Padre awataka waamini wasikubali kuendeshwa kama madori, maroboti

Na Getrude Madembwe, Iringa

WAAMINI wa madhehebu mbalimbali ya kidini nchini wametakiwa kuacha kuendeshwa kama madori au maroboti na badala yake wamehimizwa kutafakari kwa makini yale wanayoambiwa na viongozi wao likiwemo suala la kuacha kuamini matumizi ya kondomu kama kinga ya UKIMWI.

Hayo yalisemwa na Padre Paul Msombe wakati akifungua semina ya Kitengo cha Maendeleo ya Akinamama (WID), Vikaria ya Konsolata Jimbo Katoliki la Iringa, iliyomalizika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Parokia ya Ipogolo jimboni humo.

Padre Msombe ambaye ni Paroko wa Parokia ya Ipogolo, alisema kuwa jamii haina budi kujihadhari na ugonjwa wa UKIMWI, hivyo isikubali mafundisho yoyote potofu.

“Ni lazima uutawale mwili wako na wala siyo kukubali kila kitu mnachoambiwa kuwa ili kujikinga na ugonjwa huo kwamba tumia kitu fulani hiyo siyo kweli; kamwe tusikubali kuendeshwa kama maroboti au madori” alisisitiza Padre Msombe.

Aliongeza,  Tusiwe waoga kufanya mabadiliko kwamba utaonekana unapitwa na wakati tufanye mabadiliko sahihi na siyo batili”.

Alisema kuwa njia pekee ya kudhibiti ugonjwa huo usiendelee kuenea,ni kuacha zinaa na wanandoa kuwa waaminifu kwa asilimia 100 kwa wenzi wao.

Aidha padre Msombe aliwataka washiriki wa semina hiyo kuwa na sifa ambazo zinamfanya binadamu aonekane ni mtu.

“Tumekuwa tukiwasikia wazee wetu wakisema aah! Yule siyo mtu sababu matendo anayoyafanya yanafanana na mnyama wakati ni binadamu”.

Pia alisema kuwa unyang’anywaji wa mali kwa wajane na yatima, unyanyasaji kwa akinamama na hata ubakaji kwa watoto wadogo unaosababishwa na baadhi ya watu kwa ajili ya kuwa matajiri au uendeshaji wa biashara zao, ni baadhi ya vitendo vinavyomuonesha kuwa binadamu huyo ni sawa na mnyama.

Naye Mkurugenzi wa CARITAS Jimbo la Iringa,Padre Gasper Makombe amekemea baadhi ya akina baba ambao wana mitala (nyumba ndogo) kwani zinachangia ongezeko la ugonjwa wa UKIMWI.

“Utakuta mtu ana mkewe wa ndoa lakini bado huko nje ana mitala kibao sasa hapo UKIMWI utakwisha au…”alisema.

 Aliwataka wazazi kuwalea watoto wote kwa misingi imara na wala wasibaguliwe kwa kuwagawia kazi kwamba huyu ni wa kiume hatakiwa kufanya hivi au hizo ni kazi za mtoto wa kike.

Pia, aliwataka wanandoa kuandika wosia ili kuondoa usumbufu au familia yake kuteseka iwapo mwanaume au wazazi wote wawili wakifariki.

“Muwe na utaratibu wa kuandika wosia angalau kila baada ya  miaka mitatu nikiwa na maana kwamba kama utaandika wosia mwaka huu  na mwaka 2005 bado utakuwa hai badilisha au ongezea vitu ambavyo umevipata katika miaka hiyo na utaondoa usumbufu ukifa maana kuna ndugu wengine wakiona ndugu  yao kafa huanza kukimbilia mali” aliasa.

Mmoja wa wakufunzi wa semina hiyo Paskalina Chavaligino aliwataka wanasemina hao kuzingatia yale yote waliyojifunza katika semina hiyo na wala wasiyapuuzie.

“Mpo katika vita vya ugonjwa huu hatari sasa yale mliyojifunza hapa  msiyapuuzie na mkawafundishe wengine ni jinsi gani wanapaswa kuishi katika mienendo inayompendeza Bwana.

Mratibu wa Maendeleo ya Akinamama na Watoto Jimboni Iringa,Sista Sabina Witness alisema semina hiyo ina lengo la kuelimisha watu juu ya UKIMWI, jinsia na maendeleo.

Alisema semina kama hiyo imekwisha tolewa hata katika Vikaria tatu za jimbo hilo ambazo alizitaja kuwa ni Tosamaganga, Kilolo na Mafinga

‘Viongozi wa dini inusuruni jamii isizidi kuangamia’

    Na Reginald Barhe, Morogoro

UJAMBAZI, unyanyasaji wa kijinsia na maradhi yasiyopona ukiwemo UKIMWI ni matokeo ya jamii kufilisika kimaadili, hivyo viongozi wa dini wanao wajibu kuongeza nguzu katika kubuni mbinu za kuinusuru jamii isiendelee kuangamia.

Rai hiyo hiyo ilitolewa hivi karibuni na Kiongozi wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Upadre kwa mapadre 54 wa shirika hilo.

Katika sherehe hizo zilizofanyika jimboni Morogoro, Padre Bozeli alisema kuwa jamii inazidi kumomonyoka katika maadili ya kidini na kijamii na kwamba hali hiyo  inawadai viongozi wa dini kuongeza juhudi na kuboresha mafundisho yao kwa jamii ili kukidhi mahitaji yaliyopo kiroho.

Alisema, bila viongozi hao wa kiroho kuwa macho zaidi na kuchukua juhudi za makusudi, ipo hatari taifa na jamii kwa jumla, likazidi kuangamia.

