Make your own free website on Tripod.com

SAKATA LA SHILINGI MILIONI 5/= ZA KUPINGA UCHAGUZI:

Bunge lisikalie Mahakama- Mwanasheria

l   Mbona wananchi hawachangii miswada?’

l Asema demokrasia nchini ni kiini macho, maigizo

Na Lilian Timbuka

MWANASHERIA na Wakili wa Kujitegemea, Julius Francis Ndyanabo,  amesema Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, liheshimu Mahakama, badala ya kuonesha ubabe na kutaka kukaa juu ya Mahakama.

Ndyanabo ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Kitivo cha Sheria, alisema hayo katikati ya juma wakati akizungumza na KIONGOZI mintarafu muswada wa kupinga matokeo ya uchaguzi wa wabunge, kulipiwa shilingi milioni 5 taslimu.

Miongoni mwa miswaada inayotazamiwa kujadiliwa na Kikao cha sasa cha Bunge, ni ule unaohusu malipo ya dhamana ya shilingi milioni tano taslimu kwa mlalamikaji anayefungua kesi ya madai kupinga matokeo ya ubunge kabla shauri lake halijapangiwa jaji wa kulisikiliza.

Ndyanabo alisema, azima ya Serikali kuupeleka muswaada huo bungeni kwa ajili ya kuirudisha tena sheria hiyo, inaonesha wazi kuwa Idara ya Mahakama haithaminiwi.

Muswada huo umerejeshwa bungeni ikiwa ni miezi michache tu, baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kuitengua kwa kuwa iko kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nayotaka mtu anayepinga matokeo hayo ya uchaguzi kulipa sh. 500.

Wananchi wengi wameilalamikia hoja ya kutaka mpinga matokeo alipe shilingi milioni 5 kwa kuwa inatoa fursa kwa watu wasio waadilifu, kujipatia madaraka kwa kuwa Watanzania wasio na uwezo wa kulipa milioni 5, hawataweza kupinga matokeo hayo hata kama utaratibu wa uchaguzi ulikiukwa.

Muswada huu umerejeshwa bungeni, wakati Mahakama ya Rufani ikiwa bado haijatolea ufumbuzi wa mwisho na inamtafuta jaji wa kuisimamia.

Alisema kitendo cha Bunge kuurudisha muswada huo bungeni ili ujadiliwe wakati Mahakama haijatolea uamuzi ni ubabe wa Bunge dhidi ya Mahakama na wananchi.

“Lazima Bunge lijue kuwa, kazi yake ni kutunga sheria na mahakama ainazitafsiri… sasa isifikie hatua Bunge likajichukulia mamlaka yote,’ alisema.

“Tofauti na ilivyokuwa mwanzo, safari hii umeongezewa makali, na hivyo kuzidi kuwatenga wananchi kati ya maskini na matajiri. Bunge lisitumiwe vibaya kwani kitendo kinachofanywa sasa ni kukaidi na kuonesha ubabe…, Serikali isilifanye Bunge kuwa juu ya sheria na Mahakama,” alisema.

Alisisitiza kuwa hali hiyo inaonesha dhahiri kuwa kama jamii na vyombo husika havitakuwa makini, Mahakama haitathaminika.

Awali, Mahakama ya Rufani ilibatilisha na kuzuia sheria hii isitumike kwa kuwa Katiba ya nchi na haki za binadamu vilikiukwa.

“…Unaona sasa Serikali imeandaa muswaada mwingine ili kuhakikisha kuwa sheria hiyo inayowabana wananchi na kuruhusu hata viongozi wabovu kuongoza, inafanya kazi,” alisema.

Alisema hali hiyo inaonesha kuwa, licha ya Mahakama ya Rufani kuwa na mamlaka ya kufuta sheria yoyote ambayo ni batili, lakini Serikali inaweza kukaidi amri ya mahakama. Bunge lisitumiwe vibaya kwani kitendo kinachofanywa sasa ni kukaidi na kuonesha ubabe, Serikali isilifanye Bunge kuwa juu ya sheria na Mahakama,” alisema.

Alisema inasikitisha kuona kuwa  muswada huo ukipitishwa, utawaumiza wananchi na kuwafanya wanung’unike kama taratibu za uchaguzi zitakiukwa, lakini wakawa hawana uwezo wa kufungua kesi mahakamani kutokana na kiwango hicho cha malipo kuwa kikubwa zaidi (milioni 5).

Ndyanabo alisema ni vema ikaeleweka kwamba mawakili wa Tanzania hawalalamikii suala la pesa, bali haki ya raia kwenda katika chombo cha haki na uhuru na kupata haki yao katika vyombo vya sheria.

“Hatua ya kupeleka tena muswada huo bungeni ni dalili za kuidhalilisha, kuidhihaki na kuidharau Mahakama, pia ni upokonyaji wa kupindukia wa demokrasia,” alisema.

Alifafanua kuwa, kisheria muswada halali unapaswa kutangazwa katika gazeti la serikali kwa muda wa siku 21 ili kuwapa wananchi nafasi ya kutoa maoni yao.

