Askofu Mwoleka afariki

l Ni muasisi wa Jumuiya Ndogo Ndogo nchini

l Ni mnyenyekevu mpaka kaburini

Na Mwandishi Wetu, Rulenge

Askofu Mstaafu wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Mhashamu Christopher Mwoleka, amefariki dunia na anazikwa Jumamosi hii jimboni kwake.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana toka kwa Askofu wa Jimbo la Rulenge ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Severine NiweMugizi, Marehemu Mwoleka aliyekuwa Askofu Mstaafu wa Jimbo la Rulenge alifariki dunia Jumatano iliyopita na kulifanya Jimbo hilo kujawa na simanzi.

Alisema, “Oktoba 16, mwaka huu yaani Jumatano, Jimbo lilijawa na wingu la majonzi lililofunika mbingu na nyoyo za Wanajimbo wa Rulenge walipopewa taarifa juu ya kifo hiki”

Akinukuu taarifa ya simu toka kwa Paroko wa Parokia ya Biharamulo, Padre Valentine, Askofu NiweMugizi alisema, “Baba Askofu Mwoleka ameaga dunia katika hospitali  hiyo ya Dk. Leonard Washington, amethibitisha kuwa Askofu amefariki kwa ugonjwa wa kisukari.”

Hayati Askofu Mwoleka, alizaliwa Agosti 9,1927 katika familia ya Bernardo Ndyetabura Mwoleka na Belina Nobireki, kijijini Kyeigoromora, Kagando – Kitwe, Parokia ya Itahwa, Jimbo la Bukoba.

Marehemu alikuwa MUHYOZA wa ukoo wa OMUGIRI.

Alibatizwa toka Uislamu akiwa na umri wa miaka  14,  Oktoba 4, 1941, katika Kanisa la Itahwa iliyokuwa chini ya Parokia ya Bunena kwa wakati huo.

Baada ya masomo  ya  sekondari katika shule za Kashasha na Nyakato-Bukoba, mwaka 1949, alipata mafunzo ya Ukarani jijini Dar es Salaam.

Kisha alifanya kazi serikalini kwa miaka 5 kama karani Idara  ya Elimu, Dar es Salaam.

Mwaka 1954 akajiunga na Seminari Ndogo ya Rubya kwa miaka miwili. Baadaye, alichaguliwa kuendelea na malezi ya Upadre katika Seminari Kuu ya Katigondo, Uganda mwaka 1956. Mwaka 1960, alikwenda Uingereza kuendelea na malezi ya Upadre katika Chuo cha Wamisionari wa Afrika cha Totterdge, London.

Alipewa Daraja ya Ushemasi MdogoJulai,12, 1961 na Ushemasi Mkubwa Septemba 13, 1961 kabla ya marekebisho ya Mtaguso wa pili wa Vaticano.

Alipata Daraja ya Upadre Juni 30, 1962, katika Kanisa la Whetstone, London na Kardinali Godfrey.

Kisha Marehemu Mwoleka alifanya kozi ya mwaka mmoja katika Sayansi na Jamii kwenye Chuo cha Claver – House, London, Oktoba 1962 hadi Julai 1963.

Baada ya kurejea jimboni, Askofu MWOLEKA akiwa Padre Mpya, alifanya kazi ya kichungaji ndani na nje ya Jimbo la Rulenge.

Kuanzia Agosti 20, 1963 hadi Februari 1965, alihudumia Parokia ya Rulenge akiwa Paroko Msaidizi.

Machi 1965 hadi Mei 20, 1966, alihudumia Parokia ya Katoke akiwa Paroko Msaidizi.

Mei 26,1965 hadi Mei 1966, alihudumia Parokia ya Kibondo jimboni Kigoma akiwa Paroko Msaidizi.

Juni 4, 1966, alirejea jimboni na kuhudumia Parokia ya Buhororo akiwa Paroko Msaidizi. Novemba 1967 hadi Novemba 1968 alikuwa Seminari Ndogo ya Katoke akiwa Mwalimu. Desemba 8, 1968 hadi Machi 5, 1969, alihamia Parokia ya Ntungamo akiwa Paroko.

Machi 6, 1969, aliteuliwa kuwa Askofu Msaidizi na Juni 19, 1969 alipewa Uaskofu katika Kanisa Kuu la Bukoba na Askofu Mkuu Sartorelli.

