Kitabu cha Kiada kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo (29)

BAADA ya kumaliza mfululizo wa chapisho la kitabu kiitwacho HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA- TANZANIA BARA, kwa kuwa tumegundua kuwa kitabu hicho kimewanufaisha zaidi wasomaji wetu, kwa kuwafanya wajue mambo mengi juu yao ambayo awali hawakuwa wakiyafahamu kuwa ni wajibu na haki yao, kuyapata na kuyafanya, na kwa kuwa tunawajali wasomaji wetu, sasa tunazidi kuwafaidisha kwa kukidhi zaidi kiu yao. Tunaendelea na chapisho la kitabu kiitwacho KITABU CHA KIADA KWA MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO ambacho tunaamini si tu kwamba kitawanufaisha mahakimu peke yao, bali pia jamii nzima ya Watanzania; nacho, tunakichapa kama kilivyotolewa na Tume ya Haki na Amani(TEC). Tulianza na dibaji iliyoandikwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Barnabas Samatta, ukafuatia utangulizi, sasa tunaendelea na Namba 3.6" Aina za Utoaji wa Adhabu..."

Aidha Mahakama ya Wilaya inayo madaraka kufanya masahihisho (mapitio) katika mienendo ya kesi za Mahakama ya Mwanzo kwa kupitia mafaili ya kesi za mahakama ya Mwanzo (revision) mara kwa mara. Mahakama ya Mwanzo yaweza pia kujikosoa na kusahihisha makosa yake inapogundua kuwa ilifanya makosa katika maamuzi. Yaweza kufanya hivyo kwa njia ya marejeo (review).

Hata hivyo tujiulize ni mara ngapi hakimu amekubali kujisahihisha makosa yake hata kama anaona bayana kuwa alifanya makosa katika maamuzi.

Hii inaweza kutokea kama kwa bahati mbaya au kutofahamu, hakimu ametumia sheria ambayo tayari imekwisha badilishwa na chombo husika au hakubaini kuwepo uamuzi wa mahakama ya juu zaidi kuhusu jambo analolishughulikia na ameamua kupingana na uamuzi wa hiyo mahakama ya juu (per incuriam).

Mara nyingi utawasikia mahakimu katika hali kama hizi wakiwakatisha tamaa walalamikaji na kutetea maamuzi yao potofu au kuwaambia wakate rufaa kama watapenda kupoteza muda wao.

Uzoefu umeonyesha kuwa utaratibu huu wa hakimu kujikosoa mwenyewe hautumiki kabisa.

Inawezekana mahakimu wanahofia kuonekana kwamba hajui sheria au kuhisiwa kuwa wanakuwa wamepokea hongo mpaka kubadili maamuzi yao ya hapo awali. Hakimu akiogopa kutenda haki kwa kuhofia kuhisiwa vibaya inakuwa ni dalili tosha ya kutojiamini na anakuwa ameshindwa wajibu wake. Haki inapaswa kutendeka hata kama mbingu zitashuka (Justice should be done even if heavens fall).

Kazi ya kukagua na kupitia mafaili ya mahakama ya mwanzo (revision) ni jukumu la Mahakama ya Wilaya. Kama tulivyoishajadili hapo awali, Mahakama ya Wilaya yaweza kupitia mafaili haya wakati wa kutekeleza jukumu lake la ukaguzi na ikanyoosha kile ambacho itagundua kilipindwa kwa makusudi au kwa bahati mbaya ili mradi haki itendeke.

Wakati mwingine Mahakama ya Wilaya yaweza kupokea malalamiko kutoka kwa mtu yeyote kuhusu mwenendo mzima wa kesi na ikabidi iitishe faili kwa ukaguzi kutokana na matatizo ya uhaba wa watendaji, usafi na ufinyu wa bajeti imekuwa vigumu kwa Mahakama za Wilaya kufanya ukaguzi kwenye Mahakama za Mwanzo mara kwa mara. Hata inapotokea mtu akiwasilisha malalamiko yake Mahakama ya Wilaya bado kwa sababu zilizotajwa hapo awali ufuatiliaji wake ni mgumu kwani inalazimu faili liitwe kwa ajili ya ukaguzi na marekebisho yafanyike kama itabidi.

Hali hii ni kama changamoto kwa Mahakimu wa mahakama za Mwanzo.

Inawapasa kufanya kazi zao kwa uangalifu wakijua kuwa wanapofanya makosa katika maamuzi na uadilifu zaidi hali wakijua kuwa wanapofanya makosa katika maauzi nafasi ya Wilaya kuyarekebisha ni ndogo kutokana na matatizo yaliyopo.

Kazi kubwa iko katika utaratibu wa kukata rufaa ambapo lazima faili zima la kesi liwepo na mwenendo wa kesi upigwe chapa ili uambatane na hukumu inayokatiwa rufaa.

Kuna ugumu mkubwa katika kuwapatia wafungwa waliohukumiwa hukumu iliyochapwa kwa ajili ya kukata rufaa.

Sababu kuu huwa ni tatizo la kupatikana huduma ya kisheria gerezani kwa karatasi katika mahakama na pia huduma ya kisheria gerezani kwa wafungwa ambao wanataka kukata rufaa hupatikana kwa baadhi tu ya magereza/mikoa nchini.

Hii huchelewesha rufaa za washitakiwa kupelekwa mahakama iliyo juu.

Maadili ya Uhakimu

"Kuna kazi katika jamii yetu ambazo zinaweza kufanywa na watu wasio na nidhamu. Watu ambao uadilifu wao unatia mashaka. Kuwa Jaji au Hakimu siyo moja za kazi hizi. "

Mwalimu Julius K. Nyerere"

 

4.1 Maana ya Maadili

Maadili hutokana na neno "Adili" ikimaanisha hali ya kutenda mema, uelekevu na unyoofu. Hivyo maadili ni mambo, taratibu au miongozo inayotufanya tutende mema, tuwe waelekevu na wanyoofu.

Kila kazi, taaluma, au fani ina maadili yake. Kwa upande wa fani ya Uhakimu ambamo wamo wale wote ambao kazi yao ni kuhukumu yaani Mahakimu na Majaji yapo maadili yaliyo na umuhimu kwa ufanisi bora wa kazi yao. Kiutendaji maadili ya uhakimu yanapingana na tabia ya upendeleo katika kutoa hukumu ya kesi yoyote inayohusisha watu binafsi au watu binafsi/raia na mamlaka ya nchi. Sheria inamlinda hakimu anapotoa maamuzi ya haki bila upendeleo.

Hivyo basi, hakimu anatakiwa kuwa mtu thabiti asiye tetereka katika kutenda haki bila kuwa na upendeleo hata kama serikali nayo inaletwa mbele yake kujibu tuhuma au madai. Uthabiti wa mtu binafsi, kwa hiyo, ni moja ya maadili makubwa ya kazi ya uhakimu.

Kwa kuzingatia umuhirnu mkubwa wa maadili katika kazi ya uhakimu, Idara ya Mahakama kupitia Mkutano wa Majaji na Mahakimu Wakazi imetunga na kupitisha Kanuni ya Tabia ya Maafisa wa Mahakama Tanzania, Machi 1984 (Code of Conduct for Judicial Officers of Tanzania). Kanuni hiyo inaweka masharti mbali mbali ya maadili ya Mahakimu na Majaji wa Tanzania Bara na ukiukwaji wa masharti haya unapelekea kuchukuliwa hatua za kinidhamu dhidi ya afisa husika."

Hakimu anapaswa kufanya maamuzi siyo kwa sababu ya ahadi alizopewa au mafao ambayo amekwishapatiwa au atakayopatiwa au hata kwa kuogopa kudhuriwa au hata pengine kupoteza haki yake. Hakimu anapaswa kufanya kazi kulingana na maadili ya taaluma yake, kuzingatia sheria na ushahidi uliotolewa mbele yake na kutenda haki bila uoga.

