Make your own free website on Tripod.com

Wafadhili gaweni vitabu kama mnatupenda sio kondomu - Kanisa Katoliki

Na Innocent Ndwewe,RCJ.

KANISA Katoliki nchini limewataka wafadhili wa mashirika na asasi mbalimbali zinazo jishughulisha na ugawaji wa kondomu nchini, kuacha shughuli hiyo na badala yake yajihusishe na ugawaji wa vitabu vitakavyo saidai kuboresha maendeleo ya watu kiroho na kimwili kama kweli wanawatakia mema Watanzania.

Kauli hiyo ilitolewa Jumapili iliyopita na Padre Christopher Luoga wa Parokia Katoliki ya Mwenge, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, wakati alipokuwa akihubiri Injili katika Misa Takatifu iliyofanyika kanisani hapo.

Alisema kugawa kondomu kwa makundi haya ni sawa na kuwambia wananchi kwamba sasa wasifikirie suala lolote la maendeleo la badala yake wawazie tu suala la ngono, jambo ambalo ni hatari kwani linachangia kasi ya maambukizi ya ugonjwa hatari wa UKIMWI.

"Wasigawe kondomu na badala yake watumie nafasi yao kuleta kontena la vitabu ambavyo vitasaidia taifa kupata maendeleo," alisema.

Aidha, Padre Luoga aliwataka wale ambao hawajaolewa ama kuoa kubaki kama walivyo huku wakizingatia kuwa, tendo hilo linaruhusiwa kwa watu walio oana na wanaishi katika maisha safi ya ndoa pekee.

"Tendo la ndoa linaruhusiwa kufanywa na watu waliofunga ndoa tu, ndio maana Kanisa linapinga ugawaji wa kondomu kwa vijana na watoto, kwani ni tofauti na maadili ya Kanisa," alisema.

Alisema kuwa, anashangazwa na kusikitishwa kuona wanandoa wanaangamia kwa kutokuwa waaminifu katika ndoa zao.

"Huko ni kujilegeza. Ili kumshinda shetani wa ngono kwenye mwili wako, usijilegeze na usitegemee mipira hiyo (kondomu),"alisema.

Alisema, "Japokuwa tupo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambalo linaongoza kwa umaskini ni vizuri kujikomboa kwa kutumia miili yetu katika maendeleo kama Yesu alivyotumia mwili wake katika kutukomboa sisi wanadamu.

LICHA YA KUWA WATAALAMU WA MAMBO MBALIMBALI

Wasomi wabainika kutolipa nafasi suala la imani

l Utandawazi wasababisha kuingizwa dini zisizo eleweka

Na Dalphina Rubyema

LICHA ya kuwa wataalamu wa mambo mbalimbali, wahitimu katika Vyuo Vikuu wameelezwa kuwa ni miongoni mwa kundi la watu ambao hawalipi kipaumbele suala la imani katika nafsi zao.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa Idara ya Katekesi katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Telesphor Mkude wakati wa mkutano wa Katekesi ulio wakutanisha walimu Wakatoliki wanaofundisha somo la dini katika Shule za Msingi,Sekondari na Vyuo mbalimbali nchini pamoja na Wakurugenzi wa Katekesi majimboni.

Katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa TEC, Mhashamu Mkude alisema kuwa kutokana na sababu kama hizo za kutolipa kupaumbele suala la imani,thamani ya ubinadamu imekuwa ikipuuzwa ambapo watu wanafanya vituko visivyo elezeka.

"Kwa kweli suala la imani baadhi ya watu wamekuwa hawalipi kipaumbele, hata wasomi waliomaliza Chuo Kikuu,waulize mambo ya imani,ni kwamba wanafahamu kidogo sana" alisema Mhashamu Mkude.

Mhashamu Mkude ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro,alisema tatizo hilo la watu kutozielewa imani zao ipasavyo,ni moja ya sababu zinazo changia matatizo mengi duniani mojapo likiwa ni lile la mapigano ya kidini.

Aliwataka washiriki wa mkutano huo kufanya ipasavyo kazi ya kueneza neno la Mungu.

Wakati huo huo; imeelezwa kuwa suala la utandawazi limesababisha kuingia kwa dini za ajabu na michezo mbalimbali inayopotosha maadili nchini.

