Kumbe vichaa wanatumwa kurusha mawe!

l      Wakipata amri, wanatimiza, wakiona                             kisichoonekana, wanacheka na kujibu

Na Pastory  Nguvu.

Na Pastory  Nguvu.

 

GHAFLA, Moris (33),  alibadili mawazo na kukataa katakata kula nyumbani kwake akihofu kuwa, mkewe atamuwekea sumu katika chakula; akaamua kwenda katika hoteli moja jirani na nyumbani kwake, alipofika, aliagiza chakula alichopenda.

Haukupita muda mrefu, mhudumu akafika na kuweka vyakula mezani kwa Moris. Bw. huyu akanawa mikono, lakini kabla ya kula, akakumbuka kuwa hoteli hiyo ipo jirani na nyumbani kwao hivyo, huenda mkewe anaweza kuwa amempa sumu meneja wa hoteli ambaye aliamini kuwa wana uhusiano, ili Moris akienda pale, amuwekee katika chakula alichoagiza.

Moris akabadili mawazo, akalipia na kuondoka bila kuonja chakula hicho.

Akaona heri anunue mkate dukani na kuutumia kwa mlo wake. Hali haikubadilika. Akakumbuka kuwa duka lile haliko mbali, inawezekana mkewe huyo alitawanya dawa ile na kumpa mwenye duka ili aiweke kwenye mkate atakaonunua Moris ili akila, afe.

Safari hii Moris akautawanya mkate ule katika vipande vingi huku akiwarushia kuku waliojipatia mawindo nafuu.

Watu waliokuwa wakifuatilia nyendo za Moris, walihisi kuwapo kwa jambo baya.

Kwa mujibu wa Daktari mmoja wa magonjwa ya akili, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliyopo Dar es Salaam, msichana mmoja (hakumtaja), alifikishwa hospitalini hapo baada ya kubainika akiongea peke yake na hata wakati mwingine, kuokota makopo na makasha matupu ya viberiti kila alipoyaona. Wakati mwingine, msichana huyo, alifurahi na kucheka sana, bila sababu yoyote iliyoonekana kwa waliokuwa wakimshuhudia.

Baadaye alipoulizwa kulikoni, alisema alikuwa anatii sauti iliyomtuma kufanya matendo hayo na wakati mwingine, alikuwa akiona vitu vilivyomfanya acheke sana. Tena alishangaa kuona kuwa kumbe watu wengine walikuwa hawasikii wala kuona vitu hivyo.

Alikiri kuwa kimsingi, hata yeye alijua kuwa amri zilizomsonga zilikuwa za kipuuzi, lakini alipaswa kuzitii vinginevyo, angekuwa hatarini na pengine hata angeweza kulaaniwa.

Pamoja na mifano mingi halisi ya namna hiyo, sio jambo geni kusikia kuwa mtu fulani, ndugu, jamaa, rafiki au jirani, amechanganyikiwa. Wengi wetu tumekwisha kutana na watu wenye hali kama hiyo.

Lakini cha msingi kujiuliza, ni kitu gani hasa huwafanya watu wachanganyikiwe na wengine kuwa vichaa kabisa?

Zipo sababu nyingi, lakini kwanza tuangalie dalili za mtu aliyechanganyikiwa.

Ni rahisi kumtambua mtu aliyechanganyikiwa hata katika mazungumzo. Mara nyingi, mtu huyo huzungumza kupita kiasi, hucheka kupita kiasi, ovyovyo na pengine hata akiwa  peke yake.

Upo uwezekano pia kuwa, mtu huyo akawa na ukimya usio katika hali yake ya kawaida, na hata akafanya vitu visivyo vya kawaida vikiwamo vitendo vya kuokota makopo, makaratasi na kurusha mawe ovyo.

Wataalamu wa magonjwa ya akili, wanasema mawazo ya mtu aliyechanganyikiwa humuongoza kuwa watu walio karibu naye wanamchukia na hivyo, hutaka kujitenga nao kabisa na ndio maana wengine wanapochanganyikiwa, hutoroka nyumbani, na kushambulia watu huku wao wakiona kuwa wanajihami dhidi ya watu hao ambao sasa wanachukuliwa kama adui.

Hata hivyo, hutokea wakati mwingine, watu hao wakawachagua na kuwapenda baadhi ya watu wakiwamo, mama na kaka na rafiki wa karibu zaidi au wenye matatizo kama yao.

Mara nyingi watu waliochanganyikiwa huwa na matatizo katika mifumo yao ya fahamu na hivyo, husikia sauti zisizokuwapo wala kusikika kwa watu wengine, na huona vitu visivyokuwapo wala visivyoonekana kwa watu wengine.

Sauti hizo huwa na maagizo mbalimbali kwa mtu aliyechanganyikiwa. Katika kuzitii sauti hizo ambazo mara nyingi huwa katika hali ya kuamuru, ndipo mtu aliyechanganyikiwa hufanya mambo yasiyo ya kawaida.

Inadaiwa kuwa, usikivu wake huwa wa matatizo kwa kuwa sasa husikia sauti mbalimbali kutoka kusikojulikana zikimuagiza kufanya mambo kadhaa.

Mtu aliyechanganyikiwa hali yake kwa kawaida hubadilika. Anaweza kulia au kucheka mwenyewe. Anaweza kuwa mnyonge bila sababu na anaweza kuogopesha, akagoma kula na hata kuongea.

Mtu huyo anaweza asipende usafi, hivyo anaweza kuvaa nguo chafu, akazichana nguo nyingine, asichane nywele, asioge na hata asifanye jambo lolote linalohusu usafi.

Hubadili hali halisi ya uhusiano baina yake na wanajamii inayomzunguka kwani sasa anaweza kutumia lugha ya matusi na hata kuwapiga watu kwa kuwa anaamini na kupokea sauti zinazomjulisha kuwa watu hao wanamchukia.

Baadhi ya watu huchukulia kitendo cha mtu aliyechanganyikiwa kuwa ni fumbo, hivyo kushindwa kutambua chanzo halisi cha tatizo.

Hata hivyo, watu wengi huhisi kuwa magonjwa ya akili husababishwa na Mungu kukasirika, kupandwa na mashetani, chuki za mizimu au uchawi.

Mtaalumu wa magonjwa ya akili na Mwanasaikolojia wa Kijerumani, Sigmund Freud (1856 – 1939), anabainisha kuwa, maisha ya binadamu hujengwa tangu akiwa mtoto mdogo.

Anasema, “Maisha magumu na matatizo mengi wakati wa utotoni, uhusiano mbaya wa mtoto na wazazi wake, kaka zake, dada zake, walimu na marafiki zake, humsababisha mtoto akose raha, hivyo kumfanya ahuzunike ukubwani. Hali hiyo huandaa mazingira mazuri ya mtu kuchanganyikiwa.”

Pia, anasema kuchanganyikiwa kunatokana na tabia ya baadhi ya watu kupenda starehe.

Anasema wakati moyo ukihangaika kupata kitakachouridhisha kwa haraka, mazingira yanakuwa magumu na hivyo kuzuia au kuchelewesha kupatikana kwa kile kinachohitajika.

Freud anaitaja sababu nyingine ya kuchanganyikiwa kuwa ni mgongano wa ndani kwa ndani kwa mtu. Huu ni ushindani wa kimawazo baina ya matarajio binafsi ambayo hayawezi kuwa pamoja.

Endapo mtu hakuridhishwa alipokuwa mdogo, basi hata anapokuwa mkubwa, anaendelea kuwa na huzuni ile, anaendelea kuchanganyikiwa.

Inapotokea mtu akashindwa kutatua mgongano huu wa kimawazo, kunakuwa na uwezekano mkubwa wa mtu kuchanganyikiwa.

Anatoa mfano kuwa, “Kama mtu alitaka maisha ya usista au upadre, lakini mazingira yakamkwaza na kumfanya asifikie matamanio yake, akaamua kuoa au kuolewa( kwa mwanamke), upo uwezekano mkubwa wa mwanandoa huyo kumchukia mwenzi wake kwa kuwa mazingira yalimlazimisha; maisha ya unyumba hayakuwapo akilini kwake tangu akiwa mtoto. Anamuona mwenzie kama aliyemlazimisha kuishi maisha hayo.

“…Endapo mtu atakuwa padre, lakini akili yake tangu utotoni haikuwa imejiandaa kuishi maisha kama hayo, padre huyo anaishi maisha yasiyo kuwa na furaha, anajiona yupo tu, ili siku zipite. Huyo ni rahisi kuchanganyikiwa na kuiacha kazi na maadili ya utumishi wake, akawa padre mwenye vimada, padre mwenye miradi na anayetafuta maslahi binafsi na kibaya zaidi, anaweza kuwa padre anayekimbizana na wasichana parokiani kwake.”

Ni vema pia kujua kuwa, magonjwa ya akili yanaweza kuwa ya kurithi katika familia.

Pia, magonjwa ya akili yanaweza kuanza tokana na maradhi yanayompata mama mwenye mimba. Endapo mama mjamzito ana ugonjwa kama kaswende, mtoto anaweza kuwa na kifafa au punguani.

Homa ya malaria pia ni chanzo kikubwa cha magonjwa ya akili.

Kwa Mujibu wa Wizara ya Afya, Ukosefu wa chakula bora husababisha magonjwa ya akili.

“Mwili dhaifu husababisha akili dhaifu. Mwili huweza kupona, akili pengine hushindwa kupona.”

Ni wazi kuwa, vileo vingi ikiwa ni pamoja na bangi, dawa za kulevya na pombe, vinaweza kusababisha matatizo ya kiakili na kimwili.

“Matumizi ya bangi ni jambo la kawaida kwa vijana siku hizi. Mirungi hupendelewa na madereva wanaokwenda safari ndefu. Vyote hivi vinaweza kusababisha mtu kuvurugikiwa na akili.”

Dk. Joseph Mbatia wa Wizara ya Afya, katika Kitengo cha Magonjwa ya Akili, anasema,’ Ajali zinazoumiza ubongo zikiwamo za barabarani, zinaweza  kumsababisha mtu kupoteza fahamu au kuwa na kiharusi.”

Anasema maisha magumu wakati wa utoto pia, ni chanzo cha kuchanganyikiwa hivyo, watoto wapewe muda wa kustarehe na kucheza kwa kuwa jambo hilo si anasa, bali ni muhimu kiafya.

Anaongeza, “Mila pia zinaweza kuchokoza magonjwa ya akili…wanawake wengi huugua magonjwa ya akili kuliko wanaume kwa sababu wanaume wanawakandamiza wanawake.”

Mambo mengine yanayoweza kumfanya  mtu achanganyikiwe, ni huzuni na mikosi mbalimbali.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO),  ya mwaka 1998, inaonesha kuwa karibu watu milioni 1500 ), wanasumbuliwa na magonjwa ya akili duniani.

Mwandishi wa makala haya hakupata takwimu rasmi za Watanzania walioathirika na magonjwa ya akili kwa kuwa Kitengo kinachohusika na magonjwa haya hakina takwimu hizo ingawa Dk. Mbatia wa Kitengo hicho, amekiri kuwa idadi ya watu wanaochanganyikiwa ni kubwa husasan maeneo ya vijijini.

Ukatili kwa watoto tutavuna shubiri

Na Feruzi Mathias, Shinyanga

Ndugu zangu huwa kuna swali linalokisumbua sana kichwa changu kwa takribani kila siku. Mara kwa mara  huwa ninajiuliza, hivi kwa sasa hii dunia  yetu inakwenda wapi? Au ndio mwisho wake umekaribia?

Siku hizi kuna msemo ulioshamiri midomoni mwa watu kuwa ni heri ukutane na simba usiku, au porini lakini siyo binadamu! Lakini ni kwanini imekuwa hivi?

Pia, labda niulize kuwa ule ustaarabu tulioenziwa na wazee wetu tumeusahau wapi ili tukautafute?

 Ukarimu pamoja na huruma tuliorithishwa na wahenga wetu tumeudondosha wapi? Sina budi kuuuliza maswali haya baada ya kukerwa na vitendo vya kikatili tunavyofanya sisi binadamu kila kukicha.

Kwa tuliobahatika kuiona siku ya Jumatano Oktoba 8, mwaka huu majira ya saa mbili usiku, moja ya vituo vya kurushia matangazo ya televisheni hapa nchini, kilionesha tukio moja la kusikitisha sana na hata kutufanya baadhi ya watu wenye mioyo myepesi, wadondoshe machozi.

Mtoto mdogo wa kike mwenye umri wa miaka mitano, alionekana akiwa na makovu kadhaa mwilini mwake baada ya kuchomwa moto yaani kisu kiliwekwa kwenye moto kisha kikabandikwa maungoni mwa malaika huyo asiyejua lolote!

Waliofanya hayo hawakuwa na huruma hata chembe kwani ni dhahiri mtoto huyo alipata maumivu makali kutokana na unyama waliomtendea.

Ukatili huu unastahili adhabu kali kwa walioutenda na pia, ukemewe kwa nguvu zote.

Kisa kilichotolewa na hata kupelekea walezi wa mtoto kutoa adhabu kama hiyo isiyostahili kwa mujibu wa mtangazaji, kilitokana na malaika huyo eti kwenda haja kubwa na ndogo kitandani!

Mimi binafsi, ninaiona sababu hiyo kuwa haiingii akilini kwa mtu mwenye akili timamu, na wala binafsi sikubaliani nalo kutokana na adhabu hiyo isiyo ya kibinadamu kutolewa.

Nasema hivyo nikiamini kuwa, hata kama mtoto huyo ni kweli angetenda kosa kubwa kiasi gani, lakini bado hakustahili kuadhibiwa kiasi kile! Ninashindwa kuelewa endapo walezi hao wenye mioyo ya kikatili walifanya vile wakiwa na lengo la kumrekebisha mtoto huyo ili asirudie makosa yale, au tu walichoka kuishi naye kwa vile hawakumzaa.

