Daktari wa Kiongozi/Makala

Magonjwa ya mara kwa mara (7)

Ugonjwa wa kuharisha ni wa hatari sana hasa kwa watoto wadogo sana. Kwa kawaida hakuna haja ya kutumia dawa, ila kuna muhimu wa kuwahifadhi vizuri kwa sababu wanaweza kufa kwa ukosefu wa maji mwilini.

• Endelea kumnyonyesha na kumpa maji ya dawa.

• Kama kuna tatizo la kutapika, mnyonyqshe mara kwa mara lakini kidogo kidogo kila baada ya dakika 5 au 10.

• Kama hakuna maziwa ya mama mpe maziwa ya aina nyingine kidogo kidogo ukiyachanganya nusu kwa nusu na maji yaliyochemshwa. Kama maziwa yanazidisha kuharisha mpe protini ya aina nyingine kama vile kuku, mayai, nyama au maharagwe yote yawe yamepondwa na kuchanganywa na asali.

Ikiwa mtoto ni mdogo zaidi chini ya mwezi mmoja jaribu kumpata bwana mganga kabla hujampa mtoto huyo dawa yeyote. Ikiwa hakuna mganga yeyote na mtoto anaumwa sana mpe kinywaji kitamu kizito cha watoto "infant syrup" ambacho kina ampicillini.

Nusu kijiko cha chai mara 4 kwa siku

Wakati wa Kutafuta msaada wa waganga kwa maradhi ya kuharisha

Ugonjwa wa kuharisha unaweza kuwa wa hatari sana hasa kwa watoto wachanga. Katika hali zifuatazo tafuta msaada wa mganga:

• Kama kuharisha kunaendelea zaidi ya siku 4 na haielekei kuwa kuna nafuu au zaidi ya siku moja kwa mtoto mdogo mwenye kuharisha sana.

• Kama mtu anaendelea kuwa na ukosefu wa maji mwilini.

• Kama mtoto anatapika chochote anachokula au kunywa.

• Kama mtoto anaanza kupata dogedoge au miguu na mikono inaanza kuvimba.

• Kama alikuwa mgonjwa sana, mdhaifu au alikuwa na utapiamlo kabla ya kuharisha (hasa kwa mtoto mdogo au mtu wa makamo).

• Kama kuna damu nyingi ndani ya choo ambayo ni dalili mbaya hata kama anaharisha kidogo tu tazama kuziba utumbo.

Mwisho

Kitabu cha Kiada kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo (28)

BAADA ya kumaliza mfululizo wa chapisho la kitabu kiitwacho HAKI ZA WAFUNGWA NA HALI YA MAGEREZA- TANZANIA BARA, kwa kuwa tumegundua kuwa kitabu hicho kimewanufaisha zaidi wasomaji wetu, kwa kuwafanya wajue mambo mengi juu yao ambayo awali hawakuwa wakiyafahamu kuwa ni wajibu na haki yao, kuyapata na kuyafanya, na kwa kuwa tunawajali wasomaji wetu, sasa tunazidi kuwafaidisha kwa kukidhi zaidi kiu yao. Tunaendelea na chapisho la kitabu kiitwacho KITABU CHA KIADA KWA MAHAKIMU WA MAHAKAMA ZA MWANZO ambacho tunaamini si tu kwamba kitawanufaisha mahakimu peke yao, bali pia jamii nzima ya Watanzania; nacho, tunakichapa kama kilivyotolewa na Tume ya Haki na Amani(TEC). Tulianza na dibaji iliyoandikwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Barnabas Samatta, ukafuatia utangulizi, sasa tunaendelea na Namba 3.6" Aina za Utoaji wa Adhabu..."

Hii ni hali ya hatari na kuna haja ya Serikali kuangalia vizuri sera yake ya magereza na kukumbuka kwamba wafungwa na wote walio mahabusu ni binadamu ambao wana utu wao na wanastahili kuishi mahali pazuri wakati wakitumikia adhabu zao au wakati wakisubiri kesi zao kusikilizwa.

Hii ni muhimu kusisitizwa kwa sababu kila mmoja kati yetu ana uwezekano wa siku moja kujikuta huko huko gerezani.

Imetokea katika nchi nyingi kwamba Rais au waziri wa leo ni mfungwa wa kesho na mfungwa wa leo kuwa Rais au waziri wa kesho.

Hivyo, siyo busara kupuuzia hali ya magereza yetu.

Tunasema hivi kwa sababu kwa sasa msongamano magerezani ni mkubwa sana.

Hali ni mbaya zaidi kwa magereza yaliyo katika sehemu za mjini kuliko yale ya vijijini.

Hapa chini tunatoa takwimu

Kiasi cha msongamano wa kuonyesha hali ilivyo mbaya.

Kiasi cha msongamano wa mahabusu/wafungwa katika baadhi ya magereza nchini Tanzania imefikia zaidi ya asili mia sita (600%).

 

 

Na Gereza Idadi ya Wafungwa ldadi ya Asilimia ya

Wanaotakiwa Wafungwa Msongamano

Kisheria Waliokuwamo

Kuwekwa Gerezani Ndani ya Gereza (%)

Kufuatana na Husika kurikia

Ukubwa na Gereza 1.4.1999

1 Kahama 70 424 606%

2. Ruanda 400 2,025 506%

3. Morogoro 90 380 422%

4. Keko 349 1154 339%

5. Bukoba 360 837 233%

Maisha ya mahabusulwafungwa gerezani siyo mazuri kwani malazi na mahitaji ya lazima ni shida sana kwao na hali inazidi kuwa mbaya kwani ongezeko la kila mwaka ni kubwa.

Huko gerezani kuna magonjwa mbalimbali mengi yakiwa yale ya kuambukiza mathalani kifua kikuu, upele, kuhara na hata ukimwi. Kuna ukosefu wa chakula na madawa na usalama wao kimaadili pia uko hatarini kwani askari hushindwa kuwadhibiti kutokana na idadi ya wafungwa kuwa kubwa sana. Mahakimu wengi wanafahamu haya kupitia ziara zao magerezani kwani ni wajibu wao kuwatembelea wafungwa/mahabusu huko gerezani mara kwa mara na kukagua hali zao.

Hii inabidi iwe changamoto kwa mahakama kuwa makini na isimnyime mshitakiwa dhamana bila sababu za msingi, na isimpe mshitakiwa kifungo cha ndani wakati sheria inatoa hiari (option) ya adhabu zingine mbadala kama faini, kumwachia mshitakiwa kwa masharti, kumweka chini ya uangalizi wa Ustawi wa Jamii (under probation) nk.

