Watanzania jifunzeni toka Ivory coast -  Kardinali Pengo

l Asema vurugu za kidini huanzishwa na wanasiasa

l  'Wanasiasa wengi ni wa kukimbilia Ikulu’

l       Dar kuna washirikina wengi kuliko mikoani wanakoua vikongwe

l       Azungumzia uteuzi wake huko Vatican

Pd. Revocatus Makonge na Joseph Sabinus

 

MWADHAMA Polycarp Kardinali Pengo, amehofia hali ya usalama nchini huku akiwahimiza wanasiasa, wanasayansi ya jamii na waandishi wa habari, kuchunguza ili kubaini kama Tanzania itapona au itaangamia kwa kile kilichosababisha machafuko nchini Ivory coast.

Kardinali Pengo aliyasema hayo wakati akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake katikati ya juma juu ya hali ya siasa nchini, ushirikiano wa kidini na kuteuliwa kwake kuwa Mjumbe katika Idara ya Mafundisho ya Imani ya Kanisa katoliki Duniani, yenye makao yake makuu nchini Vatican.

Hivi karibuni waasi nchini Ivory coast walifanya jaribio la Mapinduzi  kumng'oa madarakani Rais Laurent Gbagbo, na hivyo kuzuka ghasia nchini humo.

Hadi mwishoni mwa juma, waasi walikuwa wamekataa wito wa Rais Gbagbo wa kuweka silaha chini ili kufanya mazungumzo.

Msemaji wa waasi hao alisema, Rais alitoa wito huo baada ya kuona ameshindwa kuwaondoa katika mji wa pili kwa ukubwa nchini humo Bouake.

Alisema anafurahi kuona kuwa hali imebadilika miongoni mwa wananchi wa nchi hiyo.

Wananchi wa Burkina Fasso waishio nchini humo wamekuwa wakionekana kama wavamizi na wamekuwa wakitishiwa kila kukicha.

Naye Kamanda wa waasi huko Bouake, Wo Tuo Foziem, alikaririwa akisema Rais huyo alikuwa anafanya mchezo ambao alisema hawezi kuuamini.

"Hatuwezi kuacha silaha kabla ya mazungumzo."

Katika mazungumzo hayo, Kardinali Pengo ambaye ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, alisema, “Matatizo yaliyozuka Ivory Coast yamenitia baridi na hofu sana kuhusu siasa yetu hapa Tanzania hasa siku zijazo maana Ivory Coast ilikuwa moja ya nchi zenye amani na utulivu kama Tanzania. Hukuwa unafikiria wala kuhofu juu ya amani,” alisema.

Akaongeza, “Mimi nina hofu kwamba tunaweza kuwa tunaelekea kule ambako wenzetu wa Ivory Coast wamefikia bila sisi wenyewe kujua.Ndiyo maana natoa wito kwa wanasiasa, wandishi wa habari, wataalamu wa sayansi ya jamii, na jamii kwa jumla, watafiti ili waone ni kitu gani kimetokea kule na je, sisi tuko wapi? Kinachotokea kule hakiwezi kutokea hapa kwetu?, ama sisi hatuelekei huko? Wote tulitafakari hilo tuone kama tutapona ama tutaangamia ninayo hofu kubwa.”

Akizungumzia mang’amuzi yake mintarafu uhusiano wa kidini nchini Tanzania,Kardinali Pengo,alisema hali ya Tanzania ni nzuri ikilinganishwa na nchi nyingine ambazo dini zake zina uhasama na chuki.

Alidokeza kuwa kinacholeta vurugu katika uhusiano baina ya dini nchini, ni siasa kali za kidini ambazo alisema ni hatari na hazina budi kukemewa na kila mwenye mapenzi mema.

Alisema, “Watanzania tujichunge sana tusiingie kwenye mkondo wa siasa kali kwani maafa kama tunayosikia yakitokea Nigeria, na sehemu nyingine si vitu vya kufurahisha na vinaweza kuanzishwa na sisi Wakristo au na wenzetu Waislamu endapo hatutakuwa makini.”

 Aidha, Kardinali Pengo alibainisha ukweli kuwa, mara nyingi katika sehemu mbalimbali duniani, matatizo na machafuko ya kidini, hutokana na wanasiasa wanaotumia dini kujinufaisha kisiasa.

“Baadhi ya wanasiasa wanatafuta sababu ya kupendeka kwa watu hasa wanaoonekana kuwa ni wengi kwa kutumia dini zao. Na ili waonekane kuwa wako upande wa dini hiyo, wanaanza kuzusha maneno ya uhasama dhidi ya wanasiasa wenzao walio na dini tofauti kwa kuwa wanajua wakipambana kisiasa moja kwa moja, hawawezi kuwashinda, lakini wanaona wakipitia dini, wanaweza kuwashinda,” alisema.

Akaongeza, “Wanaifanya dini kuwa mbinu tu, au chombo kinachotumiwa ili kufanikisha malengo ya kisiasa. Unajua mara nyingi wanasiasa wanatumia dini kama ngao ambayo kazi yake ni kumlinda mtu anayepigana. Akishafanikiwa, kama ngao imeharibika au haikuharibika, haina maana tena; ataitupa pembeni. Na ndivyo unavyofanyika uhasama baina ya dini mbalimbali unaojengwa na wanasiasa.”

Mwadhama Pengo alisema inasikitisha kuona kuwa, pindi wanasiasa wanapotimiza malengo yao, huzisahau na hata kuzitelekeza dini zao bila kuzifanyia chochote cha maana.

“Wataiweka huko kwenye mizimu kama ngao iliyokwishatumika na kuchanika na itakaa huko mpaka watakapoihitaji tena ndipo wataiokota, lakini sio kitu cha kubeba ngao kila wakati, mpaka mtu anapojua kuna mashambulizi na anahitaji kujikinga,” alisema.

Alisema inatia moyo kwa viongozi wa dini nchini Tanzania, kukataa kwa kauli moja, kutumiwa kama ngao ya wanasiasa na akasema hiyo ni bahati kubwa kwa Watanzania.

Kuhusu vikundi vyenye itikadi kali vinavyotumiwa kama ngao ya wanasiasa,

Kardinali Pengo, alisema kama ingetokea bahati mbaya vikapata nguvu ya kujihesabu kuwa dini, hali ya amani  ingekuwa mbaya nchini.

