Maskini unganeni kuondokana na umaskini(4)

Hali hii inatudhihirishia kwamba tunakabiliana na tatizo kubwa sana la kijamii na vile vile la kiuchumi. Uchumi wa Tanzania ni mdogo sana hivyo kwamba hauwiani na tatizo lenyewe. Hivyo si rahisi kupata ufumbuzi rahisi wa tatizo hilo.

Kwa upande wa Serikali tunachoshuhudia ni kwamba jitihada za dhati na zisizo na nia ya udanganyifu zinafanyika. Hapo hapana shaka yoyote, ingawa tunadhani kwamba bado kungeweza kufanyika uboreshaji katika mipango na utekelezaji.

Licha ya Serikali, tumeshuhudia pia wafadhili wa nje na mashirika ya ndani yasiyo ya kiserikali (NGO) nao wakitoa michango inayopaswa kuheshimiwa, kuthaminiwa na kusifiwa.

Zaidi ya hayo Benki ya Dunia na Serikali sasa wamezindua "Mpango wa kupunguza Umaskini nchini," hatua ambayo imefuata baada ya Tanzania kutambulika na kuchukuliwa kama miongoni mwa nchi maskini na zenye madeni makubwa.

Kigezo kikubwa kinachotumika kuiingiza nchi katika mpango huo ni nchi yenyewe kuonyesha kuwa imefanya jitihada za pekee katika kuleta mabadiliko yenye kuthibitisha matokeo ya kuboresha hali ya maisha ya watu. Tanzania imeonekana imehitimu katika hilo.

Kinachofuata ndio msamaha wa madeni ambapo fedha ambazo zingelipia madeni hayo yaliyosamehewa, sasa zitatumika katika kuboresha huduma za jamii nchini. Hizi zote ni habari nzuri.

Hata hivyo ni muhimu sasa tuangalie kama hatua hizi zitaweza kushughulikia tatizo la mgawanyo wa matabaka katika. nchi yetu ambalo linaendelea kukua siku hadi siku. Kwa maneno mengine je, hatua hii ya ongezeko la fedha kwa ajili ya huduma za jamii itaweza kupunguza tofauti kati ya watanzania wachache wenye hali nzuri sana na wale wengi wenye hali mbaya kabisa? Kwa kuweza kufikiri kwa makini yafaa tujiulize ni vipi nyongeza hii ya fedha itatumika na ni nani ataamua fedha hizo zitumike kwa namna gani. ‘Pia ni nani ataweka vipaumbele katika mahitaji.

Kwa kadri ya utaratibu tunafahamishwa kuwa fedha zitatumwa toka Serikali Kuu kwenda wilayani. Kisha vigezo na masharti

vitawekwa kutoa maelekezo ya kuweka vipaumbele na maamuzi katika ngazi ya wilaya. Hata hivyo haielezwi bayana kuwa ni nani ataweka vipaumbele na maamuzi yatafanywa na nani. Watu wataweza kushiriki moja kwa moja katika kuweka vipaumbele na kutoa maamuzi? Hili ni swali la msingi kabisa. Mfano nani ataamua hitaji lipi litimizwe kwanza - mahitaji ya hospitaii ya wilaya au ya zahanati za vijijini, shule za sekondari au za msingi wilayani.

Kuweza kuanza kujibu maswali haya tunapaswa kutambua uwajibikaji na nia ya baadhi ya watu katika jamii yetu ambao wanaweza kuamua kwa faida ya tabaka la watu wa chini ambao ndio wengi. Kupata kundi la aina hii :- la watu wanaowajibika na kujitoa kwa ajili ya maskini halitakuwa jambo rahisi kwani unahitajika ubora, uelewa na uadilifu fulani wa mtu mwenyewe. Ni mtu ambaye yuko tayari kufanya kazi kwa faida ya wengine bila kutafuta kujinufaisha kibinafsi. Kwa bahati nzuri bado katika jamii ya Tanzania ya leo tunao watu wa kutosha wa aina hii - wenye sifa za kiutu. Tunachotakiwa ni kuweza kubainisha sifa bora za uongozi ambazo zitaweza kutumika kutuletea mapinduzi ya kweli tunayohitaji. Mapinduzi hayo hasa ni kule kuruhusu kundi la wengi kuwa na kauli katika mambo ya nchi na jinsi nchi inavyoongozwa.