Hata hivyo ni mahakama chache ambazo mahakimu wao wanatekeleza jukumu lao la kutembelea magereza mara kwa mara na kufanya mikutano pamoja na mahabusu/wafungwa ambao waliwapeleka huko wenyewe.

Mahakimu wengine hawajui hali ilivyo gerezani bali wanasikia na kusoma magazetini kuwa kwa sababu ya kucheleweshwa kesi zao wafungwa/mahabusu wamegoma kula au kupelekwa mahakamani siku za kesi zao nk.

Kinachoshangaza ni kuona pamoja na haya yote bado hakuna mabadiliko katika mtazamo wa mahakimu mahakama juu ya utoaji adhabu na dhamana kwa washitakiwa.

Jambo jingine kwa mahakimu kufanya ni kuwa wakali kwa polisi wanaoleta kesi mahakamani. Kwanza, hakimu ana uwezo kisheria kufutilia kwa mbali vikesi vidogo vidogo visivyo na kichwa wala miguu vinavyoletwa na polisi.

Hivi ni vikesi ambavyo kama polisi

walikuwa wanafanya kazi yao kwa uadilifu vingefaa kuishia vituoni.

Pili, polisi wasipewe mwanya wa kuahirisha kesi jinsi wanavyotaka bila ya kuwa na sababu za kutosha na ambazo zimeliwa viapo.

Kwa mfano, haitoshi polisi kuja mahakamani na kusema kwamba jalada la kesi halionekani au mashahidi hawakuja.

Sheria ipo wazi kwamba ikifikia siku sitini (60 days) hakimu anawajibika kuifuta kesi hiyo kama polisi wakipata ushahidi mpya bado wanao uwezo wa kuifungua tena kesi hiyo. Hakimu akitumia madaraka yake vizuri atasaidia kupunguza msongamano ambao siyo lazima katika magereza yetu.

3.8 Utaratibu wa Rufaa, Marejeo na Mapitio

Ili kuhakikisha haki inatendeka, sheria inampa mtu yeyote ambaye hakuridhika na maamuzi ya Mahakama ya Mwanzo fursa ya kukata rufaa (appeal) hadi mahakama iliyoko juu. Kuhusu jambo hilo Katiba ya Nchi iko wazi na inasema: Wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa mahakama au chombo kinginecho kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu, na pia haki ya kukata rufaa au kupata nafuu nyingine ya kisheria kutokana na maamuzi ya mahakama au chombo hicho kinginecho kinachohusika."

Aidha Mahakama ya Wilaya inayo madaraka kufanya masahihisho (mapitio) katika mienendo ya kesi za Mahakama ya Mwanzo kwa kupitia mafaili ya kesi za mahakama ya Mwanzo (revision) mara kwa mara. Mahakama ya Mwanzo yaweza pia kujikosoa na kusahihisha makosa yake inapogundua kuwa ilifanya makosa katika maamuzi. Yaweza kufanya hivyo kwa njia ya marejeo (review).

Hata hivyo tujiulize ni mara ngapi hakimu amekubali kujisahihisha makosa yake hata kama anaona bayana kuwa alifanya makosa katika maamuzi.

Hii inaweza kutokea kama kwa bahati mbaya au kutofahamu, hakimu ametumia sheria ambayo tayari imekwisha badilishwa na chombo husika au hakubaini kuwepo uamuzi wa mahakama ya juu zaidi kuhusu jambo analolishughulikia na ameamua kupingana na uamuzi wa hiyo mahakama Itaendelea toleo lijalo

Maskini unganeni kuondokana na umaskini(5)

c. Kuunda vikundi vya kijamii

Katika kila jamii vipo vikundi mbalimbali vya watu ambapo mahitaji na mapendeleo yao hutofautiana. Vikundi hivyo vinaweza kuwa vya vijana, wanawake, wakulima ama wafanyabiashara. Hali ilivyo katika ngazi ya Wilaya vikundi hivi havijajijenga na kuimarika vizuri. Kwa ujumla kuna udhaifu mkubwa hiyo ili kuviimarisha vikundi hivyo viweze kutekeleza wajibu wake ipasavyo, kazi kubwa inahitajika kufanyika.

Inafaa ieleweke wazi kwamba kuundwa kwa mashirika yasiyo ya Kiserikali bado sio ufumbuzi ingawaje ukweli unabaki kuwa NGOs zinasaidia katika mambo fulani fulani lakini kamwe NGOs haziwezi kuchukua nafasi ya vikundi hivyo vya kijamii. Kwa hiyo basi bado ipo haja ya kuweka mfumo unaoruhusu na kuhimiza kuundwa kwa vikundi hivyo na kuviimarisha vile ambavyo vimeshaundwa hasa katika ngazi za chini. Vile vile vikundi hivi vinatakiwa viwe na uwezo wake badala ya kutegemea mno fedha toka wafadhili.

Kuna haja pia ya kuwasaidia watu kuona umuhimu wa kuungana pamoja na kusimama kidete kutetea matakwa yao. Njia rahisi na nzuri ambayo ingesaidia watu kuelewa hilo ni kuwawezesha watu kutembelea sehemu kwenda kuona na kushuhudia mafanikio yaliyopatikana kwa jirani zao - kuona namna kijiji na kikundi fulani walivyofanikiwa kupata walichokuwa wanataka kwa sababu ya nguvu ya umoja wao. Kwa kweli hatua hii ni ngumu sana kuifikia, lakini ndipo hasa tunapotakiwa kufika .

Pamoja na ugumu huo, bado tunapaswa kufikiri ni kwa namna gani watu wanaweza kuungana, wakae na kujadili, kupanga mipango na kuweka mikakati ya utekelezaji huku wakiwa wanaaminiana.

Kutunza uaminifu kati ya wanakikundi ni muhimu licha ya makosa mengi yanayojitokeza miongoni mwa wanakikundi. Bila kuwa na vikundi vinavyowajibika na vyenye kuongozwa na watu wanaowajibika, hatutaweza kufanikiwa kuwa na ushiriki wa watu katika ngazi za chini. Ni ngazi hizi za chini ambazo zinatakiwa kuwa nguzo ya demokrasia japo kwa sasa kuna udhaifu mkubwa. Hii inatoka katika historia yetu kwani wakati wa siasa ya Chama kimoja watu hawakuruhusiwa kuunda vikundi huria vya kijamii vyenye lengo la kushinikiza mambo yafanyike ndani ya jamii.