“Kwa mfano  tuseme Wakatoliki tungekuwa na msimamo huo wa itikadi kali, halafu mmoja aje kwa upande wetu, hiyo ingekuwa ni mbaya kuliko hali inayokuwapo kwa sasa. Na hata kwa Waislamu, kuna vikundi hivi vya siasa kali, lakini si dini ya Kiislamu; viongozi wa Kiislamu wanahakikisha kwamba hao si wenzao na hali hii imesaidia sana amani,” alibainisha.

Alisema anashangazwa na mtindo wa wanasiasa wa Tanzania kuwa wanaokimbilia ikulu, badala ya kutoa changamoto kwa chama tawala ili kijikosoe na kuboresha maendeleo ya kijamii.

“Ndiyo maana utaona tunapoelekea Uchaguzi wa Rais na Wabunge, ndipo vikundi vya siasa kali vinapoibuka. Hii ni kwa sababu wanasiasa wetu kwa sasa hawaoni sababu ya kugombana; siasa yao ni kutaka kuingia ikulu.”

Akitoa mfano wa kuthibitisha namna wanasiasa wengi wa tanzania walivyo, Kardinali Pengo alisema, “Katika kipindi hiki chote tutakuwa kimya, tutakapokaribia uchaguzi, ndipo utaanza kuwasikia hata wakielezea sera zao huku zikiendana na matusi kati ya vyama na vyama ndipo wanaanza kutumia chokochoko za kidini. hali hii si ya kungoja wakati wa kwenda ikulu ndipo waanze kueleza sera zao, haipendezi.”

Kuhusu mapambano na migogoro ndani ya vyama vya siasa, alisema, “Badala ya kutumia muda huu kujenga na kuimarisha vyama vyao, wanaanza kusambaratishana. Wanaona ni wakati wa kucheza ndani kwa ndani, uchaguzi ukifika, tunajifanya kuwa ni chama kimoja. Sasa tutaamini vipi kuwa nyie ni chama kimoja wakati juzi mlikuwa mnagombana mmepatana lini, au mmehongana kitu gani ili tusadiki kuwa sasa mko pamoja.”

Alipoulizwa mtazamo wake juu ya uinjilishaji kwa watu wenye imani za jadi, Kardinali Pengo alitoa wito kwa wataalamu katika asasi mbalimbali za kanisa zikiwamo seminari na vyuo vikuu vya Kanisa, vifanye uchunguzi wa kina ili kubaini tunu zinazowavuta waamini mbalimbali wakiwamo wakristu na waislamu, kushiriki katika dini hizo kwa kificho.

"Watalaamu, walimu na wanafunzi wakiweza kujifunza na kueleza tunu ambazo watu wanazifuata kwa siri, wakaeleza zinavyokaa, hapo tunaweza kujua na kusahihisha" Alisema .

Alisema moja ya mapungufu yaliyopo katika dini za jadi nchini, tofauti na hali ilivyo huko Afrika Magharibi, hapa Kanisa ni kama hakuna linachojifunza na kupata kutoka dini za jadi maana zinafanyika kwa siri siri tu.

“Dini za jadi kule zina mpangilio mzuri kuliko huku kwetu… huko unajua umuendee nani ili ufanye uinjilishaji au kubadilishana naye mawazo. Lakini, hapa kwetu hujui uende kwa nani; tumeshikilia kuwa dini ni Ukristo, Uislam na labda na Wahindu,” alisema.

Alibainisha kuwa ingawa wengi wa Watanzania wako katika imani za kijidi, bado wanaonekana kama imani zao wanazionea haya na pengine kujiona kama watu walioko safarini; kuelekea kuchagua Uislamu ama Ukristo.

“Hivyo, ukimuita mmoja ni mpagani au muumini wa dini za jadi, atajisikia kama umemdharau au umemdhalilisha kinyume na ilivyo kule Afrika Magharibi. Wao wanavikundi kabisa vya dini za jadi na wana viongozi wao wasomi,” alisema.

Alisema asasi za kanisa zikibaini tunu zinazowavuta baadhi ya waamini wetu katika dini za jadi, Kanisa litajiimarisha na kuziona kama zinafaa kupokelewa, na kama zinamchango wa kumfanya Kristu aeleweke zaidi.

“Tunaenda kwa wachawi, tunapiga bao ambalo kwa Waislamu hulipati na kwa Wakristo halipo, lakini lipo kwa dini za jadi, lakini kwa sababu tunaenda kule na ni kitu hakiko katika mpangilio, tunaenda kule kwa kujifichaficha watu wasione na vitu vinavyofanywa kwa siri ni hatari kwa sababu tunaweza kusema tunachukua vinavyofaa kwa utamadunisho kumbe tunachukua ngoma tunaanza kupiga kanisani kumbe ni ngoma iliyokuwa inapigwa katika uchawi nasi tukaanza kuitumia katika Pasaka.

Alisema inashangaza kuwa ingawa Dar es Salaam, kuna watu wengi wasomi, na walio katika dini zinazojulikana, lakini bado kuna washirikina wakubwa zaidi kuliko hata sehemu nyingine za mikoani wanakofanya mauaji ya vikongwe kwa imani za uchawi.

Kardinali Pengo ni miongoni mwa Makardinali na Maaskofu saba ambao hivi karibuni Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, aliwateua kuwa wajumbe katika Idara ya Mafundisho ya Imani ya Kanisa Katoliki yenye makao makuu yake nchini Vatican.

Alisema uteuzi huo, unafuatia utaratibu wa kawaida ambapo zinapotokea nafasi zozote kuachwa wazi katika idara mbalimbali, baba Mtakatifu huchagua makardinali, maaskofu wakuu  au Maaskofu kujaza nafasi zilizo wazi kwa kipindi fulani.

"Makardinali hatupigi kampeni hivyo, hata nafasi kama hiyo ni uteuzi tu, anaoufanya baba Mtakatifu kwa sababu zake mwenyewe". Alisema.

Alisema miongoni mwa sababu zinazoweza kuifanya idara ikawa na nafasi ya wazi, ni kung’atuka kwa ajili ya umri, ama kufariki dunia..

“Kwa mujibu wa Kanisa, Kardinali akifikisha umri wa miaka 80, anakuwa amestaafu shughuli zote hata kama ni ushauri.

Baada ya miaka 80 hata kukiwa na uchaguzi wa baba Mtakatifu, haruhusiwi kuingia katika chumba cha kura.

Alikanusha hisia za baadhi ya watu kuwa huenda yeye ndiye kiongozi mkuu wa idara hiyo kwani kiongozi yupo na yeye ni mmoja wa wajumbe hao saba, wanaokwenda kuongezea nafasi zilizokuwa wazi.

