Kwanini watu huogopa maiti, makaburi, chumba na nguo za marehemu?

l Wanawake na watoto wanaongoza

l Mawe yana maana gani juu ya kaburi?

Na Joseph Sabinus

WATU wengi huogopa kupita katika maeneo ya mskaburi hususan nyakati za usiku. Wengine wakiogopa kulala chumba chenye maiti au hata mahali ambapo mtu fulani alifia.

Robi Mashauri na Mdogo wake Shida (20) wa Sabasaba Tarime, walikataa katakata kuingia katika chumba chao kwa kuwa mwili wa mmoja wa wapangaji wao, Mariamu Nyangarya, aliyefariki kutokana na ujauzito katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, ulikuwa katika mojawapo ya vyumba vya nyumba wanayoishi.

Kila walipotaka kuingia ndani, walilazimika kukusanyana na wadogo zao, wakawasha taa na kuingia kwa pamoja wakiwa kundi kubwa.

Philotea Temu (26), mkazi wa Kinondoni Dar es Salaam, anasema, ‘Baba alipofariki tulipeleka maiti nyumbani kwetu huko Moshi kwa mazishi, lakini sisi tulitangulia kurudi ili tuendelee na masomo na mambo mengine ya nyumbani.’ ‘mama alituagiza tukifika nyumbani, tutoe vitu vyote kwenye chumba cha marehemu baba ili tufanye usafi, lakini tulipofika huku nyumbani (Dar), wote ; mimi na ndugu zangu watatu tulibaki kutupiana ingia wewe ; ingia wewe na mwishowe, wote tukataa kabisa hadi mama aliporudi baada ya wiki.’

Anaongeza, ‘Unajua kama mimi huwa ninajihisi kuwa labda nitakutana na marehemu huko ndani na kwamba huenda alikuwa ananipenda sana hivyo, atataka tukae nae pamoja, hapo ndani, au atataka twende naye katika makao yake mapya na ya milele.’

Kwa mujibu wa mmoja wa vyanzo vyetu vya habari ambaye hakutaka jina lake litajwe, kaka yao alipofariki dunia mwezi Julai mwaka huu, ndugu wengine walikubali kurithi chochote cha kaka yao walichopangiwa lakini mmoja wa ndugu zao ambaye ni wa kiume, aligoma kabisa kupokea shati na suruali zilizokuwa sehemu ya urithi wake, kwa mujibu wa kabila la Wakabwa.

Anasema hata baada ya wazee kuingilia kwa nguvu na kumuonya kuwa alikuwa anavunja mila kwa kuwa kitu cha marehemu hakikataliwi kupokewa na kwamba jamii ingemtazama kama aliyefurahi ndugu yao kufariki ili baadaye alirithi vitu vya thamani, alipokea, lakini baada ya muda mfupi kuwa na mavazi hayo bila kuyavaa, vitu hivyo havikuonekana tena wala hakuwa tayari kufafanua kwa yeyote kuwa vilikwenda wapi.

Wao waliofikiri kuwa labda aliuza ili kuganga njaa na wengine, walifikiri kuwa ametupa mradi tu, hakuna aliyekuwa na uhakika bwana huyo kapeleka wapi nguo hizo.

Hii tuliyoitaja, ni baadhi tu ya mifano kwani ni wazi kuwa baadhi ya watu hushindwa kulala peke yao baada ya kuona maiti.

Uchunguzi uliofanywa na KIONGOZI kwa nyakati tofauti katika misiba minane jijini Dar es Salaam hususan wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa marehemu, ulibaini kuwa wanawake watatu hadi wanne kati ya wanane, wanaopita mbele ya marehemu kutoa heshima za mwisho, hukwepa kuangalia sura ya marehemu huku wakiangali chini ama pembeni .

Ukabaini kuwa wanaume wanne hadi sita, kati ya wanane wanaopita mbele ya mwili wa marehemu kwa heshima za mwisho, humudu kuiangalia sura ya marehemu japo kwa muda mfupi huku uchunguzi huo ukibaini kuwa, wanaume wawili tu, kati ya hao wanane, hupita wakiwa wameangalia chini au bila kupinda kuangalia mwili wa maremu.

Hii ina maana kuwa hupita wakiwa wameangalia mbele.

Uchunguzi huo usio rasmi, ukabaini kuwa watoto kati ya miaka mitatu hadi mitano hivi, huwa hawaogopi kupita mbele ya marehemu, bali huogopa macho na mkusanyiko wa watu hivyo, wengine hukataa.

Hata hivyo, ukagundua kuwa wanapoona maiti na kisha mazishi yakafanywa, ndipo hutambua kuwa wamempoteza mpendwa wao.

Wengi hujikuta wakiwa na upweke mkali kwa vipindi kadha wanavyowakumbuka marehmu na kisha wakifarijiwa kwa namna fulani, ni wepesi kusahau tena.

Iligundulika katika uchunguzi huo kuwa, watoto zaidi ya mika mitano na chini ya 12, huogopa zaidi kuona mwili wa marehemu ingawa wengine hupenda kuona ili wapate namna ya kusimulia watakapokutana na watoto wenzao.

Na hao, sio rahisi kupita katika maeneo ya makaburi peke yao. Wengi, huamini kuwa nyakati za jioni au usiku, mizimu na mshetani mbalimbali hutembelea maeneo ya makaburi na wafu wengine, kutoka na kukaa juu ya mawe yaliyojengewa makaburi hayo.

Kwa ufupi, uchunguzi huo usio rasmi ulibainisha kuwa watoto huongoza kwa kuogopa wafu wakifuatiwa na wanawake, bila kujali umri.

Afisa nayeshughulikia mambo ya uhamiaji katika baraza la maaskofu Katoliki tanzania TEC, Bw. Steven Msowoya, yeye anasema, ‘Nimeona na kusikia wengine wakisema mimi sipiti hapo au siwezi kuingia humo alimokuwa maiti. Wanadai wanakuwa kama wanamuona marehemu akiwa hai na akiwatokea machoni. Hali hii inategemea zaidi umri na malezi aliyokulia mtoto.

Kama amekulia katika malezi ya kuogopaogopa vitu, inamuwia vigumu sana na ndiyo maana wengine hasa wasichana naweza kumtishia kwa jongoo akakimbia na kulia sana, lakini wengine ni shupavu kutokana na malezi aliyokulia, unaweza kumuona mtoto wa miaka kumi akipambana hadi kumuuua nyoka.’

Msowoya anaongeza,  "Pengine wanaokuwa waoga sana, huenda mama zao wakati wakiwa wajawazito, walikuwa waoga, hivyo wakawarithisha uoga tangu tumboni mwao.’

Hata hivyo, kwa sababu za kisaikolojia, si vema kuwashirikisha watoto wadogo kuona au kuugusa mwili wa marehemu maana kumbukumbu hiyo itadumu kichwani . Lakini, licha ya maelezo yote hayo, hebu muulize yeyote kati ya watu wenye woga huo kwamba, huwa anaogopa nini hasa.

Ni dhahiri hakuna anayeweza kukueleza sababu inayoingia akilini.

Dk. Dafrossa Lyimo, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Amana, Ilala, jijini Dar es Salaam, anasema, hali ya kuogopa maiti, makaburi vyumba na baadhi ya vitu vya marehemu, inatokana na hisia za kibinafsi na ukaribu wa kinasaba uliopo baina ya mtu huyo na marehemu.

‘Jambo hili linahitaji wataalamu wa mambo ya kisaikolojia, kwa sababu kila mtu anahisia zake na ndio maana hata madaktari, wapo wengine wanaoogopa kumpasua chura, lakini wanaweza kumpasua binadamu bila tatizo,’ alisema.

Akaongeza, ‘ …Hii haiwapati watu wote maana wengine wanaweza kufiwa, wakafumba macho na mdomo wa maiti na pengine hata kubeba wenyewe ndiyo maana nasema inategemea pia, uzoefu katika mambo kama hayo. Mfano, walioshuhudia mauaji ya Rwanda na Burundi, ataogopa maiti ?’

Naye Dk. Nargis Simmons, Mtaalamu wa Mambo ya Kisaikolojia, katika Kituo cha Mental Health Resource Center, kilichopo ndani ya eneo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema hali ya kuogopa mazingira yoyote ya kifo, inatokana na hisia alizokuwa nazo mtu tangu akiwa kadogo hasa kama akiwa mdogo alikuwa anatishiwa juu ya mambo ya vifo.

Dk. Nargis anasema, mila zilizopo katika jamii, zinachangia mtu kukua akiwa na fikra fulani kichwani, kuwa kama hili likiwa hivi, hili linaweza kutokea na hii mara nyingi ilikuwa ni mbinu iliyotumika katika jamii kuzuia baadhi ya mambo ambayo hayakutakiwa hivyo, fikra hiyo ikarithiwa toka kizazi hadi kizazi.

Hata hivyo, mwanasaikolojia huyo, alisema hajawahi kuona utafiti maalumu juu ya sababu hasa za watu kuogopa kifo na mazingira yanayoendana na msiba.

‘Wengine walikuwa wakisimuliwa au kutishiwa wakiwa watoto kuwa ukifanya hivi, wafu watakutokea na kukuchukua, hivyo wazo hilo la hofu linakuwa gumu kubanduka kichwani, na inapotokea msiba, basi anakumbuka na kupatwa na hali hiyo ya woga, ‘ alisema.

Akaongeza, ‘Jamii nyingine zimekuwa zikiwatishia watoto kuwa ukiongopa, wafu watakuja kukuchukua, sasa anakumbuka akilini pengine hata bila yeye mwenyewe kujijua kuwa, aliwahi kuongopa, hapo ndipo hofu humpata.’

Akatoa mfano zaidi kuwa, ‘Makabila mengine yana mila kuwa mtu mzima kama baba yako akifariki, lazima umzike kijijini ; wanasema ukimzika mjini, mizimu itachukia na kukufanya vibaya, wanaweza kusema usipofanya hivyo, marehemu baba (ndugu) yako, utakujia. Sasa, hata akilazimika kumzika sehemu nyingine, halafu likatokea tatizo la kawaida tu, anakumbuka kuwa alivunja miiko kwa kumzika baba yake mjini badala ya kijijini kwao. Hofu hiyo hivyo anairithisha kwa jamii nyingine inayomzunguka kupita masimulizi na mazungumzo’

Kitabu cha CORE PSYCHIATRY, kilichaoandikwa na James V Lucey,  Uk.201, kinasema, kuwa kibailojia, sababu za hofu hizo hazijulikani.

Hata hivyo, woga huo basi ndio ulio asili ya watu kuweka mawe makaburini. Lakini je, ilianzaje ?

Katika jamii zenye utamaduni huo yakiwemo maeneo ya Mashariki ya Kati watu waliweka mawe katika makaburi wakihofu kuwa wafu wangeweza kutoka humo hata baada ya kuzikwa na kuleta madhara kwa walio hai. Hivyo, wakijaribu kujihakikishia usalama wao, ndipo walipoamua kuweka mawe mazito katika lango la kaburi ambalo waliamini kuwa, marehemu hawezi kulisogeza na kutoka.

Ukiuliza juu ya lini utamaduni huu ulianza, jibu litakuwa zaidi ya miaka 2000 iliyopita kwani kule kuwekwa jiwe kubwa katika mlango wa kaburi la Yesu Kristo, nje ya mji wa Yerusalemu katika Kilima cha Golgotha, kunathibitisha hivyo.

Mwanzoni, watu walizikiwa popote; mara nyingi katika au karibu na maeneo walikofia au kuuawa.

Makaburi yalizagaa hata katika maeneo ambayo leo hii usingewazia yawepo.

Baadhi ya watu wa kale waliona maiti kama kitu cha kutisha mno, kiasi kwamba kuigusa au hata kupita eneo lenye kaburi kwao ilikuwa kama nuksi.

Kwa sababu hiyo, waliyatia makaburi alama kwa kuweka mawe ili yaonekane na kutambuliwa mapema na mpita njia.

 Hiyo, ilifanywa kama alama ya onyo kwa wapitaji wasije wakasogelea kile walichoamini kuwa kinaweza kuwa balaa lingine kwa jamii.

Pia, ili kuyafanya mawe hayo ya tahadhari yaonekane kwa uwazi zaidi, mara nyingi yalipakwa chokaa.

Hatimaye wazo la kuweka makaburi katika eneo moja lilianza na ndipo maeneo maalum yaliyo mbali na makazi ya watu yakatengwa kwa maana ile ile ya kuwaweka wafu mbali na walio hai kwa ajili ya usalama.

Katika hatua juu ya kukua kwa woga wa walio hai kwa wafu, pole pole mtindo wa kuyaabudu makaburi ulianza.

Jiwe juu ya kaburi liliwakilisha nguvu za kiungu au za mzimu wa aliyeabudiwa na hii huenda ndiyo inayotumika kama njia ya kuwaomba radhi marehemu ili wasifanye mabaya katika jamii.

