Baba Mtakatifu atuma barua kwa Rais Mkapa

Na Joseph Sabinus

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amemtumia barua sambamba na Ahadi za Asizi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa ili ahadi hizo ziamshe utendaji wa kijamii na kisiasa nchini Tanzania.

Barua ya Baba Mtakatifu kwa Rais Mkapa, ni miongoni mwa barua za namna hiyo alizozituma Baba Mtakatifu kwa wakuu wa nchi na Serikali mbalimbali duniani.

"Ninayo heshima kukuletea, Mheshimiwa, matini ya ahadi hizo za pamoja nikiamini kwamba ahadi hizo zitaamsha utendaji wa kijamii na kisiasa wa Serikali yako," inasema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Baba Mtakatifu mwenyewe Februari 24, mwaka huu.

Barua hiyo inaongeza, "...Natamani kwamba moyo huo na ahadi za Asizi ziwaongoze watu wote wenye mapenzi mema kufanya utafiti wa ukweli, wa haki, wa uhuru, wa mapendo ili wanadamu wote waweze kufurahia haki zao zisizoondolewa, na kila taifa, amani".

Katika barua hiyo kwa wakuu wa nchi na serikali, Baba Mtakatifu amesema, majadiliano hayo yaliyofanyika hivi karibuni wakati wa Siku ya Sala kwa ajili ya amani ya ulimwengu yaliyofanyika na kuhudhuriwa na kuwakilishwa na viongozi wa dini wa mataifa mbalimbali, yaliwaamsha wawakilishi wengi wa imani tofauti za dini, hamu ya dhati ya kufanya kazi kwa ajili ya mapatano, utafiti wa pamoja wa maendeleo ya kweli na amani moyoni mwa familia nzima ya wanadamu.

Alisema mafanikio ya majadiliano hayo yalikuwa ni pamoja na, udhihirisho wao ulioinuliwa kabisa na kuthibitishwa katika ahadi kumi (decalogue) zilizotamkwa mwishoni mwa siku ile ya pekee.

Ujumbe Kamili wa Baba Mtakatifu pamoja na Ahadi za Asizi,

Kwa Waheshimiwa

Wakuu wa Nchi au Serikali

Ni mwezi mmoja tu umepita tangu tulipokuwa na Siku ya Sala kwa ajili ya amani ya ulimwengu Assizi. Leo mara moja fikira zangu zinawaendea wale wenye dhamana ya maisha ya kijamii na kisiasa ya nchi zile zilizowakilishwa na viongozi wa dini wa mataifa mengi sana.

Majadiliano yaliwaamsha wake kwa waume wawakilishi wengi wa imani tofauti za dini, hivi hata hamu yao ya dhati ya kufanya kazi kwa ajili ya mapatano, utafiti wa pamoja wa maendeleo ya kweli na amani moyoni mwa familia nzima ya wanadamu, ilipata udhihirisho wao ulioinuliwa kabisa na kuthibitishwa katika ahadi kumi zilizotamkwa mwishoni mwa siku ile ya pekee.

Ninayo heshima kukuletea, Mheshimiwa, matini ya ahadi hizo za pamoja nikiamini kwamba ahadi hizo zitaamsha utendaji wa kijamii na kisiasa wa Serikali yako.

Niliweza kubaini kwamba washiriki katika mkutano wa Assizi, kuliko mara nyingine zote, walikuwa na imani moja: wanadamu hawana budi kuchagua kati ya upendo na chuki. Na wote wakijisikia kama wanafamilia moja ya mwanadamu, wamefasiri matamanio haya kwa njia ya ahadi wakisukumwa na imani kwamba chuki huangamiza, kinyume chake upendo hujenga.

Natamani kwamba moyo huo na ahadi za Assizi ziwaongoze watu wote wenye mapenzi mema kufanya utafiti wa ukweli, wa haki, wa uhuru, wa mapendo ili wanadamu wote waweze kufurahia haki zao zisizoondolewa, na kila taifa, amani.

Kwa upande wake, Kanisa Katoliki linaloweka tumaini lake katika "Mungu wa upendo na amani" ("2Kor 1: 11) litaendelea kujishughulisha mpaka mjadala wa dhati, kusameheana na mapatano ya pamoja yatie moyo njia ya wanadamu katika milenia hii ya tatu.

Nikiwa na hakika kwamba, Mheshimiwa, utaupa ujumbe wangu uzito unaostahili, ninachukua fursa hii kukuhakikishia heshima zangu za hali ya juu.

Kutoka Vatikano, 24 Februari, 2002

AHADI KUMI ZA ASIZI KWA AJILI YA AMANI

1. Tunaahidi kutangaza imani yetu thabiti kwamba utumiaji nguvu na ugaidi unapinga roho ya kweli ya kidini na kulaani njia yoyote ya kukimbilia utumiaji nguvu na vita katika jina la Mungu au la dini, tunaahidi kufanya kila linalowezekana kukomesha sababu zote za ugaidi.

2. Tunaahidi kuelimisha watu katika heshima na kuheshimiana ili kufikia kuishi pamoja kwa amani na kutegemeana miongoni mwa watu wa makabila, tamaduni na dini mbalimbali.

3. Tunaahidi kuendeleza utamaduni wa mazungumzo ili kuendeleza maelewano na matumaini ya kukubaliana kati ya watu mmoja mmoja na kati ya mataifa, kwani hayo ndiyo masharti ya amani ya kweli.