Juni 26, mwaka huo huo, Baba Mtakatifu Paulo wa Sita, alimtangaza kuwa Askofu wa Jimbo la Rulenge, na akasimikwa Novemba 18, 1969, akiwa Askofu  wa Pili na Askofu wa Kwanza Mzalendo jimboni humo.

 Alistaafu kazi ya Uongozi wa Jimbo mwaka  1996 kwa sababu ya afya mbaya kutokana na ugonjwa wa kisukari. 

Miongoni mwa mambo aliyohimiza wakati wa uongozi wake jimboni ni ujenzi wa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo na Mkamilishano.

Maaskofu wa AMECEA walipopitisha uamuzi kuwa uchungaji katika eneo la AMECEA ufanywe kwa njia ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo, alianza utekelezaji wake mwaka 1979 huo huo.

Aliporejea kutoka mkutano huo alianza kuandika mawazo yake juu ya muundo wa huduma mbalimbali katika Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo ziweje katika Jimbo lake.

Akatayarisha na kutoa semina kwa makundi ya Waamini, mapadre, masista na Walei kuhusu jambo hili.

Marehemu Askofu Mwoleka hatasahaulika kwa misamiati yake ya MTUMISHI, MNYUMBA, MJIMA, MLEZI, MCHUMI na mingine.

Lakini, kabla ya jumuiya hizi katika miaka ya 70, alikuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono Vijiji vya Ujamaa ambapo yeye mwenyewe aliishi katika Kijiji cha Nyabihanga akifanya kazi kwa mikono yake pamoja na wanakijiji. Huko ndiko alianza kupata umaarufu kama ‘Askofu anayepekua’ asiye na viatu. Jambo hili alikuja kuliendeleza katika sura ya Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo. Katika hatua iliyowashtua wengi, baada ya harakati za ujenzi wa jumuiya hizo, mwaka 1983, alianzisha jumuiya ya kwanza kubwa ya Mkamilishano baada ya kuvunja vikundi vitatu vikubwa kimoja kila dekania vya Wahamasishaji wakuu na wafuatiliaji uimarishaji wa Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo lilililokuwa kilele  cha lengo lake juu ya jumuiya.

 Na mara nyingi alitamka kuwa uaskofu wake wote hadi anastaafu ulijishughulisha na kutekeleza wazo hilo la Mkamilishano. Na kama kuthibitisha ukweli huo aliandika barua ya kichungaji aliyoiita ‘Katekesi Hai ya Kiumbe Kipya’ mwaka 1995.

Alisema barua hiyo ndiyo wosia wake kwa Jimbo la Rulenge. Katekesi hiyo alitaka iwe DIRA ya kuongoza Wakristo na Wachungaji na kuwawezesha kutambua walenge wapi ili kwa juhudi zao Ufalme wa Mungu ufike. Ingawa aliivunja rasmi Jumuia ya Mkamilishano Januari 1996, bado tunamshukuru sana kwa barua hiyo.

Pamoja na shughuli hiyo kubwa chini ya uongozi wake kwa miaka 27 yamekuwapo maendeleo makubwa katika Sekta mbalimbali.

Wakati wa uongozi wake zilianzishwa Parokia mpya tisa, katika kipindi cha uongozi wake, wamezaliwa Mapadre Wazalendo 58 na Shemasi mmoja, 55 wako hai akiwamo Askofu wa sasa wa Jimbo hilo.

Katika harakati za kufuta ujinga, alianzisha shule tano za Sekondari za Rulenge, Chato, Kaisho, Nyabiyonza na Rwambaizi. Pia, alianzisha vyuo vya ufundi stadi na Maarifa ya Nyumbani vya Mbuba RVTC, iliyokuwa Bugene Homecraft na Isingiro Homecraft.

Aliunga mkono juhudi za Serikali kupambana na maradhi. Chini yake, zilianzishwa Hospitali za Biharamulo, Isingiro na Nyakaiga. Pia zilianzishwa zahanati za Nyamirembe na Rwenkende.

Aliyakaribisha Jimboni Mashirika ya Dada Wadogo na Kaka Wadogo wa Yesu, na Mabruda wa Bene- Yosef toka Burundi ili wafanye kazi za kimisionari jimboni humo.

Pia, kama Tawi la Mkamilishano, alianzisha Usharika wa Masista Mitume wa Upendo upeo, ambao bado wanalelewa jimboni humo ili baadaye wawe shirika kamili.

Amelea pia, Shirika la Masista wa Mt. Bernadetta hadi tukasimika kama Shirika la Jimbo.

