Vatican yataka utafiti wa viinitete vya binadamu upigwe marufuku

l "Ni kashfa dhidi ya thamani ya mtu"

 l  California yakiuka sera ya Bush, yahalalisha utafiti huo

 

Na Eric Samba

Hivi karibuni Umoja wa Mataifa kupitia Kamati yake ya Sheria ya Kimataifa Dhidi ya Uzalishaji Watu kwa njia ya kuunganisha chembe hai za binadamu bila kupitia njia za asili, ulifanya mkutano uliojadili pamoja na mambo mengine kupiga marufuku uzalishaji huo. Katika mkutano huo Vatican kama kawaida iliwakilishwa na mjumbe wake wa kudumu katika Umoja wa Mataifa, Mhashamu Askofu Mkuu Renato Martino.

Katika mkutano huo Askofu Mkuu Martino alizishauri serikali na wadau wengine katika utafiti wa kisayansi juu ya viinitete vya binadamu kupiga marufuku utafiti na majaribio yoyote katika eneo hilo.

Alisema kuwa msimamo wa Vatican juu ya suala hili unajulikana sana. Vatican inaunga mkono na kushauri upigaji marufuku ulimwenguni kote tafiti zote juu ya uzalishaji watu kwa kutumia viini tete vya binadamu, na pia kwa malengo ya kisayansi.

Utafiti wa kutumia viinitete vya binadamu, hata pale unapofanyika kwa jina la kuboresha maisha ya binadamu, bado ni kashfa dhidi ya heshima ya mtu.

Utafiti wa kutumia viini tete vya binadamu unazuia ujinsia wa binadamu na uhusiano wa kingono pamoja na kufanya maisha ya binadamu kuwa kama biashara.

Kama Papa Yohane Paulo wa Pili alivyosema hivi karibuni, “Maisha ya binadamu hayawezi kuonekana kama kitu tunachoweza kufanya kama tunavyotaka, ni kitu kitakatifu sana”.

Aliongeza “hapawezi kuwepo na amani ya kweli iwapo kitu hiki chema kimsingi hakitatunzwa.

Katika orodha ya uvunjaji wa haki duniani, ni lazima tuongeze, vitendo visivyowajibisha vya uhandisi wa kinasaba (genetic engineering) kama vile uungaji wa seli za binadamu na matumizi ya viinitete vya binadamu katika utafiti, ambavyo vinahalalishwa kwa visingizio visivyo halali vya kuwa vinaonesha uhuru, maendeleo ya kiutamaduni na maendeleo ya binadamu kwa jumla.”

Pia alisisitiza kwamba “pale watu dhaifu na walio rahisi kudhurika katika jamii wanapokabiliwa na maovu ya aina hiyo, dhana nzima ya familia ya binadamu iliyojengwa juu ya tunu ya mtu-nafsi, imani, heshima na kusaidiana, inamomonyolewa vibaya kabisa. Usitaarabu uliojikita kwenye upendo na amani lazima upinge mambo haya ambayo hayana mema kwa binadamu.”

Alisema kuwa kwa msingi wa hadhi ya kibaiolojia na kianthropolojia ya viinitete vya binadamu na juu ya msingi wa maadili na utawala wa sheria ni haramu kuua asiye na hatia hata kama ni kwa lengo la kuleta mema kwa jamii.

Alisema kwamba Vatican inachunguza utofautishaji kati ya lengo la “kuzalisha watu” na kile kinachoitwa lengo la “kitabibu” (au “majaribio ya kisayansi”) ili kuona kama uungaji seli za binadamu kama unaweza kukubaliwa.

Alisema kuwa utofautishaji huu unaficha ukweli juu ya uumbaji wa binadamu kwa kusudi la kumharibu ili kuzalisha seli shina za viinitete au kufanya majaribio ya kisayansi.

Alisisitiza kuwa uunganishaji wa viinitete vya binadamu ni lazima upigwe marufuku kwa kila kesi bila kujali malengo yanayokusudiwa.  Itaendelea Toleo lijalo

Kardinali Pengo na Mji wa Yesu

Na Peter Dominic, Mkuranga  

HIVI karibuni, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliweka jiwe la msingi  kuruhusu ujenzi wa Kanisa katika Parokia ya Vikindu, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam. 

