Kitabu cha Kiada kwa Mahakimu wa Mahakama za Mwanzo (39)

5.8 Haki za Binadamu Katika Tanzania

Haki za binadamu ziliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 hapo mwaka 1984 kupitia Mabadiliko ya Tano ya Katiba." Hii ilikuwa baada ya mapambano ya muda mrefu kati ya utawala wa nchi kwa upande mmoja na wale wanaharakati wa haki za binadamu waliokuwa wanapigania haki hizi kuwekwa rasmi katika katiba ya nchi tokea wakati wa uhuru. Kuingia kwa haki hizi muhimu katika Katiba yalikuwa mafanikio makubwa kwa wote wanaopenda haki. Hivyo kuna haja ya kuangalia kwa ufupi historia ya haki hizi katika nchi yetu ili kuweza kuzielewa vizuri na kuzienzi.

5.8.1 Haki za Binadamu Wakati wa Ukoloni

Kusema kweli wakati wa ukoloni wa Wajerumani na Waingereza hapakuwa na haki za binadamu katika nchi yetu. Ingawa wao wakoloni walikuwa waumini wakubwa wa haki hizi katika nchi zao, lakini hawakuja nazo huku. Wakoloni kama Carl Peters wa Kampuni ya Kijerumani ya Deutsch Ostafrika ambayo ilikuwa ya kwanza kutawala sehemu hii mara ya kwanza kabla ya ukoloni halisi kuja alikuwa mkatili mkubwa kwa wananchi. Alichapa watu viboko na kuwafanyisha kazi kama punda. Kunyongwa kwa wazalendo lilikuwa jambo la kawaida lililofanywa hadharani ili kuwaogofya watu wengine ili waendelee kuutumikia ukoloni kwa uaminifu, adabu na bila ubishi. Wenzake waliofuata hawakuwa na nafuu.

Mazungumzo kuhusu haki za binadamu yalianza katika mwisho wa miaka ya hamsini wakati uhuru ulipoanza kunukia. Waingereza walipoona kwamba ni vigumu sana kushindana na upepo wa uhuru ambao ulikuwa unavuma kwa nguvu katika Bara lote la Afrika na kwingineko katika dunia ya tatu walianzisha mazungumzo na wazalendo kuhusu mpangilio wa kutoa uhuru. Ni katika mazungumzo haya ndipo mambo ya haki za binadamu yalipokuja. Waingereza wakasema kwamba Katiba ya Tanganyika huru ni lazima iweze kulinda haki za binadamu kwa kuwa na sehemu inayozilinda kwa dhati haki hizi (Bill of Rights). Jambo hili lilibishiwa kwa nguvu sana na wapigania uhuru katika chama cha Tanganyika African National Union (TANU).

Wao walitoa sababu mbili muhimu kwa msimamo huu. Kwanza, kwamba serikali mpya itakuwa serikali iliyochangamka na inayotaka kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi na katika serikali ya namna hiyo hapakuwa na nafasi kwa vitu kama haki za binadamu. Kilichokuwa muhimu kwa wanasiasa au watawala hawa wapya ni kuwa na Maadili ya Kitaifa (National Ethics) ambayo yatawaongoza katika kazi zao. Pili, wakati huo mahakama zote zilikuwa zinaendeshwa na mahakimu na majaji wazungu.

Hivyo, wangechukulia mwanya wa kuwa na haki hizi katika Katiba kutangaza maamuzi mengi ya serikali kuwa batili kwa kukiuka haki za binadamu. Hivyo, Waingereza hawakuweza kuwaridhisha wazalendo kukubali kuweka haki hizi muhimu katika Katiba ya Uhuru (Independence Constitution) ya Mwaka 1961.

