Katiba ya nchi haitutendei haki- Walemavu

l ‘Polisi wanatudhihaki, nyumbani wanatucheka’

l     Wengine tunaajiriwa kwenye gorofa    zisizo na lifti, tutapandaje?

l     ‘Wanawake walemavu ni mawindo rahisi ya wabakaji'

Na Joseph Sabinus

KATIBA ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeliliwa na Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), kuwa haiwatendei haki walemavu kwa kuwa haitamki bayana juu ya haki zao jambo linalowafanya wadhihakiwe wanapobakwa, wakose ajira wanazostahili na kuishi kwa kuombaomba.

Katibu Mkuu wa SHIVYAWATA, Bw. Kaganzi Rutachwamagyo, aliliambia KIONGOZI mwanzoni mwa juma ofisini kwake jijini Dar es Salaam kuwa, mateso na maisha magumu wanayoishi walemavu nchini, yanatokana na Katiba kutotamka bayana juu ya haki zao na jamii kuwapuuza walemavu wa namna zote.

“Hatupewi haki na mamlaka husika. Kwa mfano, Katiba ya nchi imekaa kimya, itazungumzia rangi na jinsia, lakini haitamki bayana juu ya haki za mtu mwenye ulemavu.

Hali hii inatunyima nguvu za kisheria kudai haki na badala yake, eti tunabaki kutumia matamko ya kimataifa. Haki za binadamu na utawala bora, ni kwa wote bila kujali umbile la mtu, lakini sasa utashangaa yanayoangaliwa ni makundi maalumu, hasa wanawake na watoto, lakini walemavu hawazungumziwi kabisa,” alisema Bw. Kaganzi.

Alisema kutokana na hali hiyo, walemavu wamekuwa wakiishi kwa hali ya kutegemea badala ya kujengwa na kuendelezwa katika misingi ya kujitegemea kutokana na uwezo wa maumbile yao.

Alipoulizwa ni haki za namna gani wasizopewa walemavu, Bw. Kaganzi alisema, “Kuishi ni moja ya haki za msingi ya kila mtu. Sasa kama mimi ni mlemavu, sina ajira na hakuna mpango wowote mimi nitaishije?

Mataifa mengine yana mpango mahsusi kwa jamii kuona kwamba walemavu wanapewa ajira, na wasioweza kufanya kazi kabisa, wanasaidiwa na jamii kupata mahitaji yao, lakini hapa kwetu, kama wewe ni mlemavu, ole wako na hasa kama utakuwa katika familia isiyo na uwezo,” alisema.

Akaongeza, “Kutokana na hali hiyo, ikitokea aliyekuwa anakuhifadhi akafa, sijui utafanyaje au utaenda wapi, maana yake ni kwamba na wewe ufe sasa.”

Alisema ni wajibu wa jamii ya Watanzania kutambua kuwa walemavu wengine wana uwezo wa kuajiriwa au kujiajiri na hivyo, iwasaidia ili wajitegemee na kuondokana na mazingira yanayohatarisha utu na maisha yao.

“Ukimkuta mtu anaishi kwa kuchakurachakura, kuombaomba barabarani huku akipewa masazo, utu wake unashushwa na kuwa chini ya utu,” alisema Katibu Mkuu huyo wa SHIVYAWATA.

Akaongeza, “Tunasikitika kwa sababu nchi hii sio masikini, tatizo ni mipango mibaya ya kijamii na baadhi ya watu kutaka maisha ya anasa. Hebu jiulize, mtu anafikiria kununua ndege ya mabilioni ya pesa wakati kuna watu ambao hawana uhakika wa kuishi.”

Alitoa mfano akisema kuwa, kuna baadhi ya mataifa makubwa kama Uingereza na Ujerumani, lakini viongozi wao hawana ndege zao na akahoji kuwa kama hivyo ndivyo, iweje kwa nchi changa kama Tanzania kuwapo kwa wazo hilo?

Alisema kutokana na kasumba iliyojengeka miongoni mwa wanajamii wengi ya kutowathamini walemavu, ni wanaume wachache wanaowaoa wanawake wenye ulemavu na kwamba hali hiyo, imesababisha walemavu kuoana wenyewe kwa wenyewe.

Aidha, Bw. Kaganzi alibainisha kuwa, kutokana na maumbile yao na namna jamii inavyowatazama, wanawake walemavu wamekuwa wahanga wakubwa wa watu wenye nia mbaya na mawindo rahisi ya wabakaji.