Akasema, Kwa Tanzania wananchi wamekuwa hawapati muswada katika kipindi hicho kutokana na utekelezaji wa jukumu hilo kwa viongozi wa ngazi ya kati ya serikali ambao wamekuwa wakikwepa baadhi ya majukumu yao.

“Chini ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kifungu cha 18, kila mwananchi ana haki ya kupata habari, lakini katika siku za hivi karibuni hili limekuwa halifanyiki na ni kosa kikatiba na wananchi wengi wanalalamikia miswaada hii kwa vile hawaioni hata kidogo,” alibainisha.

Akilinganisha hali ya kisiasa katika Mfumo wa Siasa wa Vyama vingi nchini tangu uanze kutumika mwaka 1992 nchini, Wakili Ndyanabo alisema vyama vya siasa kwa hivi sasa vimekuwa dhaifu ukilinganisha na miaka ya nyuma.

Alibainisha sababu kubwa ni hali mbaya ya kiuchumi inayovikabili vyama hivyo, pamoja na kushindwa kujipanga vema ili kukabiliana na ushindani mkubwa kutoka kwa Chama Tawala (C.C.M).

Alisema sababu nyingine inayoidhoofisha kambi ya upinzani nchini ni pamoja na kambi hiyo kuingiliwa na baadhi ya mamluki wenye uroho wa kuingia Ikulu.

Amevishauri vyama vya upinzani kushirikiana na kuweka mikakati ya pamoja sambamba na kuepuka malumbano ya ndani kwa ndani ya vyama.

Hata hivyo, Ndyanabo alisema licha ya tanzania kuendesha mfumo wa vyama vingi kwa amani, bado hali ya kidemokrasia sio ya kuridhisha.

 “Kwa kweli demokrasia tuliyonayo ni ya kiini macho kwa vile bado vyama vya upinzani vinaendelea kunyanyaswa kwa kunyimwa nafasi ya kufanya mikutano ya hadhara, halafu viongozi wake wamekuwa wakikamatwa ovyo na vyombo vya dola”.

Ushindi wa Kopa, Tambalizeni; CCM imepata sura gani?

Na Boniphace Makene

USIKU wa kuamkia  Oktoba 30, Wajumbe wa CCM wapatao 1,700 waliokuwa Dodoma wakisubiri uchaguzi hawakupata nafasi nzuri ya kulala kutokana na kampeni kali zilizokuwa zikifanywa na wagombea waliokuwa wakiwania nafasi mbalimbali nyeti za kukiwakilisha Chama hicho Tawala hapa nchini.

 Karibu hoteli zote, migahawa na baa zilizopo Dodoma   zilifurika wawakilishi wa Chama hicho kutoka mikoa mbalimbali.

Wajumbe hawa walikuwa katika pilikapilika za kuhakikisha wanakamilisha kazi ya kuwapigia debe wagombea wao na pia, kuhakikisha wale wasiowataka wanawamaliza kwa kampeni mbaya dhidi yao kabla ya uchaguzi siku iliyofuata.

Hawakuuthamini usingizi wa siku hiyo kufuatia kazi kubwa iliyokuwa ikiwakabili na waliamini kuwa wangepumzika tu, baada ya kuimaliza.

Walifahamu ni nani wanataka kumchagua na nani hawataki kusikia anarejeatena katika kiti alichokuwa nacho katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Si  uongo, wajumbe walipania na hata wagombea nao walionesha nia ya kulinda heshima zao kwa wale waliokuwa na nyadhifa hapo awali na wale waliokuwa wanawania kwa mara ya kwanza, walikuwa na kazi ya kutafuta mapungufu ya wazoefu ili kuwamaliza.

Kutokana na ugumu huu, yaliibuka makundi mbalimbali kama ambavyo yamekuwa yakionekana ndani ya chaguzi za Chama hicho kwa miaka kadhaa.

Masuala ya Ujimbo,Umikoa na Ukanda yaliyozoeleka ndani ya Chama hichokama kawaida, yaliendelea kuvinjari.

Suala la Waasisi wa Chama ama Wazee wa Chama na Vijana, nalo lilikuwa na picha fulani. Wapo walioamini kuwa  dawa ya kukilinda Chama ni kuendelea na viongozi wengi wazee na wapo waliosadiki kuwa nyakati hizi ni za vijana hasa katika kukirutubisha Chama.

Wagombea waliozoea kutumia takrima safari hii walipata wakati mgumu kufuatia kuwepo kwa wafanyakazi wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa Nchini (PCB), waliokuwa  wamemwangwa kama njugu mjini humo.

Hata hivyo, mawasiliano yalibakia yale ya simu za mkononi ambazo zilionekana kuongezeka kwa wingi kwani asilimia kubwa ya wajumbe walikuwa nazo. Kulikuwa na kila sababu ya uchaguzi huu kuwa mgumuhasa ukifahamika kuwa hiki ni kipindi cha mwisho kwa Rais Mkapa.

Rais Mkapa hatagombea tena Urais kupitia Chama hicho katika Uchaguzi Mkuu ujao, kufuatia kumaliza vipindi vyake viwili ambavyo Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inamruhusu kutumikia kama Rais. Kipindi cha mwisho kinamalizika mwaka 2005.

