Make your own free website on Tripod.com

Wajue maaskofu na majimbo ya AMECEA

WAKATI Tanzania ikijiandaa kuupokea ugeni mkubwa kutoka nchi nane zinazounda Umoja wa Ushirikiano wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Nchi za Mashariki mwa Afrika (AMECEA), gazeti hili katika kumfanya kila msomaji wake afahamu kwa undani juu ya umoja huu, litakuwa likitoa habari za kila jimbo kwa nchi zote nane zinazounda AMECEA. Katika toleo hili, Mwandishi Wetu Maalumu, Pd. Raphael Kilumanga, anaendelea na majimbo ya Rulenge, Same, Shinyanga na Singida.

JIMBO KATOLIKI LA RULENGE

Jimbo Katoliki la Rulenge linaongozwa na Mhashamu Askofu Severine NiweMugizi. Linao wakazi wapatao 871, 436. Kati yao Wakristo Wakatoliki ni 504, 500.

Jimbo linahudumiwa na mapadre wanajimbo wapatao 69. Mbali na mapadre wa jimbo wapo pia Mapadre Wamisionari wa Afrika.

Mashirika ya mabradha jimboni humo ni pamoja na Mabradha Ndugu Wadogo wa Yesu na Mabradha wa Mt. Joseph.

Jimbo pia linao Masista Wafransiskani wa Mt. Bernadetta 150 (wa jimbo), Masista wa Mt. Theresa wa Mtoto Yesu, Masista wa Bibi Yetu Malkia wa Malaika na Masista Wafransiskani wa Heythuysen.

Wengine ni Masista Mitume wa Upendo Mkamilifu na Masista Wamisionari wa Upendo (Masista wa Mama Theresa wa Calcutta).

Jimbo lina parokia zipatazo 23 ambazo ni pamoja na Biharamulo, Bugene, Bugomora, Buhororo, Bushangaro, Businde, Buziku, Chato na Isingiro.

Parokia nyingine ni Kaaro, Katoke, Kibehe, Mabira, Murusagamba, Ntungamo, Nyaishozi, Nyakahura, Nyakato, Nyamigere, Rukora, Rulenge, Rwambaizi na Rwinyana.

Askofu Severine NiweMugizi, alizaliwa Juni 3, 1956 Parokiani Katoke Jimbo Katoliki la Rulenge. Alipata Daraja Takatifu ya Upadre Desemba 16, 1984. Alipata Daraja ya Uaskofu Februari 16, 1997 jimboni Rulenge akichukua nafasi ya Askofu Christopher Mwoleka aliyestaafu. Mhashamu Mwoleka alizaliwa Agosti 9, 1927, parokiani Itahwa Jimbo Katoliki la Bukoba. Alipata Daraja ya Upadre Juni 30, 1962. Aliwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa pili wa Rulenge, Juni 19, 1969 jimboni Rulenge.

JIMBO KATOLIKI LA SAME

Jimbo Katoliki la Same linaloongozwa na Mhashamu Askofu Jacob Venance Koda, lina wakazi wapatao 559, 384 ambapo kati yao 67, 202 ni Wakristo Wakatoliki.

Jimbo hilo linahudumiwa na Mapadre wazalendo 50. Pia yupo Padre wa Fidei Donum kutoka jimbo la Munich Ujerumani, Mapadre wa Roho Mtakatifu (Waspiritani) na Wafransiskani Wakonventuale.

Pia wapo Mabradha wa Mchungaji Mwema na Mabradha wa Ndugu Wafransiskani Wakapuchini.

Mashirika ya masista ni pamoja na Masista wa Grail wapatao 100, Masista Dada Wadogo wa Mt. Fransisko, Masista wa Bibi Yetu wa Usambara na Masista wa Moyo Safi wa Maria.

Wapo pia Wakatekista 180.

Jimbo lina parokia zipatazo 18 ambazo ni pamoja na Chabaru, Chanjale, Dido, Gonja Kighare, Gonja Maore, Hedaru, Kilomeni na Kisangara.

Parokia nyingine ni Kisiwani, Lembeni, Mamba, Manolo Kwizu, Mwanga, Ngulu, Same, Ugweno, Usangi na Vudee.

Askofu Jacob V. Koda, alizaliwa Desemba 9, 1957, Parokiani Kilomeni jimboni Same. Alipata Daraja ya Upadre Juni 25, 1987. Alipata Daraja ya Uaskofu Mei 30, 1999 jimboni Same.

 

JIMBO KATOLIKI LA SHINYANGA

Jimbo Katoliki la Shinyanga linaongozwa na Mhashamu Askofu Aloysius Balina. Lina wakazi 1, 773, 158 ambapo kati yao 158, 400 ni Wakristo Wakatoliki.

