Wanaolia msibani hulizwa na mengi siyo kifo tu

l Njiani, wengine hucheka, wanapokaribia msiba, wanalia kwa sauti

l Wengine hulia huku wakishangilia kupata madaraka, mali

l              Wenye uchungu zaidi, ni wanaolia sana, au wasiolia?

Na Mwandishi Wetu

KILIO cha machozi na sauti kubwa katika msiba, kwa baadhi ya makabila huchukuliwa kama kipimo cha upendo wa mtu kwa marehemu, ingawa wengine hucheka wakiwa njiani hadi wanapokaribia nyumba ya msiba na kuanza kulia kwa sauti.

Ni dhahiri kuwa msiba unapotokea, huwa kuna makundi tofauti miongoni mwa waombolezaji wakiwamo wenye huzuni ya kweli na wanaotimiza wajibu wa kuhuzunika na hata kulia ili wasionekane kuwa tofauti na wengine.

Wapo wanaofurahia moyoni ili ama washike madaraka, au kurithi nafasi ya marehemu, wapo wanaoshukuru Mungu kwani kwa kipindi cha maombolezo watautumia msiba huo kupunguza makali yao ya maisha, wapo wanaotumia nafasi ya kifo au maafa kupora mali za marehemu katika janga na kutaka kujitajirisha, na pia wapo wanaolia kwa maana halisi ya kulia kwa kuondokewa na wapendwa wao.

Kama ilivyo kawaida ya binadamu na hata viumbe wengine wakiwamo ndege aina ya kunguru, wengi huhuzunika ikiwa ni hatua muhimu katika msiba; hatua ambayo kupitia kwayo, wafiwa hujirekebisha na mazingira na hivyo, kuukabili na kuupokea msiba kama ulivyokuja.

Ingawa mara nyingine mtu anaweza kulia kwa furaha, bado kuhuzunika kwa wafiwa mara nyingi huhusisha kulia ingawa sio sharti wala kipimo muhimu cha huzuni.

Katika jamii nyingi, kulia huchukuliwa kama hatua muhimu inayowaunganisha waombolezaji na imekuwa tabia inayoelekea kuzoeleka kuwa, katika msiba mtu asipolia, hutazamwa kama muujiza au mchawi na pengine kwa wenye imani potofu za ushirikina, pengine hudiriki hata kumhusisha muombolezaji huyo asiyelia kama mtu ambaye pengine amehusika au anayefurahishwa na kifo hicho. Katika mtazamo wa kawaida, kulia msibani kwa wafiwa inaonyesha kushindwa kwa juhudi zao za kupambana na kifo. Kwa kiasi kikubwa huonekana kama ishara ya kuzidiwa uwezo au kukata tama.

“Unaweza kukuta watu wakiwa wanaelekea msibani, huko njiani kote wakiwa wanazungumza na kucheka kwa furaha, lakini wanapofika karibu na nyumba yenye msiba, huanza kupiga kelele za vilio kama vile sio wao waliokuwa wakicheka kwa furaha muda mfupi nyuma,” liliandika Gazeti moja nchini.

Ni dhahiri kuwa msiba wa mtu unaemjua unahuzunisha uwe unamhusu ndugu, mpenzi, jamaa au jirani, ukweli unabaki palepale kuwa msiba unahuzunisha.

Ukweli huu unabainisha kuwa, sio kweli kwamba wote wanaolia sana katika msiba huwa wanalia kwa sababu wana huzuni na majonzi mengi kuliko wengine, bali wapo wanaolia ili wasionekane na jamii kuwa wamefurahia kifo cha marehemu.

Wataalamu wa masuala ya kisaikolojia wanasema kuwa, watu wenye huzuni na mshituko mkubwa, mara nyingi huwa hawana uwezo wa kulia.

Wanasema, mtu anayeweza kulia sana ni yule mwenye majonzi na machungu ya kawaida au ya chini ya wastani.

Sababu za wanasaikolojia hao ni kuwa,  mtu mwenye majonzi makubwa hususan yatokanayo na kufiwa, huwa haamini hayo yaliyotokea na kwa kutoamini hivyo, huwa vigumu kulia.

Kwa kawaida, watu hawa huwa wanaanza kulia baada ya mazishi kwani ndipo sasa huamini yaliyotokea na wakati mwingine, hata baada ya siku kadhaa kutokana na matokeo halisi ya kifo hicho.

Hii ni pamoja na namna wafiwa wakiwamo watoto, ndugu na mjane wanavyoishi katika majonzi na maisha yao yanavyokuwa baada ya kufiwa. Hili pia, linahusiana na hali anavyoiona ikimkabiri baada ya kifo hicho.

