Make your own free website on Tripod.com

Mtazamo wa Kikatoliki kuhusu namba za Biblia

 

Na Mwandishi Wetu

 

 

SUALA la namba katika Biblia, limekuwa likizisumbua akili za wakristo na watu wengine wengi huku wasomaji wengine huyumbisha na kupotosha maana ya namba hizo ama kwa makusudi, au kutokana na usomaji duni na uelewa mdogo wa Neno la Mungu.

ENDELEA UK. 3

Maandalizi ya Jubilei Kuu ya Ukristu 2000, yanatilia mkazo wa pekee utume wa kibiblia Utume huu una lengo la kuwafanya hususani Wakatoliki wapende kulisoma, kulitafakari na kulielewa Neno la Mungu.

Mara nyingi usomaji na hata uelewaji wa Neno hilo la Mungu hupotoshwa, kwa maneno mengine, maudhui na dhana ya Biblia huweza kuyumbishwa kutokana na maelezo potofu au finyu yanayotolewa na baadhi ya wasomaji wa Biblia kuhusu maana ya namba (tarakimu) katika mazingira na uandishi wa Biblia.

 

Je, namba zina maana gani katika Biblia?

Namba kama ishara:

 

Kwa miaka mingi namba au tarakimu zimekuwa zikitumika kama alama za Hisabati.

Aidha, namba zimekuwa zikitumiwa na wanadamu kama ishara au vielelezo viletavyo maana fulani fulani. Zaidi ya hayo, yapo pia mataifa mbalimbali mfano, Wapersia, Waasria, Wayunani, Wamisri, Wachina, Wajapani na Wahindi ambao wamekuwa wakitumia namba au tarakimu katika nyanja za ushirikina, utamaduni, dini, mawasiliano na hata falsafa. Waisraeli nao walizitumia tarakimu au namba kwa kuzipa maana fulani za kiteolojia.

Namba Moja (1) :  Hii inamwakilisha Mungu ambaye ni MMOJA TU!.

Namba mbili (2) : Hii ni namba inayoashiria mlinganisho mpambano au tofauti. Aidha, zaidi ya hayo, namba hii inadokeza utimilifu mfano: mwanaume au mwanamke, uzuri na ubaya, mwanga na giza.

Namba Tatu (3) : Hii inaonesha utimilifu. Mfano:

Nuhu anao watoto watatu Sem, Ham na Jafet ambao ni mababu wa mataifa yote. Pia, kulikuwa siku tatu za giza kule Misri kabla ya lile tukio la kutoka utumwani Waisraeli.

Mfano mwingine ni hekalu la Yerusalemu lilikuwa na sehemu kuu tatu, Yona alikaa tumboni mwa Nyangumi kwa siku tatu mchana na usiku, Yesu alipatwa na vishawishi au majaribu matatu kule jangwani alipofunga, Yesu alikaa kaburini kwa siku tatu na pia, Utatu Mtakatifu una nafsi tatu. Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Namba Nne (4): Kibiblia namba hii inadokeza mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na zile ncha kuu nne za dira za dunia-Kaskazini, Kusini, Mashariki na Magharibi; Ile mito mikuu minne inayomwagilia maji ulimwengu wote katika Ufunuo wa Yohani na wale wanyama wanne wanaovuta gari la Mungu kwenye Ufunuo wa Yohani.

Namba tano (5): Kibiblia namba hii inadokeza juu ya Milango Mikuu ya maarifa yaani macho, masikio, ulimi, pua na vidole (ngozi); Wanyama watano wa kutolea sadaka;Yale mawe matano ya Mfalme Daudi; Vile vitabu vitano vya Musa; Wale wanawali watano wenye busara katika Injili na Mgawanyo wa Injili ya Marko katika sehemu kuu tano.

Wadau wa Injili wapewa changamoto

l ‘Ndoa za majaribio ni feki’

Na Joseph Sabinus

WADAU wa Injili wamepewa changamoto ya kuwa chachu na wanaochochea karama za Mungu kufanya kazi ndani ya kila mtu licha ya mazingira magumu na changamoto zinazowakabili.

Changamoto hiyo ilitolewa Jumamosi iliyopita wakati Padre Richard Mjigwa, alipokuwa akizungumza katika Maadhimisho ya Siku ya Miito katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, yaliyofanyika katika Kituo cha Don Bosco, Upanga jijini Dar es Salaam.