Katika wakati huo, watu hawakuhofia tena sana makaburini, bali waliweka mawe makubwa ili kuzuia wanyama wasiyaharibu makaburi hayo na kufukua miili ya marehemu.

Maelezo juu ya mawe ya makaburini ni jambo lililofuata baadaye kuonesha vyeo na hadhi ya marehemu na hivyo, kuwafanya wapita njia waziombea roho za marehemu hao.

Wengi wetu tumekuwa tukisoma tu juu ya kuwekwa huko kwa jiwe kaburini, lakini hatujui utamaduni huu wa kuweka mawe kaburini ulitoka wapi.

Hebu sasa tuangalie machache kuhusiana na utamaduni na sababu za kijiografia za matumizi ya mawe na mimea juu ya kaburi.

Kwa mujibu wa masimulizi, wakati Mtoto wa Adamu, Abel, alipomuua mdogo wake, Kaini, hakujua amfanyeje zaidi wala ampeleke wapi.

Kama ishara ya kumuongoza la kufanya, wakatokea kunguru wawili wakipigana, mmoja alipofariki, kunguru mmoja alichimba chini kwa kucha zake na kisha kumfukia kunguru aliyefariki.

Baadaye, kunguru yule mzima akatumia mdomo wake kuchukua kijiti na kukichomeka alipofukia.

Huo ukawa mwanzo wa kukumbuka sehemu kilichowekwa kitu kilichokufa ili pasisahaulike.

Lakini, huko Mashariki ya Kati, kulikuwa na mchanga mwingi hivyo, mvua iliponyesha, uliondoka kirahisi na hata kutokana na upepo, iliwezekana kabisa kuwapo shimo.

Inaelezwa kuwa, kutokana na mabadiliko hayo ya kijiografia, ndipo ikajitokeza haja ya kuweka mawe kwani hayakuwa rahisi kuhamishwa na maji ya kawaida au upepo.

Baadaye, kadiri maendeleo yalivyozidi, ndipo watu wakaanza kujenga makaburi kwa kutumia saluji, kuandika majina na hata kuweka alama kama msalaba ili kutofautisha dini.

Hata hivyo, bado mawe yana maana tofauti hadi sasa toka jamii moja hadi nyingine.

Mfano, kwa Kabila la Wasukuma, mawe huwekwa katika kaburi la mtu aliyeacha uzao yaani aliyeacha watoto watakaoendeleza ukoo wake.

Aidha, mimea inayostahimili ukame kama minyaa, kupandwa kaburini huashiria umilele wa kukumbukwa kwa marehemu.

Hata hivyo, ni vema kutambua kuwa, mtu akisha kufa, amekufa; amekwenda moja kwa moja; ameitwa na Mungu.

Imani za kuogopa makaburi, maiti na hata mali halali za marehemu kwa imani zisizo za kitaalamu hazina maana.

Ni vema jamii itambue kuwa imani hizo zinaweza kutumiwa na wachache wakiwamo matapeli na walaghai wanaopiga ramli ili kuwaibia watu pesa zao.

Vitu kama mawe au mimea katika ulimwengu wa sasa, hutumika kuepusha usahaulifu wa mahali kaburi lilipo endapo litakaa muda mrefu huku likinyeshewa mvua na kuwapo uwezekano wa kutawanyika.

Ujenzi wa makaburi na matumizi ya mawe na mimea ni kumbukumbu ya jamii kwa ndugu yao aliyefariki.

Vatican yataka utafiti wa viinitete vya binadamu upigwe marufuku (2)

l "Ni kashfa dhidi ya thamani ya mtu"

 l  Califonia yakiuka sera ya Bush, yahalalisha utafiti huo

Na Eric Samba

Inatoka Toleo lililopita

 

Alisema kuwa Vatican inaunga mkono ule utafiti juu ya seli shina zenye asili isiyo yakibayolojia kwa kuwa njia hii kama ilivyoonyeshwa na mafunzo ya kisayansi ya hivi karibuni, “hii ni njia nzuri, inayotia matumaini na njia ya kimaadili ya kupata misuli ya kupandikiza pamoja na matibabu ya kiseli ambayo inaweza kuwafidia wanadamu.

Kama Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alivyosema, “katika tukio lolote, njia za kisayansi zinazoshindwa kuheshimu thamani ya binadamu na tunu ya mtu-nafsi lazima ziepukwe daima.

Ninafikiria hasa juu ya majaribio ya utafiti wa viinitete vya binadamu kwa lengo la kupata viungo vya kupandikiza: utaalamu huu kadiri unavyohusisha kuchezea na kuharibu viinitete vya binadamu, hauwezi kukubalika kimaadili, hata pale lengo lake linapokuwa jema katika lenyewe.”

Aidha Baba Mtakatifu anaendelea kusema,”Sayansi yenyewe inaonyesha kuwa zipo njia nyingine za utabibu ambazo zinaweza kufikia malengo husika bila kuhusisha viinitete, lakini kwa kutumia seli shina kutoka kwa watu wazima.

Huu ndio mwelekeo ambao utafiti unapaswa kufuata iwapo unataka kuheshimu thamani ya kila mtu, hata yule ambaye bado yupo katika hatua ya kiinitete.”

Askofu Mkuu Martino aliendelea kusema kuwa uunganishaji wa viinitete kwa ajili ya utafiti wa kibayolojia na kitabibu au kuzalisha seli shina vyote huchangia mashambulizi dhidi ya thamani na ukamilifu wa mwanadamu.

Alisema kuwa kustawisha kiinitete cha binadamu wakati mipango ya kukiangamiza inafanyika, kungeanzisha uharibifu wa makusudi wa uhai wa binadamu anayetarajiwa kwa kisingizio cha “uzuri” usiojulikana wa utabibu tarajiwa au ugunduzi wa kisayansi.

 Aidha alisema kuwa jambo hili linachukiza watu wengi hata wale wanaopigia debe maendeleo ya kisayansi na utabibu.

Alisema uunganishaji wa viinitete huzalisha uhai mpya wa binadamu usioelekezwa kwenye ustawi wa baadaye wa mtu bali kwa utumiwaji na uharibifu, ni mchakato ambao hauwezi kuhalalishwa kwa sababu kwamba unaweza kusaidia wanadamu.

Pia Mhashamu Martino alisisitiza kuwa uunganishaji wa viinitete hukiuka vipengele muhimu vya haki za binadamu.

Alisema “tangu mwaka 1988, migawanyiko miwili ya ulimwengu imekua zaidi: wa kwanza ni umaskini na unyanyasaji wa kijamii, na mwingine unahusu watoto wasio zaliwa bado ambao wamefanywa kuwa vyombo vya majaribio ya kisayansi na kiteknolojia.”

Aliongeza “hapa kuna hatari ya kuwa na aina mpya ya ubaguzi, kwa kuendeleza mbinu hizi ambazo zinaweza kupelekea uumbaji wa watu wa kiwango cha nusu mtu, ambao kimsingi hulengwa kutumiwa na watu wengine.”

Alisisitiza kuwa “hili lingekuwa muundo mpya na wa kutisha wa utumwa. Kwa masikitiko, kishawishi cha kukiuka maadili bado kipo, hasa pale maslahi ya kibiashara yanakapojiingiza. Serikali na jumuiya ya kisayansi ni lazima iwe macho katika eneo hili.”

Wakati hayo yakiendelea, katika hatua ambayo inapingana na sera ya utawala wa Rais George W. Bush, jimbo la California nchini Marekani limeridhia sheria mpya inayolenga kufungua milango kwa watafiti wa seli shina za binadamu.

Gavana Gray Davis, alitia saini sheria hiyo kuruhusu utafiti wa namna hiyo kufanyika, utafiti ambao umekuwa ukipingwa vikali na makundi pinzani dhidi ya utoaji mimba pamoja na Kanisa Katoliki kwa sababu utafiti huo unahusisha matumizi ya mimba changa pamoja na viinitete.

Suala hilo lilitawala vyombo vya habari zaidi ya mwaka mmoja uliopita pale Rais Bush alipokataa kutoa fedha za walipa kodi kugharimia utafiti wa seli shina za viinitete vya binadamu.

Hata hivyo, waungaji mkono wa sheria hiyo ya California wanasema kuwa hatua hiyo itavuta wanasayansi ambao siku fulani wanaweza kufanikiwa kutibu magonjwa sugu kwa njia ya utafiti huo.

 Waungaji mkono wa sheria hiyo ni pamoja na Christopher Reeve, ambaye amekuwa mwanaharakati wa utafiti huo tangu alipopata ajali na kupooza kuanzia shingo kwenda chini.

Reeve anaamini kuwa utafiti huo unaweza kusaidia kutibu ugonjwa wa kupooza unaomsumbua.

“Tangu seli shina za binadamu zilipotenganishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1998, mdahala wa kisiasa umekuwa na athari kwa wanasayansi,” alisema Reeve na kuongeza “inaumiza kutafakari kwamba ni hatua gani ambazo zingekuwa tayari zimepigwa iwapo utafiti huo usingezuiwa.”

Seli hizo ambazo hupatikana katika viinitete vya binadamu, ‘umbilical cords’ na ‘placentas’, zinaweza kugawanyika na kuwa aina yoyote ya seli katika mwili.

Wapinzani wa utafiti huo wanadai kuwa utafiti huo ni sawa na uuaji kwa sababu unaanzia na kuharibu viinitete vya binadamu, ambavyo tayari huwa ni binadamu hai.

Akiwa ndani ya ndege yake, ‘Air Force One’, Rais Bush akisafiri kwenda New Jersey pamoja na katibu wa habari wa Ikulu ya Marekani, Ari Fleischer ambaye mwanzoni alisema kuwa sheria ya California inatokana na haki ya jimbo hilo kuwa na sheria zake. Alisisitiza  ‘Rais amesema kuwa kuna mamlaka ndani ya majimbo ya kutunga sheria zake,” alisema Fleisher.

Hata hivyo baadaye Fleisher alirekebisha maelezo yake na kusema “Rais anadhani kwamba sera zote za majimbo na za serikali ya shirikisho zinapaswa kukuza utamaduni unaoheshimu uhai, na kwamba anatofautiana na kile ambacho jimbo la California na gavana wake amefanya.”

Seneta wa jimbo hilo, Deborah Ortiz aliandika muswada unaoelezea kuwa California itaruhusu kwa uwazi kabisa utafiti wa seli shina za viinitete vya binadamu na kuruhusu uharibifu na utoaji wa viinitete hivyo.

Muswada huo unataka kliniki za urutubishaji kufanya hatua za urutubishaji wa      invitro ili kuwataarifu wanawake kwamba wana uchaguzi wa kutoa viinitete vilivyoachwa bila kutumiwa katika utafiti.

Aidha muswada huo unamtaka mwanamke anayehusika na viinitete kukubali kuvitoa kwa maandishi na unapiga marufuku uuzwaji wake.

Ortiz na waungaji mkono wa mswada wake walisema kuwa utafiti huo ungeweza kusaidia katika upatikanaji wa tiba ya magonjwa sugu, kama vile ugonjwa wa ‘Parkinson’, ‘Alzheimer’ na maumivu katika uti wa mgongo.

Sheria hiyo itavuta watafiti “wazuri na mahiri” kwenda California na hivyo kukomesha uhamaji wa watafiti katika eneo hilo kwenda katika nchi ambazo jambo hilo linaruhusiwa, alisema profesa Larry Goldstein, wa Chuo Kikuu cha California, San Diego.

Naye mtafiti katika Chuo Kikuu cha California, Susanne Huttner, alisema kwamba kwa kuwa serikali ya shirikisho haitalipia utafiti huo, watafiti katika California itawabidi wawe macho ili kutenganisha utafiti huo na masomo mengine.

Naye Mwongoza filamu Jerry Zucker aliungana na Davis na Reeve katika kutangaza sheria hiyo mpya, akisema kuwa alijifunza juu ya utafiti wa seli shina baada ya kugundua kwamba binti yake mdogo alikuwa na ugonjwa wa kisukari.

“Baada ya kujua utaratibu kwa kina, tulianza kuuliza nini kingefanyika ili kutibu kisukari,” alisema na kuongeza “kila mtu alitwambia kwamba utafiti wa seli shina za viinitete ndiyo tumaini lake bora ili aweze kupona.”

Zucker alisema kuwa baada ya hayo mara moja aligundua kuwa “kikwazo kikubwa katika kutafuta tiba kwa binti yetu ni serikali yetu wenyewe.”

Baraza la Congress halijashughulikia muswada wa utafiti wa seli shina au muswada unaopiga marufuku utafiti huo na Ortiz alisema kwamba bado kulikuwa na swali juu ya iwapo sheria ya California ingefyonzwa na sheria za shirikisho.

Masuala yanayosubiri kushughulikiwa na Baraza la Congress ni pamoja na kuruhusu utafiti huo ama kuufanya kama kosa la jinai hivyo na kuwashitaki wale walioenda nchi za ng’ambo na kupata matibabu kutokana na utafiti wa seli shina.