Naelewa, na pia nimekwisha shuhudia baadhi ya wazazi wakiwatendea udhalimu kama huo watoto wao wa kuzaa wenyewe!

Hapo ndipo inatubidi tujiulize; Je mambo haya yanatendeka yakiashiria dunia yetu inakwenda mwisho au ndio mwisho wenyewe huo?

Suala la unyanyasaji kwa watoto limekuwa likikemewa na viongozi wetu wa dini na hata Serikali, takribani duniani kote.

Watoto ni baraka tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu, hivyo tunapaswa kuelewa kuwa, kutokana na ukatili tunaowatendea, ni wazi kabisa kuwa tunamchukiza Mungu.

 Tunapaswa kutambua kuwa watoto ndio hazina ya Kanisa, Taifa na jamii duniani kote kwa jumla, ama wawe wa kuzaa sisi wenyewe au wa “kufikia” (yaani wa kulea).

Hebu tujiulize, je ni mara ngapi tumewaona watoto hao wa kufikia wakisaidia watu ambao sio wazazi wao? Siyo kwa pesa tu, bali hata kimawazo, yote hiyo ni misaada.

Kwa upande mwingine, ninakiri wazi kuwa watoto wetu wamekuwa watukutu, hawashikiki na wala hawaambiliki, lakini tabia zao hizo zisiwafanye wazazi kupata tiketi ya kuwadhuru, badala ya kuwapa adhabu za kawaida.

Adhabu hizo zitolewe kulingana na umri wa mtoto husika. Ni vema tukazingatia kuwa adhabu kali, siyo kipimo cha kufundisha mtoto, bali ni chanzo cha matatizo mengine kwa kuwa adhabu kama hizo, zinamuathiri mtoto kisaikolojia na hata baadaye kumpotezea mwelekeo wake wa maisha.

Utafiti uliofanywa na wataalamu wa Saikolojia kwa miaka kadhaa ulibaini kuwa mtoto ni mwepesi sana wa kutunza kumbukumbu katika ubongo wake. Ninachokihofia mimi, endapo tutaendelea kuwatendea ukatili watoto wetu, basi tukae tukifahamu tunawaandaa kwa kuwajengea msingi wenye maadili yasiyofaa katika jamii yetu na hivyo, tutarajie kuvuna maovu tunayofanya dhidi yao.

Mnamo miaka ya tisini nilibahatika kutembelea kambi moja ya wakimbizi iliyopo kule Wilayani Ngara. Siku moja niliwashuhudia watoto watatu wenye wastani wa miaka kumi kila mmoja, walikuwa wakitenda jambo ambalo liliniacha mdomo wazi.

Watoto wale walikuwa wakimchangia bwana mmoja wa makamo, walikuwa wakipigana naye ! Watoto walikuwa jasiri utafikiri watu wazima, ni dhahiri walionekana kuwa na nia madhubuti ya kumpiga mzee mzima!

Bwana yule alijitahidi kujibu mashambulizi ili asiaibike, alipoelekea kutaka kuwashinda, ghafla lilitokea kundi la watoto wengine wapatao kumi hivi, waliokuja kutoa msaada kwa wenzao, ilikuwa ni patashika!

Bwana yule ambaye alikuwa Mtanzania alishambuliwa vilivyo! Bahati nzuri iliyotokea kwa mheshimiwa yule ambaye tayari alikwisha kuwa taabani kutokana na kipigo alichokuwa akikipata, ilikuwa ni watu wengine kuingilia kati nikiwemo mimi. Na hiyo ndiyo ikawa pona yake toka mikononi mwa wakimbizi hao.

Baada ya hali kuwa shwari, nilitaka kuelewa ni nini kilikuwa chanzo cha kadhia ile. Majibu niliyopewa, yalibainisha kuwa, watoto wale walimlazimisha yule bwana awapatie pesa, na alipokataa kuwapa ndipo yakampata yale !

Huu ni mfano halisi unaoonesha namna mazingira tunayowakuzia watoto, yanavyoweza kuwaathiri.

Suala la chuki na vita limekuwa la muda mrefu kwa nchi za Rwanda na Burundi pamoja na nchi nyinginezo zenye mfumo huo.

Jamii inatarajia nini kitatokea hapo baadae kwa watoto wanaokuwa wakiona jinsi watu wanavyochinjwa kama ndege au wanyama ? Kwa wale walio bahatika kufika ama kutembelea kwenye kambi hizo za wakimbizi, nina imani watakubaliana nami juu ya tabia hiyo ya kusikitisha waliorithi watoto hao.

Ndugu zangu nilichokidhamiria katika makala haya ni kwetu sisi wazazi au walezi kuacha tabia ya kuwafanyia ukatili watoto wetu ili tuwanusuru kurithi maovu, tuwalee na tuwakuze katika mazingira ya amani na upendo, vinginevyo tutarajie kutendewa maovu na watoto wetu pindi tutakapozeeka kwa vile ukatili tunaowafanyia utakuwa tayari umo ndani ya damu zao.

 

Unywaji pombe na imani za dini (2)

AGANO JIPYA

Tunaona Muujiza wa kwanza alioufanya Yesu Kristo katika Harusi ya Kana, ni kugeuza maji kuwa divai, tena nzuri kuliko iliyokuwa ikitumika (Yn. 2 :10).

Tena Bwana Yesu kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake, alikunywa divai. (Mt. 11 :18-19 ;26 :27-29). aligeuza divai kuwa damu yake !

Sio hayo tu, bali alifundisha waziwazi kuhusu ulaji wa vyakula vyote na akaeleza ni vitu gani vimtiavyo mtu unajisi.

Kwamba hakuna chakula (ni pamoja na unywaji) ambacho ni dhambi (Mk. 7 :14-20).

Yesu Kristo aliorodhesha mambo yote yanayotia mtu katika dhambi, lakini divai/mvinyo havikutajwa (Mk. 7 :21-23).

Mtume Paulo, katika Waraka wake kwa Wagalatia, anasisitiza mafundisho hayo ya Kristo kwa kuorodhesha tena mizizi yote ya dhambi pamoja na fadhila ponya saba ambazo ni mizizi ya dhambi ; yaani, majivuno, uchoyo, uchafu, wivu, ulevi, ulafi, hasira na uvivu.

Anazitaja Fadhila Ponya kuwa ni unyenyekevu, ukarimu, usafi wa moyo, mapendo, kiasi, upole na bidii.

Hakuna mahali popote ambapo divai/mvinyo au chakula cha aina fulani kimetajwa kama mzizi wa dhambi au najisi.

Jumuiya za Kikristo za mwanzoni ziliishi kwa kushirikiana kwa ukaribu sana. Zilizoea kukutana na kumegeana mikate na kushirikishana vikombe vya divai.

Waliokuwa na mikate na divai walivipeleka katika Jumuiya na kugawana na wale ambao hawakuwa navyo. Lakini, wengine waliokuwa na uchoyo na ulafi kiasi cha kwamba walikula na kunywa na kushiba sana na kulewa wakati wengine walitoka wakiwa na njaa. Mtume Paulo anakemea tabia hii, hakemei unywaji wa ile divai. (1Wakor. 11 :17-22).

Kama hivyo ndivyo, basi tujiulize na kutumia ushahidi kama viongozi wa Kanisa wanaruhusiwa kunywa pombe.

Ukweli ni kwamba wanaruhusiwa kunywa kwa kiasi. Wasiwe walevi (1Tim. 3: 2-3). Wasiwe watu wa kutumia pombe mno. (1 Tim 3:8).

Mtume Paulo anatufundisha waziwazi kuwa vyote vilivyoumbwa na Mungu ni halali na yatupasa kuvipokea kwa sala ya shukrani (1Tim. 4:1-5).

 

Tena anawaambia watu wasikubali kupewa masharti na mtu yeyote kuhusu vyakula na vinywaji. Wala wasikubali kuhukumiwa na mtu yeyote anayejitakia kuwa na maana kwa maono ya pekee na ambaye anasisitiza juu unyenyekevu wa uongo na ibada kwa malaika.

Mtu wa namna hiyo amepumbazika kwa fikra danganyifu za kidunia na amejitenga na Kristo aliye kichwa cha mwili. Chini ya uongozi wa Kristo, mwili wote unalishwa na kuunganishwa pamoja kwa viungo na mishipa yake nao hukua kama atakavyo Mungu (Kol 2 :16-19).

Anaendelea kufundisha ukweli kuwa Wakristo wamekufa pamoja na Kristo na kukombolewa katika nguvu za pepo watawala wa ulimwengu. Hatupaswi tena kuishi kama wafungwa wa sheria.

Hakuna sababu ya kuwekeana masharti juu ya kushika hiki, kula au kunywa kile. Kufanya hivyo ni kuutendea tu mwili kwa ukali, lakini haifai chochote kuzuia tamaa za mwili (Kor 2 :20-23).

Ukweli ni kwamba Mungu hakukataza kunywa pombe. Na kama tukisema kuwa pombe ni dhambi, basi tunamhukumu Mungu kuwa ni mdhambi. Hivi kweli hawamhukumu na kumkana Mungu ?

Watu wengine huzidi kupotosha kwa kusema kuwa divai/mvinyo sio pombe bali ni juisi ya mizabibu. Ni kama togwa ! Biblia inabainisha wazi kuwa divai ni pombe tena kali (Isaya 5 :11;28 :7. Mw 19 :32, Kumb 14 :26, Hes 28 :7) na sehemu nyingine nyingi katika Biblia.

Je, mafundisho ya kweli kufuatana na Biblia Takatifu ni yapi?

Mwenyezi Mungu tangu zamani anatukataza kuwa walevi, ulevi ni chukizo kwake (Isaya 5:11, 22 Isaya 28:1).

Tunakatazwa kuwa walevi kwa kuwa ulevi una madhara mengi si kwa roho tu, bali hata kwa mwili (Methali 23:19-21;29-35).

Ulevi ni mojawapo ya mizizi ya dhambi, hivyo inatupasa kuepukana na aina zote za ulevi. Iwapo mtu anashindwa kutawala tamaa katika kunywa, kwamba anashindwa kunywa kiasi, basi ni bora mtu huyo aache kabisa kunywa. Hii itakuwa sawa na alivyofundisha Bwana wetu Yesu Kristo kuwa kama jicho lako linakukosesha ling’oe na kulitupa, kama mkono wako wa kulia wakukosesha, ung'oe na kuutupa mbali nawe.

Afadhali zaidi kupoteza kiungo kimoja cha mwili wako, kuliko mwili wako wote kutupwa katika moto wa Jehanamu (Mt 5:29-30).

Inatupasa kuzishinda tamaa za mwili ili tuuendee ufalme wa Mbingu. Tushinde tamaa ya kupenda kunywa mno na tufanye hivyo kwa ajili ya kumpendeza Mungu.

Baadhi ya mafundisho ya Biblia kuhusu kinywaji pombe:

(Mwa 14:18-19 )Melkizdeki kuhani anambariki Abrahamu kwa divai, anasema, “Na Melkizedeki Mfalme wa Salem akaleta mkate na divai naye alikuwa Kuhani wa  Mungu aliye juu sana.

Akambariki, akasema, Abrahamu na abarikiwe na Mungu aliye juu sana, Muumba Mbingu na nchi’.

(Hes 15:5) mvinyo unaotolewa sadaka kwa Mungu. ‘Na divai kwa sadaka ya kinywaji, robo ya hini, utaiandaa sadaka ya kuteketezwa au kwa dhabihu ya kuchinjwa kwa ajili ya kila Mwana kondoo’.

(Hes 28:7) Kinywaji kikali kinatolewa kama sadaka mahali patakatifu.

“Na sadaka yake ya kinywaji itakuwa roho ya hini kwa mwanakondoo mmoja hiyo sadaka ya kinywaji ya kileo utammiminia Bwana katika mahali hapo patakatifu.

(Law 23:13). Sadaka ya kinywaji cha divai inatolewa kwa Mungu. ‘na sadaka yake ya unga itakuwa za kumimbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta ni sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini.

(Kumb 14:25-26.) Maneno yaliyo katika kifungu hiki yanaonesha ridhaa ya Mwenyezi Mungu kuwa wanaweza kutumia vinywaji vikali kwa lengo la burudani. ‘… na zile fedha zitumie kwa chochote itakachotamani roho yako, ng’ombe au kondoo au divai au kileo au roho yako itakacho kwako chochote; nawe utakula huko mbele za Bwana, Mungu wako; tena furahi wewe na nyumba yako.’

Zab 104:15. Divai imeumbwa imfurahishe mwanadamu.

“Na divai imfurahishe mtu moyo wake, aung’aze uso wake kwa mafuta, na mkate umburudishe mtu moyo wake”.

Yoh 2:1-11. Katika harusi ya Kana pombe ilikuwa kinywaji muhimu katika kufanikisha sherehe ya harusi.

Mt 11:18-19. Katika maisha ya duniani, Yesu Kristo alitumia divai pia.

“Maana Yohana alikuja hali wala hanywi, wakasema yuna na pepo. Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, wakasema mlafi huyu na mlevi, rafiki yao watoza ushuru na wenye dhambi! Na hekima imejulikana kuwa ina haki kwa kazi zake.

Mt 26:26-29. Kwa desturi ile ile ya Wayahudi kumtolea Mungu sadaka ya mvinyo, Yesu anatumia kinywaji hicho kufanyiza Ekaristi ambayo ni sadaka ya mwili na damu yake aliyoitoa msalabani.

1Tim.5:23. Kifungu hiki kinaonesha pombe ikitumiwa kama dawa. “Tokea sasa, usinywe maji tu, lakini tumia mvinyo kidogo kwa ajili ya tumbo lako, na magonjwa yakupatayo mara kwa mara.”

Lk 10:34. Divai inatumika kutibu majeraha. “Akakaribia, akamfunga jeraha zake akazitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni akamtunza.”

Meth 20:1. Tahadhari inatolewa kwani kileo kinaweza kumwongoza mtumiaji katika maovu. Mvinyo hudhihaki kileo huleta ugomvi; na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima”.