4. Tunaahidi kutetea haki za kibinadamu ili kuleta maisha sitahiki, kulingana na utambulisho wa utamaduni wao na uhuru wa kuunda familia.

5. Tunaahidi kufanya mazungumzo kwa unyofu na uvumilivu bila kujali yale yanayotutenga, kama ukuta usiopitika, bali kinyume chake, kukiri kwamba makabiliano na tofauti za wengine yanaweza kuwa fursa ya kufahamiana.

6. Tunaahidi kusameheana makosa yaliyopita na ya sasa, pamoja na hukumu mbovu, na kusaidia kwa nguvu ya pamoja kushinda ubinafsi na manung’uniko, chuki na utumiaji nguvu, na kujifunza kwa mambo yaliyopita kwamba amani bila haki si amani ya kweli.

7. Tunaahidi kuwa karibu na wale wanaoteswa kwa dhiki na upweke. Tutakuwa sauti ya wasiokuwa na sauti na kufanya kazi kwa dhati ili kushinda mazingira ya namna hiyo, tukiamini kwamba hakuna mtu anayeweza kuwa na furaha peke yake.

8. Tunaahidi kukifanya kilio cha wale wasiokubali utumiaji nguvu na uovu kiwe chetu, na tunatamani kuchangia nguvu zetu ili kuupa ubinadamu wa wakati wetu matumaini ya kweli ya haki na amani.

9. Tunaahidi kuhimiza kila jitihada inayostawisha urafiki kati ya mataifa tukiamini kwamba kama hukumu thabiti ikikosekana kati ya mataifa maendeleo ya kiteknolojia yatauanika ulimwengu katika hatari zinazoongezeka za maangamizi na kifo.

10. Tuaahidi kudai kutoka kwa viongozi wa mataifa kufanya jitihada zinazowezekana kitaifa au kimataifa, kwamba ulimwengu wa mshikamano na amani wenye msingi wake juu ya haki unajengwa na kuimarishwa.

Kanisa la Pentekoste lawaponda wachungaji wanaojali pesa kuliko kondoo

l Ataka wasiwe wachungaji wa mishahara

l Ataka waamini wasilazimishwe kutoa hata wasicho nacho

Na Lilian Timbuka

  BAADHI ya Wachungaji wamesahau wito wao na sasa wamebaki kuangalia idadi ya waamini waliopo makanisani mwao ili wapate pesa huku wakilitegemea Kanisa liwafanyie kitu badala ya kufanya kazi sawa na wito wao.

Hayo yalisemwa na Mchungaji Philemon Tibanenason wa Kanisa la Kipentekost Tanzania wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi yalipo makao Mkuu ya kanisa hilo Mgomeni jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.

Alisema wachungaji wazingatie wito wao walioshushiwa na Mungu kwa kutenda kazi yao ya kuchunga Kondoo wa Mungu na kuwarudisha kundini waliopotea.

Alisema wachungaji na watumishi wote wa Mungu hawapaswi kujiweka katika kundi la watumishi wa mishahara kwa kuwa wito wao hauwaruhusu kufanya hivyo.

Mchungaji huyo alizidi kufafanua kuwa hali ya baadhi ya watumishi wa Mungu kujiweka katika kundi la watumishi wa mishahara, limesababisha migogoro mingi makanisani baina ya waamini na viongozi a kiroho.

Alisema hali hiyo imechangia pia baadhi ya washiriki kutengwa kwa vile wameshindwa kutoa fungu la kumi ama kushirikiana na makanisa mengine.

Aliendelea kuwa, suala la viongozi kula madhabahuni haliwafanyi waamini kulazimishwa kutoa pesa hata kama hawana kwa vile ni wazi kuwa Neno la Mungu linamtaka kila mtu kutoa alicho nacho na ambacho roho yake ilimgusa kutoa.

"Mchungaji hukosa muda wa kuongea na Mungu kwa sababu amechanganya wito na huduma kwa lengo la kujipatia kipato hali inayochangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa maadili katika makanisa wanayoyaongoza" aliongeza.

"Kukosekana kwa wito wa kimungu ndani ya mioyo yetu, kumesababisha kukosekana kwa upendo na umoja ingawa tunajidai tunamtumikia Mungu wetu aliye hai. Tumekuwa kama viazi kwenye gunia vinavyokuwa pamoja lakini pindi tu vimwagwapo chini, kila kimoja hushika njia yake," alisema Mchungaji Tibanenason.

Alisema kuwa, wachungaji wote wanapaswa kuutumikia wito huo waliotunukiwa na Mungu kwani ndiyo thawabu itakayowafanya wauone ufalme wa mbinguni pindi siku zao za kuishi duniani zitakapokoma.

Mchungaji Menonite ataka wenye UKIMWI wawekwe kambini

Na Christopher Gamanya, Tarime

SERIKALI imeshauriwa kuanzisha kambi maalumu za kuwatunzia waathirika wa ugonjwa hatari wa UKIMWI ili kupunguza kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo katika jamii na kuwapunguzia waathirika manyanyaso wapatayo toka kwa baadhi ya ndugu zao.

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Mchungaji Chriss Kateti wa Kanisa la Menonite la mjini Tarime, wakati akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake katika Barabara ya Biafra mjini hapa.