Kanisa hilo linalotarajiwa kuchukua waamini 400, linajengwa katika eneo liitwalo Mji wa Yesu (Jesus Town), baada ya Parokia hiyo kukosa kanisa la kuendeshea ibada zake kwa muda mrefu.

Kwa wakati wote huo, ibada zilikuwa zikifanyika katika banda bovu lililotishia usalama wa maisha ya waamini.

Parokia ya Vikindu ilianzishwa na Mkristo mmoja Bw. Joseph Namiva kutoka Jimbo Katoliki la Zanzibar, mwaka 1960. Wakati huo ikiwa kama jumuiya ndogondogo na imekuwa ikiendelea kupata waamini hadi ilipotajwa kuwa kigango.

Kutokana na ongezeko la waamini aliyekuwa Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Marehemu Mwadhama Laurian Kardnali Rugambwa, mwaka 1969, alilitaja eneo hilo la Vikindu kuwa kigango.

Historia ya Parokia hiyo imechangiwa na watu mbalimbali lakini wanaokumbukwa sana ni Bw. Joseph Mtahagarwa, ambaye mwaka 1980, alitoa ekari kumi za eneo lake kwa ajili ya matumizi ya Parokia.

Kisha, mwaka 1996, akatoa nyingine 8 kwa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo na Bw. Joseph Namiva aliyeanzisha jumuiya miaka ya nyuma.

Mapadre wa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo kutoka Karela nchini india walifika katika eneo hilo la Vikindu mwaka 1997 kuanza mara moja, kazi ya kichungaji na mara moja waliliita eneo hilo kuwa ni Mji wa Yesu (Jesus Town) kutokana na mandhari yake ya kuvutia.,

Ilikuwa ni sehemu ambayo imekwa ikipambwa kwa miti mifupi na majani mafupi na kusudio lao la kulifanya eneo hilo kuwa la miradi mingi ya kutoa huduma kwa jamii kiroho na kimwili.

Kibao kilichowekwa katika eneo hilo lililotulia likiwa na upepo mzuri kilicoandikwa kwa herufi kubwa (Jesus Town) kinakujulisha moja kwa moja eneo hilo. 

Jina hilo sasa si geni miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, hata kwa wale wanaosafiri kwa basi kuelekea katika Wilaya ya Mkuranga.

Awali kabla ya kufanywa Parokia, ilikuwa chini ya Parokia Katoliki ya Mbagala Zakhem. Mchango mkubwa uliotolewa na Paroko wa Parokia ya Mkuranga Padre Patric (SDS), umeiwezesha Parokia hiyo kuweka msingi kwa hatua ya awali.

Lakini, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo,akiizindua Januari 21 mwaka 2001, Parokia hiyo haikuwa na kanisa la kudumu. Ilikabidhiwa kwa Mapadre hao wa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo ambao walishirikiana vema na Paroko wa Parokia ya Mkuranga.

 Parokia hiyo hadi sasa ina vigango saba (7).

 “ Shida iliyopo hapa ni waamini, wapo wachache sana ni karibu familia 50 za Kikristo, wanaonesha moyo wa ushirikiano tatizo wengi wao wana kipato kidogo,” alisema Paroko.

Kituo hicho kinachotoa huduma kwa wajawazito, watoto na huduma nyingine za afya, kilizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa na kubarikiwa na Kardinali Pengo Agosti  21, 2002.  Kardinali Pengo aliweka jiwe la msingi kituoni hapo Agosti 21, 2001.

Paroko huyo alisema hata hivyo hali ya utulivu iliyopo nchini inatosha kuleta maendeleo kwa vile ni tofauti na kwao (India) ambapo kuna mapigano ya hapa na pale ya ya Kanisa Katoliki.

“Utulivu na ushirikiano kati ya madhehebu unatosha kuendeleza kazi ya kichungaji, tunashirikiana vizuri na Serikali na madhebu mengine ya kidini.”alisema.

Mashirika mengine yaliyofika na kuanzisha makazi yao ni pamoja na Shirika la Kitawa la Masista wa Mtakatifu Vincent wa Paulo kutoka Austria waliofika Vikindu mwaka 2000. Watawa hao tayari wamejenga kituo cha afya na shule ya awali.