Law 10:8-9. Mungu anaelekeza wakati usiofaa kunywa kileo yaani wakati wa kusali hekaluni.

“Kisha Bwana akanena na Haruni, akawaambia usinywe divai wala kileo chochote, wewe wala wanao pamoja nawe hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutana, ili kwamba msife. Amri  hii itakuwa amri ya milele katika vizazi vyenu”.

Isa 5:11. Ole wao wanaoamka na pombe asubuhi na kuendelea kunywa bila kiasi.

Isa 5:22. Usijitafutie ubingwa au umaarufu katika kileo.

1Pt  4:3. Ulevi au kunywa kupita kiasi ni moja ya mambo wanayoyafanya watu wasiomjua Mungu.

Tit 1:7 Kiongozi wa Kanisa asiwe mlevi.

Waam 13:4. Hana anakatazwa kunywa pombe kama alama ya shukrani kwa fadhili aliyopewa na Mungu (Pia 1Sam 1:14-15).

Lk 1:15. Yohane Mbatizaji hakunywa divai wala kileo, kama nadhiri yake kwa Mungu.

YbS 31:25-31. Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inazungumzia kwa ufasaha sana maadili ya pombe.

Matumizi ya kileo hayajitokezi katika Maandiko Matakatifu peke yake, bali yako katika maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Hapa kwetu Afrika pombe imekuwa ikitumika kukidhi mahitaji mbalimbali ya watu kama kuweka na kuwaunganisha watu pamoja katika burudani kama harusi, mapumziko na starehe.

Nyingine ni kufanya kazi za kijami kama kilimo na ujenzi, kupatanisha, kuposa na kufariji katika msiba.

Pamoja na matumizi hayo mazuri ya pombe, daima kumekuwa na watu wanaotumia pombe vibaya. Wanakosa kushika kiasi cha unywaji.

Wanashindwa kujiongoza wanapokuwa wamekunywa pombe haramu. Wengine wanakunywa pombe haramu chang’aa (gongo) ambayo ni hatari kwa afya zao na jamii kwa jumla.

Tena kuna wale ambao wakishaonja pombe japo kidogo tu, wanashindwa kujitawala na kutenda mambo kama wendawazimu.

Bila shaka ni kwa sababu ya matumizi hayo mabaya ya pombe, madhehebu ya dini na vikundi mbalimbali vimejitokeza kulaani matumizi kama hayo.

Lakini ikumbukwe kuwa, ni wajibu wa kila raia mwema kukemea maovu ukiwemo ulevi uliokithiri.

Katika  kufanya hivyo, tahadhari lazima ichukuliwe maana kuna tofauti kati ya kunywa pombe na kulewa pombe.

Wale wanaokunywa pombe kwa kiasi na kwa kujali wakati wasiingizwe kwenye kundi la kukemewa (YbS 31:28).

Inapobidi mtu kuacha kunywa au kula kitu fulani kwa sababu zake mwenyewe au pamoja na kufanya hivyo kwa ajili ya nadhiri yake kwa Mungu wake, basi isiwe kikwazo kwa wengine, na afanye hivyo, lakini ajue kuwa hakuna chochote kilicho najisi kwa asili yake (Rum 14:13-18).

Si vyema yule asiyekula/kunywa kuwaona wale wengine ni wadhambi. Usihukumu!

Yeye amejifunga mwenyewe. Na si vyema kwa wale wanaokula/kunywa wakawaona wale wasiokula/kunywa kuwa wamepotoka au haifai na ni dhambi kwani kila mmoja wetu inampasa kushikilia anachoamini kati yake na Mungu wake.

Inatupasa kuzingatia daima mambo yenye kuleta amani na yanayotusaidia kujengana Rum 14:19-23.

Biblia Takatifu iko wazi sana kuhusu tunachopaswa na tusichopaswa kuamini, kutenda, na kufundisha.

Tusiisome Biblia Takatifu kwa woga, au kwa kificho, wala tusigeuze Maandiko ili yasomeke kama tunavyopenda kwa nafsi zetu. Tena tusifiche ukweli na kujionesha kama vile sisi ni wema na wanyenyekevu kuliko wengine au hata kumzidi Bwana wetu Yesu Kristo.

Tuwe wakweli wa kila hali kimatendo, kimaneno na kifikra na katika kukemea maovu. Yesu Kristo aliuishi ukweli wote na mambo yote ya ukweli aliyabainisha pamoja na matendo yote maovu aliyakemea.

Tukiuishi ukweli tutakuwa huru na hivyo tutakuwa kweli watoto wa Mungu na sio wa Ibilisi (Yn 8:31-47).

Wanaohubiri kuwa pombe ni dhambi au kula chakula fulani ni dhambi ni sawa na walimu wa uongo ambao wamejaa duniani, na wengine wanafanya hivyo kwa kujitafutia umaarufu na utajiri, lakini inatupasa kuhubiri ukweli. 

 

Makala ya uinjilishaji

 

Uamsho ni Ulokole katika Ukatoliki? (5)

 

Katika toleo lilipopita, Askofu Method Kilaini,  alimaliza kwa kusema kuwa, Uamsho ni kundi moja wapo; tena dogo tu, linalosisitiza suala juu ya Roho Mtakatifu kwa namna ya pekee. Sio kwamba linaleta kitu kipya.Kwa mfano, mtu anaweza kusema kuwa anakwenda kujiunga na Karismatiki, wanaweza kumuingiza huko wakamfanyia ibada ya Roho Mtakatifu, hapa sio kwamba atapata sakramenti mpya, hapana. Roho Mtakatifu ni yule yule isipokuwa yeye sasa anaifanya rasmi na kwa namna ya pekee kuwa NITAIFANYA IWE KARAMA YANGU, lakini sio kwamba hakuwa nayo, anakuwa nayo kama watu wengine. Sasa endelea.

Ni roho Mtakatifu yule yule isipokuwa yeye sasa anaifanya hiyo iwe karama yake kwa namna ya pekee. Na hii haina maana kwamba hakuwa nayo, alikuwa nayo ila sasa, anaifanya kwa namna ya pekee.

Kwa mfano, mtu anaingia Lejio ya Maria, sasa anajiweka chini ya ulinzi wa Mama Maria, alipopata Komunyo ya Kwanza, alijiweka chini ya ulinzi wa Mama Maria, sio kwamba alikuwa hasali Rozari, sio kwamba hasali kwa Mama Maria, ila ni kwamba anapokuwa Lejio ya Maria, sasa anajiweka rasmi kwa ajili ya Mama Maria.

Hivyo hivyo, Karismatiki ni kama vyama vingine sio kwamba ni kitu kipya, ni kitu kile kile, ila sasa huyu anajiweka kwa namna ya pekee.

Huwa natoa mfano kwa watu wasioona (vipofu), wanaokwenda kumtazama tembo.

Sasa mmoja akishika mguu anaweza kusema tembo ni kama mti mkubwa; mmoja akishika pembe anasema tembo ni kitu kigumu kama jiwe; kigumu halafu kinakwenda kinachongoka kidogo.

Ni tembo yule yule. Mwingine anashika sikio, anasema tembo ni kama jani linalopeperuka peperuka, na sisi ni hivyo hivyo ni Mungu yule yule.

Ni Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, Amina. Hakuna zaidi ya hapo. Sasa, kila mmoja anashika kitu fulani anasisitiza, lakini ni Mungu yule yule.

Na ndivyo kwa tembo, aliyeshika mguu alishika tembo aliyeshika pembe, alishika tembo, aliyeshika sikio alishika tembo, lakini kwa sababu wewe ni mdogo utashika tu mguu na utabakia unatembea na tembo”.

Hali kadhalika, utakuwa Karismatiki, umeshika ka mguu usidhanie kwamba umeshika tembo mzima, hapana umeshika ka-mguu tu, na wewe hata ukiwa na Moyo Mtakatifu wa Yesu, umeshika pembe sawa, umeshika tembo na unatembea naye.

Lakini sasa, usijidai kwamba tembo ni wa kwako. Na yule aliyeshika pembe nae asijidai, tembo siyo wake. Nyote mko pamoja na huyo tembo; ndivyo ilivyo kwa Karismatiki.

Sasa, kwa kuwa Karismatiki inafanyika mara moja kwa miaka 2 au 3, inakuwa na tamasha kubwa. Inakuwa hivyo kwa kuwa unakuta hata maaskofu wanakuja kuhubiri, lakini hizo ni mbinu tu, za kualika, lakini na vyama vingine vingeweza kualika tu.

Kwa mfano, hapa Dar es Salaam siku ya kwanza tunasikia Tamasha kubwa la Karismatiki lilitendeka mwaka 2000 na lingine likatendeka mwaka huu.

 Hata hivyo, Moyo Mtakatifu una wanachama wengi kuliko Karismatiki ni wengi zaidi. Na Karismatiki inapanda kweli na kuenea.

Hata hivyo Karismatiki iko katika majimbo machache tu, ambayo ni Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Morogoro, Tanga na mahali pengine kidogo, lakini ndiyo inaingia.

Sasa Waswahili wanasema kipya kinyemi. Kitu kipya kinaleta msisimko. Watu wanakipenda; wanakwenda kukitazama ni kitu gani, lakini huwezi kusema kina watu wakubwa zaidi, eti Karismatiki ina maaskofu zaidi, hapana.

Juu ya kunena kwa lugha, mimi hiyo lugha siielewi. Ila tunaambiwa katika Kanisa la Kwanza watu waliongea kwa lugha.

Hivyo, unapoongea kwa lugha uwe kweli umepata kitu cha kuongea, unaweza kuja hapa  lap lap..lap !! haina maana yoyote.

Kama kweli Roho Mtakatifu amekuingia eti uongee kwa lugha hapo ni tofauti, lakini sio blaa.. blaa eti kwa sababu tu, ni kunena kwa lugha.

Mara nyingi kwa kweli utakuta wanaofanya hivyo, hawaneni kwa lugha, wanachofanya ni kwamba mara nyingine wanarudiarudia maneno wanajaribu kufanya dhamira fulani iwaendee kichwani mfano, “Kristo ni Bwana utuokoe Kristo ni Bwana utuokoe x 4”.

Ndio maana mara nyingi ninapowahubiria, nawahubiria kwa maneno ya Mtakatifu Paulo aliyowaambia Wakristo Wakorintho, akasema, kuna kuongea kwa lugha, lakini kama lugha yako haieleweki na hakuna anayekuelewa unaongea nini nyamaza. Hakuna sababu ya kuongea.

Lugha ziko pale kwa ajili ya watu sio kwa ajili ya kuongea tu. Mtakatifu Paulo alikuwa wazi kabisa.

Na kama kuna mtu aliyesisitiza juu ya Roho Mtakatifu, ni Mtakatifu Paulo, lakini alipokwenda kwa Wakorintho ambao kweli walionekana kuiva zaidi na Roho Mtakatifu, lakini wakaenda zaidi ya kiasi.

Ikafikia hatua Korintho ikatafaruka sababu ya Ukarismatiki wake ambao hawakuwa na mpangilio. Kama wewe umepata paji la lugha, lugha ni kwa ajili ya watu kama watu hawaelewi unaongea nini nyamaza. Na mimi ndiyo nawaambia watu KAMA HATUELEWI UNAONGEA NINI, nyamaza kwa sababu kuongea si kuongea tu.

Kuhusu maombi, tofauti iliyopo ni kwamba kuna watu wanaotaka kujisikia kuwa wameombewa. Mimi kila mara nawaambia watu, tuko watu tofauti. Mimi nitakuja hapa nitaketi chini nitaomba vizuri tu, na najisikia niko sawa.

Na mwingine anataka arudie kabisa. Ndipo anajua kwamba sasa ameomba. Kwa hiyo tunachohitaji ni kukidhi mahitaji ya watu, lakini sala ni hiyo hiyo ambayo tunakuwa tumeifanya.

Hivyo, katika Karismatiki utakuta ile sala inamfanya mtu ajione kuwa ni ya mtu binafsi, yaani inamgusa yeye binafsi.

Ndipo utasikia hata wanasema, “Wewe ambaye tumbo linakuuma mwamini Mungu sasa akuponye…” … hivyo sasa inakuwa ni sala binafsi.

 Ila sasa, tunachoogopa ni kwamba isije ikafanywa hivyo kwamba dini nzima ikarudia hapo. Hiyo naogopa kila wakati.

Na ndiyo unakuta watu wengine wengi wanapiga vita mambo mengine ya Karisimatiki kwa uoga kwamba tutakuja kudhania Karismatiki au Roho Mtakatifu, ni “wewe pona! Pona! Pona! Kama mtu haponi wanamvuta, Ikiwa hivyo, hiyo sio dini; siyo dini kabisa. Tunakuombea Mungu akitaka utapona kwa imani yako, sio mimi; ni Mungu ndiye anaponya.

Lakini, ukijifanya wewe ndiye mwenyewe mwenye karama, ukilazimisha, Pona! Pona! Pona asipopona unamvuta, pona, amka, unakuwa eti unamuamsha. kama Mungu anamuamsha, utamuasha, lakini siyo wewe.

Hapo ndipo kidogo inakera watu, sasa tunajaribu kuzungumza na viongozi wao tukiwaeleza kabisa kuwa MKIFANYA HIVYO, MTAFUKUZWA KANISANI watu hawatawaelewa.

Mtakuwa ni kama mnafanya shoo; haiji kabisa. Watu wawaombee sawa weka mikono omba omba basi, Mungu akipenda atawaponya, lakini msijifanye na kujichukulia kuwa mnauwezo wa kuponya, halafu eti mtu asipopona mnasema hana imani.

“Pona, kuwa na imani! Pona; mbona huponi, hauna imani sasa hauna imani. Mbona Kristo aliponya watu wengi na baadhi ya Watakatifu hawakupona; wakafa na magonjwa?”

Hivyo sio kwamba dini ni kuponya na nawaeleza kabisa na hao Wanakarismatiki wakifanya hivyo, watakuwa wameharibu 'misheni' yao ya Ukarismatiki.