Davis alisaini muswada mwingine unaifanya kuwa ya kudumu ile marufuku iliyokuwa ya muda dhidi ya utafiti kwa makusudi ya kuzalisha watu, alisema msemaji wake Steve Maviglio. Marufuku hiyo ya muda ilitarajiwa kuisha mwishoni mwa mwaka huu.

Uamsho ni Ulokole katika Ukatoliki? (3)

Katika Toleo lililopita, Askofu Method Kilaini, aliishia katika kusema kuwa, kwa bahati mbaya, kwa kuwa walioanza walikuwa Walokole, utakuta mara nyingine katika Uamsho wa Kikatoliki Walokole utakuta pia wamo humo na hata wanajaribu kuleta vitu vyao vya Ulokole humo ndani. Endelea.

Kwa maana hiyo, Uamsho unakuwa ni kitu ambacho badala ya kuwa na vya kufundisha, unakuta unabakia tu ni kitu cha kuimba, kusema lugha na na katika kujaribu kuponya vyote unakuta vinabaki hapo. Uamsho unabaki ni hapohapo ambapo unakuwa kama vile hauna maana.

Uamsho ni kitu kikubwa zaidi. Ni katika kujaribu kuingiza dini katika mtu ili aweze kumuamini Kristo katika roho inayosema, hauwezi kusema Kristo ni Bwana bila nguvu ya Roho Mtakatifu.

Hiki ndicho kiini chake; kusema kwamba Kristo ni Bwana kwa nguvu za Roho Mtakatifu, hivyo vitu vingine vya lugha, kuponya, kuimba na kurukaruka ni vitu vya kusaidia, wala siyo kiini cha Uamsho.

Hivyo, utakuta kosa linalofanyika mara nyingine ni kufanya hivyo kama ndiyo kiini cha Uamsho na hoja inakuwa ni Uamsho.  wanapoimba na kuruka, inakuwa Uamsho wanaponena kwa lugha, unakuwa Uamsho wanapoponya, hivyo inaendelea hata kufikia kwamba pengine watu wasiende hospitali tena.

Hivyo, pengine unaambiwa nenda kwa Wanauamsho utaponywa. Kwa hali kama hiyo, mtabakia kila wakati mnawahubiria watu kuwa wakienda kwenye Ulokole, wanaenda kupona.

Ukweli siyo huo. Hata Kristo mwenyewe hakuponya kila mtu, ila kuponya ilikuwa ni ishara ya ujumbe alioutoa. Hiki ni kitu kimojawapo ambacho Uamsho kama unataka kufanikiwa, unapaswa kujihadhari nacho.

Uamsho tunauita Uinjilishaji wa Kina, ili   watu waseme Kristo ni Bwana, na hivyo wabadili maisha yao.

Ndiyo maana Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alianzisha Kituo cha Agape (Agape Center).  Kwa kweli kilikuwa Kituo cha kwenda kuandaa watu na kuwafanya kuwa wainjilishaji wenye moyo na dhamira kubwa ya kwenda kufundisha na kuleta uinjilishaji wa kina. Na hii ndiyo iliyokuwa dhamira kuu ya Mkutano wa AMECEA wa Mwaka huu.

Hivyo, wanapokwenda waingie katika parokia wakiwa wanyenyekevu.

Na jambo tunalowaomba mapadre ni kuwa karibu nao. Hii itasaidia kuwafanya wasiiache iende peke yake. Pia, wasiseme hawaijui. Wajaribu kuielewa kwa sababu ni sehemu mojawapo ya karama za Bwana.

Nilikwenda katika parokia moja, nikakuta Kamati Tendaji, tukaongea. Lakini, mmoja akasema eti kama angekuwa na uwezo, angefuta hii Karismatiki eti ili Kanisa liwe na amani.

Nikasema hapana, hatuwezi kufuta Uamsho. Uamsho upo.

Hata ukiwafukuza katika parokia yako, au katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, bado Nairobi watafanya, Kampala watafanya; na wale wa Nairobi watakuja huku, sijui sasa tuwafukuze kanisani!

Kuwafukuza kanisani sio suluhisho, suluhisho ni kuwaelewa na kuwasaidia kulijenga Kanisa.

Ukiwafukuza katika parokia, haimaanishi kuwa Wakristo wako wakiwa Wanauamsho, utawakatalia sakramenti. Huwezi. Watakwenda katika parokia nyingine, watakuwa Wanauamsho watarudi na kufanya chinichini na hii itaharibu uchungaji.

Mfano, katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, tunaweza kusema tunafuta Uamsho, lakini wakatoka kwingine mfano, Morogoro, Arusha, Mbeya, Nairobi; watakuja, wataingia na huwezi kuwakataza wala kuwasimamisha sakramenti kwa sababu eti umepiga marufuku Uamsho.

Uamsho ni kitu halali hata toka Roma, hivyo suluhu ni kuukubali, kuishika na kuilea Karismatiki ili iendelee vizuri.

Kuhusu karama za uponyaji, huu ni msisitizo wa Roho Mtakatifu. Unapokuwa na karama za Moyo Mtakatifu wa Yesu, hapo huwa una msisitizo tu, wa moyo mwanana wa Bwana Yesu na huruma yake.

Mfano, Lejio Maria msisitizo wake ni ibada kwa Bikira Maria kama Mama, lakini Karismatiki msisitizo wake ni kujua nafasi ya Roho Mtakatifu katika imani yetu; ile ya kwenda na kuhubiri. Yaani hapa kila mtu aseme, “Ole wangu nisipohubiri Neno la Mungu.”

Haya mambo mengine ya kunena kwa lugha, mambo ya kuimba, ni namna tu, za kusaidia.

Ni muhimu pia watu wajue kuwa wasipopona, wasiseme kuwa Roho Mtakatifu hayupo, vinginevyo wagonjwa wote tungewatoa hospitali ili waende pale wakapone. Lazima watu wajue kuwa Mungu akipenda, anaweza kumponya hata mtu mmoja tu.

Na hii nasema sio kwa Karismatiki peke yake, hata kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu; wanaweza kuombea mtu, Mungu akipenda, anapona, Lakini hakuna anayeweza kusema eti mimi kama Mkarismatiki nasema kuwa pona na hivyo eti mtu yule naye apone. Hapa ni Mungu ndiye anayeponya na sio Mkarismatiki na wala sio dini. Karama za Karismatiki ni kueleza Neno la Mungu; kuinjilisha kwa kina.

Itaendelea

UTAMADUNI

Wakurya: Kuwatahiri wanawake kwa siri ni kujikomoa wenyewe

l Wajawazito hutahiriwa wakati wa kujifungua

l Watoto wachanga wanapozaliwa je nini hutokea?

Joseph Sabinus na Lilian Timbuka

KIJANA! Njoo utazame vyumba vipo viwili, sasa wewe chagua unachopenda, ulipie kwa miezi sita au mwaka mzima; uhamie hata leo,” akasema Mzee mmoja eneo la Kurasini, Dar es Salaam Samweli Matiko, alilipofika kwake kutafuta chumba kwa ajili ya kuanza maisha yangu.

Matiko alifurahi mno na hata akaridhika na chumba huku akiwa tayari kulipia kwa msimu mzima wa mwaka. Balozi katika shina lile akaitwa kushuhudia kutiliana saini katika mkataba ule wa kupanga katika nyumba hiyo yenye uzio mzuri na wapangaji wengine mchanganyiko, wa kike na wa kiume.

Huku kikao! hicho kikiwa katika mtindo wa mzunguko, mmoja wa wajumbe wa kikao kile akataka wazidi kujuana zaidi maana  binadamu bwana, pengine hata labda wale ni ndugu wasiojuana.

Akarudia tena, “Ninaitwa Samweli Matiko.” Akauliza zaidi, “Mwenyeji wa mkoa gani?” “Mimi mwenyeji wa Musoma mae…”. Ghafla, Baba mwenye nyumba akadakiza kwa mshituko, “Wewe ni mtu wa Musoma? Ni Mkurya?” Matiko akawahi kuitikia kwa ufahari, “Ndiyo mimi mtu wa Musoma na ni Mkurya kabisa vipi na wewe ni mtu wa huko nini?”.

“Sikia kijana kama wewe ni Mkurya (akiwa na maana ya Mkoa wa Mara), afadhali nimejua kabisa. Utanisamehe nyumba yangu sipangishi Mkurya. Siwezi! Siwezi kijana utanisamehe; samahani kwa kuwasumbua.,” akasema huku akininyooshea mkono kunirudishia pesa aliyokuwa nayo tayari mkononi mwake.

Kibaya zaidi, kadiri Matiko alivyozidi kumsihi Mzee yule ampe chumba, ndivyo Mzee alivyozidi kuwa mkali. Matiko akafyata mkia na wapambe wake aliokuwa nao.

“Twende bwana mimi siwezi kuficha kabila langu,” akasema huku wakiondoka pale.

Wakaendelea na juhudi za kutafuta chumba mahali pengine huku wakitoa tenda kwa watafuta vyumba maarufu mtaani wanaoitwa madalali.

Hazikupita siku tatu, dalali akafika akimtafuta pale alipokuwa anaishi. kwa hifadhi “Mali (chumba) imepatikana sasa ulaze damu mwenyewe.” Wakaenda jioni hiyo.

Wakamkuta mama mwenye nyumba hapo Kekomachungwa. wakasalimia na kisha yule dalali akamwambia mama yule, “Mama huyu ndiye mgeni wako.”

“Baba wewe mtu wa wapi?”  “Kwetu ni Musoma. Baba ni Mkurya na mama ni Mkurya.”

Mama akaguna kidogo na kusema, “Umeishapata mwenzako baba (akimaanisha kama Matiko ameoa). Akamjibu, “Kwa kweli bado ; ndio ninaanza maisha sasa.”

“Bahati mbaya mwanangu.”  “Kwanini unasema hivyo?” Matiko akasaili ili kujua kulikoni tena. “Ni bahati mbaya kwa sababu kwanza sipangishi kijana ambaye hajaoa au ambaye hajaolewa. Hilo ni moja, la pili, siwezi kukaa na Wakurya wala binti wangu hawezi kuolewa na Wakurya.”

Sasa Matiko akachanganyikiwa maana aliyeumwa na nyoka, hata akiguswa na nyasi anashituka.

Safari hii hakutaka ubishi wala kubembeleza. akaaga wakaondoka.

Njiani kila mmoja wetu alikuwa na lake alililojiuliza.

“Kumbe ndiyo maana siku hizi sio jambo geni kumsikia kijana yeyote hata akiwa mtaani akijitambulisha kwa watu kuwa ni mtu wa kabila lingine (si Mkurya au hatoki mkoani Mara)!” Mmoja akasema kwa sauti.

Mambo haya yakamchanganya sana Matiko maana kwa kiasi kikubwa, jambo la ukabila hutokea hasa kwa vijana wanaotafuta vyumba vya kupanga au wale wanaochumbia au kuchumbiwa.

Sasa sababu za vijana hao kuficha kabila lao zikaanza kubainika. Ikabainika siri iliyofichika sirini.

Mara nyingi unapojitambulisha katika jamii kuwa wewe ni Mkurya, uwe na uhakika kuwa huenda lengo lako litaishia patupu kwa kukatalaiwa kila unapoenda .

Hii ni kwa sababu kuna dhana iliyojengeka miongoni mwa jamii kuwa Wakurya ni wakorofi, wagomvi na mengine mengi ya namna hiyo.

Kwa mazingira na uelewa wa kawaida, dhana hiyo inaweza kweli ikawa sahihi au isiwe sahihi kwani, wote wanaopiga au kuua wake zao ni Wakurya?

Ni vigumu kuafiki moja kwa moja dhana ya jumla kuwa Wakurya ni wakorofi kwani ninajua kuwa tabia ya mtu licha ya kutegemea mazingira ya malezi aliyozaliwa na kulelewa, bado inategemea mtu mwenyewe.

Hata hivyo, ukweli unabaki palepale kuwa mila na desturi za kabila hilo, zinakuwa kichocheo kikubwa katika dhana hii. Ugomvi wa namna zote pamoja na unyanyasaji wa wanawake, ni vitendo vilivyokithiri na hata kuwa tishio kwa makabila mengine.

Inasikitisha kwa ndugu zetu Wakurya wameulinganisha na kuuchukulia ugomvi kuwa kama moja ya mahitaji yao muhimu.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekuwa vitu vya kawaida kusikika masikioni mwa watu na ni dhahiri kuwa, kama  Serikali isingeamua kuingilia kati, sijui jamii ya Wakurya ingekuwa na tofauti gani na Wahutu na Watutsi.

Kinachosikitisha hapa ni kwamba, badala ya Wakurya kuutambua upendo wa Kimungu kama ndugu, bado majaribio ya kumwagiana damu yanajirudia miongoni mwao.