Hali inavyoonyesha mpaka sasa hatujafanikiwa sana katika kuviunda upya vikundi kijamii katika ngazi ya chini. Katika ngazi ya Kitaifa kinachoonekana ni utegemezi mkubwa kwa wafadhili ambao hutoa fedha zao kupitia mashirika yasiyo ya kiserikali.(NGOs).

Kwa upande wa viongozi wa Kisiasa bado hakuna uelewa wa kutosha, hivyo nao hawawezi kuhimiza kuundwa kwa vikundi vyenye mwelekeo wa kujitegemea, na wala hawafikiri namna ya kuviunga mkono kwa kuvisaidia kifedha. Na hii haimaanishi kuwa vikundi hivyo vipate ruzuku moja kwa moja toka Serikali, bali ni kuvizawadia vikundi vile vinavyojitahidi katika maeneo yao kufanya shughuli zake kwa faida ya wote ama sekta fulani ya jamii. Mfano vikundi vya wazazi vinavyojitahidi kujitolea kuboresha shule zao. Hapa kinachotakiwa ni kuwa na fungu maalum la fedha Wilayani litakalokuwa likitumiwa kuviongezea nguvu vikundi vinavyofanya vizuri.

Mpaka sasa utekelezaji wa jambo la namna hii hautakuwa rahisi kwani maamuzi ya jinsi hii ni magumu kiutawala na pia watenda maofisini wanapendelea zaidi mfumo ule ambao mambo hutekelezwa katika mtindo unaofanana. Kuangalia suala fulani kwa namna tofauti kwa kuzingatia mazingira yake ni kitu ambacho watu hawapendelei.

d) Mafunzo kwa viongozi wa vikundi vya kijamii.

Katika kikundi chochote kile cha kijamii wamo watu ambao wana kipaji cha uongozi. Kwa upande mwingine sio watu wote wanaopenda kujiunga na vyama vya siasa na kufanya kazi nao. Kwa mantiki hiyo basi inafaa tuelewe kuwa uongozi wa kisiasa ni sehemu moja tu ya uongozi na hivyo hawapaswi kushikilia mamlaka yote ya kufanyia maamuzi. Zipo aina nyingine za uongozi ambazo nazo zina umuhimu mkubwa. Aina hizi ni pamoja na Uongozi wa kidini, Uongozi wa Sherehe za kijamii, uongozi wa vikundi huru kama wazazi, vijana, wanawake na michezo inafaa kama Taifa kutambua na kuheshimu uongozi wa aina hizi na hivyo kuwa tayari kutumia mali ya umma kuhimiza na kutoa mafunzo kwa uongozi wa kijamii. Kwa kuwa ni wajibu wa mamlaka ya Serikali na Vyama kuhakikisha zinatengwa fedha kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa viongozi na makada wao, basi kwa nia hiyo hiyo Serikali inapaswa kutenga fedha kwa ajili ya mafunzo ya viongozi wa kijamii.

Viongozi wa vikundi wanatakiwa wafundishwe namna ya kuviongoza vikundi vyao viweze kuwa na uwezo wa kusukuma na kushinikiza mambo, namna ya kushiriki katika, kufanya maamuzi na pia kujua mbinu za kushawishi (lobby) Bunge na Taasisi za Kiserikali.

Zijue vema huduma za Agape Centre

Hivi karibuni mwandishi wetu John P. Mbonde, alitembelea Kituo kimoja cha Kanisa Katoliki kinachojulikana kwa jina la Agape Centre kilichopo katika Parokia ya Mbezi kwa Luisi katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Alifanya mahojiano na Romano Lyimo ambaye ni Mratibu wa Programu za Agape ili kujua Agape Center ni nini na inafanya shughuli gani. Ufuatao ni ufupisho wa mahoiiano hayo.

Swali: Agape Centre ni nini?

Jibu: Agape Centre ni shule ya Kanisa Katoliki ya Biblia; ikiwa ni ya ufuasi na Uenezaji Injili. Ni shule ya kwanza ya aina yake hapa nchini Tanzania.

Watu wengi wanafikiri kuwa Agape ni kifupi cha jina fulani. Agape ni neno la Kigiriki lenye maana ya upendo wa Kimungu, upendo ambao hauna masharti wala mipaka. Upendo ambao hauna sababu ila kupenda tu.

Swali: Madhumuni hasa ya chuo hiki ni yapi?

Jibu: Chuo hiki hutoa huduma za Karismatiki kwa waamini Wakatoliki ili mradi kutekeleza mwito wa Bwana Wetu Yesu Kristo: "Mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe Mk. 16 : 15 hadi 16).

Aidha, chuo hiki ni jibu la mwito wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili mintarafu "Uinjilishaj; Mpya" katika milenia ya tatu na kuendelea.

Hali kadhalika, hutoa jibu kwa mwito wa Kanisa, mwito wa Mtaguso Mkuu wa Vatikano na mwito wa Sinodi ya Maaskofu wa Bara la Afrika.

Agape Centre inatoa nafasi kwa washiriki wengi zaidi kupata mafunzo ya Uenezaji Injili madhali isingekuwa rahisi kwa hao wote kujiunga na seminari, au nyumba za kitawa, au vyuo vya Makatekista.

Swali: Agape Centre ilianzishwa lini?

Jibu: Agape Centre ilianzishwa kwa kibali cha Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam ambaye kwa sasa ni Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, mwezi Januari 1996, chini ya Ukurugenzi wa Padre Etiene Sion M. Afr. Kilizinduliwa rasmi na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo Novemba 30, 2001.

Historia chachu ya chuo hiki cha Agape, imetokea tangu Karismatiki ilipoanzishwa hapa Tanzania mwaka 1981 wakati wa semina ya kwanza iliyofanyika Mzumbe, Morogoro.

Semina hiyo ilifuatiwa na nyingine kadha wa kadha kwenye vituo vya mikutano vya Bigwa, Morogoro na kile cha Kiroho cha Mbagala jijini Dar es Salaam.

Wakufunzi mbalimbali akiwemo Padre Rufus Pereira waliwatanabaisha washiriki jinsi ya kuinjilisha mtu kwa mtu, na nyumba kwa nyumba.

Ilikuwa katika mikutano na semina hizo, likazaliwa wazo la kuanzisha chuo kitakachowaanda wakristo jinsi ya kuinjilisha mtu kwa mtu, na nyumba kwa nyumba.

