Maskini unganeni kuondokana na umaskini(13)

Inatoka Toleo lililopita

Katika toleo lililopita, tulianza kutazama namna ya kutengeneza mpango wa kazi. Tuliishia katika kipengele kinachouliza kuwa JE, TUNAJUA NI KWA SABABU GANI MAMBO HUSIKA YANATOKEA? Hapa, tujiulize maswali haya: Nini sababu na chanzo chake. Kisha, endelea na swali lifuatalo na mengine yanayofuatia

Ni mambo gani ambayo yanaweza kuhusishwa na mambo ama hali husika?

Mifumo iliyopo inashughulikia vipi tatizo/ hali husika kutoka maisha watu wanayoishi ni hali zipi zipo na zinasukuma hayo kutokea. Pia tujiulize;

Ni taasisi zipi zinajihusisha na suala hilo? Ni sheria na taratibu zipi zinahusiana nalo?Ni thamani zipi ambazo watu wanazo juu ya suala husika? Je, wanao ushawishi wowote?

Kwa kifupi tunaweza kuzitaja hatua za kupanga mipango kama ifuatavyo;

i. Chagua mada ama suala maalum la kushughulikia

ii. Kusanya taarifa na takwimu ama data zinazohitajika

iii. Tafuta sababu za hali ama tatizo husika

iv. Elewa vizuri thamani zinazotawala na kuongoza watu katika hali ama tatizo hilo

v. Ni muundo gani inayohusika

vi. Ni mitandao gani inayoweza kusaidia

vii.Weka vipaumbele katika maamuzi yao

viii. Eleza hatua za kupata majibu (nani kwa kutumia nini lini na vipi)

ix. Anza utekelezaji

x. Fanya tathimini mara kwa mara katika mpango maalumu kwa mfano kila wiki ama kila mwezi.

2) Marekebisho yanayofanyika sasa Serikalini

Marekebisho hayo yataendelea kuongoza utendaji wa Serikali katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo.

Kwa upande wa mpango wa msamaha wa madeni, ni kwa miaka ishirini ijayo.

Kwa upande wetu wana-Tume ya Haki na Amani katika ngazi ya majimbo, hatua ya kwanza na ya muhimu ni kutafuta taarifa pamoja na mipango iliyopo katika Wilaya zetu. Baada ya kupata hayo hatua inayofuata ni kuzisoma na kuzitafakari ili kuzielewa kikamilifu.

Kisha uamuzi wa kuchukua kitu maalum na kukifanyia kazi ufanyike. Mfano suala la afya, elimu ama maji.

Hatua inayofuata baada ya kuelewa mipango ya Wilayani ni kutafuta kuelewa vizuri lengo mnalojiwekea na kutafuta mikakati itakayowawezesha kufikia lengo hilo.

Upatikanaji wa taarifa pengine siyo kitu rahisi lakini pia sio kitu kisichowezekana. Kilicho cha msingi ni lazima kujua nini unatafuta na ndipo utaelewa vizuri mahali pa kuweza kupata.

Mfano; Kama unatafuta taarifa zinazohusiana na elimu, afya au maji utazipata katika ofisi ya utawala Wilayani.

Takwimu hizo zimo katika taarifa ambazo ofisi hiyo huziandaa na kuzituma katika tawala za serikali ngazi za juu. Katika taarifa hizo unaweza pia kupata malengo na mikakati iliyowekwa na Serikali Kuu.

Kuhusu suala la ajira na mapato katika eneo lako, taarifa zake zinapatikana katika ripoti za tafiti maalum zilizokwishafanyika na sensa zinazofanywa mara kwa mara ndani ya vipindi maalum na Serikali.

Mfano hapa ni utafiti uliofanyika juu ya bajeti za familia na juu ya nguvu kazi.

Kama unatafuta taarifa toka ngazi ya chini lazima kwenda kwa msajili wa kijiji. Njia nyingine ni kuwauliza maswali watu katika kijiji au kata husika.

Hata hivyo Serikali ina mpango wa kuweka taarifa zake katika kompyuta ili kuwa na hifadhi moja ya taarifa za kijamii na kiuchumi. Kama hatua hii itafanikiwa itasaidia sana watu kupata takwimu na taarifa wanazohitaji.

Hapa tuchukue mifano miwili itakayotusaidia kuelewa

i) Wilayani kwako kuhusu elimu;

Ni asilimia ngapi ya watoto wanaoingia shule ya msingi. Watoto wangapi wanaacha shule kabla ya kumaliza. Ni wangapi wanaofaulu mtihani wa darasa la saba

Ni asilimia ngapi ya shule ambazo.wanafunzi wake hufaulu kwenda sekondari.

ii) Wilayani kwako kuhusu afya;

Nini kiwango cha vifo vya watoto

Nini kiwango cha vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Nini kiwango cha vifo vya kina mama wajawazito

Ni wananchi wangapi wanapata maji safi na salama

Baada ya kupata taarifa hizo, anza kupanga mpango wa utekelezaji kwa kuzingatia haya;

Ni kitu gani maalum mnaamua kufanya.