Utendaji haki ndiyo tengo mama la uhakimu na masharti yote ya kimaadili yanalenga katika kutekeleza hilo lengo kuu. Hivyo basi hakimu hapaswi kujiweka katika mazingira ambayo yanapendekeza kwa watu kuamini kuwa hayuko huru bali kuna watu ambao wana nafasi maalum kiasi cha kumshawishi hakimu katika maamuzi yake. Wakati wote hakimu lazima awe mfano kwa jamii kitabia na hii husaidia kujenga imani ya watu kwake na mahak-ama kwa ujumla kama chombo kisicho kuwa na upendeleo.

Hii ni pamoja na kuwa mwangalifu katika kuchagua marafiki na mahali pa kutembelea. Kwa mfano inatia shaka sana kuhusu tabia, uhuru na mwenendo wa hakimu ambaye rafiki zake ni wale watu ambao ni wahalifu au watu ambao jamii inatilia mashaka mienendo yao.

Mbali na hayo kuzingatia maadili ya kazi kunampatia heshima hakimu binafsi na pia kunaipatia heshima kazi ya uhakimu na mahakama kwa ujumla.

Kama tulivyokwishaongelea hapo hawali, uhuru wa mahakama unaheshimiwa zaidi pale ambapo mahakama yenyewe inajionyesha kuwa ni chombo cha hadhi na kinachojiheshimu.

Inafaa pia mahakimu waelewe na kukumbuka daima kwamba watu wanaohukumiwa wana uwezo wa kutambua hukurnu iliyo ya haki na si lazima mtu awe hakimu au mwanasheiia katika kuelewa hilo. Bila shaka mahakimu wanaweza kuthibitisha hilo kutokana na uzoefu wao wanapokutana na watu ambao waliwahukumu kwa makosa mbalimbali hapo awali.

Lazima hakimu anapokuwa mahakamani akisikiliza kesi akumbuke kuwa hata na yeye pia anahukumiwa na jamii ikiwakilishwa na watu wanaokuwemo mahakamani kwake wakimwangalia jinsi anavyoendesha kesi.

Mara nyingi ukiukwaji wa maadih ya uhakimu kama vile upokeaji rushwa (hongo) husababishwa na tamaa au uchu wa kupenda kujilimbikizia mali. Hakimu ni lazima aepukane na tamaa ya kuwa na mali kuliko uwezo wake. Tamaa ni adui mkubwa wa haki na bila kuishinda tamaa, haki. hugeuzwa bidhaa ya kuuzwa sokoni.

Si jambo rahisi kutoa hukumu ya haki na ni vigumu zaidi kuwathibitishia wenye kesi hasa wanaoshindwa kuwa haki imetendeka. Hakimu ni lazima awe mtu mvumilivu sana. Anatakiwa asikilize kwa makini na kwa urefu maelezo ya kila upande katika kesi. Siyo jambo jema kusikiliza upande mmoja tu na kuunyima upande wa pili nafasi ya kutosha kutoa maelezo yake kwa kina. Hakimu akiweza kutoa nafasi sawa kwa wote hii huondoa ile hisia ya upendeleo.

Hata hivyo, kuna matatizo mengi ambayo yanaweza kuingilia shughuli za hukumu na hakimu akaonekana kuwa ni dhalimu au kapokea chochote ndiyo maana akafikia uamuzi aliotoa. Hii husababishwa na ushahidi unaotolewa mahakamani kupingana lakini lazima hakimu akubaliane au aamini ushahidi wa upande mmoja wapo vinginevyo hawezi kuandika hukumu. Ngumu zaidi ni pale hakimu anapotakiwa kutolea hukumu kesi ambayo imekuwa na mashahidi wawili tu, mlalamikaji na mlalamikiwa. Ni wajibu wa hakimu kutumia ujuzi wake wa kuchambua ushahidi na pia kuangalia na kuchambua mwenendo au tabia ya shahidi akiwa kizimbani ili aweze kumwamini au kutomwamini

Wajibu wa hakimu ni kufanya uadilifu kadiri ya upeo wake.

Mambo huwa magumu zaidi pale hakimu anapokabiliwa na mashauri ambayo yanawahusu wenye nguvu, utajiri mkubwa, mamlaka na uwezo. Wakati mwingine baadhi ya wanasiasa hupenda kesi ziendeshwe na kuamuliwa kisiasa au jinsi wanavyotaka wao bila kujali maelekezo ya sheria na haki.

Hata katika ugumu huu, hakimu muadilifu hatayumba na atafanya yaliyo ya haki tu. Mfano ni ile kesi ya R. v. Idd Mtegule" iliyotokea huko Dodoma ambapo mshitakiwa alikamatwa na kupelekwa Mahakama ya Mwanzo Kibakwe huko Mpwapwa akishitakiwa na kosa la kutotii anui halali chini ya kifungu cha 124 cha Kanuni ya Adhabu. Mshitakiwa alikutwa akiuza maandazi kinyume na amri aliyotoa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa katika harakati za kupambana na ugonjwa wa kipindupindu. Hata hivyo katika orodha ya vyakula ambavyo vilizuiliwa na amri ya Mkuu wa Wilaya, maandazi hayakuwemo.

Baada ya kuangalia ushahidi, hakimu alimwachia huru mshitakiwa kwa kuwa maandazi ni chakula cha moto na isitoshe hayakuwa katika orodha ya vyakula vilivyozuiliwa.

Hii ilimkasirisha Mkuu wa Wilaya ambaye alimwandikia barua Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ajieleze kwa nini hakumwadhibu mshitakiwa huyo.

Itaendelea Toleo lijalo

Maskini unganeni kuondokana na umaskini(6)

d) Mafunzo kwa viongozi wa vikundi vya kijamii.

Katika kikundi chochote kile cha kijamii wamo watu ambao wana kipaji cha uongozi. Kwa upande mwingine sio watu wote wanaopenda kujiunga na vyama vya siasa na kufanya kazi nao. Kwa mantiki hiyo basi inafaa tuelewe kuwa uongozi wa kisiasa ni sehemu moja tu ya uongozi na hivyo hawapaswi kushikilia mamlaka yote ya kufanyia maamuzi. Zipo aina nyingine za uongozi ambazo nazo zina umuhimu mkubwa.

Aina hizi ni pamoja na Uongozi wa kidini, Uongozi wa Sherehe za kijamii, uongozi wa vikundi huru kama wazazi, vijana, wanawake na michezo inafaa kama Taifa kutambua na kuheshimu uongozi wa aina hizi na hivyo kuwa tayari kutumia mali ya umma kuhimiza na kutoa mafunzo kwa uongozi wa kijamii.

Kwa kuwa ni wajibu wa mamlaka ya Serikali na Vyama kuhakikisha zinatengwa fedha kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa viongozi na makada wao, basi kwa nia hiyo hiyo Serikali inapaswa kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo ya viongozi wa kijamii.

Viongozi wa vikundi wanatakiwa wafundishwe namna ya kuviongoza vikundi vyao viweze kuwa na uwezo wa kusukuma na kushinikiza mambo, namna ya kushiriki katika, kufanya maamuzi na pia kujua mbinu za kushawishi (lobby) Bunge na Taasisi za Kiserikali.

Hili sio jukumu la kuachiwa Wafadhili kama inavyofanyika sasa, kwani hatari yake ni kwamba maoni na vigezo vinavyotumiwa na wafadhili ndivyo vinavyoamua ajenda za vikundi vyetu vya kijamii.

Kwa bahati mbaya viongozi wa kisiasa wanavichukulia vikundi vya kijamii kama vipo kwa malengo ya kushindania au kunyang’anyana madaraka nao. Kumbe ukweli ni kwamba viongozi hawa wa pande hizi mbili wanatakiwa kuchukuliana kama wenzi katika kutafuta na kuunda sera nzuri kwa faida ya jamii nzima.

Ushirikiano huu ni muhimu kwa ngazi zote toka ngazi ya chini kabisa wanamoishi watu. Kwani ushirikiano huu ndio unaoweza kuhakikisha uwakilishi wa watu kwa ngazi mbalimbali kuanzia vikundi, kijiji, wilaya na hatimaye mkoa hadi taifa. Kama mambo hayatakwenda katika ushirikiano huo kamwe ushiriki wa watu kupitia vikundi vya watu vilivyo katika ngazi za chini hautaweza kuwepo.