Alisema kuwa wagonjwa wengi hurudishwa katika familia zao mara wanapoonekana kuzidiwa na ugonjwa huo katika sehemu mbalimbali wanakofanyia kazi hali ambayo husababisha hofu katika familia na kuwepo uwezekano wa kuambukiza wengine kutokana na kutokuwepo utaratibu mzuri wa kuwahudumia.

Mchungaji Kateti alisema kuwa, Serikali haina budi kukaa chini na kubuni mpango wa kujenga kambi maalumu kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa wa UKIMWI katika mikoa kadhaa nchini ili kila mwathirika wa ugonjwa huo aondolewe katika familia yake.

Alisema wagonjwa wa UKIMWI wakiwekwa kambini, itakuwa rahisi kwa Serikali, asasi mbalimbali na watu wenye mapenzi mema kuwahudumia kwa michango na misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupewa huduma zinazostahili chini ya ungalizi wa kitaalamu.

"Kwa kuwa hakuna anayefurahia kitendo cha kutengwa na familia yake, bila shaka utaratibu huo utawasaidia watu waogope kujihusisha na vitendo ambavyo huchangia maambukizi ya ugonjwa ukiwemo uzinzi na tohara za kienyeji," alisema Mchungaji Kateti.

Aidha, kiongozi huyo wa kiroho amewataka watu wote katika jamii kuisaidia Serikali katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Alizitaja baadhi ya njia muafaka katika vita hiyo kuwa ni pamoja na kupiga marufuku vitendo na mambo yanayochochea ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo kama vile kutazama picha chafu za ngono, kuhudhuria disko za usiku na ulevi.

Ametoa wito kwa watu wote, hususani, vijana wa jinsia zote kujenga utamaduni wa kupenda kufanya mazoezi ya mwili ikiwemo michezo ya mpira, kukimbia, kuimba na mingine.

Alisema michezo pamoja na kujishughulisha kwa kazi mbalimbali kikiwamo kilimo, kutasaidia kuepusha fikira na tamaa za mwili kufanya vitendo vya zinaa ambavyo ni njia kuu ya kueneza UKIMWI.

Waislamu, Wakristo waungana pamoja

l Waipinga serikali kuhusu kondomu

l TEC yashikilia tamko la miaka 15 iliyopita

Na Dalphina Rubyema

VIONGOZI wa dini ya Kiislamu na wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo, wameungana pamoja na kuendelea kushikilia msimamo wao wa kupinga matumizi ya kondomu kama njia ya kuzuia maambukizi ya UKIMWI.

Katika Kongamano la siku mbili la Viongozi Wakuu wa Dini kuhusu udhibiti wa UKIMWI, lililomalizikika mwishoni mwa juma katika Hoteli ya White Sands jijini Dar es Salaam, kwa kauli moja viongozi hao walisema kuwa kuruhusu matumizi ya kondonu ni kuruhusu jamii ifanye vitendo vinavyokwenda kinyume na Maandiko Matakatifu katika Kurani na Biblia.

Waliitaka Serikali na wanataaluma kupitia njia mbalimbali zinazofaa kupambana na kuudhibiti UKIMWI huku wakiwapa viongozi wa dini nafasi kwani wanayo nafasi ya kuzungumza na kueleweka mbele ya waamini wao.

Vile vile waliitaka Serikali na asasi mbalimbali kutoweka tena mada ya kondomu pindi watakapoitisha kongamano ama kitu kingine cha namna hiyo kitakachowahusisha wao kama viongozi wa dini.

Katibu Mkuu wa Shehe Mkuu wa Tanzania(Mufti), Sheikh Suleiman Gorogosi, alisema kuwaambia viongozi wa dini wahamasishe waamini wao juu ya matumizi ya kondomu ni sawa na kuwawekea viongozi hao kitanzi shingoni.

"Sisi leo hii turuhusu utumiaji wa kondomu! tutaonekanaje mbele ya waamini wetu na huku wanafahamu fika kwamba vitabu vitakatifu vinakataza?" Alihoji Sheikh Gorogosi.

Aliongeza, "Leo hii mtuwekee kitanzi eti tutamke rasmi kuhalalisha kondomu! hii haiwezekani".

Sheikh Gorogosi ambaye pia ni Shehe wa Mkoa wa Lindi, alisema kuwa Korani Tukufu inawakataza Waislamu kufanya zinaa maana ni uchafu wa kimwili na kiroho.

Licha ya kupinga matumizi ya kondomu, viongozi hao walisema kuwa hakuna maana sana kujenga mahekalu ya makanisa na misikiti huku baadhi ya makundi ya watu wakiteseka kwa kukosa kitu cha kufanya hivyo kujiingiza katika vitendo vya uasherati.

Walisema mbali na nyumba hizo kujengwa, lakini vile vile liangaliwe suala la kuwepo shule ama vyuo ambavyo vitawezesha kukuza vipaji vya wasichana na vijana ambao kujihusisha kwao katika kufanya uasherati kunatokana na kutokuwa na kazi ya kufanya na wengine kushindwa kujipatia riziki, vitu vinavyowasababisha kupata UKIMWI.

Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Songea, Mhashamu Norbert Mtega aliliambia kongamano hilo kuwa kuna haja kwa wasichana kupewa nguvu kwamba wanaweza kuzalisha mali na kumudu maisha badala ya kutumia miili yao kwa kujistarehesha na kujipatia vipato.