Ilikuwa hisani ya Bwana na Bibi Joseph Linder Mishili walipotoa eneo la shamba lao la hekta 3.072 likiwa ni pamoja na jengo la vyumba 12, hapo Mbezi Dar es Salaam ndipo Agape Centre ikafanya makazi yake.

Tulianza katika hali ya mazingira magumu, lakini kwa ushirikiano mkubwa wa uongozi wa Kanisa na Wanakarismatiki wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, tulijitoa mhanga kujenga, na kufanya kazi mbalimbali na kutoa misaada ya hali na mali.

Swali: Kuna mafanikio gani?

Jibu: Tangu Agape Centre ilipoanza, imehudumia watu wengi sana; wa ndani na nje ya Tanzania, hususan Kenya.

Licha ya kutoa mafunzo mintarafu uenezaji Injili, pia tunatoa huduma ya kuwaombea wagonjwa na kutoa ushauri nasaha kwa wenye shida mbalimbali.

Katika utoaji huduma hizo, tumegundua kuwa watu wanahitaji sana kutembelewa na kusikilizwa kwa karibu. Ni dhahiri kwamba watu wana matatizo mengi binafsi yanayowakabili dhidi ya matarajio yao ya kuipokea na kuiishi Injili.

Kwa mazungumzo na mtu mmoja mmoja, yaani mtu kwa mtu, watu wanaweka wazi matatizo yao ya ndani, wanapata fursa ya kuyakabidhi matatizo yao kwa Yesu na kuombewa. Kwa jinsi hiyo, wanapona ndani na kufunguka kuipokea na kuiishi Injili.

Ni matumaini yetu kwamba chuo kama hiki kitaweza kufunguliwa katika kila jimbo nchini.

Swali: Pamoja na mafanikio hayo, Agape Centre hukabiliwa na matatizo gani?

Jibu: Shida kubwa tuliyo nayo ni majengo. Uhaba wa majengo hutuzuia tusiweze kuwapokea washiriki wengi zaidi. Kwa bahati, kwa kupitia Nuncio Propaganda Fide, tumeanza kujenga mabweni na vyumba vingine vya huduma mbalimbali.

Mwisho, ningependa kutoa mwito kwa watu wote wanaopenda kujiunga na Agape Centre kupata maelezo zaidi kutoka kwa maparoko wao.

Sambamba na hilo, kwa watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kutoa misaada ya hali na mali ili kuweza kukiboresha chuo hiki.

Kama UKIMWI umeniacha mwaka uliopita,...

Na Josephs Sabinus

MSICHANA Blandina alisikika akiwalaumu majirani zake kijijini huku akilia machozi, akisema, "Jamani mngeniambia mapema nisingekuwa hivi sasa. Lakini mkaniacha tu jamani mimi nawalaumu nyie kwa kuwa sasa nitakufa niwaache watoto wangu."

"Hivi Benson siku hizi yuko wapi; ni mzima?’ anazidi kuulizia kwa hofu. Blandina alijuta namna alivyomsaliti mume wake Benson.

Alimsaliti kwa kuwa Benson na Dickson, walikuwa marafiki walioishi katika nyumba moja yenye vyumba tofauti. Dickson akiwa hana mke, alikuja pale kijijini kwa Benson kwa lengo la kujihusisha na shughuli za uchimbaji mdogo wa madini.

Ilikuwa bahati kwake kila alipojaribu uchimbaji, alipata pesa nyingi. Hali hiyoilimfanya aonekane wa kipato cha juu kuliko hata wenyeji na muhimu zaidi, kuliko rafiki yake Benson.

Benson alipopata nafasi ya masomo jijini Nairobi kwa kipindi cha miezi mitatu, uaminifu ulishindikana baina ya Dickson na Blandina; wakaiona hiyo ni nafasi tosha ya kumsaliti vilivyo Benson.

Lakini, wachache waliojaribu kumzuia Blandina kwa njia ya utani kuwa anachokifanya si chema kwake, kwa mume wake, kwa jamii na hata kwa Mungu yeye mwenyewe alisema kwa kujiamini.

"Huyu (Benson) si tumekaa naye tu kwani tumeoana kabisa." Ndipo mshangao ulizidi kuwavamia watu hata wasiamini kuwa kweli ni Blandina ndiye anayesema hayo. Kila mwenye mapenzi mema, anayejua thamani ya ndoa na uhai, alifumba kimya na kuinamisha kichwa kwa mshangao. Alivamiwa na butwaa la aina yake. Wengine wakasema UPANDACHO, NDICHO UVUNACHO

Wanaojua, walijua kuwa Blandina na mwenzake walikuwa tayari wamekufa kidhamira na sasa wanasubiri kifo cha UKIMWI.

Walisema hivyo maana walijua kwa tabia hiyo, UKIMWI hautakuwa tayari kumsamehe Blandina, hawakuongopa.

Labda mtu anaweza kujiuliza kuwa dhamiri ni nini? Dhamiri ni sauti ya Mungu iliyo katika roho ya kila mwanadamu inayomsaidia kujua jema na baya. Mtu anapokufa kidhamiri, matendo yake hayatofautiani na ya mnyama na wakati mwingine kuliko mnyama kamili.

Hata katika mazingira ya sasa, uovu wa aina yoyote unaofanyika duniani, ni matokeo ya kufa kidhamira.

Uovu mwingine ni chanzo cha kuenea kwa ugonjwa hatari wa UKIMWI. Hakuna asiyejua kuwa UKIMWI sasa limekuwa ni tatizo ambalo limeikumba jamii na kuwa sugu kutokana na ugumu wa mioyo ya watu unaosababishwa na watu kufa kidhamira.

Sote tunaitambua njia kuu ya kuenea kwa UKIMWI kuwa ni kushiriki vitendo vya uzinzi na uasherati, lakini kutokana na ugumu wa mioyo na dhamira zetu, tunapoonywa ili tusishiriki vitendo hivyo, hatusikii.

Katika mahubiri ya Jumapili ya Pili ya Pasaka Mwaka uliopita, Frateri Evarist S. Tarimo, alisema parokiani Chang’ombe, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam kuwa, "Kinachotufanya tuwe wagumu wa mioyo ni kwa sababu ile sauti ya Mungu inayotufanya tumwogope Mungu haipo tena katika mioyo yetu."