Hivi hata katika mwanzo huu wa miaka ya 2000, ambao dunia imo katika Karne mpya, bado Wakurya wanataka kubaki katika zama zile za miaka ya huko kisogoni?

Hivi kimantiki, kwanini Walenchoka na Wanchali wapigane na kumwagiana damu, kusababishiana vilema na kugeuzana wakimbizi?  Kama ilivyokuwa nyuma, kwanini Wakira na Wanyabasi wapigane ? Uadui unatoka wapi wakati wote ni familia moja ya Wakurya ndani ya nyumba moja ya Tanzania?

Tukiachana na vita hiyo ya wenyewe kwa wenyewe, miaka ya hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa matukio ya wanaume kufanya ukatili dhidi ya wanawake.

Mfano, mwaka 1999, huko Ronsoti wilayani Tarime, Bw. Turia Nyakemu, alimgecha (kumkata mtu kwa panga) mithili ya mti wa porini, mkewe, Ester Turia eti kwa madai kuwa, akizaa watoto wanakufa (kwa sasa hatujui hatima ya shauri hilo).

Hivi kama sio unyanyasaji unaoogopesha hata makabila mengine, alipimwa na nani hata ikabainika kuwa tatizo la Ester kutozaa lilitokana na yeye na wala si mwanaume au vinginevyo?

Hivi mwanamke kama alivyo, anaweza kuzuia watoto wasife?

Pia, katika Kijiji cha Borenga wilayani Serengeti, Bw. Mwikwabe Ryoba, aliwahi kufungwa na kukalizwa juu ya moto ulioandaliwa kwa makusudi eti akituhumiwa kufanya mapenzi na mke wa jirani yake.

Labda jambo muhimu la kujiuliza hususan kwa jamii ya sasa ya Wakurya ni kwamba, mtindo huo wa maisha wa kujichukulia sheria mkononi, bado uko kwenye fasheni hadi sasa au la?

Hivi tukiwa wakweli, ni nani asiyejua ukweli juu ya adhabu kali wanazopewa wanawake wa Kikurya toka kwa waume zao? Ni wangapi tumewasikia kuwa wamechomwa hata sehemu nyeti na waume zao?

Tunajua avumaye baharini ni papa, lakini na wengine wapo, lakini ukweli ni kwamba, licha ya kuwa madhambi hayo sasa yanafanywa hata na makabila mengine yakiwamo ya mikoa ya Kusini mwa Tanzania, bado hapa ninajadili Wakurya kwa sababu ndio jina lao limeenea sifa hiyo mbaya.

Mfano, hivi karibuni Mahakama Kuu ya Tanzania ilipokutana wilayani Tarime, iliwatia hatiani baadhi ya watu kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya mauaji.

Mahakama hiyo ilimhukumu Oranda Nyakua (35), mkazi wa Utegi, kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe, Pamela Nyakua, kwa kumgecha mapanga.

Tukio hilo lilidaiwa kutendeka Oktoba 11, 1995 katika kijiji cha Masike wilayani Tarime.

Septemba 30, mwaka huu, Mahakama Kuu hiyo, ikamtia hatiani na kumpa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, mkazi mmoja wa Kijiji cha Tagota wilayani Tarime, Lucas Kimito(69), kwa kosa l;a kumuua mkewe Wegesa Kimito.

Ilidaiwa kuwa, tukio hilo lilitokea Machi 12, 1995, baada ya Bw. Kimito kumshambulia kwa ngumi na ufagio hadi kumuua mkewe kutokana na ugomvi wa kifamilia.

Ninajua dhahiri kama nilivyotangulia kusema kuwa, unyanyasaji wa namna hiyo unatokea kabisa hata kwa makabila mengine, ila kinachonisikitisha, ni kukithiri kwa kwa unyanyasaji huo ndani ya Wakurya.

Hivi ni kweli kuwa licha ya umuhimu wa mwanamke yeyote kujulikana kwa kiasi kikubwa namna hii ndani ya jamii, bado Mtanzania mwenzako mwenye majukumu mengi namna hii, ananyanyaswa kwa ukatili wa makusudi; Tanzania ya kesho italindwa na kujengwa na nani?

Tukiachilia mbali unyanyasaji huo unaomfanya mwanadamu aonekane mnyama kuliko mnyama halisi kwa njia ya vita, hebu sasa tuutazame huu unaofanyika kwa kisingizio cha mila na desturi.

Ninajua zipo mila nyingine nzuri ambazo hazina budi kuigwa na kuboreshwa ili ziendelee zaidi, pia zipo ambazo kwa udi na uvumba hazina budi kuachwa kabisa kwani zimepitwa na wakati na zina madhara makubwa katika jamii kiroho na kimwili.

Ni kweli kuwa unapofikia umri wa ujana; kijana wa Kikurya hupelekwa jandoni ambako hufanyiwa tohara hali inayoonesha kuwa yuko tayari kuoa au kuolewa na kuwa baba au mama safi wa familia; hivyo kipindi hiki ni muhimu sana kwani ni huko wanapoadilishwa namna ya kuishi vema.

Hata hivyo kipindi cha jando kimekuwa na umuhimu mkubwa kwani  hapo vijana wanafunzwa na kuchochewa moyo wa ari na ujasiri. Pia kupitia jando na tohara kwa vijana, kumekuwepo na heshima kati ya rika moja na nyingine maana pamoja na umri, bado rika iliyotanguliwa kutahiriwa (kwa Kikurya huitwa Esaro), huweza kuheshimika sawa na baba au mama maana hata makamo yao huranda.

Tofauti na hali ilivyo sasa kuwa mzee anayelingana na baba anaweza kumtania binti mdogo sawa na mwanae kama nionavyo mijini na hata wanataka ‘kujenga mazoea ya karibuhilo katika jamii ya Wakruya halifanyiki kutokana na msaada wa rika ya jando.

Kwa wenzetu hawa wenyeji wa Mkoa wa Mara, hususani Tarime Musoma-Vijijini na Bunda, mvulana ambaye hajatahiriwa (Umurisya), msichana (Omosaghane) na mwanamke aliyezaa kabla ya kutahiriwa (Irikunene) ni watu wanaochukuliwa na jamii kama watoto wadogo na hawana sauti ndani ya jamii. Kufanya mapenzi nao ni aibu, dhambi na kashfa.

Katika makala haya ya leo ugomvi haupo katika neno tohara, bali TOHARA KWA WANAWAKE licha ya juhudi za Serikali na wataalamu wa afya kubainisha athari zote za tohara kwa wanawake ikiwa ni pamoja na kupelekea vifo wakati wa kujifungua, kuvuja damu baada ya kitendo hicho na pengine kupotezaa maisha, bado Wakurya wanayo ile dhana kuwa kitendo hicho ni sawa na Speed Governer yaani hupunguza taama za kimwili kwa wanawake.

Ni kutokana na imani hiyo ambapo licha ya juhudi za Serikali, vikundi vya afya, pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA), kuuelimisha umma madhara hayo, na kwa kuwa Serikali imetangaza bayana vita dhidi ya unyanyasaji huu wa wanawake, unaofanywa hata na Wagogo, Wapare na Wachaga, na wenyeji wa Mkoa wa Singida, wenzetu Wakurya sasa wameamua kufanya madhambi  hayo kwa kificho.

Kwa ndugu zetu Wakurya, kwa miaka ya hivi karibuni na pasi na shaka mtindo huu bado unaendelea, wamekuwa na tabia ya kumfanyia tohara Mtoto wa kike ndani ya nyumba na kufungiwa humo hadi atakapopona ili kukwepa ‘jicho’ na ‘mkono wa Serikali’ yaani kwa siri.

Si hivyo tu, bali pia saa kwa mwanamke mjamzito ambaye hajatahiriwa (Irikunene) ili kukwepa kubumbuluka kwa siri hizo, sasa kwa Wakurya na kungwi huandaliwa mpango maalumu wa siri ambapo pasipo yeye mjamzito kujua, tena wakati ule wa kujifungua, ndio huwa nafasi ya kuwafanyia wanawake tohara bila hata wenyewe kujua.

Kwa bahati mbaya sana, wanawake wanaoathirika zaidi na mtindo huu, ni walioolewa toka katika makabila mengine yasiyofanya ukatili huu.

Ni wazi ni ukatili kwa sababu unapomfanyia ukeketaji mwanamke wakati wa kujifungua tena bila yeye kujijua, huwa katika maumivu ya kuathirika kwa tohara pamoja na uzazi (Double effects).

Hivi ndugu zangu Wakurya na makabila mengine katika jamii zote za ki-Afrika, kinachowahangaisha ni nini na kina faida gani? Hivi kweli kitendo hicho ni spidi gavana ya ufuska? Ni ufahari? Mbona nanihii amefanya lakini ….. tandiko la kukodi? Au….. mbona nani hii  hajafanyiwa lakini; ni mtu mtii wa maadili?

JULAI,1998 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya makosa ya kujamiiana ikaweka adhabu ya kifungo cha miaka 30 kwa anaepatikana na kosa la kubaka, kunajisi ama kulawiti.

Sheria hiyo pia inambana mtu anayepatikana na hatia ya kuhusika na kukeketa kwa namna yoyote ile, ambapo adhabu yake ni kifungo miaka mitano jela.

Pamoja na kuwepo kwa sheria hiyo, vitendo vya ukeketaji na ubakaji bado vinazidi kushamiri badala ya kupungua tangu kupitishwa kwa sheria hiyo.

Kwa upande wa ukeketaji wa wanawake, hivi sasa wadau mbalimbali hapa nchini wamejitokeza kupambana na mila hii potofu ambapo hutoa elimu juu ya madhara ya mila hii.

Hata hivyo, pengine ni vizuri kwanza tukaelewa zaidi kuwa mtu anaposema ukeketaji ; anakuwa na maana gani.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), ukeketaji ni kitendo cha kushona au kukata kipande au kuondoa sehemu ya juu ya siri ya mwanamke kwa sababu yoyote ile (tohara kwa wanawake).

Utafiti umebainisha kuwa hali hiyo huleta madhara ya muda mrefu kwa wale wanaotendewa kitendo hicho.

Takwimu kuhusu idadi ya wanawake wanaofanyiwa tohara hii katika Tanzania inasemekana kuwa kwa hivi sasa ni zaidi ya asilimia 18, na kwa inakisiwa kwamba zaidi ya wanawake milioni 130 hufanyiwa ukeketaji kila mwaka duniani.

Mojawapo wa Wadau hao ni Kanisa Katoliki kupitia kitengo chake Maedendeleo ya Akinamama kilichopo chini ya Shirika la Misaada,CARITAS tawi la Tanzania (WID).

Kitengo hicho kimeandaa mpango wa miaka 3 wa kuelimisha umma madhara yatokanayo na ukeketwaji wa mwanamke.

Madhumuni ya mpango huo ni kuwakutanisha watu wa aina mbalimbali ili kuwaelimsha madhara ya mila hii ili kuwezesha kupata njia mbadala ya kuweza kuitokomeza.

Mratibu wa WID kitaifa,Bibi Oliver Kinabo, anasema Kitengo chake kama chombo cha Kanisa kimeamua kupambana na mila ya ukeketaji kwa kutambua madhara makubwa ayapatayo mwanamke aliyekeketwa.

Mpango huo unawashirikisha wananchi katika kubuni mbinu zinazofaa katika kutokomeza mila ya ukeketaji wanawake .

Bibi Kinabo anasema mpango huu umebuniwa baada ya kuona mila hii ya kukeketa wanawake haikomi na badala yake, inashamiri hususan katika Mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania, Kanda ya Kati, ambayo ni Dodoma na Singida.

Kwa mujibu wa Bibi Kinabo, Mikoa mingine ambayo inaongoza kwa mila hii kwa hivi sasa ni pamoja na Arusha, Kilimanjaro, Mara na Manyara.

“Mpango huu wa kutoa elimu ya madhara ya ukeketaji ambao utadumu kwa muda wa miaka mitatu mfululizo, tumeupanga kimajimbo, na kwa kuanzia tumeanza na Dayosisi ya Musoma, Arusha, Same pamoja na Mbulu”. Alisema Bibi Kinabo.

Anasema Kanisa linapambana na ukeketaji ili kukomesha ukatili wa kijinsia ambao pia, unachangia maambukizi ya virus vya HIV vinavyosababisha UKIMWI.

Utafiti umebaini kuwa mara nyingi vifaa vinavyotumika katika ukeketaji si salama kiafya.  Vifaa hivi ni pamoja na visu, vipande vya chupa, vyuma, nyembe na vitu vingine vyenye ncha kali.

Kibaya zaidi ni kwamba vitu hivyo hutumika mfululizo kukeketa mtu zaidi ya mmoja bila kufanyiwa usafi wa aina yoyote kama tahadhari ya kuzuia maambukizo ya virus vya maradhi mbalimbali.

Katika mpango huo wa kuelimsha jamii, WID pia, inashirikiana na kitengo kama hicho kutoka nchini Eritrea kupitia CARITAS Eritrea ambacho kinafadhili mpango huo katika Jimbo la Mbulu.