"Sisi tukiwa viongozi wa kiroho ni lazima kuwaenzi wasichana hata vijana kwa kuendeleza vipaji vyao hata kama ni katika michezo. Sote twende vitani na sote tupewe silaha," alisema Mhashamu Mtega.

Naye Mwenyekiti wa Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Mhashamu Aloysius Balina, alisema miongoni mwa sababu zinazoendeleza maambukizi ya UKIMWI, ni imani za ushirikina na mila potofu za jadi.

Hoja hiyo pia ilisisitizwa na Askofu John Mkora wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (K.K.K.T), Shinyanga, aliungana na Mhashamu Balina juu ya mila hizo potofu kwa baadhi ya makabila kuchangia kueneza UKIMWI.

Askofu Balina ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) na Askofu wa Jimbo Katoliki la Shinyanga, alisema kuwa katika jimbo lake waathirika bado hawaamini kama wana UKIMWI na badala yake huenda kwa waganga ambao hupiga ramli maarufu kama "uchembe lwa ngogo".

Alisema huko, waganga wa kienyeji huwalaghai kuwa wagonjwa wao wamerogwa jambo ambalo huzidi kuwapa nafasi ya kuambukiza wengine.

Kongamano hilo pia lilipendekeza kufanyiwa marekebisho kwa baadhi ya sheria ikiwemo ile inayo wakataza madaktari kutaja ugonjwa uliomuua mtu aliyeugua UKIMWI.

Wakati huo huo; Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limesema kuwa tamko lake lililotolewa miaka 15 iliyopita juu ya ugonjwa huo wa UKIMWI hadi sasa bado lina maana ile ile na halioni sababu yoyote mpaka sasa ya kulitengua.

Akitoa maelezo kwenye kongamano hilo juu ya uzoefu wa TEC katika kupambana na UKIMWI, Katibu Mkuu wa TEC, Padre Pius Rutechura, alisema TEC bado lina heshimu yote yaliyoainishwa kwenye tamko la Novemba 23,1987.

Aliyataja baadhi yake kuwa ni pamoja na kutambua kuwa UKIMWI ni janga la Taifa, hatua za kinga zifuate maadili na mafundisho ya dini, kuwatahadharisha waamini kutowahukumu waathirika, waamini kuwa na moyo wa kujali, kuheshimu na kuthamini maisha ya wanadamu katika shughuli zote za tiba na mwisho, kuwaasa wagonjwa kuwa na matumaini.

Kongamano hilo liliandaliwa na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI nchini (TACAIDS) kwa kushirikiana na Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kudhibiti UKIMWI (UNAIDS) na Shirika la Afya duniani (WHO).

Maaskofu wataka seminari zisiwe visiwa

Na Festus Mangwangi, Songea

BAADHI ya maaskofu wa Kanisa Katoliki wamesisitiza kuwa seminari siyo visiwa hivyo, elimu ya Teolojia itolewayo seminarini iimarishe uhusiano mzuri baina ya Wakristo na jamii inayowazunguka ikiwafanya mapadre watarajiwa kuwa safi ndani na nje ili waiongoze vema safari ya kwenda kwa Mungu.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea, Mhashamu Nobert Mtega, Askofu wa Jimbo la Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa na Askofu wa Jimbo la Lindi, Mhashamu Bruno Ngonyani, waliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza katika Seminari Kuu Peramiho, Songea hivi karibuni.

Wakizungumza na waseminaristi wa Peramiho, Maaskofu hao waliwataka vijana wa wito wa upadre kudumisha uhusiano mwema wa Kikristo na jamii nyingine ili kumdhihirsha Yesu Kristo katika maisha na pia, kuwafanya kuwa chachu ya maisha ya uadilifu katika jamii.

"Kama ilivyo kwamba binadamu siyo kisiwa, vivyo hivyo seminari au waseminaristi siyo visiwa; mnapaswa kuendeleza uhusiano mzuri wa Kikristo na majirani pamoja na asasi zinazoizunguka seminari yenu," alisema Mhashamu Bruno Ngonyani.

Aliwataka waseminaristi na mashemasi kupanua wigo wa uhusiano kwa kuendelea kufundisha Katekesi katika shule ya msingi jirani kutoa mada mbalimbali za Kiteolojia na asasi, vyuo, sekondari pamoja na kuwahubiria watu Neno la Mungu.

Naye Mhashamu Mtega alisisitiza umuhimu wa taaluma akichambua kushindwa kwa sayansi na teknolojia kuelezea Teolojia ambayo kueleweka kwake kunahitaji akili inayoongozwa na imani.

"Pamoja na maendeleo mazuri ya Sayansi na Teknolojia, kamwe haijatokea na wala haitatokea masuala ya imani na mahusiano kati ya mwanadamu na Muumba wake, kuweza kupimwa katika maabara," alibainisha Mhashamu Mtega.

Alifafanua kuwa, kushindwa kwa Sayansi kuupima uhuru wa mtu kimawazo na msukumo wa ndani wa vionjo vyake, haina maana kuwa vitu hivyo na imani ya kweli ya Mungu havipo.

Alisema ni jukumu la kila mwanadamu, kumjua, kumpenda na kumtumikia Mungu ili kufika mbinguni japo vitu hivyo havipimiki kimaabara.