Mtu aliyekufa kidhamiri utamsikia akijitahidi kupotosha maana na kutoa kirefu cha neno AIDS kuwa ni "Acha Iniue Dogodogo Siachi" au hata akijigamba kuwa, UKIMWI ni ugonjwa kama mafua tu... "Majibu hayo yanaonesha jinsi watu walivyokufa kidhamiri. Wazo la kumuogopa Mungu tena halipo," alisema.

Mawazo hayo yamepitwa na wakati na ni upotoshaji na uuaji unaofanywa na "maiti wa dhamiri" kwa makusudi. Ni wakati muafaka kuyakana.

Madaktari, viongozi wa serikali na asasi za kibinafsi, hawajatambua kuwa hawatafanikiwa katika vita dhidi ya UKIMWI kwa kuwa ‘silaha" wanazotumia ni mbovu na zinapingana na mapenzi ya Mungu.

"Njia ya kutumia kondomu au kuwa na mpenzi mmoja hazisaidii kabisa kutokomeza UKIMWI bali zinaongeza UKIMWI na kuchochea ufuska katika jamii.

Hata viongozi wanasahau kitu cha msingi ambacho kitasaidia kabisa kuutokomeza UKIMWI; yaani MUNGU." alisema.

Ni dhahiri kuwa kwa kuwa watu hao na wengine wamemweka Mungu pembeni, jamii haitafanikiwa katika vita hiyo. Hali hiyo inatazamwa kuwa ni sawa na kutatua tazizo kuanzia kwenye majani badala ya kuanzia kwenye mizizi yaani, shinani.

Kila mmoja lazima ajue kuwa UKIMWI utaisha endapo tu, jamii itamuogopa Mungu na kuacha uzinzi.

Frateri Tarimo katika mahubiri hayo alisema kuwa, kutokana na wazazi kuishi maisha ya ovyo ovyo, watoto nao wanawaiga wazazi wao katika kuishi maisha ya ovyovyo. Watoto wamekosa mwelekeo katika maisha na kuamua kufuata hata mitindo ovyo ovyo ya maisha toka kwa wazazi wao.

Hapa ni dhahiri kila mmoja anapaswa kujua kuwa kama baba ana tabia ya kuwa na nyumba ndogo, ni vigumu kumfundisha mtoto wake kuacha uasherati.

Kadhalika, kama mama ana tabia ya kuwa na "buzi la kuchuna", ni vigumu kumfundisha mtoto namna ya kuepukana na uasherati.

Kama kweli tunataka kushinda vita dhidi ya UKIMWI, ni lazima kila mmoja kwa nafasi yak aanze kujijengea dhamiri. Wazazi tukiwa na dhamii nzuri, tutaweza kuwajengea watoto wetu dhamiri nzuri maana hata Waswahili wanasema, "Mtoto anapobebwa hutazama kisogo cha mamaye." Na hata Yesu anasema kuwa, "Mti mzuri hauwezi kuzaa matunda mabaya na wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri. Mt. 7: 15-20.

Kama wazazi hatutaanza kubadili tabia, tutaangamia pamoja na watoto wetu. UKIMWI utatumaliza wote. Hali yetu sasa ni mbaya mno.

Watoto na hata wanafunzi wengi katika miji mbalimbali tayari wana UKIMWI. Hawa wanasubiri kifo tu; waende; wafe.

Watoto hawa wamepata UKIMWI kwa kuwa wazazi, walezi wao na jamii nzima, hawakutimiza wajibu wao ipasavyo. Walishindwa kuwajengea dhamiri ili wamwogope Mungu na kuitunza miili yao ambayo ni Hekalu la Roho Mtakatifu.

Inasikitisha kwani baadhi ya watoto na wanafunzi wameathirika kwa kuwa baadhi ya wazazi na walezi walifanya nao mapenzi na hali hii mara nyingi imekuwa ikidhihirika wazi.

Wazazi hao bila aibu wamediriki kuwadanganyia watoto hawa chips, kuwapa fedha na kuwapa lifti katika magari yao, aibu na dhambi iliyoje.

Ni dhahiri hali hii inabainisha namna jamii ilivyokufa kidhamiri. Baba mzima au mama mzima na heshima zako, unapata wapi ujasiri wa kufanya mapenzi na mtoto wako hata umwambukize UKIMWI?

"Ama kweli sasa tunaishi kama wanyama. Akina baba na akina mama kama hawa, hawamwogopi Mungu kabisa. Hii ni kwa sababu dhamira zao zimekufa.

Kwanza hawana habari na kuvunja Amri ya Sita ya Mungu inayokataza kuzini, hawaoni aibu kufanya mapenzi na watoto, hawaogopi kuwaua watoto hawa na hata wenyewe kujiua na pia, hawaogopi kuziacha familia zao zikiteseka mara baada ya kufa kwa UKIMWI na zaidi, hawaogopi kuwaua wake au waume zao.," alisema.

Kila mtu anapaswa kujua kuwa akizini akapata UKIMWI, atakuwa na hatia nyingi mbele za Mungu: Atakuwa na adhabu ya kuzini, atakuwa na hatia ya kujiua mwenyewe kama aliyejiua wa kisu, kujinyonga kwa kamba au kujiua kwa sumu.

Kama mtu huyu ameoa, atakuwa na hatia ya kumuua mke wake na kama akifanya mapenzi nje ya ndoa atakuwa na hatia ya kuwaua watu wengine.

Zaidi na zaidi, mtu huyu kama ameolewa au ameoa, atakuwa na hatia ya kuiacha familai yake katika kipindi cha mateso.

Pamoja na njia nyingine zinazohimizwa na wataalamu wa afya, njia sahihi za kuepukana na UKIMWI ni kuepuka kabisa uzinzi na uasherati. Jibu la kuutokomeza kabisa UKIMWI liko kwa Mungu. Wote hatuna budi kufungua mioyo yetu na kumsikiliza Mungu anatuambia nini.

Njia nyingine ni kusali, kusoma Maandiko Matakatifu (Biblia) na kuwaomba watakatifu waliotunza usafi wa moyo wakati wa maisha yao hapa duniani.

Njia nyingine ya kupambana na UKIMWI ni kwa wanandoa kukumbuka maagano waliyoyafanya siku ya ndoa. Kwamba kila mmoja atakuwa mwaminifu daima kwa mwenzie.