Ni kwa vipi mtaweza kukamilisha utekelezaji wake ; nani atafanya nini.

Tafuta wengine mnaoweza kushirikiana nao

Hakikisha unajenga mtandao na wale wanaoweza kukusaidia. Mfano-. Wataalam na watumishi wa serikali, Halmashauri walei na vyama vya kitume (WAWATA, VIWAWA, CPT, CARITAS).

Pia, fanya jitihada kuwasiliana na viongozi wa kisiasa- wabunge, madiwani, wakuu wa mikoa na wilaya n.k. Vile vile shirikiana na watu wanaoshughulika na vyombo vya habari.

Baada ya hapo, unda kikundi maalum (task force) kwa kila suala mnalotaka kulishughulikia. Kitu cha muhimu ambacho inafaa kutosahau ama kudharau ni kuwashirikisha wanakijiji na jamii husika.

Inafaa kujadiliana nao waweze kuelewa namna watakavyosaidia na kuwajibika katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo fulani, kutetea haki zao ama kujipatia huduma bora zaidi.

3) Mfano Halisi

Elimu

Kama mnaona kuwa kiwango cha elimu katika shule zenu za msingi ni cha chini na mngependa kuboresha, anza kwa kutafuta taarifa zifuatazo;

Hatua ya kwanza

Tafuta mipango ya Wilaya juu ya elimu katika Wilaya nzima na pia mipango ya wilaya juu ya shule zilizomo katika eneo la parokia yenu.

Itaendelea toleo lijalo

haki za raia Kitabu cha Tatu

Sheria ya ardhi Tanzania (16)

Wajumbe wa Baraza la Ardhi ya Kijiji watamchagua mjumbe mmoja wao kuwa kiongozi wao ambaye ndiye -atakayetunza kumbukumbu za vikao. Kikao kitakuwa rasmi iwapo watafika wajumbe wanne na kati yao wawili lazima wawe wanawake. Katika kupigia kura jambo lotote kiongozi wa baraza atakuwa na ‘kura turufu pale ambapo itatokea kura zimelingana.

Jukumu kuu la Baraza la Ardhi la kijiji ni kupatanisha pande zinazofarakana ili kufikia rnuafaka. Katika kusuluhisha baraza litazingatia taratibu zote za kimila za usuluhishi, haki za msingi za binadamu ikiwa ni pamoja na kuwapatia fursa ya kusikilizwa pande zote mbili. Pili taratibu nyingine zozote za kimila ambazo wajumbe watakuwa wameelimishwa.

Mjumbe yeyote wa baraza hataweza kuwa msuluhishi wa mgogoro ambao yeye mwenyewe au mtu wa familia yake anahusika nao. Kama itatokea hivyo itamlazimu mjumbe kutohudhuria kikao cha baraza kwa usuluhishi anaohusika nao.

Sheria inabainisha kwamba sio lazima kwa mtu au taasisi yeyote kutumia huduma ya baraza la ardhi ya kijiji ikiwa ataona kuna njia nyingine ya ufumbuzi.

Yawezekana wahusika katika mgogoro hawakuridhika na uamuzi wa baraza, hivyo wanaweza kupeleka suala lao katika mahakama yenye mamlaka hayo, kama ilivyoelezwa hapo juu.

Wakati mwingine migogoro huanza kutokea katika hatua za awali kabla ya hatua ya kupata haki-miliki. Kwa kuona uzito wa matatizo ya aina hii na kuona umuhimu wa kuyashughulikia sheria pia imeweka vyombo vya kushughulikia na taratibu za kufuata katika utatuzi wa migogoro ya aina hiyo. Kwa kutambua kuwa wamilikaji wa ardhi na wengine wote waliotegemea kupata manufaa fulani kutoka kwenye haki miliki ya ardhi husika wanaweza wakaathiriwa au/na wanapoathiriwa na vitendo, ilani, amri au matangazo yalitolewa na Serikali ya kijiji au kamishna wa ardhi na watendaji walio chini yao, sheria inawapa fursa kupeleka mashauri yao mbele ya mahakama.

Yawezekana, rnwombaji wa haki miliki akakataliwa kupewa haki miliki kwa hati hiyo anaweza kukata rufaa katika Halmashauri ya Wilaya iliyomo katika eneo hilo na kama bado hataridhika na maamuzi ya Halmashauri ya Wilaya husika anaweza kupeleka suala lake kwa kamishna na zaidi ya hapo anaweza kulifikisha shauri hilo Mahakama Kuu.

Wakati wa kuainisha haki miliki na haki nyingine zilizopo katika ardhi, sheria imeeleza nani watakao husika. Halmashauri ya kijiji na ya Wilaya ndizo zitakazohusika. Kwa hiyo basi malalamiko yote yatakayohusika na uainishaji huo yatashughulikiwa na Halmashauri ya Wilaya endapo watalamikaji watafikia idadi ya watu ishirini na zaidi.