Hivyo, vikundi vya Wakarismatiki vina viongozi wao na ndio sababu mahali vinapotendeka kuna Baraza la Kichungaji kwa sababu mapadre ndio wanaokaa kule wanaona vitu ambavyo haviendi vizuri, wanapaswa kuvirekebisha.

Mwisho

 

Teolojia kwa Walei

 

Mafundisho juu ya pesa, madaraka na kazi

 

Sasa tuNaanza kuwalEtea mfululizo wa Chapisho la Kitabu kiitwacho, TEOLOJIA KWA WALEI- MAFUNDISHO JUU YA PESA, MADARAKA NA KAZI kama kilivyoandikwa na Padre Vic Missiaen na kuidhinishwa na Mhashamu Paul R. Ruzoka, Askofu wa Jimbo Katoliki la Kigoma.

Teolojia ya Pesa

 

UTANGULIZI

 

Kwa nini tunataka kutafakari juu ya maswali yanayohusu pesa, madaraka na kazi na tena kwa nini tafakari hiyo inafanyika katika mawazo ya kiteolojia?

Kujifunza teolojia ni kutafakari uzoefu wetu wa kidini katika yale yanayoonekana katika vitabu vya maandiko na pia katika utamaduni ule ambao jumuiya ya waamini ilikabidhi kwetu.

Tunataka kutafakari juu  ya nini wanachotaka kusema kuhusiana na  mambo ya pesa, madaraka na kazi na kwa tafakari hiyo

tuweze kujua ni vipi tabia yetu inapaswa kuwa na ni kwa vipi tunapaswa kutumia pesa madaraka na kazi kulingana na maongozi na matakwa ya Mungu.

Kwa kuanza mafundisho yetu, tutafakari juu  ya matumizi ya pesa na ni Mungu anatufundisha katika mada hiyo.

Ni vema tuanze na maelezo yanayotoa ufafanuzi kuhusu maana ya pesa.

Tunajua kwamba kabla ya kufikia katika njia za sasa na za pesa na matumizi ya sik hizi ya pesa, kuna historia ya namna ambavyo pesa kama tunavyoifahamu leo ilivyofikia hatua yake ya kuwepo.

Kabla watu hawajaanza kutumia pesa kulikuwa na mfumo wa kubadilishana, ambapo biashara ilifanyika kwa njia ya kubadilishana bidhaa. Baada ya hapo watu walianza kutumia bidhaa mbalimbali kuwezesha au kuhudumia biashara hiyo badala ya kubadilishana vitu. Vitu vilivyotumika kuhudumia biashara ni ya kubadilishana vitu. Vitu vilivyotumika kuhudumia biashara ni pamoja na mifugo, ngozi, tumbaku, koa, vitov ya thamani, fedha, na dhahabu iliyowekwa katika uzito Fulani. Kisha ikafika hatua ya kutumia vipande vya vyuma vilivyotengenezwa katika uzito maalum vilivyoitwa sarafu. Baaaye, karatasi zilianza kutumika kama stakabadhi ya thamani Fulani – hizi zilitumiwa na wafua dhahabu ambao walikuwa ndio wenye mabenki. Hasa ni katika karne ya 19 ndipo pesa za noti zilipozoeleka na kuweza kupokelewa na kukubalika na hivyo kuonekana ni za kawaida.

Hii inamaanisha kwamba noti hizo ziliaminika na kwamba watu walizikubali.

Siku hizi pesa zilizo nyingi sasa sio noti tena zilizo mikononi bali zinawekwa katika mabenki, kama amana na katika malipo ya hundi. Uwekaji fedha katika benki ikawa ndiyo njia iliyozoeleka na kuonekana ya kawaida ya kutunzia fedha.

 

Nini kazi kubwa ya Pesa?

 

-      Ni kipimo cha amana, inaeleza bei au thamani ya kipesa ya bidhaa – vitu au huduma.

-      Inaonyesha uwezo wa kununua alio naomtu na inawezesha ubadilishanaji wa bidhaa yaani vitu na huduma.

-      Inatunza au kuhifadhi thamani kwa kuonyesha uwezo wa kununulia katika siku za mbele, inawezesha mtu kufanya manunuzi kwa siku zijazo, ni usalama au kinga na ni akiba.

 Kazi hizi za fedha zinawezesha thamani ya fedha kubaki imara.

 Thamani ya pesa ni kama chombo au kifaa kinachotumika kununulia vitu na kukamilisha mahitaji yetu. Kuwa na hiari ya kutoa fedha ili kupata kitu kingine au huduma, inamaanisha kuwa tunataka kitu kile au huduma ile na ya kwamba hilo ni hitaji lililopo linalohitaji kukamilishwa.

 Kazi ya tatu ya fedha iliyoelezwa hapo juu ambayo ni kuhifadhi thamani, ilianzishwa katika karne ya 16 ikiwa katika namna iliyo tofauti kabisa iliyojulikana kama utoaji wa mikopo na ukopeshaji wa mitaji. Hii inampa mtu kutumia fedha za mwingine na kulipe bei fulani kwa kutumia fedha hizo. Bei hiyo ndiyo riba ya mtaji. – Itaendelea toleo lijalo

 

MILA NA UTAMADUNI

 

Wahaya: Kabila linalotumia majani ya migomba kulia chakula badala ya sinia

 

l Senene ni kipimo cha upendo

l Msichana anapoanza kuchumbiwa marufuku                     kuonekana      nyumbani kwa mchumba wake

 

Na Dalphina Rubyema

 

WAHAYA ni miongoni mwa makabila 120 yanayopatikana nchini Tanzania. Kama yalivyo makabila mengine, Kabila la Wahaya nalo linaheshimu na kuendeleza mila na desturi zake za tokea enzi na enzi.

Kabila hili linapatikana Kanda ya Ziwa katika Mkoa wa Kagera  wenye wilaya sita ambazo ni Bukoba-Mjini, Bukoba-Vijijini, Ngara, Biharamulo, Karagwe na Muleba.

Mkoa huo unayo makabila mengine pia ambayo ni Wanyambo, Wasubi, Wahangaza, Wahamba, Waziba, Waganda-Kyaka, Wayoza na Wanyahiangiro na chakula chao kikuu ni ndizi.

Bibi Stelia Mkarutinwa, Mkazi wa Kishanda wilayani Muleba, anasema kuwa si jambo la ajabu ndizi kuliwa kila siku kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mwaka.

Anasema zamani kama ingetokea familia moja ikapika ugali, basi ilikuwa ikihesabika kama familia maskini na yenye ufukara.

“Nakumbuka mimi nilivyokuwa na umri kati ya miaka 12-16 hivi, ikitokea nyumbani tukapika ugali, basi sufuria lilikuwa likioshewa katikati ya shamba kusudi usionekana na wapita njia kwamba unaosha sufuria lililopikiwa ugali,”anasema mama huyo ambaye kwa sasa umri wake ni miaka 51.

Hata hivyo mama huyo anasema kwa sasa hali imebadilika kutokana na migomba kuharibiwa na mdudu aliyemtaja kwa jina la ‘ekiuka’ ambaye hukausha migomba.

“Sasa hivi hatuoni tena aibu ya kula ugali, tunakula tu tena wakati mwingine hata mara tatu kwa wiki pamoja na mihogo, viazi vitamu na viazi vikuu,”anasema.

Anasema kwa Wahaya, wakati wa chakula hususan cha mchana, mlango hurudishiwa kidogo (haufungwi kabisa) na birika au jagi la maji huachwa nje.

Hii inamuashiria mtu yeyote akiwamo mgeni kujua kuwa, ndani kuna watu wanakula., hivyo kama ana njaa au anahitaji kula, anaruhusiwa kugonga na kuigia na kama tumbo lake liko sawa, basi ni nafasi yake kuutumia muda huo kupumzika nje huku akiwasubiri wenyeji wake wamalize kula, badala ya kuwaingilia katika mlo, shughuli ambayo ni nyeti na isiyohitaji usumbufu wa namna yoyote. Hii ni ishara thabiti ya heshima kwa chakula.

Chakula hupakuliwa kwenye sinia ambapo chini yake huwekwa majani ya migomba “embabi” na wakati mwingine chakula hicho kinaweza kupakuliwa kwenye majani tu, bila kuweka sinia ekiyulo’.

Wanafamilia wa Kabila hilo wamezoea kulia sehemu moja bila kujali jinsia isipokuwa, wanaopakuliwa ni watoto wadogo. “Lakini kama ni suala la mboga, kila mtu hupewa bakuli yake,” anasema Bibi Mkarutinwa.

Kabila hili ni miongoni mwa makabila machache yanayothamini suala la elimu ambapo wazazi mkoani humo hujitahidi kuwapa elimu watoto wao, bila kujali jinsia na hii ni moja ya sababu inayowafanya Wahaya katika sehemu mbalimbali nchini kuitwa jina na “Nshomile” ikiwa na maana kwamba NIMESOMA.

Wakazi wa Mkoa wa Kagera, licha ya kujishughulisha na kilimo, vile vile wanajihusisha na ufugaji, ufinyanzi wa vitu mbalimbali, uvuvi, uwindaji na kazi za mikono ukiwemo ufundi seremala na ususi.

Zamani, wakazi hawa walikuwa wanaishi kwenye nyumba za misonge, lakini kwa hivi sasa hali hiyo imebadilika kwani wengi wanaishi kwenye nyumba za kisasa na zile za msonge zimebaki kwa familia chache, hususan zile za Kitemi “Abakama” ambazo zinajulikana kamaekikale”.

Tofauti na makabila mengi nchini, kabila hili la Wahaya lina koo mbalimbali.

Bw. Fredeick Kamugisha, mkazi wa Itahwa, Bukoba-Mjini, anasema kwa misingi ya kabila hilo, mvulana wa ukoo fulani hawezi kumuoa msichana wa ukoo huo huo ama kuoa msichana ambaye ukoo wake umefanana na wa mama yake.

Anataja baadhi ya koo hizo kuwa ni Abalisa, Ababele, Abakuba, Abasimba, Abahiyuzi, Abalili na koo nyingine nyingi ambazo anasema idadi yake zinaweza kuzidi hata hamsini.

Kwa mujibu wa Bw. Kamugisha, mara nyingi wasichana wa mkoa huo, huolewa wakiwa na umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea, jambo ambalo ni tofauti kidogo na baadhi ya mikoa hapa nchini ambayo huoza mabinti zao wakiwa na umri wa miaka 13 na kuendelea.

Bibi Bededicta Rutabanzibwa, anasema kuwa kwa kawaida binti akipata mchumba, mara nyingi kwanza huwa anamwambia mama yake, ama shangazi yake na baada ya hapo, maongezi baina ya mama na shangazi hufanyika kwa siri bila baba kufahamu.

Anasema kama mvulana anafaa, basi humwambia binti yao kwamba ampe ruhusa ya kuja nyumbani kutangaza posa “okusherela” na kama hafai, vile vile binti anayehusika huambiwa bila kufichwa.

Anasema kwa upande wa mwanamume, naye akipata mchumba, kwanza hutoa taarifa kwa ndugu wa karibu kabisa na baba yake,pengine anaweza kuwa kaka, baba mdogo, rafiki wa karibu kabisa na baba na wakati mwingine, anaweza kuwaambia moja kwa moja wazazi wake yaani baba na mama.

Anasema baada ya kuona binti anafaa, baba huwa na jukumu la kumtafuta mshenga “omushelezi”ambaye hutumwa kwenda nyumbani kwa wazazi wa huyo binti.

Anasema kwa kawaida mshenga kwa siku ya kwanza, huenda nyumbani kwa binti huyo saa za asubuhi ambapo akisha bisha hodi na kufungiliwa, huenda moja kwa moja kuketi chini bila kukalia kiti ama kitu kingine cha namna hiyo.

Wazazi wa binti wakisha ona hivyo, moja kwa moja huwa wameisha hisi kwamba huyo mtu anatafuta posa nyumbani hapo ila swali kichwani mwao hubaki je, ni binti yupi (kama wana binti zaidi ya mmoja).

“Hata kama mshenga huyo atakuwa ameizoea hiyo nyumba kwa kiasi gani, akitumwa kupeleka posa kamwe hawezi kukalia kiti bila kuruhusiwa na hili zoezi huendelea hadi siku watakapo mkabidhi mke (mgole),” anasema Bibi Benedicta.

Baada ya hapo, mshenga huyo husema kile alichotumwa na baba wa yule mvulana na baada ya hapo wazazi wa msichana humuuliza huyo mshenga wazazi wa huyo mvulana, ukoo na wakati mwingine kabila.

Kwa mujibu wa Bibi Benedicta, baada ya mshenga kujibu maswali aliyoulizwa, kwa kawaida wazazi wa binti hawawezi kutoa jibu la moja kwa moja kwa siku hiyo na badala yake, humwambia aondoke na kurudi siku maalumu ambayo humpangia.

Anasema wazazi wa binti hutumia mwanya huo kumuuliza binti yao kama anamfahamu huyo mvulana pamoja na kuwapa taarifa ndugu wa karibu.

Siku ya siku inapotimia, mshenga hupewa jibu, kama posa imekubalika au la. Basi mshenga huyo hunyanyuka chini kwa furaha na kuanza kuwashika miguu watu wote wanaokuwepo nyumbani kwa wakati huo.

“Kwa upande wa wanawake, mshenga huyo huwashika miguu na sehemu ya kifua huku akipiga makofi mawili mawili kila anapommaliza mtu mmoja na kumwendea mwingine”.

Anasema baada ya hapo hupewa barua maalumu ambayo huwa na orodha ya vitu vinavyohitajika ambapo anasema jumla ya vitu vyote haiwezi kuzidi 250,000.

Hata hivyo, kiasi hicho hupungua kulingana na jinsi upande wa mwanaume wanavyo jieleza.