Alisema, baadhi ya watu wakiwamo Wakristo hufanya makosa kwa kutojichunguza vema ili kutambua na kutumia karama zao na hivyo, kukata tama na kupotoka wanapokumbwa na matatizo.

“Unapokumbwa na matatizo, usidhani kuwa ni wewe peke yako na sasa eti unakata tamaa. Lazima tujue kuwa sauti ya Mungu huita polepole na tena kwa hali na mazingira tofauti,” alisema.

Aliongeza kuwa, kila mwanajamii hana budi kutumia karama yake katika kutangaza sifa na utukufu wa Kanisa ili Kanisa na kazi ya Mungu ziendelee.

Alisema mambo ya kidunia na maamuzi ya kijuujuu miongoni mwa jamii, ndiyo yanayokwamisha utambuzi na matumizi sahihi ya karama za Mungu kwa watu hivyo, ni vema kila mmoja awe makini ili awe mwanzo sahihi wa kuchipua mwanga utakaoifanya jamii imuone na kumtambua Mungu.

‘Wadau wa Injili lazima wawe chachu zaidi katika kutangaza Habari Njema… Pia, lazima tujue kuwa, maisha ni mtihani, lazima kuushinda,’ alisema.

Akitoa semina juu ya Wito wa Upadre, Padre Mjigwa alisema, kila mmoja awe makini kutambua karama zinazomuita kumtumikia Mungu.

’…Kama wewe ni padre wa Shirika la Kitawa la Kimisionari, ujue utafanya kazi mahali popote utakapotumwa huku ukisukumwa na nadhiri za kitawa yaani, utii, ufukara na usafi wa moyo,’ alisema.

Akaongeza, ‘Ukiwa Mmisionari wa Shirika la Kazi za Kitume, wewe hutakuwa na nadhiri yoyote, lakini utafungwa na mshikamano wa maisha ya kijumuia.

Naye Sista Klara Gaspary wa Shirika la Dada Wadogo, katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es, Salaam, katika mada yake juu ya Maisha ya Utawa kuwa, alieleza maana ya Utawa kuwa ni mtindo wa maisha unaomfanya mtu ajitoe kiroho na kimwili kwa ajili ya Ufalme wa Mungu huku akimshuhudia Kristo kwa sala na kazi.

Alisema, ‘Mashirika mbalimbali katika Kanisa, ni karama ambazo Roho Mtakatifu analijalia Kanisa na kwamba, kila shirika linakuwa na karama yake ili kukidhi mahitaji ya Kanisa.’

Alisema Mwanzilishi wa Shirika ni Nabii anayesoma Alama za Nyakati na kuzitafsiri katika mwanga wa Injili.

Naye Mweka Hazina wa WAWATA Parokia ya Upanga, Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Bibi Theonestina Rweikiza,  katika mada yake juu ya Maisha ya Ndoa, alisema wanandoa wawe shupavu, jasiri na wavumilivu kwani wakati wowote ndoa zao zinaweza kuingiliwa na shetani na hatimaye kuwa katika matatizo.

Alisema vijana wanahitaji kuwa na msimamo thabiti na uaminifu katika maisha yao ili wasijihusishe katika vitendo vya ndoa kabla ya ndoa zao halali.

Aidha, aliwaasa wanandoa kuishi kiaminifu huku wakizingatia sala.

“Wanandoa wanahitaji kuvumiliana; na huwezi kumvumilia mwenzako bila kuwa na neema na pia, huwezi kupata neema bila kusali,” alisema Bibi Rweikiza.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Parokia ya Upanga, Bw. Steven Rweikiza, alisema juu ya maisha ya ndoa kuwa, vijana waepuke kujiingiza katika ndoa za majaribio.

“Kwenye ndoa hakuna majaribio. Ikiona ndoa ya majaribio, ujue hiyo ni feki na matokeo yake ni hayo matatizo yakiwamo magonjwa na mifarakano,” alisema. Shirika la Maisha Wakfu ya Kidunia (UNITAS) kwa ajili ya Afrika, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, liliwakilishwa na Madada Sura Ngenzi, Crescentia Mahinga, Victoria Mnyasenga, Esther Lyimo na Margareth Mahenge.

