Make your own free website on Tripod.com

Wajue maaskofu na majimbo ya AMECEA

WAKATI Tanzania ikijiandaa kuupokea ugeni mkubwa kutoka nchi nane zinazounda Umoja wa Ushirikiano wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Nchi za Mashariki mwa Afrika (AMECEA), gazeti hili katika kumfanya kila msomaji wake afahamu kwa undani juu ya umoja huu, litakuwa likitoa habari za kila jimbo kwa nchi zote nane zinazounda AMECEA. Katika toleo hili, Mwandishi Wetu Maalumu, Pd. Raphael Kilumanga, anaendelea na majimbo ya Songea, Sumbawanga, Tabora na Tanga.

Jimbo Kuu la Songea linaongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu Nobert W. Mtega. Linao wakazi wapatao 594, 992 ambapo 238, 910 ni Wakristo Wakatoliki. Jimbo linahudumiwa na mapadre wazalendo 62.

Mbali na mapadre wa jimbo, wapo Mapadre Wabenediktini wa St. Ottilien kutoka Bavaria, Ujerumani, Mapadre Wabenediktini wa Hanga, Mapadre Waagustiniani, Mapadre Wavincentiani na Mapadre Wafransiskani Wakapuchini.

Mabradha ni pamoja na Mabradha Wabenediktini wa St. Ottilien wa Bavaria, Ujerumani, Mabradha Wabenediktini wa Mt. Paulo Lighano (Shirika la Jimbo) Mabradha Wabenediktini wa Hanga na Mabradha Waagustiniani.

Mashirika ya Masista ni pamoja na Masista Wabenediktini wa Mt. Agnes Chipole, Masista Wabenediktini wa Tutzing, Masista Waagustiniani, Masista wa Huruma wa Mt. Vincent wa Paulo, Masista Waklara Fukara Wakoletini na Masista wa Maamkio (Visitation Sisters).

Pia yupo msaidizi wa Utume (auxiliary of the apostolate), mmoja asiye mzalendo na wasaidizi wa utume 16 wazalendo, Walei Wamisionari na

Wakatekista 191.

Jimbo linazo parokia zipatazo 25, ambazo ni Chengena, Hanga, Ifinga, Kitanda, Liganga, Ligera, Ligunga, Litapwasi, Lusonga, Magagura, Mgazini, Mahanje na Matimira.

Nyingine ni Matogoro, Mkongo, Mpandangindo, Mpitimbi, Msalaba Mkuu, Mtyangimbole, Namabengo, Namtumbo, Ndongozi, Peramiho, Songea-Town na Wino.

Askofu Mkuu Nobert W. Mtega, alizaliwa Kinyika (Lupanga-Njombe), Agosti 17, 1945. Alipata Daraja ya Upadre Novemba 14, 1973. Alipewa Daraja ya Uaskofu Januari 6, 1986 Roma na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili. Alisimikwa kuwa Askofu wa Jimbo la Iringa Machi 9, 1986. Aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Songea Julai 9, 1992 na kusimikwa Septemba 20, 1992 akichukua nafasi ya Askofu Mkuu Yakobo Komba.

Jimbo Katoliki la Sumbawanga linaongozwa na Mhashamu Askofu Damian Kyaruzi. Lina wakazi wapatao 748, 821 na kati ya hao 580, 000 ni Wakristo Wakatoliki.

Jimbo linahudumiwa na mapadre wazalendo 54. Aidha wapo Mapadre wa Wamisionari wa Afrika, Mapadre Wabenediktini wa Mvimwa na Mapadre wa Fidei Donum.

Pia wapo Mabradha Wamisionari wa Afrika na Mabradha Wabenediktini wa Mvimwa.

Mashirika ya masista ni pamoja na Masista wa Maria Malkia wa Afrika (MMMA) (Shirika la Jimbo) na Masista Wabenediktini wa Songea. Pia wapo Wakatekista 480.

Jimbo linazo parokia 19 ambazo ni pamoja na Chala, Kaengesa, Kala, Kasanga, Kate, Kirando, Laela, Matai, Mpui, Mwanzye, Namanyere na Pito.