Kila mnapolala na kuamka, sala ya kila mmoja iwe "Nitakuwa mwaminifu kwako daima." Kila mara baba aogope kumuua mama na mama aogope kumuua baba. Baba na mama wakiogopa kuuana, watakuwa wamesadia sana kupambana na UKIMWI. Kadhalika wazazi hao wote waogope kufa kwa UKIMWI na kuacha watoto, familia na jamii zao zikiteseka.

Ni wajibu wa kila mmoja kujua kuwa vita dhidi ya UKIMWI haitengani na namna sahihi ya kuishi na kuwahudumia wale ambao tayari walishaathirika.

Jamii haipaswi kuwaona walioathirika na UKIMWI kuwa wao ni wadhambi kuliko watu wengine la hasha! Hiyo si kweli.

Lazima kila mmoja ajue kuwa inawezekana anapomcheka, kumbeza na kumdharau mgonjwa wa UKIMWI, huenda hata yeye alishaambukizwa kwa njia yoyote isipokuwa tu, hajui kwa sababu hajapimwa.

Inakera kwani wengi wetu katika jamii wana tabia ya kuwaona kuwa ni wadhambi; watu ambao wamekwishaambukizwa UKIMWI. Hii si kweli na ni dhana mbaya kwa kuwa zipo dhambi nyingi na sio kuzini pekee.

Kuiba, kupokea rushwa, masengenyo, chuki dhidi ya wenzio, kusema uongo, kuua, na mengine mengi, yote hayo ni dhambi Kumbe sote tu wadhambi.

Tunachopaswa kufanya ni kuwapenda na kuwahudumia vizuri wagonjwa wa UKIMWI sio kuwakimbia, kuwachukia, kuwasimanga, kuwadhulumu wala kuwacheka

Ni wakati sasa kuanza mwaka huu kila mmoja akijisemea kuwa: "Kama sikuambukizwa UKIMWI mwaka uliopita, basi sitaambukizwa."

Ni wakati sasa kujiuliza kwanini kitendo cha zinaa ambacho ni cha dakika chache kinipe mateso na kunipeleka katika moto wa milele?

haki za raia Kitabu cha Tatu

Sheria ya Ardhi Tanzania (9)

Mbali na maelezo hayo ya jumla itakuwa ni sharti kwa kila haki miliki iliyotolewa kwa lengo la ujenzi wa nyumba kuomba kibali cha kufanya maendelezo katika kiwanja kama inavyoelezwa na sheria ya mipango miji na kanuni nyingine za ujenzi mijini katika kipindi cha miezi sita mara baada ya kupewa hati ya haki miliki.

Vile vile watu wanaomiliki ardhi kimila watakuwa na haki halali na wataweza tu kuondolewa toka maeneo yao na kupelekwa kwinine iwapo tu kufanya hivyo kutasaidia kuwezesha utekelezaji wa masharti ya haki miliki iliyotolewa. Sheria inaagiza kuwa katika kuwahamisha watu hawa mambo yafuatayo yazingatiwe;

a) Wapewe ilani ya uhamisho ya kipindi cha siku mia moja na themanini ya kuwataka wahame

b) Vile vile watapewa fursa ya kuvuna mazao yao waliyopanda kabla ya ilani hiyo kutekelezwa.

c) Pia wataendelea kutumia maji waliyokuwa wanatumia kabla ya ilani hiyo kutolewa

d) Pia watapewa fidia ya hasara inayotokana na kukosa maslahi yao yanayotokana na kukosa ardhi hiyo ama gharama zitokanazo na kuhamishwa huko nausumbufu ulioambatana na kuhamishwa huko.

Fidia yao kamili itapaswa kulipwa mapema kadri itakavyowezekana.

Mbali na maelezo hayo kiutendaji mambo yafuatayo pia yatazingatiwa;

iii ) Vivyo hivyo Kamishna atashauriana na Serikali ya mtaa na atazingatia ushauri na mapendekezo ya Serikali ya mtaa wakati

inataka kutoa haki miliki ya ardhi iliyoko kwenye mtaa husika

iv). Sheria hii ya ardhi imeweka bayana kuwa itakuwa ni sharti Kamishna wa ardhi na Afisa mteule anaweza kutembelea na kuchunguza iwapo masharti ya uendelezaji yanafuatwa. Lakini kabla hajafanya hivyo lazima atoe taarifa kwa mwenye haki miliki au mwakilishi wake.

Kwa upande wa ardhi ya vijiji wamiliki watapaswa kuzingatia masharti yafuatayo;

i) Kutunza na kuhifadhi ardhi ili ibakie katika hali nzuri.

ii) Kwa wakulima na wafugaji waitumie ardhi kulingana na taratibu za kimila za eneo husika katika ufugaji na ukulima.

iii) Inapohitajika kufanya ujenzi ruhusa maalumu inapaswa kutolewa kabla ya jengo husika kuanza kujengwa.

iv) Mmiliki anapaswa kulipa malipo yote yanayohitajika kulingana na matumizi ya ardhi anayomiliki na itakavyoelekezwa na serikali.

v) Mmiliki anapaswa kufuatana na sheria kuu sheria ndogo ndogo na maelekezo mengine atakayopewa na halmashauri ya kijiji au mtu mwingine mwenye mamlaka kisheria.

vi) Mmiliki anatakiwa kutunza mipaka ya eneo lake

vii) Mmiliki anapoondoka kwa muda anatakiwa aache taratibu za jinsi gani ardhi yake itaendelea kusimamiwa na kutunzwa na kuendelezwa.

Vile vile kamishna ama afisa mteule wa halmashauri ya kijiji au idara ya serikali watapaswa kufanya ukaguzi kuona kama masharti ya umiliki wa ardhi kimila yanazingatiwa.

6.2 Matumizi ya Ardhi

Haki Miliki inaweza kutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za makazi na biashara, viwanda, sehemu za burudani, maegesho ya magari, ofisi, taasisi, huduma za jamii, maeneo ya kuabudia, kuzikia, maeneo ya.wazi, barabara, bustani za wanyama. Mbali na hayo ardhi pia inaweza kutumika kwa shughuli za kilimo na ufugaji.

Inawezekana mmilikaji kwa sababu moja ama nyingine akaona matumizi yaliyo-oanishwa katika haki miliki yake sio ya manufaa kwake baada ya muda fulani. Hapo anaweza kuomba kwa kamishna kubadili matumizi ya sehemu ya ardhi yake ama kwa eneo lote.