Hali hii iliufanya Uchaguzi huu wa CCM kuwa kioo cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005. Yeyote mwenye nia ya kugombea nafasi fulani muhimu katika Uchaguzi Mkuu ujao, alitakiwa kujiangalia kama anakubalika kwanza ndani ya Chama katika uchaguzi huu, kabla ya kuanza jitihada za kuwania nafasi katika Uchaguzi Mkuu ujaowa 2005.

Matokeo ya Uchaguzi huu ambao hasa ndiyo mada ninayotazamia kuijadili, yaliutia mashaka upande  fulani wa watu na wengine wakabaki wakitabasamu. Naamini wapo waliofahamu nini kitatokea, lakini wengi  walikaa kimya hadi matokeo yalipotangazwa.

Matokeo haya yaliwatupa nje mawaziri na baadhi ya watu maarufu ndani ya CCM ambao walidhaniwa kuibuka washindi katika uchaguzi huo.

Haikufahamika mapema nini hasa kilichowafanya wana CCM kuwapiga mwereka Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Emanuel Nchimbi,Waziri Edgar Maokola Majogo, Waziri Wilson Masilingi na Profesa David Mwakyusa.

Wengine walioanguka katika kinyang’anyanyiro hicho ni; Dk. Pius Ngw’andu, Naibu Waziri wa Viwanda, Ritta Mlaki na mwenzie Naibu Waziri wa Sayansi Teknolojia na Elimu ya Juu, Zubein Mhita.

Hawa ni wachache tu, wapo walioonesha kushuka chati kama Waziri Jakaya Kikwete ambaye mwaka 1997, alishika nafasi ya pili katika kundi la wajumbe 20 kutoka Tanzania Bara, lakini safari hii ameshika nafasi ya 12.

Edward Lowassa katika kundi hili hili, mwaka 1997 alishika nafasi ya tano, lakini sasa amepata nafasi ya 15.

Waheshimiwa hawa wawili wanazidisha maswali mengi kwa wachambuzi wa mambo ya Siasa hapa nchini. Wote wawili wameshuka chini kwa hatua kumi na ifahamike walikuwa kati ya wagombea wenye nakshi wakati wa kuwania nafasi ya kugombea Uraisi kupitia CCM mwaka 1995 ambapo Rais Mkapa aliibuka 'kidedea'.washindi.

Mawaziri hawa licha ya kubakia ndani ya Halmashauri Kuu ya CCM, bado walitarajiwa kufurukuta tena katika kuwania Urais mara baada ya Mkapa kumaliza muda wake, lakini matokeo ya namna hii yanaacha maswali mengi.

Hadi sasa haifahamiki kama waheshimiwa hawa walishushwa kimakusudi na wapiga kura ili kuwakatisha tamaa, ila naamini haya ni matukio ya kawaida sana katika siasa.  Inawezekana walisahau nafasi ya wakati katika kutafuta mbinu mpya za kunasia kura.

Kwa sasa mawaziri hawa huenda wamefunua ukurasa mpya na huenda watayasoma mazingira na kuufahamu wakati ili kuhakikisha wanarejesha heshima zao ndani ya CCM kama kweli wana lengo la kusonga mbele. Naamini watafanya hivyo na kamwe hawatalala usingizi kwani safari bado inaendelea.

Mjumbe mmoja wa CCM, aliyekuwepo Dodoma ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini alielezea kuwa, ulikuwapo mkakati maridhawa wa kumaliza uchu wa madaraka walionao mawaziri wa Serikali hii. Mkakati ulipangwa ukapangika na matokeo yake yameonekana.

Mjumbe huyo alifafanua kuwa hata mbinu walizotumia kuomba kura mawaziri hazikuwa kama zile walizokuwa wakizitumia wakati ule walipokuwa hawajapata nyadhifa hizo.

Walionekana kuweka mikono mifukoni na kamwe hawakupoteza muda kuomba kura kama walivyofanya wagombea wasiokuwa na majina.

Inasemekana kuwa mawaziri hawa waliamini kuwa nyadhifa zao zilitosha kuwapa kura. Waliamini wanaaminika hivyo kuomba kura katika staili ile ya zamani ilikuwa kujidhalilisha.

Na tuwaache mawaziri hao, turejee katika kundi hili la akina  Hadija Kopa,  Salum Tambalizeni na Ibrahim Jongo ambao waliwashinda wasomi kama Dk. Hassy Kitine.

Hii siasa ndani ya CCM inatoa wigo mpya wa jamii  iliyopo hivi leo.

Katika pitapita zangu ndani ya wasomi wa Chuo Kikuu (Mlimani), nilikutana na mjadala wa aina hii. Wengi kati ya wale niliopata nafasi ya kuzungumza nao walihoji uhalali wa wana CCM kuanza kuchagua wajumbe  wa staili hii ya akina Kopa.

Walisikika baadhi wakisema kuwa, hali hii inakatisha tamaa wasomi kwani wasanii kama akina Kopa waliwamwaga chini wasomi kadhaa.