5.8.2 Haki za Binadamu Baada ya Uhuru

Katika Katiba ya Jamhuri iliyofuata hapo mwaka 1962 haki za binadainu hazikuwekwa tena. Kilichofanywa ni kuweka haki hizo kwenye utangulizi wa Katiba (Preamble) ili kuonyesha kwamba serikali ina nia ya kuziheshimu haki hizi. Kisheria utangulizi wa Katiba, kama ulivyo utangulizi wa sheria yoyote ile, siyo sehemu ya Katiba. Hivyo, mtu hawezi kwenda mahakamani na kudai kwamba haki zake za msingi kama zilivyoainishwa kwenye Utangulizi wa Katiba zimekiukwa. Msimamo huu wa sheria umeelezewa vizuri na Mheshimiwa Jaji Biron katika kesi ya Hatimali Adamji v. East African Posts and Telecommunications Corporation." Pia umerudiwa kwa ufasaha zaidi na Mheshimiwa Jaji Kisanga wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania katika kesi ya Attomey-General v. Lesinoi Ndeinai & Joseph Selayo Laizer and Two Others."’ Hivyo, kwa maana ingine, kuwekwa kwa haki za binadainu katika utangulizi wa Katiba hakukuwa na maana yoyote ile kwa mwananchi wa kawaida wa Tanzania.

Jambo hili la kuweka haki na uhuru muhimu wa mwananchi katika utangulizi wa Katiba lilirudiwa tena katika Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1965 (Interim Constitution of 1965). Kilichoongezeka hapa ni kwamba Katiba ya chama pekee tawala wakati huo TANU iliwekwa kama Nyongeza (Schedule) ya Katiba hiyo. Katiba ya TANU, kama chama cha ukombozi, ilikuwa imeainisha haki nyingi muhimu za binadamu kama vile usawa na kadhalika.

Kisheria, Nyongeza, tofauti na utangulizi, ni sehemu ya Katiba. Hivyo, ilikuwa ni rahisi kuweza kwenda mahakamani na kudai haki hizi, siyo kupitia utangulizi bali kupitia nyongeza.

Hii ilifanyika kwa mafanikio katika kesi ya Thabiti Ngaka v. Regional Fisheries Officer’’ ya Morogoro ambapo madai yalikuwa kuhusu haki ya mfanyakazi kulipwa mshahara wake. Vile vile, pamoja na kuweka Katiba ya TANU kama Nyongeza katika Katiba, Serikali iliamua kuunda ofisi ya Mchunguzi Maalum (Ombudsman). Hii ilikuwa Tume ya Kudumu ya Uchunguzi (Permanent Commission of Enquiry au PCE). Tume hii iliwekwa ndani ya Katiba na pia ilitungwa sheria ya kuelezea mipaka na utendaji wake wa kazi."’

Hali hii itiendelea hadi mwaka 1977 Tanzania ilipopata Katiba ya Kudumu. Hii ilikuwa miezi michache baada ya kuunganishwa kwa vyama viwili tawala yaani Afro Shiraz Party (ASP) cha Zanzibar na Tanganyika African National Union (TANU) cha Tanzania Bara kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa bahati mbaya, Katiba mpya ya kudumu haikuwa na haki za binadamu ndani yake (ila utangulizi ulibaki pale pale) na pia Katiba ya Chama tawala CCM haikubakizwa kama Nyongeza katika Katiba hii. Hivyo, hapakuwa na njia tena ya kudai haki hizi muhimu kisheria.

Haki za binadamu zilikuja kuingizwa ndani ya Katiba mwaka 1984 kufuatia Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya Nchi. Hata hivyo, mabadiliko haya hayakuanza kutumika mara moja. Serikali ilipewa muda wa miaka mitatu ili kusawazisha mambo katika sheria zake. Hii ilikuwa muhimu"kwa sababu kulikuwa na sheria nyingi ambazo zilikiuka moja kwa moja haki za binadamu na uhuru wa mwananchi. Kuahirisha kwa haki hizi na uhuru muhimu kwa mwananchi kulimaanisha kwamba ingawa Serikali iliwajibika kuheshimu haki hizi, lakini pindi zikikiukwa basi mwananchi aliyeathirika na ukiukwaji huo hangeweza kwenda mahakamani na kufungua kesi na kufanya madai. Hata hivyo, baada ya miaka mitatu Serikali ilijikuta njia panda. Ilikuwa imebadili sheria moja tu. Hivyo, ilibidi iamue. Kuendelea kuzuia haki za binadamu kutumika nchini au iziruhusu zianze kutumika. Kwa busara zake, Serikali iliamua haki za binadamu zianze kutumika rasmi Tanzania mwaka 1988. Jukumu la kuamua ni sheria gani inakiuka haki hizi ziliachiwa, mahakama.