Ili kuhakikisha ushiriki wa vikundi hivi, inabidi mwelekeo huo wa ushiriki kutoka chini uhimizwe na pia watu wahimizwe kuunganika. Na hii ni kazi ya wale wanaowajibika na Serikali.

Lazima ieleweke na kukumbukwa daima kwamba watu hawa wanaounda vikundi vya kijamii katika ngazi ya chini ndio lile kundi la wale walio wengi nchini, ambao maoni yao hatuwezi kuendelea kuyaweka pembeni ama kuyadharau.

Viongozi wa kijamii wanao wajibu wa pekee kwa watu. Viongozi hao wanapaswa kuwasaidia watu katika kuweka mawazo yao vizuri na kuweza kuyaona mawazo yao ndani ya mpango mzima wa Serikali na miundo ya Taasisi zinazotoa huduma.

Ni muhimu pia watu wasaidiwe kushawishi na kuunda mitandao kwa lengo la kuungwa mkono na vile vile wajue mbinu za kufuatilia mambo katika mpango wa kudumu ikiwa ni pamoja na kuuliza maswali katika mikutano ya hadhara na kutafuta taarifa toka wawakilishi wao.

3. Kutumia fursa zilizopo katika mpango wa Mikakati ya kupunguza umaskini nchini (PRSP).

Mpango wa sasa wa kupunguza umaskini kama ulivyofafanuliwa na PRSP unalenga kuzipa Serikali za Wilaya wajibu zaidi ya hapo awali katika kugawanya fedha kwa matumizi mbalimbali. Kwa sasa ngazi ya Wilaya itawajibika katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maendeleo ya kijamii, Sheria na taratibu, utoaji wa huduma za elimu, afya, maji na barabara na pia utoaji wa huduma za kilimo.

Serikali Kuu itabaki na wajibu wa kutuma fedha Wilayani kwa ajili ya majukumu yaliyo chini ya Wilaya.

lnafaa pia ieleweke kuwa mpango huu si kwamba tu umeingizwa na Benki ya dunia na jumuiya ya wafadhili bali pia unaoungwa mkono vikali na watu hawa. Vile vile mpango huo wa Mikakati ya Kupunguza Umaskini (PRSP) ndio unaotoa mwongozo wa utendaji kwa miaka ijayo.

PRSP imechambua vizuri hali halisi ya umaskini nchini ambapo umaskini umeelezwa kuwa ndio hali ya maisha ya watu wa vijijini hasa kwa wale ambao hawana zao la biashara. Kwa upande wa mijini umaskini unazidi kuongezeka. Kwa kuangalia makundi- maalum umaskini zaidi uko kwa vijana, wazee na pia katika familia zenye idadi kubwa ya watu kwa kulinganisha wanawake wanaelekea kuishi katika umaskini zaidi ya wanaume.

PRSP inaendelea kueleza kuwa hali ya umaskini inaonyesha kuwa tofauti ya kipato miongoni mwa wananchi inazidi kuwa kubwa; na pia matunda ya urekebishaji wa uchumi yamechangia kuongeza hali hiyo ya tofauti ya kipato.

Kwa maneno mengine marekebisho mapya ya uchumi yanazidi kuleta mzunguko ambao utaendelea kutowanufaisha maskini, kwa sababu watafaidika kidogo tu katika elimu, huduma za afya na wataendelea kusumbuka na hali duni ya lishe. Watabaki pia kuendelea kutumia maji toka vyanzo ambavyo havitunzwi na vile vile kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na matukio yasiyotabirika.

Wakati huo huo uchambuzi wa PRSP unaonyesha kuwa baadhi ya mikoa imeachwa nyuma kabisa, na mikoa hii ni Kagera, Kigoma, Dodoma, Pwani na Lindi, wakati mikoa mingine ina nafuu.

Katika mwelekeo huu wa kuwa na sera zinazofanana kwa mikoa yote katika mpango wa uboreshaji wa mfumo wa Serikaii za Mitaa, hapana shaka tofauti hiyo itaendelea kukua.

Wakati wa kuandaa PRSP baadhi ya watu walishirikishwa kutoa mawazo ambapo picha ilijionyesha kuwa watu wanayaelewa matatizo waliyo nayo katika maeneo mbalimbali.

Katika sekta ya Kilimo zana za kilimo zinazotumika ni duni licha ya kwamba kuna ukosefu wa pembejeo za kilimo. Kwa upande wa usafirishaji barabara ni mbovu na hakuna soko la kutosha wala la uhakika kwa kuuzia mazao yao.

Katika Sekta ya Elimu hali ilivyo sasa elimu ya msingi haipatikani kwa wote hasa linapokuja suala la uchangiaji wa gharama. Kwa upande mwingine ipo tabia ya kuwa na matumizi mabaya ya fedha zinazotokana na michango ya wazazi, licha ya kuwa hali ya ufundishaji ni duni.

Kwa sababu hizi na nyinginezo pia idadi ya watoto wanaoacha shule ni kubwa. Kwa ujumla miongoni mwa maskini, idadi ya wasiojua kusoma na kuandika inazidi kuongezeka.

Haya ni baadhi tu ya maelezo toka PRSP ambayo yanadhihirisha kuwa watu wanajua matatizo yao. Kinachoonekana ni kwamba tatizo lipo katika hatua inayofuata yaani namna ya kutatua matatizo hayo. Hapa ndipo watu wanahitaji kupewa mwanga na maelekezo. Sasa tujiulize, Je, mpango wa uboreshaji wa Serikali za Mitaa utaweza kutoa maelekezo yanayohitajika? Mpango wa uboreshaji katika Serikali za Mitaa utaweka nguvu zake katika ngazi za chini kusaidia watu kujinasua toka hali ya umaskini iliyodumu kwa muda mrefu na ambayo inawakabili watu hadi leo?

Yafaa pia tujiulize kama Serikali za Mitaa zinao uwezo wa kutekeleza wajibu wao katika mpango huo wa urekebishaji na uboreshaji ambao kwa kweli una malengo mazuri tu.

Serikali za Mitaa zitakuwa tayari kupokea majukumu hayo kwa moyo safi na fikra nzuri uu ya kushirikisha watu wa chini katika kufikia uamuzi juu ya namna gani utekelizaji wa majukumu yaliyoongezeka utafanyika hivyo kwamba fedha zinazoongezwa katika Serikali za Wilaya zitatumika vizuri kwa malengo yaliyowekwa na kuleta matokeo yaliyokusudiwa

Ukweli ni kwamba mpango wa urekebishaji wa mfumo wa Serikali za Mitaa unatoa fursa kwa watu kunufaika zaidi katika huduma za jamii. Lakini ili kuhakikisha hilo linafanikiwa ni lazima Serikali za Wilaya ziwe zinasukumwa na kushinikizwa na vikundi vya kijamii vilivyomo Wilayani. Hivyo Serikali hizo zikubali kuruhusu vikundi hivyo kushiriki katika kutoa maamuzi ya jinsi gani fedha zinazoongezeka Wilayani zitatumika. Bila kuwa macho na kuhimiza ushiriki wa vikundi hivyo, basi utekelezaji utafanyika bila watu, na hii itaendeleza yale yale ya kuleta mambo toka juu bila ushiriki wa kweli wa watu. Na katika hali hiyo ni wazi watakaonufaika ni wale tu ambao wako karibu sana na mamlaka zenye kufanya maamuzi. Wale walio mbali pengine kijiografia kwa maana ya pembezoni, kisiasa au kielimu watanufaika kidogo sana. Hapa ni wazi watakaonufaika ni wachache, na hivyo tofauti za hali ya maisha itaendelea kukua.