Wasomi hawa walidiriki hata kuiona jamii kuwa haithamini tena umuhimu wa wawakilishi ndani ya nchi kuchaguliwa huku viwango vyao vya elimu vikichukuliwa kama taswira.

Dai hili linanifanya nianze kuamini kuwa jamii haioni tena thamani kwa wasomi waliopo kwani huenda wametumia usomi wao katika upande mwingine wa shilingi. Wametumia taaluma zao kujinufaisha badala ya kuisaidia jamii jambo ambalo linajionesha wazi siku hizi.

Jamii sasa inawathamini wasanii kama akina Kopa na Tambalizeni kwani afadhali wao wanasikika wakijadili masuala mbalimbali ya jamii kupitia tungo zao. Huu ni ukweli uliowazi kwani wasomi wa sasa wanajadili zaidi maslahi yao kwanza kabla ya yale ya jamii.

Hoja hii inasawiri sana kwani wasanii mathalani wa muziki wa kufokafok,a huyazungumza matatizo ya jamii pasi kificho na woga tofauti na wasomi wetu. Wasomi wamebakia kuhudhuria warsha na semina wakijadili mipango ambayo mingi haina maslahi ya moja kwa moja na wananchi wa kipato cha chini.

Wapo watu wanaotamka bayana kuwa uchaguzi wa staili hii ya akina Tambalizeni na Kopa ndani ya CCM unaonesha namna Chama hicho kilivyochoka ukiritimba wa kuwaachia baadhi kuwa wafalme ndani ya Chama hicho.

Sasa hata wananchi wa chini nao wanataka kupata haki muhimu ya kuwawakilisha wenzao ndani ya Chama hicho.

Tukio kama hili linatoa taswira pana sana ya nini kilichopo ndani ya jamii ya sasa. Inawezekana mara nyingi kamati za vyama mbalimbali zimekuwa haziwapi nafasi ya kuwania madaraka wananchi wa chini hali iliyowapa kiburi wasomi na wale wenye mali kudhani ni haki yao kuongoza.

Suala la wenye pesa lilikuwa linatoa taswira mpya ya nani anapaswa kuchaguliwa. Nafasi ya kupigiwa kura imekuwa ikiangalia nani aliye na uwezo wa kujinadi kwa mbinu yoyote ili kukipa Chama ushindi.

Naamini jamii imekuwa ikipewa viongozi ambao haiwahitaji siku nyingi ili tu, kulinda heshima za vyama.

Hapa kinachojaliwa zaidi si uwakilishi kwa mujibu wa mapenzi ya wananchi bali nafasi ambazo Chama kinazihitaji kuwa nazo katika Bunge ama Halmashauri.

Uwezo wa utoaji takrima katika kundi la akina Kopa ambalo linatuwakilisha watu wa chini ni gumu kulijadili hapa.

Imani ya mgombea imekuwa haiangalii tena uwezo wa mtu kifikra ama namna anavyokubalika tu, bali kumeongezeka uwezo wa yeye kuwa na fedha.

Mgombea tajiri amekuwa akithaminika kwani anaweza kuwanunua wapiga kura na hivyo, kutokiangusha Chama pale ambapo atashindwa uchaguzi hivyo chama nacho pengine kikaongeza idadi ya viti vya uwakilishi. Kopa hakuwa na kipeperushi na wala hakujipigia debe kama walivyokuwa wengine kabla ya uchaguzi, lakini aliibuka mshindi!

Aliutumia usanii wake na kwa kipaji chake akaomba fadhila kwa wapiga kura, mwisho wapiga kura wakamuonea huruma wakamzawadia kura.

Hili funzo lisiishie hapa liende hadi Uchaguzi Mkuu ujao ili hata sisi watu wa chini tupewe nafasi sawa na wenye mali katika kuwania nafasi za ubunge hata udiwani.

Funzo hili liviendee vyama vyote vya siasa ili vifahamu kuwa kuna haja ya kubadili mfumo wa kutafuta wagombea. Vyama visiangalie tena nani ana nini kwa hali ya fedha, bali nani ana uwezo upi katika kuipatia jamii maendeleo kufuatia nafasi anayoiomba.

Kwa kufanya hivi, naamini hakutakuwa na haja ya kupambania madaraka kwa mbinu za Kikabila, Kimikoa, Kikanda na Kivyama. Wananchi watakuwa na uhuru zaidi wa kuchagua wawakilishi wao kwa mujibu wa unyenyekevu, uadilifu na uwezo wao wa kuimarisha harakati za kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

Hii ni mbegu ambayo wana CCM wameanza kuipanda, inapaswa kuoteshwa hata vijijini ili katika uchaguzi ujao, wananchi wazikimbie takrima. Wasikubali tena kuuza kura kama ambavyo wamekuwa wakifanya.

Tena wasichague viongozi ndani ya kioo cha chama anachotoka mgombea bali wahakikishe wanaangalia sifa halisi za wagombea. Katika kufanya hivi kutasaidia sana hata kurejesha siasa safi ambazo zilipandwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Kwanini wanaume hujionesha bora kuliko wanawake?

l Ubaguzi wa kijinsia hufanywa bila mtu kujijua

Na Pastory Nguvu

TARATIBU, maisha yake yakakatika huku yakiwa ni majira ya saa saba na nusu mchana wa Ijumaa hiyo, ambapo msichana Jackline (27), akiwa amevalia gauni la kijani, alikutwa akihema kwa tabu kitandani kwake, maeneo ya Mabibo-Jeshini, jijini Dar es Salaam, mapema mwaka huu.