Paroko Padre Jemes alisema, eneo hilo hata hivyo siyo la Shirika moja tu la bali wanajitahidi kuyahimiza mashirika mengine yafike na kuanzisha makao yao. “ Huku siyo pabaya tunashukuru kuwa Serika imejenga barabara nzuri;… lakini kama ingejenga barabara za kuelekea vijijini ndani zaidi nadhani maendeleo yangekuwa makubwa zaidi”.

Shirika lingine lililoweka makao yake ni lile na Masista wa Mama wa Karmeli kutoka nchini India waliofika Vikindu mwaka 2001 amabao tayari wamejenga makazi yao na nyumba ya malezi ya kwa ajili ya wasichana. Makazi hayo yamezinduliwa hivi karibuni.

Akiweka jiwe la msingi hivi karibuni, Kardinal Pengo alimtaja Msimamizi wa Parokia hiyo Mtakatifu Vincent wa Paulo kuwa alipenda kuishi maisha ya kimasikini na kuwasaidia fukara, pia alipendelea zaidi kuwalea mapadre katika hali hiyo. “Maana ya ufukara wa Mt. Vincent alikuwa na nia ya kuwahubiria masikini habari njema,” alisema.

Alisema mara nyingi mafukara wamekuwa wakijiona kama kwamba hawana mchango wowote mbele ya jamii na kwa Mwenyezi Mungu ndiyo maana Mtakatifu huyo aliona haja ya kuwa karibu na kundi hilo la mafukara ili watambue mchango na umuhimu wao.

“ Kuwasaidia masikini ni wajibu wetu sisi tulio katika hali nafuu,” alisema Kardinal Pengo.

Alifafanua kuwa, jukumu la kuwasadia wanyonge, maskini na fukara ni la kila mmoja na kwa wakati wake.

 “Mwenye uwezo asiridhike kukaa katika hekalu la Bwana, bali wenye uwezo na mafukara tunapata faraja kwa Mungu,” alisema. Akaongeza, “Mtu asiseme kuwa kama nisingalikuwa mimi Kanisa lisingalikuwapo, bali sote tuna hadhi sawa mbele ya Mungu”

Kardinal Pengo alisisitiza kuwa Kanisa siyo mahari ambapo fukara wanajiona kuwa hawawezi kukaa hivyo kusukumizwa pembeni, bali fukara na tajiri wana uwezo sawa mbele ya Mungu.

Kamati ya harembee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa hilo ikiongozwa na Mbunge wa CCM Viti Maalum, Bibi Janeth Kahama, Brigedia Msitaafu Jerali Francis Mbena, Katibu wa Parokia , Luten Mstaaf Mgaya, Bw. Peter Macha, na wajumbe mbalimbali  walipata shilingi milioni nane (8) ambapo michango ya papo kwa papo ilipatikana shilingi laki tano (5).

Jengo hilo litakaloweza kuchukua waamini 400 litagharimu kiasi cha shilingi milion 155.

Kardinali Pengo aliwatia moyo waamini wa Parokia hiyo kuwa, “Msione aibu kuitwa ombaomba sisi sote ni ombaomba.”

Uamsho ni Ulokole katika Ukatoliki? (2)

Inatoka Toleo lililopita

Hicho ndicho kikundi cha Karismatiki au Uamsho. Kuanzia Papa Paulo wa Sita, Baba Mtakatifu alianza kutamka na kukubali kikundi hicho cha Uamsho. Papa  John Paulo wa Pili huyo kabisa kwa sehemu mbalimbali na kwa nyakati mbalimbali ametamka akionesha kukubali hiki Kikundi cha Uamsho kwa kukipa nguvu na wakati ule ule akiwaomba Kanisa, Maaskofu na Watu wengine wakifuatilie kisije kikaenda nje ya mipaka.

Hivyo, Kikundi cha Uamsho ni kitu ambacho kimekuwapo kanisani ila kilikuwa kimewekwa chini kidogo. Sasa kimerudi. Ni kitu ambacho kiko halali.

Sasa, linakuja swali la pili, je,  watu wengine hawajisikii vibaya juu ya hivi Vikundi vya Uamsho?

Nimetembea katika parokia zaidi ya ishirini na saba hivi, nimekutana na Halmashauri za Walei, Maparoko, Vyama vya Kitume; katika zaidi ya nusu ya hizi parokia wameniuliza juu ya suala hili la Uamsho.