Wakati wa kuainisha miliki wahusika wote washirikishwe ikiwa ni pamoja na kueleza madai na haki zao pamoja na mipaka ya maeneo yao. Endapo rntu yeyote hataridhika na uainishaji huo ana haki ya kukata rufaa katika Baraza la Ardhi la Kijiji ndani ya siku thelathini. Baraza la Ardhi la Kijiji limepewa madaraka mbali mbali hivyo linaweza kumwagiza mjumbe mshauri wa kamati ya uanishaji kushughulikia jambo fulani.

Kiutendaji kutakuwa na kamati hiyo ya uanishaji ambayo itaidhinishwa na mkutano mkuu na kuundwa na Halmashauri ya Kijiji ambapo wajumbe wake watachaguliwa na mkutano mkuu wa kijiji. Kamati ya uainishaji itaundwa na wajumbe tisa na wanne kati yao lazima wawe wanawake. Kamati hiyo itafanya kazi kwa muda wa miaka mitatu na wajumbe hao wanaweza kuchaguliwa tena kwa kazi hiyo.

Maelezo ya hapo juu ni ya utendaji hivyo kama mhusika hataridhika ama ataathirika itambidi atumie mkondo wa sheria kwa kufuata taratibu na ngazi za mahakama kwa kadri ilivyoelekezwa katika maelezo yaliyotangulia.

Kwenye maeneo ambamo kuna matumizi mseto ya ardhi kwa mfano wafugaji na wakulima, mshauri wa kamati ya uainishaji kwa kushirikiana na wahusika wataweka mpango mzuri wa matumizi ya ardhi husika kama vile wafugaji watafuga kwa kutumia eneo lipi hapo kijijini.

Wakati uainishaji unaendelea kushughulikiwa sheria inaeleza kuwa hakuna mtu yeyote atakayepeleka malalamiko yake mahakamani. Mpango wa uainishaji utakapokamilika endapo yeyote hataridhika anaweza kupelekea malalamiko yake mahakamani au katika Baraza la Ardhi la Kijiji na asiporidhika anaweza kukata rufaa kwa vyombo vya juu kama ilivyokwishaelezwa hapo juu.

Maswali

1. Kwa nini kuna migogoro mingi ya ardhi?

Je mwananchi wa kawaida anao uwezo wa kugharamia shauri linalohusu mgogoto wa ardhi mahakamani hasa kwa kutumia wakili?

Maelezo mengine muhimu

Katika sehemu hii kwa ujumla sheria zinazungumzia mambo ambayo kwa namna moja ama nyingine hayakuainishwa kinagaubaga katika Sheria yenyewe.

 

12.1. Usambazwaji wa Matangazo na Taarifa.

Kamishna anapoona kwamba tangazo haliwezi kufikia walengwa kibinafsi ana kwa ana au kwa njia ya posta anaweza kuweka nakata ya tangazo mahati ambapo,watu wataweza kuliona. Kwa hiyo basi endapo inabidi tangazo hilo liwafikie watu ambao wataathirika nalo basi taratibu zifuatazo zitafuatwa;

a) Kama ardhi husika ni ya kijiji nakala ya tangazo

i) Iwekwe mahali ambapo watu wa eneo hilo wataliona na hata wale wa eneo la jirani

ii) Iwekwe mahali pa wazi ambapo watu wataliona katika ofisi ya kijiji na katika sehemu nyingine za umma (public places) kulingana na maagizo ya serikali ya kijiji.

b) Kama ardhi ni ya Jumla" tangazo liwekwe katika ofisi za mamlaka zenye uwezo kimahakama zilizomo katika eneo ardhi husika ilipo. Pia Tangazo liwekwe katika sehemu za wazi za mikusanyiko zilizomo katika eneo ardhi husika ilipo.

c) Njia nyingine ambazo zinaweza kuonekana zinafaa ni kuweka matangazo hayo katika gazeti moja ama zaidi kati ya magazeti yanayosambazwa nchi nzima.

Ijue vema Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa

Na Pd. David Mubirigi, Seminari ya Segerea

Bila kuingilia maswali ya Kihistoria, Kiliturjia na Kiteojia, mababa wa Mtaguso wa 11 wa Vatikani mwaka wa 1963 walipendekeza marekebisho, uimarishaji wa nidhamu na adhimisho la sakramenti hii.

Kwa ufupi, Mababa wa Mtaguso wanasema kuwa Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa siyo sakramenti kwa ajili ya wale wanaokufa. Muumini yeyote katika hatari ya kifo kwa sababu ya ugonjwa au uzee apewe sakramenti hii upesi iwezekanavyo(SC, 73-75).

Ni sakramenti iliyowekwa na Bwana Yesu ambayo kwayo kwa njia ya mpako wa mafuta matakatifu na sala ya padre, afya ya roho na hata ya mwili, iwapo ni kwa manufaa ya roho, inarudishiwa muumini aliye mgonjwa sana.