"Nawaombeni wanangu mzidishe ari ya kusoma zaidi ili mkajiunge na wenzenu kuihubiri Injili ya kweli kwa utaalmu wa hali ya juu wa kiteolojia na hivyo, kupambana na wimbi la dini potofu," alisema Mhashamu Mtega.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Seminari Kuu ya Peramiho, Mhashamu Ngalalekumtwa, ameelezea kuridhika kwao katika ziara ya kichungaji waliyoifanya kwa takriban siku tano seminarini hapo.

Katika ziara hiyo, maaskofu walishiriki ratiba yote tangu kanisani, darasani na katika michezo.

Alisema, "Katika uchunguzi wetu tumeona karibu katika kila nyanja mnaendelea vizuri, lakini ongezeni bidii kwani sumu ya maendeleo ni kuridhika. Msikubali dhana yoyote potofu iwaondoe katika nia hii njema ya kutaka kuwa watumishi wa Bwana katika shamba lake,... twekeni nyavu hadi kilindini ili kuvua samaki wengi na bora."

Awali, Gambera wa Seminari hiyo, Padre Titus Amigu, aliwataka waseminaristi kuwa wazi na huru kwani nia ya ziara hiyo ni kuboresha mazingira yao na seminari kwa jumla.

Sheria inawanyang’anya wanawake watoto- Mwanasheria WLAC

Na Lilian Timbuka

MWANASHERIA mmoja wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC), amesema mapungufu yaliyopo katika sheria, yanachangia wanawake kunyimwa haki zao ikiwa ni pamoja na kunyan’anywa watoto kwa madai ya uraia.

Mwanasheria huyo, Bi. Rehema Kerefu, alisema hivi karibuni katika mazungumzo yake na KIONGOZI jijini Dar es Salaam, sheria juu ya uraia iliyopo sasa, inachangia kwa kiasi kikubwa kuwakandamiza wanawake katika kupata haki zao.

Alisema kutokana na mapungufu yaliyomo katika sheria hiyo, wanawake wengi wamekuwa wakinyimwa watoto wao pindi uraia wa mwanamke huyo unapomalizika.

Alisema mapungufu hayo yanachangia pia watoto kutambuliwa uraia wao kutokana na baba zao.

"Kutokana na hali hiyo wanawake hujikuta wakiwa na wakati mgumu wa kupata watoto wao toka kwa waume zao kwa sababu tu wao si raia wa nchi husika," alisema.

Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake (WLAC) hutoa msaada wa kisheria kwa wanawake wenye matatizo mbalimbali yakiwemo ya ndoa, mirathi, uraia na ardhi bila ya malipo yoyote.

Aidha, Wanasheria huyo alisema utafiti unaonesha kuwa, wanawake wengi bado hawazielewi vema sheria zinazowahusu.

Uzazi wa mpango wa kisasa ni dhambi tupu - Kanisa Katoliki

Na Ferdinand Ngowi

"NJIA zote za kupanga uzazi zisizo za asili na zisizofuata maumbile ni dhambi na wote wanaozishiriki wanatenda dhambi, wakaungame" imeelezwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Msimbazi ambaye pia ni Mratibu wa semina za wanandoa, Padre Benedikti Shayo, aliyasema hayo wiki iliyopita wakati akitoa mada katika semina ya wanandoa iliyofanyika katika Parokia ya Mavurunza, jimboni humo.

Alisema, matumizi ya mipira (kondomu), vidonge vya majira au vitanzi ili kuzuia mimba zisizotarajiwa, ni dhambi na hivyo wanaofanya hivyo watubu.

Alisema vitendo vya baadhi ya wanandoa, hususan, wanaume kutumia kondomu au kujichua, na wanawake kutumia vidonge vya majira au vitanzi kama njia za kuzuia mimba, vinaenda kinyume na maumbile na kwamba havimfurahishi Mungu.

"...kutumia kondomu au mama kutumia vidonge vya majira ni kwenda kinyume na maumbile.... wote wanaoshiriki wanastahili kuungama," alisema.

Padre Shayo alikuwa akijibu swali la mshiriki mmoja wa semina hiyo aliyedai Kanisa liende na wakati kwa kuruhusu matumizi ya vitanzi na vidonge vya majira kwa akinamama wanandoa ambao hawakusudii kupata mtoto.

Padri Shayo alisema kuwa, njia zinazokubalika na Kanisa katika kupanga uzazi ni ile inayoitwa Utaratibu wa Billing’s (Billing’s Method) na ile ya kutumia kalenda yaani njia za asili zilizotumika tangu zamani kabla ya mageuzi ya teknolojia duniani.

Awali, ilielezwa katika semina hiyo na mtaalamu mmoja wa mambo ya uzazi kuwa zipo njia nyingi za kuzuia mimba kwa wanandoa wasiopenda kupata mtoto katika kipindi hicho.

Alizitaja njia hizo zinazokwenda kinyume na mafundisho ya dini kuwa ni pamoja na matumizi ya vidonge vya majira, vitanzi na mipira.

Baadhi ya watoa mada katika Semina hiyo walikuwa ni Bibi Betty Mwaluli kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Benedikti Shayo na Dk. Andrew Swai.

Wakati huo huo: Mmoja wa watoa mada katika semina hiyo Bibi Betty Mwaluli, aliwakumbusha wanawake kuzingatia kuwa licha ya mageuzi yanayokuja ya akina mama kutambua na kudai haki zao, bado wanalo jukumu kubwa la kuwatii waume zao.