Akitoa mada juu ya Utandawazi katika mkutano huo wa Katekesi,Mwenyekiti wa Idara ya Fedha TEC,Mhashamu Methodi Kilaini alisema kuwa hali hii inasababishwa na uingiaji wa tamaduni za kigeni zinazotokana na suala hili la utandawazi.

"Vidini vingi vya ajabu vinakuja kwa ghafla. Si hiyo tu hata tunaingiliwa na tamaduni za wengine,ukifungulia TV unakuta michezo ya Marekani na kwa upande wa Afrika unakuta ile ya Afrika ya Kusini. Tena afadhali sasa unaweza kukuta angalau mchezo wa Zembwera" alisema Mhashamu Kilaini ambaye pia ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Tume yawataka Wamoravian kutaja watumiao dawa za kulevya

Na Lilian Timbuka

TUME ya Kudhibiti na Kuratibu Dawa za Kulevya Nchini, imewashauri waamini wa Kanisa la Moravian Tanzania (KMT) na Watanzania kwa jumla, kuwafichua wazalishaji, wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya nchini ili kuokoa maisha ya Watanzania ambayo yako hatarini kuangamizwa.

Kamishna wa Tume hiyo, George Timbuka, alitoa wito huo Jumapili iliyopia, alipopewa nafasi ya kuzungumzia madhara ya matumizi ya dawa za kulevya nchini na namna ya kupambana nayo katika Kanisa la Moravian Tanzania (KMT), Ushirika wa Kariakoo, Wilaya ya Mashariki, Jimbo la Kusini.

Alisema matumizi ya dawa hizo yanachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la vitendo vya uhalifu katika jamii ikiwa ni pamoja na wizi, ujambazi, ubakaji na mauaji.

Aliwahimiza viongozi wa makanisa na misikiti kuungana katika vita dhidi ya dawa hizo kwa kuwahamasisha waamini wao kuungana katika kuzipiga vita dawa hizi. Alisema moja ya silaha imara katika kupambana na vita dhidi ya uzalishaji, biashara na matumizi ya dawa za kulevya katika jamii, ni kumuweka Mungu mbele.

Alisema inasikitisha kwani awali Tanzania ilikuwa ikipambana na dawa hizi ikidaiwa kutumika kama kituo cha kupitisha dawa hizo, lakini hivi sasa, hali ni mbaya ka kuwa Tanzania imegeuka na kuwa kituo cha watumiaji na wazalishaji wa dawa hizo haramu na hatari kwa maisha ya watu.

Aliwaomba wote wenye mapenzi mema nchini, kushirikiana katika kutoa taarifa za uingizwaji, utengenezwaji, uuzwaji na utumiaji wa dawa hizo haramu ili kukiokoa kizazi kinachoendelea kuteketea.

Aidha, aliwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao na kuwashauri mara kwa mara ili watende yaliyo mema na yanayompendeza Mungu.

Hata hivyo, alisema malezi ya vijana yasiachwe mikononi mwa wazazi pekee, bali wajue kuwa kazi hiyo ni jukumu la jamii nzima.

Makamba awataka viongozi wa dini wasihukumiane

l Ayashauri makanisa kuweka maduka kujiongezea kipato

Na Jenifa Benedicto

MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam, Luteni Yusuph Makamba, amewataka viongozi wa dini mbalimbali nchini kuheshimiana katika dini zao na kushirikiana kuipiga vita tabia ya kuhukumiana kwamba dini moja ni nzuri kuliko nyingine.

Mkuu huyo wa Mkoa alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa chakula cha mchana kilichoandaliwa na Kanisa la Evangelist Assemblies of God, Temeke, kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Ustawi wa Jamii na pesa za kununulia gari la kwaya ya kanisa hilo.

Aliendelea kusema asiwepo mtu wa kuhukumu kuwa dini ya mwengine haifai na yake ndiyo nzuri kwani kazi ya kuhukumu ni ya Mungu pekee.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema ili kuwa na amani nchini ni lazima viongozi wa dini zote wavumiliane kwa kila hali.

"Watu wengine hutumia kengele na wengine hadhana katika kuwaita watu wao katika ibada, hivyo inabidi kuvumiliana na asiwepo mtu wa kumuona mwenzake kuwa anapiga kelele," alisema Makamba.

Aliongeza kuwa, kama kutakuwa na kiongozi wa dini ambaye atasababisha kutokuelewana baina ya dini na dini, yeye kama Mkuu wa Mkoa yuko tayari kuingilia kati suala hilo.

