WAWATA wakabidhiwa kulea Utoto Mtakatifu wa Yesu

l Mkurugenzi asema kazi ya watoto huzaa matunda                           mengi, wanaweza kuwafundisha hata maaskofu

Na Neema Massawe, DSJ

WAKATI Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) wamekabidhiwa jukumu la kulilea Shirika la Kimisionari la Utoto Mtakatifu wa Yesu nchini, Shirika hilo limesema kazi ya watoto ni muhimu duniani na mbele ya Mungu kwani wanaweza kuwafundisha hata Maaskofu.

Mkurugenzi wa Shirika hilo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padre Timothy Maganga Nyasulu, aliyasema hayo Jumamosi iliyopita katika mkutano wa walezi mbalimbali, waliokutana katika Ukumbi wa Mikutano wa Parokia ya Mtakatifu Yosefu jijini Dar es Salaam,ili kujadili maandalizi ya Sikukuu ya Watoto Mashahidi inayoadhimishwa Desemba 28 kila mwaka.

Katika Mkutano huo ambao pia ulijadili juu ya siku maalumu ya watoto kufanya matendo ya huruma jimboni humo Desemba 26, Padre Timoth alisema kuwa, wazazi na jamii kwa jumla, hawana budi kuwafundisha watoto kuishi kwa upendo na kusaidiana huku wazazi nao wakionesha mifano bora na hai.

“Tuwe wakweli na tusimamie ukweli siku zote…mtoto akioneshwa mtu kwa lugha ya chuki, atakuwa na chuki hiyo naye atafundisha wengine… Mara nyingi tumeona na kuthibitisha kuwa watoto wanaweza kuwafundisha hata Maaskofu wakaelewa vitu vingi…” alisema.

Akaongeza, “Kazi ya watoto haipotei; inazaa matunda na kazi ya watoto, ina thamani kubwa si mbele ya watu tu, bali hata mbele ya Mungu.”

Mintarafu siku hiyo, Padre Timothy alishauri parokia zote kufanya mipango maalumu ili watoto ambao hawatapata nafasi ya kufanya matendo hayo ya huruma katika vituo maalumu, waandaliwe utaratibu ili watoe huduma zao kwa watu wenye matatizo katika maeneo wanayoishi watoto hao.

“ …Tuwe makini ili watoto wasijenge utamaduni wa kudhani kuwa matendo ya huruma ni kwa hospitali, magereza na katika vituo maalumu pekee. Wanaokosa nafasi wafanyiwe utaratibu wa kuwatembelea wenye matatizo waliopo katika maeneo yao,” alisema.

Alisisitiza watoto wenye ulemavu washirikishwe katika mambo mbalimbali ya kijamii. “Watoto ni rahisi kujikubali hali zao na wenzao kuwakubali,” alisema.

Katika siku ya matendo ya huruma, watoto hao huwatembelea watoto wanaolelewa katika vituo mbalimbali wakiwamo yatima, wagonjwa, na pia watu mbalimbali wenye shida huku wakiwapa misaada waliyonayo kusali, pamoja na kuzungumza nao.

Katika Mkutano huo ambao uliwashirikisha wawakilishi wa WAWATA toka maparokiani, masista na wadau wengine, Bw. Majani, alisema kuwa, katika tamasha la Utoto Mtakatifu wa Yesu lililoadhimishwa hivi karibuni katika Parokia ya Tabata, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari nchini (PMS), Padre Liberatus Mwenda, alitangaza rasmi kuwa WAWATA ndio Walezi rasmi wa Shirika la Kimisionari la Utoto Mtakatifu wa Yesu nchini.

Msiende Kanisani kuonesha mavazi, nendeni kusali - Mch. Moravian

Na  Brown  Sunza

KIONGOZI mmoja wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), ameiaumu tabia ya baadhi ya waamini wa madhehebu mbalimbali kwenda kanisani kwa nia ya kuonesha mavazi badala kupeleka maombi yao kwa Mungu na akawataka waiache mara moja kwani inakwaza wengine.