Utafiti zaidi umebaini kuwa baada ya Serikali kupiga vita suala, hivi sasa wahusika wamebaini mtindo wa kuwakeketa watoto wadogo kwa madai kuwa ni kuondoa fedheha katika familia.

Ni jambo la wazi kuwa huu nu ukatili wa kutisha.

Kulingana na utafiti huo uliofanywa na WID, baadhi ya makabila yanafanya ukeketaji kama njia ya kumwingiza msichana katika utu uzima.

Jamii nyingi nchini zimeonesha kuwa tohara hii inasisitizwa na vijana wenyewe wanaodhani kwamba kama hawatakeketwa hawatakubalika katika jamii hizo.

Bibi Kinabo anatoa wito kwa wahanga wa vitendo hivyo, kuwa mstari wa mbele kuvikemea na kuielimisha jamii kwa kuwa wanajua madhara yake.

“Sisi kama Kanisa hatukatai mila na desturi za makabila mbalimbali ambazo zinatumika kwa hivi sasa, lakini hatuko tayari kabisa kuona mwanamke akidhalilishwa kwa kukeketwa na kufa kwa mateso makali pasipokuwa na hatia. Tutaendelea kuipiga vita mila hii mbovu,” alinasema

Katika nchi nyingi duniani imeonekana kuwa elimu ndiyo njia bora zaidi inayoweza kutumika katika kupiga vita mila ya ukeketaji.

Nchini Sierra Leone, mila ya ukeketaji imekuwapo kwa karne nyingi, lakini hivi sasa kuna majimbo 588 ambayo yanawakilisha zaidi ya watu 200,000 ambako ukeketaji umeachwa kabisa baada ya wanachi kuelimshwa na kujua madhara yake.

 Cha msingi kujiuliza hapa ni kuwa, inapoelezwa kuwa kitendo cha tohara kwa mwanamke (ukeketaji) kinapunguza tamaa na hisia za kawaida za kimwili, maana yake ni nini; kwamba jamii zinazofanya vitendo hivyo huwa zinalenga kuwatia vilema wanawake au kuwafanya tasa au vipi?

Kwa nini jamii ilazimishe kuwapa watu wake vilema vya uzazi? Hivi unamuondelea mtu tamaa ya mwili ili afanye nini kupata watoto ndani ya ndoa yake halali ya kidini, kiserikali na hata kijamii? Tena ikumbukwe kuwa hiyo ni ndoa ile mnayosherehekea huku mkila na kunywa kwa mbwembwe.

Nina wasiwasi kuwa Serikali na jami yenyewe wakiwamo Wakurya visiposhirikiana kuupiga vita unyama huu, utafikia wakati utakuwa ni utaratibu kabisa kuwa watoto wa kike watahiriwe wakiwa wachanga tena wakati ule wanapozaliwa. Mateso, aibu na unyama tupu.

Hivyo, nguvu za pamoja zinahitajika sana kukemea vitendo hivi viovu.

Mara nyingi Wakurya wenyewe wameshuhudia namna vifo vanavyotokea wakati wa kujifungua kutokana na tohara hizo haramu, namna wanavyovuja damu  baada ya kitendo hicho. Ni nani asiyejua tabu na maumivu makali wanayoyapata wanawake wanapotolewa damu ile inayotokana na tohara (amakoha)?

Nani hajui namna wengine wanavyozimia huku wakipiga mayowe ya vilio vya uchungu? Ndani ya mateso hayo ambayo wengine huyashangilia kwa kula na kunywa huku mwingine akinusurika au kufa?

Hivi ni mzazi gani mwenye busara anayefurahia kumjeruhi mwanae kwa makusudi huku yeye akila na kunywa kwa furaha hali anajua hakuna faida yoyote bali hasara tupu? Hivi Wakurya kuna nini wanachong’ang’ania . Kilicho cha maana ni kipi chenye faida katika suala hilo la tohara kwa wanawake?

Umefika wakati jamii ya Wakurya sasa ijiulize inatoka wapi, na inakwenda wapi. Jamii haina budi kuzitazama upya mila na desturi.

Zipo nyingine ambazo hazina budi kuigwa na kurithishwa toka kizazi kimoja hata kingine kama zile za kushirikiana katika kazi kama kilimo, ujenzi, ulinzi na usalama, kusaidiana wakati wa maafa na mengine ya namna hiyo.

Hawana budi kuzitambua haki za watoto wote; wa kike na wa kiume na kuwapa huduma za jamii kama elimu na afya.

Wajue kuwa dhana ya kuwatahiri watoto wa kike kwa kificho na wakati wa kujifungua ni sawa ujanja wa popo kutaka kumnyea Mungu kumbe anajinyea mwenyewe.

Jamii ijue kuwa njia za kumuangalisha mtoto wa kike zipo nyingi na hata kwa vipindi vingi tofauti.

Hizo zinawezekana hata bila ya kufayika tohara. Kwani  makabila yasiyo na tohara kwa watoto wa kike hawana maadili?

Inabidi sasa Wakurya na Watanzania kwa jumla, waijenge jamii yao kijamii na kiafya; siyo kuzidi kujimaliza na kujibomoa wenyewe kutokana na mila na desturi zilizopitwa na wakati; tena zisizo na faida.

Ni kutokana na athari za tohara kwa wanawake ndiyo maana labda hatutakosea kusema kuwa nakabila yanayofanya hivyo wakiwamo Wakurya, pamoja na mengine yooote mazuri; lakini hili linawaharibia hadhi, afya na jamii yao, achilia mbali suala la ugomvi wa ovyo ovyo. Hata hivyo, inafurahisha kuona walio wengi sasa wanabadilika na kwenda na wakati.'

UCHAMBUZI WA KITABU

Tamthilia na Ulimwengu Ulivyo Sasa(2)

 

Kitabu:   Kivuli Kinaishi

 

Inaonekana kuwa Bi. Kirembwe alikuwa hajiamini katika utawala wake ndio maana akategemea ushirikina, wale wasiozugika wanaangamizwa. Mfano, mkulima na mwalimu, pia Mtolewa na Wari walipojaribu kueleza ukweli.

Dawa ya mto ni moto. Mtolewa naye anaibuka na unga wa rutuba unaoonekana kufanya kazi kweli kweli.

“..Nikulambisheni unga wa rutuba…” (Uk. 100).

Uchawi upo katika jamii zetu tena sana, ambapo pia viogozi wanajizindika ili waendelee kuwa madarakani. Mara ngapi wewe na mimi ambao hatujazugika tumewasikia viongozi wetu wakisema kuwa nyeusi ni nyeupe na watu bado wanakubali isipokuwa sisi wachache?

Vyombo vya habari vimeripoti matukio kadha wa kadha. Mfano “Sangoma” kule Tanga kuchuna ngozi na watu kufanywa mazuzu.

Pia, wasanii wamejitokeza kujadili hili mfano wimbo wa ‘Mzee wa Busara’ hii yote inatudhihirishia kuwepo kwa vitendo vya kichawi katika jamii yetu kama ilivyo Giningi. Ingawaje katika nchi yetu Tanzania hatujashuhudia uongozi kama wa Bi Kirembwe na hivyo Mungu aupitishie mbali.

 

Nafasi ya  Mwanamke:

 

Katika Tamthiliya ya KIVULI KINAISHI, mwanamke amechorwa katika sura kuu mbili. Kwanza, kama mzalendo na mpenda haki na pili kama Kiongozi na kiumbe cha kutisha na pia mchawi.

Bi. Kizee ni mzalendo na mpenda haki ndio maana ameamua kusimulia kwa vitendo hadithi za Giningi ili watoto (vijana) waone uovu wenyewe na hivyo wakabiliane nao. Anachukua jukumu la kuwafunua macho kwa kutumia miti shamba ili wayaone hayo. “Hayo sio macho ni makupekupe tu…” (Uk. 6).

Kwa upande mwingine, mwanamke anaonekana kama kiongozi na mchawi pia.

 Bi. Kirembwe ndiye Kiongozi wa Giningi anayeongoza kwa ukatili na imani za kichawi. Ukatili ndio unaomfanya awaangamize wazee na Wazi, Mtangazaji na Mtolewa.

“Mmelaaniwa na wazee wetu… walinzi! Tusiwaone hawa …”

“Kwa sababu ya uchawi, uchawi ndio  roho za watu wengine” (Uk. 79).

Mwanamke huyu huyu anaonekana ni mwenye uchu wa madaraka. Kila kofia anataka aivae yeye; mara mchawi, mara malkia, huku Kiongozi wa Giningi huko ni mfalme waliyebebwa mimba miezi kumi na moja

“…..Ndiye mchawi mkuu…” (Uk. 71).

“Mama … baba… mama upande mmoja na baba upande mwingine…” (Uk. 33)

“Nimechukuwa umbo la uhakimu …” (Uk. 66).

Ni kweli kuwa mwanamke katika jamii yetu ni mzalendo na mpenda haki, lakini si kweli kwamba katika jamii ya Tanzania mwanamke ana uchu wa uongozi na mkatili kama ni uchawi ni pande zote mbili kwa wanaume na wanawake.

Viongozi wa kike tunao, lakini hawako kama Bi. Kirembwe.

Kujitoa Mhanga :

Ni hali ya kupambana bila kujali litakalotokea kwako litakuwa jema au baya. Mtolewa baada ya kuamsha na kulaumiwa vikali na sauti za wahenge, anaamua kuanzisha vita na Bi. Kirembwe.

Unatusikia kutoka huku mbali tuliko? Huku mbali zinakotoka sauti zetu... ?’ (Uk 84).

‘Nakusikieni …. Nakusikia’ (Uk. 84)

‘Huchipuki kwa nini ukapasua ardhi kuvuta hewa ya uhuru… ?’ (Uk. 85).

Maneno haya ya ndotoni yalikuwa kama msumari wa moto katika donda kali. Maneno ya waliyoangamizwa na Giningi yananata akilini mwa Mtolewa. Maisha waliyonayo Wanaginingi ni sababu tosha ya kumfanya Mtolewa apambane na Bi. Kirembwe ingawaje alijua kuwa ni hatari kwake.

‘…Natambua kuwa natangaza ugomvi ; ugomvi baina ya mimi na Bi. Kirembwe. Haiwezekani kulalia kitanda cha mawaridi, wakati wengine ubaridi wa sakafu unawatafuna…” (Uk 92).

Nitamwonesha kwamba si yeye  ni sisi …. Nitamwonesha kwamba mwanadamu yeyote ana mwisho ….” ( Uk. 93).

Vuguvugu hili linaendelea hata mara baada ya Mtolewa na Wari kuangamizwa. Vizazi vipya vinairithi shughuli na harakati za kuikomboa Giningi kutoka mikononi mwa Dikteta Bi. Kirembwe.

Msanii anasema : ‘Sisi ni vizazi vipya vya Giningi

Vizazi vya waliodidimia…’(Uk. 128).

Na kweli hadithi inaishia kuzuri kwani ukombozi umefanywa na Bi. Kirembwa anaangushwa.

‘Hakika wakati si wangu tena’ (Uk. 129).

Nchi nyingi za Afrika zinajitahidi kwa udi na uvumba kutetea haki za wananchi wake japo vikwazo vimekuwepo, lakini watu wamejitoa mhanga.

Bila kujitoa mhanga kwa babu zetu, pengine bado ukoloni ungekuwepo. Mara ngapi vikundi mbalimbali vinajitahidi kuangusha tawala mbalimbali kama za Bi. Kirembwe na mwishowe, kuitwa waasi. Rwanda, Uganda, Kongo na Afighanistan ni baadhi ya mifano.

 

Hitimisho

 

KIVULI KINAISHI ni kivuli kinachoishi vipi ?

 

Bi. Kirembwe sio kwamba yuko hai halisi, bali alikufa na anatumia uwezo wa kichawi kuwa hai. Amekufa, lakini kivunli chake bado kinafanya mambo halisi. Msanii anasema :

Bi. Kirembwe aliyekufa, lakini yu hai na mwenye uwezo wake…uwezo wa kichawi mwenye kujali nafsi yake’ (Uk 82).

Pia, tunaelezwa kuwa mungu wa wachawi bado kivuli chake kinaishi.

Octavious Caesar Mungu wa wachawi…. Kivuli chako kinaishi mpaka leo’ (Uk 40 – 41).

Pia, Mtolewa na Wari baada ya kuangamizwa na kutupwa kuzimu, wanaibuka ambapo Bi. Kirembwe anaisikia sauti ya Mtolewa ikiongea.

‘Kivuli changu kinaishi na sauti  yangu ni sauti thabiti…’ (Uk. 118).

‘… lakini kivuli na roho yake haiwezi kuoza’ (Uk 109.)

Aidha, mawazo na harakati za kimapinduzi zilizoanzishwa na Mtolewa hazidumai, bali zinaendelezwa na vizazi vipya, hivyo kivuli cha Mtolewa kinaishi kupitia hata kwa vizazi vipya.