Pamoja na hayo yote hatuwezi kubweteka na kukubali kuwa hilo liwe ndilo neno la mwisho. Huko ni kukata tamaa na hatuwezi kukubali Urekebishaji wa mfumo wa kijamii bado ni jambo linalowezekana. Uwezekano mmojawapo ni kuona na kutumia vikundi vile ambavyo vinaweza kujiunga na kuchukua jukumu la kushinikiza kikamilifu. Njia mojawapo ni kuvifanya vikundi vya kidini nchini viwe macho kujua nini kinaendelea na pia viweze kuwa tayari kuwajibika kijamii na hivyo vitaweza kuwatia moyo watu katika jumuiya zao ili washiriki kikamilifu katika mambo ya kijamii yanayotakiwa kufanyika katika Serikali za Mitaa.

Jambo lingine katika mpango wa uboreshaji linalopaswa kuangaliwa ni mfumo wa utekelezaji shirikishi. Kwa sasa watendaji waliopo katika ngazi za Wilaya hawajaandaliwa vya kutosha kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unashirikisha watu kikamilifu.

Itaendelea Toleo lijalo

haki za raia Kitabu cha Tatu

Sheria ya Ardhi Tanzania (10)

UHAMISHO WA HAKI MILIKI

Sheria ya ardhi imeweka taratibu za namna ya kufanya uhamisho wa haki miliki toka mmiliki mmoja kwenda mmiliki mwingine ambapo uhamisho huo unapaswa upate kibali cha kamishna au afisa mteule. Utaratibu huu umewekwa ili kuhakikisha kwenye uhamisho kama vile kuuza, kuweka rehani au kupangisha sheria ya ardhi na nyinginezo husika zinazingatiwa.

Masuala ya kuzingatiwa ni;

a) Taratibu za uendelezaji

b) Kuepuka ulanguzi wa ardhi

c) Fursa ya kupata ardhi kwa wageni kwa kadri ya sheria ya ardhi na ile ya uwekezaji.

d) Kuzingatia masilahi ya makundi maalum ya watu wenye uwezo na kipato kidogo.

e) Kuzuia kujilimbikizia ardhi bila kuitumia kimaendelezo.

f) Kodi ya serikali inalipwa kwa mujibu wa sheria.

g) Mabadiliko ya miliki kuwekwa kwenye kumbukumbu za ardhi ikiwemo ile hatua ya kusajiliwa.

Mbali na maelezo ya jumla ya hapo juu tuangalie kwa undani kidogo juu ya kuuzwa na kukodishwa kwa haki miliki.

Mmilikaji ndiye anayetakiwa kuomba kibali cha kuuza miliki yake kwa kamishna wa ardhi. Endapo atakuwa ameomba kibali hicho na kibali kikatolewa na taratibu zote kufuatwa makubaliano mengine tofauti yataangaliwa na mahakama, kama kutakuwa na matatizo yatakayojitokeza.

7. 1. Mauziano ya haki Miliki ya Ardhi

Pale ambapo masharti yanayoambatana na miliki yametekelezwa na kama kamishna hatakuwa na kipingamizi kingine basi haki miliki inaweza kuuzwa baada ya kamishna kutoa kibali ambacho huombwa na mmiliki.

Kwa vile kuuza haki miliki ni mambo yanayohusu mkataba,

atashindwa masharti ya ikiwa mmojawapo wa wahusika kutimiza mkataba, wanaweza kutafuta njia ya ufumbuzi ikiwa ni pamoia na kwenda mahakamani.

7.2. Upangishaji wa Haki Miliki ya Ardhi

Sheria inatoa mwanya kwa mtu mwenye haki miliki kupangisha miliki yote au sehemu ya miliki ya ardhi kwa muda maalum ambao ni chini ya muda utioelezwa kwenye hati ya haki miliki. Kwa mfano mwenye haki miliki anamiliki ardhi kwa miaka tisini na tisa, huyu anaweza kupangisha shamba/kiwanja kwa muda wa miaka sitini. Makubaliano ya upangishaji yanaweza kufanyika kwa maandishi ama bila maandishi. Maelezo haya hayahusu Miliki za kimila ingawaje sheria ya ardhi ya vijiji inatoa mwanya kwa mwanakijiji kutoa kibali, ardhi yake itumike ama kupangishwa alimradi apate kibali cha serikali ya kijiji na kwa kuzingatia sheria za kimila za eneo ardhi husika ilipo.

Kwa kuwa upangishaji ni mkataba, mpangishaji hatamwingilia mpangaji kwa nia ya kumnyang’anya au nia nyingine bila sababu za msingi.

Ili kulinda masharti ya upangishaji ambapo upangishaji ni wa msimu mmoja chini ya upangishaji uliosajiliwa chini ya usajili wa haki miliki, sheria inaelekeza kuwa upangishaji huo usajiliwe pia.

Katika upangishaji wa ardhi ya serikali sheria inatoa nafasi kwa mpangishaji kupangisha kwa siku za mbeleni. Kwa mfano mtu anaelewa atakuwa na upangishaji hapo mbeleni tuseme miaka mitatu ijayo.

Huyu anaweza akapangisha na kuingia mkataba wa upanishaji wa mbeleni.

Yawezekana muda wa upangishaji ukaisha na mpangaji akaendelea kubakia, katika hali hiyo mpangaji ataendelea kuwajibika na mkataba. Lakini pia ieleweke kuwa kupokea kodi pekee hakumfanyi mpangaji kuendelea kubakia kwenye eneo hilo.

Vivyo hivyo sheria inabainisha kuwa iwapo mpangishaji atakayeendelea kupokea kodi kwa muda wa miaka miwili mfululuzo, upangishaji utaendelea kuwa halali na kuchukuliwa kama upangaji wa mwezi hadi wezi.

Mpangaji anaweza kuiwka reheani ardhi ama kuipangisha baada tu ya kupata kiali cha mpangishaji kwa maandishi ambacho kinashuhudiwa na msajili.

Baada ya maelekezo hapo juu ni vema pia kuangalia masharti ya upangishaji kama yalivyoelekezwa katika sheria.

Masharti ya upangishaji:

a) Mpangaji anayohaki kutumia ardhi aliyopangishwa bila usumbufu toka kwa mpangishaji au mtu yeyote alimradi anatimiza masharti ya mkataba wa upangishaji.

b) Mpangaji atawajibika kutumia ardhi hiyo kama ilivyoelekezwa kwenye hati ya haki miliki bila kufanya uharibifu wowote katika nyumba ama ardhi hiyo ikiwa ni pamoja na kuitunza nyumba ama ardhi katika mazingira yanayofaa kukalika kwa muda wote wa upangishaji.

c) Endapo ardhi au nyumba vitaharibiwa na moto, mafuriko, mlipuko radi au tetemeko la ardhi ama madhara mengine ya aina hiyo kwa kiasi kisichofaa kutumika mpangaji hatalipa kodi mpaka hapo uharibifu uliotokea utakapokuwa umefanyiwa ukarabati.

Kama katika kipindi cha miezi sita ardhi haitaweza kurekebishika kwa matumizi, mapangishaji anaweza kutoa ilani ya mwezi mmoja kusitisha upangishaji.

Ieleweke wazi katika upangishaji ni wajibu wa mpangishaji kulipa kodi ya majengo (inayolipwa na serikali ya mitaa) na kodi nyingine husika zinazodaiwa na zitakazotakiwa kulipwa kisheria.

Kwa upande mwingine mpangishaji anaweza kufanya ukaguzi katika nyumba au shamba lake katika nyakati zinazofaa alimradi asimwingilie mpangishaji na kama itaonekana mpangaji anakiuka masharti, mpangishaji anaweza kutoa ilani ya kusitisha mkataba wa upangishaji.

Katika upangishaji, mpangaji atalipa kodi na kutumia ardhi kwa namna walivyokubaliana, sheria inavyotaka na Jamii miliki inavyoeleza.

Sheria inaweka bayana kuwa mwisho wa upangaji mpangaji hatapaswa kulipa gharama za uharibifu zilizotokana na moto, mafuriko na mambo kama hayo yaani uharilbifu unaotokana na majanga.

Ni wajibu pia wa mpangaji kufanya matengenezo ya nyumba kwa maelekezo ya mpangishaji. Vilevile katika kuweka rehani nyumba husika au kuweka mpangaji mwingine kibali cha mpangishaji kinahitajika na kibali cha mpangishaji hakipaswi kuzuiwa bila sababu za msingi.