Hii haina maana kuwa wanaolia baada ya mazishi ndio pekee wenye uchungu na majonzi au pengine kuliko wote wanaolia sana kabla ya mazishi, hapana.

Jambo la msingi hapa ni kuonesha tofauti na ndio maana wakati mwingine mtu anaweza kuwa na furaha hadi akalia na mwingine akawa na huzuni kiasi cha kumfanya acheke.

Wanasaikolojia wamebainisha kuwa kuna kulia zaidi ya namna moja.

Miongoni mwa aina hizo, ni ile ya kulia kutokana na uchungu wa kweli, ipo aina nyingine ambayo huibuka kama mazoea na nyingine ni ile ya kulia kwa kuambukizwa kutokana na vilio na kauli za waliaji wengine na pia, athari zinazotokana na kifo hicho katika maisha.

Watu hawa wenye uchungu mkubwa sana huwa na ugumu katika kulia hasa baada ya msiba, lakini kulia kwa watu hawa siyo kule kulia kwa kelele na vurugu, bali wao hulia kwa ishara na hata kukosa nguvu ya kutoa sauti na kelele nyingi zenye shutuma na maelezo mengi kumhusu marehemu na nafasi anayoiacha.

Waliaji wa namna hii ni wale wanaoguswa kwa namna ya pekee na kwa undani zaidi kwani hata kama marehemu alikuwa hawasaidii kwa lolote, bado hujikuta wakiwa na uchungu mintarafu kuondoka kwake.

Wakati mwingine baadhi yao huwa wanashutumu kifo na kuzungumza mengi kumhusu marehemu ingawa huwa haitokei mara nyingi.

“Kuna wale watu ambao hulia kwenye msiba kwa sababu ya mazoea, yaani wameshajizoesha kwamba wakisikia mtu fulani wanayemfahamu kafa ni lazima walie bila kujali ukaribu wao au kujali kama wana sababu ya msingi zaidi ya kuwafanya walie zaidi ya hiyo ya kumfahamu,” inasema sehemu ya gazeti hilo.

Wanawake, ni wanachama wakubwa wa kundi hili.

Kuna watu ambao huwa inaelezwa kwamba wana machozi ya karibu, miongoni mwao ni hawa ambao wasikiapo  fulani wanayemfahamu amekufa, na hasa wanapokwenda kwenye misiba yao ni lazima walie.

Inawezekana hawakuwa karibu sana na marehemu, bali tu kwa sababu wanamfahamu na wamefika kwenye msiba wake.

Kuna watu ambao hulia kwa kulizwa. Watu hawa wanapokwenda misibani huwa wanachotwa kirahisi na haraka na kauli za waombolezaji na hasa zile za wale wanaolia huku wakitoa kauli kali na zenye kusikitisha kuhusu marehemu au kifo.

Kuna watu ambao wanapolia hutaja kila kitu alichokuwa akikitoa marehemu; au kukifanya na hata namna alivyosema dakika chache kabla hajafa au mengine ya aina hiyo. Waliaji hao tunaweza kuwaita “wenye hisia kali”

Kwa kusikia kauli za aina hiyo, baadhi ya watu huwa wanajibainisha au kujiweka karibu sana na marehemu na hivyo, kujikuta wakitokwa na machozi. Kulia huku hata hivyo huwa ni kulia kusiko na nguvu, mliaji hutokwa na machozi kidogo na kuyafuta.

Mara nyingi anaweza hata asionwe na watu alionao karibu.

Aina nyingine ni ile inayohusisha kulia kwa nguvu sana na kuropoka maneno mengi kiasi kwamba hufikia hatua ya kuwa kero hata kwa waombolezaji wengine.

Hapa waliaji huwa wanalia bila kujali mazingira na bila kujali muda.

Imebainika kwamba wengi wa waliaji hawa huwa ni wale ambao wanajua wazi kwamba kifo cha mhusika kimewaacha pabaya kimaisha.

Unaweza kukuta marehemu ndiye aliyekuwa akiwapa kila kitu katika maisha yao hasa mahitaji ya msingi kama kula, kuvaa na hata makazi. Kinachowaliza siyo kumkosa marehemu au hata kama ni pamoja na kumkosa marehemu, lakini kwa sehemu kubwa ni kukosa huduma hizo na kuwaza ugumu wa maisha yaliyo mbele yao.

Wengi kati ya watu hawa ni ndugu, wazazi, watoto, waume au wake wa marehemu.