Mtaguso wa Trenti ulisema kuwa yeyote atakayesema kwamba Mpako wa Wagonjwa siyo sakramenti iliyowekwa na Bwana Yesu atengwe (Dz-Sch., 1716). Bwana Yesu aliweka sakrementi hii alipowatuma mitume wake kwenda kuhubiri na kuwaponyesha watu.

Tunasoma "Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza", (Mk. 6.12-13). Ilitangazwa rasmi na Mtume Yakobo kwa maneno yafuatayo: "Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa, (Yak. 5.14-15).

Mafuta yanayotumika ni ya mzeituni au ya mimea mingine kama vile Karanga au nazi. Lazima yabarikiwe na Askofu au na yule mwenye mamlaka sawa na Askofu wa Jimbo kisheria au wakati wa shida maalumu yanaweza kubarikiwa na padre yeyote wakati wa adhimisho la sakramenti. (Kan.999).

Mpako ufanyike penye paji la uso na mikononi kwa uangalifu. Maneno yatumike na utaratibu ufuatwe kadiri ya miongozo ya vitabu vya Liturjia. Wakati wa shida maalumu mpako mmoja penye paji la uso au kwa sehemu yoyote ya mwiti unatosha bila kupunguza maneno au utaratibu wa kiliturjia. Shida maalumu ni pamoja na hatari ya kifo ambapo Komunyopamba inatolewa mara moja baada ya mpako mmoja. Aidha, mpako mmoja unakubalika pale ambapo kuna kizuizi katika kupaka mikono. Aidha, unakubalika pia pale ambapo idadi ya wapakwa ni kubwa sana na muda wa adhimisho la Sakrarnenti ni mfupi muno. Hali kadhalika Sheria inaruhusu mpako mmoja kwa sehemu yoyote ya mwili iwapo mpako mmoja penye paji la uso hauwezekani na hasa wakati wa ajaii ambapo kichwa hakifikiki. Mwisho, hati yenyewe ya mgonjwa inaweza kuruhusu mpako mmoja tu.

Sababu kubwa sana inamruhusu mhudumu wa sakramenti hii kutumia chombo cha kupakia mafuta matakatifu badata ya mikono ili kuepukana na mgusano wa moja kwa moja na mgonjwa. Sababu kubwa ni kama vile kuepukana na hatari ya maambukizo au kinyaa.

Kwa kawaida, hata wauguzi hospitalini uchukua tahadhari kama hizo. Vyombo vya kutumia ni kama vile glavu au kimti kilichofungiwa pamba (Abbot - Hannan, 11, 69).

Sakramenti hii inazo faida nyingi kwa mgonjwa. Kwanza, inaleta neema (Dz-Sch., 1717).

Kwa kuwa sakramenti hii inahesabiwa kati ya sakramenti za wazima, mpokeaji anapaswa kuwa katika haii ya kutokuwa na dhambi ya mauti. lwapo mpokeaji hajui kuwa ana dhambi ya mauti, akapokea sakramenti hii baada ya kufanya majuto, atapokea neema.

lwapo mgonjwa ana dhambi za mauti na hawezi kufanya kitubio, upokeaji wa Sakramenti ya Wagonjwa utamwondolea dhambi za mauti ikiwa amefanya majuto kwa ajili ya dhambi zake (Dz-Sch.,1669). Fundisho hilo linaungwa mkono na Mtume Yakobo anayesema kuwa sala ya imani itamwokoa mgonjwa na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa (Yak. 5.14-15).

Faida ya kwanza na halisi ni kwamba sakramenti hii inaleta tiba ya kiroho iii mgonjwa haweze kupata nguvu ya kuvumilia mateso au maumivu na kushinda maovu. Kitulizo na nguvu ya neema ya Sakramenti ya Wagonjwa vinaleta tiba ya Kiroho. Aidha, udhaifu wa kiroho wa mgonjwa ulioletwa na dhambi ya asili au na dhambi binafsi au na hali ya ugonjwa unaponyeshwa na sakramenti.

Mtaguso wa 11 wa Vatikani unasema kuwa kwa njia ya mpako mtakatifu na sala ya padre Kanisa zima linaweka wagonjwa mikononi mwa Bwana, mteswa na mtukuka, likiomba kuwa apunguze mateso yao na kuokoa (LG, II).

Pia, mtu aliye mgonjwa sana anahita i msaada wa pekee wa neema ya Mungu katika muda huo wa wasiwasi asije akakata tamaa na kuingia vishawishini na kudhoofisha imani.

Kwa hiyo, sakramenti hii inatoa neema ili kuweza kushinda: wasiwasi, huzuni, kukata tamaa na kudhoofisha imani kwa kuamsha ndani yake matumaini katika huruma ya Mungu.

Kuhusu mpokeaji, ni muumini yeyote, aliyekwishafikia umri wa mang’amuzi, anapoanza kuwa katika hatari ya kifo kwa sababu ya ugonjwa au uzee (Kan. 1004 Kif. 1). Kwa maneno mengine, hatari ya kifo ndio wakati muafaka wa kupokea Sakramenti ya mpako wa Wagonjwa (Kan.1001). lwapo kuna mashaka kuhusu hali ya ugonjwa au umri wa mpokeaji, sakramenti itolewe bila kusita au kukawia (Kan. 1005). Twapo kuna mashaka kama kweli mtu anaishi au amekufa, sakramenti itolewe bila kusita au kukawia kwa masharti (Kan. 1005).