Dakika chache kabla ya alasiri hiyo, Jackline aliyekuwa akitetea sana haki za wanawake, alifariki dunia na kuacha ujumbe usemao, “Ningetamani sana kama ningebaki na kuishi maisha ya afya na ya kawaida.”

Hayo ni baadhi ya maneno yaliyoandikwa katika ujumbe aliouacha Jackline kwa ndugu na jamaa zake.

Hii ilikuwa hatua iliyofikiwa baada ya miaka mingi ya ushindani ndani ya moyo wake akijiuliza ama ampe penzi Meneja wa Kampuni aliyofanya kazi (jina tunalihifadhi), au akatae na akubali kufukuzwa kazi.

Jackline akaona kwake njia sahihi ya kuepuka vurugu hilo ndani ya moyo wake, ni kujimaliza kimaisha na kuondoka kabisa hapa duniani.

 Akabugia idadi kubwa ya vidonge aina ya klorokwini, alivyovisukumiza kwa bia. Ujumbe wake ukamalizia kwa maandishi, “Utukufu uwe kwa Mungu.”

Hata hivyo, hali iliyomkumba Jackline, bado inawakumba wanawake wengi duniani na hususan hapa nchini Tanzania.

Ubaguzi wa kijinsia limekuwa tatizo ambalo linaathiri na pengine kukatiza maisha ya watu wengi hususan, wanawake.

Katika mazungumzo yake naGazeti la KIONGOZI, Mwanasheria, Adamu Mambi, amekiri kuwa tatizo la ubaguzi wa kijinsia ni kubwa na hivyo, linahitaji kupewa umakini wa hali ya juu.

“Ni tatizo kubwa ambalo inatubidi sote tulikabili kwa makini,” alisema Mambi.

Akakiri kuwa ni kazi kubwa kuondoa ubaguzi huo kwani wengi huufanya bila kujijua.

Lengo la makala haya ni kuweka bayana madhara yatokanayo na ubaguzi wa kijinsia. Katika toleo hili, tutaangalia maana ya ubaguzi wa kijinsia na kibaolojia baina ya wanawake na wanaume na kisha, tuendelee kuona maeneo yanayoshamiri kwa ubaguzi huo na athari zake na pia, tuangalie ni sababu zipi zinazotosha jamii kuamua kupiga vita ubaguzi huo wa kijinsia.

Kwa kuanzia, hebu tuangalie maneno UBAGUZI WA KIJINSIA yana maana gani hasa.

Mtaalamu mmoja wa Lugha ya Kiswahili, Bw. Emil Hagamu, anautafsiri ubaguzi wa kijinsia kuwa ni hali au hatua ya jinsia moja kukandamizwa au kunyonywa na jinsia nyingine.

“Hata hivyo, msemo huu mara nyingi unatumika zaidi kumaanisha ile yali ya wanawake kukandamizwa na wanaume katika jamii mbalimbali duniani,” anasema Bw. Hagamu.

Kwa mujibu wa wanabaiolojia, yapo maeneo matano makubwa yanayowatofautisha wanawake na wanaume.

Kwanza, kuna tofauti katika Chromosones au genes kati ya mwanamke na mwanaume.

Wanabaiolojia wamebainisha kuwa, wakati wanawake wa XX genes, wanaume wao wana XY.

Tofauti nyingine ni katika homoni. Wanawake wana homoni aina ya endrogens, lakini wanaume wanazo homoni zinazoitwa estrogens.

Tofauti nyingine ipo katika viungo vya ndani vya mfumo mzima wa uzazi.

Viungo vya uzazi vya wanawake ni uterus na fallopian tubes, lakini wanaume wana seminal vescles.

Mwisho, viungo vya nje vya mfumo wa uzazi. Wanawake wanavyo vinavyoitwa uke, wakati wanaume viungo vyao vya nje vya uzazi huuitwa uume.

Kwa jumla zipo tofauti kati ya uzito na maumbile ya mwili, baina ya mwanamke na mwanaume.

Makala haya hayakusudii pia kufundisha baiolojia, lakini tujiulize kuwa, je, sababu hizo za kibaiolojia zinaweza kutosha kuhalalisha ubaguzi wa kijinsia baina ya wanawake na wanaume katika kazi, tabia na nafasi kama inavyoonekana katika jamii zetu?

                                            Itaendelea

'Ni rahisi mwenye UKIMWI kuingia peponi endapo...'

Na Meryna Chillonji

 

WAGONJWA wa UKIMWI wameelezwa kuwa watu wenye nafasi rahisi zaidi ya kuingia peponi endapo wataamua kufanya toba ya kweli .

Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali la Never Loose Hope Bw. Emmanuel Mziray wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kipawa, Dar es Salaam, aliyasema hayo mbele ya waamini wakati akitoa ushuhuda wake wa maisha.