Kwamba hiki ni kitu gani, huyu ni mnyama gani anayetaka kutuharibia Ukatoliki wetu na kutupeleka kutufanya tuwe Walokole?

Ni kweli. Ni kitu ambacho kidogo kinaleta mtafaruku katika Kanisa kwa sababu wanasali kwa mara nyingine kwa namna tofauti, wanafanya vitu kwa namna tofauti.

Kila mara niliwaeleza juu ya uhalali wa Uamsho, lakini pili hata nilipowaeleza juu ya masuala yanayohusu Uamsho niliwaeleza kwamba Uamsho hauna maana kama kazi hiyo ya Uamsho haisadii kuamsha (kusisimua) Kanisa mahalia.

Hivyo, katika parokia katika kigango, jumuiya ndogondogo zile karama za Uamsho hazina maana kama hazisaidii kujenga jumuiya nzima ili wale  wana Uamsho wachangie katika kujenga umoja wa jumiya siyo kuleta mtafaruku au kugawanya waamini.

Pili, nikawaambia kabisa kuwa Uamsho unakuwa na maana kama wale Wanauamsho hawajaribu kuwaonesha wengine kwamba wao ni bora zaidi.; kwamba wao wanajua zaidi; wao wana karama zaidi. Karama zote ni sawa kila mmoja anashika karama moja na mwingine anashika karama nyingine.

Nikiwa na watu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, najisikia vizuri sana, ni watu wenye karama nzuri. Ukienda kwa Lejio Maria ni watu wenye karama nzuri sana wana mchango mkubwa sana.

Ukienda kwa wana Uamsho nao wana mchango wao. Lakini inakuwa ni mbaya sana kwa chama chochote cha kitume kikijiona kuwa wao ni bora zaidi ya wengine. Niliwaambia kuwa chama cha namna hii cha kitume hakifai kuwa na nafasi katika Jumuiya ya Jimbo Kuu la Dar Es Salaam.

Ila chama kile ambacho kina unyenyekevu kinachojua kuwa chenyewe ni mojawapo ya vyama vingi vyenye karama nyingi, nao wanafanya juu chini kusisitiza hilo, ukienda kwa mfano katika chama cha wawili katika Kristo (Couples for Christ), hao ni juu ya ndoa. Wanateseka juu ya ndoa. Ni karama nzuri sana ya kujaribu kuwafundisha watu wawe kitu kimoja katika ndoa nao ni karama ya hiyo.

 Kanisa utajiri wake ni kwamba lina karama nyingi mbalimbali, ila karama moja isijione kwamba ni nzuri zaidi ya nyingine na hiyo haikubaliki kabisa.

Tatu, Ili Uamsho ufanikiwe wanapaswa kutambua kuwa huu ni Uamsho wa Kikatoliki.

Bahati mbaya, kwa kuwa walioanza walikuwa Walokole, utakuta mara nyingine katika Uamsho wa Kikatoliki Walokole utakuta wamo humo humo na wanaleta vitu vyao vya Ulokole humo ndani.

Hivyo, Uamsho unakuwa ni kitu ambacho badala ya kuwa vya kufundisha, unakuta unabakia tu ni kitu cha kuimba, kusema lugha na na katika kujaribu kuponya vyote unakuta vinabaki hapo. Uamsho unabaki ni hapohapo ambapo hauna maana.

Uamsho ni kitu kikubwa zaidi. Ni katika kujaribu kuingiza dini katika mtu ili aweze kumuamini Kristo katika roho inayosema, hauwezi kusema Kristo ni Bwana bila nguvu ya Roho Mtakatifu.

Itaendelea toleo lijalo

Mwalimu Nyerere: kuugua, kuuguzwa, kufa na sasa…

OKTOBA 14, mwaka huu, Watanzania wanaadhimisha miaka mitatu tangu kifo cha Baba wa taifa Mwalimu Julius kambarage Nyrerere. siku hiyo pia itakuwa ya maadhimisho ya Wiki ya Vijana na Maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge Mwaka huu, yanayofanyika mkoani Tanga.Ifuatayo, ni historia fupi ya maisha yake, alivyougua hadi kifo.

Marehemu Nyerere alizaliwa Aprili 13, 1922, kijijini Butiama katika Kabila la Wazanaki.

Baba yake, Chifu Nyerere Burito, alifariki mwaka 1942 na mama yake, Mugaya Nyang'ombe, aliyekuwa mke wa 18 wa Mzee Burito, alifariki mwaka 1998, akiwa na umri wa miaka 105.