“Wanabakwa na ushahidi upo, lakini hawana pa kulilia, wakienda polisi, askari wanawadhihaki eti aliyekubaki alitamani nini kwako kwa jinsi ulivyo, akija nyumbani, wanamcheka kuwa anajifanya; hana kinga wala tiba ni kana kwamba hakubaliki kwenye jamii; sijui aende wapi?”

Alisema takribani wanawake 4 kati ya 10 wanaosimulia kubakwa katika mikutano na semina mbalimbali, wanasema wanapoeleza hali hiyo nyumbani kwao, huishia kuchekwa na kudhihakiwa na kwamba hali hiyo haitofatiani na hali wanayokumbana nayo katika vituo vya polisi.

Alisema mang’amuzi yake yamebaini kuwa, Serikali na jamii kwa jumla wanafanya kosa la kufikiri kuwa suala la walemavu linawahusu wahisani wa nje na hasa asasi za kidini, jambo ambalo halina budi kupuuzwa.

Alisema, “Sasa, utagundua kuwa mtu mwenye ulemavu ni vigumu na fursa ni ndogo  kufanyiwa usaili na akapata kazi hata kama amefanya vizuri usaili”.

“Hata ukipata kazi, wakati mwingine tunaenda tu, kwa kuwa tuna shida na tuna hamu ya kufanya kazi, lakini mazingira yanatuondoa. Kwa mfano, baadhi ya majengo yana gorofa 8 na hakuna lifti, utaendaji, inabidi ujitoe mwenyewe,” alisema.

Alisema Tanzania haina budi kuiga mfano bora wa nchi nyingine, zenye utaratibu na sheria maalumu kuwa asilimia fulani ya wafanyakazi, lazima wawe walemavu na pia, kampuni au shirika linaloajiri walemavu wengi,  linapunguziwa kodi.

KIONGOZI lilipomuuliza kuwa asasi za dini zinawasaidia vipi, Bw. Kaganzi alisema, “Bahati mbaya zaidi ni kwamba, baadhi ya dini, zinawatumia walemavu kama ngazi ya kujijengea nafasi ya kuingia peponi,”“…hao wanataka walemavu mbaki hivyo hivyo kimaendeleo ili uendelee kuja kwake, atoe sadaka akupe, ajijengee suna; dini na madhehebu ya namna hiyo sisi walemavu tunaziona kama maadui zetu kwa sababu hawatupendi.”

Akaongeza, “Kutusaidia ni vizuri, lakini, hatuwezi kuufanya msaada huo katika njia nyingine bora zaidi, labda tukaanzisha mfuko ili kama walemavu wanataka kujenga, wajenge na kama ni kuanzisha mradi mwingine, waanzishe ili mradi tu, utu wao haudhaliliki.”

Alisema hali ya kuwajenga na kuwaendeleza walemavu katika misingi ya kuwa tegemezi, inavipatia shida vyama vya walemavu kwani inawafanya walemavu washindwe kujitambua, kujikubali na kuvitumia vipaji vyao kujiendeleza kiuchumi.

“Ukishajikubali, utajitafuta mpaka uone una uwezo gani uliobaki nao na uutumieje, lakini baadhi wanajengwa kuamini kuwa mlemavu, unaweza kuoshwa na Neno la Mungu; wanasema kuna miujiza njoo uombewe siku moja ujikute umeuvua ulemavu wako na hawafanyi kitu wanabaki kukaa kusubiri miujiza.”

Alisema kwa sasa SHIVYAWATA imejiwekea malengo ya jumla katika Programu ya kitaifa kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema malengo haya yana uhakika wa kutekelezwa kwa kipindi hicho kwa kuwa yapo ndani ya uwezo wa SHIVYAWATA, jambo mojawapo la msingi likiwa kujenga uwezo wa ndani.

“Unajua viongozi tunachaguliwa kutoka mazingira tofauti, yupo aliyesoma sana, ambaye hakusoma kabisa, kuna aliyewahi kuwa Kiongozi na mwingine hakuwahi; sasa wote mnajikuta ni viongozi wa taifa, hivyo, kumwambia mtu mpaka akubali, akusikilize, akuelewe, akubali kutenda unachomwambia, unahitaji sanaa. Sasa hilo sisi hatuna,” alisema Kaganzi.