Alisema ingawa wagonjwa wengi huonekana kukata tamaa na kuchukuliwa na baadhi ya watu kuwa wao ndio wadhambi, lakini wanayo nafsi kubwa ya kujitoa kwa Mungu na kufanya toba ya kweli na hivyo, kuwa na uhakika wa kuingia peponi.

Alisema kuwa shirika lake la Never Loose Hope limekuwa likijishughulisha na watu wa jinsi hiyo kwa muda mrefu kwa kuzunguka sehemu mbalimbali ambazo anaamini ujumbe wake ungeweza kuwafikia watu wengi kwa wakati mmoja kama shuleni, makanisani pamoja na kuitisha mikutano sehemu mbalimbali

Mziray alisema sababu hasa iliyompelekea kulielimisha Kanisa kuhusu ugonjwa wa UKIMWI ni kuguswa na Roho wa Mungu, hivyo asingependa kuliona Kanisa likiangamia wakati anao uwezo wa kulinusuru lisiangamie zaidi.

Aliwashauri Wakristo wanaoshabikia ngono kwa kutumia kondomu kama kinga dhidi ya UKIMWI, kutambua kuwa wanajidanganya na kuweka uweezekano wa kuangamiza maisha yao.

Alisema njia imara ya kuepuka UKIMWI ni kuacha vitendo vya ngono kabla ama nje ya ndoa na badala yake, kufanya mambo yote kuzingatia mapenzi ya Mungu.

“Mwenye UKIMWI akitubu Mungu atamgeukia na kumsamehe dhambi zake zote kwani Mungu atamhukumu mzinifu na siyo mwenye UKIMWI kwa sababu wapo watu ambao wanazini na hawana UKIMWI na wengine wana UKIMWI, lakini hawakuzini,”alisema Mziray.

Utandawazi unatuua-TYCS walia

l  Wataka vijana waache 'umalaya' wa kidini

Na Joseph Sabinus

 

UMOJA wa Wanafunzi Wakatoliki wa Shule za Sekondari na Vyuo Tanzania (TYCS), umeishauri Serikali kudhibiti habari ziingiazo nchini kupitia mtandao wa internate kwani unawaua vijana kiroho na umewataka vijana kuepuka umalaya wa kidini.

Wakizungumza na KIONGOZI, Kurasini Dar e Salaam, Katibu Mkuu Mstaafu wa TYCS, Taifa, Bw. Leonard Gastori na Mjumbe Mstaafu wa TYCS, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Bw. Robert Rweyemamu,  walisema kwa pamoja kuwa katika ziara zao kwa baadhi ya majimbo ya Kanisa Katoliki nchini, wamebaini kuwa utandawazi umewaathiri vibaya vijana katika maeneo yenye mawasiliano ya internate kuliko vijana wa maeneo ambayo hayajafikiwa na teknolojia hiyo ya mawasiliano.

Kuanzia Oktoba 2 hadi 21, mwaka huu, wawakilishi hao wa TYCS walizuru baadhi ya majimbo ya Kanda ya Ziwa yakiwamo ya Musoma, Geita na Bukoba na pia, katika majimbo ya Kanda ya Kaskazini katika majimbo ya Mbulu, Moshi na Jimbo Kuu la Arusha.

Huko Kanda ya Kaskazini, vijana hao waliambatana na Makamu-Mwenyekiti Mstaafu wa TYCS Taifa, Bw. Renatus Rugonzibwa na mmoja wa Wajumbe Wastaafu wa TYCS, Taifa, Bw. Paulo Marwa. Lengo la ziara hiyo lilikuwa kutathmini na kuhamasisha shughuli za TYCS majimboni.

Katika Jimbo la Mbulu, vijana hao waliambatana pia na Mlezi wa TYCS kitaifa, Padre Lucas Mzuanda.

“Tulijaribu kuangalia mwamko wa imani kwa vijana na kuangalia kama kweli wanaishi kama Wana-YCS kwa kutekeleza maazimio ya kitaifa,” alisema Bw. Rweyemamu.

Walipoulizwa na KIONGOZI kuwa walibaini nini hasa, Bw. Gastori alisema, “Wengi hasa majimbo ya Kanda ya Ziwa, walisema utandawazi haujawaathiri sana kwa sababu sehemu nyingi hawapati huduma za teknolojia ya internate na hata sehemu nyingine ambapo huduma hiyo inapatikana, gharama ni kubwa hivyo wengi kushindwa kuitumia”

Akaongeza, “Wao hawajaathirika kama huku (Dar) kwa kuwa mazingira yao walau yanawahifadhi kiimani na kimaadili na yanawalinda hata watoto.”

Akifafanua zaidi, Bw. Gastori alisema, tofauti hiyo inabainika kutokana na ukweli kuwa vijana wengi wa mijini wanaopata mawasiliano ya internate, wamebomoka kimaadili kwa kuwa wengi wao badala ya kujifunza mambo yanayowajenga kiimani na kijamii, wanajifunza mbinu za uhalifu na mitindo ya kihuni.

