, chakula kutumezea, kwa niaba ya kaimu, kwa maringo watembea, matumbo yenye karamu, lakini yajulikana, kujua tu haitoshi” (Uk.10)

Kutoka katika shairi lake la  “Chini ya Mti Mkavu,” msanii anawashambulia viongozi wananyonya jasho la wenziwe bila kufanya kazi. Msanii anasema wakae wakijua kuwa arobaini zao bado ila ziko karibu hasa tukirejea mstari wake, anasema:

Ila walima korosho, wana msemo wa jadi, uchao unao mwisho,….” (Uk. 10).

Bado viongozi wanatumia ubabe katika kuongoza kwao, kila kiongozi mmoja anataka amwoneshe mwenzake kuwa anao uwezo. Hasa msanii anasema katika “Tishio la Binadamu” kuwa:

“Mashindano ya silaha yamekuwa ni mchezo,

Wakubwa wanona raha kwa silaha waundazo,

Mabomu yaso na siha, Ndiyo yawapa uwezo,

Urusi na Marekani, Dunia mwaipa adha” (Uk.2)

 Nchi kubwa hasa za Magharibi zimekuwa zikitengeneza silaha ambazo ni hatari kwa binadamu, ndizo zinazowafanya  wapigane ili kudhihirisha umwamba wao. Laiti silaha hizi zingekuwa zinaishia huko mbali, ingekuwa heri kidogo, lakini hata hapa Afrika zinaletwa ili watu wapigane mfano Rwanda, Burundi, Angola, JK Congo,  Ivory Coast na nchi nyingi za Kiafrika.

Athari za vita zinajulikana huwakumba waliomo na wasiomo, kwani vita havina macho.

Bado msanii  suala hili la uongozi mbaya linamshughulisha katika shairi la "Chanzo ni Wenye Kauli" (Uk. 28), Tunaona jinsi viongozi wanavyofanya ulanguzi, magendo, uzembe na kujitwalia mali huku uzalishaji, sarafu na upungufu wa bidhaa ukizidi kujongea. msanii anasema:

"Kwanza ule upungufu

Wa bidhaa maarufu

Kwa uzembe ulokifu

Na uzalishaji mfu

Na ule uharibifu

Wa mitambo na sarafu".

Katika shairi la "Wimbo Wake Hatubani" msanii anawashambulia viongozi wote wapendao kuelekeza tu, bila wao kufanya kazi, mchana kutwa wamo ofisini wakati labda shughuli zi shambani  mfano mabwana shamba na mabwana mifugo.

Wengine hata ofisini hawapatikani wanakuwa kwenye pombe wakilewa. Magavana majimboni wanaishia ofisini badala ya kwenda vijijini.

Msanii anasema:

"Cheo kiko mkononi,

Agizo li mdomoni

Kila siku yu pombeni,

Wimbo wake hotubani,

Raia kazi fanyeni' (Uk. 29).

 Udikteta ni dalili mojawapo ya kutoweka kwa demokrasia, kuungausha utawala wa kidikteta huhitaji jeshi, lakini msanii anatuonesha kuwa hata baada ya jeshi kuchukua madaraka mambo huenda kijeshi kijeshi:

"Barani mabavu yatumika,

Dikteta asijeanguka,

Na majungu pia ayapika

Udikteta pasi shufaka,

Nasimulia ya Afrika" (Uk. 30).

Hapa inabidi tujiulize ni sababu gani hasa inayowafanya viongozi wang'ang'anie madaraka. Ni kulinda maslahi yao au kuwasaidia wananchi waliokupa idhini ya kuwa kiongozi wao, na kama wananchi hao hao sasa wanakupigia kelele kuwa uondoke kwa nini ubaki tena uongozini wakati idhini umeshanyanganywa.

 

2. Umaskini na Uvumilivu:

 

Watu wa chini wamekumbwa na matokeo ya uongozi wa tabaka la juu. wenye vyeo wanafanya lolote wanavyotaka bila kujali litawaathiri vipi wengine hasa wale wavuja jasho.

"Mekumbusha pia matumaini,

Ya wale walio chini

Wavuja jasho la ziada

Na kinyimwa faida" (Uk. 1).

Ni katika shairi la "Chungu Tamu" ambapo msanii anaonesha jinsi watu wa chini, wanavyonyimwa faida huku wanavuja jasho na wanaovuna ni wale ambao wimbo wao huko hotubani.

Msanii anaendelea kuakisi hali mbaya iliyomo katika jamii yetu. Wakulima wa vijijini wanaonekana wana hali mbaya wakati wao ndio wazalishaji wakuu kwani hata wale walio mijini chakula chao hutoka vijijini.

Yote hayo ni katika shairi la "Wanajua Kuvumilia".

"Afadhali kuimba ukweli,

Wimbo mchomo mkali,

Wimbo unalilia hali,

Ya vijiji vilivyo mbali,

Kwa wale wasio kauli" (Uk. 26).