“Kwa fursa hii tunaishukuru sana Jumuiya ya Mkamilishano ya Ujerumani na Tawi lake la Tanzania waliosaidia kumtibu na kumtunza kwa vipindi tofauti huko Ujerumani katika kliniki yao ya Mt. COSMAS, NEUBIBERG na huko Merela Morogoro na Kijitonyama Dar es Salaam,” alisema Askofu Niwemugizi katika taarifa yake kwa KIONGOZI.

Akaongeza, “Kwa nyakati tofauti akiwa Ujerumani na Morogoro, aliniandikia mara tatu kuwa ameamua kuishi na Wanajumuiya hiyo hadi kufa kwake na kuzikwa Ujerumani au Morogoro, lakini baadaye mwaka jana mwezi Machi, aliamua upya kuwa anarudi Rulenge, tunafurahi kumpokea tena jimboni.”

Raha ya Milele umpe Ee Bwana na Mwanga wa milele apumzike kwa amani Amina.

‘Msitumie watoto mnaozaa kuwa kipimo cha UKIMWI’

Na Getrude  Madembwe, Iringa

“JAMANI! Acheni kujipa matumaini kwamba hamjaathirika na UKIMWI eti kwa vile  umejifungua mtoto salama na labda eti na mtoto huyo sasa umri wake ni miaka mitano na anaendelea vizuri kiafya”.

Kauli hiyo imetolewa na Mshauri wa Kituo kinachojishughulisha na masuala ya UKIMWI mkoani Iringa kinachojulikana kwa jina la Aramano, Bibi Roida Kimbe.

Alikuwa akitoa mada mintarafu haki za watoto katika semina ya Tume ya Haki na Amani Jimboni Iringa, iliyofanyika hivi karibuni  katika Hoteli ya Babtisti.

Alisema kuwa, kudhani kuwa mtu hajaathirika eti kwa vile mtoto wake anaendelea vizuri, ni  kujidanganya kwani watoto walioathirika na UKIMWI baadhi yao hufika hadi elimu ya sekondari, hivyo ni bora kujichunguza afya kiutaalamu.

Katika semina hiyo iliyohudhuriwa na mapadre, masista pamoja na walei kutoka katika parokia mbalimbali za Jimbo hilo, Bibi Kimbe aliwashauri akinamama kuchunguza afya zao kabla ya kupata ujauzito kwani kufanya hivyo, kutamnusuru mtoto.

“Mtoto anapozaliwa na virusi vya UKIMWI anakuwa amekosewa haki ya kuishi kwani si kosa la mtoto bali ni kosa ambalo limefanywa na mzazi wake,” alisema. Aliongeza, “Jichunguzeni kwanza kabla hamjaamua kuzaa kwani pindi mtakapozaa na ikagundulika kuwa mtoto wenu ana Virusi vya UKIMWI, mnakuwa mmemkosea haki yake ya kuishi kama binadamu wengine”. Aidha, Mshauri huyo alisema kuwa, watoto wachanga wenye virusi vya UKIMWI hugundulika kuanzia umri wa miezi 18 hadi 24 na baada ya miezi 24 huonesha dalili za ugonjwa wengine ambao hawapati matunzo mazuri hufa baada ya muda mfupi.

Pia, alisema kuwa mama mjamzito anapogundulika kuwa na virusi vya UKIMWI hupewa dawa aina ya NEVIRAPINE ambapo kidonge kimoja hukitumia kabla hajajifungua na kingine hukitumia anapokaribia kujifungua lengo likiwa ni  kuzuia kasi ya maambukizo kwa mtoto.

“Dawa hii huzuia maambukizo kwa mtoto kwa asilimia 90 lakini mama  anashauriwa  kutomnyonyesha  mtoto baada ya kujifungua,” alisema.

Aliongeza kuwa, mtoto aliyeambukizwa virusi vya UKIMWI ana haki ya kusoma na kupendwa kama watoto wengine, badala ya kuwaacha kwa kisingizio kwamba watakufa wakati wowote.

“Tuwaelimishe watoto wetu tuwaweke karibu na dini na tukifanya hivyo, Mungu atatusaidia kwani yeye ni mwema kwetu,” alisema.

Naye Shemasi Paul wa Ndugu Wadogo Wapya, alisema kuwa kila jumuiya haina budi kuwa na mpango maalumu wa kuwasaidia yatima.