Anasema utaratibu wa kutoa mahari, hupangwa na wazazi wa mwanaume ambao hutoa kwa awamu na inaweza ikafika hata awamu kumi, kulingana na uwezo wa mtu.

Anasema kila siku ya kuleta mahari inapowadia, wazazi wa binti huwaarika ndugu jamaa, marafiki na majirani (abanyansi) kwa ajili ya kushuhudia kitu hicho na mara nyingi mahari inayotolewa kwa kabila hilo ni pombe aina ya “olubisi”.

Anasema wanaopewa mahari (amakula), ni pamoja na baba, mama, mama wa ubatizo, babu na bibi wa pande zote mbili (wazaa baba na wazaa mama), shangazi, mjomba, baba mdogo na mama mdogo.

Baada ya mahari kukamilika, hufuatia suala la kupanga tarehe ya ndoa na zoezi hili huwahusisha wazazi wa pande zote mbili na ndoa ikisha fungwa, wazazi wa mwanamke hawaruhusiwi kumsindikiza bibi harusi kwenda kwa mume wake na badala yake, majukumu yote huachiwa shangazi.

Wanawake ambao ni ukoo mmoja na mama wa bibi harusi, siku ya harusi, huzungushia uzi mweupe kichwani (eseisa)kama alama ya kutambulisha kwamba hawa ndiyo mama wazaa chema na hupewa heshima kama ile ambayo angepewa mama mzazi.

Kwa upande wa wanaume, mama Rutambazibwa anasema wazazi wa kiume kutoka pande zote mbili, huvaa kanzu nyeupe na pengine kwa juu huweka koti huku wakiwa wameshikilia vifaa maalumu vya kunywea pombe ‘ebilele’ (kwa wale Wakristo).

Kwa mujibu wa Mama Rutambazibwa, wakati wa uchumba, msichana (bibi harusi mtarajiwa) haruhusiwi kukanyaga nyumbani kwa mchumba wake hadi siku ya ndoa.

“Hata kama mchumba wake atapata matatizo gani, msichana wake haruhusiwi kukanyaga kwake. Na hata kama atafiwa na nani, watatumwa wawakilishi, lakini siyo yeye. Ila ikitokea huyo mchumba wa kiume akafariki, basi msichana wake ataruhusiwi kufika na kumuaga mpendwa wake na si vinginevyo” anasema.

Kwa mujibu wa mila na desturi za Kihaya, mvulana aliyeoa haruhusiwi kula akiwa sehemu moja na mama mkwe wake (Nyinazala), na pia, mwanamke aliyeolewa katika ukoo fulani, haruhusiwi kula akiwa sehemu moja na baba mkwe wake (Ishezala).

Kabila hilo pia linahusudu wadudu aina ya SENENE ambao hupewa heshima kubwa kuliko kitu kingine.Senene ni wadudu wanaofanana sana na panzi. Wengi waliokwisha wala, husimulia utamu wa wadudu hao ambao kwa kawaida hukaangwa bila kutumia mafuta.

Kutokana na heshima hiyo, wakati wa uchumba, bibi harusi mtarajiwa hulazimika kupata senene wa kutosha ambao msimu wake ni miezi ya Oktoba hadi Novemba, na baada ya hapo, wasichana wa rika yake, humsaidi kupeleka senene hao kwa mchumba wake.

Huko nako, bwana harusi mtarajiwa huwaarika vijana wenzake ambao huupokea ugeni usiopungua watu 25-50 na kuungana naye kula hao senene.

Kwa mujibu wa taratibu na kanuni za kabila hilo, kila anayeonja senene hao, hulazimika kutoa kiasi fulani cha pesa kama shukrani (elongolo) bila kujali idadi ya senene aliokula.

Bibi Benedicta anasema kuwa hata kama utakula senene mmoja ama wawili, lazima utoe pesa na wingi wa pesa inayokusanywa hutegemea ushapu wa hao wajumbe wanaokuwa wametumwa na bibi harusi mtarajiwa.

“Wapambe kutoka kwa bibi harusi mtarajiwa hushika sahani ama kifaa maalumu kinachojulikana  kwa jina la ekibo ambacho hukipitisha kwa kila mvulana anayekuwa pale huku wakiimba nyimbo za kuwashawishi waongoze pesa”

Aliongeza, “Utasikia wanaimba, shemeji bahiri, ongeza kidogo, bado hatujaona, na kwa vile watoto wa kiume hutaka sifa, basi hujikuta wakitoa pesa kila nyimbo hizo zikiimbwa.

Wengine hutaka hata kujionesha jinsi walivyo na pesa kwani wakati huo pia huutumia kupata wachumba kutoka miongoni mwa hao wasichana”.

Anasema baada ya hapo, pesa yote hukusanywa na mara nyingine huweza kufika hata 50,000 na hupelekwa kwa msichana, lakini vifaa vinavyokuwa vimebeba hao senene, hubaki nyumbani kwa bwana harusi mtarajiwa ambapo upande wa mwanamme hukusanya hela na zawadi nyingine ambazo huambatana na vifaa hivyo wakati wa kuvirudisha kwa mhusika na kazi hii ya kurudisha vifaa, hufanywa na dada zake mvulana zoezi ambalo linaweza likachukuwa hata wiki mbili.

Mama huyo anaendelea kusimulia kuwa zoezi la senene haliishii kwa mabibi harusi watarajiwa tu, bali hata wasichana wengine ambao uchumba wao unakuwa haujahalalishwa ambao nao kwa vificho, huiba visosi kutoka kwa wazazi wao na kuwawekea wavulana wao senene ambao nao pi huwapokea kwa vificho na vikirudishwa (visosi) vile vile huja na pesa ama zawadi nyingine.

Anasema endapo mvulana atakubali kula hao senene bila kurejesha kisosi chenye pesa, basi ni dhahiri kuwa huyo msichana hampendwi na kama msichana hatampelekea mvulana wake senene, basi ni wazi kuwa hampendi mvulana huyo.

“Senene ni kipimo kizuri cha kujua kama mtu fulani anakupenda. Pia, ni wazi kwa Wahaya, unapokula senene peke yako, ni ishara ya uchoyo miongoni mwa vijana wenzako na inashiria kuwa wewe ni mroho, huna ushirikiano na wenzio na hata humpendi kiasi cha kutosha mwenzio.”

Utamaduni wa kutumia senene kama heshima pekee na ishara maalumu ya upendo katika ndoa, zinarithishwa toka vizazi na vizazi.

Inapotokea waliooana hasa mwanamke akampa mumewe senene, ni sharti, tena lazima mwanaume amtafutie zawadi mkewe hususan kitenge, vinginevyo, mwanamke huyo atakula senene tena mbele ya mumewe huyo.

Kwa kawaida kwa mila za awali Mwanamke wa Kihaya, haruhusiwi kula Senene mbele ya mumewe kwani kufanya hivyoo ni kumuabisha.

Ukifika msimu wake wazazi wengi hupotelewa na vifaa kama visosi na sahani ambavyo huwapelekea senene wavulana wao. Ukifika msimu kama huu wazazi huwa macho sana,” anasema.

Anasema tofauti na zamani ambapo mvulana wa Kihaya akikua anaruhusiwa kuoa msichana wa kabila lake tu, hivi sasa mila hizo zimepitwa na wakati vijana hao wanaoa ama kuolewa na watu wa kabila lingine ili mradi wawe wamekubaliana.

 

UCHAMBUZI WA KITABU

 

Kitabu: CHUNGU TAMU

Mwandishi: Theobald Mvungi

Mhakiki: Projest M. Christopher

 

"Majambazi wanayo idhini,

Kufanya lijalo akilini

Na hawataingia nguvuni,

Ma'na walinzi wamo njamani

Tabu yaanzia kileleni" (Uk. 32)

Lakini haya yote sio kwamba watu wa chini hawajayajua la hasha, wamesha yajua na dawa yake inatafutiwa vikombe ili inywewe wapo tu wanavumilia ili suluhu ipatikane, haya yamejidhihirisha katika shairi la "Mjanja yu Mashakani":

"Shangilio zimekwisha miguno imeenea,

Wasema ati yatosha, nguvu zimetuishia,

Miaka ya kupotosha, ishirini yazidi,

Watwana wakiamka mjanja yu mashakani" (Uk. 26).

Watu hawa wa chini wameanzisha migomo baridi ya kugomea mfumo wa wanaovuna bila kupanda.

3. Mapenzi na ndoa: Mapenzi yanayoongelewa hapa ni yale yanayolenga uchumba na ndoa sio yale ya mtu na nduguye.

Katika Chungu Tamu yameoneshwa mapenzi ya dhati na yasiyodhati. Mapenzi ya dhati ni yale ya Thomas na Doto na Mashaka na Dorothy, yasiyo ya dhati ni yale ya Ana na Nania. Pia Adam Kiende na Eva ni mapenzi ya dhati.

Mapenzi ya dhati ni yale yasiyojali tabu wala raha, utajiri wala umaskini bali kama moyo umependa umependa tu.

Thomas (mzungu) alimpenda sana Doto (mwafrika) na pia Doto alimpenda Thomas. Mzee Roland na mama Thomas walijaribu kumkanya mwanao asimwoe mwafrika kwani ni mikosi mitupu lakini hayo ni bure

"Mtoto Thomas Penda tena sana,

Weusi wana laana,

Mweusi hamtapatana

Utaharibu wako uungwana" (Uk. 41)

Thomas anayepuuza maneno ya mamake kwani si ya busara yamejaa ubaguzi na uchaguzi wa mpenzi ni kwa mhusika mwenyewe.

"....Kauli yetu ndoa tutaiweka,

Wote walitamka, .....(uk. 40)

Mwishowe Thomas anasema

"..Busara yenu naihofu" (Uk. 43).

 

Mashaka na Dorothy nao walikuwa na mapenzi ya dhati kwani tunaona mpaka mwisho wanaoana na kupata mtoto mbali na vikwazo vilivyowekwa na wazazi wa Dorothy eti kupendana na kijana wa Manzese na sio Ostabei.

Mama yake anamuasa:

"Binti usijefanya kosa,

Ukaolewa na Mkora,

..................

Gabrieli anakufaa" (Uk. 53).

Lakini hayo yote bure Mashaka na Dorothy wanaoana na kuamua kuishi Buguruni. Kigezo cha wazazi wa Dorothy walichokitumia hakina msingi kuwa ni maskini na anaishi Manzese wakati  wazazi wa Dorothy matajiri baba yak ni Waziri.wanasahau kuwa mapenzi ni majani huota popote.

".....wewe iko bwana yangu maisha" 9uk 23)

"Sasa nina mke"Uk 25

Hizi ni baadhi ya nukuu kuonesha mapenzi kati  ya Adam na Evadore walivyoona bila kujali vita ambavyo ilikuwa kazi iliyowapelekea kule walipokutana:

"But this is war sir" 9Uk. 20).

Katika shairi la "Fikira za waungwana" tumeona jinsi Ana alivyokiuka maadili ya ndoa na hivyo hana mapenzi  ya dhati kwa Nania. Ana anapenda wawili mara Nania mara Josefu, anataka haki ya kumiliki waume wawili kama wanaume wawezavyo kuwa na wake wawili:

"Mume wangu nakupenda, Josefu amenikuna,

Nimekula naye tunda, nampendelea sana,

Ila usifanye Inda, mimi ni wako kimwana,

Nitaishi kwa mpango kwako na kwake Josefu" (Uk 56)

Lakini waungwana ni waungwana siku zote wanaamua kuwa Ana kavunja ndoa:

"Fikira za waungwana, Ana kaivunja ndoa" (Uk 57)

Hivyo mapenzi tuwaachie wapendanao.

 

Matabaka: Kutokana na mfuno mzima wa uongozi jamii katika Chungu Tamu imegawanywa katika matabaka wenye nacho (watawala) na Wasio nacho (watawaliwa) upo pia ubaguzi wa rangi kwani  wazazi wa Thomas wazungu hawa kupenda kuchanganya rangi hasa nyeusi wanasema ina hawa kupenda kuchanganya rangi hasa nyeusi wanasema ina laana:

"Mtoto Thomas penda tena sana

Weusi wana laan

Mweusi hamtapatana

Utaharibu wako uungwana" (Uk. 41)

Wazazi  wa Doroth ( Mzee Shibe) wanamkataa Mashaka sababu ni mtu wa chini (hanacho). Pili anaishi Manzese wakati wao wanaishi Ostabei. hii inatuonesha jinsi jiji letu Dar na hata nchi nzima ilivyogawanywa, watu wenye fedha wanaishi Ostabei wakati maskini wanaishi Manzese:

Sijui kama ni kweli, lakini maisha ya Masaki na Ostabei ni sawa na yale ya Tandika na Mtoni? Je viongozi wetu wanaishi Manzese au Ostabei?

 

5. Urafiki usio dhati: Pengine waweza kusema usaliti, Chatu aliyeachiwa dhamana ya kuwalinda watoto wa Marehemu  kuku Piku na Paku anawageuka na kujifanyia kitoweo. Baada ya mauti kumfika kuku alitoa maneno ya mwisho ili urafiki udumu lazima muishi tofauti kwa sababu maumbile yenu.

"Basi Chatu urafiki udumu

Hata japo sipo humu,

Naye mwewe mtafute hakimu

Adhabu impate" (Uk.4).

Lakini Chatu anawarubuni Piku na Paku ili waishi wote pangoni.

 

Muislamu, Mkatoliki mnataka kuoana ; mnayajua haya? (2)

Katika toleo lililopita, tuliishia katika kazi za ndoa kwa mtazamo wa Dini ya Kiislamu. Tuliona kuwa ibada ya Muislamu aliyeoa au kuolewa, ina thawabu kubwa kuliko ibada za Waislamu ambao hawajaoa au kuolewa. Sasa endelea na kazi za ndoa kwa Wakristo

Kwa Wakristo, kukutana kimwili kwa mwanamke na mwanaume ambao hawajaoana ndani ya ndoa takatifu, ni dhambi na ukiukaji wa sheria.