Aidha, alisema ingawa nafasi hiyo itamfanya mara nyingine asiwepo jimboni kwake, bado uteuzi huo ni heshima kubwa kwa Kanisa la Tanzania kwani ufanisi wa Utume wake unatokana kwa kiasi kikubwa, na ushirikiano uliopo ndani ya Kanisa zima la Tanzania.

Aidha alisema, nafasi hiyo inampa nafasi ya kujifunza mazuri na kurekebisha mabaya kutokana na uzoefu wa nchi zingine.

Waislamu sasa kumpata Mufti

Na Dalphina Rubyema

WAISLAMU nchini kote wapo katika kitendawili kinachopata jibu Jumapili hii mkoani Dodoma katika Uchaguzi wa atakayerithi kiti cha Marehemu Sheikh Mkuu Mufti Bin Jumaa Bin Hemed, aliyefariki dunia hivi karibuni.

Mufti Hamed Bin Jumaa Bin Hemed, alifariki dunia Aprili 8, mwaka huu katika Hopitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa  baada ya kuugua muda mfupi.

Taarifa kutoka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), zinasema kuwa Uchaguzi huo utakaosimamiwa na  Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi huo, Sheikh Salim Gereza, utawashirikishika Masheikh wote wa Tanzania.

Taarifa hizo zilizothibitishwa na Kiongozi wa Masuala ya Dini wa BAKWATA, Sheikh Hassan Chizenda, zinasema kuwa hadi sasa (tunapokwenda mitamboni), idadi ya wagombea wa nafasi hiyo ya Sheikh Mkuu wa Tanzania ni 11.

Aliwataja wagombea hao na Mikoa wanakotoka ikiwa katika mabano kuwa ni Sheikh Suleiman Amran Kilemile, Sheikh Hemed Masoud Jongo, Sheikh Twarib Ahmad Abdalah, Sheikh Abubakar Zuberi  na Sheikh Twaha Omar Majaliwa (wote wa Dar es Salaam).

Wengine ni Sheikh Suleiman Gorogosi (Lindi), Seikh Profesa Jumaa Mikidadi (Kilwa), Sheikh Taufiq Ibrahim Malilo (Kigoma), Sheikh Mohamed Ally Mkanga (Tanga), Sheikh Ahmad Zuber (Dodoma) na Sheikh  Issa Shaban Simba (Shinyanga).

Sheikh Chizenga alisema kuwa Masheikh mbalimbali tayari wamekwisha wasili mkoani Dodoma ambapo wamefikia eneo la Chuo cha Biashara (CBE).

“Uchaguzi huu utawahusisha Masheikh wote wa Tanzania na tayari baadhi yao wameisha wasili Dodoma tayari kushiriki uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili,” alisema Sheikh Chizenga.

Gazeti hili pia lilishuhudia Masheikh kutoka sehemu mbalimbali wakiingia na kutoka katika ofisi za BAKWATA kuangalia taratibu za safari.

Mmoja wa wagombea wa nafasi hiyo, Sheikh Twaha Omar Majaliwa (Dar es Salaam), aliliambia KIONGOZI kuwa anawataka wagombea wenzake watambue kuwa kugombea huku isiwe ni kujenga husuda na chuki miongoni mwa Waislamu na badala yake, uchaguzi ukisha waendelee kuonana kama watu wa jamii moja.

Pia, alisema matokeo ya uchaguzi huo yawe ni mwanzo wa mabadiliko ndani ya Uislamu ambapo alisema kwa sasa duniani Waisalamu wamefarakana jambo linalomfanya hata Mwenyezi Mungu akatae kupokea dua zao mbalimbali.

“Baada ya uchaguzi,yule atakayeshinda na watakaoshindwa, wote turudi katika hali zetu za awali, lengo ni kuuendeleza Uislamu ambao kwa kweli tusipokuwa makini, unaonekana kuporomoka,”alisema.

Alisema, tangu awali lengo lake la kusoma ni kwa ajili ya kuwa Mufti Sheikh Mkuu wa Tanzania na si vinginevyo.

Marehemu Mufti, Hemed Bin Jumaa Bin Hemed alifariki akiwa na miaka 74. Alizikwa Aprili 8, 2002 mkoani Tanga.

Baada ya kufariki kwa Mufti, Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) lilitangaza nafasi ya mtu wa kushika nafasi.

Mgombea mmoja wa nafasi hiyo, Sheikh Mohamed Basafar (Dar es Salaam), kujitoa katika kinyang’anyiro hicho na hivyo, kubaki wagombea 11.

 

Wakatoliki na namba 666 katika Ufunuo wa Yohana

Na Mwandishi Wetu

Katika Ulimwengu wa kidini kuna mafundisho mengi kuhusu ‘namba ndani ya Biblia’kwa mfano yapo baadhi ya madhehebu ya dini yanayohusisha namba 666 inayotajwa katika kitabu cha Ufunuo cha Yohana na mamlaka ya Kipapa. Katika Makala hii, MWANDISHI WETU anaelezea maana ya namba katika mafundisho ya Kanisa Katoliki ikiwa ni sehemu ya pili ya mfululizo wa makala yake juu ya namba ndani ya Biblia.

Kadiri ya Wayahudi (Waebrania) na mataifa mengine ya nyakati hizo, kila neno liliweza kugeuzwa kuwa namba na kila namba iliweza kubadilishwa kuwa neno! Mfano mzuri ni ile namba iletayo malumbano mengi, siku hizi, namba 666 inayotajwa katika kitabu cha Ufunuo wa Yohane.

 

Je namba hii 666 inawakilisha maneno gani?

 

1. Historia fupi ya namba hii 666 :

 

-          Yohane aliandika barua au maandishi haya wakati wa utawala wa mfalem, Domitiani wa Roma. Alikumbuka ule udhalimu na madhulumu dhidi ya Wakristo yaliyofanywa na NERO kama Kaisari (NERON CEASER), mwaka 54-68 baada ya kristu.

-          Yohane alimfikiria Nero kuwa dhalimu na fashisti mkubwa kuliko wote wa Ukristu na Kanisa mwanzo mwaka 64B.K Tazama Uf. 13:18

-          Hivyo basi, Yohane alitamani sana kuweka kifupisho cha jina la Kaisari Nero katika lugha ya Kiyunani (Kigiriki) kuwakilisha yule hayawani anayetajwa katika kitabu chake (Ufunuo) kama ifuatavyo:-

 

2.        Kifupi cha Neron Caeser kwa Kigiriki ni Konsonanti hizi:

 

NRWN/OSR

Namba zinazowakilisha konsonati hizo:

N-       50

R-       200

W-      6

N-       50

Q-       100

S-       60

R-       +200

Jumla yake – 666

 

Hivyo konsonati hizi NRWN/QRS zinazowakilisha  jina la Kirumi la Kaisari Nero zina muhtasari wake kama 666 (Mia sita na sitini na sita).