Kiongozi huyo wa Usharika  wa Magomeni katika Wilaya  ya  Mashariki, Jimbo  la Kusini, Mchungaji Arimanura Masongera, alisema wakati akizungumza na KIONGOZI  jijini Dar es Salaam, kuwa wapo baadhi ya waamini wenye tabia mbaya ya kwenda kanisani ili kuwatia vishawishini waamini wengine wenye  nia  ya  kumwomba  Mungu.

“Baadhi hawana lengo la kusali ila wanafika kanisani ili kutimiza wajibu na baadhi yao wanafika kanisani kwa ajili ya kujionesha  kimavazi. Tabia hii ni mbaya maanainawatia kishawishini na kuwakwaza wenye nia njema ya kusali,” alisema Mchungaji Arimanura.

Aliwataka waamini wenye tabia hiyo watambue kuwa kanisani ni  mahali patakatifu ambapo kila mtu anaruhusiwa kuingia na kusali  kadiri ya imani yake, lakini si mahali pa kuoneshana uwezo wa mtu kiuchumi.

Aidha, Mchungaji Alimanura alisema kuwa, kukithiri kwa  ubinafsi miongoni mwa jamii, uumedumaza maendeleo.

Alisema baadhi ya watu wana uchoyo wa kushiriki katika  shughuli za  kuleta maendeleo ama kimawazo, au kivitendo.

Alisema, kuwa si sahihi jamii kusingizia uduni na ugumu wa maisha kuwa ndiyo chanzo cha kudidimiza maendeleo.

“Ubinafsi  hauna  tajiri , msomi , wala masikini  ni kitu  kilichopo ndani  ya moyo  wa mtu” alisema .

Aliwataka waamini kushirikiana pindi linapotokea jambo la kuweza kuleta maendeleo katika mazingira wanayoishi.

Mchungaji huyo alisema  katika  jitihada  za kuleta  maendeleo ya kweli,kuna haja kwa serikali  kurejesha Mashirika ya Umma  vijijini. Sambamba na hayo amewataka  watu  wenye mawazo  binafsi  wayatoe  katika  barua  za wasomaji  hususani  kwa magazeti  yote  yenye utaratibu   wa  kutoa nafasi hizo  ili kubaini  matatizo  yanayoikabili  jamii  kwa wakati unaofaa  na kupelekwa mahali panapohusika  ili kupewa ufumbuzi  wa  haraka  kabla  ya  madhara  kutokea.

Chuo Kikuu kuchangia Milioni 20/- kuzuia mmomonyoko

          Na Dalphina Rubyema

UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ,umesema kuwa uko tayari kuchangia  kiasi cha sh.milioni 20 kwaajili ya kuzuia mmomonyoko wa undongo unaoendelea katika bonde la Chuo hicho.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni  na Afisa Mkuu wa Utawala chuoni hapo, Profesa John Mshana wakati akijibu risala kutoka kwa Mwenyekiti  wa Utunzaji Mazingira, Bw.Emmanuel Mbasha, aliyoitoa wakati wa sherehe za upandaji miti chuoni hapo.

Katika risala yake hiyo,Bw.Mbasha alieleza kuwa zaidi ya sh.milioni 20 zinahitajika kwa ajili ya kununulia vifaa mbalimbali ili kuweza kujaza katika bonde hilo linalozidi kumomonyoka.

Akijibu risala hiyo,Profesa Mshana ambaye alikuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo za upandaji miti,alisema ofisi yake itasaidia kutatua tatizo hilo ambapo alitaka viorodheshwe vifaa vinavyohitajika.

“Ofisi ya chuo iko tayari kutoa msaada,mnachotakiwa  kufanya ni kuorodhesha idadi ya vitu vinavyohitajika nasi tutawataarifu nini tutachangia”alisema Profesa Mshana.