Akaongeza, “Kwa hali hiyo, mnaweza kujikuta kuwa mnapoweka mikakati, viwango vya utendaji vinaweza kupishana ndiyo maana tunataka kujengeana kwanza uwezo wa ndani; kwamba wote tuwe na uwezo, ama tuwe na kikundi maalumu kinachoweza kuongea na jamii kikasikika.”

Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (SHIVYAWATA), linavihusisha Vyama vya Wasioona, Wenye Ulemavu wa Viungo, Albino, Walemavu wa Akili, Viziwi na Wasioona Viziwi.

Viongozi wengine wa SHIVYAWATA ni Israel Kagaruki( Mwenyekiti), Eva Bwisaro(Makamu Mwenyekiti),Dickson Mnveyange(Naibu Katibu Mkuu), Abdillah Omari (Mweka Hazina) na Lupi Maswanya (naibu Mweka Hazina).

Umefika wakati Watanzania wakatambua kuwa ulemavu au jinsia sio sababu ya mtu kubaguliwa wala kutoshirikishwa katika shughuli za kijamii.

Wapo wengi wenye ulemavu, lakini wanaweza kufanya mambo makubwa na yenye manufaa kwa Kanisa na jamii kwa jumla.

Ni vema jamii isiwatenge walemavu na pia, Serikali isikilize kilio chao. Iwakumbuke katika mipango yake ili wawe na uhakika wa namna ya kuendesha maisha yao.

Hali hii itasaidia kuondokana na tatizo la ombaomba na kasi ya kuongezeka kwa watoto wa mitaani. Pia, itapunguza wimbi la umaskini na kupunguza kasi ya maambukizi ya UKIMWI.

Kila mtu ana haki mbele ya sheria, kumpuuza na kumdhihaki mtu aliyetendewa unyama, ni unyama zaidi kuliko ule wa mtenda.

Muislamu, Mkatoliki mnataka kuoana; mnayajua haya?

l Waislamu wanaamini Ibada ya mwenye                  ndoa inathawabu zaidi

 

MIONGONI mwa mambo yanayohangaisha vichwa vya  wengi, ni suala kuwa Muislamu akipendana na Mkatoliki, wanaweza kuoana, na kama ndiyo au siyo, ni mambo gani ya msingi kuyajua.

Inaendelea Uk. 3

 

ILI kujibu swali kama Muislamu anaweza kuoana na Mkatoliki, ni vema tukajua kwanza mafundisho muhimu ya ndoa yaliyo katika dini hizi ambapo ikitokea wakaoana, ndoa hiyo huitwa ndoa  mchanganyiko.

Ujuvi wa mafundisho ya kidini katika ndoa hizi ni muhimu kwani kinyume na hapo, upo uwezekano mkubwa wa  ndoa baina ya Muislamu na Mkristo kuchukuliwa kama isiyowezekana kumbe inawezekana na pia, upo uwezekano kuwa ndoa baina ya watu hao waliopendena, ikawa ya furaha, lakini maisha ya kila siku yakawa magumu.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Kanisa Katoliki,  mchumba Mkatoliki anayetaka kuoana na Muislamu, hana budi kupata kibali maalumu toka katika mamlaka maalumu ya Kanisa.

Kibali (ruhusa) hiyo maalumu, ni lazima kitoke kwa kiongozi wa Kanisa mwenye mamlaka  ya kisheria ili ndoa hiyo iwepo na ikubalike yaani Askofu wa Jimbo husika.

Kwanza, ni muhimu Mkatoliki huyo akatambua kuwa lazima awe tayari kutoa mafundisho ya Kikatoliki kwa watoto atakaowapata ndani ya ndoa hiyo na kuwakuza katika misingi ya imani ya Kikatoliki.(Rejea Sheria za Kanisa 1124, 125, 1086).

Kwa ruhusa hiyo maalumu ya Kanisa, mtu huyo ataruhusiwa kuendelea na mipango yao na ndoa itafungwa mbele ya Padre kwa mujibu wa Sheria ya Kanisa.

Kabla hatujaingia zaidi katika kujua mafundisho hayo ya ndoa za Kiislamu na Kikatoliki, hebu tuangalie kwa undani na kumjua Muislamu ni nani, na Mkatoliki ni nani.

Muislamu ni mfuasi wa wa dini ya Kiislamu. Dini hii ilianzishwa na Mtume Muhammad, wakati Mkatoliki, ni Mkristo na mfuasi wa Yesu Kristo. Yesu Kristo ndiye Muasisi wa Ukristo katika Karne ya Kwanza.