Vijana wanahimizwa kuzitawala tamaa zao za kimwili hadi wanapoingia katika ndoa halali ya kikanisa.

Kwa mujibu wa mapokeo ya Kanisa, mke na mume waliooana, wanayo haki kamili ya kuwasiliana kimwili na hivyo, kutimiza haja zao za kimwili. Kitendo hicho ni halali na ndicho huikamilisha ndoa husika.

Maneno hayo yote yanafupishwa na kuhitimishwa na ukweli kuwa, ndoa baina ya wabatizwa, haijakamilika kama wanandoa husika hawajakutana kimwili (Rejea Sheria ya Kanisa Na. 1141-1150).

Pia, kwa Wakristo na hususan Wakatoliki, ndoa ni njia pekee na sahihi ya kuzamisha na kuimarisha uhusiano bora baina ya wahusika; tena kwa muda wa watu wa maisha yao.

Hii inatokana na ukweli kuwa, watu hao sasa wamekuwa mwili mmoja, akili moja na roho moja ambayo isingewezekana kabla ya ndoa.

Kwa Wakristo, ndoa ndiyo njia pekee sahihi inayowezesha watoto kuzaliwa.

Pia, ndoa hutumika kuunganisha watu na kuimarisha uhusiano miongoni mwa jamii. Ndugu, jamaa na marafiki toka pande zote za wanandoa, hutumia ndoa kujenga uhusiano mpya baina yao.

Ndoa takatifu inavunja na kuondoa mipaka yote ya kijamii baina ya ndugu, jamaa na marafiki wa pande zote; kwa upande wa mume na mke.

Hii ni kusema kuwa, ndoa huondoa tofauti na ubaguzi wa kikabila, kidini, matabaka na mengineyo yakiwamo masuala ya kiuchumi, na hivyo kuwaweka katika umoja, amani na upendo wa ki-Mungu.

Ni dhahiri kuwa wanaume na wanawake wana vipaji tofauti. Ni kupitia ndoa, waliooana wanashirikishana vipawa vyao kwa kadiri wanavyozidi kuwa pamoja.

Kadiri watu hawa wanavyoimarisha upendo miongoni mwao, hisia zao zinawafunga pamoja na kuwafanya wahudumiane kwa siku zote za shida, na za raha huku wakivumiliana kama walivyoahidi.

Katika Agano Jipya, ndoa inatazamwa kama taswira ya uhusiano mkubwa , mzito na imara, uliopo baina ya Kristo na Kanisa.

Ndoa huakisi upendo wa juu kabisa baina ya Mungu na watu (Rejea. Rv21: 1-4).

Mafundisho ya kimaadili katika ndoa ya Kiislamu.

Uislamu unahimiza hali ya kujisikia haya na kuepuka kufanya mambo kinyume na taratibu. Hali ya kuwa na haya, inamfanya Muislam asiwakwaze na kuwatia waamini wengine vishawishini.

Kwa Waislamu, muonekano wa kutamanisha ni marufuku kwani unaweza kuwavuta na kuwatumbukiza katika tamaa ya kimwili (msukumo wa kingono).

Kwa Waislamu, uzinzi ni dhambi (kosa) linaloweza kutolewa adhabu katika mahakama ya Kiislamu. Kama mwanamke na mwanaume ambao si wanandoa, watapatikana na hatia hii, adhabu yao imeandikwa kwenye Kurani.

Kwa mujibu wa Kitabu cha ABOUT CATHOLIC/MUSLIM MARRIAGE, kilichoandikwa na Prisca M. Wagura, kama mwanaume au mwanamke ambaye hajaoa au kuolewa atashitakiwa zaidi ya mara moja, anaadhibiwa mara tatu na kama watarudia tendo hilo, kwa mara ya nne, wanahukumiwa kifo.

Matendo la kujamiiana kabla ya ndoa, punyeto (masturbation), ulawiti na usagaji (lesbianism), kama njia ya kukidhi tamaa ya kimwili, yanakataliwa vikali sana.

Mambo mengine yanayozuilika kwa mujibu wa mafundisho ya kiroho yaliyo katika Kitabu hicho, ni MATUMIZI YA PAFYUMU KWA MWANAMKE ANAPOTOKA NJE.

Mengine yanayozuiwa kabisa na Uislam, ni mwanaume kutumia muda mwingi kuwa pamoja na wanawake wengine wa nje badala ya mke wa ndoa, kugusa miili ya wanawake, kucheza muziki, kwenda kwenye sinema, unywaji pombe na mengineyo mengi.

Uislam unafundisha kila mmoja kutambua umuhimu wa matumizi sahihi ya viungo vyake vya mwili vikiwamo viungo vya uzazi.

Inaruhusiwa na kuhimizwa kuwa, kijana wa kike au wa kiume, aoe au kuolewa mara moja wanapofikia umri wa kukomaa au kubalehe

Baada ya kubalehe mvulana na msichana wanaweza kuweka mkataba wa makubaliano ya ndoa na kisha kuahirisha sherehe za ndoa huku wakiendelea kuishi na wazazi wao hadi wanapomaliza masomo.

Wanapashwa kuheshimu usafi wa Roho na kuepa.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislam, Useja si tu ukiukaji wa sheria hivyo ni uharifu, unaopinga mpango wa Mungu. Ni hali inayokatazwa kabisa

Pia, Uislam unakataza mwanaume kumuoa mama na mama mkwe wake, binti yake, bibi zake, dada zake, mashemeji . (Rejea Kuran 4:22-24).

Inaelezwa kuwa, Uislam pia unatakataza kuoa mtu wa dini tofauti. Inasadikika kuwa, wanandoa hawataishi kwa upendo wa kutosha kwa kuwa watatofautiana namna ya kuishi (Rejea Kuran 2:221).

Mwanamke Muislam kuolewa na mtu asiye Muisalm ni kitu kinachozuiwa vikali sana, lakini kwa mwanaume kumuoa asiye Muislam, inaruhusiwa kwa mtazamo wa kuwa, lazima mwanamke huyo atasilimu na kuwa Muislam.

Ndoa za muda kwa Waislamu zinachukuliwa kama uzinzi na uasherati; zinapunguza heshima ya ndoa.

 

Maandalizi ya Ndoa kwa Wakatoliki.

 

Kwa Wakatoliki, wavulana na wasichana wanaruhusiwa kuchanganyika na kujenga urafiki miongoni mwao wote hata kabla ya ndoa, isipokuwa urafiki wa kimapenzi (tendo la kukutana kimwili), ni kitu kinachokatazwa sana.

Lengo la kuruhusu wavulana na wasichana kuwa pamoja ni kuwapa fursa ya kujifunza vitu mbalimbali, kuchangiana mawazo na kuwajengea msingi bora wa kujiamini katika kuhusiana na watu wengine wa jinsia tofauti.

Katika Bara la Afrika, kwa kawaida suala la kuchagua mchumba hufanywa na wazazi na vijana wenyewe. Hatua kubwa na ya kwanza kabisa katika suala la ndoa, ni wachumba wenyewe kuchaguana na kisha, kuwajulisha wazazi na rafiki zao.

Kwa kawaida, wazazi wa mvulana, ndugu, jamaa na marafiki, hufanya mazungumzo na mipango muhimu na kisha, kujitambulisha kwa wazazi wa mchumba wa kike (msichana) juu ya azima yao.

Kwa Waislamu, vijana wa kike na wa kiume, wanahimizwa na kutiwa moyo, kuingia katika maisha ya ndoa wanapofikia umri wa kupevuka (wastani kwa wavulana ni miaka 20 na wasichana ni miaka 17).

Endapo wazazi watazuia mvulana na msichana kuoana baada ya kutimiza umri wa kupevuka, kisha vijana hao wakatenda dhambi, adhabu ya dhambi hiyo itawaangukia wazazi hao.

Kuhusu kuchagua mchumba, wazazi wa mvulana huhusishwa katika kumchagua binti kwa ajili ya kijana wao.

Msichana huyo anapaswa kuwa mwenye uchaji, usafi wa moyo, mrembo, mwenye afya njema, mwenye uelewa wa kutosha juu ya dini yake (Uislam), aoneshe uwezo wa kutunza familia na awe na uwezo wa kuzaa. Lazima pia awe na tabia njema.

Taarifa juu ya msichana huyo, huchunguzwa na kukusanywa bila msichana huyo kujua.

 

Itaendelea toleo lijalo.

Utalii ni mtaji wa Watanzania

Na John Mapepele

Msemo kuwa Mtaji wa Maskini ni Nguvu Zake Mwenyewe ni baadhi ya misemo ambayo imekuwa ikisikika sana katika kipindi cha Awamu ya Tatu ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) nchini.

Msemo huu umekubalika sana na wananchi baada ya viongozi wa juu wa kitaifa akiwamo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamini Wiliam Mkapa, kuutumia katika majukwaa ya kisiasa.

Rais Mkapa amekuwa akitoa ufafanuzi wa msemo huu kuwa  wananchi wanahitaji kutumia maliasili walizo nazo katika kujiletea maendeleo ya kiuchumi.

Sote tutakubaliana kuwa kuhimiza maendeleo kwa wananchi ni baadhi ya majukumu ya  Rais wa nchi. Hata kama  kiti hicho cha Urais kisingekaliwa na Mkapa, kitu kinachoweza kumfurahisha mpenda maendeleo yoyote, ni mfumo wa Rais Mkapa kupenda wananchi wapate maendeleo. “Mfumo wa mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe.

Ni ukweli usiopingika kuwa  Mkapa  amekuwa na tabia  ya kuyatumia majukwaa ya siasa na ziara mbalimbali ndani ya nchi kuzungumza na wananchi na kuwawahimiza watumie nguvu  na uwezo walio nao, kujiletea maendeleo kwa kutumia uwezo wao bila kujidanganya kutegemea maendeleo kwa misaada kutoka kwa wahisani.

Kwa mfano, katika ziara aliyofanya katika Mikoa ya Kusini mwa Tanzania, Rais Mkapa alikaririwa akitoa rai kwa wananchi kujenga shule za misingi, kuchimba na kutumia vyoo.

Amesema kwa kuchimba na kutumia vyoo, wananchi watapiga hatua ya kimaendeleo itakayowawezesha kuepuka magonjwa ya kuambukizwa kama  vile  kipindupindu na kuhara damu.

Amekuwa akisisitiza pia kuwa, maendeleo siyo tu kufanya mambo makubwa yanayohitaji  fedha  za kigeni, bali hata kutoka katika hatua moja kwenda katika hatua nyingine bora, ni maendeleo.

Mfano wa hatua hizo, ni kama kutoka katika hali ya kutotumia vyoo na kuanza kutumia vyoo!

Mara kwa mara vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti Rais Mkapa  akiwaelimisha wananchi kutumia njia rahisi ya kuzuia mazalia ya mbu kuliko kutumia  vyandarua  au dawa za kujitibu.

Hapo, ni wazi kuwa Rais ameonesha kwa vitendo kuwa wananchi wanaweza kutumia uwezo wao mdogo wa nguvu na maarifa, kuzuia  mazalia ya mbu kwa  gharama nafuu, badala ya kusubiri fedha za kigeni  kuagiza  vyandarua na dawa  ambazo wananchi walio wengi hawawezi kumudu.

Jambo zuri zaidi ni kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele katika kutafuta njia rahisi zitakazosaidia  kuliletea Taifa maendeleo kwa kutumia nguvu na raslimali ambazo Taifa hili limebahatika kuwa nazo.

Pengine hapa  ni wazi kuwa ile dhana ya kutumia nguvu za wananchi au rasilimali  nyingi ambazo nchi nyingi hazina, inaweza kulisaidia Taifa kama kweli Serikali itadhamilia kufanya kama ambavyo Rais  Mkapa alivyoionesha dhana hiyo wakati akifungua Mkutano wa Kimataita wa Wawekezaji katika Sekta ya Utalii hapa nchini.

Katika Mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), Rais Mkapa alisema hivi karibuni kuwa, Tanzania inayo fursa nzuri ya kutumia  sehemu mbalimbali za utalii ilizo nazo ili kukuza uchumi wa nchi.

Amesema Tanzania imebahatika kuwa na vivutio vingi vya utalii ambavyo havipatikani sehemu nyingine  za dunia, hivyo endapo vitatumika ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwapa wazalendo kuwekeza,  vinaweza  kuinua  uchumi kwa wananchi wake.

Kwa  mujibu wa  Rais Mkapa,  sekta ya  utalii  imekuwa kwa kasi ukilinganisha na sekta nyingine kwani imeliingizia Taifa kiasi cha Dola milioni 32. 47 mwaka 1996 ambapo mpaka mwaka 2000, Dola  739 milioni za Kimarekani, zilipatikana kutoka katika sekta hii.

Takwimu za ripoti ya uchumi  barani Afrika,  zinaonesha kuwa, hata  baada ya ugaidi  uliofanyika katika  Balozi za Marekani katika nchi za Tanzaia na Kenya,  bado  sekta ya utalii inakuwa; ambapo inachangia  asilimia11 ya pato lote la Taifa  na kuna mategemeo ya kukua zaidi kwa  asilimia 5 hadi kufikia mwaka 2010.

Kwa upande wa Tanzania, ripoti hiyo inaonesha kuwa hata baada ya ugaidi huo,  watalii waliongezeka.

Takwimu zinaonesha kuwa, hata wazalendo Watanzania wamekuwa wakichangia kwa kiasi kikubwa katika sekta ya utalii, kwa mfano, katika hoteli za kitalii zilizopo katika Jiji la Dar es Salaam, wazalendo walipanga katika vyumba kwa  asilimia 44 na asilimia 48 mwaka 2000.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonesha kuwa katika miaka kumi utalii umekuwa kwa asilimia mia moja. Kwa mfano, kutoka mwaka 1990  fedha za kigeni zilipanda  kutoka  Dola za Kimarekani milioni  65 hadi Dola za Kimarekani 739.10 kutokana na utalii hapa nchini.