Alisema wanawake hawana budi kuwatii waume zao kwa kuwa mwanaume ni kichwa cha nyumba na Maandiko Matakatifu (Biblia), yanaagiza hivyo.

Mwenyekiti Moravian duniani kusherehekea Pasaka Temeke

l‘Wakristo nchini wamekua, wachangie maendeleo ya Kanisa’

Na Joseph Sabinus

MWENYEKITI wa Kanisa la Moravian Duniani, Mchungaji Angetile Y. Msomba, na Katibu Mkuu wa Kanisa katika Jimbo la Kusini nchini Tanzania, Mchungaji Nelson Mwaisango, wataendesha ibada ya Pasaka katika ushirika wa Temeke jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kanisa la Moravian Tanzania(KMT), Wilaya ya Mashariki katika Jimbo la Kusini, Mchungaji Eli Ambukege, ameliambia KIONGOZI juma lililopita ofisini kwake jijini Dar es Salaam kuwa, katika ibada hiyo itakayofanyika kitaifa usharikani Temeke Machi 31, mahubiri yatatolewa na Mchungaji Msomba na ibada ya Liturujia itaongozwa na Mchungaji Mwaisango.

Alisema Wakristo na wanajamii wengine wakitumue kipindi cha Pasaka kujihoji na kujipeleleza juu ya maisha yao wakiyahusisha na upendo wa Mungu wa kumtoa Yesu kufa msalabani kwa ajili ya dhambi za watu.

Akinukuu Kitabu cha Warumi 3:10, Mchungaji Ambukege alisema, "Kwa kuwa wanadamu wote ni wenye dhambi, basi tujitambue kuwa kweli ni wenye dhambi, lakini kwa neema ya Mungu, tumeokolewa kwa kifo cha Yesu Msalabani."

Aliongeza,"...Hiki ni kipindi cha watu wote kujua maana halisi ya Pasaka...wanadamu tumepewa msamaha wa dhambi. Tumepatanishwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.

Lazima tujue kuwa ushindi wa Kristo na ufufuko wa Yesu ndio uhai na uwepo wa Kanisa maana asingekuja, Kanisa nalo lisingekuwapo na wala lisingehubiri Injili.

Alishauri jamii kuzingatia kuwa siku zote za mwaka ni siku takatifu za Mungu hivyo, jamii iachane na mtindo wa kuishi kiadilifu katika katika mkesha wa Sikukuu za kidini, lakini baada ya mchana wa siku ya sikukuu, wanaanza kufanya maasi na vitendo mbalimbali vinavyopingana na mapenzi ya Mungu.

"Inashangaza wengine wanachagua siku, nyingine wanafanya mema na hata kusali usiku, lakini siku nyingine wanakunywa ovyo, wanafanya vitendo ambavyo ni hatari kiroho na kimwili na hilo siyo kusudi la Mungu," alisema.

Alisema katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, kila mmoja azingatie kuwa Yesu amefufuka kwa ajili yake na kujiuliza kama Yesu huyo amefufuka ndani ya roho yake. Kila mmoja ajiulize kuwa je, sasa Yesu amefufuka ndani ya roho yangu? Na chakula kiwe ni sehemu ya shukurani katika familia ya Mungu. Watu wale, wanywe pamoja huku wakiomba, wakiabudu na kumshukuru Mungu".

Wakati huo huo: Mchungaji Ambukege amesema Kanisa la Tanzania lijitambue kuwa linazo rasilimali imara ambazo ni Wakristo wake hivyo, watumike kuliletea maendeleo.

Alikuwa akisisitiza umuhimu wa Wakristo kuchangia ujenzi wa Kanisa nchini bila kutegemea misaada toka kwa nchi wahisani.

Kauli ya Mchungaji Ambukege imekuja wakati akiwahimiza Wamoravian wa Ushirika wa Kawe, Wilaya ya Mashariki, na wote wenye mapenzi mema kuchangia kwa moyo, katika harambee inayofanyika Jumapili hii kuchangia ujenzi wa kanisa katika ushirika huo.

"Alisema, "Miaka zaidi ya 100 ya uinjilishaji ni mingi sana, lazima Watanzania wenyewe tujenge na kuimarisha utamaduni wa kujiletea maendeleo yetu wenyewe kiroho na kimwili."

Alisema kila Mkristo ajue kuwa ujenzi wa Kanisa nchini ni wajibu wa Wakrito wa Tanzania wenyewe. "...Mtu anapoingia Ukristo, anaingia katika wajibu wa Ukristo hivyo, atumie mali, akili na nguvu zake kulitumikia Kanisa kwa moyo,"

Tusiwahukumu wenye UKIMWI, tuwapende, tuwasaidie - Askofu Balina

Na Peter Dominic

KANISA Katoliki linashikilia msimamo wake kuwa njia pekee ya kuudhibiti ugonjwa wa UKIMWI, ni kubadili tabia na sio matumizi ya kondomu na pia, limetaka jamii isiwahukumu wagonjwa wa UKIMWI kuwa ni wazinzi na waasherati.

Mwenyekiti wa Idara ya Afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mhashamu Aloysius Balina, aliyasema hayo wakati akizungumza katika semina ya siku mbili iliyowahusisha Wakurugenzi wa Vyuo vya Katekesi wa majimbo na walimu Wakatoliki katika shule za msingi, sekondari na vyuo kutoka katika majimbo Kanisa Katoliki nchini.