Ni wazi kuwa ingawa Uislamu na Ukristo ni dini tofauti, lakini zinafanana kwa mambo mengi ya kiimani. Miongoni mwa mambo haya ni ukweli kwamba dini zote hizi yaani Uislamu na Ukristo, waamini wake wanaamini na kumuambudu Mungu mmoja wa kweli. Wote wanaamini  kuwa Mungu huyo ndiye Muumba Mbingu na nchi na vyote vinavyoijaza.

Hata hivyo, dini hizi pia zinatofautiana katika mambo mbalimbali kama siku za kuabudu, kwani Waislamu siku yao kuu ya kuabudu ni Ijumaa wakati Wakristo wengi huitumia Jumapili kama siku maalumu ya kuabudu.

Mengine ni tofauti juu ya maisha ya sakramenti na taratibu na sheria zinazoongoza maisha ya kila siku.

Wakati Waislamu wanatumia Kurani katika mafundisho yao na maadili, Wakristo hutumia Biblia.

Waislamu wanaamini kuwa Kurani ina Ufunuo wa Mungu kwa Mtume Mohammad.

Pia, mafundisho ya maadili ya Kiislamu hutoka katika rekodi (kumbukumbu) za matendo ya Mtume, zinazojulikana kama SUNNA ikiwamo mifano ya matendo na isiyo ya matendo.

 Hata hivyo, mkusanyiko huu huitwa HADITH na zinaikamilisha Kurani.

SHARIA ina mafundisho ya  Kanuni za Maadili na inagusa muundo wa kuabudu na namna ya kuishi katika jamii.

Sheria na taratibu za ndoa kwa Waislamu, huongozwa na SHARIA.

Mafundisho yote yanayohusu ndoa katika Uislamu, huchukuliwa kutoka katika Kurani na SUNNA ya Mtume Mohammad.

Kwa mujibu wa Kijitabu cha Kiingereza kiitwacho, ABOUT CATHOLIC/ MUSLIM MARRIAGE, kilichoandikwa na Prisca M. Wagura, Kwa Wakatoliki, Biblia ndiyo (Maandiko Matakatifu) yanayoeleza namna Mungu alivyoanzisha ndoa alipompatia Adamu mwenzi wake (Mwanzo 2: 18).

Hivyo, Wakristo kwa jumla na hususan Wakatoliki, huchukua mafundisho yao mengi juu ya ndoa toka kwenye Biblia.

Katika Biblia, imeelezwa kuwa Mungu ndiye asili ya ndoa. Kwamba alishuhudia ndoa ya kwanza aliyoiweka baina ya Adamu na Eva.

Pia, kazi ya ndoa, maisha ya Sakramenti na ya kiroho katika ndoa, yanaelezwa kutoka katika Biblia. (Rejea Mwanzo: 26- 27; 1Kor 7:39).

Biblia ni Neno la Mungu, hivyo Mungu anahimiza kuwafundisha na kushuhudia ndoa zote za Kikristo kwa kusoma Maandiko Matakatifu.

Kanisa lina sheria na taratibu zinazoliongoza na kuwalinda wafuasi wake katika njia sahihi katika masuala yote yakiwamo ya ndoa. Taratibu hizi zipo katika Sheria za Kanisa (Canon Law).

Hivyo, Biblia, Kanisa na Sheria za Kanisa ni nguzo na msingi wa mafundisho katika mitazamo yote ya maisha ikiwamo ndoa.

Kwa mujibu wa Waislamu, ndoa ni muunganiko wa watu wawili wa jinsia tofauti wanaokuwa mwili mmoja. Suala hili katika jamii linatazamwa kwamba wameungana, na ndivyo jamii inavyowachukulia.

Kwa mujibu wa Waislamu, kila mtu; mume au mke, lazima aoe au aolewe (mke). Hivyo, ndoa ni sehemu ya kutimiza mapenzi ya Mungu (wao humuita ALLAH).

Kwa Waislamu ndoa ni mkataba ambao kila Muislamu lazima aingie labda tu, awe amezuiliwa kwa sababu nzito zinazokubalika (Kurani 24: 32)

Ndoa huchukuliwa kama takatifu na tendo takatifu na mkataba wa kijamiii wenye wajibu na majukumu mazito na mengi.

Kwa Wakatoliki, Sheria za Kanisa za Mwaka 1983, ndoa ni agano muhimu itolewayo baina ya mwanamke na mwanaume ili iwape muunganiko utakaowafanya kila mmoja awe na wenzake kwa maisha yao yote (CAN 10551).