Wakati umefika ambapo urekebishaji wa Mfumo wa Serikali za Mitaa hauna budi kuangaliwa kwa upana zaidi ili kuhusisha pia mfumo wa mawasiliano na kufikia maamuzi ya kijamii.

Hapa ndipo pa kuanzia - kuangalia kwa makini ni kwa namna gani tunaweza kuwasaidia watu waweze kushiriki katika maamuzi yanayofanywa katika ngazi ya chini.

2. Namna gani ushiriki wa watu unaweza kuimarishwa.

Wakati mipango na maamuzi vinafanywa na Serikali ama na Taasisi nyingine ni vema kukawa na hatua ya kutafuta ushauri (consultation). Lakini hatua hiyo hatuwezi kuchukulia kuwa ndio ushiriki wa kweli wa watu. Kuna nafasi vile vile ya mmoja ama mwingine kualikwa na kuchukuliwa kama mwakilishi wa kikundi cha kijamii. Lakini kwa kweli nafasi hii bado iko mbali sana na ule ushiriki wa kweli wa watu. Viongozi wa kuchaguliwa wakiwemo Madiwani ni kwa nadra sana wanatumia nafasi hizo kutetea mambo kwa faida ya wanakijiji.

Huu ndio ukweli halisi kuanzia ngazi ya kitaifa hadi ya Wilayani. Wakati huo huo watu wanayo mawazo mazuri sana juu ya vipaumbele katika mahitaji yao, lakini hawathubutu kujitokeza kuwasilisha mawazo yao kwa hao wenye mamlaka mbalimbali. Inafaa kuelewa sababu za watu kutotoa mawazo yao na kisha kujua hatua za kuchukua kujenga mwamko wa kujitokeza na kusimama kutoa mawazo pale panapohitajika.

Njia zinazoweza kutumika ni kama hizi zifuatazo;

a) Upatikanaji wa habari na taarifa.

Hatua ya kwanza ni kuwawezesha watu kupata taarifa juu ya nini kinaendelea katika Ofisi za Serikali ngazi ya Wilaya - Mipango gani ipo na mikakati gani imepangwa kwa utekelezaji.

Mfano: Zipo fedha kiasi gani kwa ajili ya Elimu. Ni kiasi gani zimetengwa kwa ajili ya shule za msingi, na shule zinazolengwa ni zipi. Je, ni kiasi gani cha fedha kinatumika kwa ajili ya kulipia mishahara ya walimu, kununulia vitabu na kutengenezea madawati.

Taarifa hizi ni kwa ajili ya watu na sio siri za kutunzwa Ofisini. Ni haki ya kila raia kufahamu taarifa hizi. Kwa hiyo siyo tu juu ya mtu binafsi au jumuiya fulani kutafuta habari hizi bali pia ni wajibu wa Serikali za Mitaa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa hizi kwa urahisi. Ni haki pia ya wananchi kujua pesa gani zipo na zinapaswa kutumika kwa mambo gani. Vile vile lazima watu wafahamu vigezo vinavyotumika katika kuzigawa fedha hizo kwa matumizi mbalimbali. Upatikanaji wa habari na taarifa ni muhimu kama kweli tunataka watu washiriki maamuzi yanapofanyika. Vile vile inafaa watu wapatiwe taarifa sahihi ili ziweze kuwasaidia kikamilifu.

b) Wawakilishi waliochaguliwa kuwa sauti ya watu.

Kwa hali ya sasa ya kidemokrasia nchini, hili linakuwa na ugumu fulani. Lakini lazima tuelewe ukweli kuwa wawakilishi hawa wamachaguliwa na watu kuwakilisha kwanza matakwa ya watu na wala sio kuwakilisha matakwa ya Chama wala maoni ya serikali. Viongozi sharti wajifunze kuheshimu maoni na matakwa ya watu ikiwa ni pamoja na mahitaji ya watu hao ambao ndio waliowapa nafasi hiyo kwa kuwapigia kura. Hata hivyo katika hali halisi tunamoishi kazi kubwa inahitajika kufanyia marekebisho mfumo wetu wa uwakilishi ili tuweze kushuhudia hilo katika ukweli halisi wa maisha hapa Tanzania.