Mbali na Luteni Makamba, wageni wengine walio shiriki hafla ya chakula hicho iliyofanyika ndani ya ukumbi wa J.K.T Mgulani ni Mbunge wa Temeke,Bi. Khadija Kusaga, Naibu Waziri wa Elimu na Utamaduni,Bw. Bujiku Sakila, Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Kapteni Seif Mpembenwe na baadhi ya viongozi wa kanisa hilo.

Hata hivyo, kutokana na kutofikia lengo, Luteni Makamba aliliambia kanisa hilo liandae chakula kingine cha mchana na yeye atakuwa msimamizi wa maandalizi hayo.

Katika chakula hicho, shilingi milioni 60 zilihitajika kukidhi mahitaji.

Pia, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es Salaam amewashauri viongozi wa makanisa, kujenga maduka pembeni mwa makanisa yao ili kuongezea kipato kitakacho wasaidia katika shughuli za kikanisa.

Msifikiri UKIMWI ni kwa watu wa mjini pekee - Askofu

l Sheikh asema umekwisha kuwa lahaula!

Na Mwandishi Wetu

Baadhi ya Watanzania bado hawajauelewa vizuri ugonjwa wa UKIMWI na wanaamini kuwa unawaathiri wakazi wa mjini pekee, imeelezwa.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Mhashamu Jacob Koda alipokuwa akichangia mada wakati wa Kongamano la Viongozi Wakuu wa dini juu ya UKIMWI lililofanyika hivi karibuni katika Hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam.

Mhashamu Koda ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Same alisema katika kutatua tatizo hilo, ipo haja ya viongozi wa dini kukutana katika mazingira yanayo wazunguka ili kuwaelimisha baadhi ya watu wenye dhana hiyo kwamba UKIMWI ni ugonjwa wa watu wanaoishi mjini.

Akitoa mfano wa jimbo lake alisema,"Katika eneo ninalo fanyia kazi mimi bado watu hawajaelewa UKIMWI. Ukiwauliza wanakuambia ni wa watu wanaoishi mjini,hii ni kutokana na sababu kwamba wanaona ndugu zao wanatolewa mjini baada ya kuumwa".

Alishauri Wizara ya Elimu kuzingatia wajibu wake wa kuwafundisha watu namna ya kulea dhamiri zao badala ya kuwafundisha masuala ya masomo tu.

Wakati huo huo;Katibu Mkuu wa Mufti Tanzania,Sheikh Suleiman Gorogosi ameuita ugonjwa wa UKIMWI kuwa tayari umeisha kuwa lahaula akimaanisha suala la ushirikishwaji wa viongozi wa dini katika suala la kupambana nao, limechelewa.

Tamko la Katibu Mkuu huyo alililolitoa wakati wa kongamano hilo,lilikuja kufuatia Mwenyekiti wa Kongamano hilo ,Rais Mstaafu Alhaji Alli Hassan Mwinyi, kuwaambia viongozi hao kuwa waufananishe UKIMWI kama ugonjwa wowote ulioingia ghafla na sasa wanatafuta mbinu za haraka za kupambana nao.

Kufuatia kauli hiyo ya Mwinyi,Sheikh Gorogosi alipinga kauli hiyo kuwa UKIMWi ni ugonjwa wa muda mrefu na sasa umeisha kuwa lahaula akimanisha kuwa mipango ya haraka ya kuudhibiti tayari imeisha haribika.

"Sisi Waislamu mkitusikia misikitini tunasema lahaula,ina maana jambo limeisha haribika tayari. Sasa hata huu UKIMWI tayari umeisha kuwa lahaula!"alisema.

Aliishauri Serikali kutafuta ushauri wa viongozi wa dini mapema pindi jambo linapotokea badala ya kusubiri jambo hilo liharibike hatimaye ndio eti wawashirikishe.

"Viongozi wa dini tuitwe mapema siyo kuacha jambo limeharibika ndiyo mtuite. Sasa leo hii mnatuita tutoe mchango wetu juu ya UKIMWI wakati UKIMWI mwenyewe umeisha kuwa lahaula", alisema kauli hiyo iliyofanya washiriki wa kongamano kuvunja mbavu kwa vicheko licha ya kwamba jambo lililokuwa likiongelewa lilikuwa la kusikitisha.