 

3.        Je namba hii inaweza ikawa na maana gain nje ya Biblia?

 

Katika fani ya hisabati namba hii 666 ni jumla ya namba zote nzima (Whole numbers) kuanzia 1 hadi 36 yaani 1+2+3+4+5+6…+36 = 666

Jaribu kufanya na kuhakikisha ukweli huu.

 

4.        Mifano mingine ya Kibilia:

 

a)            Katika Injili ya Matayo 1:1-7 ukoo wa Yesu unaonyeshwa katika makundi matatu yenye vizazi 14. kila kundi limepewa tafsiri ya namba ya jina la Mfalme Daudi! Kwa Kiebrania jina daudi linawkailishwa na herufi au konsonati hizi tatu DWD.

Yaani:

D- 4

W-6

D-+4

Jumla = 14

 

i.         Namba hii 14, ni mara mbili ya ile namba kamilifu yaani 7. hivyo 14 = 2X7.

ii.        Makundi hayo matatu ni herufi tatu DWD za jina la Daudi!

B.       Mfano wa Pili : kwa Kiebrania neno mimba linawakilishwa na konsonanti hizi : HRYWN

Hii inawakilisha nini kibiblia ?

 

H – 2

R – 200

Y- 10

W- 6

N- + 50

Jumla 268

 

Maana yake : Mimba ya kawaida hukaa kwa muda wa siku 268. yaani miezi 9 = (268)

 

C.       Mfano wa tatu : kwa Waisraeli (Waebrania) waliamini kabisa kuwa ‘kisirani chema’ (good omen) kwa mtu kilikuwa ni kubadili divai iwe maji !!!. hii ni ajabu kabisa kwa nini ? je Konsonati za maji ni zipi ? Na je zinawakilisha nini ? ama kweli Wayahudi walikuwa na divai nyingi kuliko maji.

 

Jangwa lilikuwa kubwa.

 

Hapa kwetu Tanzania  huenda tungalitamani kubadili mito  yote inayotiririka kutoka milimani  iwe divai !!

Kwa Waisraeli maji yaliwakilishwa na konsonati hizi

M- 40

Y- 10

M- +40

Jumla – 90

 

Hivyo, kumtakia mtu uwezo wa kubadili Divai iwe maji ni kumtakia maisha marefu hadi miaka 90. kama Walatini wasemavyo (Ad Multons Annos).

Tafsiri, kauli inayojenga na kubomoa unyumba

l Maneno yanaweza kuficha  au kufichua kilichofichwa

Joseph Sabinus

MTAALAM mmoja wa mambo ya Kisaikolojia, aliwahi kusema kuwa ulimi ni nyama nzuri kuliko zote, na ndiyo nyama mbaya kuliko zote duniani, lakini mwingine akasema unaweza kuwadanganya watu fulani kwa muda wote, lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote.

Kwa asili, Fema alikuwa ni mtu wa mambo ya kisaikolojia, yeye mwenyewe hakulijua hilo na hivyo, kila alipoitumia elimu hiyo ambayo hakuipata darasani, alipofanikiwa alitamba na kujiita mtoto wa mjini.

Ni kwa mtindo huo, alikuwa maarufu kwa kutumia ulimi (maneno) wake kupata huduma mbalimbali zilizokuwa ngumu kupatikana kwa watu wengine.

Wakati ikijulikana kuwa huwezi kupata tiketi ya treni bila kutoa kitu kidogo, kwa wauzaji yeye alikuwa na mbinu aliyotumia kuwadanganya na kuvuna kwa ndugu zake kile asichopanda kwao.

Kila mgeni walipotaka tiketi ya treni kwenda Bara ni yeye aliyepewa shilingi 20,000/= kwa ajili ya tiketi badala ya shilingi 12,900/=.

Siku moja, uchunguzi ukafanywa kwa abiria wengine. Kila aliyefika dirishani aliambiwa tiketi zimekwisha kwa wakati huo, nao wengine walitoka wakisema, “Huo ni ulanguzi tu, watu wawili tu, zimekwisha, hiyo ni rushwa tu.” “Tanzania rushwa haitaisha.” Hiyo ndiyo ilikuwa kauli ya wengi na mara nyingi ilihitimishwa na ugomvi.

Lakini kilichoshangaza Uchunguzi huu, ni kwamba Fema alipofika licha ya wengi kukosa tikiti, yeye alipata mbili tena kwa ulaini tu.

Mwandishi wa makala akajenga urafiki wa kujikomba mradi tu, ajue mbinu anazotumia. Fema akaona si vema agawe bure hazina yake ya uelewa. Akagoma.

Ikabidi mbinu nyingine itumike. Mwandishi siku nyingine akampa ndugu wa Bw. Fema kinasa sauti chake (tape recorder) ambayo hakujua kilichofanyika. Alimwambia, “Naomba unishikie kidogo”. Kisha yule bwana akabaki kwenye benchi akimtazama.

Tape recorder ilikuwa imewashwa na inarekodi.

Baada ya kurudi, akaeleza wageni pale nyumbani kuwa badala ya kulipa shilling 12,9000 amelipa shillingi 20,000 baada ya kudaiwa kitu kidogo.

Lakini, tuliposikiliza kaseti tulibaini maneno na kauli alizotumia, alisikika akisema dirishani, “Poleni sana inaonekana anti leo mmebanwa sana; na watu ni wengi. Hiviina mana shirika halioni umuhimu wa kuwaongeza wasaidizi; huu sio ubinadamu kabisa.”

Yule dada pale dirishani akasema, “Tunashangaa na sisi tunalia tu.” Kisha bwana akasema, “Yaani kwa hali kama hii, hata kusema kitu ni sawa na kuzidi kukuonea tu na kukuchanganya,” yule dada akavutwa na maneno ya kaka yule, akaona kuwa ni afadhali yake yeye anatambua shida zao na kama angeweza, angewasaidia.

Hivyo, nae akataka kuonesha ukarimu na kulipa fadhila akasema; “Kwani kuna mtu ulikuwa unamhitaji au una shida gani?” “Hapana anti, nisikuchoshe bure nami nilikuwa natafuta tikiti, lakini kwa hali ilivyo, nitakuwa ninakuonea endapo nitakuomba msaada kama huo.”