Maelezo yaliyotolewa hapo juu yanaweza kutumika katika upangishaji wa haki miliki za kimila. Kwa vyovyote vile upangishwaji huu utapaswa kusajiliwa na msajili wa hati. Hata hivyo usajili huu hautahusu upangishaji ambao si lazima kusajiliwa kama ilivyoelekezwa na sheria.

Kuvunjika kwa mkataba wa upangishaji.

Yawezekana ukafika muda, mmoja wa wahusika katika mkataba akashindwa kutimiza wajibu wake. Katika hali hiyo sheria imeweka taratibu kusaidia mhusika kupata haki yake halali kisheria kwa jinsi hiyo basi, sheria inasema sio halali kwa mpangishaji kusitisha upangaji kwa kumwondoa mpangaji. Lakini hata hivyo mpangishaji anaweza kusitisha upangishaji kama mpangaji atashindwa kulipa kodi au kukiuka sharti lolote lililoelekezwa kwenye sheria.

Vile vile mpangishaji hatatakiwa kumwondoa mpangaji au kushikilia vitu vyake kwa nia ya kumshinikiza aondoke ama atimize masharti aliyokiuka, bali anachoweza kufanya ni kupeleka suala hilo mahakamani, kama inavyoelekezwa na sheria.

Pale ambapo mpangaji anashindwa kulipa kodi au anakiuka masharti mengine mpangishaji atasitisha mkataba na kupeleka shauri hilo mahakamani.

Na wakati wa kutoa maamuzi kuhusu upangaji wa nyumba za kuishi, mahakama itazingatia maelekezo ya upangaji wa nyumba kisheria; pili uzito wa ukiukaji wa upangishaji, mantiki ya adhabu ambayo ingeweza kutolewa ikitiliwa maanani umri wa jengo, mahali lilipo na hali yake. Pia kiasi cha fidia inayodaiwa na mpangaji inayotokana na mpangishaji kutozingatia masharti ya mkataba, kiasi cha uvumilivu ulioonyeshwa na mpangishaji kuanzia wakati mpangaji alipoanza kuvunja masharti ya mkataba.

Umri, afya na njia ya kumpatia riziki mpangishaji pamoja na wategemezi wake vitaangaliwa pia. Kwa mfano iwapo itaonekana mpangaji:

i) Hatapata mahala pengine pa kuishi.

ii) Hatakuwa na njia nyingine ya kujikimu yeye na wategemezi wake au

iii) Mwenzi au wenzi wa ndoa wa mpangaji watateseka kwa namna fulani kutokana na hatua hiyo kuchukuliwa.

Vinginevyo mahakama inaweza kuangalia kama uamuzi tofauti unaweza kufanyika. Mahakama pia itaangalia matakwa ya watu wengine nje ya mpangaji na wategemezi wake, au vinginevyo kwa kadri mahtikama itakavyoona inafaa.

Wakati wa kutoa ilani ya kusitisha mkataba wa upangishaji, mambo haya lazima yazingatiwe:

a) Kama mpangaji amelimbikiza kodi kwa muda usiopungua siku thelathini.

b) Endapo mpangishaji atatoa ilani ya usitishaji wa upangaji, sheria inamtaka wakati huo huo ama mapema iwezekanavyo kutoa nakala ya usitishwaji huo kwa wote waliopangishwa na mpangishaji, mwenzi ama wenzi wa ndoa wa mpangaji, mtu yeyote aliyehusisha na nyumba hiyo katika mambo ya rehani na iwapo mpangaji amefilisika nakala ipelekwe kwa mdhamini wa mpangaji aliyefilisika.

Kwa vyovyote vile utoaji wa ilani ya kusitisha upangishaji utatolewa kwa fomu maalum zitakazotayarishwa na Waziri husika, vinginevyo ilani hiyo itakuwa batili.

Iwapo mpangishaji anataka kusitisha upangishaji atapaswa kupeleka maombi yake katika mahakama ya wilaya kwani hilo sio suala la kujiamulia tu.

Mbali na maelezo ya hapo juu iwapo mpangaji amekiuka masharti ya upangishaji, mpangishaji badala ya kutoa ilani ya kusitisha upangishaji, anaweza kupeleka shauri hili mahakamani. Vivyo hivyo mpangaji anaweza akafungua mashtaka dhidi ya mpangishaji akidai kuwa kwa mfano amekiuka masharti ya upangishaji.

Iwapo mpangishaji atashindwa kutekeleza wajibu wake kadri inavyoelekezwa na sheria mpangaji anaweza kutoa ilani kwa mpangishaji akieleza kuwa kwa mfano gharama alizoingia kwa matengenezo, itapunguza kodi ambayo angelipa.

Hivyo hivyo endapo mpangishaji amekiuka masharti kama inavyoelekezwa na sheria mpangaji anaweza kupunguza kiasi cha kodi kinachodaiwa katika matipo ya kodi mfano ya kilemba.

Mwisho mpangaji anaweza akasitisha upangishaji iwapo itaonekana mpangishaji hana kusudio la kuendelea na mkataba huo.

Mpangaji pia anaweza kudai fidia inayotokana na uharibifu, usumbufu na hasara zilizosababishwa na uzembe wa mpangishaji katika kutekeleza majukumu yake kimkataba.

Iwapo mpangaji ataondolewa kwenye nyumba au ardhi bila kufuata taratibu zilizoelekezwa katika sheria hii hatapaswa kulipa kodi ama kuwajibika kwa vyovyote vile katika mkataba wa upangishaji kwa kadri walivyokuwa wamekubaliana.

7.3. Kuweka Rehani haki miliki.

Bwana Alhaji ana wake watatu na kila mke anaishi katika nyumba yake. Katika mipango ya maendeleo anayopanga bwana Alhaji humshirikisha mke wake wa tatu tu. Waliamua kuomba mkopo benki ili waweze kufanya biashara walizokuwa ya upanuzi wanaendesha.

Mkopo ukakubaliwa na nyumba anayoishi mke mkubwa ndiyo ikawekwa reheni, bila hata yeye mwenyewe kuwa na taarifa yoyote.

Kwa bahati mbaya biashara hazikwenda kama walivyotarajia na wakashindwa kulipa mkopo. Kilichofuata ni nyumba iliyokuwa imewekwa rehani kuchukuliwa kwa amri ya mahakama. Jambo hili lilimshtua sana mama huyo (mke mkubwa na watoto wake) kwani hakuwa na mahala pengine pa kuishi na wala mumewe hakumjali.

Maana ya Rehani

Rehani ni pale ambapo mmiliki wa mali anaiweka mali yake kama atashindwa mali hiyo itachukuliwa na mkopeshaji; kama malipo ya mkopo na riba itokanayo na ukopaji. Yawezekana kuweka hati ya haki miliki rehani alimradi maelekezo ya sheria zote husika vimezingatiwa hasa kwa kuwa kisheria ardhi ina thamani.

Sheria ya ardhi nchini inagawa rehani katika mafungu mawili yaani rehani kubwa na rehani ndogo. Itaendelea Toleo lijalo

CHILIGATI: Enzi za magari mabovu zinamalizika

l‘Dereva asiyejua kanuni ni muuaji’

Na Josephs Sabinus

"UDEREVA ni sawa na taaluma ya Udaktari ambayo ni lazima uwe na ujuzi ndipo ukatibu watu, maana daktari asipokuwa na taaluma ya Udaktari, ni sawa na kumwomba aende akaue. Udereva vile vile ni taaluma inayofanana na udaktari; ukimpa dereva asiyejua kanuni, alama, michoro na sheria za usalama barabarani ni sawa na kumwambia aende akaue."

"Mifano hai inaonekana hata pale ambapo madereva wanawapigia honi watembea kwa miguu mahali paliporuhusiwa kisheria waenda miguu wapite; kuovateki, kuegesha, kupakia au kuteremsha abiria sehemu zisizoruhusiwa.

Hii ni mifano michache inayoonesha jinsi madereva wengi wasivyojua sheria na hawajapitia mafunzo ya taaluma hiyo."