Hata ukisikiliza kauli zao katika kulia kuna wakati hutaja hofu ya kuishi peke yao, hofu za kushindwa kumudu na hofu za kuukabili ukweli wa kujitegemea. “Wewe ndiye uliyekuwa ukinijali kwa hii hali yangu, nani atakayenijali tena…” hizi ni  miongoni mwa kauli ambazo zinaweza kusikika sana.

Miongoni mwa hawa waliaji kuna wale ambao kifo cha mhusika kina maana wao kupoteza kitu fulani (kama kazi) kuonewa, na familia kusambaratika. Inawezekana marehemu alikuwa akiwalinda wasifukuzwe kazi au kunyang’anywa mahali au eneo au kitu kilichokuwa kinawapa riziki.

Kuna wakati inawezekana marehemu alikuwa ndiye anayetatua migogoro mingi na mikubwa ya kifamilia na hivyo, kufa kwake huchukuliwa kama kusambaratika kwa familia.

Siyo kwamba watu wanaolia sana kwa sababu ya kujua kwamba kifo cha mhusika kitawapa mzigo mkubwa kimaisha, huwa hawana uchungu na marehemu.

Kwa sehemu kubwa wana uchungu wa kumpoteza mhusika kama ambavyo wengine wana uchungu na

pengine wana  uchungu zaidi, lakini ukweli ni kwamba wanazingatia zaidi watakavyokabili ugumu wa maisha.

Ukiangalia kwa makini utaona kwamba wengi kati ya wale wanaolia kwenye misiba, hulilia nafsi zao zaidi kuliko kumlilia marehemu.

Hata hivyo, ukweli unabaki palepale kwamba kulia sana kwenye misiba hakumaanishi kwamba ulikuwa unampenda sana marehemu, sana sana huonesha udhaifu wa waliaji.

Kulia sana kuna maana ya mtu kujaribu kukataa ukweli wa kimaumbile ambao huwa haubadilishwi na kulia au kucheka, kuomba au kulalamika.

Dini zetu kuu zinafahamu sana jambo hili la mtu kutoshindana na maumbile na kuliheshimu ukweli huu. Zinasisitiza watu kutolia hasa kwa kelele katika misiba kwani kwa kufanya hivyo ni sawa na kumdhihaki Mungu.

Ni kumdhihaki kwa sababu kifo au uhai ni maamuzi  yake na hivyo, kulia ni sawa na kumwambia kwamba amekosea.

Inabidi jamii ikubali kwamba hakuna anayeweza kuishi milele isipokuwa Mungu ambaye alikuwapo tangu milele, yupo hadi sasa na bado atakuwapo katika milele yote.

Lazima watu waone umuhimu wa kuishi maisha ambayo kifo kinapotokea, iwe ni miili tu iliyokufa lakini, imani, mawazo na busara za marehemu ziwe bado hai.

Huo ni wakati ambapo wazazi, ndugu na marafiki,  hawana budi kuwasaidia wanaowategemea ili wajitegemee na kuepuka kuendelea kuwa wategemezi.

Kama ni mume, basi amruhusu mkewe kuanza kufanya shughuli ambazo zitaweza kumfanya ajitegemee badala ya kumfanya kuwa mtu wa kupewa tu. Kujitegemea huku kutamfanya mke kumlilia kwa sababu alikuwa anampenda na kifo chake kimemgusa na siyo kumlilia kwa sababu sasa atashindwa kuwapeleka watoto shuleni, na kuwapatia huduma zingine.

Hata kwa ndugu ambao kwa kiasi kikubwa wanamtegemea mtu fulani dawa ni kuwafanya wajitegemee na siyo kuona ufahari kwa kuwa tegemezi.

Lakini, kubwa zaidi ni kwamba kulia kwa sababu fulani amekufa na sasa maisha yetu yatakuwa magumu ni udhaifu mbaya sana.

Kulia kwa namna hii kunaonesha ni kwa kiasi gani hatujiamini na ni kiasi gani tunadhani utu na ukamilifu wetu uko mikononi mwa watu wengine.

Tunapolia kwa sababu fulani amekufa na sasa maisha yatatuwia magumu, tunadhihirisha kwamba hatuko kamili na tunahitaji kujitazama upya.

(JITAMBUE Mei 23-29, 2001).

‘Mnaokosea makusudi kutegemea msamaha, mnajidanganya’

Na Damasus Mtalaze, Dodoma

MUNGU hatoi msamaha kwa makosa yanayotendwa kwa makusudi na watu eti ili baadaye waungame; Amesema Paroko wa Parokia ya Kibakwe, Jimbo Katoliki la Dodoma.

