Serikali haitatetea dini zinazohubiri vurugu - Jaji Bomani

l Ataka wanahabari kupuuza viongozi wa dini wanaochochea fujo

l Akiri kuwapo udhaifu katika haki za binadamu nchini

Na Joseph Sabinus

MWENYEKITI wa Tume ya Utangazaji, Jaji Mark Bomani amesema kikundi chochote cha dini kisijidanganye kufanya vurugu kikitegemea kutetewa na Serikali na amevishauri vyombo vya habari kuwapuuza viongozi wa dini wanaohubiri fujo.

Aliyasema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi baada ya Mahafali ya Nne ya Chuo cha Uandishi wa Habari cha Dar es Salaam (DSJ).

Mwandishi alitaka kujua maoni ya Jaji Bomani kama vyombo vya habari vina mchango wowote katika vurugu za kidini na pia, kupata maoni juu ya uhusiano baina ya Serikali na dini mbalimbali nchini.

Alisema wakati mwingine vyombo vya habari vimekuwa vikitangaza habari za viongozi wa dini ambazo zinachochea vurugu jambo ambalo alisema si zuri. Hata hivyo, alisema vyombo vya habari vinapotangaza kauli za uchochezi na za vurugu toka kwa viongozi wa dini, vitangaze kwa lengo la kuionesha jamii na kuitahadharisha na sio kuunga mkono kauli hizo hatari.

"Vyombo vya habari visitoe nafasi kwa watu wanaoleta vurugu...hata kama ni sherehe maana vinginevyo, mtakuwa (wanahabari) mumemsaidia kuchochea fujo. Sana sana ukiripoti kauli zake, ripoti kwa nia ya kuitahadharisha jamii iwe macho nae," alisema.

Aidha, alisema kikundi au kiongozi yeyote wa dini asijidanganye kuhubiri na kuchochea vurugu akidhani kwamba Serikali itamtetea.

Alisema kwa kuwa Serikali ya Tanzania haina dini, haiwezi kuingilia wala kupendelea dini yoyote lakini, haitamvumilia wala kumfumbia macho kiongozi au kikundi chochote cha dini kitakachohubiri vurugu.

"Serikali haiwezi kuingilia wala kuikandamiza dini yoyote mradi tu, dini hiyo isilete fujo," alisema.

Awali akizungumza katika mahafali hayo, Jaji Bomani aliyekuwa mgeni rasmi alisema, kuundwa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni hatua muhimu nchini kwa kuwa yapo mapungufu katika usimamizi wa haki za binadamu nchini.

"Kuundwa kwa Tume hii ni jambo kubwa sana hapa nchini. Mpaka sasa pamekuwa na upungufu mkubwa kwenye usimamizi wa haki za binadamu, pamoja na kwamba haki hizo zimetajwa kwenye Katiba," alisema.

Aliwashauri wanahabari kufanya utafiti wa kina ili kutoa habari sahihi bila kupendelea wala kuonea upande wowote.

"Kamwe msiwe waoga katika kudadisi habari na kufichua madhambi au vitendo vyovyote vya ubadhirifu na wala msipendelee mtu yeyote awe amewapa kitu chochote au hapana...

Msikubali kutumiwa kumjenga mtu au kiongozi yeyote au kumbomoa mtu au kiongozi yeyote hasa wakati ukifika kuelekea kwenye uchaguzi," alisema.

Jaji Bomani alikiri kuwa wapo vijana wengi wanaotaka kuchukua mafunzo ya uandishi wa habari chuoni hapo (DSJ), lakini, hawana uwezo wa kujitosheleza kimahitaji hivyo, ni muhimu vijana hao kupatiwa mikopo.

Katika mahafari hayo, wahitimu 108 walitunukiwa vyeti mbalimbali.

Wanaotumia dini kufanya maovu wanazinajisi dini zao

l Anglikana wasisitiza kuombea amani

l Mpentekoste wasema ukosefu wa amani umeanza kunuka

Na Mwandishi Wetu, Mtwara

KITENDO cha kiongozi wa dini kuutumia dini kuendesha vitendo viovu vikiwamo vya ugaidi, ni sawa na kiongozi huyo kuinajisi dini yake, amesema Abate Dionys wa Abasia ya Ndanda.