Pia, Maandiko Matakatifu yanathibitisha kuwa mke na mume waliumbwa na Mungu ili kila mmoja awe kwa ajili ya mwenzake na ndiyo maana Mungu alisema kuwa, haikuwa vema kwa mume kuwa peke yake (Mwanzo  2:18).

Hivyo, ndoa ni mapenzi ya Mungu aliyempa Adamu msaidizi wake, mwili katika mwili wake (Mwanzo 2: 24).

Katika umoja wao wa upendo, mume na mke wamekuwa mwili mmoja katika ndoa.

Uwepo wa Yesu Kristo katika harusi ya Kana, unathibitisha utimilifu na uzuri wa ndoa (Yn 2:1-11).

Ndoa kama Sakramenti ni ishara ya upendo wa Mungu kwa binadamu, na upendo kati ya mume na mke unaoashiria upendo mkuu wa Mungu kwa watu.

Hivyo, ndoa inaweza pia kuelezwa kuwa ni matokeo ya uamuzi uliofikiwa na wawili kwa heshima, uaminifu na upendo wa kila mmoja kwa mwenzi wake hadi kifo.

Tukija upande wa kazi za ndoa, tuanze na Waislamu.Kwa Waislamu, ndoa ndiyo njia pekee ambayo wameruhusiwa kukidhi tamaa za kimwili. Uhusiano mwingine wa namna hiyo nje ya ndoa, ni kinyume cha sheria (Kuran 25: 54).

Pia, kwa Waislamu ndoa ndiyo njia halali ya kupata watoto na kuendeleza kizazi. Pia, ndoa huwafanya waamini wa dini hiyo ya Kiislamu waishi kimaadili tangu kwa mtu mmoja mmoja, familia na jamii kwa jumla.

Ndoa huwasaidia waamini waepuke kutenda dhambi na inadaiwa kuwa, ibada au (sala) za mtu aliyeoa au kuolewa, zinathawabu kubwa kuliko ndoa za waislamu ambao hawajaoa au kuolewa. (Moula in Kitaabun Nikah P 22).

Lakini pia, kupitia ndoa, Muislamu anampata mtu kamili wa kupendana ambaye pia atampenda yeye (kupenda na kupendwa).

Ni baraka kubwa kwa Waislamu, kwa upande mmoja kupata mwenza; na ndoa inajenga uhusiano na watu wengine.

Usikose toleo lijalo kupata mwrendelezo.

Muumini wa kweli huisaidia Serikali, Kanisa kuleta maendeleo- Askofu Banzi

Na Lazaro Blassius, Tanga

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Tanga, Mhashamu Anthony Banzi, amesema waamini wa kweli katika dini yoyote ni wale wanaoshirikiana na Serikali kuleta maendeleo na amani ikiwa ni pamoja na kulipa kodi ili taifa lisiwe tegemezi.

Aliyasema hayo hivi karibuni wakati wa sherehe za ufunguzi wa nyumba ya mapadre iliyojengwa na Wanaparokia ya Mtakatifu Augustino iliyoko Manundu mjini Korogwe.

Ujenzi wa nyumba hiyo ulianza miaka mitatu iliyopita kwa shilingi milioni 18.Nyumba hiyo  imejengwa kwa michango ya watu mbalimbali wa ndani na nje ya mji wa Korogwe.

Katika sherehe hizo zilizofanyika Jumapili iliyopita (Oktoba 20), katika Ukumbi wa Parokia hiyo na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, vyama vya siasa na Serikali wilayani humo akiwemo Mkuu wa Wilaya, Victoria Katambala, Askofu Banzi alisema waamini wa kweli ni wale wanaoshirikiana na Serikali katika kutimiza haki na wajibu wao.

Aliongeza kuwa, ni wajibu wa waamini kushirikiana na Serikali yao katika kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kujenga shule, hospitali, barabara, na huduma muhimu za kijamii na kulipa kodi.

Alisema sambamba na kutimiza wajibu huo, waamini hao hawana budi kuzishika vema Amri za Mungu na kuyaishi mafundisho ya imani zao.

Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa viongozi kuishi maisha ya uadilifu katika imani zao, kuzingatia haki, uaminifu na kuwajibika ili kuiandaa jamii na kizazi kijacho kuwa na viongozi bora.