Katika mada yake juu ya Shirika la UNITAS, Dada Sura Ngenzi, alisema, wanashirika hilo hufanya kazi zao pale walipo. “Utume wetu ni utume wa uwepo. Mahali ninapokuwapo ndipo ninapotimiza utume wangu kama mwanadunia wakfu. Kwamba mimi kama mwalimu nitajitahidi kuishi vizuri nikiwa mfano mzuri kwa wanafunzi na walimu wenzangu”.

Wanashirika huishi na kufanya kazi mbalimbali za kujiajiri na za kuajiriwa mahali popote na hawana sare.

Baadhi ya mashirika mengine ya kitawa yaliyohudhuria maadhimisho hayo ni pamoja na Holy Union Sister ambalo karama yake ni kutafakari muungano thabiti uliopo baina ya Yesu na Maria katika Fumbo la Umwilisho; Shirika la Masista wa Upendo wa Mtakatifu Karoli Borromeo lenye karama ya huruma  na upendo usiopimika wa Yesu Kristo Msalabani na Shirika la Masista Wamisionari wa Dada Yetu wa Afrika.

Mengine ni Shirika la Mtakatifu Kamili Lellis lenye karama ya kutumikia wagonjwa na maskini ; Shirika la Masista wa Misericordia na Shirika la Masista wa Msalaba Mtakatifu.

Mengine ni Shirika la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu la Bukoba, Shirika la Watawa Waselesian wa Don Bosco.

Sharia: Inamwadhibu nani; mama au mtoto?

l Inaongeza mgawanyiko katika jamii

Na Dalphina Rubyema

MATUMIZI ya Sheria ya Kiislamu nchini Nigeria maarufu kwa jina la SHARIA, yanajenga kizazi cha kulipizana kisasi kisichokwisha nchini humo, Imesema ECAWIDNET.

Mratibu wa Mtandao wa Maendeleo ya Akina Mama chini ya Kanisa Katoliki katika nchi za Afrika Mashariki na Kati (ECAWIDNET), Bibi Oliva Kinabo, aliyasema hayo mwanzoni mwa juma wakati akizungumza na KIONGOZI  ofisini kwake, jijini Dar es Salaam.

Chini ya Sharia mwanamke aliyezaa nje ya ndoa huhukumiwa na mahakama adhabu ya kupigwa mawe hadi kufa.

Katika tukio la hivi karibuni mwanamke mmoja, Amina Lawal, alihukumiwa kuuawa chini ya Sharia, baada ya kubainika kumzaa mwanae Wasila, nje ya ndoa. Hukumu ilipangwa kutekelezwa baada ya mtoto kufikisha umri wa miaka miwili au baada ya kuachishwa kunyonya.

Bibi Kinabo alisema utekelezaji wa hukumu ya kifo utajenga jamii yenye kizazi chenye tabia ya kulipizana kisasi, hali ambayo ni hatari katika jamii.

“Mtoto huyo atakuwa mkubwa na ataanza kuulizia alipo mama yake, akishaelewa kuwa aliuwawa, hatafurahishwa; atataka ajue kisa na wahusika, na matokeo yake, ni kuungana na wote wasioridhika na hali hiyo kulipiza kisasi”, alisema.

Aliongeza kuwa, hukumu ya kumuua mwanamke huyo baada ya mtoto kufikisha umri wa miaka miwili, ni unyanyasaji dhidi yamtoto kwa kumkosesha mapenzi na malezi ya mama.

Bibi Kinabo aliongeza kuwa, hali hiyo ni ukiukaji wa haki za binadamu juu ya maisha pia, ni kosa kwani inamuadhibu mtoto ambaye hakuhusika na kosa na kumfanya mtoto awe yatima.

“Kwa kweli kitendo hicho ni kumuonea mtoto, kumhalalisha awe mtoto wa mitaani, “ alisema.

Akizidi kukosoa kipengele hicho, Bibi Kinabo alisema kinambana mwanamke pekee na mwanamke peke yake hawezi kuzaa mtoto bila kukutana na mwanaume.

“Kwa nini mwanaume aliyezaa naye asibanwe pia? Hiki kipengele kinawanyanyasa wanawake,” alisema.

Baada ya hukumu hiyo,mwanamke huyo Amina Lawal (30), alikata rufaa kupinga hukumu hiyo, lakini Mahakama ya Kiislamu nchini humo (Sharia Court) iliyopo katika mji wa Funtua, katika Jimbo la Katsina, iliikataa rufani hiyo.