Aliyataja madhara hayo kuwa ni pamoja na kujifunza mbinu za uhalifu ikiwa ni pamoja na matumizi ya silaha na ugomvi, mitindo mibaya ya mavazi na kutoga masikio na pua hata kwa wavulana, hali aliyosema sio utamaduni sahihi wa Mtanzania.

“Mfano, vijana wa Kimarekani wanavaa suruali na kuzishusha hadi mapajani, lakini baadhi ya vijana wa mijini wakiona hivyo kwenye intrenate au TV, bila kuchuja uzuri na ubaya wa kufanya hivyo, nao wanaiga. Wanatafuta umaarufu kupitia wanayoyaona kwenye internate na TV,  alisema Bw. Rweyemamu.

Akaongeza, “Wengine wanamuona Michael Jordani amevaa hereni, bila kujua ni kwanini  na ana maana gani, wanaiga tu. Vijana Watanzania hawana budi kuwa macho, tunatawaliwa kisaikolojia, sasa hatuvithamini tena vipaji vyetu tunadhani vinavyoonekana kwenye TV na internate ndivyo bora.”

Walisema ingawa hawapingi matumizi ya jumla ya internate na utandawazi kwa jumla, lakini vijana na wanajamii wengine wanaotumia njia hizo za mawasiliano, hawana budi kuchuja yaliyomo ili wawafikishie mazuri wanaopokea habari kupitia kwao hususan walioko vijijini.

“Tusipokuwa makini, Dar es Salaam tutapokea bila kuchuja, tutapeleka mikoani, watapokea bila kuchuja, watapeleka vijijini nao, wakipokea bila kuchuja unategemea Kanisa na Taifa la kesho kuanzia kule kijijini litakuwa na watu gani!” Alisema Rweyemamu.

Waliisisitiza jamii ya Watanzania kuendeleza vipaji vya vijana toka vijijini ili waendelezwe hata nje ya nchi kuliko, kukazania kupokea tu, tamaduni za nje na kujifunza bila kujali athari zake kwa jamii ya Watanzania na kwa Kanisa.

Walisema katika ziara yao, wamebaini kuwa vijana wengi wanaopata fursa ya kutazama televisheni, hukazania vipindi vya maigizo, lakini hawana uelewa wala matumizi yoyote ya habari za maendeleo.

“Sasa kwa hali kama hiyo, ukimueleza kijana kuwa vijana wameharibikia, anakubali, ukimuuliza mazingira wanayoishi vijana pamoja na yeye kama yameharibika, anakubali, lakini ukimuuliza yeye mwenyewe ameharibikiwa, anakataa, hakubali kuharibikiwa…,” alisema Bw. Gastori.

Vijana hao waliwahimiza vijana na wote wenye mapenzi mema, kukubali mapungufu yao ili wajipe nafasi ya kujirekebisha na kujifunza mengine mazuri toka kwa watu wengine.

Walisema vijana hawana budi kutumia elimu yao kuchambua na kuyakabili mazingira yao.  “…Wajue kuwa kijana anayesoma huku mawazo yake yako kwenye ngono na michezo ya kuigiza tu, anasoma elimu negative (hasi) na anajiandaa kwa UKIMWI tu, pia hata mbele ya watu, mtu kama huyo hawezi akajieleza kitu chochote,” alisema Rweyemamu.

Aliongeza kuwa, inasikitisha kuona vijana wengi hawataki kukubali kuwa UKIMWI ni sehemu ya wanayokutana nayo katika maisha yao, lakini sio wao .

Aidha, waliwahimiza vijana na wanajamii kwa jumla, kuepuka tabia ya kuwa malaya wa kidini kwani hali hiyo inawabomoa kiimani kutokana na wengine kukutana na vikundi vya dini vinavyoendesha shughuli zao kitapeli.

“Mfano, kuna dini nyingine zinaibuka na kuwagawia watu mikate kama njugu, lakini baada ya siku mbili huwezi kujua dini hiyo sasa iko wapi…. Bila uimara wa kiroho ni hatari kiroho kwani unaweza kuyumba sana.”

Katika mazungumzo hayo na KIONGOZI wiki iliyopita, vijana hao wa TYCS, waliihimiza Serikali kuwa karibu na kuinua vipaji vyao kwa kuwapa miongozo sahihi ya maisha na kuwasaidia wanapokwama, badala ya kukalia kuwalaumu wanaposhindwa kufanya wanavyotakiwa.

“Wazazi na Serikali wawe karibu na vijana, wasikalie kuwalaumu tu eti vijana wa siku hizi wako hivi, wasikate tamaa maana malezi ya vijana yanahitaji busara za wazazi…, wazazi wakileta msukumo, tutafika mahali pazuri.” Alisema mmoja wao.

‘Wasichana msijichukie kwa kuchelewa kuolewa’

Na Margareth Charles

WASICHANA wameshauriwa kutambua kuwa thamani yao haiongezeki wala kupungua kutokana na  kuolewa au kotokuolewa, bali kutegemea matendo yao katika jamii, hivyo wasioolewa wasijichukie wala kukata tamaa.