“Wanakanisa na wakazi wa Korogwe mmeonesha mfano halisi wa ushirikiano wa pamoja; mnaweza kufanya mengi huu ni mfano wa kuigwa na parokia nyingine, kutegemea misaada ya nje kabla ya kuonesha juhudi za wananchi ni kudumaza vipaji vyetu,” alisema Mhashamu Banzi.

Aidha, ameipongeza Kamati ya Ujenzi chini ya ushirikiano wa Padre Silas Singano na Mwenyekiti, Francis Mbuya, kwa kuwashirikisha watu katika kujiletea maendeleo yao kiroho na kimwili.

Habari zaidi zilizopatikana zinasema kuwa, akisoma risala ya waamini, Katibu wa Parokia ya Manundu, alisema kuwa Parokia hiyo ina kusudia kujenga makanisa 11 ya kudumu vigangoni, hosteli, nyumba ya masista na shule ya awali parokiani hapo.

Shule ya awali iliyopo imejengwa kwenye kilima kirefu hivyo inawawia vigumu watoto kufika kituoni hapo, hivyo itahamishwa na kujengwa eneo jingine karibu na Kanisa.

Wakati huo huo: Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi, Fedha na Mipango katika Parokia hiyo, Francis Mbuya, amesema kuwa Parokia hiyo inatarajia kuanza ujenzi wa Kigango cha Msambiazi na wanao mpango wa kukiboresha ili kiwe kituo cha sala na tafakari.

 

Mapadre, Walei tumikianeni kwa upendo – Wito

Na Sarah Siwingwa

WITO umetolewa kwa mapadre na walei wote ndani ya Kanisa kutumikiana na kushirikiana kwa upendo kwa kuwa wote ni viungo muhimu katika kulijenga Kanisa.

Wito huo ulitolewa Jumamosi iliyopita na Kaimu Katibu Mtendaji wa Idara ya Mawasiliano ya Jamii, katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Revocatus Makonge, wakati akitoa mada katika semina ya viongozi wa jumuiya zote za Parokia  ya Tabata, Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam.

Alisema ni muhimu waamini wa ngazi zote za kanisa wakatambua kuwa, Walei ni watu muhimu badala ya hali ilivyo sasa ambapo baadhi ya waamini hufikiria kuwa, Walei ni watu wa mwisho katika kanisa.

Padre Makonge alisema kuwa, kasumba ya kudhani kuwa walei ni watu wa mwisho katika kanisa, imechangia kuchelewesha maendeleo ya haraka ya kukua kwa utume katika kanisa.

 “Tunapofikiria kuhusu Walei, lazima tujue kuwa sisi sote ndani ya Kanisa ni Walei, hivyo basi mapadre na Walei tutumikiane kwa upendo. Toa utume wako pale ulipo, tuheshimu dhamiri zetu zilizo safi kwa kutekeleza imani yetu,” alisema.

Katika semina hiyo, Padre Makonge alisema, walei hawana budi kuwa wanyenyekevu mbele ya Mungu ili wawavute watu wengine kumtangaza Yesu ili waamini wasiyumbishwe kiimani na madhehebu mengine.

Ili tumkiri Kristo, tunatakiwa tujue imani yetu inatudai kitu gani ili tusimamie na kuitetea,” alisema.

Alisema bila kuielewa vema imani ya Kanisa, ipo hatari ya waamini kuzitumia vibaya sakramenti za kanisa.

Naye katibu wa Tume ya Haki na Amani ya TEC, Padre Vic Missiaen, alisema katika semina hiyo kuwa, kiongozi yeyote wa Kanisa ni mfuasi wa Yesu na hana budi kuwa mfano bora wa kuigwa na wanakanisa wengine.

“Kiongozi wa Kanisa ni mtu anayeongoza watu kuwaonesha njia ya kumfuata Yesu na sio sawa na viongozi wengine. Lazima awe na msingi bora wa kiroho na anayetafuta hekima katika Neno la Mungu,” alisema.

Alisema kiongozi bora wa Kanisa ni yule anayefurahia pindi anapoona jamii inaishi kwa kumfuata Yesu Kristo kwa kuwa kazi ya kiongozi huyo ni kujenga na kuimarisha imani ya jamii.

“Uongozi ni kujitoa kwa jamii, kuonesha moyo wa kujitolea kwa watu kwa kuwa mshahara wake ni Mungu kuingia moyoni mwako,” alisema.