Pia katika shairi la "Wengine Wabaki Taabani"

Msanii anaonesha jinsi watu wa chini wanavyobaki taabani. Viongozi (tabaka la juu) wanawakandamiza watu wa chini hata uhalifu unatokea huku viongozi wakishindwa kudhibiti. Inadhihirika dhahiri kuwa taabu hii inaanzia kileleni kwani:

"Majambazi wanayo idhini,

Kufanya lijalo akilini

Na hawataingia nguvuni,

Ma'na walinzi wamo njamani

Tabu yaanzia kileleni" (Uk. 32)

Lakini haya yote sio kwamba watu wa chini hawajayajua la hasha, wamesha yajua na dawa yake inatafutiwa vikombe ili inywewe wapo tu wanavumilia ili suluhu ipatikane, haya yamejidhihirisha katika shairi la "Mjanja yu Mashakani":

MAKALA YA JAMII

Wanaopata mimba shuleni watoe mimba, wajifungue au…

Na Dalphina Rubyema

UTARATIBU wa kuwafukuza shule wanafunzi wanaopata mimba wakiwa shuleni ni mzuri kwani utasaidia juhudi za Kanisa kuifanya jamii iishi kiadilifu na kwa kuzishika Amri za Mungu ikiwamo inayozuia kuzini (kushiriki tendo la ndoa kabla au nje ya ndoa halali).

Hata hivyo, ni wazi kuwa kila jambo lina ubaya na uzuri wake. Tunasema hivyo kwani tukigeuka na kuangalia upande mwingine wa shilingi, tunakuta kwamba adhabu hii isipotazamwa kwa makini, inaweza ikawa badala ya kuondoa tatizo, sasa inaongeza tatizo lingine; tena kubwa zaidi.

Bibi Martha Rwenyendela, anasema kuwa katika mila za kabila lake la Wahaya, binti akizaa kabla ya ndoa, anakuwa amejipunguzia heshima miongoni mwa jamii, anakuwa hana tena thamani mbele ya watu kama ilivyokuwa awali.

 “Hata kama akipata mume, basi huyo mwanaume anaweza akamuoa bila kutoa mahari yoyote na kama atatozwa ni kiasi kidogo sana pengine hata sh. 5,000 tu. Mwanamke huyo anakuwa hana thamani tena mara nyingi huitwa enyailya,” anasema.

Anasema ili kuepuka kashfa ya namna hiyo, wasichana wa kabila hilo hujitunza kwa adabu ya hali ya juu hadi wanapoolewa.

Bi. Anastazia Amon, (Siyo jina lake halisi) Mwanafunzi wa Mwaka wa Tatu katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Ardhi (UCLAS) Dar es Salaam, akichukuwa Shahada ya Usanifu wa Majengo, anasema kuwa alipokuwa Kidato cha Tano katika shule moja ya wasichana mkoani Kilimanjaro, alipata mimba na baada ya uongozi kubaini hali hiyo, akafukuzwa shule.

Anasema baada ya kumweleza kijana aliyempa ujauzito huo, kijana alicharuka, akaja juu na kudai kuwa hakuwa mhusika wa mimba hiyo.

Anasema kwa kuzingatia umuhimu wa elimu, wazazi wake walimtafutia shule nyingine baada ya kujifungua.

Aliendelea na masomo yake katika Shule moja ya Sekondari (jina tunalo) iliyopo jijini Dar es Salaam, alipohitimu Kidato cha Sita na akapata Daraja la Pili. Baadaye, akajiunga na Chuo cha Usanifu wa Majengo (Ardhi) kilichopo jijini Dar es Salaam.

“Si kwamba wazazi wangu wana uwezo kifedha, labda pengine ndiyo maana walinirudisha shuleni, hapana! Kipato chao ni cha kawaida tu, lakini kwa kufahamu umuhimu wa elimu, waliamua kunitafuatia shule japokuwa nilikuwa nimeisha fanya kosa la kuzaa kabla ya wakati,” anasema.

Anaongeza kuwa kabla ya kupata ujauzito, alikuwa halitilii maanani suala la elimu, lakini baada ya kujifungua na kurudishwa shuleni aliona sasa ni wakati muafaka kwake binafsi kujitambua yanayomkabili na hivyo, aongeze bidii na kwamba alikuwa akifanya makosa kwa kutowatii wazazi, walezi na kikubwa zaidi, kwa kutomtii Mungu.

“Sasa ndipo ninatambua kuwa nilikuwa ninawafanyia vibaya wazi wangu na Mungu mwenyewe,” alisema.

Anaongeza, “Niliona sasa tayari nimeisha kuwa na majukumu, kwani mbali na kujitunza mimi mwenyewe, pia nina jukumu la kumtunza mtoto wangu. Pia, niliona niuoneshe umma kwamba hata aliyezaa ana uwezo wa kuendelea kufanya vizuri katika taaluma licha ya kosa analokuwa amelifanya ama kwa bahati mbaya au kwa makusudi mradi tu, ajute.”

