Wajue maaskofu na majimbo ya AMECEA

WAKATI Tanzania ikijiandaa kuupokea ugeni mkubwa kutoka nchi nane zinazounda Umoja wa Ushirikiano wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Nchi za Mashariki mwa Afrika (AMECEA) , gazeti hili katika kumfanya kila msomaji wake afahamu kwa undani juu ya umoja huu, litakuwa likitoa habari za kila jimbo kwa nchi zote nane zinazounda AMECEA. Katika toleo hili, tunaendelea na majimbo ya Mtwara, Musoma, Mwanza na Njombe.

JIMBO KATOLIKI LA MTWARA

Jimbo Katoliki la Mtwara linaongozwa na Askofu Gabriel Mmole. Lina wakazi wapatao 731, 988. Kati yao 62, 877 ni Wakristo Wakatoliki.

Jimbo hilo linahudumiwa na mapadre wanajimbo wapatao 20. Mbali na mapadre wa jimbo pia wapo Mapadre 19 wa Shirika la Mapadre Wabenediktini. Aidha wapo Mabradha 27 Wabenediktini.

Mashirika ya masista ni pamoja na Masista Wabenediktini Waafrika wa Bibi Yetu wa Msaada wa Wakristo Ndanda, Masista Wabenediktini Wamisionari wa Tutzing na Masista Mabinti wa Mkombozi Mtakatifu. Jimbo pia linao Wakatekista wapatao 162.

Jimbo Katoliki la Mtwara linazo parokia zipatazo 15, ambazo ni Chigugu, Chihangu, Chikundi, Kitangali, Luagala, Mahurunga, Mikindani na Mtwara-All Saints.

Parokia nyingine ni Mtwara-St. Paul, Mtwara-Magomeni, Nangoo, Nanyamba, Ndanda, Newala na Tandahimba.

Askofu Gabriel Mmole, alizaliwa mwaka 1939 Nangoo jimboni Mtwara. Alipata Daraja ya Upadre Oktoba 14 1971. Aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa Mtwara Mei 25, 1988 jimboni Mtwara.

JIMBO KATOLIKI LA MUSOMA

Jimbo Katoliki la Musoma linaongozwa na Mhashamu Askofu Justin Samba. Lina idadi ya wakazi wapatao 1, 200,000. Kati ya hao 250, 000 ni Wakristo Wakatoliki.

Jimbo linahudumiwa na Mapadre wanajimbo wapatao 36. Pia wapo mapadre wa mashirika ambao ni pamoja na Mapadre wa Fidei Donum kutoka Poland, Mapadre wa Maryknoll na Mapadre wa Shirika la Mitume wa Yesu.

Mashirika mengine ni ya Mapadre Waklaretiani (Claretian), Mapadre wa Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP/OSS) na Mapadre wa Ndugu Wafransiskani Wakapuchini.

Mashirika ya mabradha ni Mabradha wa Maryknoll, Mabradha wa Marist, Mabradha wa Ndugu Wafransiskani Wakapuchini na Mabradha wa Montfort wa Mt. Gabriel.

Aidha yapo mashirika ya masista ambayo ni pamoja na Masista 118 wa Moyo Safi wa Maria wa Afrika (IHSA) ambao ni wa jimbo, Masista wa Maryknoll, Masista wa Mabinti wa Maria, Masista Wakarmeli wa Mtoto Yesu, Masista wa Canossa, Masista wa Sakramenti Takatifu, Masista wa Mama wa Mlima Karmeli.

Masista wengine ni Masista wa Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCS/OSS), Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, Masista wa Neno Aliyejifanya Mtu (Incarnate Word Sisters) na Masista wa Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili wa Ivrea.

Jimbo lina parokia 31 ambazo ni pamoja na Bunda, Butiama, Ingri, Iramba, Issenye, Kiabakari, Kiagata, Kibara, Kisorya, Komuge, Kowak, Mabui, Masonga, Mugango, Mugumu na Musoma-Cathedral.

Parokia nyingine ni Mwisenge, Nyamiongo, Nyamongo, Nyamwaga, Nyamuswa, Nyarombo, Nyegina, Rogoro Quasi, Rosana, Rwamlimi, Shirati, Sirari, Tarime, Tatwe na Zanaki.