Kufuatia hukumu hiyo, asasi za haki za binadamu ndani na nje ya Nigeria, zimekaririwa zikilaumu kwamba Mahakama za Kiislamu zinazofanya kazi katika majimbo 12 yenye Waislamu wengi nchini Nigeria, hazijali ukweli kuwa nchi hiyo ina watoto wengi wa mitaani wanaohitaji malezi, uangalizi na msaada wa jamii na Serikali.

Kwa mujibu wa habari zilizo andikwa na Gazeti la The Observer la Uingereza hivi karibuni, asasi hizo zinasema kuwa kuongezeka kwa idadi ya watoto hao kwa kuwaua wanawake wanaokumbwa na hatia hiyo, kunazidi kutia dosari Dini ya Kiislamu nchini humo kwani wanadai hakuna dini isiyojali zawadi ya uhai toka kwa Mungu.

kwa mujibu wa gazeti hilo, vikundi mbalimbali vya akina mama pia vinakasirishwa na msimamo wa Mahakama za Sharia kuwa wakati mwanamke anapigwa mawe na kuwaua kwa kuwa hawezi kuficha ushahidi wa mimba nje ya ndoa, mwanamume anayehusika anaweza kuhukumiwa adhabu kama hiyo iwapo watapatikana mashahidi wanne kuthibitisha kuwa walimshuhudia akishiriki kitendo cha ngono na mwanamke huyo.

Kuna habari kuwa, kufuatia hukumu dhidi ya mwanamke huyo, warembo mbalimbali duniani, wametishia kutoshiriki mashindano ya kuwania taji la dunia ‘Miss Word’ yaliyopangwa kufanyika nchini humo, Novemba mwaka huu ambayo yatashirikisha zaidi ya nchi 100.

Hata hivyo Lawal siyo mwanamke pekee nchini humo kuhukumiwa kuuawa kwa mawe, kwani yupo Bibi Safiya Husaini, kutoka Jimbo la Sokoto ambaye aliishi chini ya kivuli cha hukumu ya kifo kwa takriban miezi sita kwa dhambi ya uasherati.

Hata hivyo, hukumu hiyo ilibatilishwa na Mahakama ya juu zaidi ya Sharia, Machi mwaka huu.

Mwanamume aliyezaa na Safiya, tayari alikuwa na wake wawili.

Baba yake Safiya alimtaka mwanamume huyo ama kumuoa kwa kumfanya Safiya mke wa tatu ama kugharimia matunzo ya mtoto wake.

Kwa mujibu wa Gazeti hilo Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, naye amelaani hukumu dhidi ya Lawal, lakini wachunguzi wa mambo wanasema ni uongozi wake legelege kutaka kuwafurahisha watu wa Kaskazini kwa sababu za kisiasa.

Rais Obasanjo akisema hivi karibuni alikaririwa na vyombo vya habari nchini humo hivi “Siamini kama yote yanayoendelea yanaishia kwenye kifo cha Lawal. Kwa hakika kama hilo litatokea basi nitajililia mwenyewe, nitamlilia Amina na nitaililia Nigeria”.

Hata hivyo Rais huyo alizungumza kimafumbo badala ya kuweka bayana endapo Mahakama ya Kiislamu itashikilia msimamo wa kumuua Lawal, yeye kama Rais atachukuwa hatua gani kumnusuru mama huyo.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Obasanjo, Kanu  Agabi ametamka waziwazi kuwa hukumu hizo ni kinyume cha Katiba na ni kitendo cha ubaguzi kuziingiza Sheria za Kiislamu katika majimbo 12 ya Kaskazini mwa Nigeria.

“Hii itakuwa changamoto kwa Katiba mpya ya mwaka 1999 ya Nigeria ambayo ndiyo msingi mkuu wa mwenendo wa kidemokrasia,  alisisitiza 

Askofu Msarikie awaasa watawa

Anneth Mwakatobe Moshi, SAUT

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Moshi, Mhashamu Amedeus Msarikie, amewataka Watawa kutoka katika mashirika mbalimbali nchini, kudumisha moyo wa sala, imani, upendo na mshikamano ndani ya Kanisa na jamii kwa jumla.

Mhashamu Msarikie alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akitoa nasaha zake kwenye Maadhimisho ya kuweka Nadhiri za Kwanza na zile za Maisha kwa Masista wa Shirika la Bibi Yetu wa Kilimanjaro.