Wakati Bi. Amoni anasema hayo, msichana mmoja (jina tunalo) (23), Mkazi wa Tabata, jijini Dar es Salaam, anasimulia yaliyomfika huku akisema anaumia sana moyoni anapokumbuka yaliyomkuta na hukumu aliyopewa na jamii.

Anasema:  “Nimezaliwa katika familia fukara sana, lakini nashukuru Mungu pamoja na ufukara wa familia yangu, wazazi walifanikiwa kunisomesha hadi darasa la saba.

Bahati nzuri, nilichaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Wasichana ya Kilakala, mkoani Morogoro.

Pamoja na kupata bahati hiyo, kutokana na kipato kidogo cha wazazi wangu, iliwawia vigumu kumudu gharama za kunisomesha.”

Anaendelea, “Tukiwa tumeisha kata tamaa, alijitokeza msamaria mwema aliyejitolea kunisomesha hadi uwezo wangu wa kuyakabili na kuyamudu masomo utakapoishia.

Nilifurahi sana kwani mfadhili huyo alijitahidi kuninunulia kila kitu kilichohitajika kwa ajili ya shule.

Furaha yangu ilizimika ghafla pale mfadhili huyo alipofariki dunia kutokana na ajali ya gari. Wakati huo nilikuwa  kidato cha pili na kwa jumla, maendeleo yangu kimasomo yalikuwa yanaridhisha.

Baada ya msiba huo mzito, ilibidi wazazi wafanye kila mbinu ili niendelee kusoma angalau hadi Kidato cha Nne.”

“Wakaanza kuuza pombe ya kienyeji ambayo kwa kweli, iliwaingizia kiasi kidogo cha fedha ambayo hata hivyo, ilikidhi mahitaji muhimu ya nyumbani.

Mara kwa mara walinihimiza niongeze bidii katika masomo na nisikimbilie mambo ya anasa.

Nakumbuka mama alikuwa akiniadhibu pengine hata kunicharaza bakora pale ilipotokea mmoja wa wasichana pale kijijini akafukuzwa shule kwa sababu ya kupata mimba. Ingawa alijua dhahiri kuwa kosa limefanywa na mwingine, lakini alinipa hukumu hiyo kama angalisho kali huku akisema, “Unaona mwenzako aliyoyafanya, na wewe najua utakuwa kama yule, kwani watoto wa siku hizi mnatofautiana nini si wote ni hao hao tu.”

Rozi anaendelea,"Ulikuwa usiku mmoja, majira ya saa 2 :10 hivi, baba aliponituma niende kwa jirani yetu kumdai shilingi 200, zilizokuwa malipo ya chupa mbili za pombe aliyokopa.

Wakati ninarudi kutoka kwa Mzee huyo, ghafla nikavamiwa na kundi la vijana wa kiume wapatao sita.

Miongoni mwao, wapo waliokuwa na silaha kama panga na visu. Kibaya zaidi, hakuna hata mmoja niliyemtambua.

Walinikaba shingo, wakaniangusha chini. Huku wakinitishia kuwa wangeniua kama ningethubutu kupiga kelele, wengine wakaniwekea vitambaa mdomoni ili nikose uwezo wa kupiga yowe kuomba msaada,” anasema.

Anazidi kusimulia kuwa hadi sasa anashindwa namna ya kueleza kwa sababu hata akikumbuka mwenyewe, anajionea aibu, anafadhaishwa sana na kumbukumbu hiyo kila inapomrejea.

“Kila mmoja alifanya kila aonalo linamfaa ili mradi tu, walitekeleza unyama wao dhidi yangu, hasa kwa kunishika kwa nguvu. Tena eti kwa kufanyiana zamu.

Baada ya kutimiza haja yao, ninashukuru hawakutaka kunidhuru zaidi, wakaniamuru niondoke haraka. Nikatii amri na baada ya kufika nyumbani, nikahisi uchovu na maumivu, lakini, kwanza nikawa naona aibu mimi mwenyewe na kibaya zaidi, naona nitaiaibisha na kuifedhehesha familia yangu.”

“Nikajua endapo nitasema, nijue haitakuwa siri kwani dunia hii haina siri tena siku hizi. Dunia sasa ni kama kijiji.

Kutokana na uzoefu aliokuwa nao kutokana na umri wake wa kiutu uzima, mama, akabaini kuwapo kwa hali isiyo ya kawaida kwangu. Akaanza kunisaili ili ajue kulikoni huko nilikotumwa.

Hata hivyo, nilikataa katakata kusema ukweli juu ya yaliyonisibu.

Mama akamuita bibi mmoja aliyekuwa miongoni mwa watu waliokuwa wamejaa pale nyumbani wakinywa pombe.”

Anaongeza, “Mama akamuomba anichunguze mwili wangu na bibi huyo bila hiyana, akafanya alivyoambiwa na kubaini yaliyonisibu.”

“Mama akaniijia juu huku akinituhumu kwa kukiuka maadili ambayo amekuwa akinipa na kikubwa zaidi, akanikaripia kwa tuhuma kuwa nimevunja Amri ya Mungu inayokataza kuzini.