‘Sisi ni vizazi vipya vya Giningi, vizazi vya walioangamia… vizazi vya waliodidimia … (Uk. 128).

Mbona hii inadhihirika wazi kwa viongozi na waasisi mbalimbali wa Afrika. Mfano, Nkwame Nkurumah, Kenyatta, Sam Nujoma, Mwalimu Julius K. Nyerere, Banda waliokufa, lakini shughuli walizozianzisha zimeendelea hadi kufikia maendeleo.

Sisi vijana ndio vizazi vipya, ndio tunapewa kuendeleza mbegu walizopanda wahenga wetu, lakini mbegu hizi ziwe za kuleta manufaa kwetu na kwa wengine.

MAKALA YA MAZINGIRA

Victoria: Ziwa linaloliingizia Taifa mabilioni ya pesa

l Limeajiri vijana wapatao 500,000

l Gugumaji bado tishio ndani ya ziwa hilo

PAMOJA na Tazania kuwa miongoni mwa nchi maskini dunia, lakini imejaliwa kuwa na vivutio vizuri vya asili ambavyo licha ya kuwaingizia wananchi kipato, pia vimekuwa vikiinua uchumi wa Taifa. Moja ya vivutio hivyo ni Ziwa Victoria. Katika makala haya, Mwandishi Dalphina Rubyema anaeleza.

TANZANIA licha ya kuwa miongoni mwa nchi maskini duniani, bado imejizolea heshima kubwa ya kuwa na vivutio vizuri vya mali ya asili na utalii ambavyo huliingizia Taifa Mabilioni ya pesa, pia vimekuwa vikisaidia kwa kiasi kikubwa kulitangaza jina la nchi hii.

Vivutio hivi vimekuwa vikisaidia kupunguza wimbi la vijana wasio na ajira nchini ambao wengi wao wamejikita katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kujipatia kipato kwa njia iliyo halali.

Vivutio hivi vya mali ya asili na utalii ni pamoja na mito, maziwa, milima, mbuga za wanyama, maeneo ya historia na machimbo ya madini mbalimbali.

Madini ynayopatikana nchini Tanzania ni pamoja a almasi, huko Mwadui, tanzanite, huko Mererani Arusha na hata dhahabu huko katika maeneo ya Nyarugusu na Bulyanhuru, mkoani Shinyanga.

Ziwa Victoria ni mbiogoni mwa vyanzo vinavyochangia kwa kiasi kikubwa kulitangaza jina la Tanzania.

Ziwa hili pia limekuwa mkombozi mkuu kwa watu mbalimbali hususan wale wa Mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera katika masuala ya kiuchumi kwani wakazi wa mikoa hiyo hutumia uvuvi kama kazi yao ya kiuchumi.

Ziwa hili ambalo ni la pili kwa ukubwa duniani, lina ukubwa wa kilomita za mraba ,68,000 na linahudumia zaidi ya watu milioni sita.

Huduma kubwa zaidi inayo tolewa katika Ziwa hili ni uvuvi, sekta ambayo imewaajiri zaidi ya vijana 500,000  na kati yao, 56,000 ni wavuvi wa kudumu na 3,650 wameajiriwa katika viwanda vya kusindika samaki.

Ziwa hili pia licha ya kuwapatia wananchi kitoweo na maji kwa ajili ya kumwagilia mashamba, pia limekuwa likitumika kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka nchini kwenda nchi jirani za Kenya na Uganda.

Mbali na hayo, Serikali imekuwa ikipata mapato mbalimbali kutokana na usafiri ndani ya ziwa hili ukiwemo ule wa abiria na bidhaa nyingine  ndani na nje ya nchini.

Kwa upande wa uvuvi, tani 170,000 za samaki zinazalishwa nchini kila mwaka. Asilimia 60 ambazo ni sawa na shilingi Bilioni 81.6, zinatoka ndani ya Ziwa hilo la Victoria.

Licha ya faida zinazopatikana, bado ziwa hilo linakabiliwa na matatizo makubwa na hatua za haraka zisipochukuliwa, kuna hatari kubwa ziwa hilo likageuka kero kwa Watanzania badala ya kuwa mkombozi.

Miongoni mwa matatizo hayo ni kutoweka kwa baadhi ya aina ya samaki ‘Samaki wa asili’ ambao huliwa na samaki aina ya sangara ambao walipandikizwa ziwani humo mwaka 1960.

Aidha, wakazi wanaozunguka eneo hilo wamekuwa wakilima kwenye vyanzo vya maji ya Ziwa hilo.

Pia, uchafu kutoka katika viwanda mbalimbali vinavyozunguka eneo hilo vikiwemo vya hapa hapa nchini na nchi jirani za Kenya na Uganda, na ule uchafu wa kutoka majumbani, umekuwa zikielekezwa ndani ya Ziwa hilo.

Mradi wa Hifadhi ya Mazingira Ziwa Victoria (LVEMP) unaolenga kuliweka Ziwa hilo litumike kukidhi mahitaji ya chakula, mapato,maji salama ,ajira,mazingira yasiyo na magonjwa na kudumisha uhusiano wa viumbe hai na Mazingira  (Bio anuwai), umekuwa ukifuatilia kwa karibu usalama wa ziwa hili.

Mradi huo unaozishirikisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda (Afrika Mashariki), umebaini kuwa Ziwa hilo pia linakabiliwa na tatizo la magugumaji.

Magugumaji ni mmea ambayo inashambulia kwa urahisi maji ambapo kutiririka kwake ni kwa kasi ndogo kama vile maji ya ziwani, mfereji, baharini na mabwawa.

LVEMP imebaini kuwa gugumaji hili limezagaa ndani ya ziwa hilo hali inayochangia kuongezeka kwa virutubisho vya maji machafu na kuongezeka kwa mmea aina ya mwani ,mmea unaosababisha kuondoka kwa gesi ya Oksijeni katika kina cha chini cha ziwa hali inayotishia shughuli ya uvuvi.

Hata hivyo katika hali ya kuondoa tatizo hilo la gugumaji,tayari Taasisi zinazohusika na masuala ya mazingira,zimekwisha weka kizuizi cha mmea huo.

Kizuizi hicho kinachosaidia kuwaangamiza gugumaji hao ni ‘mbawakavu’.

Japo sababu zinazotolewa na wataalamu zinasema  mbawakavu hawezi kuishi kwenye mmea mwingine zaidi ya gugumaji, bado kuna wasiwasi kwamba kuna uwezekano mbawakavu hao wakaleta madhara kwa mimea mingine ya majini.

Ni changamoto kwa Serikali kupitia taasisi husika, kuhakikisha mbawakavu hao hawaleti madhara zaidi na kujaribu kufuatilia kwa ukaribu kama kweli wanazaliana ili wamudu kuliangamiza kwa kiasi kikubwa gugumaji.

Vile vile LVEMP kwa kushirikiana na Wizara ya Mali ya Asili na Utalii pamoja na Mradi wa Taifa wa Kusimamia Mazingira na asasi nyingine, wasimame kidete kuhakikisha kuwa Ziwa Victoria linatunzwa katika hali inayostahili bila viwanda kuelekeza maji machafu ndani yake na vyanzo vyake haviharibiwi na wakulima.

Pia, vyombo hivyo visimamie uondoaji wa uvuvi haramu wa samaki kutokana na ukweli kwamba baadhi ya wavuvi hutumia baruti na dawa za sumu katika uvuvi wao.

Mbali na yote, pia kuna haja ya kutafuta mbinu mbadala za kupunguza namba ya samaki aina ya sangara na kupandikiza aina nyingine ili kuwepo na uwiano wa aina zote za samaki.

MAKALA YA UCHUMI

Watanzania wengi wako vijijini, kukua kwa uchumi kunapimwa mjini, tutafika?

Na John Mapepele

HIVI karibuni Tanzania ilikuwa miongoni mwa mataifa yaliyoadhimisha Siku ya Chakula Duniani ambayo ilianzishwa kwa lengo la kutathimini hali halisi ya chakula.

Ni siku ambayo Serikali hujumuika pamoja na watu wake katika kutafakari na kutathimini masuala mbalimbali yanayohusu chakula na kilimo.

Kimsingi, Siku hii ni muhimu sana kutokana na ukweli kuwa ili taifa lolote liendelee, lazima watu wake wawe na chakula cha kutosha ili wawe na afya  bora.

 Kwa bahati nzuri, Serikali ilisema hali ya chakula kwa mwaka huu ni nzuri ukilinganisha na  baadhi nchi za Afrika hususan Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Cha kufurahisha zaidi, katika maadhimisho ya Siku hiyo ambayo kitaifa ilifanyika mjini Mbeya, Waziri wa Kilimo na Chakula, Charles Keenja, alitoa rai kwa wananchi  kuachana na kilimo cha kutegemea mvua na badala yake, akawahimiza kutumia kilimo cha umwagiliaji.

Makala hii haikusudii kuelezea umuhimu wa chakula wala kilimo kwa kuwa sote tunafahamu, bali binafsi katika kuiandika, nimevutwa na kauli ya Waziri ya  kuwakumbusha wananchi kubadili uendeshaji wa kilimo cha kutegemea mvua na kuingia katika umwagiliaji.

Wengi tutakubaliana kuwa wimbo wa “kilimo ni uti wa mgogo wa taifa hili”, umekuwa ukiimbwa na viongozi kwa muda mrefu bila kuzaa matunda, licha ya ukweli kuwa, zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania, wapo katika sekta hii hususan vijijini.

Jambo la muhimu la kujiuliza hapa ni kwanini huu uti wa mgongo ambao umewaajiri asilimia kubwa ya Watanzaniaa haupewi kipaumbele kinachositahili? Nasema hivyo kwa kuwa sote tunaelewa kuwa, uchumi wa wananchi wetu unategemea zaidi kilimo.

Labda kabla hatujaenda mbali, hebu tuangalie maana hasa ya KUKUA AU KUSHUKA KWA UCHUMI.

Wataalamu wa mambo ya uchumi wanasema, kukua au kushuka kwa uchumi kunaangaliwa kwa njia mbalimbali, lakini kuu mbili kati ya hizo ni hizi; mosi ulinganisho wa pato la taifa la kila mwananchi na ya pili, kuangalia hali halisi ya maisha ya mwananchi.

Ili tuweze kupata picha nzuri zaidi ya hali halisi ya uchumi nchini kwa wananchi hususan wakulima, walio wengi vijijini wanaombwa na Serikali ili waachane na kilimo cha kutegemea mvua, ningependa kujibu maswali yafuatayo, kwanza ni kwanini  wananchi walio wengi wameshindwa hata kutoka katika jembe la mkono na kuingia katika kilimo cha kutumia  jembe la kukokwa  na ng’ombe?

Hapo jibu liko wazi kuwa sekta ya kilimo nchini haijapewa kipaumbele ukilinganisha na sekta nyingine, sekta hii imekuwa ikitiliwa mkazo katika makaratasi tu, kwa mfano kumekuwa na kipaumbele cha uingizaji wa bidhaa mbalimbali tofauti na uingizaji wa pembejeo na vifaa mbalimbali vya kilimo.

Pia, sekta  ya kilimo imekuwa ikikimbiwa na wawekezaji kutokana na ukweli kuwa haiwezi kuwalipa. Wawekezaji wengi wamekuwa wakikimbilia katika  biashara, migodi benki na elimu ukilinganisha na hali ilivyo katika sekta ya kilimo.

Kwa upande mwingine, uchumi wa wananchi unaendelea kuwa wa chini kwa kuwa hata hayo mazao yanayolimwa hayapati masoko ya kuaminika na hivyo, yanaishia kupata  hasara kubwa.

Kwa mfano, vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti mara kadhaa kuwa wakulima wa  kahawa  walianza kung’oa  miti ya kahawa  katika sehemu ambazo zinalima kahawa hapa nchini.

Hii inatokana na ukweli kuwa, bei ya kahawa imekuwa  chini  kwa asilimia zaidi ya 50.

Ukweli ni kuwa, wanachi bado hawajawezeshwa kujimudu kiuchumi na kuingia katika kilimo cha kisasa. Labda hapa Serikali ijiulize kuwa, wakati inasema uchumi umekuwa na kuhimiza mabadaliko katika sekta ya kilimo, imefanya uchunguzi wa kina kubainisha  kwanini hadi sasa, jamii inatumia jembe la mkono badala ya jembe la ng’ombe au trekta?

Imefanya uchunguzi kujua sababu za madai kuwa wananchi wa mipakani wanauza mazao nje ya nchi, badala ya kuunza nchini? Kama imechunguza majibu sahihi ni yapi?

Ni dhahiri wakulima wanafikia hatua hiyo kutokana na ukosefu wa soko imara na linalowalinda wakulima na maslahi yao.

Sekta ya kilimo imekuwa haina uhusiano wa jirani na sekta nyingine.