“Usijali tu, hebu leta hiyo pesa nijaribu kukutafutia tuone kama tutafanikiwa… una bahati.”

Hivyo ndivyo Fema alivyopata dawa ya kisaikolojia ingawa naye siri yake iligunduliwa.

Kwa mtindo huo, pia wanawake wawili wenye ndoa wanaweza kuwa na tatizo la aina moja kwa wakati mmoja, lakini kwa wengine tatizo hilo likajenga na kuimarisha ndoa huku kwa upande mwingine likibomoa.

Jesca na Janeth, labda ni marafiki wakubwa pia waume zao Jacob na James ni marafiki wasioachana.

Marafiki hawa kwa kawaida hutembea na kurudi usiku wa manane huku wanawake na watoto wamelala fofofo.

Hebu tujiulize kuwa inakuwaje wakati mwanaume anaporudi nyumbani akiwa amechelewa usiku? Ni dhahiri kuna kuwa na maswali mengi.

Jesca yeye humuuliza mmewe, “Hivi unapochelewa kurudi nyumbani namna hii unakuwa na maana gani? Au basi unaona ugumu gani, si ungenipigia simu sasa wewe unauchuna tu, unategemea mimi nitakueleweje?”

Kwa mtindo huo maswali hayo yanasikika vingine masikioni mwa mumewe, Jacob, yeye anayasikia, anayapokea na kuyatafsiri kuwa ameambiwa hivi. “Ulipitia sehemu unazojua mwenyewe na hukuwa na sababu yoyote ya maana kukufanya uchelewe; kazi gani hadi usiku. Wewe sema ukweli tu, na hata hivyo sikuamini kabisa.”

Sasa, kama kweli mwanaume ni mwaminifu na amechelewa kwa sababu za uaminifu mbele za Mungu, mbele  yake mwenyewe na mbele ya familia yake, lazima atasema maneno kama haya; “Mihangaiko mingi; ni muhimu kutafuta dili hapa mjini tutaishije.” “Foleni leo ilikuwa kubwa.”

Pia, mwanaume anaweza kusema, “Yaani kuchelewa leo tu, ndiyo inakuwa nongwa namna hiyo?! Aaah!”

Hapo, kibao tena kinageuka majibu ya mwanaume nayo yanapokewa kwa namna, hisia na tafsiri tofauti.Mwanamke anajisikia kama vile labda ameambiwa hivi,  “Huna sababu ya kuchukia kwa hilo, nadhani unajua kuwa kazi ni muhimu kuliko wewe. Halafu tatizo lako unataka tukae nyumbani muda wote tukitazamana.” Ndiyo mwanamke anavyofikiri sasa.

Wote wako sahihi kwani kila mmoja anajaribu kuonesha namna anavyomjali mwenzake isipokuwa ndimi (lugha) zinazotumika ndizo zinachochea sumu katika uelewano wa wanandoa hao.Hali ya kuhisi na kutafsiri kwamba unaambiwa mambo mengine tofauti na ulivyotarajia ndiyo husababisha migogoro hata kusambaratika kwa ndoa baina ya watu kama Jacob na Jesca.

Bahati ni kwamba kila mgogoro huo ulipotokea Janeth aliufahamu. Akamfuata na kumsaili polepole ili ajue namna  shoga yake alivyoanza kumuuliza mumewe.Jesca akawa anayaweka yote hadharani kwa Janeth.

Akamwambia, ”Shoga yangu, ngoja leo nikueleze namna ya kumuuliza au kumuonya mmeo juu ya tabia kama hiyo. Si unaona mume wangu mie siku hizi ameiacha. Unajua mume hapendi umkaripie wala kumkosoa wazi wazi. Wao ukiwafanyia hivyo, wanajiona kama kwamba umemgeuza kuwa mtoto mdogo. Au eti umechukua madaraka ya nyumba na sasa unamtawala.

Ni haki yako kufanya hivyo, lakini lazima umsome vizuri na kumjua mwenzio ili ujue uwezo wake wa kupokea, kubeba, kutafsiri na kutekeleza mambo.”

Akaendelea, “Kama mume akikukosea kwa lolote, njia bora ya kumrudi ni ile ya kutambua hadhi yako ya kuwa MKE WAKE. Yaani, uoneshe, upendo, heshima, upole, unyenyekevu na pia, uwe mtu wa subira.

Mumeo asichelewe kurudi nyumbani ukamfungulia mlango huku ukimshambulia kwa maneno hata hamjasalimiana, hajakaa na wala hajala.

Ukimjua vizuri mmeo, ukamfanyia mambo kwa ufundi wa namna ya kuishi na mume, akizidi kuwa mbogo, basi ujue lazima atakuwa na matatizo ya akili.

Siwatetei, lakini mwanaume akioneshwa upendo wa dhahiri, na wenye sura ya mashindano, na kwa kuwa ni kawaida wanaume huwa hawapendi kuonekana wameshindwa mbele ya wanawake, atajitahidi na yeye akufanyie mazuri ili akushinde kwa upendo.

Na hii wanaifanya kwa vile mara nyingi wanaume hawataki watazamwe na jamii kuwa ndio chanzo cha kulegalega katika familia.

Hiyo ndiyo siri ya wanaume wengi, mkifanya mashindano ya upendo katika ndoa, anataka akushinde, mkitaka mashindano ya ushetani, anataka akushinde, mkifanya mashindano ya darasani, wanaona vibaya kushindwa na mwanamke.

Kwa kawaida, wanaume wanaoridhika na kufurahia kushindwa na wanawake katika nyanja hizo, hata kiuchumi, ni dhahiri huwa wana dosari katika ubongo.

Janeth akafichua, “Unajua mimi kinachofanya hatugombani na mume wangu hata kama atachelewana badala yake tunazidi kupendana?  “…Ni kwamba akichelewa kurudi, kwanza nampa pole, namuuliza kama angependa kunywa chai, kula au aanze kwanza kuoga. Anachagua alitakalo huku akivua viatu na kuendelea kuitazama television kwa kuibia na kwa hali ya kuchoka.

Akishafanya hayo sasa ametulia, ndipo ninapomwambuia, “Mume wangu, baba …naomba ikitokea unachelewa, unijulishe. Unajua ukifika muda huu haujafika na sijui ulipo, ninakuwa na wasiwasi sana juu yako. Ukifanya hivi baba… utakuwa umenisaidia sana.

Sasa, hebu tujadili kinachotokea wakati mwanamke akitamani kitu na kumbe mumewe akakisahau; hali inakuwaje. Kwa kawaida hapa huwa kuna namna fulani ya zogo au mgomo baridi kwa mwanamke dhidi ya mwanamme.