Parokia yazindua Wiki ya Imani

Na Adolph Mbata, RCJ

KATIKA kuwarudisha kundini kondoo waliopotea, Kanisa Katoliki Parokia ya Makuburi, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, imezindua Wiki ya Imani ambapo semina mbalimbali zinatolewa sambamba na wataalamu mbalimbali wa imani kufanya tafsiri fasaha ya Biblia Takatifu.

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi kanisani hapo hivi karibuni,Mwenyekiti wa Balaza la Walei parokiani hapo Bw. Massawe alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya uongozi kubaini kuwa baadhi ya waamini wa parokia hiyo wamekuwa na tabia ya kukimbilia kusali katika makanisa mengine huku wakidhania kuwa huko kuna Mungu mwingine zaidi.

Alisema Wiki hiyo ya Imani ambayo imetolewa wakati wa kipindi hiki cha Kwaresima, imeafikiwa ifanyike nyakati za jioni ili kuwapa watu wa ofisini nafasi ya kushiriki ipasavyo.

Alisema, "Unajua kuna baadhi ya waamini ambao japokuwa kweli wamebatizwa lakini tayari wameisha potoka,wanaenda kusali kwenye makanisa mengine tofauti na Kanisa Katoliki ambapo eti huoneshwa ishara na miujiza; inasikitisha sana" .

Aliendelea kusema kuwa waamini hao kwa kufuata mafundisho ya makanisa mengine, hujikuta tayari wamesahau mafundisho ya Kanisa Katoliki.

"Mnapo ombewa kwenye hayo makanisa yanayojiita ya uponyaji, mnakuwa mumetekwa kisaikolojia na kujiona kuwa mumepona lakini baada ya muda mnaendelea ama mtaendelea kuumwa" alisema Mwenyeketi huyo wa Halmashauri ya Walei.

Aliwaomba waamini wote na wale wenye mapenzi mema kuhudhuria wiki ya Imani ili wajionee jinsi Biblia Takatifu inavyo fasiriwa na mapadre amabo siyo wababaishaji wa Maandiko Matakatifu bali wanasoma Neno hilo kwa uangalifu na umakini.

Wiki ya Imani parokiani hapo ilizinduliwa Jumapili ya nne ya Kwaresima na itamalizika Machi 24 mwaka huu.

Utandawazi wailiza YCS

Na Mwandishi Wetu

VIJANA Wakatoliki katika shule za Sekondari na Vyuo nchini, (TYCS) wametoa ujumbe wa Pasaka kwa wanachama wote wa TYCS wa kuwataka kuwa makini dhidi ya utandawazi kwa vile unaua tunu njema walizonazo.

Katika ujumbe huo vijana wanakumbushwa kuwa madhumuni makuu ya YCS ni kumleta Kristo katika mazingira yao na kwamba wanapaswa kufahamu vizuri mazingira waliyomo ili kazi zao ziwe na ufanisi mkubwa.

"Wapendwa katika Kristo, Kamati ya Taifa inatukumbusha madhumuni yetu makuu kama wana YCS, ambayo ni kumleta Kristo katika mazingira yetu. Sisi sote tunapaswa kuyafahamu mazingira tuliyomo ili kazi yetu hiyo iwe na ufanisi mkubwa,"inasema sehemu ya ujumbe huo.

Hata hivyo ujumbe huo umewataka vijana kutambua kuwa pamoja na kuwepo kwa mfumo huo wa utandawazi, hautakuwa na madhara iwapo watauchukulia kwa upande mwingine kama changamoto kwao.

"Tuuchukulie ni sehemu ya kujifunza ili tutumie vitu, rasilimali zilizopo kwenye mfumo huu kama njia ya kujielimisha." unasema ujumbe huo.

Katika ujumbe huo, vile vile vijana wametakiwa kukumbuka bahati ya kusoma waliyoipata wakati vijana wengi wapo wanaoitamani nafasi hiyo na wameikosa.

"Yatupasa tuitumie nafasi hii vema ili tupate kuwa viongozi wa taifa hili," inasema sehemu ya ujumbe huo.

Aidha risala hiyo ilisisitiza umuhimu wa sala na Neno la Mungu katika maisha yao katika kutakatifuza malimwengu.

Pia risala inawataka vijana wauombee Mkutano wa AMECEA utakaofanyika Kurasini Dar es Salaam Julai 14-28, 2002 ili yatokanayo na mkutano yawe kwa ujenzi wa Taifa la Mungu, uimarishaji wa Utume wa Walei katika maisha ya Jumuia Ndogo Ndogo za Kikristo.