Ushahidi wa kihistoria unaonesha kuwa, hata nchi za Magharibi zimepata maendeleo kutokana na uhusiano wa sekta ya kilimo na sekta nyingine kama viwanda.

Hapa kwetu wananchi wamekuwa wakiendelea kufuata mfumo wa kikoloni ambao ulimfanya mwananchi kuzalisha mazao yaliyotumika kama malighafi katika nchi za Ulaya.

Hali hii imewafanya wananchi kulima mazao yao na kuendelea kupeleka nchi za nje kwa kukosa viwanda ambavyo vingeweza kumeza malighafi hizo na hivyo, kuwafanya wakulima kuendelea kupangiwa bei za chini za mazao yao na kuendelea kuitikia, hewala!

Lakini, tumefika mahali ambapo wakulima hawawezi tena kusema hewala kwa kuwa gharama za uzalishaji imekuwa kubwa na hivyo, kuanza kung’oa hata mazao yaliyopo shambani.

Pia, katika vijiji vingi nchini, njia za usafirisha  mazao kuja mjini hazipitiki kiasi kwamba  baadhi ya bidhaa huishia kuharibikia njiani pindi mazao hayo yanapokuja mjini kuuzwa.

  Siyo jambo la kushangaza kuona kuwa katika mkoa mmoja, wilaya moja ina chakula cha kutosha wakati wilaya nyingine ina uhaba mkubwa wa chakula na inashindikana kupeleka chakula katika wilaya yenye uhaba kutokana tatizo la barabara.

Kutokana na ukweli huu wa chakula kuwa mashakani inaniaminisha kukubaliana na   taarifa  ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa uliojadili mpango wa maendeleo endelevu (WSSD), hivi karibuni jijini  Johanenesburg, Afrika Kusini kuwa, hali ya chakula katika nchi nyingi za Afrika ni mbaya  ikiwemo Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nchi nyingine ni Angola, Zimbabwe, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Eritrea, Ethiopia, Guinnea, Kenya, Lethoto, Liberia, Malawi, Mauritania, Msumbiji, Sierra leone, Somalia, Sudan, Swaziland, Uganda na Zambia.

Leo, tunafurahi kuona Serikali inatilia mkazo katika suala zima la  kilimo  cha umwagiliaji, kwa kuwa  inaonesha nia madhubuti ya kuweza kumkomboa mwananchi wa  kijijini, lakini pengine kitu cha kujiuliza hapa ni mipango gani Serikali imefanya ili kumfundisha huyu mwananchi aina hii mpya ya kilimo cha umwagiliaji? Ama  ni wimbo uleule wa  kilimo ni uti wa mgongo sasa umegeuka kilimo cha umwagiliaji?

Kilimo cha umwagiliaji kinahitaji mtaji kukiendesha, kwa mfano utaalamu wa kutosha wa kuchimba mifereji ya kudumu kutoka katika vianzio mbalimbali vya  maji.

Pia, mashine za kuvutia maji ambazo zote zinahitaji pesa. Hata hivyo, swali ambalo bado linasumbua ni kuwa, kama mkulima huyu wa kijembe cha mkono ameshindwa kulima kwa jembe la maksai, atapata wapi uwezo wa kununua hiyo pampu ya kuvutia maji kama  siyo kurudi katika hali ileile?

Jibu bado lile lile kuwa Serikali inahitaji kutafuta njia za kumwezesha mwananchi ili aweze kumudu kilimo cha kisasa ambacho taifa letu linakubali kuwa ndicho uti wa mgongo na kinatoa ajira kwa  wananchi wake kwa asilimia zaidi ya 75.

Serikali kwa  mfano, itoe  mikopo kwa  wakulima ili waweze kupata mtaji, vinginevyo  wananchi wataendelea kuwa na uwezo mdogo wa kiuchumi na hivyo, kushindwa kupata maendeleo  kwa taifa  kama vile elimu na  kuwaachia wageni kuwekeza katika kila sekta.

Nasema taifa litaendelea kushindwa kupata maendeleo katika elimu kwa kuwa hata mazingira ya elimu hususan katika shule za msingi vijijini, yanatisha.

Ingawa ni wazi kuwa hivi sasa kuna shule nyingi hata za sekondari, hebu tujiulize kuwa watoto wengi ambao ni wa wakulima wasio na soko la uhakika, watawezaje kumudu gharama za kusomesha watoto wao katika shule hizo?

Ni nani asiyejua kuwa hata imani na ongezeko la tiba za asili na imani za ushirikina, zinatokana na wazazi na jamii kwa jumla kushindwa nenda rudi za hospitali ambazo hatima yake ni malipo yanayotolewa kwa namna yoyote inayoweza kuitwa?

Ni wazi ingawa jamii inahimizwa kujiletea maendeleo na inaitikia kujenga shule, lakini bado shule nyingi hazina vyumba vya kutosha vya madarasa, madawati ya kutosha  hata walimu.

Ukweli huu pia, umeelezewa vizuri katika ripoti iliyowasilishwa na ujumbe wa UN katika Mkutano kati ya Maafisa wa Tanzania na Ujumbe wa Shirika la Kimataifa la Fedha (IFM), likiongozwa na  Mkurugenzi Mtendaji, Korst Kohler, hivi karibuni

Katika ripoti hiyo, takwimu zinaonesha kuwa, kiwango cha uandikishaji  kwa watoto kimekuwa kikipungua kwa Tanzania Bara ukilinganisha na Visiwani.

Kwa mfano, kati ya mwaka 1990 na 1999, kiwango cha uandikishaji Tanzania bara kiliongezeka kwa asilimia 2.9 tu, wakati  Visiwani, kati ya  mwaka 1990 na 1997 kiwango cha uandikishaji kilikuwa asilimia 16.1 . Kwa mwenendo huu, ripoti inasema kuwa kutekeleza kwa ukamilifu mpango wa kuhakikisha kuwa watoto wenye umri wa kwenda shule ifikapo 2015 kutashindikana.

 Uhaba wa vyumba vya madarasa, ufukara wa wazazi, mgawanyo mbaya wa walimu ambapo sehemu za mjini walimu ni wengi zaidi ya vijijini ambapo pia, baadhi ya sehemu kumekuwa hakuna walimu ni mambo ambayo tumekuwa tukiyashuhudia kila siku.

Hali hii inaonesha picha ya mazingira ya wananchi wa vijijini hapa nchini kuwa ni ya kimasikini ndiyo maana watu wengi wamekuwa wakikimbilia mijini kwa kuogopa ukali wa maisha ya vijijini.

Kutokana na ugumu kwa wananchi wengi walioko vijijini na kutokuwa na elimu ya kutosha, ndiyo maana hata baadhi ya magonjwa ambayo yangeweza kutibika  yanasababisha vifo  vingi kwa  watoto wadogo na  mama  wajawazito.

Kwa mfano, ugonjwa wa malaria unaweza kuepukwa kirasihi kwa kuzuia mazalio ya mbu badala ya kutumia  fedha  nyingi za Serikali kwa kununua vyandarua na dawa  za SP ambazo zimekuwa gumzo  kila kukicha.

Uthibitisho wa kitaalam unaonesha kuwa, ugonjwa wa malaria ni miongoni mwa magonjwa matatu makubwa yanayolisumbua taifa letu ukiongozwa na UKIMWI wakati ugonjwa wa kifua kikuu  ukiwa ni watatu.

Takwimu zinaonesha kuwa  kila dakika moja watu 5 wanakufa  kwa ugonjwa wa malaria ambapo watoto na wanawake wajawazito ndiyo wanaoongoza.

Kwa maana halisi ni kuwa kutokana, na umasikini unaowakabili wananchi walio wengi waishio vijijini (wakulima), unawafanya wawe na maisha ya duni ya kukosa  huduma  muhimu za jamii.

Suala la msingi hapa ni kwa Serikali  kuwawezesha wananchi walio wengi  kujimudu kiuchumi kwa kuwasaidia kuwapa nyenzo muhimu zitakazowasaidia katika kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa taifa na kuihusisha sekta ya kilimo na sekta nyingine  kama vile viwanda na miundo mbinu ili wakulima wawe na soko la kuaminika ndani  na nje ya nchi.

Ni vema Serikali inapotathimini kwa jumla suala la kukua kwa uchumi, iangalie wastani wa maisha ya wananchi wengi, labda zaidi izingatie vijijini kuliko kutazama mjini ambapo kuna mlolongo wa magari yanayokosa pa kupita huku, barabara za vijijini (kama zipo) zikipitwa na gari moja kwa kutwa.

Kwa mtaji huo, ni vipi wastani wa maisha ya Mtanzania ukue badala ya kushuka? Tujiulize, ni wazi sasa kuna uwezekano mkubwa watu wengi wana mawasiliano ya simu zikiwamo za mkononi, je hali ikoje kwa wale wa vijijini; wanzao, na hata kama itatokea muuijiza sasa vijijini wakawa nazo, kipato chao kitawawezesha kulipia gharama za matumizi ya simu hizo? dola tano kutwa wakati uwezo wao wa kuishi kwa kutwa ni nusu dola.

Umeme ambao ni nishati muhimu inayowarahisishia watu utendaji kazi ukiwamo usagishaji, unawafaa vipi Watanzania wa vijijini?

Kama mifano hiyo haiwafai wala kuwanufaisha kwa lolote Watanzania wa vijijini,  hivyo, Serikali inaposema uchumi umekuwa inaangalia nini, nyumba za mijini au hata za vijijini?

Labda umefika wakati, kigezo cha maisha mazuri kwa wananchi na kukua kwa uchumi wa nchi kutazamwe kuanzia vijijini kule ambako mjamzito anapelekwa hospitali kwa mkokoteni wa kukokotwa na punda si mjini ambapo barabara ni chache gari ni nyingi huku kila mmoja akiwa na la kwake.

Tanzania kubwa iko vijijini siyo mijini.

MAKALA YA UINJILISHAJI

Jimbo Katoliki la Same lapiga hatua kumkomboa mwanamke

l Lina kitengo kuhudumia watoto yatima,wenye mtindio wa akili

MAJIMBO mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini,yamebuni miradi mbalimbali ya kumwendeleza mwanamke kiroho na kimwili likiwemo suala la  kumwinua kiuchumi. Miradi hii inaendeshwa kulingana na hali halisi ya eneo husika. Miongoni mwa Majimbo hayo ni Jimbo la Same ambalo kwa kiasi kikubwa limefanikiwa katika azma yake ya kumkomboa mwanamke kama Makala haya ya Mwandishi Dalphina Rubyema inavyoleza kama alivyohojiana na Askofu wa Jimbo hilo, Mhashamu Jacob Koda.

“Nadhani jimbo  lolote lile haliwezi likaendelea bila kujishughulisha na shughuli za maendeleo ya akina mama katika mambo mbalimbali yakiwemo ya uchungaji na maendeleo ya kiroho na kimwili”ananza kueleza Askofu wa Jimbo Katoliki la Same,Mhashamu Jacob Koda.

Anasema akina mama kwa vyovyote vile lazima wahusishwe katika shughuli zote za maendeleo  na uchungaji.

Akielezea jinsi gani Jimbo lake linavyojihusisha na suala hili,Mhashamu Koda anasema mwanzoni shughuli za maendeleo jimboni humo lilikuwa linaangaliwa kwa ujumla bila kujali masuala ya jinsia.

Anasema katika kumkomboa mwanamke, pole pole jimbo liliianza kuangalia shughuli zinazomuhusu mama na jamii,mama na familia na suala la mama na mtoto.

Anasema katika kutimiza lengo hilo, kitu cha kwanza ilikuwa ni kuwandaa akina mama kuwa makini  kujitambua kwamba nafasi yao ni hii katika jamii na namna gani watashiriki kikamilifu katika kujikwamua kutokana na ile hali ya ugumu wa maisha na masuala yanayo wakandamiza.

Mhashamu Koda anasema kati ya mambo waliyobaini kwamba suala la mila na desturi linachangia katika kumkandamiza mwanamama likifuatiwa na suala la  umaskini uliokithiri katika famili.

Vile vile walibaini kuwa  akina mama hawashirikishwi katika kufanya maamzi juu ya masuala mbalimbali.

Baada ya kubaini hayo,lilifuatia suala la kuanzisha shughuli za maendeleo katika jamii  ambapo akina mama walihamasishwa kuanzia ngazi ya familia na kupitia kwenye jumuiya ndogo ndogo.

Anabainisha kuwa baada ya hapo liliangaliwa suala la mama na mtoto yaani namna ya kumuandaa mama  katika shughuli za kumlea kijana ambaye atashughulikia familia hapo baadaye.

Anasema juhudi hizo hazikuishia hapo kwani lilifuatia zoezi la kukabiliana na mila potofu zinazomkandamiza mwanamke kama ukeketaji.