Katika utoto wake, alijishughulisha na uchungaji wa ng'ombe na kilimo.

Akiwa na miaka 13, alijiunga na shule ya msingiMwisenge, mjini Musoma.

Katika mtihani wa darasa la nane, alikuwa wa nane na alichaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Tabaora iliyokuwa maalumu kwa ajili ya watoto wa watemi.

Mwaka 1943,alijiunga na Chuo Kikuu cha Makelele, nchini Uganda alikohitimu Shahada.

Desemba 23, 1943, alibatizwa na Padre Mathias  Koenen na baba yake wa Ubatizo alikuwa Paetro Masive.

            KUUGUA

Agosti, 1998: Madaktari walifanya uchunguzi na kugundua mwalimu alikuwa na kansa ya  damu na kisha madaktari waliompima walimpa kitabu kinachoelezea athari na namna ya kuishi na ugonjwa huo ambao huweza kudhoofisha kinga ya mwili kupambana na maradhi.

Baba wa taifa aliendelea kufanya kazi zake kama kawaida kwa zaidi ya mwaka mmoja zikwia ni pamoja na kilimo na shughuli nyingine huko kijijini kwake Butiama na shughuli mbalimbali za kimataifa.

Septemba Mosi: 1999: Mwalimu aliondoka nchini akiwaaga baadhi ya Watanzania waishio jijini Dar es Salaam akaenda London Uingereza kushughulikia afya yake na katika safari hiyo, aliambatana na mkewe na David Mwakyusa ambaye ni Daktari wake.

Septemba 24: Baba wa Taifa aliugua ghafla na kupelekwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas alikolazwa akiwa taabani ikiwa ni siku ya 23 tangu awasili London.

Septemba 26: mwaka huu Rais wa Jamhuri ya Muungano wea Tanzania Mheshimiwa Benjamini William Mkapa kwa sauti ya huzuni iliyojaa maombezi aliutangazia rasmi umma kuwa hayati Mwalimu Nyerere alikuwa anasumbuliwa na Kansa ya damu na kwamba hali yake ilikuwa “si nzuri sana” akitoa wito kwa Watanzania wote kila mmoja kwa imani yake kumwombea Mwalimu ili apate  nafuu na kurudi nyumbani Tanzania kuungana na Watanzania wenzake kulijenga taifa lao.

Septemba 29: Kingunge Ngombale Mwiru ambaye ni Waziri wa Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa aliondoka nchini kwenda Uingereza kumjulia hali Msoshalisti mwenzake.

Huko, pia alikuwa na jukumu la kuratibu usambazaji wa habari toka kwa madaktari wanaomtibu.

Siku hiyo pia Mzee Rashid Kawawa mshirika wa mwalimu Nyerere katika harakati za kupigania uhuru wa nchi hii nae aliomba Watanzania kumuombea Baba wa Taifa ili apone haraka.

Alisema “Ninapatwa na huzuni kuona hali ya Baba wa Taifa inaendelea kuzorota… Tunamhitaji sasa kuliko wakati mwingine wowote.”

Ikulu pia ilitangaza kuwa Mwalimu Nyerere amepatwa na matatizo mengine. Alikuwa amekumbwa na ugonjwa wa majano (Jaundice).

Septemba taarifa kutoka Ikulu zilisema hali ya Baba wa Taifa ilikuwa inaendelea vizuri maana kwa mara ya kwanza, sasa alikuwa anaweza kugeuka mwenyewe tangu alipolazwa na siku hiyo alikula chakula kidogo lakini kwa kutumia mpira.

ROHO MKONONI

Ni Oktoba Mosi mwaka huu: Hofu na mashaka ya kumpoteza Mwalimu toka miongoni mwa Watanzania vilitanda na kutawala sana. Mara kwa mara Ikulu ilikuwa na kazi ya kutoa taarifa mbalimbali juu ya maendeleo ya hali ya Baba wa Taifa kwa kila taarifa zilizotolewa baada ya saa tatu, zote zilisema ‘Hali ya Baba wa Taifa inabadilika kuwa mbaya’

Madaktari walisema wanaendelea na juhudi zao za makusudi kupigana kiume ili kuyanusuru maisha yake na alitolewa chumba chenye utegemezi wa hali ya juu kiitwacho High Dependence Unit (HDU) na kukimbizwa Intensive Care Unit (ICU) ambacho ni chumba cha wagonjwa mahututi.