Katika semina hiyo iliyofanyika katika Kituo cha Mafunzo na Mikutano cha TEC, Kurasini Dar es Salaam, na kufanyika katika Kituo cha Mafunzo na Mikutano wiki iliyopita, Mhashamu Balina alisema, kondomu si kinga ya UKIMWI bali kinga sahihi ni mafundisho sahihi juu ya Neno la Mungu.

"Ukirnwi ni janga la taifa, hatua za kinga zifuate maadiii na mafundisho ya Kanisa," alisisitiza Mhashamu Balina ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS).

Alisema, ingawa inapopigwa yowe, watu hukusanyika kumshambulia adui bila kuulizana kwanza ni silaha ipi inayofaa kutumika katika vita hiyo, TEC inaamini na kusisitiza kuwa kuwa silaha pekee ya kutumika katika

kupambana na adui huyo (UKIMWI), ni kufuata maadiii na mafundisho ya Kanisa.

Alisema, makatekista na viongozi wengine wanawajibika kubadili tabia za vijana na jamii nzima kwa jumla kwa kuwafundisha maadili mema yanayozingatia mafundisho juu ya Neno la Mungu. "Muwafudishe waamini kujali na kuheshimu hatua zote za tiba," alisema.

Hata hivyo, alisema jamii imekuwa na muelekeo mbaya wa kuwahukumu watu walioathirika na ugonjwa huo kwa madai kuwa, wamepata ugonjwa huo kutokana na uzinzi na vitendo vya uasherati.

Ingawa UKIMWI huenezwa zaidi kwa njia ya zinaa, zipo pia njia nyingine za maambukizi ikiwa ni pamoja na kuongezwa damu iliyoathirika na virusi vya UKIMWI, kuchangia vyombo vya kutogea kama nyembe na sindano zisizochemshwa vema, pamoja na mjamzito kumuambukiza mtoto ambaye hajazaliwa. Badhi ya wanandoa wasio waaminifu, wamekuwa pia wakiwaambukiza wenzao licha ya kuwa wanajiheshimu katika ndoa zao.

Aliitaka jamii kuacha tabia hiyo badala yake wawatunze na kuwaheshimu, waathirika wa virusi vya UKIMWI na wagonjwa wa UKIMWI kwa upendo mkamilifu.

"Sisi tunawajibika kuwafariji wagonjwa na kuwapa matumaini; imepita miaka 15 tangu tulipopitisha tamko hili, janga hili bado linaendelea, Mkapa ametoa tamko, hili ni janga la taifa," alisema.

Askofu Balina aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa mmoja wa Makamishna wa TACAIDS, alisema, Makamishna walioteuliwa ni kwa ajili ya kuiangalia jamii ya Watanzania wote.

"Kazi yetu ni kujihusisha kikamilifu kuutokomeza ugonjwa wa UKIMWI na kuzuia kuenea kwake; tumshirikishe kila mmoja ili autokomeze na kuzuia usambazaji wake," alisema.

Aidha, alisema pamoja na mambo mengine, asasi hiyo itazishauri Hospitali juu ya dawa zinazotumika.

"Mtu anaweza kutumia zaidi ya shilingi 60,000 kununulia dawa za kuongeza nguvu, lakini siku akikosa atakaribisha zaidi virusi kumshambulia, tusiruhusu hali hiyo," alionya.

Alisema Wakristo wote wanalo jukumu la kuwajibika kwa pamoja kuwapenda majirani na kuwasaidia. "Sisi tunasukumwa na moyo wa lnjili kuishi imani yetu na tunasukumwa pia kuwapenda majirani zetu na kuwasaidia."

Aliyetapeli parokiani Dar atiwa mbaroni

Na Mwandishi Wetu

HATIMAYE polisi imefanikiwa kumtia mbaroni mwanamke anayedaiwa kuwa tapeli,ambaye amekuwa akizisumbua baadhi ya Parokia za Jimbo Katoliki la Dar es Salaam kwa kuzifanyia utapeli wa fedha.

Kufanikiwa kukamatwa kwa mwanamke huyo ambaye amekuwa akijitambulisha kwa jina la Rosemary na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu iliyopo jijini Dar es Salaam,kumekuja baada ya kwenda kufanya utaperi wake katika Parokia ya Makuburi.

Habari zilizopatikana parokiani hapo na kudhibitishwa na Paroko wa Parokia hiyo ya Makuburi Padre Gereldo Derksen,zinasema kuwa Machi Mosi mwaka huu majira ya saa 11.30 jioni,mama huyo anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka 35 alifika parokiani hapo kwa lengo la kuomba msaada wa fedha.

Habari zinasema kuwa mama huyo ambaye ni mtaalam wa kujua kujieleza kwa kutaja shida mbalimbali,alifanikiwa kumshawishi katekista wa parokia hiyo aliyefahamika kwa jina la Bw.John Mwarenga na kujipatia kitita cha shilingi 7,000.

Hata hivyo kutokana na sababu kwamba kiasi hicho kisingemtosha mama huyo kama alivyojieleza kwa katekista huyo kwamba angehitaji sh.20,000,katekista alimwambia arudi kesho yake ambapo angekuja kueleza shida ya ke kwa Paroko.