Wakirejea ujumbe wa Papa kwa Vijana ulimwenguni unaotarajiwa kusomwa Jumapili ya Matawi;Ijumbe uliwataka vijana kutumia karama zao ili kuwa chumvi na mwanga na vijana wenzao.

Mwaibula awataka wamiliki wa magari kupeleka huduma Kigamboni

l Awataka wananchi kuwaadhibu madereva, makondakta wasiokuwa na nidhamu

Na Anthony Ngonyani

MWENYEKITI wa Mamlaka ya Leseni Mkoani Dar es Salaam, Bw. David Mwaibula, amewataka wamiliki wa magari ya usafirishaji kupeleka magari yao Kigamboni ili kuimarisha utoaji wa huduma ya usafiri katika eneo hilo.

Mwaibula aliyasema hayo hivi karibuni wakati alipokuwa akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake.

Alisema kama ilivyo sera ya Mammlaka hiyo kuwa ni kuimarisha huduma ya usafirishaji kwa kutoa maamuzi ya ubunifu wa kutatua matatizo kisayansi, hivyo wamiliki wa magari makubwa (DCM) hawana budi kupeleka huko huduma ili kuwapunguzia adha wakazi wa eneo hilo ambao wamekuwa wakisumbuka kutokana na kuwa na usafiri usioeleweka.

Bw.Mwaibula alisema kuwa eneo hilo la Kigamboni lina wakazi wengi ambao wanahitaji kutumia usafiri unao ridhisha na ofisi yake tayari imekwisha anza kuto vibali kwa wamiliki wanaopenda njia (ruti) za huko.

Aidha Mwaibula pia amewataka wananchi kushirikiana kikamilifu katika kuwadhibiti madereva na makondakta wenye lugha za matusi.

"Wananchi washirikiane kuwadhibiti madereva na makondakta wasio na nidhamu kwani biashara ya mabasi ni sawa na biashara nyingine na wawe na heshima kama watu wengine wanavyo ziheshimu ofisi zao" alisema Bw.Mwaibula.

Nina hamu ya kuendelea kufanya kazi shambani kwa Bwana - Askofu Kilaini

l Aadhimisha miaka 30 ya Daraja ya Upadre

Na Anthony Ngonyani

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,Mhashamu Method Kilaini amesema kuwa bado ana hamu ya kuendelea kufanya kazi katika shamba la Bwana.

Mhashamu Kilaini alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na gazeti hili nyumbani kwake Msasani katikati juma,muda mfupi baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu ya kutimiza miaka 30 tangu apate daraja ya upadre.

Alisema pamoja na kufanya kazi katika shamba la Bwana kwa muda wa miaka 30 sasa,bado anaona ni muda mfupi sana hivyo bado anahamu kubwa ya kuendelea kufanya kazi katika shamba hilo.

Alisema sababu kubwa ambayo inampelekea kuwa na hamu ya kuendelea kufanya kazi katika shamba hilo ni kutokana na ushirikiano uliopo kati yake na watumishi wengine wa Mungu.

Aliongeza kusema kuwa njia muafaka ya kuimarisha na kujenga kanisa ni kuwa na ushirikiano kwani ni kinga ya mitafaruku.

Askofu Kilaini alisema katika kipindi chote cha utumishi kwa Mungu hakupata matatizo ambayo ameweza kuweka katika kumbukumbu ya utumishi wake.

"Kipindi chote nimekuwa nikifanya kazi bila ya matatizo na kama yapo basi ni madogo madogo ambayo nimekuwa nikiweza kuyamaliza kwa wakati muhafaka"alisema .

Akitaja moja ya matatizo hayo madogo,Mhashamu Kilaini alisema kipindi cha mwanzo wa utumishi wake alikuwa anatumia baikeli katika kutoa huduma kwa wananchi.

Lakini alisema aliweza kushinda na kufanikiwa kwa sababu alikuwa ni kijana na aliweza kufika sehemu mbalimbali kutoa huduma za kiroho.

Mhashamu Method Kilaini alipata daraja ya upadre Machi 18,1972 nchini Roma na Machi 18 alisimikwa kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Kanisa Katoliki nchini lashauriwa kuongeza seminari ndogo majimboni

Na Lazaro Blassius,Tanga

BALOZI wa Vatican nchini, Askofu Mkuu Luigi Pezzuto amelishauri Kanisa Katoliki nchini kuongeza idadi ya seminari ndogo majimboni.