 Akihubiri parokiani kwake hivi karibuni, Paroko huyo, Padre Faustin Mwenda,  alisema  baadhi ya watu hufanya makosa kwa makusudi huku wakitegemea kupata msamaha baada ya kuomba radhi na kuungama hali aliyosema, ni kinyume na mapenzi ya Mungu.

 “Wengine wanatenda makosa kwa makusudi eti kwa kuwa Injili inawalinda, hao wanajidanganya kwa sababu Mungu husamehe makosa yanayotokana na kushindwa kuyakwepa au yanayofanywa bila mtu mwenyewe kujua kuwa anafanya kosa; sio kufanya mambo makusudi ukitarajia kusamehewa,” alisema Padre Mwenda.

Akaongeza, “Siku zote; mtu asiuangalie wema wa Mungu kwa kuuchezea maana ukicheza na huruma ya Mungu, ujue unacheza na ghadhabu yake.”

 Akitoa mfano, Padre Mwenda, alisema kuwa hukumu dhidi ya Adamu na Hawa, inatokana na kosa lililowaponza la kudharau na kukosa kuitii Amri ya Mungu na hivyo, wakala tunda walilokatazwa wakitegemea kuwa watasamehewa kwa kuwa tangu awali walikuwa wakitii maagizo ya Mungu isipokuwa hilo moja.

 “Ukiamua kutii, ni vema utii kabisa maana Mungu hutoa adhabu palepale unapoanza kutenda kosa,” alionya.

 Alisisitiza kuwa, sio vema kwa mtu yeyote kutatiza maisha ya mwingine kwa kutomsamehe anapokukosea hali wewe mwenyewe ukimkosea mtu, unahitaji kusamehewa.

 

Wanasayansi wakiri sala zinatibu kuliko dawa

l Profesa asema imani katika Mungu ina manufaa

l ‘Hatutaki kuuza dini kwa jina la sayansi’

Na Joseph Sabinus

MANENO “Imani katika matendo,  sasa yameleta maana mpya kwa jamii duniani kote hasa baada ya wanasayansi kuthibitisha kuwa imani katika Mungu, ni dawa yenye nguvu dhidi ya magonjwa.

Katika makala ya “Imani Ni Dawa Yenye Nguvu”, iliyoandikwa na Phyllis McIntosh na kuchapishwa katika kitabu cha “Than Diabetes,” kundi la wanawake lilikuwa likikutana kwa wiki mjini humo ili kufanya mazoezi ya  kiroho na kimwili sambamba na dawa zilizoambatana na baraka za asubuhi za Wayahudi.

Roberta Schweitzer, Mmoja wa washiriki ambaye ni Muuguzi, alifurahishwa na utulivu uliokuwapo kutokana na sala zilizokuwa zikiendelea.

Schweitzer ambae ni Profesa Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Nevada, Reno, alifanya utafiti akilinganisha manufaa ya sala na mwenendo wa utamaduni.

Alisaidia pia kuandaa mpango maalumu wa kuwafundisha watu kutumia matibabu ya kiroho kukabiliana na magonjwa.

Dhana kuwa mwili unaweza kuponywa kwa imani ya kiroho, si kitu kigeni. Watu wamekuwa wakisikia mara nyingi kuwa wagonjwa wanapona katika imani na maombi baada ya kuugua kwa muda mrefu au hata kupona  na pengine, kuishi na maradhi kwa muda mrefu kuliko hata madaktari walivyofikiri kuwa inawezekana.

Kwa sasa, jambo lililo jipya, ni kwamba imani ya kidini sasa inakuwa chanzo  na msukumo wa sayansi duniani.

“…Hatuwezi kuthibitisha kisayansi kuwa Mungu anaponya, lakini ninaamini kuwa tunaweza kuthibitisha kuwa imani katika Mungu ina manufaa makubwa,” alisema Dk. Dale A. Matthews ambaye ni Profesa Mshiriki katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Georgetown, kilichopo Washington,D.C.

“Mashaka yaliyopo ni madogo sana kuwa afya ya kidini katika imani na matendo, inaweza kuwasaidia watu kupata nafuu.”

Nguvu za ushahidi wa wanasayansi zinasema kuwa zaidi ya tafiti 30 zimebaini kuwapo uhusinao wa kiroho (imani ya kidini), na maisha marefu ya watu.

Katika utafiti uliofanywa kwa Wacarifonia 5286, ilibainika kuwa Wanakanisa wana kiwango kidogo cha uwezekano wa vifo kuliko wasio na dini, ukiachilia mbali vigezo vinavyotokana na tabia na matatizo ya kuvuta sigara, unywaji pombe, vitambi na kutofanya kazi na mazoezi.