Abate Dionys aliyasema hayo wakati wa ibada maalumu ya kuombea Umoja wa Wakristo Duniani. Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa la Abasia hiyo na kuwajumuisha Wakristo wa madhehebu mbalimbali wakiwamo Wakatoliki, Walutheri, Wapentekoste na Waanglikana.

Akinukuu hotuba ya Baba Mtakatifu, Yohane Paulo wa Pili, aliyoitoa Januari Mosi, mwaka huu kuhusu umuhimu wa amani duniani, Abate Dionys aliwataka viongozi wa dini zote kupinga vitendo vyote vya uhalifu vikiwamo vya ugaidi.

Alisema kuwa mtu anayejitangaza kuwa yeye ni gaidi kwa Jina la Mungu na kuwatendea wengine maovu yakiwamo mauaji na mateso mbalimbali, anapingana na mapenzi ya Mungu.

Naye mwakilishi wa Kanisa la Anglikana, Mchungaji Hokororo kutoka Usharika wa Chikundi- Masasi, alisema katika ibada hiyo kuwa chanzo cha ukosefu wa umoja katika Kanisa ni ukosefu wa amani. Aliwataka Wakristo kuomba neema ya umoja toka kwa Mungu.

"Tuone utengano katika Kanisa kama alama ya kukosekana kwa amani kitu ambacho ni kinyume cha mafundisho ya Bwana Wetu Yesu Kristo," alisema.

Akizungumzia vitendo vya kigaidi vinavyoendelea duniani, Mchungaji Hokororo alisema kuwa kuna kila sababu kwa Wakristo kuomba na kuishi kwa amani katika maisha yao.

Mwakilishi wa madhehebu ya Pentekoste, Bw. Maiko Mushi, alisema kuwa hali ya kukosekana kwa amani nchini, imeaanza kuonekana kutokana na vitendo vinavyoendelea kila siku vikiwemo vya watu kuchinjana.

Alisema ili amani iliyozoeleka nchini iendelee kuwapo, ipo haja ya kuwa waaminifu bila kuwa na tamaa ya uhalifu.

"Siyo kuwa tu pamoja huku mmoja anamezea mate fedha za mwingine zilizoko mfukoni mwake, au wivu kwa maendeleo yake na hasira baina yetu. Wivu kama huo hautatufikisha mahali popote," alisema.

Katika ibada hiyo iliyodumu kwa takribani saa moja na nusu, licha ya masomo kutoka Maandiko Matakatifu,mahubiri mbalimbali na maombi ya kuchangiana, vile vile wanafunzi wa utawa wa Abasia ya Ndanda walitumbuiza kwa matarumbeta ambayo yaliongeza burudani katika ibada hiyo.

Kanisa kuwaadhibu vimada wanaodangaya ndoa

Na Salvatory Magangira, Sengerema

JIMBO Katoliki la Geita limeanzishda utaratibu wa kuwatoza faini ya shilingi 20,000 watu waliojiandikisha kufunga ndoa kwa muda mrefu lakini bado wanaishi kimada.

Kwa mujibu wa Paroko wa Parokia ya Segerema Padre Stephen Idili adhabu hiyo haitawahusu wazazi ambao vijana wao (wachumba) walitoa na kupokea mahari lakini vijana wao hawajafunga ndoa ingawa bado wanaishi pamoja kama mume na mke.

Padre Idili ambaye alikuwa akizungumza na KIONGOZI parokiani kwake katika Jimbo Katoliki la Geita alisema mpango huo wa Jimbo zima ni miongoni mwa mambo mbalimbali yaliyofanyika na kukubalika ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 ya Ukristo yaliyomalizika mwishoni mwa mwaka jana.

Alisema katika maadhimisho ya jubilei ya mwaka 2000 ya ukristo na miaka 100 ya uinjilishaji Jimbo la Geita pia lilitoa ofa kwa watoto waliozaliwa nje ya ndoa kupata Sakramenti ya ubatizo kwa mujibu wa taratibu na mwongozo wa kanisa.

Naye Paroko msaidizi wa Parokia hiyo Padre Flavian Kasala alidokeza kuwa jimbo liliweka utaratibu wa pekee katika kutoa Sakramenti ya Kitubio kwa waliotoa mimba kwa ruhusu ya Askofu Mkuu Mhashamu Anthony Mayalla.