Mhashamu Pezzuto alitoa ushauri huo katikati ya juma lililopita wakati wa Misa Takatifu katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Fedha kwa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Yosefu iliyopo katika Jimbo Katoliki la Tanga.

Alisema licha seminari hizo kuwalea vizuri vijana wenye wito wa upadre ambalo ndilo lengo kuu la Kanisa, pia seminari ndogo zimechangia kuwalea vema kimaadili hata vijana wanaoshindwa kufikia lengo hilo.

Akizungumza juu ya umuhimu wa seminari hizo, Mhashamu Pezutto alisema kuwa, hata baadhi ya viongozi wa Serikali ambao wamepitia kwenye seminari kama hizo, wamekuwa waaminifu na waadilifu kwa jamii.

Askofu Mkuu Pezzuto amezitaka jumuiya mbalimbali za kanisa kuwatia moyo vijana wanapoitwa na Mungu katika wito Mtakatifu na kuwaandalia mazingira mazuri yasiyokatisha tamaa.

Askofu Mkuu huyo ambaye alikuwa anahitimisha ziara yake ya kichungaji ya siku 10 jimboni Tanga,vile vile amewataka vijana wanaosoma seminarini kuonesha utii kwa moyo na kutafakari ukarimu wa Mungu kwao.

Katika ziara yake hiyo jimboni Tanga, Askofu Mkuu Pezuto alitembelea maeneo mbalimbali.

Wakazi wa Dar kaeni chonjo kipindupindu chaja

Na Brown Sunza, DSJ

HUENDA kukatokea tena mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika eneo la jiji la Dar es Salaam endapo wakazi wa eneo hilo watakuwa makini kuzingatia kanuni za usafi hasa katika kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia hali ya uchafu katika maeneo mbalimbali ya jijiji huku watoto wakiwa wanachezea maji machafu kwenye baadhi ya maeneo hayo.

Katika eneo la Kigamboni wilayani Temeke,mwandishi alishuhudia maji machafu yakiwemo yanatiririka hovyo huku nzi wakizunguka makazi ya wakazi wa eneo hilo.

Hata hivyo, hali ya usafi katika sehemu ya feri ambapo wakazi wengi wa jijini Dar es Salaam hujipatia samaki kwa ajili ya kiteweo, siyo mbaya sana kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.

Shirika la masoko Kariakoo kukusanya milioni 770

Na Joseph Kiboga

KATIKA jitihada za kuimarisha na kuinua hali ya Shirika la Masoko Kariakoo, uongozi wa shirika hilo unatarajia kukusanya jumla ya shilingi 771, 668,046 katika kipindi cha mwaka 2001/2002, imefahamika.

Taarifa iliyotolewa kwa Mkuu wa Mkuu wa Dar es Salaam, Luteni Yusuph Makamba wakati alipotembelea soko hilo ambayo gazeti hili ina nakala yake zinazema kuwa kiwango hicho kitakuwa ni kikubwa ikilinganishwa na kile kilicho kusanywa mwaka uliopita.

Taarifa hiyo iliyosomwa na Meneja wa soko hilo Bw. Kuboja Ng’ungu imekitaja kiwango hicho kilichokusanywa mwaka jana kuwa ni shilingi 631,530,813.

Taarifa unachanganua baadhi ya matumizi ya fedha hiyo itakayokusanywa kuwa ni pamoja na kutengeneza maumbo yapatayo 175 kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo ambapo jumla ya shilingi milioni saba zinatarajiwa kutumika.

Vile vile kiasi cha shilingi milioni moja kinatarajiwa kutumika katika kusakafia na kujenga maturubai eneo la nasi na mchicha ambapo shilingi milioni sita zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kuchimba kisima chenye futi 100 ili kuliwezesha soko kuwa na maji ya kuaminika.

Katika mpango wa muda mrefu, taarifa hiyo inasema kuwa ili kuweza kujenga uwezo wa kutoa huduma zaidi, shirika katika kipindi cha miaka 5-10 linatarajia kujenga orofa moja juu ya soko dogo ili kupanua nafasi ya biashara.

"Nafasi 222 zinatarajiwa kupatikana na hivyo kuweza kuliingizia shirika kiasi cha shilingi 888,000 kila mwezi chini ya mpango wa ulipaji wa kodi ya shilingi 4,000 kwa ubao kila mtu kila mwezi" inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Shirika la Masoko Kariakoo kwa wastani hukusanya mapato ya shilingi milioni 59 kwa mwezi.