Waumini waelimishwe kuhusu umuhimu wa sakramenti hii. Wawe tayari kuiomba wenyewe wakati hali zao kiafya zinapokuwa mbaya.

Aidha, wawe tayari kuipokea kwa imani na kwa moyo wa ibada. Uahirishaji wa upokeaji wa sakramenti unapoteza au kupunguza faida zake za kiroho kwa mgonjwa.

Kwa hiyo, hata wahudumu wa wagonjwa waelimishwe kuhusu wajibu wo wa kumwita padre kwa ajili ya wagonjwa wao.

Adhimisho la Sakramenti linaweza kurudiwa iwapo haii ya mgonjwa imekuwa mbaya zaidi au amepona na kuugua tena hata kama ni ugonjwa ule ule.

Aidha, linaweza kurudiwa iwapo mgonjwa amepatwa na ugonjwa mwingine.

Ijue Pasaka, undani na matukio yake(2)

KANISA linapoelekea kusherehekea kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo Machi 31, mwaka huu, tutaendelea kuwaletea mfululizo wa chapisho hili kwa msaada wa Kitabu cha ZIJUE BARABARA SIKUU ZA NOEL na PASAKA KILICHOANDIKWA NA PD. TITUS AMIGU.

Lengo la chapisho hili ni kuondoa mashaka ya waamini wengi ambao wanataka kujua undani wa PASAKA ambao huuliza maswali mbalimbali.

KATIKA Toleo lililopita, tuliishia katika kipengele cha vii cha mfululizo wa mambo yaliyofanyika katika Siku ya Pasaka; Endelea na sehemu ya viii.

viii. Baada ya hapo, ziliimbwa Zaburi zingine za Halleluya, yaani tangu Zab 115 hadi 118.

ix. Hatimaye, karamu ilifungwa kwa kukinywea kikombe cha nne cha divai. Endapo kulikuwa na kitu kilichobaki, yaani chakula au nyama, vyote viliteketezwa kwa moto kusudi watu wasichafue sherehe za Pasaka kwa labda kuiacha nyama iharibike, ama kwa wengine kutaka kujiwekea ukumbusho.

Yesu alikula karamu yake ya mwisho pamoja na wafuasi wake kumi na wawili: Simoni aliyempa jina la Petro, Yakobo wa Zabedayo na Yohane nduguye Yakobo aliowapa jina la Boanerge, yaani wana wa ngurumo, Andrea, Filipo, Yakobo wa Alfayo, Bartholomayo, Mathayo, Thomaso, Yuda Thadayo, Simoni Mkananayo na Yuda Iskariote ambaye angelikuwa rnsaliti wake.

e) Upekee wa karamu ya mwisho ya Yesu

Wainjili wote wanne, hawatupi kinaganaga cha mwendo wa ulaji wa karamu yenyewe.

Lakini mambo yanavyosomeka, yaonekana mlo ulifuata hatua zile za kawaida kwa karamu ya Pasaka ya kiyahudi.

Labda hapakuwepo mwanakondoo.

Hata hivyo, hata kama karamu ya mwisho ya Yesu, hata kama ilifanana na karamu ya Pasaka ya Wayahudi wengi, bado ilipata utofauti katika kuwa na mambo matatu ya pekee sana.

Hayo tunayapata kutokana na maneno Yesu aliyosemea mkate na kikombe cha divai. Kifupi, siku ile aliweka mambo matatu mapya: mosi, wosia wa maneno yaani Amri ya Mapendo (Amri Kuu), pili, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na tatu, Sakramenti ya Daraja Takatifu, yaani Daraja ya Upadre.

Kama tulivyokwisha kusema, kati ya wanafunzi, Yesu anachukua nafasi ya Baba, napo akafanya mambo ya ajabu matatu.

Kwanza, kama Baba anayekaribia kufa aliwaachia wosia wa maneno, wapendane. Halafu anawaachia chakula, Ekaristi Takatifu, ili wasije wakafa. Na mwisho, aliwaachia viongozi, yaani watu wa kuwaangalia watoto wake wakati atakapokuwa amekufa.

Wosia wa maneno aliusema kwa mfano wa tendo.

Aliwaosha miguu wanafunzi wake. Wakati ule, watumwa walipaswa kuvua viatu vya bwana wao na kuiosha miguu yake.

Ilikuwa haiwezekani Bwana kuiosha miguu ya watumwa au mwalimu miguu ya wanafunzi wake. Kumbe, Yesu aliwaosha wanafunzi wake miguu kwa kusudi la kuwaachia mfano wa kupendana utakaodumu milele.