Kesho yake mama huyo alifika tena parokiani hapo ambapo alifanikiwa kumkuta Paroko na baada ya kueleza shida yake ,Paroko alibaini kuwa huenda mwanamke huyo ndiye yule anayefanya utapeli katika parokia mbambali kama alivyo kwisha pata tetesi siku za nyuma hali iliyomfanya paroko huyo aende kwenye vyombo vya usalama na hatimaye kufanikiwa kumtia nguvu mwanamke huyo.

Wanaovaa nusu uchi kuzuiliwa katika milango makanisani?

l Yaelezwa kuwa kanisani, mikusanyiko sio sehemu ya wasichana kujinadi

l Padre akerwa na Big G, simu za mkononi kanisani

Na Lilian Timbuka

WASICHANA na waamini wengine wanaovaa mavazi yanayokaribia kuwa uchi, huenda sasa wakazuiliwa milangoni katika makanisa mbalimbali ya Kanisa Katoliki endapo ushauri uliotolewa kufanya hivyo, utazingatiwa.

Padre Paul Haule wa Kanisa Katoliki la Mashahidi wa Uganda, Parokia ya Magomeni, na Mwenyekiti Msaidizi wa Kigango cha Mikocheni, katika Parokia ya Mwenge, Bi. Bernadeta Sebastian, walizungumza na KIONGOZI jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Parokia za Mwenge na Magomeni zipo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Walitoa ushauri sambamba na kuwahimiza wasichana na baadhi ya vijana wa kiume kuepuka kabisa mtindo wa kuvaa nguo fupi au zinazoonesha maungo husasan wawapo kanisani kwani mavazi hayo ni kinyume cha maadili ya Kanisa.

Katika mazungumzo hayo, kwa pamoja wamewaomba viongozi na waamini wote wa Kanisa Katoliki kukemea na kutowaruhusu vijana na wote wenye mavazi yanayokwenda kinyume na maadili, kuingia kanisani.

Bi. Bernadeta alisema kuwa, sasa ni wakati muafaka kwa vijana Wakristo kutambua wenyewe kuwa ni mavazi yapi yanayowastahili wayavae katika sehemu za ibada, starehe na sehemu nyingine.

Alisema ni utovu wa nidhamu na ukiukaji wa maadili ya jamii na Kanisa kwa vijana wa kike kuvaa nguo fupi na zinazowabana na kuonesha wazi maungo yao hata wawapo katika nyumba takatifu za ibada.

Aliwaomba wasichana na wanawake kwa jumla, kuzingatia kuvaa mavazi yanayofaa na yanayolinda hadhi yao mbele ya Kanisa na mbele ya jamii.

Aliilaumu tabia ya baadhi ya wasichana na wanawake kutumia mikusanyiko mbalimbali ikiwamo ya ibada kama sehemu za kufanyia maonesho ya mavazi huku wakijua kuwa, mavazi mengine yanakiuka maadili ya kidini na kijamii.

"Umefika wakati sasa mabinti zetu waelewe kuwa Kanisa ni nyumba ya ibada na si eneo au ukumbi wa maonesho ya mavazi kama badhi yao wanavyofanya hivi sasa," alisema.

Naye Padre Paul Haule alisema mavazi ya namna hiyo hayana budi kuwa vitu vya aibu hasa kwa msichana anayejijua kuwa ni Mkatoliki safi kwani yanalitia doa Kanisa na kuonesha hali isiyopendeza.

"Inawapasa waamini wote waelewe kuwa kanisani si sehemu ya starehe, bali ni sehemu ambayo tunakwenda kupeleka shida zetu na maombi yetu ili Mwenyezi Mungu atusaidie. Sasa kama unafanya mambo yako mengine, kweli sala yako itapokewa?" alihoji Padre Haule.

Wakati huo huo: Padre Haule amewahimiza waamini kuzima simu zao za mikononi na kuacha tabia ya kutafuna bazoka (Big G) wawapo kanisani katika ibada.

Askofu Kilaini ataka vijana waimarishe uhusiano

Na Anthony Ngonyani

ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Method Kilaini amewataka vijana kujenga utamaduni wa kuwa na mahusiano mema ili wawe na mikakati imara ya kuboresha maisha yao.

Mhashamu Kilaini aliyasema hayo juma lililopita wakati akitoa mada katika semina ya vijana iliyofanyika katika Parokia ya Oyster-bay, jimboni humo.

Alisema vijana wawe na tabia ya kufurahi pamoja ili kujenga uhusiano mwema na wenzao kwani wanaweza kwa kutafakari pamoja na kujifunza ujuzi na mikakati mingi ya kuboresha maisha yao na kuwaendeleza kiroho na kimwili.

Alisema kwa kuboresha uhusiano baina yao, watajenga nidhamu kwani watajipenda, watajiheshimu na watajitambua hadhi yao.

Alisema kijana ambaye hana nidhamu ni rahisi kujiingiza katika matendo maovu kama vile utumiaji wa dawa ya kulenya, umalaya, wizi na ubakaji.

Alisema ili kujenga nidhamu na uhusiano bora, ni lazima vijana wawe na uchaguzi mzuri wa vikundi vinavyofaa kuimarisha uhusiano navyo.

Askofu Kilaini aliongeza kusema kuwa, kutokana na uchaguzi huo unaofaa, Mwenyezi Mungu atawaimarisha uwezo na vipaji mbalimbali vya vijana hao.

Semina hiyo ya siku moja iliandaliwa na Umoja wa Vijana wa Oster-bay na iliwajumuhisha vijana wote kutoka Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo za Parokia hiyo.