Tabia hubadilika japo siyo sana na kwa wazi zaidi. Hakika hali hii huwa ni kovu dogo, lakini lenye sumu kali katika maisha ya ndoa.

Mara nyingi mwanaume anaposahau kitu kilichotegemewa na mwanamke, mwanamke huweza kutoa kauli kama hizi, “Kweli hicho tu, ndicho unachosahau vingine hausahau; unavikumbuka hata bila kuambiwa. Unafanya hata nishindwe kukuamini maana naona…”

Ugonjwa unakuja kwamba kwa mwanaume, kauli kama hiyo inapenya na kusikika vingine masikioni, inaweza kuwa inasikika na kutafsirika vibaya  kama hivi, “Huna sababu ya kusahau kitu kama hicho, labda una matatizo ya akili na wewe sio mtu wa kuaminika kabisa.”

Pia, kauli kama hiyo ya mwanamke japo hakupanga isikike wala kueleweka hivyo, lakini inaweza kusikika masikioni mwa mwanaume kama hivi, “Inaonenkana kama mimi (mwanamke) ndiye ninajikomba kwako (mwanaume) na pengine inaonekana mimi ndiye ninayetoa zaidi kwenye uhusiano wetu kuliko wewe mwanaume.”

Sasa, mwanaume naye anaposikia maneno hayo huku yakiingia masikioni kwake na kutafsiriwa kwa namna hiyo hapo juu, hujaribu kujibu mapigo kwa staili anayoijua yeye.

Mara nyingi wengi wanaweza kujibu hivi, “Lakini mbona hilo ni jambo dogo kuliko unavyolichukulia? Siyo kwamba sikujali hapana, ni kusahau tu, ni kitu ambacho ni cha kawaida maana nilikuwa nimetingwa sana na majukumu.”

Kwa mwanamke nayo haya yanatafsiriwa vingine, yeye anajisikia kana kwamba ameambiwa vibaya zaidi, anakuwa mbogo na kusema, “Utasikitishwaje na mtu mdogo kama mimi, si ndiyo maana unaona ni kitu kidogo na cha kawaida.”

Sasa, matokeo ya tafsiri za namna hii, zinazotokana na usikivu, uchambuzi na uamuzi wa maana ipi itumike kwa manufaa yako na mwenzio kuwa tofauti na ilivyotolewa, huwa ni songombingo katika ndoa.

Lakini, kama mtu anajua kutoa kauli nzuri hata kwa jambo baya, hivi ni vitu vidogo sana  kwa mwanandoa mwenzio na kwa mshirika wako wa namna yoyote, kazini, shuleni na katika maeneo ya makazi ikiwa  pamoja na katika biashara.

Janeth yeye alisema  kuwa yanapomtokea mazingira ya mumewe kusahau kile ambacho yeye Janeth alitarajia kupata toka kwa mumewe, au amesahau kufanya jambo fulani, humwambia, “Mume wangu siku ukininunulia kitu fulani nitafurahi,” “Mwenzangu ninatamani uninulie kitu hiki, nikipata nitashukuru kweli, lakini usihangaike kama kwa sasa huwezi ila, ukipata nafasi siku yoyote.”

Janeth anaonya kuwa, “Kamwe usimwambie mumeo kuwa amesahau, wewe jifanye kuwa hujui kwamba kasahau. Hii ni kwa sababu ukimwambia hivyo mumeo wakati anajua ulishamwambia, au alishapanga hivyo, atajua kuwa amesahau na atajitahidi mara nyingine akumbuke.”

Lakini, ili kujenga ushindani wa upendo na mvuto wa wanandoa kwa hali iliyo sawa, ni wajibu mwanaume anapobaini ukweli juu ya kusahau kwake, basi ajue namna ya kumwambia mkewe ili ajenge nguzo thabiti ya upendo na imani.

Anaweza kusema hivi, “Kwa kweli mke wangu au mama fulani, hicho kitu nilikuwa ninakikumbuka sana, lakini sijui nimeghafirika vipi nikasahau, naomba unisamehe bwana ni bahati mbaya. Nadhani umechukia sana, usichukie bwana ni bahati mbaya nisamehe.”

Akishasema maneno kwa namna hiyo, mwanamke atajisikia vizuri na huru. vibaya.

Sasa, wakati huu pia, mwanaume hana budi asiseme kitu. Akitulia tu, mwanamke akimaliza atajisikia vizuri kwa kuwa amesikilizwa maana miongoni mwa vitu anavyovipenda mwanamke katika ndoa, ni haki ya kusikilizwa.

Ni vema kuzingatia kuwa ndoa ni kitu muhimu kisichohitaji mchezo, mzaha, majaribio wala kutiana vishawishini.

Dawa yake kubwa ni kila mmoja kujitoa kuwa zawadi kwa mwenzake kwa kila jambo,  kiroho na kimwili.

Ni muhimu wanandoa wakajuana kwa ukaribu na uwazi zaidi kuwa kila mmoja anapenda na kuchukia nini, na kwa wakati gani.

Wanandoa wasipozingatia hayo, na kuimarisha upendo wa kweli, uvumilivu na kusameheana, wote wanaweza kujikuta katika hatari ya kuwa mazao sumu, badala ya kuwa mazao yanayoza matunda ya upendo na matumaini.

Kila mmoja ajue kuwa kosa moja linaweza kuwa na hasara kubwa kwa mwenzio kutokana na kauli zilizotumika na namna zilivyotafsiriwa.

Msomi wa KKKT ataka vijana matajiri wasipotoshe maskini

Na Brown Sunza

MSOMI mmoja  wa Chuo  Kikuu  cha  Huduma  ya Kiroho kilichopo Makumira , Arusha , Heko  Pori, amesema vijana  wenye uwezo  wa kifedha waache kuwadanganya na kuwapotosha vijana wa familia duni kiuchumi kwa sababu hali hiyo inaziongezea matatizo familia masikini.

Aliyasema hayo hivi karibuni  wakati akizungumza na KIONGOZI katika Kanisa  la Kiinjili  la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara katika Dayosisi ya Mashariki ya  Pwani, Jijini  Dar es Salaam.

“Baadhi ya vijana wanaotoka  katika mazingira  magumu  kimaisha  wamekuwa  wepesi wa kudanganywa  na vijana  wenye uwezo wa kifedha na kujikuta wanajihusisha na vitendo viovu na vyenye madhara makubwa katika jamii kiroho na kimwili,” alisema.