Awali katika risala yake,Mwenyekiti huyo wa Utunzaji wa Mazingira,alisema kuwa mbali na mvua, pia bonde hilo linazidi kuchimbika kutokana na baadhi ya watu kuendelea kuchimba mchanga kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba.

Hata hivyo Bw.Mbasha alisema kuwa  wananchi wanaozunguka eneo hilo, hawalifumbii macho suala hilo kwani wamefanikiwa kupanda miche 100 ya miti aina ya matete,kudhibiti uharibifu wa mazingira.

Kanisa Katoliki jimboni Moshi  lazindua maandalizi ya Jubilei ya Dhahabu

    Na Mwandishi Wetu

KANISA Katoliki jimboni Moshi,limezindua rasmi maandalizi ya Jubilei ya Dhababu ya Jimbo.

Uzinduzi huo ulienda sambamba na adhimisho la Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu wa Jimbo hilo,Mhashamu Amedeus Msarikie, ambaye katika mahubiri aliyoyatoa kwa .mamia ya waamini  waliohudhuria Misa hiyo iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Kristu Mfalme, aliwataka waamini kufanya maandalizi kabambe ya kusali kwa nia dhabiti wakati  wa maandalizi,maadhimisho ya baadaye.

Aliwaalika kufanya toba ya kweli ili kuitikia mwaliko wa Bwana wetu Yesu Kristu. wa kuwa wakamilifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyomkamilifu. "Kila mmoja apanie kuwa Mtakatifu”alisema.

Wakati wa maandalizi ya maadhimisho hayo,waamini watapata nafasi ya  kumwenzi Mama Bikira Maria kwa Ibada mbalimbali.

Vile vile sanamu ya Bikira Maria Mhujaji kama ishara ya wazi ya upendo wake kwa wanawe,itapelekwa na kuzunguka katika kila parokia na vigango teule jimboni humo.

Siku hiyo ya uzinduzi wa Jubilei,Mhashamu Msarikie alibariki sanamu tatu kwa ajili ya Vikariati zote tatu zilizomo jimboni humo.

Sanamu hizo zilikabidhiwa rasmi kwa Mapadre wa Vikariati  hizo ambazo ni Rombo,Vunjo na Hai.

Kipindi hicho cha Maandalizi ya Jubilei kimeanza tangu Agosti 18 mwaka huu na kilele chake ni Machi 23 mwaka kesho.

Katibu wa Miradi Moravian ahofia UKIMWI kuacha makanisa matupu

l Mch. Asema wanawake wakitaka, utakwisha

 

Na Mwandishi Wetu

KATIBU wa Miradi na Uwakili, wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), Wilaya ya Mashariki, Jimbo la Kusini, Bw. Yonah Sonelo, amesema hali inazidi kutisha kwani waamini na viongozi mbalimbali wa kiroho wanakufa kwa UKIMWI na hivyo, makanisa yamo hatarini kubaki matupu.

Bw. Sonelo alikuwa akizungumza katika ibada iliyofanyika Jumapili iliyopita katika Kanisa la KMT, Usharika wa Keko, Wilayani kwake, ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika sharika za Wilaya hiyo.

Alisema kwa kuwa awali baadhi ya watu walifikiri UKIMWI ni utani na hivyo kutozingatia tahadhari, vifo na madhara ya UKIMWI yanayoonekana sasa duniani hayana budi kuwafanya watu wamgeukie Mungu na hivyo, kufuata njia sahihi za kuepukana nao.

“Inatia uchungu, watu wanazidi kwisha na haya makanisa yetu tunayojenga tusiposhituka sasa na kumgeukia Mungu, tutakwisha wote na yatabaki makanisa matupu,” alisema.