“Tusiliachie Kanisa pekee yake katika kutunza yatima hili ni jukumu la kila mmoja wetu tuwatendee wema yatima na tuwajali na tukifanya hivyo, tutalifanya Kanisa liwe na sura ya Msamaria Mwema,” alisema

Katika semina hiyo kulifanyika uchaguzi wa viongozi wa Kamati Tendaji ya Tume ya Haki na Amani uliosimamiwa na Askofu Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, wa Jimbo la Iringa.

Bw. Jakobo Tibamanya alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Shemasi Paul, alikuwa Makamu Mwenyekiti na Katibu alikuwa Bibi Kevina Mwingira akisaidiwa naBw. Samweli Mtaki na Dada Laila wa Jumuiya ya Papa Yohane wa Kumi na Tatu alichaguliwa kuwa Mweka Hazina.

Pia, walichaguliwa Wajumbe saba wa Kamati hiyo ambao ni Panklasi Mgongolwa, Peter Mbala, Vicent Mwananilwa, Sista Rustika Mang’ong’o (CST), Sista Michela (MC), Mama Mwakabamba na Padre Gignui Tveglia.

Semina hiyo pia ilitoa tamko la kuungana na Baba Mtakatifu Yohane Paul wa Pili kuhusu mpango wa Marekani kutaka kupigana na Iraq kwani endapo vita hivyo vitatokea, watoto, akinamama na watu wengine wasio na hatia ndio wataathirika. Talaka ng'o katika Kanisa – Padre

  Na Elizabeth Stephen

KIONGOZI mmoja wa Kanisa Katoliki nchini, amesema kamwe Kanisa halitambui wala halitaruhusu talaka kwa waamini wake kwa kuwa alichounganisha Mungu, mwanadamu hawezi kutenganisha.

Paroko Msaidizi wa Parokia ya Chang’ombe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Padre Paul Njoka, aliwaambia washiriki wa semina ya siku moja juu ya uchumba na ndoa iliyofanyika parokiani kwake hivi karibuni na kuwashirikisha baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari jijini Dar es Salaam.

Alisema, “Lazima wakati huu jamii itambue kuwa Kanisa Katoliki linapowaunganisha wanandoa kutoka katika uchumba kwenda maisha ya ndoa, lazima kwanza wanandoa hao waelewe kuwa neno talaka halipo katika maisha yao na hata Kanisa halina kitu hicho,” alisema.

Padre Njoka aliishauri jamii kupitia vyombo mbalimbali vikiwamo vya kiserikali, kutoa kipaumbele katika mafunzo ya ndoa takatifu ili kuepusha ndoa kusambaratika na kusambabisha kuzagaa kwa watoto wa mitaani.

Alisema, “Inasikitisha kuona idadi ya watoto wa mitaani ikizidi kuongezeka  siku hadi siku. Hii inasababishwa zaidi na migogoro katika maisha ya ndoa ambayo hupelekea wanandoa hao kutengana na kuwaacha watoto wakihangaika.”

Alisema Kanisa linajitahidi kwa hali na mali kuhakikisha mafunzo yanawafikia wanandoa ili kuokoa ndoa zisisambaratike na akatoa wito kwa asasi nyingine kuunga mkono kwa hali na mali juhudi hizo za kanisa.

“Ni muhimu kufanya hivyo kwa sababu familia zenye tabia nzuri na maendelea hutoka katika ndoa iliyo takatifu.”

Aidha, aliwataka wanafunzi kote nchini kutojihusisha na mapenzi kabla ya ndoa kwani vitendo hivyo vinawakwaza kiroho, kielimu na kuwapa matatizo kiafya.

Akitaja madhara yanayotokana na kuolewa au kuoa katika umri mdogo, Padre Njoka alisema, msichana atakabiliwa na matatizo makubwa wakati wa kujifungua ikiwa ni pamoja na kutoka na damu nyingi, uchungu kuchukua muda mrefu kabla ya kujifungua, na kukosa uwezo kamili wa kumtunza mtoto.

Alisema sababu nyingine inayowafanya wazazi ama walezi wawaozeshe mabinti wao katika umri mdogo ni pamoja na wazazi kuogopa watoto kupata mimba kabla ya ndoa hali aliyosema inatazamwa na jamii kama kitendo cha aibu.

“Wengine eti wanataka waone wajukuu zao mapema, na kuna baadhi ya wazazi wanaofanya hivyo kwa tamaa za mali jambo ambalo sasa limepitwa na wakati na badala yake, wanawaweka watoto katika matatizo.”

