Wajue maaskofu na majimbo ya AMECEA

WAKATI Tanzania ikijiandaa kuupokea ugeni mkubwa kutoka nchi nane zinazounda Umoja wa Ushirikiano wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Nchi za Mashariki mwa Afrika (AMECEA), gazeti hili katika kumfanya kila msomaji wake afahamu kwa undani juu ya umoja huu, litakuwa likitoa habari za kila jimbo kwa nchi zote nane zinazounda AMECEA. Katika toleo hili, Mwandishi Wetu Maalumu, Pd. Raphael Kilumanga, anaendelea na majimbo ya Tunduru- Masasi na Zanzibar .

JIMBO KATOLIKI LA TUNDURU-MASASI

Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi linaongozwa na Mhashamu Askofu Magnus Mwalunyungu. Lina wakazi wapatao 669, 854 na kati yao 78, 740 ni Wakatoliki Wakatoliki. Jimbo linahudumiwa na mapadre wazalendo 22. Mbali na mapadre hao wa jimbo wapo Mapadre na Mabradha wa Shirika la Wasalvatoriani.

Mashirika ya masista ni pamoja na Masista Wabenediktini wa Ndanda, Masista Wabenediktini wa Songea, Masista Wasalvatorian na Masista wa Maria Immakulata. Pia wapo Wakatekista 135.

Jimbo linazo parokia 16 ambazo nia pamoja na Chikukwe, Chingulugulu, Chiungutwa, Hulia, Lukuledi, Lupaso na Mkanya.

Parokia nyinginejimboni humo ni Makulani, Masasi, Mangaka, Matemanga, Mahuwesi, Nakapanya, Nambaya, Nandembo na nanjota.

Askofu Magnus Mwalunyungu alizaliwa Agosti 25, 1930 jimboni Iringa. Alipata Daraja ya Upadre Agosti 23, 1959. Aliwekwa wakfu kuwa Askofu wa jimbo la Tunduru-Masasi Juni 25, 1992 jimboni humo.

JIMBO KATOLIKI LA ZANZIBAR

Jimbo Katoliki la Zanzibar linaongozwa na Mhashamu Askofu Augustine Shao, C.S.Sp. Lina wakazi wapatao 965, 000 na kati yao 13, 215 ni Wakristo Wakatoliki. Linahudumiwa na mapadre wazalendo wapatao 14.

Jimboni humo wapo Masista wa Bibi Yetu wa Usambara, Masista wa Moyo Safi wa Maria, Masista wa Damu Takatifu na Masista Wainjilishaji wa Maria. Pia wapo Wakatekista 46.

Jimbo linazo parokia 7 ambazo ni pamoja na Chakechake, Kitope, Machui, Mpendae (Sub-Parish), Kiboje (Sub-Parish), Wete na Zanzibar - St. Joseph’s Cathedral.

Askofu Augustine Shao C.S.Sp, alizaliwa Septemba 25, 1950 Mamsera Juu, Rombo jimboni Moshi. Alipata Daraja ya Upadre Juni 4, 1983. Aliewkwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa pili wa Zanzibar Aprili 28, 1997 akichukua nafasi ya Askofu Bernard Ngaviliau.