Wamoravian waja juu kujiletea maendeleo

l Baada ya harambee Kawe, sasa Kigamboni

Na Mwandishi Wetu

KANISA la Moravian Tanzania (KMT), Wilaya ya Mashariki, Jimbo la Kusini, limewapongeza waamini wake kwa juhudi zao za kujiletea maendeleo yao wenyewe bila kutegemea misaada toka kwa wafadhili.

Mwenyekiti wa KMT, wilayani humo, Mchungaji Eli Ambukege, alitoa pongezi hizo wakati akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake mwishoni mwa juma mintarafu njia zinazotumika kuleta maendeleo katika shirika mbalimbali za Wilaya yake.

Alisema siri ya mafanikio katika Kanisa hilo ni waamini wenyewe kujitambua kuwa wao ni familia moja katika Kristo na kwamba wana jukumu la kuungana pamoja katika kulitumikia Kanisa kwa hali na mali.

Mchungaji Ambukege alisema anaamini kuwa "harambee" ya kuchangia kukamilika kwa ujenzi wa jengo la kanisa katika Ushirika wa Kigamboni, na sherehe za kuwekwa wakfu kanisa hilo na nyumba ya mchungaji, itafanikiwa.

Mwandishi wa gazeti hili alipotaka kujua ni kwanini anaamini kuwa harambee hiyo itafanikiwa, Mchungaji Ambukege alisema, "Mshikamano ninaoufahamu katika ushirika huo (Kigamboni) baina ya viongozi na waamini na hata wa shirika nyingine, ndio unanifanya niamini kuwa watafanikiwa. Ni watu ambao wamejijenga katika umoja na kila mmoja anajiona anawajibika kwa Kanisa na analiona kuwa ni mali yake."

Jumapili hii waamini wa Ushirika wa Kigamboni wa KMT, Wilaya ya Mashariki, wanafanya harambee kuchangia ujenzi na uwekwaji wakfu wa kanisa na nyumba ya Mchungaji.

Jumapili iliyopita, waamini wa Ushirika wa Kawe walifanya harambee kama hiyo. Haikufahamika mara moja ni mchango kiasi gani ulipatikana.

Alitoa wito kwa waamini hao, shirika jirani na wote wenye mapenzi mema kuchangia kwa hali na mali harambee hiyo na shughuli nyingine za kuliendeleza Kanisa nchini badala ya kutegemea misaada toka mataifa ya nje.

Aliongeza kuwa, anaamini Wana-Kigamboni watafanya vizuri harmbee hiyo hasa ikizingatiwa kuwa mwanzo wa ujenzi huo takriban miaka mitatu na nusu iliyopita, walionesha moyo wa kujituma na wakafanikiwa.

"Kwa kiasi kikubwa washirika wa Kigamboni wenyewe ndio waliofanikisha ujenzi huo hadi hatua ya sasa ya kumalizia jengo. Ofisi kuu ya Jimbo (KMT- Jimbo la Kusini) na shirika nyingine za jirani na marafiki walichangia sehemu kidogo tu.

Sasa, hata hao marafiki wa madhehebu mengine walichangia kwa sababu waliona Kigamboni wenyewe kama wenyeji wamefanya kazi kubwa na hivyo ikawatia moyo na ujenzi huo umefanyika kwa kipindi kifupi ukilinganisha na idadi ya waamini," alisema.

Ushirika huo unao waamini hai takriban 120.

Alitoa wito kwa waamini wengine na Watanzania kwa jumla kuimarisha uhusiano mwema baina yao na kuongeza kuwa, juhudi katika kujiletea maendeleo ya Kanisa na nchi ni muhimu kuimarishwa kwani wakati wa kutegemea misaada umepita.

Alisema mshikamano hata kwa mke na mume katika familia, ndio chanzo cha maendeleo. "Kama mna mshikamano hata kama kipato chenu ni kidogo mtashangaa namna maendeleo yanavyowajia yenyewe.

Lazima kila Mkristo wa Tanzania ajue kuwa Kanisa la Tanzania lipo kwenye udongo wa Tanzania na kamwe halitahama liende Ulaya," alisema.

Akaongeza kuwa, anaamini mafanikio na umoja unaooneshwa na waamini wa ushirika wa Kigamboni, yatakuwa changamoto kwa shirika nyingine na Watanzania wote katika kujiletea maendeleo.