Alisema tamaa ya fedha ni miongoni mwa  vitu sugu vinavyowaingiza vijana katika ushawishi wa kushiriki vitendo vya uhalifu vikiwamo vya wizi, utumiaji wa dawa za kulevya na ufuska na hivyo, kusababisha  kupungua kwa nguvu kazi ya taifa.

Alibainisha kuwa, matokeo  ya kujihusisha  na udanganyifu miongoni  mwa  jamii ni kuwa tegemezi,  nakurudi  nyuma  kimaendeleo ikiwa ni pamoja na  kuambukizana magonjwa mbalimbali ya zinaa yakiwamo ya kisonono, kaswende na UKIMWI.

“Baadhi ya vijana hujihusisha na ngono kama starehe na hii inawafanya wasichana wapate mimba zisizotarajiwa na katika umri mdogo,” alisema.

Aidha, alisema kuwa kutokana na udanganyifu huo, baadhi ya vijana wamekuwa wakihatarisha afya zao kiakili kwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya zikiwemo bangi.

Bw. Pori alisema,  jamii inayoamini mila potofu za kishirikina, haina budi kuombewa ili epukane na madhara ya kushiriki uhalifu ukiwamo ulevi ambao huugeuza na kuona kama wanarogwa.

Watendaji wa kata Serengeti waelimishwa kuhusu UKIMWI

Na Christopher Gamaina, Serengeti

WATU 26 wakiwamo watendaji 18 wa kata zote katika Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, wamepata mafunzo ya siku 10 ya upembuzi shirikishi ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni, Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI wilayani hapa, Bw. Jackson Thoya, alisema kuwa mafunzo hayo yaliyowashirikisha pia wajumbe wanane kutoka asasi mbalimbali wilayani hapa, yaliandaliwa na Shirika la Tafiti za Dawa Afrika (AMREF) na kufanyika katika Kijiji cha Isenye wilayani hapa.

Alisema kuwa, mafunzo hayo yametolewa kwa watendaji hao ili baadaye nao waweze kufundisha watendaji wa vijiji ambao nao watatakiwa kufundisha wananchi vijijini juu ya kuanzisha miradi ya maendeleo yenye lengo la kukabiliana na maambukizi ya UKIMWI  na magonjwa ya zinaa.

Alifafanua kuwa hivi sasa magonjwa hayo yanaongezeka kwa kasi kubwa wilayani hapa kutokana na kuwa bado wananchi wana uelewa mdogo na wengine wanakuwa wagumu kubadili tabia.

Alisema, pamoja na mambo mengine, watendaji hao watafundishwa namna ya kuweza kutambua hali halisi iliyo katika jamii, kuamini kuwapo kwa UKIMWI na kufahamishwa vyanzo, madhara na kinga thabiti ya ugonjwa huo.

Mratibu huyo alisema kuwa, hatua ya kuishirikisha jamii yenyewe kwa kuifahamisha mbinu mbalimbali za kukabiliana na janga la UKIMWI, itasaidia kuwashawishi watu kuepukana na vitendo vinavyoweza kuchangia kusambaa kwa UKIMWI katika jamii.

Thoya aliongeza kuwa, baada ya mafunzo hayo, watendaji hao watapatiwa mafunzo mengine kuhusu UKIMWI yatakayowawezesha kufahamu jinsi virusi vya UKIMWI vilivyo na jinsi wanavyotakiwa kutoa elimu hiyo kwa wananchi wote vijijini.

Ametoa wito kwa jamii kutosita kutumia watendaji hao katika kujua hali halisi kuhusu UKIMWI.

CWT  Mara yataka  walimu wasiadhibiwe nje ya Katiba

Na Christopher Gamaina, Tarime

CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Mara, kimewataka viongozi wake kutumia sheria na Katiba yake kuwaadhibu walimu wanapopatikana na makosa badala ya kuadhibiwa kiholela.

Wito huo ulitolewa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa CWT mkoani Mara, Shadrack Tembe, alipokuwa akifunga semina ya siku tano juu ya uongozi bora ndani ya C.W.T.

Semina hiyo iliwashirikisha walimu 35 kutoka shule mbalimbali za msingi mkoani Mara na kufanyika katika ukumbi wa CMG Motel mjini hapa.

Tembe alisema kuwa, baadhi ya viongozi wa Chama hicho wamejenga tabia ya kuwachukulia hatua za haraka walimu ikiwa ni pamoja na kuwafukuza kazi kabla ya kufanya uchunguzi wa kina juu ya tuhuma zinazowakabili.

Aliongeza kuwa, hali hiyo inakwenda kinyume na Katiba ya C.W.T.

Naye Mratibu wa semina hiyo kutoka makao makuu, Nalonga Shani, aliwataka walimu hao kuzingatia waliyojifunza katika semina hiyo ili kuboresha utendaji kazi kwa kuelewa mipaka ya uongozi na hivyo, kuepuka migogoro ndani ya CWT.

Aidha, aliwataka viongozi wa Chama hicho kushirikiana katika kazi na kuwashirikisha wanachama katika maamuzi ya Chama ili kuhakikisha walimu wanajiendeleza kitaaluma.

Shani alisema kuwa, ni vema kuwaelimisha pia, walimu wasio wanachama kuhusu malengo ya C.W. T na faida zake kwa wanachama ili nao wavutike kujiunga na Chama hicho.

 Wakati huo huo: Afisa Elimu wa Wilaya ya Tarime, Michael Igogo ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na vyombo vya dola kufichua walimu wabadhilifu, wazembe na wanaoenda kinyume na maadili ya kazi zao.

Igogo alisema kuwa tatizo la kuwapo kwa baadhi ya walimu wanaokiuka taratibu na maadili ya taaluma yao halitatokomezwa kama wananchi watakaa kulilalamikia tu mitaani bila kufichua kwa kuwasilisha kwenye vyombo husika majina ya walimu wa aina hiyo ili wachunguzwe kwa kina.

Makamu wa Askofu ahamishiwa Roma

Na Pd. Pamphilius Kitondo, Rulenge

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Rulenge, Mhashamu Severine NiweMugizi, amemteua Padre Respicius Rugemalira kuwa Makamu wa Askofu wa Jimbo hilo badala ya Padre Protas Rugambwa anayekwenda Roma kufanya kazi katika Ofisi ya Kipapa ya Uenezaji wa Injili.

Kwa mujibu wa Mhashamu NiweMugizi, Padre Rugambwa anakwenda Roma katika Ofisi ya Uenezaji Injili katika upande wa Lugha ya Kiingereza.