Maadhimisho hayo yalitanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Mhashamu Msarikie na kufanyika katika Nyumba ya Asili ya Shirika hilo iliyopo katika eneo la Rombo, jimboni humo.

Katika nasaha zake, Askofu Msarikie alisema kuwa watawa kama wabatizwa wengine, hawana lazima maisha yao yatafute kuuishi Utakatifu.

Aliwataka watawa hao kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa huku wakizingatia mashauri makuu matatu ya Injili ambayo ni utii, usafi kamili na umaskini.

Mhashamu Msarikie aliongeza kusema kuwa, watawa wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika Uinjilishaji mpya katika Kanisa huku wakitambua kuwa, wameitwa kushiriki Utume wa Ukombozi wa Kristo kwa dunia.

Katika maadhimisho hayo, Wanovisi 13 waliweka Nadhiri za Kwanza katika Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, wakati Masista 22 waweka Nadhiri za Daima katika Shirika hilo.

KIWOHEDE kuwafumbua macho vijana wanaoshi kwenye mazinga magumu

Na Anthony Ngonyani

ILI kuwasaidi vijana wanaoishi katika mazingia magumu,Shirika lisilo la Kiserikali la Kuwaendeleza Vijana na Watoto (KIWOHEDE),limo katika mipango kuwaskusanya vijana hao na kuwapa semina ambayo inalenga kuwapa angalisho la mbinu za kupambana na maisha hayo.

Kauli hiyo ilitolewa mwanzoni mwa juma na Mtoa Ushauri Nasaha kwa vijana katika Shirika hilo,Bibi Saharifa Chomoka wakati akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Alisema Shirika lake hadi hivi sasa limo katika hekaheka za kuwakusanya vijana  hao wanaoishi katika mazingira  magumu na wakishakamilisha zoezi la kuwakusanya,litafuatia suala la semina amabyo alisema itatolewa hivi karibuni.

Alisema KIWOHEDE ilionelea itoe semina hiyo badala ya kuliacha kundi hilo lijitumbukize katika vitendo viovu likiwemo suala la  uvutaji bangi, madawa ya kulevya na biashara ya ukahaba.

“Tumeona ni bora  kuwapatia mbinu ambazo zitawasaidia kuweza kumudu kuendesha maisha yao”alisema Bibi Chomoka.

Mbali na suala hilo la kuwakusasanya vijana kwa ajili ya kuwapa semina,Shirika hilo pia lina jumla ya vijana wapatao 56 ambao hunufaika na mafunzo mbalimbali shirikani hapo.

Bibi Chomoka aliyataja mafunzo wanayoyaopata kuwa ni pamoja na ufundi mbalimbali kama ushonaji wa nguo, kutengeneza batiki na viatu.

“Kwakweli tangu tuanze kutoa mafunzo haya,tumekuwa tukipata vijana wengi ambao lengo lao ni kuwapatia ujuzi” alisema Bibi Chomoka.

Parokia Kilwa Masoko kuadhimisha Jubilei ya Fedha

Na Anthony Ngonyani

PAROKIA Katoliki ya Bikira Maria Nyota ya Bahari, Kilwa Masoko, jimboni Lindi, imo katika maandalizi kabambe kwa ajili ya kuadhimisha Jubilei ya  Miaka 25 tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Paroko wa Parokia hiyo, Padre Anthony Chilumba, alisema kuwa maadhimisho hayo yatafanyika Novemba 10, mwaka huu parokiani hapo.

Alisema maadhimisho hayo yataambatana na utoaji wa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini wapatao 25 wa Parokia hiyo. Sakramenti hiyo takatifu itakayotolewa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Bruno Ngonyani.

Padre Chilumba alisema kuwa, katika harakati za kufanikisha maadhimisho hayo, zimeundwa kamati mbalimbali zitakazosaidia kupanga mikakati ya kufanikisha sherehe hiyo muhimu parokiani hapo.

 Alisema katika kufanikisha maadhimisho hayo, waamini parokiani humo wanajitahidi kutoa michango yao ya hali na mali.

Alitoa ombi kwa waamini kutoka katika majimbo mengine na wale wenye mapenzi mema, kujitolea kwa kila hali kuwaunga mkono Wanakilwa Masoko.