Askofu Justin Samba, alizaliwa Desemba 12, 1950 Mkuu, Rombo jimboni Moshi. Alipata Daraja ya Upadre Juni 26, 1974. Alipata Daraja ya Uaskofu Januari 6, 1989 huko Roma. Na alisimikwa Februari 26, 1989 akichukua nafasi ya Askofu Anthony Mayala aliyehamishiwa Jimbo Kuu la Mwanza.

 

JIMBO KUU LA MWANZA

Jimbo Kuu la Mwanza linaongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu Anthony Mayala. Lina wakazi wapatao 3,500,000.Kati yao Wakristo Wakatoliki 775,000.

Jimbo hilo linahudumiwa na mapadre wazalendo wapatao 46. Pia wapo Mapadre Wamisionari wa Afrika, Mapadre wa Maryknoll, Mapadre Wayezuiti na Mapadre wa Shirika la Utume wa Afrika (SMA).

Pia wapo Mabradha wa Jimbo na Mabradha Wamisionari wa Afrika.

Mashirika ya masista ni pamoja na Masista Dada Wadogo wa Yesu, Masista wa Medical Missionaries of Mary (wanaoshughulikia afya) na Masista Waklara Fukara wa Colettine, Masista wa Mt. Theresa na Masista wa Mabinti wa Maria.

Masista wengine ni Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, Masista wa Moyo Safi wa Maria wa Afrika, Masista wa Loreto, Masista Wabenediktini, Masista wa Canossa, Masista Wamisionari wa Bibi Yetu wa Afrika na Masista wa Mt. Bernadetta. Pia wao Wamisionari Walei saba na Wakatekista 825.

Jimbo linazo parokia 26 ambazo ni pamoja na Bugando Cathedral, Buhingo, Bujora, Bukumbi, Butimba, Ibindo, Ilemera, Itira, Kagunguli, Kawekamo, Kikundi, Kirumba na Magu.

Parokia nyingine ni Nyakahoja, Malya, Misungwi, Murutunguru, Mwabagole, Mwamashimba, Nansio, Ngudu, Nyakato, Nyamanga, Nyambiti, Nyegezi na Sumve.

Askofu Mkuu Anthony Mayala, alizaliwa Aprili 23, 1940 Mwabagole, Kwimba jimboni Mwanza. Alipata Daraja ya Upadre Desemba 20, 1970. Aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa Musoma Aprili 22, 1979. Alisimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Mwanza Februari 28, 1988.

JIMBO KATOLIKI LA NJOMBE

Jimbo Katoliki la Njombe linaongozwa na Mhashamu Askofu Raymond Mwanyika. Lina wakazi wapatao 640, 380. Kati ya hao Wakristo Wakatoliki ni 217, 985.

Jimbo hilo linahudumiwa na mapadre wanajimbo wapatao 73. Pia wapo Mapadre Wabenediktini wa Mt. Ottilien na Mapadre Wakonsolata. Aidha wapo Mabradha Wabenediktini wa Mt. Ottilien.

Mashirika ya masista ni pamoja na Masista Wabenediktini wa Tutzing, Masista Wakonsolata, Masista wa Mt. Agnes (wa jimbo), Masista wa Mt. Theresa wa Mtoto Yesu (wa jimbo) na Masista Wakolejina (Collegine Sisters). Pia yupo Mmisionari Mlei mmoja na Wakatekista 359.

Jimbo lina parokia 31 ambazo ni pamoja na Igwachanya, Ihanga, Ikonda, Kifanya, Kifumbe, Kipengere, Kisinga, Ludewa, Luduga, Lugarawa, Lugenge, Luilo, Lumbila na Lupanga.

Nyingine ni, Lupingu, Luwana, Madunda, Makambako, Manda, Manga, Matamba, Matembwe, Matola, Mavanga, Mlangali, Mtwango, Mundindi, Njombe, Sunji, Uliwa na Uwemba.

Askofu Raymond Mwanyika, alizaliwa mwaka 1930 Parokiani Uwemba jimboni Njombe. Alipata Daraja Takatifu ya Upadre Oktoba 11, 1959. Alipata Daraja ya Uaskofu Aprili 25, 1971 jimboni Njombe.