Naye Mchungaji wa Ushirika huo, Salatieli Mwakamyanda,  alisema wanawake wanayo nafasi kubwa kuamua kama UKIMWI uishe au usiishe hivyo, ni jukumu lao kuweka nguvu ya pamoja ili kuiokoa jamii dhidi ya janga hilo.

“…Ninaamini kabisa kama wanawake wote wataunganisha nguvu, wakasema mimi siwezi kuzini wala kufanya uasherati, basi UKIMWI utaisha kwa sababu mwanaume atatoka huko anakuja na shetani wake akija kwa huyu, anaambiwa NO, akienda kwa huyu anaambiwa NO, mwisho anaona aibu anatulia,” alisema.

Ugonjwa wa UKIMWI ambao unazidi kuangamiza mamilioni ya watu, kwa kiasi kikubwa huenezwa kwa njia ya kuvunja Amri ya Mungu inayozuia kuzini.

Aidha, Mchungaji Mwakamyanda, alihimiza kila mwanandoa kuiheshimu ndoa yake na kuitii Amri ya Mungu ya kutokuzini huku, wasio na ndoa wakibaki waaminifu bila kushiriki vitendo vya ndoa.

Alisema endapo jamii itaelewa usahihi huo, upo uwezekano mkubwa wa kushinda vita hii.

Njia nyingine zinazochangia kuenea kwa ugonjwa wa UKIMWI, ni kuchangia vyombo vya kutogea visivyochemshwa sawasawa, kuongezwa damu isiyopimwa, na mawazo potofu ya kuamini kondomu kama kinga ya nguvu dhidi ya UKIMWI.

WAWATA Moshi waadhimisha miaka 30

Na Aneth Mwakatobe, SAUT, Moshi

WANAWAKE Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Jimbo la Moshi, wameadhimisha miaka 30 tangu Umoja huo uanzishwe hapa nchini sambamba na uoneshaji wa kazi za mikono.

Maadhimisho hayo, yalianzia ngazi ya vigango, parokia na hatimaye kilele chake kufanyika ngazi ya Jimbo.

Maonesho ya kazi za mikono za wana WAWATA, yalizinduliwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bibi Betty Minde ambapo katika nasaha zake, aliwataka akinamama hao watambue kuwa jukumu la malezi walilo nalo ni zito hasa siku hizi.

Aliwataka wawe walezi bora na imara, waimarishe malezi adilifu, wawe tayari kukemea na kupambana na maadili potofu na mabovu, umasikini na uchumi tegemezi na pia kupambana na kuenea kwa UKIMWI.

“Mwanamke ana nafasi muhimu kama mama mlezi, hivyo anapaswa kutumia kila mbinu kuchangia katika kuondoa matatizo mengi na sugu yanayokabili jamii,” alisema Mwakilishi huyo wa Mkuu wa Mkoa.

Maadhimisho hayo yaliyo hudhuriwa na Parokia 31 kati ya 48 za Jimbo hilo, yalitanguliwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Padre Alexander Ndesario.

Parokia za Kindi, Chekereni na Korongoni ndizo zilizoibuka washindi wa maonesho ya kazi za mikono za akina mama hao.

Bunini mikakati ya kupata pesa, msitegemee misaada-Monsinyori Kangalawe

Na Leocardia Moswery,SAUT

WAAMINI wa Kanisa Katoliki nchini wametakiwa kushirkiana katika kubuni mikakati ya kupata kipato cha kuendesha Mashirika ya Kipapa badala ya kutegemea misaada kutoka nje.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturujia katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Monsinyori  Julian Kangalawe wakati akifungua  Semina ya Mashirika ya Kipapa Kanda ya Mashariki iliyofanyika katika kituo cha Kiroho Mbagala jimboni Dar es Salaam.

Mosinyori Kangalawe alisema vongozi wakishirkiana na walei katika kuweka mikakati ya kupata pesa,mashirika hayo yataweza kujitegemea badala ya kuwa tegemezi kwa Mataifa mengine hususani yale ya Magharibi.