Wakati wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) wameyasema hayo katika risala yao katika mahafali ya hivi karibuni, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Kapteni John Chiligati, aliyekuwa mgeni rasmi, anasema,

"Ajali za barabarani ni aina ya UKIMWI unaoua Watanzania wengi na kuharibu mali zenye thamani ya mabilioni kila mwaka..."

Ni dhahiri kwa sasa ajali zimekuwa tatizo kubwa nchini Tanzania na hususan katika jiji la Dar es salaam ambako idadi ya magari inaongezeka kila kunavyokucha.

Ni ukweli ulio bayana kuwa ajali hizo zinapotokea, huzua madhara makubwa ikiwa ni pamoja na vifo, majeruhi, upotevu na hasara za mamilioni ya fedha za abiria, wamiliki wa magari na jamii kwa jumla.

Hali hiyo husababisha matatizo kwa familia zinazoguswa na taifa kwa jumla kwa kuwa hupoteza watu na mali zinazotegemewa katika kuleta maendeleo ya jamii.

Kwa kiasi kikubwa, ajali zinazotokea, hazitokei kwa sababu tu ya bahati mbaya bali kutokana na uzembe hasa kwa kutozingatia sheria na kanuni za usalama barabarani.

Yapo matatizo mengi yanayosababisha hali hii. Hayo ni pamoja na ulevi wa madereva na wamiliki wengi wa magari kujenga tabia ya kutojali kuchukua tahadhari na tamaa ya pesa kwa kukimbilia abiria bila kujali usalama.

Ipo mifano mingi tu, ya sababu za vyanzo vya ajali nchini ikiwamo ya mwendo mkali na ukosefu wa nidhamu na utii hata kwa taa za kuongozea magari. Kwa sasa, si ajabu kuona gari linapita katika taa wakati zinazowaka haziruhusu gari kupita.

Kwa magari ya abiria, sasa karibu ni jambo linaloelekea kuzoeleka kuwa dereva ana uhuru wa kumfundisha utingo wake namna ya kuendesha gari huku akiwa na abiria; Mungu wangu hivyo vyuo vinavyotembea barabarani na kuangamiza roho za watu, kwanini lakini?

Hayo yanaungana na kauli ya Waziri Chiligati ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kuwa, udereva hauna budi kupewa sura mpya tofauti na ilivyokuwa katika siku za nyuma ambapo kila aliyeweza kushika usukani gari likaondoka, aliitwa dereva.

Mkuu wa Chuo cha Usafishaji cha Taifa, Saad Fungafunga, alisema endapo madereva hata wale wa viongozi hawatapewa mafunzo maalumu ya kazi yao, ipo hatari wakawasababishia ajali viongozi. "Madereva wa viongozi wasiposoma, watawaua viongozi wetu," alisema.

Alishauri Serikali itafute uwezekano wa kufuatilia kubaini kama magari ya makampuni yanadumu kwa wakati muafaka.

"Magari ya makampuni yanakufa kabla ya wakati kwa kuwa hakuna wataalamu wanaoyaendesha. Ni vema kila kampuni ikawa na msimamizi kamili maana hali hiyo itasaidia kupunguza ajali. Ni rahisi kumbana mtu anayezembea. Watu hao waje NIT wapate mafunzo kamili," alisema Fungafunga.

Akijibu hoja hiyo, Kapteni Chiligati alisema, "Serikali imekwishaamua kuwa madereva wa mabasi ya abiria lazima wasomee fani ya udereva," akaongeza, "Tumetoa muda wa mwaka mmoja wenye mabasi wawasomeshe madereva wao. Baada ya kipindi hicho, dereva asiyosomea udereva na kupata cheti kutoka chuo cha udereva kinachotambulika na Serikali, hawezi kuendesha basi.

Napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa madereva wa mabasi wasome sasa vinginevyo, ikifikia Julai 2002, wajihesabu hawana kazi...muda si mrefu ujao kila dereva wa kiongozi atatakiwa awe amepitia hapa chuoni (NIT) na kufaulu."

Naye Mkuu wa Idara ya Usalama Barabarani chuoni hapo, R.M. Sawaka, alisema madereva wengi hawajui alama za barabarani hali ambayo ni hatari kwani inachangia ongezeko la ajali.

Sawaka alisema kuwa, ili kuondoa tatizo hilo, madereva wapate mafunzo chuoni hapo.

Pamoja na mambo mengine, NIT hufundisha udereva wa kujihami, ufundi wa magari, alama za barabarani na sheria za usalama barabarani.

Kapteni Chiligati anasema kuwa, kwa mujibu wa takwimu za miaka mitano iliyopita, yaani 1996 hadi 2000, watu 8366 wamekwishafariki dunia katika ajali 68, 645.

Hiki ni kiasi kikubwa cha vifo ambacho hakipaswi kuachwa kuendelea kwani ni hasara kubwa kwa taifa na familia.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa, kwa kila saa 10, wastani wa watu wawili wanafariki nchini kwa ajali kila siku. Asilimia 76 ya ajali za barabarani, zinatokana na uzembe wa watumiaji wa barabara ama madereva au waenda kwa miguu.

"...madereva lazima wawe makini zaidi kwa kuwa lawama zinawaendea madereva wanaoendesha bila kutii alama za barabarani au wakiwa walevi au wakiwa na magari mabovu," anasema Chiligati.

Ikumbukwe kuwa, Mkutano Mkuu wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani uliofanyika mkoani Mwanza mwezi Septemba mwaka huu, uliagiza kuwa Kamati za Usalama Barabarani za Mikoa na Wilaya nchini kote, ziunde mpango maalumu wa kutoa elimu kwa umma juu ya sheria za barabarani.

Kapteni Chiligati juu ya hili, anasema, "Napenda kutumia fursa hii kuzikumbusha Kamati hizo zifanye kazi hii kwa makini. Waathirika wakubwa wa ajali za barabarani ni waenda kwa miguu na wapanda baiskeli kwa wastani wa asilimia 80 ya vifo. Hali hii inatokana na kutokujua sheria za usalama barabarani."

Muuza mayai mmoja mkazi wa Ukonga jijini Dar es Salaam, aliyejitambulisha kwa jina la Wambura Matura, anasema waenda kwa miguu na wapanda baiskeli wana mchango mkubwa katika ongezeko la ajali kwa kuwa nao hawafuati kanuni za usalama barabarani ama kwa uzembe, au kwa kutozijua.

Dereva mmoja wa daladala aina ya Hiace aliyeomba jina wala namba za gari lake linalofanya safari zake kati ya Posta na Masaki jijini Dar es Salaam zisitajwe gazetini, alikuwa na haya, "Ajali zinaongezeka kwa kuwa idadi ya magari jijini inaongezeka wakati barabara ziko palepale haziongzeki. Sasa msululu unakuwa mrefu. Madereva wengine tunaamua kukatiza na kuchomekea ndiyo maana ajali nyingine zinatokea."

Anakiri kuwa madereva wengi wa magari ya abiria ni wale waliojifunzia kwenye miembe wakajua kuliondoa gari na akadokeza kwamba bila kubanwa, wengi hawana mpango wa kujipatia mafunzo maalumu ili wajue kanuni muhimu za usalama barabarani.

Hata hivyo, anasema madereva wengine wanajiona miungu barabarani na hivyo wanawadharau na kuwapuuza waenda kwa miguu na wapanda baiskeli. Anasema, hicho pia ni chanzo kingine cha ajali.

Chiligati anasema mafunzo yanayotolewa NIT yanalenga kuwapa madereva mbinu ili wawe makini zaidi katika kuepusha ajali za barabarani na kwamba ndiyo maana sasa Serikali haitoi leseni kwa dereva yeyote hadi awe amepata mafunzo katika chuo kinachotambuliwa na Serikali na amefaulu.

Chanzo kingine cha ajali za barabarani ambacho kinabeba aslimia 16, ni uendeshaji wa magari mabovu. Inashangaza kuona wenye magari wengi hawapeleki magari yao kukaguliwa.