Hii haikuwa kuweka taratibu ya kutawadha, isipokuwa kuacha mfano kwamba, ilitupasa wanadamu kusaidiana na kuokoana sisi kwa sisi kutoka kwenye matatizo yetu machafu.

Zaidi ya hayo, alichofanya Yesu kilikuwa vile vile ni alama ya kifo, yaani kwamba binadamu tunapaswa kufa.

Juu ya chakula alichoacha Yesu ni Ekaristi Takatifu ambayo ni MWILI na DAMU yake mwenyewe. Mkate na divai vilipata kuwa MWILI na DAMU ya Yesu Kristo kwa nguvu ya maneno yake katika ushirikiano wake na Roho Mtakatifu, Nafsi ya Tatu ya Mungu.

Ndipo tangu siku hiyo ya Alhamisi, Ekaristi Takatifu ni katika maumbo ya mkate na divai, vitu ambavyo vilikuwa ni vyakula vya kawaida kwa Wayahudi wakati ule.

Nia ya Yesu katika kuvifanya vyakula hivyo vya kawaida viliwe na Wakristo, ilikuwa ni kwamba Ekaristi Takatifu iwe pia chakula cha kila siku kwa Wakristo wote.

Hapo awali, Yesu alipozungumzia juu ya chakula hiki, watu hawakumwelewa na wengine walikwazika, wakamwacha.

Lakini hata baada ya kuanzishwa chakula hicho, mambo na maonyo kwa walaji hayajakoma, kwani Paulo anaonya kwamba, kwa yeyote kula chakula cha Bwana katika hali mbaya, ni kama kula sumu ya roho.

Juu ya viongozi wanaowekwa ili familia yake isiyumbeyumbe baada ya kifo chake ni kwamba, Yesu aliweka Sakramenti ya Daraja Takatifu.

Kwa sakramenti hiyo, Yesu alikusudia wapatikane mashemasi, mapadre na maaskofu.

Hao ndio walezi wa ndugu zao katika Kanisa. Kwa Daraja la Upadre, padre hupewa uwezo wa kuwatengenezea ndugu zake chakula, yaani Ekaristi Takatifu.

Hao hufanya hivyo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wakati wa mageuzo katika misa, yaani pale wanapomwita Roho Mtakatifu avibariki vipaji vya mkate na divai, avitakase na kuvigeuza kuwa MWILI na DAMU ya Yesu Kristo, kama alivyojitoa mwenyewe kwenye Karamu ya Mwisho na kuhitimisha sadaka yake kwa kumimina damu msalabani pale mlimani Golgota.

Kwa maneno haya jukumu la mapadre ni nyeti na wala utukufu wake hauna kifani na kazi yoyote ambayo wanadamu waweza kuifanya duniani hapa.

Ni hadhi mahsusi na takatifu na kwa jinsi hiyo, kwa haki kabisa wanadaiwa waishi kitakatifu kila siku wao wenyewe.

Kutokana na jukumu lao la kuwatunza ndugu zao, ndipo katika kifo watu hao wenye Daraja Takatifu, wataulizwa wamefanya nini katika kulitunza Kanisa la Mungu.

Siku ya kiama, watu hawa wataulizwa juu ya kazi zao za kulijenga au za kulibomoa Kanisa. Kulibomoa Kanisa, kutakuwa ni balaa yao na balaa hiyo itawasababishia hukumu ya Mungu.

Lakini kinyume chake, kitendo chochote cha kulijenga Kanisa, kitakuwa ni sifa njema kwao na hakika hawatakosa zawadi yao halali, kutoka kwa Mungu mtuza watu wema.

f) Mengineyo

Karamu ya mwisho, inafanyiwa kumbukumbu kila siku na mahali pote duniani. Ndiyo Misa Takatifu zinazosomwa na mapadre popote duniani.

Katika Misa, mateso na sadaka ya Kristo vinakumbukwa na kutendwa upya, kwa faida ya neema zake nyingi na baraka zake kwa wakati huu wa sasa, na enzi ya leo ya mahali pale Misa inaposomwa.

Hivi basi, Misa siyo madhehebu ya mzaha, bali ni madhehebu yanayounganisha mbingu na nchi, watakatifu na wanadamu.

2. Ijumaa Kuu

Baada ya kula karamu ya mwisho, Yesu aliondoka mjini Yerusatemu, akavuka bonde Kidroni akaenda mpaka mlima wa mizeituni, kwenye bustani ya Gethsemane. Hapo alikuwa anakuja mara nyingi kulala.

Kwa nini, alikuwa analala nje kama hapo? Kulala popote ilikuwa kawaida ya marabi na wanafunzi wao, kwa kweli mara nyingi, walikuwa hawana vitanda na waliona vitanda haviwajengei mazingira ya kujinyima, mazingira yalitakiwa yajengwe wakati wa kujifunza mambo ya Mungu.

Ndiyo maana Yesu alisema, hakuwa na mahali pa kulaza kichwa chake (rej. Mt 8:20, Lk 9:58). Yuda alipajua pale Gethsemane, hivyo alikwenda kuwataarifu makuhani na mafarisayo waende wakamkamate Yesu.