Pia, katika tafiti 8 juu ya kansa, tafiti 7 zilibainisha kuwa, wanaojitoa na kujishirikisha kikamilifu katika imani za kidini, wana dalili chache na wana matokeo bora ya kiafya kuliko wasiojishirikisha na imani za kidini.

Tafiti nne pia kati ya tano zilifanywa juu ya mgandamizo wa damu katika mwili wa binadamu, tafiti nne kati ya sita juu ya ugonjwa wa moyo na tafiti nne kati ya tano juu ya afya kwa jumla, zikabainisha kuwa wanaojihusisha na imani za kidini wanadalili chache au wana nafuu zaidi kuliko wasiojihusisha kabisa na dini.

Utafiti mwingine ukabainisha kuwa, watu wenye imani kali za kidini, hawana mwelekeo na wala hawavutiki katika unywaji pombe, kujiua na hata kushiriki mambo mbalimbali ya uovu.

Uchunguzi mwingine wa kina umeonesha kuwa muunganiko baina ya dini na afya, unavuka umri, jinsia, utamaduni na mipaka ya kijiografia.

Uchunguzi huo unazihusisha pia, zaidi ya tafiti 200 zilizothibitisha kuwa imani ya kidini ni kigezo muhimu katika kupambana na maradhi, alisema Jeffrey S. Levin, Profesa wa Eastern Virginia Medical School huko Norfolk.

Levin alibaini uhusiano baina ya afya njema na dini katika tafiti zilizowahusisha watoto na wazee Waprotestanti wa U.S., Wakatoliki wa barani Ulaya, Wabudha Wajapan na Wayahudi wa Israel walioishi kati ya miaka ya 1930 na 1980 wakisumbuliwa na maradhi sugu.

Mintarafu ni jinsi gani imani inaonekana kuwa na nguvu za kinga kiasi hicho, wataalamu wanatoa majibu mbalimbali.

“Tabia ya kujitoa katika imani za kidini, huwawezesha watu kushughulikia vema magonjwa na hasara,” anasema Dk. Harold G. Koeng, Mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Dini, kiroho na kifya katika Chuo Kikuu cha Duke University Medical Center.

Kusali huleta mabadiliko mengi ya manufaa katika mwili. Dk. Harvard Benson wa Havard Medical School, anasema watu wanaposali, hupunguza mgandamizo mkubwa wa damu na kuweka katika hali ya utulivu na ukawaida, kiwangi cha kupumua na mapigo ya moyo.

Kusali rozari kwa mfano, kunahusisha hatua kama hizo kuwa ni wajibu katika mapumziko na uhuru (utulivu).

Benson anazidi kusema kuwa, wanaochagua imani za kidini huwa katika nafasi kubwa ya kufaidi kama wakiiweka imani yao katika Mungu.

Katika utafiti mwingine kuthibitisha nguvu za sala kuwa bora katika uponyaji, Dk. Biyrd aliwagawa wagonjwa wa moyo 393 wa Hospitali ya San Fransisco General Hospital Medical Center, katika makundi mawili.

Kundi la kwanza, lilifanyiwa maombi na Watafiti Wakristo nchini kote, lakini kundi lingine halikufanyiwa maombi na sala hizo. Hata hivyo, wagonjwa hawakujua kuwa walikuwa katika kundi lipi katika ya hayo.

Kundi lililoombewa, lilibainika kuwa na matatizo kidogo zaidi ya magonjwa yao yakiwamo matatizo ya amonia, kushindwa kufanya kazi vizuri kwa moyo na hao walihitaji kiasi kidogo sana cha dawa  aina ya Antibaiotiki kuliko kundi ambalo halikuombewa.

Madaktari nao ni waamini wazuri sasa.

Dk. Dossey, hatimaye alishawishika juu ya nguvu za sala na akaanza  kuwaombea wagonjwa wake kwa sala zake binafsi.

Hata hivyo, yeye na wenzake, hatimaye wakaitahadharisha jamii katika eneo hilo kwa kusema, “Hatutaki kuuza dini kwa jina la sayansi,” alisema na kuongeza kuwa, Watu wanahitaji kufanya uchaguzi wao wenyewe.”

Mpaka sasa, vituo vya afya kwa kutambua umuhimu wa sala na maombezi, vimeanza kuwa makini na uhusiano ulipo baina ya afya na imani.

Mikutano juu ya roho na afya imekuwa ikidhaminiwa na Harvard Medical School, pamoja na Mayo Clinic.

Karibu nusu ya Shule za Kitabibu za U.S, sasa zinatoa kozi juu ya mada ya uhusiano baina ya afya na imani.