Hata hivyo madaktari waliokuwa wanamtibu walifanya kikao cha dharura kutathimini upya maendeleo ya afya yakena siku hiyo pia Rais Benjamin Mkapa alizidi kuwasisitiza Watanzania kuzidi kumuombea Mwalimu apate nafuu haraka.

Baadaye binti mkubwa wa Mwalimu Nyerere aliyeitwa Anna Watiku alisema ‘Oktoba Mosi ilikuwa siku ya mashaka sote tuliingiwa na hofu kuwa tutampoteza baba yetu’.

Oktoba 2: Anna Watiku alisema “NATAMANI KUWAITA MAPADRE NA MAASKOFU KUTOKA KOKOTE DUNIANI WAJE KUMUOMBEA SALA BABA HAPA HOSPITALI..”

Safari za kuwapeleka London Uingereza watoto wa Hayati mpendwa wetu Baba wa Taifa mmoja baada ya mwingine zilianza.

Wageni walikuwa wakizuiliwa kutokana na ulinzi ulioimarishwa nyumbani kwa baba wa Taifa huku zoezi la dharura la kuifanyia matengenezo nyumba yake iliyoko Msasani jijini Dar es salaam likiendelea.

Kule nyumbani kwake kijijini Butiama Machifu na majirani zake waliendesha ibada kubwa kila mmoja kwa imani yake thabiti kumuombea afya njema Baba wa Taifa.

Oktoba 3: David Mwakyusa ambaye ni Daktari wa Baba wa Taifa alizungumza na BBC na kueleza kuwa hali ya Mwalimu bado ni mbaya.

“Mimi na madaktari wengine tunajaribu kuona na kutumia kila mwanya uliopo kuyanusuru maisha ya Baba wa Taifa” alisema.

Kisha baadaye Marehemu Kipenzi cha Taifa na ulimwengu wote Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifaulu jaribio la awali la kupumua mwenyewe baada ya jopo la madaktari wanaomuuguza kumjaribu kwa kuzima mashine zilizokuwa zinamsaidia kupumua.

Oktoba 5:Madaktari walizungumza na familia ya Baba wa Taifa na waliileza kila kitu walichokiona kwa mgonjwa wao huku Watanzania wakiendelea kumuombea Duwa kwa Mwenyezi Mungu ili ayanusuru maisha yake na kumponya na wengi walianza kupata faraja baada ya kusikia kuwa Mwalimu Nyerere alifaulu jaribio la kupumua.

Mzee Rashid Mfaume Kawawa aliondoka nchini kwenda London Uingereza kuona hali ya mgonjwa wa Baba wa Taifaa ambaye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas akiwa katika wodi ya wagonjwa mahututi (ICU).

Oktoba 6: akiongozwa na mke wa mwalimu mama Maria Nyerere, mzee Kawawa aliyekuwa kiongozi maarufu katika serikali ya Awamu ya kwanza aalimtembelea wodini Baba wa Taifa na mshirika wake mkuu wakati w harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika, na kumkuta akiwa ICU.

Baba wa taifa alitembelewa na Jenerali David Bugozi Msuguriau “DB” ambaye wakati wa utawala wa awamu ya kwanza alikuwa kamanda wa vikosi vya majeshi ya Tanzania wakati wa vita ya kumwadhibu mvamizi wa ardhi ya Watanzania kule Kagera Nduli Idd Amini Dada wa Uganda, na baadaye akawa mkuu wa majeshi ya Ulinzi.

Mwalimu aliongeza matumaini ya kuishi kwake zaidi kwa Watanzania kwani mara alikuwa akifumbua na kufumba macho. Madaktari waliamua  Baba wa Taifa aendelee kupumua kwa msaada wa mashine maalumu zilizokuwa zinamsaidia kwa siku saba zaidi ili mwili wake uweze kupata nguvu zaidi kupambana na gonjwa linlomkabili au maambukizo.

Mfalme letsie wa nchi ndogo ya Lesotho, aliungana na viongozi wengine wa kimataifa kumtakia kheri baba wa taifa.