Mbali na hayo,Monsinyori Kangalawe aliwataka viongozi wa dini watambue kuwa wao ni chachu katika kuhamasisha na kuendeleza uinjilishaji wa Neno la Mungu.

“Viongozi  wajitambue kuwa wao wanapaswa kuwa mstari wa mbele ili Uinjilishaji  uweze kukomaa na kuingia ndani kwa kila mtu, awe mtoto ama  mkubwa”alisema Monsinyori Kangalawe.

Naye Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Taifa, Padre Liberatus Mwenda aliwaambia washiriki wa semina hiyo kuwa waamini wengi wanaona ugumu wa kutoa michango kwa ajili ya ujenzi wa kitu fulani kwa vile awali walizoeshwa na Wamisionari kufanyiwa kila kitu bure.

“Waamini wengi hawajui maana ya ‘toa ndugu’ kuwa ina maana gani!  kitendo hiki  kinawafanya washindwe kuchangia kanisa kwa maendeleo zaidi”alisema.

Aliongeza “Wamisionari wa zamani hawakuwashirikisha waamini wakati wa ujenzi wa makanisa, mahospitali, shule pamoja na miradi ya maendeleo ya kanisa, kitu ambacho kiliwafanya kubweteka zaidi na kushindwa kuelewa pesa ilikuwa ikitoka wapi”.

Nao washiriki wa semina hiyo ambao walitoka katika Majimbo Katoliki ya  Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mahenge na Dodoma, walishauri  Maparoko wa Parokia mbalimbali kuwashirikisha waamini katika miradi ya kanisa.

BAADA YA KUMALIZA MGOGORO WA MISHAHARA KATIKA KIWANDA CHA URAFIKI

Wayanyakazi sasa  wadai nyumba za kiwanda  ni chafu

            Na Anthony Ngonyani

BAADHI ya wafanyakazi  wa Kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichopo jijini Dar es Salaam,wanaoishi kwenye nyumba za Kiwanda hicho,wamedai kuwa nyumba hizo ni chafu.

Madai hayo yamekuja siku chache baada ya kumalizika kwa mgogoro wa nyongeza ya  mishahara baina ya wafanyakazi na uongozi wa kiwanda hicho.

Wakizungumza na KIONGOZI kwa nyakati tofauti,wafanyakazi hao walidai kuwa nyumba hizo ambazo zimejengwa kwa mtindo wa ghorofa,ni chafu na hazijapigwa rangi muda mrefu sasa.

Wafanyakazi hao ambao walizungumza kwa masharti ya majina yao kutoandikwa gazetini kwa kuhofia kufukuzwa kazi,walidai kuwa tatizo hilo tayari limekwisha pelekwa kwa uongozi wa kiwanda,lakini hakuna hatua iliyokwisha chukuliwa.

“Majengo haya yalipakwa rangi kwenye miaka ya 80,hadi leo yamechakaa sana utadhani wanakaa wanyama na si binadamu”alisema mmoja wa wafanyakazi hao.

Licha ya uchafu,wafanyakazi hao walidai kuwa nyumba hizo pia zinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa taa hususani katika ngazi za kupandia , ambapo walidai zilizokuwepo siku za nyuma, kwa sasa zimeharibika.

Walisema hali hiyo ni hatari katika maisha yao kwani hulazimika kupanda juu kwa shida wakati wa usiku.

Hivi karibuni wafanyakazi wa kiwanda hicho waligoma kufanyakazi kwa muda wa siku moja kwa kile walichodai kuwa wanafanyishwa kazi ngumu na kupewa mshahara kidogo.

Hata hivyo mgomo huo ulizimwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,Luteni Yusuph Makamba ambaye aliuita uongozi  wa kiwanda hicho ofisini kwake na kujadiliana na kufikia muafaka wa kuboresha mishahara ya wafanyakazi hao.