Aliwataka wanafunzi hao kuvishinda vishawishi ambavyo vitawapeleka wao kupoteza nafasi zao za masomo, na badala yake, wasaidiane katika masomo, njia ambayo itawafanya wakabiliane na hali halisi ya sasa, kwa  kuchagua marafiki wema.

Semina hiyo ilihudhuriwa na wanafunzi kutoka shule za sekondari za Benjamini Mkapa, Kibasila, Kisutu, Azania, Jangwani, Jitegemee na Chang’ombe zilizopo jijini Dar es Salaam.

Wanaofaidi maji salama Shinyanga waongezeka

Na Charles Hililla,Shinyanga

IDADI ya watu wanaopata huduma ya maji safi na salama katika Manispaa ya Shinyanga imeongezeka kutoka asilimia 10.52 mwaka 1993 na kufikia asilimia 60.1 mwezi Juni mwaka huu.

Akielezea juu ya mpango wa maji kwa kipindi kilichopita na kilichopo kwenye Mkutano wa Wadau wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira, uliofanyika katikati ya juma katika Ukumbi wa Vijana uliopo mjini hapa, Afisa Mipango wa Manispaa hiyo Bw. Rogasian Seda, alisema kuwa, programu ya matumizi ya maji ya nyumbani (DWSP), ilianzishwa mkoani hapa mwaka 1993.

Alisema, Pogramu hiyo iliyopangwa kumalizika mwaka 1998, iliendeshwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Uholanzi haikupata kusitishwa kutokana na sababu mbalimbali.

Alizitaja sababu hizo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya maji katika jamii, wananchi wengi kuelewa uboreshaji wa vyanzo vya maji na usafi wa mazingira kuwa siyo jukumu la Serikali pekee, bali ni la jamii husika katika maeneo hayo.

Aidha, alisema mradi huo ulilenga, kuinua hali za maisha kwa wananchi wa Manispaa hiyo pamoja na afya zao kwa kuwapatia huduma za maji safi na salama ya kutosha karibu na maeneo yao.

Ili kukidhi madhumuni hayo, jumla ya visima virefu na vifupi 181 vilijengwa kwa kipindi hicho pamoja na kukarabatiwa ikiwa ni ziada ya visima 24 kulingana na lengo lililowekwa la visima 157.

Shughuli nyingine zilizofanywa na mradi huo kwa kushirikiana na wananchi ni ujenzi wa matanki yenye ujazo wa lita 30 hadi 35,000 yaliyojengwa kwenye shule za msingi na asasi mbalimbali kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wataalamu mbalimbali kutoka sekta ya maji, mazingira, afya na viongozi wa madhehebu ya dini, wanasiasa, wabunge na madiwani wa manispaa hiyo pamoja na watendaji wa kata na vijiji.

Aidha, wajumbe hao walijadili kwa pamoja mambo mbalimbali yanayoathiri utoaji wa huduma hiyo na kuweka mikakati ya kuboresha huduma hiyo kwa kushirikiana na wananchi ambao ndio walengwa wa huduma hizo.

 

Vijana watakiwa kutumia karama zao kujenga umoja

  Na Brigitha Nungu

VIJANA kote nchini wametakiwa kutumia akili na karama mbalimbali walizojaliwa na Mungu katika kujenga umoja.

Wito huo ulitolewa hivi karibuni na  Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,Mhashamu Method Kilaini wakati akizindua  Umoja wa Vijana Wakatoliki jimboni humo ,uzinduzi uliofanyika kwenye  viwanja vya Shule ya Sekondari  Forodhani.

Alisema malengo hayo yanaweza kufanikiwa kupitia vikundi mbalimbali vya  kitume kama  Focolare,Youth Alive,Bhakita,Viwawa na vikundi vingine vya namna hiyo.

“Vikundi vitumike kuunda umoja ambao huleta  jeshi la Bwana kwa kulieneza neno, kulitetea na kuliishi”alisema Mhashamu Kilaini.

Uzinduzi wa umoja huo uliambatana na maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka miitatu ya kifo cha Baba wa Taifa,hayati Mwalimu Julius  Nyerere.

Akieleza ni jinsi gani kanisa linavyo mkumbuka na kumuenzi Baba wa Taifa, Askofu Kilaini alisema.