Alifuatana na kikosi cha askari waliopewa jukumu la kumkamata Yesu, hadi pale bustani. Naye akamwonesha Yesu kwao kwa busu. Mmoja wa wanafunzi wake, Simoni Petro, alimkata sikio mmoja wa wale waliokuja kumkamata Yesu, kama moja ya juhudi zake za kutaka Yesu asikamatwe.

Lakini Yesu, kwa vile alivyokubali kuteswa kwa ajili ya wanadamu, alimkataza Simoni Petro asitumie upanga pale, bali aweke upanga wake alani.

Kifupi, alimwonesha Petro kwamba, hakuwa na haja ya kutetewa katika mpango ule mtakatifu wa ukombozi wa watu wote.

Baada ya hapo, Yesu alipelekwa kwenye vyombo vyenye mamlaka. Kwanza, alipelekwa mbele ya Baraza la Kiyahudi, ndani Sanhedrini, Hicho kilikuwa chombo chenye madaraka ya juu ya kidini nchini mle.

Baada ya hapo, walimpeleka kwa Gavana wa kirumi, Pontio Pilato, ambaye baadaye alimpeleka kwa mkuu wa mkoa wa Galilaya, yaani Herode Antipas, kwa vile Yesu alikuwa mwenyeji wa Nazareti katika Galilaya.

a) Yesu alihukumiwa kifo kwa makosa gani?

Kuhusiana na hukumu, Yesu alihukumiwa kwanza na wakubwa wa Wayahudi.

Kadiri ya sheria zao za kiyahudi, Yesu alionekana na hatia ya kuidhihaki nyumba ya Mungu, ndiko kudai kwamba angeliweza kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu. Kumbe, Yesu alikuwa anazungumzia mwili wake mwenyewe.

Kosa lingine, kwa kadiri ya sheria ya kiyahudi lilikuwa ni kujiita Masiha, wakati alikuwa halingani na Masiha waliyemtaka na kumsubiri wao, yaani masiha mkombozi wa kisiasa.

Na halafu kwa kadiri yao, Yesu alikufuru kwa kujiita Mwana wa Mungu. Haya ndiyo makosa yaliyomfanya Kuhani Mkuu achane nguo yake kwa hasira.

Kumbe, makosa hayo yote, hayakuwa makosa ya msingi kwa kadiri ya sheria ya kirumi. Wakati kwa sheria ya kiyahudi, Yesu alipaswa auawe, katika sheria ya kirumi, hakuwa na hatia yoyote ya kumpasa kufa.

Wayahudi hawakuwa na uwezo wa kumuua mtu yeyote, kwa vile sasa walikuwa wakitawaliwa na sheria mpya.

Na kama tulivyosema, kwa kadiri ya sheria ya kirurni, Yesu hakuwa na hatia ya kuuawa.

Hivi Yesu ilipaswa aachiliwe huru. Ndipo basi, viongozi wa kiyahudi kusudi wasishindwe jambo, na ili waichemshe hasira ya Pilato dhidi ya Yesu, wanamsingizia Yesu makosa ya kisiasa ambayo kwayo, kwa sheria ya kirumi angelipaswa auawe.

Wanamwambia kwa msisitizo Pilato, mkubwa wa kirumi, kwamba eii Yesu amejiita mfalme wa Wayahudi, wakati Wayahudi wanatawaliwa na mfalme mmoja tu Kaisari, na tena kwamba eti Yesu amewakataza watu kulipa kodi, wakati walikuwa wanapaswa kumlipa kodi Kaisari kila mwaka na halafu kwamba, Yesu alihusika kuwachochea watu wafanye mgomo.

Makosa haya ya kusingiziwa yalikuwa mazito sana, lakini Wayahudi wenyewe hawakuwa na ushuhuda wa kutosha kuyathibitisha. Ndipo Pilato anapowaambia tena kwamba, Yesu hana hatia.

Bahati mbaya, Pilato alikuwa dhaifu katika kuishikilia kweli. Anawapa Wayahudi Yesu wapate kumtenda watakavyo wao.

Ndipo anaposulibiwa. Huu kweli ulikuwa ni uonevu mkubwa, mtu ambaye sheria imeshindwa kumtia hatiani, anahukumiwa kama mkosefu.

b) Kesi ya Yesu iliendeshwa namna gani?

Kesi ya Yesu iliendeshwa kimchakamchaka katika saa za usiku. Kuendeshwa kwake, kulivunja kanuni nyingi zilizokubaliwa kwa ajili ya kumfanyia haki mshtakiwa.

Kwa nini walimfanyia hivyo Yesu?

Walimfanyia hivyo, kwa sababu wakuu wa Wayahudi walikuwa na nia na jazba ya kumuua na kumwondoa kati yao Yesu, waliyemhesabu adui yao mkubwa, waliyemchukia na kumwogopa sana.

Walitaka hilo litendeke haraka kabla ya sikukuu yao ya Pasaka, ama Sabato yao iliyokuwa ikikaribia.