Na ili hili lifanikiwe tunahitaji kujenga mfumo wa uwakilishi ambao ni wa uwajibikaji . huu nido ukweli si kwa ngazi ya taifa tu bali pia katika ngazi za chini. Hata hivyo hatupaswi kukata tamaa kwani mbegu imeshapandwa tunachotakiwa ni kudai kuwepo kwa mfumo wa kuwajibisha viongozi wasiotaka kupata maoni na matakwa ya watu wao. Hata hivyo kwa bahati nzuri wapo wachache wanaoweza kusimama upande wa watu na kutetea matakwa ya watu dhidi ya mamlaka za juu pale inapobidi.

c. Kuunda vikundi vya kijamii

Katika kila jamii vipo vikundi mbalimbali vya watu ambapo mahitaji na mapendeleo yao hutofautiana. Vikundi hivyo vinaweza kuwa vya vijana, wanawake, wakulima ama wafanyabiashara. Hali ilivyo katika ngazi ya Wilaya vikundi hivi havijajijenga na kuimarika vizuri. Kwa ujumla kuna udhaifu mkubwa hiyo ili kuviimarisha vikundi hivyo viweze kutekeleza wajibu wake ipasavyo, kazi kubwa inahitajika

Itaendelea toleo lijalo

haki za raia Kitabu cha Tatu

Sheria ya Ardhi Tanzania (8)

5.2.2. Mkataba wa Haki Miliki za Kimila

Halmashauri ya kijiji inapofikia uamuzi wa kumpatia mwombaji haki miliki ya ardhi itamtumia barua ya toleo iliyosainiwa na Mwenyekiti na Katibu wa Halmashauri ya Kijiji husika, ikiwa katika fomu maalum inayoeleza masharti ya haki miliki yake.

Mwombaji anapopokea barua ya toleo anatakiwa kuijibu ndani ya muda wa siku tisini kama anaikubali ama anaikataa.

Majibu yake yawekwe katika maandishi yaliyosainiwa na mwombaji husika kama ilivyokwishaelezwa. Pale ambapo barua ya toleo inaambatana na malipo ya awali ya kodi, kilemba au kodi ya kijiji ama malipo mengine yoyote yatakayotakiwa na serikali ya kijiji, barua ya toleo itakuwa imekubalika iwapo malipo yote hayo yatakuwa yamelipwa kikamilifu.

Malipo hayo yanatakiwa yathibitishwe kwa kuambatanisha stakabadhi halali zilizotolewa kwa madhumuni hayo.

Kwa kulingana na maelezo hayo, iwapo upatikanaji wa Hati ya Haki Miliki haukuzingatia maelezo hayo hapo juu na mengine yaliyo katika sheria ya haki miliki itakuwa batili.

Kwa jibu lolote lile mwenye mamlaka kushughulikia ni hati-nashauri ya kijiji na kwa hiyo basi endapo itagundulika Haki Miliki ya Kimila imepatikana kwa njia isiyo halali ikiwa ni pamoia na kutumia rushwa, basi haki miliki hiyo ya kimila itakuwa batili.

5.2.3. Hati Miliki ya Ardhi ya Kimila

Baada ya Mkataba kukamilika, Halmashauri ya Kijiji inatakiwa kumpatia mwombaji hati ya haki miliki ya ardhi ya kimila katika muda usiozidi siku tisini.

Hati ya Haki Miliki ya Kimila itakuwa;

a) Katika fomu maalum

b) Na sahihi ya Mwenyekiti na Katibu wa Halmashauri ya Kijiji.

c) Na sahihi ama alama ya mmilikaji kwa mfano dole gumba la mkono wa kushoto chini ya kila ukurasa wa hati miliki.

d) Vile vile itasainiwa, itawekwa takiri na kusajiliwa na Afisa Ardhi wa Wilaya ambamo kijiji kimo.

5.2.4. Malipo na muda wa Haki Miliki ya kimila

Serikali ya kijiji husika inaweza kutoza ada au ushuru mbali na sheria inavyoelekeza.

Wakati serikali ya kijiji inapanga kiwango cha kilemba kwa mfano itapaswa kutafuta na kuzingatia ushauri wa kamishna wa ardhi kadiri sheria inavyoelekeza.