Mhashamu NiweMugizi ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), alitangaza mabadiliko hayo katika hitimisho la mafunzo endelevu ya mapadre wa Jimbo la Rulenge, waliokusanyika katika Makao Makuu ya Jimbo.

Padre Rugemalira (38), ni mzaliwa wa Parokia ya Rubya.

Naye Padre Rugambwa (42) ni mzaliwa wa Parokia ya Nyaishozi, Karagwe.

Tangu Askofu NiweMugizi aingie madarakani,Jimbo la Rulenge limekuwa na utaratibu wa kuendesha semina maalumu za malezi endelevu ya kila mwaka kwa ajili ya mapadre wote jimboni.

Mafundi kuweni waaminifu kama vinyozi, wasusi

Na Getrude Madembwe, Iringa

“HUKO mitaani nasikia watu wakisema kuwa fundi mkweli ni kinyozi au msusi kwani hawezi kukuambia uache kichwa ukifuate kesho sasa hapa inaonesha ni jinsi gani mafundi wa nguo wasivyowaaminifu, lakini ninyi mliomaliza mafunzo haya msije mkawa mafundi wa aina hiyo; kuweni waaminifu kwa wateja wenu”.

 Padre Fransisko Msofu, aliyasema hayo wakati wa Misa ya Mahafali ya Wanafunzi wa Chuo cha Ufundi cha Sanaa House yaliyofanyika chuoni hapo mwanzoni mwa juma.

Chuo cha Sanaa House kinamilikiwa na Jimbo Katoliki la Iringa na kipo chini ya ofisi ya CARITAS, Kitengo cha Maendeleo ya Akinamama.

Alisema kuwa mara kwa mara watu wanakuwa hawaamini baadhi ya mafundi kwani hutoa visingizio vingi endapo hajamaliza kushona nguo ya mteja.

“Sasa nyie mfute hiyo dhana kuwa fundi mkweli ni msusi au kinyozi. Nanyi kuweni waaminifu katika ufundi wenu,” aliasa.

Akaongeza, “Huko mnako kwenda, jamii inataka kuona kile ambacho mmekivuna mnapaswa kuwasaidia na kuwaelekeza vizuri.”

Padre Msofu aliyekuwa mgeni rasmi, alisema katika kila roho ya mtu kuna mbegu bora na mchango kwa jamii, hivyo wahitimu wasiukalie ufundi wao bali wanautumie vizuri.

 Akijibu risala ya wanachuo iliyoeleza matatizo waliyonayo likiwemo la ukosefu wa vyumba vya kulia chakula na mabweni, Padre Msofu alisema kuwa uongozi wa chuo hicho una mpango wa kuongeza chumba kwa ajili ya kulia chakula, ofisi ya walimu pamoja na mabweni.

Walimshukuru Mlezi na Mkuu wa Chuo kwa malezi waliyoyapata tangu walipokuwa chuoni hapo kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mkuu wa Chuo ni Sista Sabina Witnes (CST) na Padre Gasper Makombe, ndiye Mlezi wa Chuo.

Chuo hicho pia hutoa mafunzo ya upishi wa vyakula vya aina mbalimbali, ufumaji wa vitambaa pamoja na kudarizi nguo za kike na za kiume na hutoa mafunzo ya bila kujali jinsia au dhehebu lolote.

Wataalamu sasa wanatumia elimu kuleta vurugu si maendeleo –Padre

   Na Lilian Timbuka

IMEELEZWA kuwa mwanadamu wa sasa amekuwa akiitumia vibaya elimu ya Sayansi ya jamii  kwa kuleta vurugu ulimwenguni badala ya kuitumia kwa manufaa ya umma.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Padre Leo Aman wa Kanisa Katoliki nchini wakati wa uzinduzi wa majengo ya Shule ya Sekondari ya Loyola  iliyopo katika Jimbo Kuu la  Dar es Salaam.

Alisema elimu haitakuwa  na maana endapo wasomi wenyewe ndio watakuwa chanzo cha vurugu, mauaji, uchochezi wa vita na kutengeneza silaha za ajabu ajabu kwa ajili ya maangamizi ya vita  kunakopelekea uvunjwaji wa amani duniani.

Alisema wazazi wanapowapeleka watoto wao shule mara zote huwa wanategemea kuwa mtoto anakwenda kujifunza mambo ambayo yatamsaidia  baadaye kwa kuwa na busara zaidi kuchangia kuleta nuru, amani na upendo miongoni mwa jamii.

Aidha,Padre huyo aliitaka jamii itambue kuwa siku zote elimu huanzia nyumbani kwa wazazi kuwafundisha watoto wao jinsi ya kuishi maisha ya kumpendeza Mungu na namna ya kuwasaidia watoto wenzao wasiojiweza.

“Daima msingi mzuri au urithi mzuri ambao mtoto hataweza  kuusahau katika maisha yake  duniani, ni urithi wa elimu. Sisi kama wazazi na wanajamii kwa jumla tusidharau kuwasomesha watoto wetu,” alisema.

Aliongeza kuwa katika karne hii ya Sayansi na Teknolojia, wasomi wengi wanapendelea kujifunza masomo yanayowasaidia kujiajiri wenyewe kuliko kutegemea ajira kutoka sehemu nyingine.

“Hivyo si budi wazazi wakaangalia shule ambazo watawapeleka watoto wao ambako watapata elimu ya kutosha kuwawezesha kujitegemea wenyewe hapo baadaye baada ya kuhitimu,” alisema.

Majengo yaliyozinduliwa yalijengwa kwa msaada ya Mapadre na Masista wa Shirika wa Jesuiti ambalo lipo chini ya Kanisa Katoliki.

Wakati huo huo; Waziri wa Elimu na Utamaduni,Bw. Joseph Mungai katika hotuba yake wakati wa ufunguzi wa majengo hayo, aliliomba Shirika la Wajesuiti  kuendelea kutoa misaada zaidi ya ujenzi wa shule hususan zile za msingi zenye uhaba wa  majengo.

Alisema Tanzaniai inaupungufu mkubwa wa shule za msingi hali inayosababisha mlundikano wa wanafunzi katika madarasa.

“Darasa moja lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 40, hivi sasa linakaliwa na wanafunzi zaidi ya 120,” alisema.

Shule ya Sekondari Loyola ilianza rasmi kutoa mafunzo mwaka 1995 kwa kuanza na wanafunzi wapatao 140.

Nusu ikiwa ni wasichana  na nusu nyingine wavulana ambapo hadi sasa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,100 wanasoma  kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Sita.