Nikajitetea kwa nguvu nikieleza ukweli wa yote yaliyonikuta japo mama hakutaka kunielewa.”

“Mama akaniambia Utakuwa ulitaka mwenyewe,” akasema na kuongeza, Kama hukutaka kwanini hukupiga kelele?”

Rozi anaendelea kusimulia, “Baba naye akayanasa yaliyokuwa yakiendelea na bila kuuliza akaja na kuninasa kibao huku akitishia kunichinja. Bado naamini kuwa msaada wangu ulikuwa wanywaji wa pombe pale nyumbani.

Wakati hayo yanatokea, zilikuwa zimebaki siku chache kukamilisha likizo yangu ya kumalizia kidato cha tatu.”

Anasema, “Ninaumia sana kwani hata muda wa kwenda shule ulipotimia, wazazi wangu wakakataa katakata kunipa japo pesa kidogo za kwendea shuleni, eti wanasema hawawezi kusomesha malaya.”

“Hatimaye baada ya kuwasihi sana nikisaidiwa na baadhi ya majirani, wazazi walikubali kunipa ada na miezi miwili baada ya kufika shuleni, ikafika siku ya siku.

Siku ambayo kwa kawaida wasichana hupimwa pale shuleni. Kaa la moto likaniangukia kwenye kidonda. Nikabainika kuwa mjamzito, Mhh!

Nilisononeka sana, kwani wanafunzi wenzangu walianza kunishauri niitoe mimba hiyo, lakini kamwe sikutaka kufanya hivyo.

Sio siri, nilikuwa katika kipindi kigumu, nilijua nimedharirishwa kwa kufanyishwa matendo hayo bila ridhaa yangu, isitoshe nimepata mimba huku bado ninasoma, sasa tena eti niue kwa utoaji mimba!?”

“Mambo yakazidi kuwa magumu, hakuna ujanja, anatolewa mwalimu mmoja ili akanikabidhi nyumbani kwetu.

Njiani, nilikuwa kama mwendawazimu, nilijua sasa siendi nyumbani, bali ninakwenda kwenye hukumu ya kifo; ninakwenda jehanamu.

Ndoto zangu za mchana, zikawa ndoto za kweli, wazazi wakaniamuru niondoke na kumtafuta aliyenipa ujauzito nami pasipo kujua niende wapi, nikatoka kama kuku aliyenyeshewa huku mama akitamka maneno ambayo hakika yaliuchoma sana moyo wangu.”

“Nilikimbilia kwa shangazi yangu ambaye anaishi kijiji jirani aliyenipokea,  lakini niliyopata huko, ni siri yangu.

Pamoja na ujauzito wangu alikuwa akinifanyisha kazi ngumu. Nakumbuka hadi siku nasikia uchungu wa kujifungua, shangazi alinipa kazi ya kuhakikisha nachochea moto kwenye pipa la pombe aliyokuwa akitengeneza.

Nakumbuka hadi navunja chupa ya uzazi, ndipo sasa alipokiri kuwa sasa, hali ni nzito.”

Bahati nzuri nikajifungua salama na kumpata mtoto wa kiume na baada ya mateso na masimango kuzidi nyumbani kwa shangazi , mama alinifuata na kunirudisha nyumba pamoja na mtoto wangu; mzazi ni mzazi bwana.”

Anaendelea, “Nasikitika kwamba baada ya kumuachisha mwanangu ziwa, alikuja mjomba wangu na kuwataka wazazi wangu waniruhusu niende naye mjini ili anitafutie shule ya Ufundi, lakini walikataa kwa madai kuwa naweza kubeba mimba nyingine.

Hivi unavyoniona mimi nimeharibikiwa maisha yangu na sijui mtoto nitamwambia nini pale atakaponiuliza baba yake ni nani.”

“Ninalia kwani sijui mtoto huyu nisiyemjua baba  yake, nitamlea vipi peke yangu, heri hata ningekuwa na hiyo elimu ya sekondari yenyewe, lakini sasa ndivyo hivyo, unyama nikafanyiwa mimi, adhabu ninapewa mimi, tena adhabu inayomhusu na mtoto asiyejua kitu,”  anasema kwa uchungu.

“Napenda sana kuendelea na masomo na nina uhakika kwamba nikipata shule licha ya mtoto niliye naye ambaye kwa sasa umri wake ni miaka miwili na nusu, nitafanya vizuri katika masomo yangu kwani chungu ya maisha nimeisha ionja.”

Mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Uhuru Mchanganyiko jijini Dar es Salaam, ambaye hakuta jina lake liandikwe gazetini, anasema kuwa inapotokea mwanafunzi akabeba ujauzito, kwa kweli uongozi wa shule husikitika sana kwani wakati mwingine mwanafunzi huyo unakuta ni miongoni mwa wanafunzi wanaotegemewa sana shuleni Kitaaluma.

Anasema kuwa baadhi yao ni wanafunzi wapole na inapotokea mmoja akapata ujauzito, mara nyingi walimu hubaki wakishangaa.