‘Ni haki na muhimu kwetu sote barani afrika na Dunia ya tatu kwa  ujumla kuendelea kumwombea apone haraka ili tuendelee kunufaika na uongozi wake wa busara na mwelekeo thabiti”, alisema na kuongeza “Mwalimu amekuwa mtumishi mwadilifu wa bara la Afrika na msemaji wa haki za wanyonge”.

Oktoba 7: “Kipenzi cha Watanzania” aliendelea kupumua kwa kusaidiwa na mitambo maalumu akisubiri majaribio mengine ya kuzimiwa mitambo oktoba 13 yaani jana.

Ghafla usiku wa manane hali yake ilibadilika kiasi cha kuwatia wasiwasi hata madaktari wake.

Familia yake ikiwemo mkewe mama Maria Nyerere, watoto wake wanazunguka kitanda na kuangalia kwa masikitiko jinsi baba yao akisaidiwa na jopo la madaktari waliokuwa wakihangaika kwa juhudi zote kuyaokoa maisha yake.

Homa kali ilipanda naa madaktari walazimika kumbadilishia dawa.

 

Hofu na wasiwasi viliongezeka

 

Oktoba 8: Madaktari walisema “Hali ya mgonjwa ni mbaya sana”.

 Alikuwa taabani kiasi cha kutisha na hofu kuu ilitanda kwa watanzania aalikuwa amepatwa na homa kali, na baadhi ya viungo vyake vya mwili viliishiwa nguvu.

Hata hivyo juhudi za kina za makusudi zilikuwa zikifanyika na madaktari wakijitahidi kuokoa maisha yake…ili Mwenyezi Mungu aweze kumnusuru maisha yake.

Oktoba 9: Hali yake bado iliendelea kuwa mbaya zaidi na wanaendelea kukokoa maisha yake.

Hali ya homa yake haina mabadiliko.  Mwanae wa kiume Charles Makongoro, asema; “Juzi tuliambiwa kuwa angekata roho kwa kipindi cha masaa 48, lakini wamesema sasa ana nafuu kidogo.

MADAKTARI WALIAZIMIA NINI SASA?

 

Oktoba 9: Walimfanyia jaribio la ubongo baada ya Baba wa Taifa kuchelewa kuzinduka kutokana na madawa mengi ya usingizi aliyopewa.

Oktoba 10: Hali yake haikuwa na mabadiliko na kwa kipindi cha siku tatu hivi mfululuzo alikuwa hawezi kufanya lolote. Madaktari wakasema, “ Ni jambo la kawaida kwa watu waliokula chumvi nyingi kama Baba wa Taifa, kuchelewa kuamka baada ya kupewa nusu kaputi”.

Oktoba 11: Hali ya mgonjwa bado ilikuwa mbaya ingawa inaaminika kwamba moyo na mapafu yake vilikuwa vinafanya kazi vizuri, hata figo zilikuwa zinafanya kazi vizuri lakini anaingia siku ya tano pasipo kuamuka.

Hata hivyo Madaktari walisema hali hiyo ilikuwa ni ya kawaida kutokana na nusu kaputi alizokuwa anapewa.

Rais wa Zamani  wa Zambia Dk. Keneth Kaunda na mwanachama mwasisi wa klabu ya Mlugushi alimtumia mwalimu salamu zilizogusa nyoyo akimtakia heri baba wa Taifa apone haraka.

“Mwalimu, tafadhali pokea salamu kutoka ndani ya moyo wangu mimi na familia yangu na pia chama changu cha UNIP ambacho pia kimekuwa chama chako. “ ninamwomba mwenyezi Mungu atapenda, ningependa niwe kandokando ya kitanda chako”.

“Mwalimu rafiki yangu mpendwa na kaka yangu natamani nikupake mafuta miguuni wakati huu mgumu wa maumivu makali ya ugonjwa. Miguu ambayo inakanyaga kila kona ya bara la Afrika ukitoa ujumbe wa kuamsha nyoyo na matumaini kwa waliokata tamaa; natamani kushika mkono wako’ mikono ya upendo na ukarimu kwa maskini, mikono miororo kama hariri wakati wa kuwasaidia kuwaenzi wenye shida lakini (migumu) kama chuma cha pua dhidi ya majizi na yanayokandamiza haki za raia na matumaini yao”.

“Kaka yangu mpendwa natamani kukufuta hayo matone ya jasho usoni …” Kaunda alisema katika salamu zake.