6.3. Mabadiliko ya Matumizi katika Haki Miliki ya Ardhi

Mmiliki anapotaka kufanya mabadiliko ya matumizi anapaswa kutuma maombi kwa kamishna. Maombi hayo yatazingatia mambo na taratibu zifuatazo:-

a) Yawekwe katika fomu maalum yenye picha ya mmilikaji

b) Yaambatanishwe na malipo yatakayoelekezwa

c) Yasainiwe na mwombaji, mwakilishi ama wakala wa mwombaji

d) Yawasilishwe kwa kamishna kwa njia zinazoaminika.

e) Yaambatanishwe na taarifa nyingine zozote zile zinazohitajika ama zile ambazo kamishna ameziomba kwa maandishi.

Ili kufikia uamuzi kamishna atapaswa kushauriana na; mamlaka inayohusika na mipango miji idara ya uthamini au mamlaka yoyote katika kufanya mabadiliko ya matumizi.

Itaendelea toleo lijalo

Riwaya

Zitto alimuacha Rozi kwa Dokta Madevu ili asaidiwe kutoa mimba. Anaporudi kupata majibu ya kinachoendelea, anamkuta Dokta katika hali ya hofu kama kuku anayetaka kutaga mayai, macho yamemuiva; kwanini, Endelea. Katika historia ya maisha yangu, ninaamini ingawa sikulewa kiasi cha kutisha, siku hiyo ilikuwa ya kumbukumbu ya siku nilizokunywa bia nyingi.

Kama nikujenga tabia njema au mbovu, siku hiyo ulikuwa mwanzo wa tabia hivyo kwani sasa nilikuwa ninakunywa na kunywa mradi tu, niondoe mawazo.

Sikuwa na uhakika hadi sasa kama unywaji ndio dawa ya matatizo, au ni kupandikiza tatizo juu ya tatizo.

Nilikunywa sana na nikaendelea kunywa siku hata siku; sikutaka kufanya tena kazi. Kazi yangu sasa ilikuwa ni kunywa bia kila siku ili kupoteza mawazo.

Bahati mbaya mawazo hayakupotea. Kila pombe ilipokwisha kichwani, nilijikuta yakinirudia na kunifanya nitafute pombe tena ili nilewe; nipoteze mawazo.

Pesa niliyokuwa nimechuma katika biashara zangu ikaanza kuyoyoma kila kulivyokucha.

Miradi na biashara zangu ikaanza kuporomoka na kukosa uangalizi na usimamizi.

Sikujali kwani baada ya kupata jibu toka kwa Massa kila kitu kilikuwa kimepoteza umuhimu na maana isipokuwa pombe. Siku hata siku nikazidi kutopea na kujisaulisha katika ulevi.

Ilinifikia hatua ya nikaanza kuuza samani na vitu mbalimbali. Afya yangu nayo ikaanza kudhoofu kwa haraka sana kutokana na ulevi usioambatama na shibe. hata hivyo, mimi sikujali;.

Ilinifikia hatua hata nikawa nimetumia pesa zote katika ulevi na kuuza kila kitu isipokuwa gari langu aina ya Toyota Mark II.

Sasa nikaanza kukopa na kuomba pesa kwa ajili ya pombe; pia nikaanza kutafuta mtu wa kumuuzia lile gari langu. Ni hapo rafiki yangu Kidevu alipojitokeza na kuniepusha na uharibifu zaidi.

Kichwa kilikuwa kinanigonga kwa nguvu kutokana na ulevi wa jana ya siku hiyo na tumbo lilikuwa linanisokota huku nikipiga miayo bila kukoma. Siku hiyo nilikuwa nime nywa pombe nyingi na wala sikuwa nimetia chochote tumboni. Japo mshale wa saa ulikuwa unaonesha kuwa ilikuwa imetimu saa 5 hivi, nilikuwa bado nimejilaza pale kitandani nikihisi uchovu na uvivu wa kuamka asubuhi hiyo iliyoelekea kumalizika.

Nikazidi kuwaza na kuwazua kuwa ni wapi nitapata pesa za kilevi siku hiyo.

Ni hapo niliposikia hodi mlangoni sikujali

"Hodi! Zitto, Zitto," ilikuwa ni sauti ya Kidevu bila kusema neno, niliamka nikaenda kumfungulia.

Aliniangalia kama vile hanifahamu kisha akatikisa kichwa na kuingia ndani . Akaa kwenye stuli.

"Vipi mbona umeniangalia hivyo na kisha ukatingisha kichwa?" nikauliza.

"Hivi rafiki yangu Zitto, umechanganyikiwa?"

"Labda! Kwanini unaniuliza hivyo,"

Kidevu akasema, "Mbona siku hizi unafanya mambo kama mwendawazimu ; umelewa kama mjinga! Una nini wewe?"

"Nina wazimu!" nilimjibu kwa kejeli na kutojali "Usifanye mzaha Zitto wewe ni rafiki yangu nataka nikusaidie."

"Unisaidie? Unisaidie nini? Unaweza kunisaidia nini wewe?" nikauliza kwa dharau.

"Chochote Zitto! Mawazo! Chochote ninachoweza."

"Mh! Kwani unanionaje Kidevu? Unafikiri nahitaji kusaidiwa na wewe?"

"Siyo nafikiri ni dhahiri unahitaji msaada. Inaweza isiwe ni mimi lakini ukweli ni kwamba unahitaji kusaidiwa"

"Kwanini?"

" Ina maana huoni Zitto? Hujashtuka kabisa!" "Labda unishtue"

"Hee Zitto! Angalia mambo yako yalivyokuwa hovyo! Hatua uliyokuwa umefikia kibiashara, kila mtu alikuwa anakusifia. Ulikuwa na pesa za uhakika, ulikuwa na maduka, una gari, ulikuwa umeshakuwa tajiri na ghafla umevuruga kila kitu kwa ulevi tu.

Na sasa nasikia unapita ukikopa kwa watu pesa ya ulevi bila hata aibu vilevile unataka kuuza gari, mbona unaharibu maisha yako. Ulevi utakusaidia nini. Jirekebishe Zitto rafiki yangu," Kidevu akanisihi.

"Sikiliza kidevu." akusikiliza

Nashukuru sana kwa ushauri na upendo wako lakini naomba nikuulize swali’

"Uliza tu."

"Ulishawahi kupenda"

"kupenda!" alishtuka na kubutwaa na bila shaka ni swali ambalo hakuwa amelitegemea.

"Ndiyo! Kupenda," nilimjibu

Kidevu aliwaza kidogo halafu kama vile hana uhakika na kila anachokisema, akanijibu, "Ndiyo nilishi.... Nishiwahi kupenda! Kwani vipi?"