Katika utafiti wa madaktari 296, katika mkutano wa American Academy of Family Physicians, asilimia 99 walisema wanaamini kabisa kuwa imani za kidini zinachangia kwa kiasi kikubwa katika uponyaji.

Walipoulizwa juu ya uzoefu wao binafsi, asilimia 63 ya madaktari hao, walisema Mungu aliwasaidia kuboresha hali zao za kitabibu.

Kwa uwazi kabisa, hata wagonjwa wao wanakubali kuwa SALA NI KIFAA CHENYE NGUVU KATIKA UPONYAJI.

“Karibu asilimia 80 ya Waamerika, wanaamini kuwa imani za kiroho(sala), zinaweza kuwasaidia watu kupona kutokana na magonjwa au maumivu waliyonayo na zaidi ya asilimia 60 wanafikiri kuwa, ni vema madaktari wangefanya mpango wa kuzungumza na wagonjwa wao juu ya imani za kidini na hata kusali pamoja na wagonjwa wanaotaka. (Polls by Time? CNN and USA Weekend).

Hata hivyo, unachotakiwa kufanya, unapougua na unahitaji imani yako ya kidini ikusaidie na kuwa sehemu ya uponyaji na kigezo cha afya yako; ni kusema wazi mbele ya Mungu wako na kuufungua moyo huku ukimkaribisha Yesu afanye kazi ndani yako.

Hapa haimaanishi kwamba umtegemee Daktari akuombee au asali pamoja na wewe tu, ingawa ni muhimu kumtegemea akusikilize mahitaji yako, apange utaratibu wa kutembelewa na padre mlezi wa hospitali au, aruhusu muda wa sala kabla ya kuingizwa katika chumba cha upasuaji.

Basi ni wakati sasa kila jambo linalofikiriwa, linalofanyika, lifanyike kwa kuzingatia mapenzi ya Mungu na imani thabiti.

Wanaopokea Kipaimara wasibweteke na mafuta Matakatifu- Pengo

Na Elizabeth Stephen

ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema wanaopokea Sakramenti katika Kanisa ikiwamo ya Kipaimara, wasiridhike kwa kupakwa mafuta matakatifu, bali waongeze bidii katika kuihubiri Injili kwa watu.

Kardinali Pengo aliyasema hayo katika Ibada ya Sakramenti ya Kipaimara iliyofanyika, Jumamosi iliyopita katika kanisa la Parokia ya Makuburi, jimboni humo.

Katika Ibada hiyo, Kardinali Pengo alitoa Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 346. Kati yao, 37 walitoka katika Kigango cha Makoka, wakati 309 walitoka parokiani Makuburi.

Aliwataka vijana waliopokea Sakramenti hiyo kuiga mfano wa Mtume Mathayo kwa kutenda mambo yanayompendeza Mungu na hivyo, kuepuka uovu wote.

“Mtume Mathayo aliacha kazi ya kutoza ushuru na kumfuata Yesu, hivyo nasi tunaopata Kipaimara tuimarike kiimani na tubaki na wito uleule aliotuelekeza Mtume Mathayo… Bwana Yesu anatuita kwa njia ya kutupaka mafuta,” alisema Kardinali.

Akaongeza, “Sakramenti hiyo iwe chimbuko la pekee kwa kila mmoja wetu kutembea pamoja na Kristo".

Wakati  huo huo: Akisoma risala kwa niaba ya Parokia hiyo, Mwenyekiti Msaidizi wa Halmashauri ya Walei, Parokia ya Makuburi Ndugu. Lyimo  alimpongeza Kardinali Pengo kwa kuteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuwa Mjumbe katika Idara ya Mafundisho ya Imani.

Aidha, walimshukuru Askofu kwa kuwaletea mapadre wenye imani na misimamo iliyonyooka ambayo imefanya Parokia ya Makuburi kuimarika kiimani na kimaadili.

Parokia ya Njombe yaongezwa wachungaji

Na Frt. Carlo Mwalongo,  Njombe

PAROKIA ya Njombe Mjini katika Jimbo Katoliki la Njombe, imeongezewa mapadre wawili ili kukidhi mahitaji ya kichungaji katika vigango vyake, imefahamika.

Mwenyekiti wa Halmashauri Walei, Jimbo la Njombe, alisema kwa niaba ya Paroko wa Parokia ya Njombe, Padre Erasmo Lugome, kuwa ingawa Parokia hiyo ina vigango 31 vinavyoweza kuunda parokia tatu, bado imekuwa ikihudumiwa na mapadre wawili.

Aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza katika Ibada ya Jumapili, katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu, Njombe Mjini.