Aliomba michango hiyo ama itumwe kupitia S.L. P 14, Kilwa Masoko ama kwenye Akaunti namba 6722, NBC Kilwa Masoko.

Padre Chilumba alisema kuwa Parokia itatumia maadhimisho hayo kuhamasisha uimarishaji wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ambazo zilikuwa zimelala ikiwa ni pamoja kuongeza  ushirikiano zaidi kati ya mapadre na waamini.

Alisema kulala kwa jumuiya hizo zaidi kunasabishwa na wingi wa waamini wa dini ya Kiislamu parokiani humo.

 PAROKIA  hiyo ya  Bikira Maria Nyota ya Bahari, Kilwa Masoko, ilianzishwa mwaka 1977. Awali, Parokia hiyo ilikuwa ni miongoni mwa Parokia za Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, lakini mwaka 1979, Parokia hiyo pamoja na Parokia za Kilwa Kipatimu na Kilwa Manzese, zilihamishiwa kwenye Jimbo la Lindi.

Kwa mujibu wa Padre Chilumba, hadi sasa Parokia hiyo ina vigango 10  alivyovitaja kuwa ni pamoja na Kivinje, Mtanga, Nangurukuru, Mattu, Njijo, Mitole, Namakongoro, Nakimula, Mavunji na Kilwa Masoko yenyewe.

Pamoja na kuwa na vigango vyote hivyo, Parokia hiyo ina jumla ya waamini Wakatoliki wapatao 890 na kati yao, waamini 320 wanatoka katika Kigango Mama cha Kilwa Masoko.

Mbali na hayo, Parokia hiyo inahudumiwa na Padre mmoja akisaidiwa na Makateksta watano na vyama vya Kitume.

Licha kuwa na idadi ndogo ya waamini, Parokia hiyo imefanikiwa kushiriki kikamilifu katika kuchangia Maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Umoja na Ushirikiano katika nchi za Mashariki mwa Afrika (AMECEA), uliomalizika hivi karibuni katika Kituo cha Malezi cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Vile vile, Paroko huyo alisema kuwa pamoja kuwa ni Padre pekee katika Parokia hiyo, amekuwa akijitahidi kila mwisho wa mwezi kutembelea Gereza la Kilwa Masoko na kutoa ibada kwa wafungwa wa gereza hilo.

Uonesheni upendo wa Kristo kwa vitendo

Na Leocardia Moswery, SAUT

WAAMINI wa Kanisa Katoliki nchini wameshauriwa kuonesha upendo wa Yesu Kristo kwa vitendo, miongoni mwa jamii na kuepuka upendo wa maneno matupu.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Utume wa familia wa Kanisa Katoliki Tanzania, Padre Baptiste Mapunda muda mfupi baada ya Ibada Takatifu ya  kuadhimisha miaka 12 tangu apate Daraja ya Upadre.

Ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la Manzese, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ilifuatiwa na tafrija ya kumpongeza Padre Mapunda iliyofanyika katika Ukumbi wa AMECEA uliopo katika Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).

Akifafanua zaidi juu kuhusu kauli yake, Padre Mapunda alisema kitendo cha kudumisha upendo miongoni mwa viongozi wa Kanisa na waamini wanao waongoza, ni cha muhimu na hakina budi kuzingatiwa kwani kinatimiza agizo la Yesu Kristo alilowapa wanadamu.

 “Hata Bwana wetu Yesu Kristo alisema, “Pendaneni, kama nilivowapenda nyinyi, nanyi pia mpendane,” alisema Padre Mapunda.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na watu mbalimbali wakiwemo Mapadre, watawa wa kike na wa kiume, wazazi, ndugu na jamaa za Padre Mapunda pamoja na waamini kutoka sehemu mbalimbali.

Miongoni mwao walikuwepo pia wageni kutoka Parokia Katoliki ya Maguu jimboni Mbinga ambao ni Paroko wa Parokia hiyo, Padre Josaphat Malunda, Padre Francis Majeshi Nduguru na Frateri Deogratias Kumburu.

Akielezea hisia zake baada ya kuadhimisha miaka 12 ya Upadre, Padre Mapunda ambaye pia ni Paroko Msaidizi wa Parokia ya Manzese, alisema katika kipindi chote hicho cha Umisionari, ameweza kufaidika na mambo mengi mojawapo likiwa lile la kuwa karibu na kujenga urafiki na watu mbalimbali.