Jimbo linahudumiwa na Mapadre wazalendo wapatao 28 na Padre wa jimbo Mmarekani mmoja.

Pia wapo Mapadre wa Maryknoll, Mapadre wa Shirika la Utume wa Afrika (SMA) na Mapadre Wasalesiani wa Don Bosco.

Aidha wapo Madradha wa Maryknoll na Mabradha Wasalesiani wa Don Bosco.

Masirika ya Masista ni pamoja na Masista wa Moyo Safi, Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, Masista wa Bibi Yetu wa Mitume na Masista wa Bibi Yetu (Notre Dame).

Jimbo la Shinyanga lina parokia 24 ambazo ni pamoja na Bariadi, Bugisi, Buhangija, Busanda au Bukunu, Chamugasa, Gula, Kilulu, Malampaka, Malili, Mipa na Mwadui.

Parokia nyingine ni Ndoleleji, Ngokolo, Ng’wamapalala, Ng’wandoya, Ng’wanangi-Nasa, Ng’wanhuzi, Nyalikungu, Old Maswa, Salawe, Sayusayu, Shinyanga Town, St. Paul the Apostle na Wira au Wila.

Askofu Aloysius Balina, alizaliwa Juni 21, 1945 Isoso, Ntuzu-Bariadi jimboni Shinyanga. Alipata Daraja ya Upadre Juni 27, 1971. Aliwekwa wakfu kuwa Askofu Januari 6, 1985 na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili huko Roma. Alisimikwa kuwa Askofu wa kwanza wa Geita Machi 10, 1985. Alihamishiwa Shinyanga Septemba 23, 1997 na kusimikwa kuwa Askofu wa tatu wa Shinyanga Novemba 16, 1997. Watangulizi wake ni Wahashamu Edward McGurkin M. M (1956-1975) na Castor Sekwa (1975-1996) ambao wote ni marehemu.

JIMBO KATOLIKI LA SINGIDA

Jimbo Katoliki la Singida linalongozwa na Mhashamu Askofu Desiderius Rwoma. Jimbo lina wakazi wapatao 1, 200, 000. Kati yao Wakristo Wakatoliki ni 130, 239.

Jimbo linahudumiwa na mapadre wazalendo 41. Mbali na hao pia wapo mapadre wa mashirika, ambao ni, Mapadre Wakonsolata, Mapadre Wapallotini, Mapadre wa Damu Azizi na Mapadre Wamisionari wa Msalaba Mtakatifu.

Pia yapo mashirika ya mabradha ambayo ni pamoja na, Mabradha wa Damu Takatifu na Mabradha Wamisionari wa Msalaba Mtakatifu.

Mashirika ya masista jimboni humo ni pamoja na Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu, Masista wa Huruma, Mabinti wa Maria, Masista wa Medical Missionaries of Mary (wanaoshughulikia afya) na Masista wa Kupalizwa Mbinguni (Assumption Sisters).

Mashirika mengine ni Masista Wamisionari wa Bibi Yetu wa Afrika, Masista Wamama wa Msalaba Mtakatifu, Masista wa Upendo wa Mt. Karoli Borromeo, Masista wa Upendo wa Mt. Vincenti wa Paulo na Masista wa Mt. Ursula (Ursoline Sisters).

Wengine ni Masista Wapallotini, Masista wa Roho Mtakatifu (Holy Spirit Sisters), Masista wa Mt. Gemma Galgani na Masista Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu na Maria (Suore Missionarie dei Sacri Cuoridi Gesu'e Maria). Pia wapo Wakatekista 328.

Jimbo la Singida linazo parokia 16 ambazo ni pamoja na Chemchem, Chibumagwa, Dung’unyi, Heka, Iguguno, Ilongero, Itaja, Itigi na Kintinku.

Parokia nyingine ni pamoja na Kiomboi, Makiungu, Manyoni, Mtinko, Ntuntu, Sanza na Singida.

Askofu Desiderius Rwoma, alizaliwa Mei 8, 1947 kijijini Ilogero, Parokia ya Rutabo Jimbo Katoliki la Bukoba. Alipata Daraja ya Upadre Julai 28, 1974. Alipata Daraja ya Uaskofu Julai 11, 1999 jimboni Singida akiwa Askofu wa pili wa Singida baada ya kustaafu Askofu Bernard Mabula. Mhashamu Mabula alizaliwa mwaka 1920, Ndala Jimbo Kuu la Tabora . Alipata Daraja ya Upadre Agosti 15, 1952. Aliwekwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Tabora Mei 4, 1969. Baadaye alihamishwa na kusimikwa Machi 25, 1972 kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Singida.