Takwimu hizi za Ongezeko la zaidi ya silimia mia moja katika pato la utalii, hazihitaji ufahamu wa juu kuelewa kuwa sekta ya utalii inaweza  kulikomboa taifa kiuchumi.

Hii inanifanya  nikubaliane na  Mheshimiwa  Rais Mkapa kuwa,  mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe, na kwamba  dhana ya sasa ambayo  amedhamilia kulinyanyua  Taifa  ni pamoja na  kutumia  rasilimali  za utalii, ambazo nyingi zinapatikana Tanzania pekee!

Baadhi ya rasilimali ambazo Tanzania inajivunia ni Mlima  Kilimanjaro, maziwa, mbuga  na  hifadhi za wanyama, vivutio vya kitalii vya kihistoria na  fukwe za Bahari ya Hindi.

Kitu kikubwa hapa ni  kuunda sera nzuri  ambazo zitatoa  wigo  na kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi  ili kuwekeza katika sekta hii.

Aidha, Serikali inahitaji kuwaelimisha wananchi wake kuhusu   umuhimu wa kutalii na kutembelea sehemu za kihistoria za kitalii kwa wananchi wake  ili kuongeza soko katika sekta hii.

Wengi mtakubaliana na mimi kuwa  asilimia  kubwa ya Watanzania  hawajawahi kutembelea sehemu mbalimbali za kitalii, za kihistoria kama vile masoko ya watumwa Zanzibar, mbuga za wanyama , Mlima  Kilimanjaro siyo kwa sababu ya  pesa, lakini pengine sababu kubwa  ni kutoona umuhimu wake.

Watu wengine wamekuwa  na dhana potofu kuwa utalii unafanywa na  wageni kutoka nje ya nchi ndiyo maana siyo jambo la kushangaza kuona wageni kutoka nje kwa  mfano  wamisionari wanaifahamu vizuri nchi yetu kuliko sisi wenyewe.!

Ni vizuri tukumbuke maneno ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu  Julius Kambarage Nyerere  aliyoyasema mwaka 1961 kuwa hifadhi  na mbuga za wanyama nchini  ni urithi wa vizazi vyote vya Tanzania.

 

Nionavyo Mimi

 

Kanisa lisipokuwa macho, Uamsho utakuwa hatari

 

Na Padre Baptist Mapunda

KWANZA kabisa napenda kuwapongeza wahusika wa gazeti letu la KIONGOZI kwa ujasiri waliotumia kuanzisha mazungumzo haya ya UAMSHO katika zama hizi za uwazi na kweli. Kwangu binafsi nilikutana na Uamsho au Karismatik mwaka 1994 huko Zambia nikiwa Mmisionari kati ya Wabemba. Nilikuwa Mkurugenzi wa Miito wakati nilipopita mashuleni nilikuta vijana motomoto kweli, na wakati wa kuuliza maswali, wakati mwingine waliniuliza vitu vya ajabu sana. Basi na muda si mrefu kikundi kilianzishwa katika Parokia niliyokuwa naishi iitwayo Serenje. Basi hapo nilianza kujionea mambo mbalimbali. Mara moja wanakarismatik au Uamsho waliondoka na kwenda sehemu za Kapiri Mposhi karibu na mji wa Lusaka, walikaa huko kwa wiki moja kwa mafungo na semina. Waliporudi walianza kujigamba kwa kusema. "sisi tuna ubatizo wa kweli, kwani tumebatizwa kwa moto' na hivi kuwadharau waumini wenzao katika jumuiya na vikundi vingine vya kitume.

Na mara moja walidiriki hata kusema kuwa mapadre hawana uwezo wa kuondoa pepo ila wao. Punde si punde walitaka misa yao ya pekee burua ya kwenda kuombea wagonjwa mahospitalini, baraka ya pekee nakadhalika; madai yakawa yanaongezeka tu. Baadaye tuliona hili ni fujo,' kama kumpokea Roho Mtakatifu ni vurugu, basi huyo si Roho wa Bwana' alisema padre mmoja. Na sehemu nyingine Maaskofu  ilibidi kuingilia kati kwa sababu kulikuwa na matabaka mawili moja la wakosefu na jingine la Watakatifu. Hii  yote ilitokana na majivuno, au majigambo. Hivi kuhusiana na Uamsho nimeona mengi sana. Hata nilipokuwa Nyakato, jimbo Kuu la Mwanza tulikuwa na kikundi, nacho hakikuwa na tofauti na kile cha Zambia kwa mfumo wake na kuishi katika jamii. Ilibidi waelimishwe, mimi nilikuwa karibu sana nao hivi nilijionea mengi sana; maajabu ya Musa namshukuru Mungu sikukwazwa. Hivi ilitupasa kuwekana sawa na hasa juu ya misingi ya Kikatoliki. Mara moja tuliona vioja vya watu kupagawa, kulia kukemea mashetani na pepo. Nadhani lazima tukubali kwamba huo si mfumo wa Kikatoliki wa Kusali. Kumbuka nabii Eliya alikutana na Mungu katika utulivu si ngurumo, na makelele ama vurugu.

 Ukweli ni kwamba Karismatik ni Chama cha Sala, huo ndiyo Utume wao baada ya kumpokea Yesu ni Bwana kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Nasema kwa Msaada kwa vile si nguvu za mtu wala akili  yake inayotumika bali ni Nguvu za Mungu.

Hata Petro ambaye alikuwa karibu sana na Yesu Kristu, alipokiri kwamba "Wewe ni Mwana wa Mungu aliyemzima" kwamba ilikuwa ni kwa Mungu Baba aliyewezesha yeye kusema hayo.. Mapato ya kutambua hayo ni kwamba Petro hakujawa majivuno na kujiona ni bora kuliko wenzake.

Alikuwa Mnyenyekevu na mvulivu. Kama walivyosema Mababa wa AMECEA kwamba, "Uinjilishaji wa kina ni changamoto la AMECEA katika Milenia ya tatu." Hapa lazima niseme wazi kwamba inashangaza kuona hata baadhi ya mapadre kuchukulia sasa Ukristu ni Ukarismatiki, lazima tuangalie na kupima mambo kwa busara. Tusitake kila mtu lazima awe mwanauamsho wala tusitake kila padre awe mwanauamsho, kwani Uamsho siyo kikundi, bali ni jinsi na hali ya mtu alivyompokea Bwana na kuishi naye hata bila kujiunga na kikundi.

Ukisoma katiba ya Karismatiki Tanzania, utafurahiia kwa vile imeweka mambo yote safi kabisa, lakini shida kubwa ni kuzingatia yaliyo ndani ya katiba. Katiba inasema kwamba Karismatiki ni Kikundi cha sala, ambacho lazima kiwe ndani ya Kanisa Katoliki, wala kisijitenge na kujitafutia mambo yake. Wanachama wake waanze kuamsha Imani katika jumuiya zao, wahamasishe huko kwanza. Kisijione ni kikundi cha watu wa pekee, kwa vile wanakiri wamempokea Roho, Roho wa unyenyekevu si majivuno na majigambo, Roho anayeunganisha na siye anayetenganisha.

Lazima tusema wazi kwamba kuna baadhi ya Wakatoliki wanaokwazika na Ukarismatiki lakini hiana maana kwamba Ukarismatiki ni kitu kibaya. Ni kweli haujazoeleka, itachukua muda, Lakini pia Wanauamsho kama watasoma KIONGOZI toleo la Oktoba 19-25,2002 watanufaika sana, kwani Baba Askofu Kilaini ametoa uelewa mzuri sana ambao ndicho kiini na msingi wa Uamsho. Amesema kwamba kiini cha uamsho ni mkristu "Kusema kwamba Kristu ni Bwana na nguvu za Roho Mtakatifu, hivi vitu vingine vya lugha, kuponya, kuimba kwa makelele, na kurukaruka ni vitu vya kusaidia tu, wala siyo kiini cha Uamsho." Hongera sana Baba kwa kutusaidia kuuelewa Uamsho au Ukarismatiki. Lakini kwa mtazamo wangu kwa vile hata hapa Manzese kikundi hiki kipo na ninajionea mwenyewe kwa macho yangu na kusikia kwa masikio yangu na moyo naona wao wakati mwingine wanaleta picha ya kukazia mambo ya nje kama alivyosema Baba Askofu Method Kilaini kwa mtazamo wangu. Siku moja nilimwuliza mwanauamsho anieleze maana ya Ukarismatiki akasema "Sisi tunanena kwa lugha, tunakemea mapepo, halafu hatunywi pombe, wala kucheza disco (hatuendi ndombolo ya solo) akamalizia kwa kusema tunasali mara nne kwa wiki" Duuu!!!!

Nilipatwa na butwaa. Baadaye nikamwambia nenda ukatafakari kama hii ndiyo maana ya uamsho kama linavyoelewa Kanisa Katoliki na Maaskofu walioruhusu hiki kikundi, halafu urudi baada ya wiki moja. Lakini hadi leo ameingia mitini. Nasikitika kusema kwamba, baadhi yao wanakazia daima mambo ya nje tu. Ndiyo  maana mwisho wa siku ni kuwadharau waumini wengine ambao hawapo katika kikundi cha uamsho, na hii inaweza kufikia hata kuwadharau mapadre na maaskofu, imewahi kutokea katika nchi fulani fulani hapa Afrika. Inafika hatua ya kumkashifu Mama Bikira Maria, Rozari Takatifu na hata kuwakashifu mapadre kwamba hawana uwezo wa kupunga pepo, naona hii ni hatari katika Kanisa. Tukumbuke kuwa imani ya Wakatoliki haijajengwa katika misingi ya kufukuzia miujiza. Hii ni imani batili, lazima itakaswe. Imani ya kweli ni kumwamini Yesu Kristu, na kuamini hata pale akili yako inaposhindwa kuelewa mambo imani thabiti ni kuamini hata katika Mateso na masumbufu. Na huu ndiyo Wokovu, tunachohitaji ni maendeleo ya Kiroho na siyo ukamilifu wa siku chache (Spiritual Progress and not Perfection) Mungu anatuita kila siku, na kila siku ni tofauti.

Pamoja  na hali hii ya kutoelewa vema maana ya Uamsho kunakuwa na  hali ya kujiona wao ni watu wa pekee, kwamba hawawezi kuchanganyika na waumini wengine katika shughuli fulani fulani, nauliza ni kwa nini? Kuna mbegu ya utengano ambayo wa mtazamo wangu viongozi wakuu wa Kanisa majimboni (Maaskofu) lazima waichunguze, wa wasaidie kuirekebisha, kama alivyosema Baba Kilaini, tusiwatenge, wala usifutwe tuwe nao karibu ili tuweze kuwarekebisha. Swali Je wanarekebishika??

Mimi napendekeza kwamba kikundi cha Karismatiki kisijitenge tenge katika Parokia, na kupenda kuonekana kama watu wa pekee. Na mara nyingine kama pengine mtu ambaye si mwanauamsho anapofundisha kanisani hasa mambo ya biblia au ya Kiroho unawasikia wakinong'ona kwa kusema ati "hatujasikia neno" maana yake ni nini?  Siku moja nilikuwa natoa semina ya wanakwaya Juu ya "Wito wa Kwaya na Maadili" katika Parokia X " mara nikaona msichana anainuka na kwenda ubaoni kuandika maneno yanayohusiana na Roho Mtakatifu mimi nikamwacha baadaye nikawaambia wanasemina, naomba mmoja amwambie alichokosea huyu binti. Basi wakamwambia kakosa adabu, kwangu ni madharau, maana yake niliyokuwa nafundisha mimi ilikuwa ni utumbo, yeye ndiye anayejua zaidi. Hilo ni moja tu. Nilijiuliza kama mimi Padre nafanyiwa hivi, je wanapokuwa wenyewe inakuwaje?

Baba Askofu Kilaini ameongelea kwamba uamsho ulianzishwa na walokole, na hivi ninasikitika kusema kwamba na hao hao wakati mwingine wanaingia ndani ya Makanisa yetu na kupandikiza mambo yao. Jingine ambalo ni muhimu kulitazama ni la walimu wao wanaofundisha semina, naomba mapadre wa Parokia husika waonane na wakufunzi hao kabla ya kuanza uinjilishaji wao, inafaa kumjua ni nani? Anafundisha nini Naogopa wakati mwingine mafundisho yanapita kimo cha mwalimu au kuna weza kujiamini mno, na ninachoogopa ni kile alichotafadhalisha Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza kwamba "Msimchokoze Roho Mtakatifu ovyo ovyo kwa maana huwezi kujua atakupeperushia wapi" maneno haya yana ukweli mwingi tu, inafaa kuyatafakari. Nionavyo mimi UKARISMATIKI NI CHAMA CHA WAUMINI WALIOKOMAA KIIMANI NA SIYO KWA KILA MTU, LA HASHA!

Na pia ni vema kwenda pole pole na hasa katika mambo ya Kiroho. Pamoja na hayo kuna kipengere cha kusali, ambacho pengine kinatia wasiwasi, unakuta mtu anakuja parokiani kila siku mara nne tano kwa wiki, yupo hapo kuanzia saa tisa na kuondoka saa 1:00 jioni, je majukumu mengine ya nyumbani yanatekelezwa saa ngapi? je hakuna hatari ya kuyumbisha ndoa takatifu hapa? Haya yametokea sehemu zingine za nchi na hata hapa Afrika, ni vema kujiuliza je ninahitaji siku tano kwenda kusali na kikundi hicho cha uamsho?

Pia katika parokia kuna vikundi vingi sana ambavyo vinahitaji nafasi, ni lazima kuwafikiria wenzetu pia, tusichukie nafasi yote, tuwe na kiasi Mtakatifu Paulo anatuasa.

Mwisho napenda kusema kwamba UAMSHO KAMA UAMSHO NI KITU KIZURI SANA, ila kibaki kikundi cha Sala kikianzia katika Jumuiya. Pia naomba misingi ya Kikatoliki katika kusali na kuimba ifuatwe ninaposema misingi ya kikatoliki haina maana kwamba imani iliyododora na nyimbo kama za wafu katika Liturujia la hasha!