“Licha ya madaraka aliyokuwanayo, hayakumfanya apoteze imani yake”

Kwa kutumia mfano huo,Askofu Kilaini aliwahimiza vijana kuwa imara katika imani yao.

Utume wa Bahari waweka mkakati wa kuwanusuru mabaharia,wavuvi

l Huduma ya kiroho kupelekwa melini, bandarini

l Wavuvi wakubwa ‘kubanwa mbavu’,wadogo kuneemekaNa Dalphina Rubyema

IMEBAINIKA kuwa,mabaharia  katika meli za wafanyabiashara, mbali na kupata malipo duni ,vile vile wanapata shida ya kutotambuliwa kama binadamu wanaohitaji msaada.

Hayo ni miongoni mwa mambo yaliyoongelewa katika Mkutano wa Kidunia wa Utume wa Bahari (World Congress of Apostolatus Maris) uliomalizika hivi karibuni katika eneo la Rio de Jeneiro  Brazil.

Mkutano huo uliwashirikisha Wakuu wa Utume wa Bahari kutoka  Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika sehemu mbalimbali duniani.

Mwakilishi wa Baraza la Maasofu Katoliki Tanzania (TEC) katika Mkutano huo uliofanyika kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 5 mwaka huu,Padre Marcel Philip Kaberwa aliliambia KIONGOZI kuwa katika kuhakikisha watu hao wanapata huduma inayotakiwa kwa binadamu yoyote,Utume wa Bahari kama mtetezi,utakuwa unatoa huduma za kiroho kwenye meli ama bandari ambazo meli za mabaharia hao hufikia.

“Mabaharia, meli zao zinaingia nchi mbalimbali,kila wanapoingia wanaonekana wageni hivyo kushindwa kupewa msaada wa kibinadamu”alisema Padre Kaberwa na kuongeza kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Mwakilishi huyo wa TEC,Mkutano huo pia uliangalia suala la kuweka uwiano baina ya wavuvi wakubwa  na wavuvi wadodo.

Alisema ilibainika kuwa licha ya kuwa na dhana za kisasa, wavuvi wakubwa wanaonekana kuwa watawala wa bahari ambapo huwabana mbavu wavuvi wadogo.

Katika kuwanusuru wavuvi hao wadogo,mkutano huo ulitoa pendekezo kwa kila nchi husika kutenga maeneo ya mbali kwa ajili ya wavuvi wakubwa na maeneo ya karibu waachiwe wavuvi wadogo.

“Kulingana na maelezo yaliyotolewa na washiriki mbalimbali wa Mkutano huo,inaonekana wavuvi wadogo,wamesahaurika. Kipato kingi kinaenda kwa  matajiri ambao wamewekeza katika sekta ya uvuvi ambao hutawala maneneo yote ya bahari kwa kutumia dhana za kisasa”alisema Padre Kaberwa.

Awali akifungua Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano,Rais wa Utume wa Bahari duniani,Askofu Mkuu Stephen Hamao,aliwataka washiriki kuhakikisha hawakati tamaa katika kutimiza malengo ya kuboresha maisha ya mabaharia na wavuvi.

Matembezi ya Nyerere kuzineemesha shule zenye kambi

Na Lilian Timbuka

SHULE za Msingi zinazotumika kama kambi za mapumziko kwa vijana wanaoshiriki Matembezi ya Kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere, zitanufaika na matembezi hayo kwa kupata huduma muhimu ikiwemo ya maji ya bomba, bafu na vyoo; Imefahamika.

Mratibu wa Habari wa Matembezi hayo, Bw.Nicodemus Banduka, alisema katika mazungumzo yake na KIONGOZI hivi karibuni jijini Dar es Salaam kuwa, huduma hizo zitakazotumika kwa ajili ya matembezi hayo, zitakuwa za kudumu katika shule hizo.

Bw. Banduka ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, alisema kwa kuzingatia msisitizo kutoka kwa Hayati Nyerere  juu ya kuboresha elimu na afya katika jamii, Kamati ya hiyo iliona umuhimu wa kuzipatia huduma hizo shule ambazo zitatumika kama kambi wakati wa matembezi hayo ambayo kilele chake ni Novemba 2 mwaka huu.

Alizitaja shule zilizopata bahati hiyo katika Mkoa wa Pwani kuwa ni Mdaula, Pingo, Vigwaza, Mdahura, zote zikiwa shule za msingi.