Basi, usiku ule ule, walimhoji wenyewe kwenye Baraza lao Kuu, na kishapo wakaenda kumwomba Pontio Pilato aidhinishe kuuawa kwa Yesu, kwa kumbadilishia na kumbambikizia mashtaka ya kisiasa, kama tulivyokwisha kusema.

Itaendelea toleo lijalo

c) Mahakama gani ilimhukumu Yesu?

Mahakama iliyomhukumu Yesu ilikuwa ya wakoloni, yaani Warumi ambao walikuwa wanawatawala Wayahudi, kwa njia ya Gavana wake aliyewekwa mjini Kaesaria Maritima. Wakati ule wa Yesu, Gavana wa kirumi alikuwa ndiye Pontio Pilato.

Lakini, ijapokuwa tunasema Pilato kama Gavana wa kirumi, ndiye aliyesema kwa amri ya mwisho achukuliwe Yesu na wakamtendee watakavyo, kwa kweli alishinikizwa na Wayahudi na wakuu wao, maana hao walihakikisha Yesu anauawa hata kwa kumtisha Pilato.

Na kweli, Pilato alitishiwa kushtakiwa kwa Kaisari, yaani Mfalme Mkuu wa Dola ya Kirumi kwa kumwachilia mtu kama Yesu, anayejiita mwenyewe mfalme, wakati mfalme ni mmoja tu, Kaisari.

Matisho kama haya, pamoja na kelele za "Msulibishe, Msulibishe", yalimshinikiza Pilato aamue Yesu achukuliwe na akatendewe kwa kadiri Mayahudi walivyotaka. Mashtaka ya mwisho, Pontio Pilato aliandika kibaoni kuwa, ni kujiita Mfalme wa Mayahudi.

Walipomburura msulibiwa kuelekea mahali atakakosulibiwa, mvulana mdogo alipewa kibao cha mashtaka na kutangulia nacho mbele ya waandamanaji, kusudi kama kuna mtu haungi mkono mashtaka yale, ayasimamishe maandamano na kuwarudisha wote mahakamani kwa ajili ya kuisikihza kesi upya.

Kwa mashtaka ya Yesu, wapo waliotaka kupinga mashtaka yale kwa kufanyiwa marekebisho kidogo, lakini siyo kuyafuta kabisa mashtaka yale. Wahtaka Pilato aandike kwamba, Yesu mwenyewe alisema kwamba yeye ni Mfahne wa Wayahudi. Pilato alikatad kufanya mabadiliko hayo, rnaana alishapotoshwa kabla hajaandika kibao kile (Yn 19:22).

d) Mateso gani alifanyiwa mfu aliyesulibiwa?

Kabla hatujaendelea mbele, tuseme kwanza neno moja. Yaani, tuseme kwamba kwa kadiri ya sheria ya kirumi na ile ya kiyahudi, mtu wa kuuawa ilibidi akauawe mara baada ya hukumu kutolewa. I-Iii ndiyo sababu Yesu alitolewa haraka haraka, kwenda kusulibiwa. Wakati ule, waliohukumiwa kuuawa hawakupata muda tena wa kiisubiri kifo, kama inavyotokea katika sheria za leo.

Ingawa kesi iliendeshwa ndani na daima kwenye makao makuu ya mtawala (rej. Mt 27:27), kusulibiwa kwenyewe kulifanyika nje ya mji, kwenye sehemu ya makutano ya njia, kusudi watu wengi kwa kadiri ilivyowezekana, wamwone aliyesulibiwa na wapate kutishika kwa tukio lile. Basi, ndivyo itivyofanyika katika kumsulibisha Yesu kilimani Golgota. Wayahudi wenyewe walipompa mtu adhabu ya kifo, walimuua kwa kumpiga mawe watu wengi kwa pamoja. Kishapoll ndipo walipomtundika mtini.

Kitabu cha Kiada kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo (36)

Kulinda na Kuboresha Haki za Binadamu Katika Nchi

Ulinzi na uboreshaji wa haki za binadamu katika nchi hufanyika kwa njia mbili. Kwanza kupitia Katiba, na pili kupitia sheria mbalimbali za nchi ikiwa ni pamoja na sheria ndogo ndogo.

Nchi mbalimbali zimefanya bidii kuhakikisha kwamba haki mbalimbali zilizopo ndani ya mikataba ya kimataifa vile vile zimewekwa ndani ya Katiba ambayo ni sheria mama na pia katika sheria nyingine za nchi.

Haki hizi muhimu ambazo huenda pamoja na wajibu huwekwa katika sehemu maalum ya Katiba ambayo hupewa ulinzi wa aina ya pekee.

Sehemu hii ya Katiba inajulikana kwa lugha ya Kiingereza kama Bill of Right.

Imepewa ulinzi mahsusi ili isiweze kubadilishwa ovyo ovyo na bunge (entrenchment). Hivyo, inahitajika idadi maalum ya wabunge na kupiga kura kubadilisha sehemu hii ya Katiba.

Itaendelea toleo lijalo