Alisema, “Ongezeko la mapadre hao litaleta mafanikio zaidi kiroho na kimwili.”

Aliongeza kuwa, ni wajibu kwa waamini wa Parokia hiyo kuwapokea vema na kuwapa ushirikiano mapadre hao wageni, ili watimize vema majukumu waliyotumwa na Mungu ili wayafanye katika Parokia hiyo.

“Inatupasa kuwaheshimu, kuwasikiliza na kuwatii kwa sababu kazi wanayoifanya wamekabidhiwa na Mungu,” alisema.

Akiwakaribisha mapadre hao, Zenobius Mtewele na Edmund Kayombo, Paroko wa Parokia hiyo, Padre Lugome, alisema mapadre hao wajisikie vema kuanza kuhudumia waamini wa eneo hilo na kwamba, kwa namna anavyowafahamu waamini hao, anaamini kuwa mapadre hao watapata ushirikiano unaotakiwa.

Katika ibada hiyo, Padre Mtewele alisema, “Bahati mbaya Wakristo hawapewi nafasi ya kuchagua mapadre wa kuwahudumia, nasi mapadre hatupewi nafasi ya kuchagua parokia za kwenda kuhudumia, hivyo tunaomba mtupokee kwa sababu sisi kama Mitume wa Yesu, tunatumwa mahali popote mradi kuna kondoo wa kuchunga.”

Naye Padre Kayombo, alisema, “Kazi tuliyopewa ni ya Mungu siyo yetu, hivyo tunaomba tushirikiane ili tuifanikishe.”

Padre Mtewele kutoka Parokia ya Matola alipata Daraja la Upadre Juni 10, 2001 katika Parokia ya Njombe Mjini. Kisha alikuwa Msaidizi wa Paroko wa Madunda na sasa ni Mlezi wa Vijana, parokiani hapo.

Naye Padre Kayombo alipata Daraja la Upadre Juni 27, 2002 katika Parokia ya Mlangali pamoja na Padre Dietram Mwinuka. Sasa ni Msaidizi wa Paroko katika Parokia  ya Njombe Mjini.

Mapadre wengine waliopata Upadre mwaka huu jimboni humo ni Padre Bosco Mwenda wa Parokia ya Njombe Mjini, Padre Bononius Mkonga na Padre Laurent Mwalongo wa Parokia ya Lugenge walipata Upadre Juni 30, 2002 katika Kanisa la Njombe Mjini.

‘UKIMWI ajali kazini! Hujui usemalo'- Askofu Ngalalekumtwa

Na Getrude Madembwe, Iringa

ETI mtu anafahamu kabisa UKIMWI ni ugonjwa hatari, lakini hajali na badala yake, anasema ni ajali kazini! Ajali gani hiyo wakati unajitakia mwenyewe!”

Hayo yalisemwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, wakati akitoa salamu kwa waamini wa Parokia ya Kihesa jimboni humo hivi karibuni.

Alisema kauli na tafsiri potofu za watu wenye uelewa finyu kuwa UKIMWI ni ajali kazini, ni hatari na zinazopaswa kupuuzwa na kila mwenye akili timamu.

Alisema UKIMWI si tatizo bali matokeo ya wanadamu kumkaidi Mwenyezi Mungu kwa kushiriki vitendo vinavyopingana na Amri za Mungu ikiwamo inayozuia kuzini.

“Watu wanakwenda kinyume na maagizo ya Mwenyezi Mungu, wanavunja miiko na ndio hao wanaowafanya hata wengine wafikirie njia haramu za kupambana na UKIMWI,” alisema.

Mhashamu Ngalalekumtwa alitoa mfano wa mti unaoanza kukauka, ambapo huanza kwa kudondosha majani na kisha, usipochunguzwa mapema, huanguka wenyewe.

“Inabidi mtu achunguze ni kwanini majani hayo yanadondoka badala ya kusubiri hadi mti huo uanguke ndipo aanze kutafuta chanzo,” alisema.

 Aliendelea kusema kuwa, watu wengine hufanya makosa kwa kutafuta njia za mkato za kupambana na tatizo la UKIMWI, badala ya kutafuta kiini ambacho ni zinaa hivyo kuachana nayo na kuishi kimaadili.

Aidha, Mhashamu Ngalalekumtwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Liturujia katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alisema viongozi wa dini wakiwemo Maaskofu hawatachoka kuwahimiza waamini juu ya kuacha zinaa kama njia sahihi ya kupambana na UKIMWI.

 “Ole wao wale watakao hamasisha matumizi ya kutumia zana mbalimbali kuzuia UKIMWI zaidi ya kumrudia Mungu, maana wanapinda ukweli juu ya jambo hilo,” alisema Mhashamu Ngalakumtwa.