Anasema ukimdadisi mwanafunzi husika, utakuta kilicho mponza zaidi ni vitu vidogo likiwemo suala la chakula chipsi na kuku ama chipsi mayai.

Anasema kwa vile ni sheria kwamba mwanafunzi akipata ujauzito lazima afukuzwe, basi hata wao kama uongozi wa shule, hulazimika kutekeleza sheria hiyo ingawa moyoni huwa inawauma.

“Wakati mwingine wanafunzi hao huonesha huruma sana pindi wanapobainika kuwa na ujauzito na hali huwa mbaya zaidi pale wanapofukuzwa shule kwani katika hali ya kuogopa nini watawaeleza wazazi wao, wengine hujikuta wakijiua kwa kumeza vidonge,” anasema.

Bibi Halima Ayubu, Mkunga wa Jadi, mkazi wa Tabata- Mawenzi jijini Dar es Salaam, anasema kumwachisha mtoto masomo kwa sababu ya mimba, si ufumbuzi wa matatizo, bali ufumbuzi ni kuangalia jinsi gani ya kumsaidia baada ya kujifungua.

Anasema yeye kama mkunga wa jadi, amekuwa akipata shida nyingi ambapo wanafunzi wengi baada ya kupata mimba hufika nyumbani kwake kwa nia ya kutoa  mimba.

Anasema mara nyingi huwaonea huruma wanafunzi hao, lakini kwa vile yeye kazi yake ni kuzalisha badala ya kuchoropoa mimba, huwapa ushauri wa kuendelea kulea mimba hizo.

Anasema, Heri mtoto anayekubali kulea ujauzito hadi kufika hatua ya kujifungua, kuliko anayetoa mimba maana huyu anakuwa amefanya makosa mawili kwa wakati mmoja.”

Anabainisha kuwa, kimsingi yeye hasemi kwamba kubeba mimba nje au kabla ya ndoa si kosa, bali anapendekeza kuwa ni vema wanafunzi wanaopata mimba watengewe shule maalumu ili pia, Serikali na jamii kwa jumla wajue namna ya kuwasaidia hata kama ni kurudia mwaka wa masomo.

 Bibi Revina Chiduo, mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, anasema kuwa yeye kama mzazi amebaini mambo mengi ambapo alisema baadhi ya wazazi huwapa watoto wao vidonge vya kuzuia mimba hali ambayo wakati mwingine huwasababishia ugumba na kuchochea dhambi ya uzinzi ambao ni chanzo kikubwa cha kuenea kwa UKIMWI.

Anasema wakati mwingine hali hii ya ugumba huchangia kwa asilimia kubwa uvunjikaji wa ndoa pindi wanapoolewa.

“Unajua mwanaume anapooa mwanamke, matarajio makubwa huwa ni kupata mtoto na ikitokea matarajio hayo yakawa kinyume, kinachofuatia ni kuvunjika kwa baadhi ya  ndoa,” anasema.

Anasema wazazi wa namna hiyo hulazimika kufanya hivyo ili kuepuka hasara ya kupoteza pesa zao inapotokea watoto wanao wasomesha wakabeba mimba.

Anasema ni kweli pengine utaratibu wa kuwarudisha wanafunzi shuleni baada ya kujifungua, utawezesha kupunguza matumizi ya vidonge kwa wanafunzi.

Hata hivyo msimamo wa madhehebu mbalimbali ya kidini ni kwamba mtu akishiriki tendo la ngono kabla ya ndoa ni uasherati na mimba zisizotarajiwa kwa wasioolewa ni matokeo ya uzinifu.

Katibu Mtendaji wa Idara ya Elimu katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Elias Msemwa, yeye anasema kuwa, kubeba mimba ni roho ya mtu, hivyo akasisitiza jamii isiwazalilishe wasichana kwamba kubeba mimba wakiwa mashuleni ni sehemu ya maisha yao.

Alisema kuruhusu wasichana hao wanaobeba mimba wakiwa shuleni waendelee na masomo baada ya kujifungua, ni sawa na kuwaondoa woga na kuwapa ujasiri wa kuzini bila hofu ya magonjwa ya zinaa wala kupoteza masomo.

 “Kinachotakiwa ni kujilinda na kujiheshimu huku wakizingatia masomo yao,” anasema.

Alishauri Serikali kutilia mkazo sheria ya kuwabana wavulana wanaohusika kuwapa mimba wanafunzi kwa kuwapa adhabu kali.

“Suala ni kuangalia jamii inawatendea nini wale wanaowapa mimba wanafunzi. Ufumbuzi wa tatizo uwe kuwapa adhabu kali, bila kujali kama anayehusika ni mwalimu, mwanafunzi mwenzake ama raia wa kawaida,” anasema Padre Msemwa.

Kwa upande wa wale wanafunzi wanaobakwa na kupata ujauzito, anasema ipo haja jamii iangalie namna ya kuwasaidia kuendelea na masomo na hii ifanyike baada ya kuthibitishwa kisheria kwamba kweli huyo mwanafunzi alibakwa.