Oktoba 12: Madaktari wake wanamfanyia uchunguzi wa kina wa ubongo wake na kuieleza familia yake kuwa matumaini ya mwalimu kuamika kutoka katika usingizi wa dawa alizopewa kumpunguzia maumivu hakuna tena.

Mzee Rashid Kawawa alirejea kutoka London Uingereza kumwangalia Mwalimu wakati wa harakati za kupigania uhuru wa Tanzania lakini alikuwa na siri kubwa moyoni mwake.

Oktoba 13: Mzee Kawawa alidamkia Ikulu kuhudhuria kikao maalumu, mashaka yanaongezeka jijini huku kukiwa na pilikapilika za kimya kimya zisizo za kawaida.

Oktoba 14: Saa nne na nusu asubuhi Mwalimu Julias Kambarage Nyerere akiwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas huko London anafariki dunia.

Amewaacha Watanzania na ulimwengu mzima katika majonzi na msiba wa hali ya juu na rais Benjamin Mkapa anautangazia Umma wa Watanzania na ulimwengu kwa ujumla juu ya kifo cha Mwalimu Nyerere kwamba sasa hatuko naye tena katika dunia hii.

Nchi nzima ya Tanzania ilikuwa imegubikwa na wingu la

Majonzi kufuatia msiba huo na vilio vilisikika kila kona mitaani, ndani ya mabasi, majumbani na hata maofisini. Watu mbalimbali, taasisi, mashirika na nchi mbalimbali zilianza kumiminina salamu za rambirambi kufuatia kifo hicho.

Oktoba 15: Wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam walikuwa katika maombolezo na walikuwa wamevaa mavazi meusi na nchi nzima ilitawaliwa kwa majonzi.

Nyumbani kwa Mwalimu huko Msasani, wageni walianza kumiminika na kutia saini kitabu chaa maombolezo wakitoa salamu za rambirambi. Hata Butiama mambo yalikuwa hivyo.

Salaam hizo ziliendelea kumiminika kutoka nchi mbalimbali duniani na kila nchi au taasisi ikielezea sifa kemkem za mwalimu.

Octoba 16: kamaati ya kitaifa ikiongozwa na makamu wa Rais, DK. Omari ali Juma iliondoka nchini kwenda London Uingereza kuuchukua mwili wa kipenzi cha taifa na ratiba ya muda kutoa heshima za mwiso na mazishi ilitangazwa.

Mwili wa Baba wa Taifa ulifanyiwa Ibada Takatifu katikaKanisa kuu la Katoliki Westminister, london Uingereza.

Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi alisaini kitabu cha maombolezo, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Msasani hapa jijini Dar es Salaam.

Oktoba 17: Ndege ya msafara wa Makamu wa Rais, Dk. Omari Ali Juma, ikiwa na mwili wa Baba wa Taifa, iliondoka London, uingereza kuja nchini.

Oktoba 18: Mwili wa Baba wa Taifa uliwasili uwanja wa Ndege wa Kimataaifa na kupokelewa na maelfu ya Watanzania wakiongozwa na Rais Benjamini Mkapa na mwili ulipelekwa nyumbani kwake Msasani baada ya kupitishwa katika mitaa mbalimbali ya Dar es Salaam

Oktoba 21: Mazishi ya Kitaifa yanafanyikakatika Uwanja wa Taifa. Wananchi wanatoa heshima zao za mwisho usiku na mchana

Oktoba 22: Mwili wa Marehemu unapelekwa Musoma kwa mazishi.

Oktoba 23: Mazishi yanafanyika kijijini Butiama eneo la Mwitongo na kuhudhuriwa na watu mbalimbali toka ndani na nje ya nchi.

Oktoba 14: 2002, maadhimisho ya miaka mitatu tangu kifo cha Mwalimu.

Matembezi ya kumuenzi Nyerere toka Dar es Salaam hadi Chamwino Dodoma.

Na hii tangu mwaka huu inakuwa ni Siku ya Nyerere (Nyerere Day), na inakuwa ya mapumziko kitaifa.

 

MUNGU  AILAZE MAHALI PEMA ROHO YA KIPENZI          CHA WATANZANIA NA ULIMWENGU    WOTE  MWALIMU JULIUS

K A M B A R A G E   NYERERE, AMINA.