Wakati huo huo: Mwenyekiti wa baraza la walei, Parokia ya Tabata, Bw. Joseph Ibreck, amesema hiyo ni semina ya kwanza kufanyika parokiani hapo kwa ajili ya viongozi wote wa jumuiya za parokia hiyo na kuongeza kuwa mahudhurio yanatia moyo.

Watoto wa mitaani, yatima watakiwa kuwatia moyo wahisani

Na Brown Sunza

ILI  kuwatia moyo wafadhili mbalimbali kuendelea kutoa misaada yao, watoto wanaolelewa katika vituo mbalimbali nchini wametakiwa kuonesha bidii katika masomo yao yakiwemo yale ya nadharia na vitendo.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Katibu Msaidizi  wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Parokia ya Kigamboni wakati akikabidhi misaada mbalimbali kwenye Kituo cha Kulelea Watoto  wa Mitaani  na Yatima cha Tuamoyo, kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi zawadi hizo kwa niaba ya wenzake, Bibi Mbagata alisema kuwa wafadhili wengi wanakata tamaa ya kuendelea kutoa misaada kwa watoto wenye matatizo, kufuatia watoto hao kujihusisha katika vitendo viovu badala ya kuzingatia masomo.

Aliwatahadharisha watoto hao wa Tuamoyo kutojihusisha na mambo ya anasa ambayo yatazidi kuwakandamiza kiutu na kuwapotosha.

“Epukeni kabisa matumizi  mabaya ya dawa za kulevya ambazo zina uwezo mkubwa wa kuwaathiri kiroho na kimwili,” alisema.

Akaongeza, “Dawa hizo zinaweza kuwasukuma kufanya vitendo visivyofaa vikiwemo vya uasherati ambavyo matokeo yake ni kupata maambukizi ya  Virusi vya UKIMWI na mimba zisizotarajiwa”.

Misaada iliyotolewa na WAWATA ni pamoja na sabuni, sukari, unga, dawa ya meno pamoja na vitabu vya sala.

Awali, akiwakaribisha WanaWAWATA hao, Mlezi wa Kituo hicho cha Tuamoyo, Bibi Annie Joseph, alisema msaada wa namna hiyo unaonesha namna akinamama hao wanavyoguswa na maisha halisi ya watoto wa mitaani na yatima.

“Moyo wa ukaribu na ushirikiano mlioonesha katika kuwakumbuka  watoto hawa, kiroho na kimwili unaonesha ni jinsi gani mnavyoguswa na maisha yao. Kwa kweli nashukuru na Mungu awazidishie moyo huo wa kujitolea” alisema.

Kituo hicho cha Tuamoyo kilianzishwa mwaka 1992 na hadi sasa kinawahudumia watoto wapatao 107 wakiwemo wa wasichana na wavulana.

Askofu Maluma awataka watawa kuwa kama mbegu inayokufa

Na Frt. Carlos Mwalongo, Njombe

MHASHAMU Alfred Maluma, Askofu wa Jimbo Katoliki la Njombe, amewaasa Watawa kumtumikia Kristo kama mbegu inavyokufa kwa ajili ya kuzaa faida.

Askofu Maluma aliyasema hayo wakati wa Jubilei ya Miaka 25 ya Watawa 25 na kufunga nadhiri za daima kwa watawa 6, iliyofanyika Oktoba 19, mwaka huu.

 Kama mbegu inavyokufa na kutoa faida kubwa baada ya kufa, vivyo hivyo Bwana Yesu Kristo alikufa msalabani kwa ajili yetu sisi na akafufuka mshindi dhidi ya mauti. Nasi tujitoe hivyo hivyo kwa ajili ya Yesu,” alisema.

Mhashamu Maluma, aliwaasa pia wanadhiri za daima kuwa maisha yao na huduma zao, zitumike kwa manufaa ya kanisa ili zizae matunda mengi na bora.

Waliofunga nadhiri za daima ni Sista Maria Letisia OSB, Sista Maria Martina OSB, Sista Maria Athanasia Lwila OSB, Sista Maria Scholastica Mtitu OSB na Sista Maria Benadicta Mmelo OSB ambaye kwa sasa yupo chuo kikuu  Dar es Salaam, Muhimbili.

Masista hao wa OSB, waliofanya Jubilee ya Miaka 25 ya Utawa wao ni Maria Irdebedeltha Mtewele, Maria Anselma Msemwa, Maria Odilia Mgaya, Maria Eliza Mbuligwe, Maria Odilia Mgaya, Maria Eliza Mbuligwe, Maria Dionisio Migodela, Bernadina Mwalongo na Sista Maria Laurentina Mhade.