Wakati huo huo: Mhashamu Ngalalekumtwa amewataka vijana kutoyumbishwa na mambo ya dunia bali waishi katika njia ya kweli ya Bwana Yesu Kristo kama Maandiko Matakatifu yanavyosema.

“Msifuatishe namna ya dunia hii, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu mpate kujua hakika ya mapenzi ya Mungu (Warumi 12:2).

Alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akihubiri katika Ibada ya Misa Takatifu ya Sakramenti ya Kipaimara kwa vijana 366,iliyofanyika katika Parokia hiyo ya Kihesa.

“Mabango, vipeperushi, video, filamu, internet Cafe na mambo mengine kama hayo kamwe haviwezi kuwa madarasa ya kujifunza njia za Mungu. Kaeni msome Biblia Takatifu…” aliasa.

Katika tukio jingine: Kanisa  Katoliki Jimbo la Iringa, limebuni mbinu mpya za kuwaepusha wenye imani ndogo wasidanganywe na kukimbilia katika madhehebu na dini nyingine.

Katika maazimio ya Mkutano wa hivi karibuni wa Halmashauri ya Kichungaji  jimboni humo, uliofanyika Tosamaganga, mbinu hizo zimetajwa kuwa ni  pamoja na kuwa na ujuzi wa kutosha kuhusu misingi ya imani ya Kanisa Katoliki hasa nyaraka zitolewazo na viongozi wa Kanisa.

Nyingine ni kutowaacha wenye upweke katika matatizo na shida mbalimbali za maisha kama magonjwa, pamoja na kanisa kuboresha uendeshaji wa makusanyiko ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo.

Mkutano huo uliongozwa na Askofu wa Jimbo katoliki la Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, pia uliazimia kutoa semina za kiroho mara kwa mara kwa wanafamilia ya Mungu, zenye lengo la kuimarisha uhusiano na Kristo na kuchochea upendo wa Kanisa Katoliki.

Maazimio hayo pia yamewasisitiza wazazi na walezi wa familia, kuyapiga vita maandishi,filamu, video na mitandao yenye kupotosha usafi wa moyo na kuimarisha uhimizaji wa yale yanayojenga akili na roho.

 

Mchungaji KKKT afananisha mwili, simu ya mkononi

Na Godwin Kaijage, DSJ

KIONGOZI mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), ameufananisha mwili wa binadamu na simu ya mkononi inayopokea kadi za njia za simu ‘line’ toka makampuni mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mkuu wa KKKT, Jimbo la Ilala, Mchungaji Julius Mong’ola, Kiongozi huyo Mchungaji Daniel Christopher wa Usharika wa Unga LTD, Arusha,  aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza usharikani Kipawa, Dar es Salaam, alipotembelea Usharika huo pamoja na Kwaya ya Vijana toka Unga LTD Arusha.

Mchungaji Mong’ola alimnukuu Mchungaji Christopher toka Arusha akisema, “Unaweza kuingiza kadi yoyote kwenye simu ya mkononi. Ukiingiza kadi ya Mobitel, itakuonesha Mobitel, ukiingiza kadi ya Vodacom, itaonesha Vodacom. Na maisha ya mtu ndivyo yalivyo, ukiingiza kadi ya shetani utaonekana kuwa ni wa shetani na ukiingiza kadi ya Yesu, utaonekana kuwa wewe ni wa Yesu.”

Alisema ni vema binadamu wote wakaamua kwa moyo kuingiza kadi ya Yesu katika maisha yao ili wamtumikie na kumpendeza Mungu.

Katika mazungumzo hayo, Mchungaji Mang’ola alisema, mtindo wa vikundi na asasi za dini kutembeleana kwa lengo la kufanya kazi ya Mungu, hauna budi kuimarishwa na wote wenye mapenzi mema katika Kristo ikiwa ni njia muhimu ya kuimarishaUkristo duniani.

Kwa mujibu wa Mchungaji Mang’ola, Mchungaji Christopher aliwasili na Kwaya ya Vijana jijini Dar es Salaam, wakiwa na kanda tano huku Kwaya hiyo ikikusudia kurekodi kanda ya sita iitwayo Maisha ya Kukaa Ndani ya Yesu.

Majina ya kanda zilizorekodiwa na tayari zinauzwa ni  Alaaniwe Mtu Yule, Jamani Mnayo habari, Tukumbuke Siku Hizi za Mwisho, Wa Kwanza Atakuwa Wa Mwisho na Dunia Ina Mafumbo Mengi.