Haki miliki ya ardhi ya kimila inaweza kutolewa kwa kipindi kisicho na muda maalum kwa raia. Vinginevyo ni kwa vipindi au kipindi ambavyo kwa jumla havitazidi miaka tisini na tisa kadiri serikali ya kijiji itakavyoona inafaa.

Vilevile Haki Miliki ya kimila inaweza ikatolewa kwa kipindi cha mwaka hadi mwaka, ambapo haki hiyo inaweza ikasitishwa kwa kutoa taarifa ya muda wa mwaka mmoja au chini ya hapo.

Endapo serikali ya kijiji inataka kupunguza muda wa Haki Miliki ya Kimila, kwa Haki Miliki za kimila za muda maalum haitafanya hivyo mpaka. hapo utakapopatikana makubaliano na wenye hati husika.

Pamoja na maelezo ya hapo juu kuhusu upatikanaji wa Hati ya Haki Miliki iwapo mwombaji amekubali barua ya toleo na kuzingatia masharti yanayoambatana nayo na siku mia moja na themanini zimepita bila kupatiwa Hati Miliki na kamishna, sheria itatambua barua ya toleo kama ni Hati ya Haki Miliki halali, na barua ya toleo itasajiliwa na msajili wa hati na itakoma kuwa hati miliki halali kuanzia tarehe ambapo hati yenyewe itakaposajiliwa.

MASWALI

1. Je, wewe unayo hati ya haki miliki kwa nyumba, shamba au kiwanja unachomiliki?

2. Kwa nini upatikanaji na usajili wa hati miliki huchukua muda mrefu kukamilika.

3. Je, kumiliki ardhi kimila kunaruhusiwa kisheria.

MASHARTI, MATUMIZI NA MABADILIKO YA HAKI MILIKI YA ARDHI

6.1. Masharti ya Haki Miliki ya Ardhi

Sheria inampa Waziri wa ardhi uwezo wa kumtaka mtu yeyote mwenye haki miliki kulipa kilemba. Malipo ya kilemba. yatalipwa mara moja ama kwa awamu kama itakavyoelekezwa na Waziri. Kiwango cha kilemba kitakachoelekezwa kitapangwa na Waziri kwa kuzingatia mambo yafuatayo:-

(a) Matumizi ya ardhi yaliyoruhusiwa.

(b) Thamani ya ardhi inayotokana na aidha mauzo au upangishaji n.k. kama ilivyoetekezwa na sheria.

(c) Thamani ya ardhi kama inavyoonyeshwa na bei iliyopatikana katika mnada uliofanywa na/au kwa niaba ya Serikali.

(d) Thamani ya ardhi iliyothibitika katika zabuni ambapo bei ya juu iliyotajwa ndiyo inayothaminisha ardhi hiyo.

(e) Maendelezo yaliyopo.

(f) Ushauri wa thamani uliotolewa na mthamini anayetambulika katika mazingira ya soko huria.

Sheria inaoanisha masharti yanayoambatana na kumilikishwa ardhi, nayo ni pamoja na:

a) Gharama zilizotumika juu ya ardhi husika kwa mfano kuweka huduma muhimu kama vile barabara, maji, mitaro ama mifereji ya maji taka, umeme n.k.

b) Muda wa miliki utatolewa kwa kipindi au kwa vipindi tofauti tofauti ambapo kwa ujumla hautazidi miaka tisini na tisa. Vile vile Miliki inaweza kutolewa kwa kipindi cha mwaka hadi mwaka ama kwa muda mfupi zaidi kama itakavyoelekezwa na kamishna na kwa vyovyote vile vipindi hivyo visizidi miaka minne.

Haki miliki maalum iliyotolewa na kamishna muda wake. Hautapunguzwa mpaka makubaliano yafikiwe na mmilikaji.

Baada ya muda wa miliki kuisha na endapo mmilikaji atakuwa amezingatia masharti ya umilikaji kwa kadri inavyowezekana anaweza akapewa nafasi ya kumiliki tena kwa masharti ambayo kamishna ataamua kabla hati ya haki miliki mpya haijatolewa kwa mtu mwingine yoyote.