Parokia nyingine ni Sopa, Sumbawanga - Cathedral, Sumbawanga - Kristo Mfalme, Sumbawanga - Familia Takatifu, Tunduma - Chiwanda, Ulumi na Zimba.

Askofu Damian Kyaruzi, alizaliwa Aprili 22, 1940 Bitainamwa, Jimbo Katoliki la Bukoba. Alipata Daraja ya Upadre Juni 29, 1968. Aliwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga Juni 29, 1997 mjini Sumawanga akichukua nafasi ya Mhashamu Askofu Charles Msakila.

JIMBO KUU LA TABORA

Jimbo Kuu la Tabora linaongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu Mario Abdallah Mgulunde. Linao wakazi wapatao 1, 409, 274 na kati ya hao Wakristo Wakatoliki ni 245, 733.

Jimbo linahudumiwa na mapadre wazalendo 34. Pia wapo Mapadre Wamisionari wa Afrika, Mapadre Wamisionari wa Mt. Fransisko wa Sale (MSFS) na Mapadre wa Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP/OSS).

Mashirika ya Mabradha nia pamoja na Mabradha (SCIM), Mabradha wa Upendo, Mabradha Wabenediktini wa Hanga na Mabradha Wamisionari wa Afrika.

Mashirika ya Masista ni pamoja na Mabinti wa Maria, Watumishi wa Moyo Safi wa Maria (SCIM), Masista wa Mt. Charles Borromeo, Masista Wamisionari wa Upendo (Masista wa Mama Theresa wa Calcuta), Masista Wakarmeli, Masista Wamisionari wa Mt. Anna, Masista wa Mt. Joseph de Cluny, Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro na Masista wa Grail.

Jimbo linazo parokia zipatazo 17 ambazo ni pamoja na Chomachankola, Igunga, Ipuli, Itaga, Kaliua, Kipalapala, Lububu na Makokola.

Parokia nyingine ni pamoja na Ndala, Ndono, Nzega, Nguruka, Sikonge, Tabora - St. Theresa Cathedral, Ulyankulu, Urambo na Ussongo (Igumo).

Askofu Mkuu Mario Abdallah Mgulunde, alizaliwa mwaka 1931 Kalenga jimboni Iringa. Alipata Daraja ya Upadre April 8, 1962. Aliwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Iringa Februari 15, 1970. Aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Tabora Machi 9, 1995 na kusimikwa Juni 16, 1985.

JIMBO KATOLIKI LA TANGA

Jimbo Katoliki la Tanga linaloongozwa na Mhashamu Askofu Anthony Banzi, lina wakazi wapatao 1, 667, 849 ambapo kati ya hao 166, 004 ni Wakristo Wakatoliki. Linahudumiwa na mapadre wazalendo 52. Pia wapo Mapadre Warosiminiani, Mapadre Wabenediktini, Mapadre wa Roho Mtakatifu na Mapadre Mmisionari wa Bethlehemu. Aidha wapo Mabradha Warosiminiani na Mabradha Wabenediktini.

Mashirika ya masista ni pamoja na Masista 480 wa Bibi Yetu wa Usambara, Masista Warosiminiani na Masista wa Damu Takatifu (CPS). Pia wapo Wakatekista 210.

Jimbo lina parokia zipatazo 26 ambazo ni pamoja na Amani, Gare, Hale, Handeni, Kabuku, Kilole, Kongoi, Kwai, Kwediboma, Lushoto, Kifungulo, Magoma, Malindi, Manundu, Maramba na Mazinde.

Parokia nyingine ni Mlingano, Muheza, Pangani, Pongwe, Potwe, Rangwi, Sakharani, Soni na Tanga - St. Anthony’s Cathedral.

Askofu Anthony Banzi, alizaliwa Oktoba 28, 1946 Tawa jimboni Morogoro. Alipta Daraja ya Upadre Julai 29, 1973. Aliteuliwa kuwa Askofu wa Tanga Juni 24, 1994 na kuwekwa wakfu Septemba 15, 1994 jimboni Tanga.