"Halafu yule mtu unayempenda akakukataa?’ nikamuuliza tena.

"Mbona sikuelewi Zitto haya maswali yanatoka wapi?" akahoji kwa hamaki

"Si unataka kunisaidia, naomba unijibu basi."

"Hapana sijawahi kukataliwa!"

"Basi huna uwezo wala uzoefu wa kuweza kunisaidia".

"Kwanini?" akaduwaa.

Sikutaka kumjibu kwa maneno nikaenda kwenye shelf ya vitabu nikaichukua ile barua ya majibu toka kwa Massa nikamrushia na kumwambia, "Soma!"

Alitumia muda mrefu akiiangalia barua ile. Bila shaka aliisoma akirudiarudia halafu akanyanyua macho kuniangalia.

Akavuta pumzi na kuzishusha kwa pamoja.

" So this is it" (yaani, ndivyo ilivyo) akatamka kwa mshangao na mduao wa aina fulani.

"Najua bado unaweza kukisia ni kiasi gani umeumia siwezi kukulaumu lakini wewe ni mwanaume Zitto na sasa wewe ni mtu mzima. Lazima uwe imara na mstahimilivu wakati wa shida na mashaka kitu kama hiki kisikufanye uharibu maisha yako.

Tuliza akili na utapata mwingine wa kukupenda na kukuliwaza," Kidevu aliendelea akunisihi.

"Unajua Kidevu mzigo usioubeba hujui uzito wake. Kwako, jambo hili ni rahisi na ndiyo maana unasema hivyo. Laiti ungelijua ninavyompanda Massa,..."

"Najua Zitto! Najua unavyompenda Massa. Na labda Massa aliwahi kukupenda kimakosa na sasa amegundua kosa na hakupendi tena.

Huo ndio ukweli na huwezi kupingana na ukweli ukashinda".

" Kwa hiyo unanishauri nifanye nini sasa?’ Nikauliza.

"Nakuomba usahau kwamba uliwahi kumpenda Massa; uamini kwamba utapata msichana mwingine zaidi ya Massa ambaye atakupenda na kukuthamini. Zaidi ya yote, achea kuharibu maisha yako kwa pombe,

Endelea na biashara yako; weka nguvu na akili zako katika kazi na mambo ya manufaa," aliniasa Kidevu.

"Lakini nampenda Massa nitamsahau kweli!"

"Utamsahau Zitto, huwezi kulazimisha kupendwa; penzi si la upande mmoja, hebu fikiria mwenyewe jinsi Rozi alivyokuwa anakupenda na hasara aliyopata kwa kulazimishwa umpende mbona bado hukumjali, kwanini iwe Rozi tu na siyo wewe!"

Maneno hayo yaliniingia sana na kunikumbusha mbali. Nilikumbuka jinsi Rozi alivyonihangaikia na kunililia, jinsi alivyokuwa ananipenda.

Nilipobaini jinsi Rozi alivyojisikia na kuumia pale nilipomtamkia kuwa simpendi na haitatokea nimpende, nikapambanua kuwa kitu nilichomtendea Rozi kilikuwa kibaya na chenye uchungu usiomithilika, nilijihisi mwenye hatia na kumhurumia.

Nilitamani nimuone na kumwomba samahani kwa unyama niliomtendea, lakini hilo lisingekuwa rahisi kwani nilipotoka jela nilipata habari kuwa Rozi aliolewa na mwanaume wa Kizungu anayefanya kazi kwenye Shirika la Kimataifa la Wakimbizi (UNHCR) na alishaondoka naye kwenda naye huko Mashariki ya Mbali.

Nilijua ilivyo, kazi ya mumuwe ilikuwa si rahisi kwao kukaa mahali pamoja kwa muda mrefu; na isitoshe, ni muda mrefu alikuwa hajafanya mawasiliano na ndugu zake.

Nilimwangalia Kidevu kwa kwa muda kisha nikapumua kwa nguvu .

"Ama kweli kupenda ni kitu cha ajabu sana kamwe sikuwahi kufikiri kupenda kunaweza kuwa kuchungu kiasi hiki kumbe nilimkatili sana Rozi," nikasema.

"Usijali yaliyopita si ndwele tugange yaliopo na yajayo," akasema Kidevu.

Kidogo sasa nilisikia kutulia na kuondokewa kiza katika akili yangu. Muda ulikuwa umesonga mbele na njaa ilikuwa inauma sana. "Twende hapo Bukenye Hoteli tukale nina njaa kweli." tukaondoka.

Wakati tunakula, nilikuwa nimechanganyikiwa huku mazungumzo yetu yamezama katika matukio ya michezo na siasa.

Baadaye, Kidevu aliaga kuondoka huku akiniambia, "Nitakupitia jioni tukaangalie sinema."

"Kwani leo kuna picha gani?" niliuliza naye akajibu, "Picha moja ya Kizungu inaitwa I was born to Die’(yaani, nimezaliwa ili nife)‘

Tuliagana akaondoka.

Xxxxxxxxxxxxxx

Sikuwa tena na mapenzi au wazo juu ya Massa.Sasa maishani sikutegemea kama nitakuja kumpenda tena msichana kama nilivyowahi kumpenda Massa .

Niliomba yaliyonitokea kwa Massa yasinitokee tena. Niliazimia kuwa mjanja na mwangalifu; na hata hivyo sikuwa na muda.

Muda, nguvu na akili zangu vyote nilikuwa nimevielekeza katika biashara zangu ambazo zilikuwa zimerejea katika hali nzuri na kustawi zaidi baada ya kutuliza akili yangu na kuifuta sasa toka kwa Massa.

Biashara yangu iligeuka na kuwa na thamani kubwa kwangu.Niliiona biashara hiyoi kama mke wangu na faraja kwangu.

Kadiri nilivyozidi kushamiri, ndivyo sifa na heshima yangu ilivyoongezeka miongoni mwa wanajamii.

mafanikio yalizidi kuongezeka na sasa nikarudi katika heshima ile ya kuitwa mzee na watu lukuku hata kama umri wangu haukustahili jina hilo.

.Kwa kiwango kikubwa, nilifanikiwa kujenga dunia yangu mbali na ile ya wanawake.

Nikakosa kabisa muda wa kuwaza juu ya wanawake. Sasa nikajiona niko salama na huru. Nikajawa imani na shukrani kwa rafiki yangu Kidevu.