Baada ya muda wa miliki kuisha na kamishna ameona si vyema kummilikisha mmiliki ambaye muda wake umekwisha kwa kipindi kingine licha ya maendelezo ambayo yamekwishafanyika mmiliki hatalipwa fidia yoyote.

c) Kodi ya Kiwanja:

Mmilikaji wa kiwanja/shamba atawajibika kulipa kodi kama inavyoelekezwa na Sheria ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Kamishna wa Ardhi ataelekeza ni vipi kodi italipwa kwa mkupuo mmoja au kwa awamu au itakavyokuwa imeelekezwa kwenye hati ya umilikaji.

Kodi italipwa kwa kamishna wa ardhi au kwa afisa mteule kama itakavyoelekezwa na kamishna.

Katika kukadiria kiwango cha kodi ya ardhi kamishna atazingatia mambo yafuatayo;

(1) Eneo la kiwanja/shamba lenye haki miliki

(2) Matumizi ya ardhi yaliyoruhusiwa kwenye Hati ya haki Miliki

(3) Thamani ya ardhi inayotokana na mauzo/ upangishaji katika soka ambapo ardhi ipo.

(4) Thamani iliyotolewa na mthamini kama ndio thamani ya soko ya ardhi katika eneo husika ikiwa ni mjini au kwenye viunga vya mji.

(5) Kiasi cha kilemba kilichohitajika kulipwa wakati wa utoaji wa hati ya haki miliki.

Katika suala la kodi, kisheria kodi inapaswa kufanyiwa marekebisho katika muda usiopungua miaka mitatu yaani kila baada ya miaka mitatu kamishna atarekebisha kodi ya kiwanja. Kamishna pia anaweza kusamehe kodi kama ardhi itatumika kwa malengo fulani fulani mfano mahala pa kuzikia au kuabudia. Kodi kidogo inaweza kutozwa endapo huduma zitakazotokewa zitakuwa kama msaada kwa jamii na sio kwa biashara kwa mfano makazi ya kulelea wazee watoto yatima n.k

Lakini mara ardhi ambayo ilikuwa ikitumika kwa kuzikia, kuabudia au kutolea huduma za jamii na siyo kwa shughuli za biashara itakapobadilishwa matumizi yake kamishna atatoza kodi au atafanya marekebisho ya kodi inayoambatana na hati ya haki miliki hiyo kwa kadri atakavyoona inafaa.

Vile vile Waziri anaweza kumwelekeza kamishna kufanya marejeo kuhusu kodi inayopaswa kulipwa na watu wanaodai kushindwa kulipa kwa ajili ya umaskini ugonjwa waliokubwa na maafa au matatizo mengine ya namna hiyo. Marekebisho ya kodi yanaweza kurekebishwa kwa kupunguzwa ama kusamehewa kabisa.

Kamishna anayo mamlaka ya kufanya marekebisho ya kodi ya viwanja/ mashamba katika kipindi cha miaka mitatu mitatu.

Kutolipa au kuchelewa kulipa Kodi ya Kiwanja

Sheria inaelekea kuwa kama itatokea sehemu ya kodi au kodi yote haijalipwa ndani ya miezi sita ya muda wa kulipa riba ya asilimia moja kwa kila mwezi itatozwa kwa kodi ambayo itakuwa haijalipwa hadi hapo kodi itakapolipwa.

Vile vile ikumbukwe kwamba kupokelewa kwa kodi ya Kiwanja na serikali hakutakuwa kigezo kwa serikali kutobatilisha haki miliki endapo masharti na kanuni nyingine zilizoelekezwa moja kwa moja ama kutokana na sheria nyingine zilizopo zimevunjwa.

Mbali na maelezo hayo ya jumla itakuwa ni sharti kwa kila haki miliki iliyotolewa kwa lengo la ujenzi wa nyumba kuomba kibali cha kufanya maendelezo katika kiwanja kama inavyoelezwa na sheria ya mipango miji na kanuni nyingine za ujenzi mijini katika kipindi cha miezi sita mara baada ya kupewa hati ya haki miliki.

Vile vile watu wanaomiliki ardhi kimila watakuwa na haki halali na wataweza tu kuondolewa toka maeneo yao na kupelekwa kwinine iwapo tu kufanya hivyo kutasaidia kuwezesha utekelezaji wa masharti ya haki miliki iliyotolewa.