"Kwa mfano, jiji la Dar es Salaam, linakadiriwa kuwa na magari 300,000 lakini, yanayokaguliwa kwa mwaka ni 12, 000 tu, sawa na aslimia 4."

Kapteni Chiligati alisema licha ya kuwapo kwa sababu nyingi za hali hiyo, Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, zinaandaa utaratibu wa kuanzisha vituo vya ukaguzi wa magari kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Anasema vituo hivi vitakuwa na wataalamu wa kutosha na zana zinazotumia teknolojia ya kisasa (kompyuta) katika kufanya ukaguzi wa magari.

"Kila mwenye gari atatakiwa kupeleka gari lake kukaguliwa walau mara moja kwa mwaka ambapo likiwa zima litabandikwa stika kwa ajili ya polisi kulitambua kuwa limekaguliwa. Hivyo, enzi za kuonekana barabarani magari mabovu yenye kusababisha ajali zinakaribia kumalizika.

Akijibu risala ya wahitimu kuwa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani wanadai na kupokea rushwa kwa wenye magari na hivyo kuchangia ajali, Kapteni Chiligati, alisema madereva na wamiliki wa magari wao pia wamekuwa kichocheo cha rushwa kwa kuwa wanakiuka kanuni za usalama barabarani na hivyo, kutumia rushwa kuwabembeleza Polisi wasiwafikishe mbele ya sheria wanapowakamata.

Alisema hali hiyo imesababisha rushwa kuota mizizi kwamba, sasa wakati wa huruma umekwisha umebaki wa utekelezaji. Aliwataka madereva kuwa mstari wa mbele kufuata kanuni za usalama barabarani na kwamba kama hawako tayari kuzifuata, basi wawe tayari kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

"... Wenye magari na madereva watusaidie kutoa taarifa kuhusu askari trafiki wanaobugudhi kwa kuwadai rushwa barabarani. Pigeni simu za polisi ambazo huhitaji kutaja jina lako ukiarifu nani, mahali gani na saa ngapi amedai rushwa. Kila taarifa inayomgusa askari mmoja, hiyo ni kura inayotosha kutufanya tumvue magwanda na kumuondoa kazini," alisema na kuongeza,

"Serikali haitasita kumtimua na haitamuonea huruma askari atakayebainika kuomba au kupokea rushwa kwa wamiliki au madereva wa magari."

Katika hali ya kutia matumaini, mmoja wa viongozi wa NIT, Henry Bantu, alisema kwa wakati tofauti kuwa Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani, ACP Leonard Mashaka, ni mchapakazi aliye makini na kwamba ana uhakika akibainika askari yeyote anayekwenda kinyume, atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Awali katika risala yao, wahitimu hao waliiomba Serikali kuweka mpango utakaowawezesha walimu wa vyuo vya mafunzo ya udereva, kupatiwa mafunzo katika chuo hicho na hata wanafunzi wa vyuo hivyo, wapite NIT kuhakikiwa.

Wakaiomba Serikali kukipatia Chuo hicho (NIT) vifaa na zana mbalimbali za kutolea mafunzo hususan magari ili kitoe elimu bora zaidi.

Umefika wakati ambao kila mmoja kwa nafasi yake, anapaswa kujua kuwa ajali zinaua. Apambane nazo. Waenda miguu na wapanda baiskeli wawe makini zaidi kuzingatia kanuni za usalama barabarani.

Ni wajibu wa kila mmoja kuziunga mkono juhudi za Jeshi la Polisi, NIT, VETA na asasi zote zinapambana na ajali za namna hiyo kwani zina madhara makubwa kwa maendeleo ya taifa.

Madereva wasitumie fimbo ya rushwa kuendeleza uzembe unaoliangamiza taifa.

Jeshi la Polisi likaze uzi kuwabana madereva wazembe na askari wanaopokea rushwa na kuruhusu roho za Watanzania kuangamia.

Vyuo vya mafunzo ya udereva katika ngazi mbalimbali kwa kupitia VETA na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), vipo kwa mafunzo mbalimbali ili kuwanufaisha Watanzania; ni vema kuvitumia kwa manufaa ya taifa zima.

Ni dhahiri endapo wadau wote wa sekta ya usarishaji na uchukuzi wataivalia njuga vita dhidi ya ajali za barabarani, zitapungua wa kiasi kikubwa kama sio kuisha kabisa. Ni vema sheria zifanye kazi.

Riwaya

Mkabala wa Kitanzi (10)

Na Emmanuel Boniface

Zitto alimuacha Rozi kwa Dokta Madevu ili asaidiwe kutoa mimba. Anaporudi kupata majibu ya kinachoendelea, anamkuta Dokta katika hali ya hofu kama kuku anayetaka kutaga mayai, macho yamemuiva; kwanini, Endelea.

Kwa kiwango kikubwa, nilifanikiwa kujenga dunia yangu mbali na ile ya wanawake.

Nikakosa kabisa muda wa kuwaza juu ya wanawake. Sasa nikajiona niko salama na huru. Nikajawa imani na shukrani kwa rafiki yangu Kidevu.

Nilimshukuru nikijua kuwa kama asingekuwa yeye, busara na ushauri wake, sijui maisha yangu yangekuwaje. Ama kweli Malaika wa Mungu ni watu wema wanaokuzunguka!

Kwa muda nilikuwa nimepata mafanikio makubwa nilikuwa na gari mbili za kutembelea Nissan Patrol na Toyota Land Cruser’ pia nilikuwa na malori mawili ya mazigo basi moja la abiria Toyota Pick Up moja gesti tatu na jengo kubwa la kufanyia biashara zangu; nyumba yangu ya kuishi ilikuwa kubwa nzuri na ya kisasa iliyozungushwa ukuta na nyaya za moto (umeme) kwa ajili ya usalama iliyojengwa sehemu za ‘uzunguni’ makazi ya watu matajiri kwa mji mdogo kama ule wa Musoma kwa mtaji huo mimi naye nilikuwa miongoni mwa matajiri wakubwa pale mjini na viunga vyake.

Na tayari nilikuwa nimeomba mkopo wa shilingi milioni mia tatu toka benki ya CRDB LTD kwa ajili ya kujenga kituo cha mafuta maeneo ya Bweri. Na kutokana na mali nilizokuwa nazo maombi yangu yalikubaliwa mara moja.

Ni hapo tena nguvu za maumbile zilipoanza kunisumbua; nilianza kupata mawazo kuwa nilikuwa naanza kuzeeka na kuhisi pamoja na mafanikio yangu ya kibiashara kuna kitu nilikuwa nakikosa. Kila nilipotoka kazini na kuingia katika nyumba yangu kubwa nilihisi ukimya umetawala na upweke na utupu vimetamalaki, nilikosa raha na amani kwa ukimya utu na upweke ulionizunguka nyumba ilionekana kupwaya na yenye kuchosha nikahisi uchovu na ganzi katika maungo na hisia. Kila asubuhi nikaona uvivu na hamasa ya kuamka mapema, maumivu ya shingo na mgongo yakawa ni tatizo kila asubuhi, nikadhani labda ni ugonjwa lakini nilipoenda hospitali na kupimwa nikaambiwa sina tatizo. Hata hivyo nikapewa vidonge na dawa za kupaka. Daktari yule aliyenihudumia akaniambia eti ni ‘stress’ na kunishauri nipunguze mawazo na kufanya mazoezi kiasi ya kuchangamsha viungo lakini ni mawazo gani hayo yaliyokuwa yananisumbua hadi kunisababishia ‘stress’ sikuelewa.

Kitu kingine, nikajikuta navutiwa na kuwapenda sana watoto; nikaanza kuwa nawanunulia watoto wa majirani zawadi na aghali kila sikuna nikahisi raha na fahari kila siku waliponikimbilia wakanisalimia kunishika na kunikumbatia wakiniuliza kama nimewaletea zawadi; nikajihisi vizuri nipowabusu na kuwapapasa nywele zao wakanizoea sana wakawa wanajazana kwangu na kuniomba niwawekee mkanda waangalie video; nami nikawa nawanunulia mikanda ya katunu na ile ya vita wakaangalia na kufurahia sana lakini kila walipoondoka na kurejea makwao nijihisi mkiwa na mwenye kupungukiwa ilikuwa ni kama walikuwa wanaondoka na sehemu ya moyo wangu. Nilitamani muda wote wawe wanakuwa pamoja nami.