Itaendelea toleo lijalo

Ijue Pasaka, undani na matukio yake(5)

l Kuhukumiwa kwa Yesu

l Yesu sasa anafufuka katika wafu kaburi sasa tupu

l Umuhimu wa Maana ya Wokovu ya Ufufuko

Inatoka toleo lililopita

Katika toleo letu lililopita, tuliishia katika kipengele kinachosema "Yesu Kristo alizikwa" na hasa "Kristo kaburini katika mwili wake". Sasa endelea na sehemu hii ya mwisho inayotufikisha katika kilele cha Maadhimisho ya Kufufuka kwa Bwana Wetu Yesu Kristo (PASAKA) Jumapili hii.

Kwanza, tunaanza na ufafanuzi mfupi mintarafu kipindi cha Kwaresima ambacho huishia Siku ya Alhamisi Kuu. (siku arobaini kabla ya Siku ya Pasaka).

Hapa, Kanisa huenda kukutana na Fumbo la Pasaka likijitayarisha kwa matendo makuu.

Kanisa hushirikiana na Kristo katika kushinda mabaya duniani yanayojidhihirisha kwa dhambi ya wanadamu ya kutomtii Mungu.

Adhimisho la Pasaka huanza ALHAMISI KUU jioni na kuendelea mpaka PENTEKOSTE. Katika maadhimisho hayo, tunaZIona wazi sehemu mbili kuu.

Sehemu ya kwanza, ni maadhimisho ya Pasaka yenyewe, siku tatu takatifu za mateso, kufa na kufufuka kwa Bwana.

Inawapasa Wakristo kuyaona matendo hayo matatu kama tendo moja. Sherehe hii ya Kanisa huyaadhimisha matendo hayo kwa sherehe ya pekee.

Kanisa lote huzamishwa katika Fumbo la Pasaka ya Kristo, maana yake huzamishwa katika mateso, kufa na kufufuka kwa Kristo.

Katika sehemu ya pili, Kanisa huufurahia na kushangilia ufufuko huu kwa muda wa siku 50.

Kama kwamba linaonja maisha mapya liliyoyapata na kukaa pamoja na Bwana Mfufuka, anayefunua utukufu wa maisha yake yaliyotukuka.

Siku arobaini baada ya Pasaka, Kanisa huadhimisha Siku ya Kupaa Bwana.

Tukio hili ni ubainifu wa ufufuko na wa maisha mapya pamoja na Mungu.

Katika siku za mwisho za shangwe la Pasaka, Kanisa humngojea Roho Mtakatifu kama kuwako kupya kwa Kristo katika Kanisa lake, ndiyo sikukuu ya Pentekoste.

Ni siku ya kuzaliwa kwa Kanisa. Kutoka siku hiyo linaanza kutimiza kazi kubwa ya utume, yaani kutangaza habari njema ya ufufuko.

Kipindi kinachofuata Pentekoste ni Kipindi cha Mwaka. Nalo Kanisa huadhimisha wakati huu maendeleo ya ukombozi na kutimiza kwake mpaka siku ya ujio mpya wa Kristo.

Tunakumbushwa ujio huo mpya wa Kristo katika utukufu wake, ndio kurudi kwake Kristo katika sehemu ya kwanza ya majilio mpaka tarehe 16 ya mwezi Desemba.

Sasa, tuendelee na muendelezo wa chapisho letu.

"Hutamwacha Mtakatifu Wako Aone Uharibifu"

Kifo cha Kristo kilikuwa kifo halisi kwamba kilimaliza uwepo wake wa kibinadamu hapa duniani. Lakini kwa sababu ya muungano ambao nafsi ya Mwana ilishikamana na mwili wake mwili wake, haukuwa maiti ya uharibifu kama miili mingine kwa sababu "Haikuwezekana ashikwe na mauti" (Mdo 2:24) na zaidi ya hayo "nguvu ya kimungu iliukinga mwili wa Kristo na uharibifu." Matamko hayo yote mawili yanaweza kusemwa juu ya Kristo:

"Alikatiliwa mbali kutoka nchi ya walio hai, " na "mwili wangu nao utakaa katika matumaini kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu "ufufuko wa Yesu siku ya tatu" ulikuwa ni ushahidi wake, kwani ilisadikiwa kuoza kulianza kufanyika toka siku ya nne baada ya kifo.

"Kuzikwa pamoja na Kristo"

Ubatizo, ambao alama yake ya asili na timilifu ni kuzamishwa, waashiria bayana kushuka kaburini kwa Mkristo anayefia dhambi pamoja na Kristo ili aishi maisha mapya. "Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.