“Sikatai, kuna wale wanaopata ujauzito kwa kubakwa ambacho ni kitendo cha kinyama. Ikitokea ikathibitishwa kisheria kwamba ni kweli mwanafunzi huyo alipata mimba kwa kubakwa, basi jamii iangalie namna ya kumsaidia ili aendelee na masomo,” anasema.

Anasema elimu pekee ndiyo itayomsaidia mwanafunzi wa namna hiyo kutoka katika unyonge atakao kuwa nao baadaye,”anasema.

Akaongeza, “Sasa sijui  Sheria ya kuruhusu wanafunzi wanaobeba mimba na baada ya kujifungua waendelee tena na masomo kama itapitishwa, kutakuwepo na shule maalum kwa ajili ya wanafunzi wa namna hiyo ama watachanganywa na wanafunzi wa kawaida? Kama watachanganywa, je wanafunzi hao wa kawaida watakuwa na mtazamo gani, watajifunza nini?” Alihoji.

Aidha, alisema bila shaka sheria hiyo hata kama itapitishwa, wanafunzi wa namna hiyo ni vigumu kufanya vizuri katika mitihani yao ya mwisho kwani wengi wao watakuwa wanawawazia watoto wao waliowaacha nyumbani.

“Kwa kweli hii itazidi kuwakandamiza wanafunzi wa kike kwamba hawafanyi vizuri katika taaluma kwani izingatiwe kuwa wengi wa wanafunzi hao wanakuwa bado hawajakomaa kiakili,” anasema.

Hivi karibuni Wizara ya Elimu na Utamaduni  iliwasilisha katika Bunge, muswada wa kutaka wanafunzi wa kike wanaobeba mimba wakiwa mashuleni, waruhusiwe kuendelea na masomo baada ya kujifungua.

Hata hivyo mswada huo utajadiliwa katika kikao cha Bunge kitakacho anza hivi karibuni.

Sasa, Rose ni kiwakilishi cha wasichana wengi ambao maisha yao yameharibika kutokana na kupata mimba wakiwa shuleni.

Ukweli ni kwamba wapo wengine wanaopata hali hiyo kwa kubakwa na wengine kupata vishawishi kutoka kwa ama kwa walimu wao, wanafunzi wenzao au raia wengine.

Sasa tujiulize, je adhabu hii ya kuwafukuza shule wanafunzi wanaopata mimba, itaisadia jamii kupambana na tatizo lililopo, au itaongeza tatizo lingine la umaskini, ongezeko la watoto wa mitaani na kasi ya maambukizi ya UKIMWI?

Hivi sasa ulimwengu mzima unapambana kumkomboa mwanamke, dhidi ya unyamyaswaji wa aina zote, sasa, hili linatazamwa vipi na jamii?

Kumuachisha masomo mtoto wa kike kutamkomboa au ndio hukumu ya kummaliza yeye na maisha yake yote sambamba na vitegemezi vyake?

Ingawa kuna haja ya kuwaadhibu hata wanaowapa mimba wanafunzi, bado hili litekelezwe kwa uchunguzi wa kisayansi na kisheria kwani upo uwezekano wasichana wanaopata mimba shuleni, wakawabambikia watu wasio husika kabisa na kuwaacha wahusika halisi.

Kama kweli Serikali ina nia dhabiti ya kumkomboa mwanamke,si vibaya ikiweka utaratibu wa kuwarejesha masomoni wanafunzi hao baada ya kujifungua. Hususan waliopata mimba hizo kwa njia za kinyama.

Ili jambo hili lifanikiwe, ni lazima kutenga madarasa ama shule kwa ajili ya wanafunzi wa namna hiyo badala ya kuwachanganya na wanafunzi wengine wasio katika mkumbo huo.

Kufanya hivyo kutawawezesha wahusika wa pande zote mbili kutoathirikika kisaikolojia, kijamii, kimaisha na kiuchumi na kikubwa zaidi, elimu ya kuzingatia mafundisho ya dini ipewe kipaumbele shuleni ili wanafunzi waishi kwa kufuata maagizo ya Mungu.

Juhudi za pamoja zinahitajika ili kuzuia mlipuko wa mimba kwa wanafunzi hivyo, walimu, walezi wote katika jamii, wazazi na viongozi wa dini waunganishe nguvu kukemea vitendo vya kujamiiana shuleni, hii itasaidia watu kumtii Mungu, na pia kuepuka mimba ovyo pamoja na janga la UKIMWI.

Hata hivyo, aliyefikwa na janga hilo, asitengwe wala kugeuzwa kuwa kisiwa katika jamii, bali upendo wa kweli uonekana sasa na asaidiwe ili asirudie kosa, wengine wajifunze toka kwake, na asaidiwe namna ya kuishi na mimba na hatimaye mwanaye.

Hii itaepusha uwezekano wa wasichana hao kujiua, kutoa mimba  kutupa watoto na kuwafanya watoto wa mitaani waongezeke sambamba na ongezeko la maambukizi ya UKIMWI.