Na nilipoenda kwa rafiki zangu kuwatembelea na hawa nilikuwa nao wengi nikawakuta wanacheza na wanacheka kufurahi pamoja na watoto wao wivu usiozoeleka ulinitekenya nikatamani mimi ndio ningekuwa kwenye nafasi zao.

Jumapili niliona wamebeba watoto wao vifuani wengine wameshikana na wake zao wakienda na kutoka kanisani nikajawa hamu sana kuwa kama wao.

Nikiwa peke yangu nikaanza kukumbuka nyuma na kuwazia kuwa pengine Massa asingenikatili nami ningekuwa na furaha kama wao pia nikaanza kwenda kwenye hoteli kubwa hususani Orange Tree Hoteli kujiburudisha mara moja moja kwa muziki na bia.

Ari na ufanisi wangu katika kazi ukapungua marafiki na watu wa karibu wakaanza kuniuliza kama nilikuwa na tatizo bahati mbaya hata kama nilikuwa nalo nilikuwa silijui na nilipowaambia sina tatizo walionekana kutia shaka kuna shetani mbaya alikuwa ananitafuna bila mimi kujielewa.

Siku moja nilikuwa Orange Tree Hoteli nikinywa bia huku bendi maafuru ya Victoria Stars wanalingalonga ikitumbuiza kwa muziki maridadi na wacheza ‘shoo’ mahiri ilikuwa ni burudani nzuri mara nilinusa harufu nzuri ya manukato nikageuka kumwangalia huyo aliyejipulizia manukato hayo yenye harufu tamu hivyo. Nilipomuana moyo ulinipiga paa! Nikabaki nimeduwaa namwagalia na kustajabia uzuru wake; mapigo yangu ya moyo yalikuwa yanaenda kasi na akili yangu imetatizwa alipita karibu kabisa na mimi akaniagalia kwa macho yake makubwa malegevu yaliyopakwa wanja akatabasamu kwa aibu kidogo baada ya kuona ninavyomkodolea macho na kubung’aa, akishakunipita niligeuza shingo nikaendelea kumtazama.

Alikuwa amejazia sawasawa kwa nyuma na miguu yake ilikuwa ni ile iliyonona na mizuri, umbile lake lilikuwa lenye kupendeza na mwendo wa madaha na wa kujiamini. Ngozi yake ilikuwa laini nyeusi inayong’aa ikidhihirisha ule msemo kuwa black is beuty. Ni dhahiri ngozi yake ilikuwa haijaguswa na mkorogo.

Nywele zake zilikuwa fupi na nyeusi tii zenye uasili wake wote zinang’aa kwa mafuta na zimechanwa vizuri.

Hata alipopata uzuru wake bila kukinai yey mwenyewe alinekana ametulia na hana habari kama kuna mtu alikuwa anamtazama karibu na kummeza.

Nilioa anapewa kinywaji aina ya Ndovu lager akawa anakunywa taratibu kama vile hana haraka.

Nikajikuta nawaza kwamba litakuwa jambo zru sana kama ningemuoa msichana yule nikazaa naye watoto na kufanya familia. Baada ya kuwaza hivyo nikajawa tamaa zaidi na faraja nikajihisi mwepesi na kikahisi furaha inaninyemelea mara nikabaini kitu nilichokuwa nikikosa na kunikosesha raha nilikuwa nahitaji mke na mke wa kunuzalia watoto. Na yule niliyekuwa namwangalia alikuwa ni mzuri sijapata kuona nilipomkumbuka Massa na kumlinganisha na yuleMassa alionekana kama makapi, nilijiuliza ni kitu gani kilikuwa kinanizuzua kwa Massa nisipate jibu nikakubali kwamba rafiki yangu kidevu hakukosea pale aliponiambia kuwa nitakuja kupata msichana mzuri kuliko Massa na sasa huyo msichana alikuwa mbele yangu akinywa bia ya Ndovu lager peke yake hana mtu. Niliamka na kuendea meza aliyokuwa amekaa.

‘Samahani dada, hujambo’ nilimsabahi

‘sijambo!’ huku akitabasamu ‘unono’

‘samahi naweza kukaa hapa’

‘Bila samahani’ tabasamu lake halibanduki

nikashakukaa nikamuuliza ‘vipi uko peke yake au unamtu unamsubiri’.

‘Hata niko peke yangu kwani vipi!’

‘Basi nilitaka kujua nisije nikawa nimevamia shamba la watu’

‘Mh! Wala’

Mhudumu alipita nikamuagizia atuongezee vinywaji pamoja na sahani mbili za nyama choma

‘sijui unaitwa nani dada?’ nikamuuliza

‘Caroline!’

‘Haa jina tamu na zuri kama wewe mwenyewe’

‘Ha ha haa ! acha utani! Mimi naye mzuri’

‘He kumbu hujapata kubaini au kuambiwa basi nakwambia sijapata kuona msichana mzuri kama wewe!. Akatabasamu tu na kunywa bia kidogo halafu anakaniuliza ‘Ehe na wewe unaitwa nani’

‘Mimi naitwa Zito!’

‘Aah kumbe wewe ndio Zito!’ alishtuka

‘Haswa! Vipi unalisikia jinahilo?’

‘sana unaonekana wewe ni maarufu! Alionekana kuchangamka na kuvutiwa.

‘kwanini?

‘Mji huu mzima pengine ni mimi tu nilikuwa sikujui’

‘si kweli!’

‘najua hutakubali’

‘OK tuachane na hilo je wewe ni mwenyeji wa hapa Musoma?’

‘ndiyo! Siyo’

‘ kwa vipi’

‘ni kweli nilizaliwa hapa lakini sijakulia hapa’

‘ulikulia wapi’

‘Arusha’

‘Na hapa wazazi wako wanaishi wapi au wanaishi huko huko Arusha?’

‘Hawapo walikufa zamani sana’

‘ooh pole sana walikufa na nin’

‘na ajali ya basi’

‘kwa hiyo wewe ni yatima’

alitikisa kichwa huku akinyanyua bilauri na kugida bia zaidi.

‘ulikuwa na umri gani’

‘miaka miwili!’

‘sasa Arusha ulikuwa unaishi na nani?’

‘Mama mdogo’

‘na huku umekuja lini?’

‘kama miezi miwili iliyopita’

‘karibu sana’

‘Ahasante’

kikafuata kimya huku tukiendelea kunywa bia zetu halafu nikavuta pumzi na kumuuliza ‘Tafadhali Caroline naweza kukutolea dukuduku langu moyoni?’

alijivuta akakaa vizuri huku akitabasamu lile tabasamu lake zuri ‘endelea’ akaniruhusu huku akionyesha shauku ya kusikia.

‘kusema kweli mimi nimetokea kukupenda sana Mara tu nilipokuona unaingia nimejikuta navutiwa sana na wewe, unaonaje tukioana’

‘Hee! Mara hii tu mtu hata hunifahamu vizuri’

‘Nimekuona! Nakupenda unataka unifahamu vipi?’

‘Kwa hiyo unanifahamu’

‘Nakupenda hilo ndilo muhimu’

‘Mh sawa!

‘Kwa hiyo.....! unanipenda unakubali tuoane! Nilipaparika kwa maneno;

‘Ndiyo nimekubali Zito’

Moyo ukanipasuka na kushangilia kwa furaha.

Tukakaa tumetumbuliana macho yaliyolewa pombe na mahaba. Nikapeleka mikono nikaushika uso wake na kumvuta kwangu nyuso zetu zikakutana na ndimu zetu zikachezeana halafu tukaachana nakutumbuliana macho. Nikatabasamu na yeye alikuwa anatabasamu nikamshika mkono nikamnyanyua tukaenda kucheza muziki.

Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu, hatutaweza kuendelea na hadithi hii ya kusismua. Tunawaomba radhi wasomaji wetu kwa kuwakatiza uhondo huo.