MUHTASARI

Kwa faida ya kila mtu, Yesu alionja mauti (rej Ebr2:9). Ni Mwana wa Mungu kweli aliyefanyika mtu, aliyekufa na kuzikwa.

Kipindi cha Kristo kaburini nafsi yake ya kimungu iliendelea kumiliki roho yake na mwili wake, ingawa vilikuwa vimetenganishwa kwa kifo. Kwa sababu hiyo mwili wa Kristo uliokufa "haukuona uharibifu" (Mdo 13:37).

Kipengee 5

"YESU KRISTO ALISHUKA KUZIMU, SIKU YA TATU ALIFUFUKA KUTOKA WAFU

Yesu "alishuka mpaka pande zilizo chini ya nchi.

Aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote". Kanuni ya mitume yaungama, katika kipengee hicho hicho cha imani, Kristo kushuka kuzimu na ufufuko wake kutoka wafu siku ya tatu, kwa sababu katika Pasaka yake ni hasa kutoka vilindi vya mauti alifanya uzima ububujike:

Kristo, Nyota ya asubuhi, aliyetoka kuzimu, akawaangaza wanadamu wote kwa utukufu, naye anaishi na kutawala daima na milele. Amina

Ibara 1:

KRISTO ALISHUKA KUZIMU

Uthibitisho wa mara nyingi wa Agano Jipya kwamba Yesu "aliinuliwa toka wafu" wamaanisha kwamba kabla ya ufufuko alikaa katika makao ya wafu.

Hii ndiyo maana ya awali iliyotolewa katika mahubiri ya kitume juu ya Yesu kushuka kuzimu: Yesu kama watu wote aliyapitia mauti na katika roho yake aliunganika nao katika makao ya wafu.

Lakini alishuka kule kama Mwokozi akitangaza Habari Njema kwa roho zilizokuwa zimefungiwa kule.

Maandiko huyaita makao ya wafu "kuzimu" Sheol kwa Kiaramayo au "hades" kwa Kigiriki, kwani wale waliomo humu hunyimwa kumwona Mungu.

Ndivyo iliyo kwa wote waliokufa, wawe ni waovu, au wenye haki, wakiwa wanamngoja Mkombozi; hii haina maana kwamba kura yao ni sawa, kama aonyeshavyo Yesu kwa njia ya mfano wa Lazaro maskini, ambaye alipokelewa "kifuani mwa Ibrahimu."

"Ni hasa roho hizi takatifu, zilizomngojea Mwokozi wao kifuani mwa Ibrahimu, ambazo Kristo aliziokoa aliposhuka kuzimu." Yesu hakushuka kuzimu kuwaokoa walaanifu, wala kuangamiza moto wa ulaanifu, bali kuwaweka huru wenye haki waliomtangulia.

"Nao waliokufa walihubiriwa Injili" Kushuka kuzimu ni utimilifu wa ujumbe wa Habari Njema ya wokovu.

Hii ndiyo awamu ya mwisho ya utume wa kinabii wa Yesu, ambao unabanwa na wakati, lakini mpana sana katika maana yake halisi ya kuenea kwa kazi ya ukombozi kwa watu wote, wa nyakati zote, na wa mahali pote, kwani wote wanaookolewa wamefanywa washiriki wa ukombozi.

Kristo alishuka katika kilindi cha mauti ili "wafu wasikie sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai."

Yesu, "Mkuu wa uzima," kwa njia ya mauti alimharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani Ibilisi, awaache huru wale ambao, kwa maisha yao yote kwa hofu ya mauti, walikuwa katika hali ya utumwa.

Tokea hapo Kristo Mfufuka "anazo funguo za mauti na za kuzimu" na "kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani na vya chini ya nchi".

Leo kuna ukimya mkubwa duniani, ukimya mkubwa, na unyamavu, ukimya mkubwa kwa sababu mfalme amelala usingizi; dunia ilikuwa katika hofu kubwa na ikawa kimya, kwa sababu Mungu katika mwili, alilala usingizi na akawaamsha wale waliokuwa wamelala tangu zamani za kale. Anakwenda kumtafuta Adamu mzazi wetu wa kwanza, kondoo aliyepotea. Anataka kuwatembelea wale wanaokaa gizani na katika uvuli wa mauti. Itaendelea toleo lijalo