 

Nionavyo Mimi

Na David Mpangile

WAKIWA wabatizwa kwa namna ya pekee daima Walei wanaitwa ‘kuyatakatifuza malimwengu’ yaani mfumo mzima wa maisha ya mwanadamu, siasa, biashara, sayansi, elimu, uchumi, michezo na vifananavyo na hivyo ili vimsaidie mwanadamu kuutunza uhusiano wake na Mungu.

Lakini, mifumo ya maisha ya mwanadamu hubadilika kwa wakati. Leo tuko katika ulimwengu wa utandawazi hata kama ufahamu wetu wa nadharia nzima ya utandawazi unatofautiana.

Hivyo, wajibu na wito wetu leo ni kuutakatifuza ulimwengu wa utandawazi.

Utandawazi una tabia na sifa ziwezazo kujaza kurasa na kurasa kwani unagusa kila nyanja ya maisha. Lakini, tuzungumzie tabia moja ambayo kwa fikra zangu, ina taahira kwa watoto na vijana wa sasa wa Kikristo.

Hii ni sifa ya muuingiliano na uhuru wa kupata na kutoa habari. Na hapa si uhuru tu, bali uharaka na uwezekano wa kupata habari hizo za leo leo, kuliko wakati mwingine wowote. Katika kipindi kifupi sana, mtoto anaweza kupata habari aitakayo kutoka pembe yoyote ya dunia; tena kwa kasi inayostajabisha na inayoifanya dunia kweli istahili kuitwa kijiji.

Kwa upande wa wasambazaji habari, yaani vyombo vya habari na watoa matangazo ya biashara,  wanafanya jitihada ya kila aina kuhakikisha habari zao zinamfikia mlengwa kwa gharama yoyote ya ushawishi.

Mwisho wa siku, mtoto au kijana anajikuta katika wasiwasi na fujo kubwa, habari zikimiminika huku zingine zikipingana zenyewe kwa zenyewe, zingine zikipinga imani yake, lakini zingine zikiichochea na kuiimarisha.

Hapa, cha msingi kukumbuka ni kushambulia. Hili linamkuta katika kipindi anachoanza kujenga uwezo wa kuamua mambo.

Hebu angalia ni aina gani ya filamu na programu zilizojaa katika televisheni au programu katika mtandao wa kumpyuta (tovuti) website na matangazo ya biashara.

Geukia magazeti na riwaya pia, picha zinazobeba kurasa za mbele zinavyoonekana, utaona ni kwa kiwango gani zinaweza kuharibu malezi ya mtoto na hata kutia donda katika makuzi ya mtoto.

Lakini, jambo moja lenye kutia moyo ni ukweli usiokanika siku zote kuwa,  hakuna jambo lolote lililo baya au zuri pekee. Kila jambo lina upande wa pili na ni wajibu wetu katika mazingira hayo ya mlipuko wa habari na kuangalia upande wa pili wa sarafu yaani, uzuri wa mfumo huu wa mawasiliano au sahihi zaidi tunawezaje kuufanya usaidie malezi.

Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba vyombo vya habari vitaendelea kuwepo na kila kimoja kikiwa na ajenda yake.

Ni kama ulimwengu. Bwana Wetu Yesu Kristo akifahamu kuwa ulimwengu una mazuri na mabaya yake, alituombea, ‘Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu, bali uwalinde na yule mwovu’ (Yoh. 17 :15).

Njia moja ya kumfanya mtoto akabiliane na msukosuko wa habari ni kumuonesha habari na vyanzo vya habari vyenye kumjenga na pia, kumfanya apende kuvitafuta na kuvifurahia.

Mfano ; katika televisheni na redio, kuna vipindi vyenye kujenga watoto kimadili, je tunawahimiza kuvitazama na kusikiliza au tumeamua kuwaacha watumie busara yao changa kuamua kiwafaacho huku tukilalama kuwa watoto wa siku hizi hawapendi vipindi hivyo, watapendaji kama hawapati msukumo wa kifikra toka kwa wazazi na walezi wao ?

Kuna mikanda mingi  ya video inayoweza kumfunza mtoto, mingine si lazima iwe ya dini moja kwa moja, lakini ina dhamira zenye kumchangamsha mtoto na wakati huo huo, kumpa mafunzo mbalimbali ya maisha. Tunayo hii ?

Hivyo hivyo, kwenye tovuti kuna tovuti nyingi tu, zenye habari za Kanisa, maadili na habari zenye kuelimisha.

Tunajisumbua kuzitafuta na kuzipitisha kwa watoto wetu ili waendapo kwenye ‘internet cafe’ zilizojaa kama uyoga wasijikute hawana cha kufanya na hivyo, kuangukia kuangalia tovuti za ‘ajabu ajabu’ na zenye kushambulia malezi na dhamira zao. 

Na Magazeti : ni aina gani ya magazeti kama wazazi tunayaleta nyumbani, je tunawahimiza kusoma magazeti yenye kuimarisha imani zao ? Tunawahimiza pia kusoma vitabu mbalimbali vya dini ambavyo kwa kweli ni vingi na vya aina mbalimbali, au hata vyenye kuongeza maarifa pasipo kusababisha mmomonyoko wa maadili ?