Akitoa mada katika Kongamano la Wasichana lililofanyika Jumamosi iliyopita katika Kanisa la African Inland Church- Tanzania (AICT), Magomeni Dar es Salaam, Bibi Mariam Salala, alisema kuwa thamani ya msichana au mwanamke mbele za Mungu ni ileile kutegemea na namna anavyoishi mtu hivyo, dhana ya kuwahi au kuchelewa kuolewa sio kipimo cha thamani ya mtu kwa Mungu.

Bibi Salala, alisema kuwa, kwa mwanamke yeyote kuwahi au kuchelewa kuolewa kunategemea mipango maalumu ya Mungu, hivyo jamii wakiwamo wasichana, waondokane na fikira potofu kuwa kuolewa au kutokuolewa kunabainisha thamani ya msichana.

Alisema kuwa akinadada wengi wamekuwa na mawazo potofu kuwa endapo watafikisha umri mkubwa bila kuolewa huenda thamani yao ikapungua mbele za jamii na mbele ya Mungu, kitu alichosema sio kweli.

Aliongeza kuwa, wanadamu wote  wameumbwa kwa Neno, mfano na sura ya Mungu, vilevile wakapewa madaraka ya kutawala vitu vyote duniani (mwanzo 1:26-27).

Alisema, msichana anatakiwa ajiulize kuwa, YEYE NI NANI KATIKA KRISTO,  na pia ajiulize,  JE KWELI ANAISHI KWA MFANO WA MUNGU?

“Sisi ni mawakili wa Mungu, tunamuwakilisha Mungu kwa mienendo yetu, kama akinadada tunatakiwa kuwa wasafi wa roho na mwili,” alisisitiza.

Hata hivyo, alisema upendo wa Mungu unadhihirisha jinsi wanadamu walivyo na thamani kwa Mungu pale alipomtoa mwanae Yesu Kristo ili afe msalabani kwa ajili ya wanadamu.

Aliwataka wasichana waliohudhuria kongamano hilo wajiulize kuwa, wao kama wasichana wanaitumiaje miili yao katika kumtukuza Mungu?

Awali, Bibi Salala alisema kuwa, mwanadamu katika maisha yake anaweza kupitia hatua tatu alizozitaja kuwa ni kuzaliwa, kuoa au kuolewa na kufa.

Akifafanua, zaidi kuhusu hatua hizo alisema, kuzaliwa na kufa ni hatua ambazo mwanadamu lazima azipitie, lakini kuoa au kuolewa, ni hatua ambayo si ya lazima isipokuwa ni mpango na mapenzi ya Mungu.

Ukristo wa kupiga ramli ni uongo- Askofu

Na Getrude Madembwe, Iringa

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, amewashauri Wakristo wanaosema kuwa wanamsadiki Yesu wakati bado wanaenda kwa waganga wa kienyeji kupiga ramli waache mara moja kwa kuwa hali hiyo sio Ukristo bali ni uongo mtupu.

Aliyasema haya wakati akihubiri katika Jumapili Ibada ya Sakramenti ya Kipaimara iliyofanyika Jumapili iliyopita katika Kanisa la Parokia ya Ifunda. Watoto 185 walipokea Kipaimara.

“Inashangaza kuona mtu amebatizwa na wakati wa Ubatizo alijazwa Roho Mtakatifu, lakini bado mtu huyo ni mpagani Kanisani haendi au anaamini waganga wa kienyeji,” alisema.

Alisema, “Mtu aliye na Roho, nafsi yake inakuwa safi na uhusiano safi na hata maneno yake watu hupenda kuyasikiliza”.

Aliwataka wakristo kutokuwa watu wa kubabaika kwani Injili ni msamaha kwa watu wote ambao wamedhamiria kuachana na dhambi.

Mhashamu Ngalalekumtwa, alisema kuwa jukumu la kila Mwana-kanisa ni kushiriki kikamilifu katika kutoa Injili ya Kristo kwa kueleza, kuifafanua na kuitangaza kwa watu wote.

Akisoma taarifa fupi ya parokia hiyo kwa Askofu, Mwenyekiti wa Baraza la Walei Parokiani, Bw. Charles Lutego, alisema shilingi milioni 1.8 zimekusanywa ambazo ni pamoja na mali zilizochangwa na waamini katika kuanzia Januari hadi Oktoba, mwaka 2002.

Alisema kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya Paroko Padre Alfonsi Mwamilawa na Paroko Msaidizi Basil Mzena, wamefanikiwa kutoa mada mbalimbali za kuwajenga Kiroho na  Maadili kwa vijana wa kike na wakiume wapatao 260 na kufanya kuongamano la vijana.

Alisema katika kipindi cha mwaka 2002, wameongeza Jumuiya Ndogondogo za Kikristo toka 44 hadi 62, na kuendesha Semina kwa viongozi wa Baraza la Walei vigangoni.

Hata hivyo alisema, “Pamoja na elimu nzuri inayotolewa na Kanisa kuhusu UKIMWI , bado walei wamekuwa sugu na bado  wanaendelea na matendo yanayosababisha ugonjwa huo hali inayosababisha ongezeko la watoto yatima 'hatujakata tamaa kwani bado tunaendelea kutoa elimu hiyo kwa waamini wote,” alisema Bw. Lutego.