“Sasa baada ya kukamilisha hayo, tukafikiria namna ya kuwapa nguvu viumbe hao (wanawake) ikiwa ni kuanzisha miradi ya kuwaingizia kipato. Na hivyo vyote wanasimamia akina mama wenyewe”anasema Mhashamu Koda.

Anasema katika kuhakikisha kila mwanamke anajikomboa,akina mama jimboni humo walijiwekea utaratibu wa kupeana mikopo  ambapo kwa wale ambao hali zao kiuchumi siyo mbaya,wanawakopesha wale wenye uwezo mdogo.

Vile vile Askofu huyo anasema baadhi ya vijiji jimboni humo vimeweza kupataiwa huduma ya maji,tatizo ambalo lilikuwa linaonekana kuwa sugu.

“Akina mama wanapata shida sana katika suala la kupata maji. Kwa hiyo kitu kimojawapo tumebuni vile vile mradi wa kuwapatia watu huduma ya maji”anasema.

Vile vile wamama hao wamepata miradi ya kutengeneza majiko ili waweze kukabiliana na utunzaji wa  mazingira badala ya kukata miti kwa ajili ya kuni, wanatumia  majiko bora ya kisasa pamoja na kutengeneza maghala kwa ajili ya kuhifadhi chakula ili visiweze kuharibika.

Katika kuhakikisha kwamba akina mama wanafauli katika shughuli zao hizo, Mhashamu Koda nasema kuwa jimbo limeweka mpango unajulikana kama Maendeleo na Jinsia (Gender and Oriented Development Programme).

“Kwanini hatukuuita mpango wa Maendeleo ya Akinamama (WID),ni kwasababu kidogo tunasema ukichukulia suala la jinsia  lihusishe  upande mmoja tu, kama ikitokea matatizo  watashindwa kumuhusisha baba”anasema.

Anasema pia akina mama jimboni humo hawapo nyuma katika suala zima la mapambano ya UKIMWI ambapo anasema kuwa wamejidhatiti katika kuwaelimisha wasichana chini ya mpango maalumu wa kupitia vijiji vile vilivyoathiriwa zaidi na suala hili la UKIMWI pamoja na  mpango mzima wa kuwahamasisha akina mama kukwepa vitendo vile vinavyoweza kuwapelekea kupata ugonjwa huo.

 “Vile  vile kuwasaidia wale waathirika wa ugonjwa huo wa UKIMWI ambao wameweza kujitokeza katika vituo vya afya”.

Mhashamu Koda anasema kuwa pia kuna baadhi ya akina mama ambao  wanachukuwa majukumu ya kuwalea watoto ambao wazazi wao wamefariki kutokana na  UKIMWI.

Hata hivyo anabainisha kuwa watoto wanaosaidiwa na jimbo hilo si wale ambao wazazi hao wamekufa na UKIMWI tu bali hata wale watoto wenye ulemavu wa viungo mbalimbali na wenye mtindio wa ubongo ambao wanapata malezi chini ya  kitengo kinachohusiana na malezi ya watoto.

Alibainisha mikakati waliyonayo katika kuhakikisha kwamba jinsia inaingia katika kila kitengo pale jimboni,Mhashamu Koda anasema jambo  la kwanza ilikuwa ni kuhamasisha na kujenga uwezo  kwa upande wa viongozi pamoja na kuandaa utaratibu wa  kutoa semina na warsha mbalimbali katika kuhamasisha .

Anasema pia akina mama hao pia wanawaalika watu wa vitengo mbalimbali katika ofisi nyingine ili waweze kushiriki kikamilifu katika   taratibu za mendeleo.

Vile vile akina mama hao wanaendesha semina zinazohusisha jamii nzima mfano wameisha endesha semina za kuhamasisha mapadre ,watawa na viongozi wa Baraza la Walei waliochaguliwa juu ya wajibu wa akina mama na vile vile mambo ya jinsia.

.Kwa upande wa matatizo,Askofu huyo anasema mengi yanatokana na mabadiliko ya uchumi katika Ulimwengu.

Sinza; ibada chini ya mkorosho hadi Kanisa la milioni 300! Hongera

Na Peter Dominic

 

WAAMINI wa Parokia ya Sinza, katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es salaam, ambao walianza kuendesha ibada zao chini ya mti wa mkorosho, ndio hao wanajenga kanisa la shilingi milioni 300. Si rahisi kuamini, lakini ndiyo hali halisi.

Hali hii inayooneshwa na waamini wa Parokia hii kuchangia ujenzi wa Kanisa hilo kwa hali na mali, inaonesha kuwa Watanzania sasa wamefika mahala wameelewa na kukubali kuwa, maendeleo ya watu, huletwa na watu wenyewe na wala hayanunuliwi dukani wala kukopwa dukani.

Kama waamini hawa wangekaa siku zote kimya na huku wakiimba wimbo wa HATUNA UWEZO WA KUJENGA KANISA, ni wazi kuwa hadi sasa hata uwezo mdogo ambao wangefikiriwa kuwa nao, tayari ungekuwa umekwisha na wangetajirika kwa lawama na msimango lakini, sasa juhudi kama hizo wanazofanya kujiletea maendeleo ya kiroho na kimwili kwa kujitegemeza, sijui wanaojua umuhimu wa maendeleo watakuwa na namna gani nzuri ya kuipongeza kazi hiyo.

Ni wazi kama wasingeamua kuvuta na kuvaa ujasiri huo, kila mwanajamii angegombea nafasi ya kuwaponda na kuwalaumu kwa kujilimbikizia utajiri wa uvivu, lakini sasa hali ni kinyume, wanafanya lililo jema, pongezi ni haki yao.

Uwezekano wa kujenga kanisa la namna hiyo, ni wazi kuwa umegharimu nafasi kubwa ya waamini kufanya mambo mengine hata katika familia zao, lakini kwa kutambua umuhimu wa kuwa na mahali panapostahili jamii kufanyia ibada, wamefanya hili lililo jema

Huku wakijituma kwa nguvu zao zote ili wafikie malengo.

Hii ni pamoja na kupunguza ama kuepuka kabisa gharama zote zisizo za lazima ili kujinyima mambo mengi ambayo wangeweza kuyafanya maishani mwao likiwemo suala zima la starehe.

Tukichukulia suala la ujenzi wa nyumba za kisasa,mara nyingi watu huwa wanajiuliza kwamba nyumba nzuri namna hii, huyu mwenye kuimiliki katumia kiasi gani cha fedha kukamilisha ujenzi wake,bila shaka huyu atakuwa ni bilionea au kafoji lakini je, madai kama hayo yana msingi kwa mwenye akili timamu?

Ukweli ni kwamba mtu huyo unakuta ni wa kipato cha kawaida tu,na pengine kima chake cha mshahara ni cha kati tu,ili mradi kabla hajajihusisha katika ujenzi wa nyumba yake, alihakikisha anaweka mikakati ambayo pia aliiheshimu, wala haijalishi ana kipato kiasi gani. Malengo yake yatatimia hasa akiunganisha imani na matendo sahihi.

Watu wengi ambao kwa sasa hali zao kimaisha ni nzuri, historia yao inaonesha kuwa walichumia juani sana, lakini sasa wanafaidi matunda ya jasho lao wakiwa kivulini.

Vivyo hivyo, hata wadau wa sekta mbalimbali zikiwemo za kidini, maendeleo yao hupatika kutokana na kujituma kwa hali ya juu, kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, si lelemama wala kutegemea misaada.

Parokia ya Sinza imekuwa mfano na kioo kizuri kwa wanakanisa wengine kukubali usemi kuwa penye nia, pana njia na kwamba, kutoa ni moyo wala si utajiri.

Paroko wa Parokia hiyo Padre Felix Kisaka (SDS), anasimulia historia ya Parokia yake na namna walivyomudu kutoka chini ya mkorosho hadi sasa wako katika ujenzi huo mzito.

“Kwa mujibu wa historia niliyoikuta hapa kutoka kwa wakuu walionitangulia, waamini wa eneo hili walikuwa wakiendesha ibada chini ya mkorosho na banda bovu, lakini ushirikiano mzuri wa viongozi na waamini ulifanikiwa kuondoa hali hiyo na enzi hizo kilikuwa kigango kilichokuwa chini ya Parokia ya Mwenge”.

Anasema pengine juhudi hizo ndizo zilizomfanya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kukitangaza Kigango hicho kuwa Parokia, Desemba,1997.

Hata hivyo, Padre Kisaka anasema kuwa, ili kuuhakikishia umma kwamba waamini wa Parokia hiyo hawajachoka katika ujenzi wa nyumba za ibada, hivi sasa wanaendelea na ujenzi wa kanisa jipya ambalo hadi kukamilika kwake, linatarajiwa kutumia milioni 300.

Anasema, “Kanisa hilo ambalo ujenzi wake uko katika hatua za mwisho, lina uwezo wa kuchukuwa watu 1,400 kwa wakati mmoja.”

Padre Kisaka anasema mafanikio hayo hayatokana na juhudi zake na waamini pekee, bali pia yanatokana na juhudi za Paroko aliyemtangulia,Padre Afrika Lokilo ambaye alichukuwa nafasi ya Paroko wa kwanza wa Parokia hiyo, Padre Eugene Reslinski (SDS).

Matayarisho ya ujenzi wa kanisa hilo yalianza tangu mwaka 1999 na jiwe la msingi liliwekwa Oktoba mwaka jana (2001) na Kardinali Pengo

Padre Kisaka ambaye alifika parokiani hapo Machi 24, 2002, anasema moyo wa ushirikiano unaooneshwa na waamini wake, unampa nguvu zaidi na anaamini kuwa malengo waliyojiwekea yatatekelezwa.

“Nawashukuru waamini kwa  moyo wa kujitoa pamoja na wahisani kwa vile wameweza kutoa michango ya hali na mali ambayo imewezesha ujenzi wa kanisa kufikia hapa ulipo. Kwa kweli ni jambo la kumshukuru Mungu,” anasema.

Anasema, shughuli za ujenzi wa kanisa haziweki kikwazo kwa uongozi wa parokia  kutoa huduma za kiroho na kimwili kwa waamini wake.

Anasema kanisa linatoa huduma hizo kupitia jumuiya ndogo ndogo za kikristo na vyama vya kitume.

Hata hivyo, Paroko huyo pamoja na kusifia kazi nzuri inayofanywa na vyama vya kitume, bado anasisitiza kuvilinda vyama hivyo katika kuhakikisha vinafanya kazi yake kwa kufuata mafundisho sahihi ya Kanisa.

“Lazima vyama vya kitume kuhakikisha kwamba vinafuata mafundisho sahihi ya imani, usipovisimamia vizuri ni vigumu kupata nguvu,” anasema.

Naye Mwenyekiti wa Parokia  hiyo Bw. Samweli Ntunduye pamoja na kutoa shukrani kwa waamini wa Parokia hiyo ya Sinza,vile vile ametoa changamoto ya kukubali mabadiliko yanayotokea parokiani hapo kuelekea maendeleo.

Anasema waamini wanatakiwa kutambua kuwa michango mbalimbali inayotolewa parokiani inalenga kujenga na kuimarisha parokia na Kanisa kwa jumla na si vinginevyo.

“Parokia ni yako, ni mahala pa kupata chakula cha roho, ni bora Wakristo wakajitoa kwa moyo na kufuta dhana potofu iliyojengeka miongoni mwao kwamba michango wanayoitoa inamnufaisha Paroko na maendeleo haya hata mimi yananifurahisha kwa sababu yanatoa picha kwa wanaokwaza wengine kushiriki vema.”

Anasema dhana hiyo haijengi na badala yake, inasababisha migogoro na kueneza chuki kati ya Paroko na waamini wenyewe.

“Ninachomba ni moyo wa ushirikiano, tufute mawazo potofu, tujitoe  kikamilifu kwa kuboresha na kujenga parokia yetu tukijua kabisa kuwa ni wajibu wetu kuwa waaminfu na wakweli mbele ya Kristo,” anasema.

Bw, Ntunduye anasema kuwa kufuatia ufinyu wa eneo la kujenga, kuna uwezekano wa kujenga jengo la ghorofa mbili ili kupatika eneo la ofisi na ukumbi wa mikutano.

“Unajua tuna tatizo la eneo, inabidi tutumie eneo hili dogo tulilo nalo, lakini kuna uwezekano mkubwa wa kujenga jengo la ghoroga mbili na zoezi hili linaweza kutekelezwa baada ya kukamilisha ujenzi wa jengo la kanisa,” anasema.

Kwa mujibu wa habari zaidi zilizopatikana parokiani hapo, miongoni mwa mitindo inayotumika kuongeza kipato cha Parokia katika Mfuko wa ujenzi, ni kwa muumini yeyote kupendekeza rangi au aina ya mabati ya kuezekea kwa kuchangia pesa; hivyo rangi au aina itakayokuwa na wafuasi waliochanga pesa nyingi, ndiyo itakayotumika.

Mtindo huo unaonekana kupokewa vizuri na waamini wameupenda kwani unawafanya wachangie kwa hiari zaidi.