Njia ya pili ni kuwa karibu na mtoto na kujadiliana nao kuhusiana na habari mbalimbali alizoona, kusoma au kusikia kwa sababu ingawa utamuelekeza asome vitabu vizuri, asikilize vipindi vizuri na atazame vipindi vizuri, hapa na pale atajikuta akisoma kitabu au programu ambayo ni mchanganyiko kwani nyingine kwa ndani, zitakuwa na sehemu zenye kumkwaza.

Ni vema katika matukio kama hayo, kuzungumza na mtoto na kuielekeza akili yake ili aione nia njema ya mwandishi au mtayarishaji wa kipindi na kuona anaweza kujifunza nini katika mchanganyiko aliokumbana nao.

Endapo leo utamwezesha mtoto kuona zuri katika mazingira hayo, ni wazi kesho ataendelea kusoma kitabu chake cha riwaya hata kama kurasa moja au mbili zinamuelekeo tofauti, atazipuuza tu, na kuendelea na riwaya yake.

Hii ni kwa sababu sasa atakuwa anajua siku zote kuupata mchele hata kama utachanganyika na chuya nyingi. Si amelelewa hivyo na anamaarifa na mang’amuzi ya kuliona jema miongoni mwa mabaya !

Watoto wanapaswa kujenga tabia ya kupenda vitu viwajengavyo kwani tabia hii ikijengeka ndani yao, inakuwa rahisi kuamua kwa busara nini cha kutazama, kusoma na kusikia na nini cha kupuuza na kuepukana nacho kabisa.

Dhana kuwa watoto na vijana wa siku hizi hawapendi programu zenye maadili, haina ukweli wowote.

Tatizo lililopo ni kuwa watu hawawafanyi waone programu za maadili kuwa zinaweza kuwafurahisha, kuwanufaisha na si kitu cha huzuni wala ugoigoi.

Mwezi uliopita nilibahatika kuangalia mfululizo wa vipindi vya maadili kwenye televisheni. Baadaye, nikaona nijaribu kumshauri rafiki yangu aangalie na nione kama atavipenda.

Alivipenda na akawa kila inapofika siku ya kipindi, ananitumia ujumbe kuniambia anaangalia (ilikuwa njia ya kunikumbusha nami niangalie).

Hapa, jambo moja linalohitaji ufafanuzi ni kuwa, kwa kusisitiza umuhimu wa kusoma vitabu vya dini, simaanishi mtoto asome vitabu hivyo tu kwani kufanya hivi kungekuwa sawa na kujichanganya mwenyewe maana nimesema kwenye ibara ya kwanza kwamba tunaitwa kuutakatifuza mfumo mzima wa maisha, tutawezaje kama hatuna maarifa ya kutosha juu ya mambo ya kidunia ?

Hivyo, kijana anapaswa pia kubobea katika maandishi na elimu yoyote itakayomfanya akili yake itawale mazingira kwa faida yake na ulimwengu wa wanadamu.

Sikuhitaji kuelezea sana hili kwa sababu si msingi wa makala hii. Makala hii inalenga katika umuhimu wa kuamsha nia na ari ya kusoma maandishi yenye maadili na  yanayojenga imani sahihi katika jamii.

Tuwaongoze watoto na vijana wetu katika wimbi hili la habari. Wanasema karamu inaua kuliko risasi.

Tunasema hivyo huku tukijiuliza kuwa ni mara ngapi maandishi yasiyo makini katika vyombo vya habari yamesababisha hata jamii kuambukizwa UKIMWI baada ya kushawishika na vitu vilivyoandikwa katika magazeti na kuingiwa tamaa ambayo ni hatari kiroho na kimwili ?

Ni mara ngapi watoto wametazama picha katika video na luninga ambazo zimewapa mwamko wa kufanya mazoezi ya kupigana teke, ujambazi na namna ya kupigana kwa bunduki ? Jamii inakwenda wapi kama tunawanunulia watoto wetu sanamu za bunduki !

Ni mara ngapi watoto wameona kwenye luninga au kusoma magazeti yanayowachochea na kuamsha hisia za kushiriki uovu wa aina yoyote ukiwamo uchochezi unaohatarisha usalama wa taifa ?

Bila shaka ikichanganyika na aina nyingine ya mawasiliano kama magazeti, tovuti na luninga, kalamu inaua zaidi na hasa dhamira ya mtumiaji kalamu ikitolewa na kutumika vibaya.

Ikiwa ‘kipofu akimuongoza kipofu mwenzake wote wanatumbukia shimoni’ itakuwaje akikosa kabisa hata kiongozi ?

Ni vema karamu zetu zitumike kuunganisha jamii ili kujiletea maendeleo ya kiroho kwa kushiriki uinjilishaji, maendeleo ya kimwili na kujenga mshikamano na umoja wa kitaifa katika jamii na pia, kujenga jamii safi na adilifu.