“Shule hizi zimefanikiwa kupata matanki ya kuhifadhia maji kiasi cha lita  10,000 kila moja na matenki haya yatawasaidia kuvuna maji ya mvua na kuyatumia wakati wowote,” alisema.

Katika Mkoa wa Morogoro iliyopata bahati hiyo ya kupata maji ya bomba ni Shule ya Msingi Mkundi iliyopo karibu na sehemu ambayo alifia Waziri Mkuu wa zamani, Hayati  Edward Moringe Sokoine pamoja na Shule za Msingi Lusinde na Kihegeya zilizopo mkoani Dodoma.

“Tulitilia mkazo zaidi katika kuchagua shule za msingi ili ziwe makambi yetu ya mapumziko kwa ajili ya kuweka huduma hizi muhimu ili hata tukipita, basi shule inabaki na kumbukumbu ya matembezi haya,” alisema Banduka.

Naye Dalphina Rubyema, anaripoti kuwa, wakati Watanzania wanasisitizwa kudumisha amani aliyoiacha Mwalimu Julius Nyerere, Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Shamsi Vuaui Nahodha, ameonesha wasiwasi kuwa udini, ubinafsi, ukabila na rushwa huenda vikaongezeka kwani dalili mbaya zimeanza kuonekana katika kipindi cha miaka mitatu tangu kifo cha Nyerere.

Waziri Nahodha alionesha wasiwasi huo wakati akizindua Matembezi ya kumuenzi Nyerere, aliyefariki Oktoba 14, 1999.

Alisema kuwa ili kuepuka kutafunwa na dhambi hizi, Watanzania hawana budi kuyaenzi mema yote aliyoacha Mwalimu na kuacha mambo yanayoleta mgawanyiko katika jamii.

Alisema Mwalimu katika uhai wake aliiasa jamii kutoyakumbatia mambo ya namna hii kwa sababu  yanaweza kuwa chanzo cha migogoro.

“Sishangai sana kwani Mwalimu alikwisha tabiri na wakati fulani aliwahi kusema tukifanya mchezo madhambi hayo yatatutafuna,” alisema Waziri Kiongozi huyo.

Aliwataka vijana walioshiriki matembezi hayo, kujifunza na kupigania falsafa na msimamo wa Mwalimu ili kuepuka makosa hayo.

Matembezi hayo yaliyoanzia jijini Dar es Salaam, yamewashirikisha vijana wapatao 276  kutoka mikoa mbalimbali nchini na yanatarajiwa kuisha Novemba 2 mwaka huu mkoani Dodoma ambapo yatapokewa na Rais Benjamin Mkapa katika ukumbi wa CCM,Chamwino.

Awali matembezi hayo yalitarajiwa kuwashirikisha vijana 300, lakini idadi hiyo ilipungua na kufikia 276 baada ya vijana 24 kupunguzwa kufuatia hali zao kiafya kutoridhisha.

Kwa mujibu wa Mratibu wa matembezi hayo,Bw. Nocodems Banduka,kutakuwa na vituo 19  na Oktoba 24 mwaka huu,watembeaji hao watapumzika kwa siku nzima katika eneo alilofia Waziri Mkuu wa zamani, Hayati Edward Moringe Sokoine, katika ajali ya gari.

TRC Dodoma Hotel yauzwa

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Tume ya Rais ya Kurekebisha Mfumo wa Mashirika ya Umma (PSRC), imeuza Hoteli ya TRC Dodoma, imefahamika .

Kwa mujibu wa taarifa ya PSRC kwa vyombo vya habari mwishoni mwa juma na kusainiwa na Mwenyekiti Mtendaji wa PSRC, Bw. John C. Rubambe, makubaliano ya kuuza hoteli hiyo yalifanywa Oktoba 16, mwaka huu baina ya Serikali na mnunuzi; World Wide Manegement Group Limited.

Mnunuzi waHoteli hiyo ni Kampuni iliyosajiliwa Uingereza (United Kingdom) na pia, ilisajiliwa nchini Tanzania, mwaka 1998. World Wide Manegement Group Limited inashirikiana na Estate Trading Company Limited inayomiliki Hoteli ya Beachcomber, ambayo itakuwa mwendeshaji wa Hoteli ya Dodoma.

World Wide Manegement Group Limited itatoa huduma za hoteli, kufanya ukarabati na kuinua kiwango cha ubora wa hoteli hiyo kwa kuanzisha duka, huduma za afya na vyombo vya mapumziko.