Wengine ni Masista Maria Maktirde Kindimba OSB, Maria Prisila Mayemba, Frolencia Mhenga, Osmunda Mtewele, Flava Sanga, Teresfora Mfikwa, Gabriela Ngole, Oestela Mwenda, Frida Ndonyalo, Hiltrude Mangang’ara, Efigenia Mng’ong’o, Adetrude Mwinuka, Elaunora Mwalongo, Anjelina Mayemba na Mariana Ndetewale.

Pia, alikuwepo Mjubilanti wa miaka 50  aliyekuwa peke yake. Sista huyo Maria Mercedes Sambala OSB, alifunga nadhiri zake za kwanza mwaka 1952 huko Peramiho pamoja na wenzake wawili Sista Maria Paula OSB na Sista Maria Immakulata, OSB wote wa Chipole.

Matukio hayo yalitanguliwa na nadhiri za muda zilizofanyika siku moja kabla ya siku hiyo ambapo masista kumi waliweka nadhiri za muda.

Masista walioweka nadhiri hizo za muda wote wakiwa wa OSB, ni Maria Sabina Mwalongo, Maria Rehema Mwalongo, Maria Zeno Mwalongo, Maria Marina Mwandu, Maria Monica Mgaya na Maria Mwinuka na msista wengine ambao majina yao hayakupatikana mara moja.

 

Ndoa bila uvumilivu huzaa majuto- Padre wa Anglikana

Na Lilian Timbuka

KIONGOZI mmoja wa Kanisa la Anglikana, amesema ndoa isiyo na upendo wala uvumilivu ni hatari kwa maisha ya baadaye na inaweza kuzaa mateso na majuto.

Padre Oscar Mbuza wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, Parish ya Yombo, aliyasema hayo hivi karibuni katika Ibada ya Ndoa iliyofanyika kanisani hapo.

 Alisema kupendana na kuvumiliana ni vitu muhimu katika maisha ili ndoa idumu na kuzaa matunda bora.

Alisema ndoa nyingi za Wakristo zinaingia doa la migogoro na hatimaye kuvunjika kwa kukosa upendo wa dhati sambamba na moyo wa kuvumiliana baina ya wanandoa.

“Ndoa ikijengwa katika misingi ya upendo wa ki-Mungu, ni wazi kuwa wanandoa watayafurahia maisha yao ikiwa ni pamoja na kujisikia raha wanapoishi kama mume na mke, kinyume na hapo ni ndoa yenye mateso na majuto maishani kabla ya kuvunjika,” alisema.

Alisema ili upendo uwepo na udumu baina ya wanandoa, lazima juhudi za kumtafuta Mungu pamoja na kusoma Neno na kulishiriki kikamilifu ziimarishwe katika familia.

Padre Oscar aliwataka wanaume wanaorubuniwa na wanawake wa nje ya ndoa, wajishinde na waache tabia hiyo kwani ni hatari kiroho na kimwili na badala yake, wawathamini, wawaheshimu na kuwapenda wake zao.

 “Leo unapita mitaani unakutana na kabinti kamepaka mkorogo kama Mzungu, eti Mzee unaanza kashfa kwa mkeo; unasema kuwa kazeeka, hivyo hana nafasi tena kwako. Jamani tuachane na kashfa hizi huyu ndiye chaguo la Muumba wako kwako. Kwani huyo Mzungu bandia wako hukumuona toka mwanzo?” alihoji.

Pia, alisema licha ya ukorofi unaotokana na wanandoa wenyewe, bado siku hizi ndoa za vijana wengi zinazidi kuwa mashakani pale inapofikia wazazi kuamua kuzitenganisha ndoa hizo takatifu kwa misingi ya kidunia.

Alisema wazazi ni watu muhimu sana hivyo pindi waonapo kuwa ndoa za watoto wao zinayumba, hawana budi, wakiwa wazazi, wazisimamie ndoa hizo zisivunjike.

“Wazazi wengine badala ya kuzinusuru ndoa za watoto wao, ndio wanakuwa chanzo cha kuvunjika; tena kwa sababu zisizokuwa na msingi. Hivi Maandiko Matakatifu yanasemaje? Kinachofungwa duniani, basi na mbinguni kimefungwa na wala binadamu hawezi kutenganisha hususan ndoa takatifu,” alisema.