Mbali na hayo, Kiongozi huyo aliwapongeza mapadre walioadhimisha Jubilei hiyo ya miaka 25 tangu wapate Daraja ya Upadre

Vile vile, aliwasisitiza mapadre hao kutumia vipaji walivyo navyo kwa manufaa ya jamii nzima.

Alivitaja vipaji hivyo kuwa ni pamoja na taaluma ya muziki, uandishi na uongozi bora.

Masista wahimizwa kuzingatia misingi ya nadhiri zao

Na Pd. Japhet Mwaya, Mtwara

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Mtwara, Mhashamu Gabriel Mmole, amewahimiza masista kuzingatia misingi ya maisha yao ya kitawa popote wanapokuwa.

Mhashamu Mmole alitoa wito huo hivi karibuni wakati akizungumza katika Maadhimisho ya Misa Takatifu ya kufunga nadhiri  kwa masista sita wa Shirika la Mkombozi. Maadhimisho hayo yalifanyika Oktoba 15, mwaka huu jimboni Mtwara.

Masista walioweka nadhiri siku  hiyo ni Agatha Nyenyembe, Brigitta Lilai, Aloisia Mapua, Agnella Mnyambe, Norberta Chilumba na Prisca Akalima.

Askofu Mmole aliitaja misingi ya maisha hayo kuwa ni usafi wa moyo, utii na ufukara.

Alisema usafi wa moyo utawasaidia masista hao kumfuata Yesu Kristo kwa moyo usiogawanyika.

Aliwahimiza daima waishi kwa kuiga mfano wa maisha ya Bikira Maria.

Akizungumzia utii, Mhashamu Mmole alisema kuwa, masista hawana budi kuwa watii kwa Mungu na kwa wakubwa wao kama Yesu alivyo kuwa mtii hadi akafa msalabani.

“Daima zingatieni utii hata kama mtajaliwa vyeo vya namna gani,” alisema.

Alisema masista wakiwa watu walioitwa na Mungu na wakajitolea kulitumikia Kanisa, hawana budi kuishi maisha ya ufukara kama alivyofanya Yesu hata kuzaliwa katika familia ya kifukara na akaishi kiufukara hadi kifo chake.

Alisema endapo watakuwa tayari kuishi ufukara hapa duniani, basi watarajie kuishi maisha ya utajiri wa utukufu watakapokuwa mbinguni.

Alisema kuzingatia misingi ya maisha ya Kitawa, ni mojawapo ya njia za kutekeleza dhamira ya AMECEA ambayo ni UINJILISHAJI WA KINA KATIKA MILENIA YA TATU: CHANGAMOTO KWA AMECEA.

AMECEA ni Umoja na Ushirikiano wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Nchi za Mashariki mwa Afrika.

Nchi hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan, Malawi, Ethiopia, Eritrea, na Zambia.

Mkutano wa AMECEA 2002, ulifanyika nchini Julai 14 hadi 28, mwaka huu.

Aidha, Mhashamu Mmole aliwashukuru Masista wa Shirika la Mkombozi kwa huduma zao bora katika Jimbo Katoliki la Mtwara.

Shirika hilo lilianzishwa Ujerumani, mwaka 1849. Mwanzilishi wake ni Elizabeth Eppnger (Sista Alfonsa Maria).

Makao Makuu ya Shirika yapo Ujerumani. Mama Mkubwa wa tawi la Afrika ni Sista Bertwalda Emmerling.

Utume wa Masista hawa ni kueneza upendo wa Mkombozi kwa watu wote hasa kwa njia ya huduma za afya na elimu kwa jamii.

Yatima, watoto wa mitaani mbioni kurejeshwa makwao

Na Brown Sunza

KITUO cha Kulelea watoto wa mitaani na yatima, cha Tuamoyo kilichopo katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, kipo katika maandalizi ya kuwarudisha nyumbani baadhi ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho.

Kwa mujibu wa Mratibu Mkuu wa Kituo hicho, Bw. Bujari Bujari, hivi sasa kituo hicho kinafanya kazi ya kuielimisha jamii kukubali kuwapokea watoto hao na namna ya kuwalea.

 Kwanza kabisa jamii husika inapaswa kuwajibika katika kuwapokea watoto hao wa mitaani na yatima waliokimbia katika familia yao kwa sababu zao maalumu hata kama wana uduni wa maisha,’ alisema.

Bw. Bujari alisema kuwa kutekelezeka kwa mpango huo kutafanikiwa kwa ushirikiano wa karibu baina ya Kituo hicho na Serikali.

“Ushirikiano wa namna hii utasaidia kupunguza idadi ya watoto wa mitaani na yatima katika vituo mbalimbali na hii itasaidi kuboresha huduma ya jamii katika maeneo ya vijijini,” alisema.

Alisema kuwa matokeo ya watoto hao kukimbia katika familia zao, ni kujikuta wakijihusisha na makundi ya udanganyifu yakiwemo ya uharifu pamoja na matumizi ya dawa za kulevya ambazo huwaathiri kiafya na wengine kujiingiza kwenye vitendo vya uasherati jambo ambalo matokeo yake ni UKIMWI.

Alitaja moja ya sababu zinazo changia wimbi la watoto wa mitaani, kuwa ni kuvurugika kwa ndoa baina ya baba na mama ambapo watoto hukimbilia mitaani kwa ajili ya kupata faraja.

“Ndoa nyingi katika jamii zinaonekana kulegalega, ugomvi ndani ya familia, unyanyasaji wa watoto yatima, ukatili wa kuwachoma mikono badala ya kuwaelimisha, pamoja na ukeketaji wa wasichana, pamoja na ndoa za lazima kwa wasichana ni sababu zinazowafanya watoto wengi wakimbie nyumbani" Alisema.