Kuwe na uchangamfu lakini siyo makelele ya kuwakwaza waumini wengine wenye imani haba kama mimi. Tena ningependa wanauamsho wenyewe kujiuliza Je wenzetu ambao siyo wanakarismatiki wanatuonaje?. Hii kama sehemu ya kujijua (Self -Knowledge) itawasaidia kujifahamu na kujupokea na kukubali kusahihishwa. Huo ndiyo mtazamo wangu juu ya Uamsho, naomba wabaki Wakarisimatiki Wakatoliki na siyo Walikole, namna nyingine kuna hatari ya kuharibu umoja ndani ya Kanisa letu ambalo ni Tunda la Roho Mtakatifu kama alivyoombea Yesu Kristu mwenyewe kwamba "nataka wawe kitu kimoja." Tukumbuke kwamba "Uamsho ni kumkubali Yesu Kristu kuwa ni Bwana (Mtawala, Mfalme wa maisha yako) kwa msaada wa nguvu za Roho Mtakatifu kwa unyenyekevu na utulivu ukiheshimu waumini wenzako."

Nimalize kwa kusema kwamba, lengo la mada hii si kulaumu, kukosoa tu bora kukosoa na kutafuta jina, bali ni kujengana katika Undugu; kama anavyotualika Baba yetu Method Kilaini kusahihishana na kusaidiana bila vinyongo wala chuki katika safari yetu ya mbinguni. Nawatakieni usomaji na uelewa mwema.

Gazeti la KIONGOZI asante sana kwa kutupa nafasi ya kutoa mitazamo yetu. KIONGOZI endelea kuongoza katika njia ya Ukweli, Haki, Amani na Uzima. Ama kweli Kristu ni Tumaini Letu!!!

 

MAKALA YA MICHEZO

'Taifa Stars sio kichwa cha Mwendawazimu'

Na Boniphace Makene

“TAIFA Stars yashika mkia wake, Kichwa cha mwendawazimu chaendelea kunyolewa, Stars hoi,” hivi ndivyo vimekuwa vichwa vya habari katika kurasa za michezo katika magazeti mbalimbali nchini,  kila timu ya Taifa inapomaliza mechi zake huku ikiwa imeambulia kipigo.

Maneno haya katika siku za hivi karibuni yalipata kujiri sana na hata baadhi ya wahariri wa magazeti hayo kuandika katika tahariri zao wakiwapongeza mashabiki wa soka kutokwenda kuangalia fainali za michuano ya Castle iliyokuwa ikifanyika katika uwanja wa Taifa.

Waandishi wa habari za michezo hususan soka,mara zote wamekuwa chachu ya kuundwa timu ya taifa na pia kuvunjika kwake.

Hawa wanafahamu ni nani wanamtaka achezee timu hiyo na mara zote wamekuwa wakiwapamba  baadhi ya wachezaji jambo ambalo limewarahisishia kupata nafasi katika timu ya Taifa. Ni ukweli ulowazi kuwa bila vyombo vya habari timu iliyochaguliwa kushiriki Kombe la Castle isingekuwa hii iliyocheza!

Pamoja na kazi hiyo inayofanywa na waandishi,ni ajabu unapomsikia waandishi hao eakiita timu ya Taifa eti ni “kichwa cha mwendawazimu’. Sishawishiki kuamini kwa nini wanafanya hivyo lakini nadhani wengi hawatambui kuwa wanajitukana wao wenyewe kwani timu hiyo ipo kwa minajili ya taifa na wao ni wadau muhimu katika taifa hili.

Hata Watanzania wengine wameiga tabia hii ya waandishi kwani nao sasa wanaiita timu yao kuwa ni kichwa cha mwendawazimu. Hawana hamu nayo tena wakidhani wanawakomoa wachezaji, viongozi wa FAT na serikali.

Hakika hawana habari kuwa wanajitukana wao wenyewe kwani timu hiyo huchukua dhamana ya kuliwakilisha taifa na kwa kufanya hivyo matokeo ya aina yoyote yanabeba hadhi ama adha ya Kitaifa miongozni mwa Mataifa! Wanashindwa kufahamu kubeba masuala ya Kitaifa wanadhani hapo pia kuna Usimba na Uyanga.

Nilipata fursa ya kuzungumza na wachezaji mbalimbali wa timu ya taifa kuhusiana na tatizo hili la timu yetu kutokufanya vizuri. Kila mchezaji alikuwa akifafanua sababu mbalimbali ambazo yeye anadhani zinachangia katika kuifanya timu hiyo kutofanya vizuri katika michuano ya Kimataifa.

“Timu ya taifa haiwezi kuandaliwa kwa siku mbili halafu ifanikiwe kushinda. angalieni timu za wenzetu wanavyoandaa timu zao. Zinakaa kambi hata miezi sita na zinakuwa ni timu za kudumu,” anasema Athuman Machuppa na kuendelea;

“Maandalizi ya timu yetu yanakuwa ya zima moto, hayana utaalamu wa kutosha kwani tunakutanishwa tu kwa siku moja halafu kesho tunasafiri na baada ya hapo tucheze mechi siku inayofuata. Kwa hali hii huwezi kupata ushindi kwani soka la sasa linajali taaluma ya kufundishwa zaidi,” alisema.

Said Swedi mchezaji chipukizi ndani ya timu hiyo ya Taifa ambaye hivi karibuni alipata balaa la kubebeshwa lawama baada ya kusababisha penati iliyowapa ushindi Sudan wa mabao 2-1 katika mchezo wa kuwania nafasi ya kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika,yeye alizungumzia zaidi matatizo ya ufundi.

Anasema Stars imekuwa ikicheza vizuri karibu kila mchezo na hii inaonyesha kuwa Tanzania ina wachezaji wenye vipaji. Anafafanua kuwa tatizo kubwa linaloikabili timu hii lipo katika umaliziaji ambalo pia suala hilo linachangiwa na makocha wetu kutokuwa na mbinu za kisasa katika kukabiliana na tatizo hilo.

“Kinachotakiwa hapa ni kuangalia kocha wa kigeni ili aweze kutoa mbinu mpya kwani hawa wa hapa wanafanana katika ujuzi. Kama hatutafanya hivi basi kasi ya kufungwa itakuwa pale pale,” anasema Said Swedi.

Kauli hiyo ya Swedi inapingana kidogo na ile ya Athuman Machuppa ambaye naye anasema tatizo halipo tu katika umaliziaji bali hata mabeki wa timu ya Taifa hawapo makini. Machupa anatumia mfano mchezo dhidi ya Taifa na Sudan ambapo Stars ndiyo iliyokuwa ya kwanza kupachika bao lakini likasawazishwa na kisha kuongezewa lile la ushindi.

“Suala lililopo ni moja tu hakuna umakini katika timu yetu licha ya kuwa Tanzania ina wachezaji mwengi wenye vipaji. Michezo mingi tunaingia tukiwa tayari tumefungwa,” anasema Machupa na kuongeza;

 

“Ninyi waandishi wa habari mnachangia sana katika kuunda timu ya Taifa na pia mnachangia tena katika kuibomoa. Mnaweza kutumia magazeti na redio zenu kuwatangaza wachezaji hata wasio na uwezo na kisha wakapata nafasi katika timu ya taifa.

“Hili mmekuwa mkilifanya na nadhani mfano mzuri ni huu wa timu iliyocheza Kombe la Castle ambayo ilitokana na waandishi wa habari kuiomba pasipo hata kuangalia viwango vya wachezaji katika kipindi husika. Tena inashangaza waandishi hawa hawa wanaiita timu ambayo hata wao wamechangia kuitengeneza kuwa ni kichwa cha mwendawazimu,” anasema Machupa.

Kutokana na kauli za wachezaji hawa ni wazi kuwa timu ya taifa inakabiliwa na matatizo ya kiufundi zaidi jambo ambalo linafahamika siku nyingi. Tena kuna kuathirika kisaikolojia kwa wachezaji wetu kunakotokana na hali iliyojijenga hapa nchini kabla ya mchezo wowote wa timu ya taifa.

Gazeti hili lilipata nafasi pia ya kuzungumza na kocha wa timu ya taifa na Simba,James Siang’a ambaye alifafanua kuwa Tanzania isitarajie kupanda chati katika soka kama hakutakuwa na mikakati ya kudumu ambayo hata sasa haipo.

“Huwezi kupata timu nzuri kwa kutegemea ligi tu lazima uwe na mikakati makini ya muda mrefu. Kwa hapa inapaswa kuanza na kikosi cha timu ya Vijana kama ambavyo imefanywa na nchi mbalimbali ambazo zimefanikiwa sasa,” anasema.

Siang’a alisema pia kuwa maendeleo ya soka yanayopatikana sasa Kenya yanatokana na mkakati wa miaka 10 uliowekwa miaka mitano iliyopita. Ndani ya mkakati huo timu ya Kenya imeanza kupata mafanikio na wanaamini kuwa itafanikiwa kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika na kisha kupata tikjeti ya kucheza Fainali za Kombe la dunia.

“Hapa Tanzania kuna pesa sana na hili si tatizo lakini hakuna mikakati ya kuwashirikisha wenye pesa hizo katika kuisaidia timu ya Taifa. Ni vigumu kwa kocha wa timu ya Taifa kufanya kazi yake kwa umakini kutokana na vizingiti vingi,” anasema.

Vizingiti anavyovizungumza Siang’a ni kama makocha kutoachiwa uhuru wa kuwa na programu zao ndani ya timu hiyo. Anasema pia kuwa siasa inachukua nafasi kubwa ndani ya timu ya taifa kuliko ilivyokuwa inahitajika.

“Huwezi kuamini kuwa ndani ya timu ya taifa kuna Usimba na Uyanga kutokana na hali hii ni vigumu sana kwa kocha kutenda haki katika usimamiaji wa timu hii.

“Uwiano wa wachezaji kwanza unaangalia Usimba na Uyanga na kisha unafuatia Ubara na Uzanzibar. hali hii ni ngumu sana kwa kocha wa kigeni kuikubali na mara nyingi imefanya makocha hao kutofanikiwa katika  kuifundisha timu ya Taifa,” anasema.

Maelezo haya ya Siang’a ambaye ni kocha mgeni toka Kenya yanatoa picha kuwa mzizi wa kuiboronga ndani ya Stars ni mgumu sana kuung’oa kutokana na matawi yake. Hali hii inaendana na kukua kwa fikra za kibinafsi kati ya Watanzania kwa siku za hivi karibuni.

Ubinafsishaji umewafanya Watanzania kuhisi hawana haki ya kumilki jambo lolote. Hata masuala ya Kitaifa nayo yamekuwa yakipuuzwa na wapo wanaofikiria kuibinafsisha hata timu hii wakidhani kuwa ubinafsishaji ndio nguzo muhimu katika maendeleo ya sasa.

Kwa mujibu wa Siang’a, wachezaji wa timu ya Taifa hawana tena ari ya kuchezea timu hiyo. Ni nusu ya timu inayocheza kwa kujituma na wengine hubakia kucheza bora mradi tu.

Siang’a anaielezea hali hii kuwa inawakwamisha hata makocha kumaliza programu zao. Tena nasema kwa makocha ambao hawakuiva katika taaluma hiyo huona mambo yote sawasawa ili mradi wanapata posho zao.

“Kuna makocha wengi hapa ambao wamefuzu na wana vyeti mbalimbali toka nje ya nchi lakini nao wanashindwa kuhamisha kile walichojifunza huko na kukipandikiza kwa wachezaji wao. Kuna ugumu katika kuhamisha taaluma toka katika Kiingereza kuja Kiswahili,” anasema Siang’a.

Kutokana na mahojiano haya inaonekana wazi kuwa timu ya Taifa inapaswa kuundiwa mkakati wake maalumu na utangazwe kuwa mkakati wa Kitaifa. Ndani ya mkakati huu serikali inatakiwa kuusimamia kwa dhati kama ambavyo Mataifa mengine yamekuwa yakifanya.

Tena mkakati huu huende hadi katika timu zetu ambazo nazo zinatakiwa kuwa na timu za vijana huku wakiwa na makocha wenye taaluma. Ikiwezekana makocha watoke nje ili kufuta hali ya kupendeleana ambayo inaonyeshwa na makocha wa hapa nchini.

Wananchi wanapaswa kuchangia katika kuunda mkakati huu na pia kufahamishwa majukumu yao tofauti na sasa ambapo kazi yao imekuwa kuandaa mawe ya kuwatupia wachezaji wa timu ya Taifa kila inapofungwa.

Tena elimu ya uzalendo inapaswa kuangaliwa upya kwani inaonekana kuwa haipo tena katika vichwa vya Watanzania. Ni elimu hii pekee ambayo itawafanya Watanzania kila walipo wafahamu majukumu yao kila wanapopata nafasi ya kuliwakilisha taifa.

Naamini pia kuwa viongozi wa vyama vya michezo nchini wanapaswa kutambua nafasi zao kuwa zinatakiwa kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi na sio kunenepesha matumbo yao. Hali hii isiishie kwa hao tu hata viongozi wa vilabu nao wazingatie maslahi ya wachezaji kuliko wao kubakia kunenepeana tu wakati wachezaji na familia zao wakilia njaa.

Nchi nyingi zinafanikiwa kutokana na kukimbia mfumo wa michezo ya ridhaa. Nakumbuka hata katika mchezo wa ndondi tumeweza kuwapata mabingwa wa Dunia akina Hassan na Rashid Matumla mara tu baada ya wao kuanza kucheza ngumi za kulipwa.

Tanzania inapaswa kupitisha mabadiliko ndani ya chama cha soka na kufanya mchezo huo kuwa wa kulipwa. Kwa kufanya hivi wachezaji watapata maslahi mazuri na itasaidia kuinua soka na kuibua vipaji vipya mathalani kipindi hiki ambapo kuna upungufu wa ajira za serikali.