"Kuungamisha dhambi ya kutoa mimba ni kazi ya Askofu pekee yake hivyo ruhusa hii kwa mapadre kuifanya kazi hiyo ni bahati tu; na itakuwa ya mwaka mmoja" alisema.

Wakati huo huo: Maandalizi ya kuanzishwa kwa Shirika la Utoto Mtakatifu jimboni Geita yapo katika hatua nzuri kimaendeleo.

Paroko Msaidizi wa Parokia ya Segerema Padre Flavian Kasala ambaye ni msimamizi wa Shirika hilo ameliambia KIONGOZI kuwa mipango yote imekwisha kamilika.

Alisema Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita Mhashamu Damian Dallu anatarajiwa kulitangaza rasmi shirika hilo.

Haya ndiyo madhara yanayowasubiri wavuta sigara:

l Magonjwa yapatayo 25 ni miongoni

l Watoto hulazimishwa kuvuta, wamo katika hatari ya kifo

  • Wengine huzaliwa na uzito wa chini

Na Mwandishi Maalumu

UVUTAJI sigara wa kulazimishwa kwa watoto bila wao kujua, licha ya kuwadhuru watoto walio tumboni, pia huwatia watoto waliozaliwa katika hatari ya kifo huku ukisababisha karibu magonjwa 25 yakiwamo ya moyo, shinikizo la damu, kansa ya mapafu, kichomi na kifua kikuu.

Kwa mujibu wa kipeperushi kilichotolewa na Blue Cross Society Tanzania kiitwacho SIGARA INAUA! ACHA! Uvutaji sigara licha ya kuwadhuru wavutaji wenyewe, pia hudhuru afya za wasiovuta ambao huishi na kufanya kazi na wavutaji.

"Hususan, WATOTO huwa katika hatari zaidi," imesema sehemu ya kipeperushi hicho na kuongeza, "Huvuta kiasi fulani cha moshi bila wao kujua au kudhamiria. Hii huitwa uvutaji wa kusababishwa (passive smoking)."

Kinazidi kufafanua kwa, uvutaji wa namna hiyo huwafanya watoto ambao wapate matatizo na usumbufu unaosababishwa na moshi wa tumbaku.

"Nao kama wavutaji wengine, huwekwa kwenye hatari ya magonjwa na kifo cha ghafla...Huwadhuru watoto ambao bado wamo tumboni," kipeperushi hicho kimesema.

Kimezidi kufafanua kuwa, watoto wanazaliwa na akina mama wavutaji, wawe wa kusababishwa au wa kujitakia, kwa kawaida huzaliwa na uzito wa chini kuliko uzito wa kawaida.

Kimeyataja baadhi ya madhara yanayowakabili wavuta sigara wengi wa kawaida kuwa ni pamoja na kuwa hatarini kukumbwa na magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na kansa ya mapafu, koo na mdomo.

Madhara mengine ni kupatwa na magonjwa ya njia ya hewa kama vile kifua cha mshipa, mafua kichomi na mapafu kujaa hewa.

Mengine ni kikohozi kibaya sana na kutema kila siku, kukuza ugonjwa wa kifua kikuu na kuleta pumu na magonjwa mengine mengi na mabaya.

Kipeperushi kimesema pia yapo madhara na hasara nyingine za kuvuta sigara ikiwa ni pamoja na kumfanya mvutaji apoteze fedha ambazo angetumia kwa mambo mengine mazuri ya kimaisha.

Pia, kwa mujibu wa kipeperushi hicho, uvutaji sigara humfanya mvutaji anuke harafu mbaya ya tumbaku na kumfanya apate makunyanzi usoni na hivyo, kuonekana mzee mapema kabla ya wakati wake.

Athari nyingine ni kuyafanya meno ya mvutaji kupata kutu na pia, kuwa msumbufu na kuhatarisha afya za rafiki zako na familia yako.

Kuhusu madai ya baadhi ya wavutaji kuwa UVUTAJI SIGARA NI STAREHE, Kipeperushi kinawakariri madaktari wakisema kuwa HII SIYO KWELI.

"Uvutaji huufanya moyo wako kufanya kazi zaidi, husababisha shinikizo la damu na kuifanya misuli yako kukomaa," inasema sehemu ya kipeperushi hicho.

Kinatoa pia jibu la kitu gani mtu anayejisikia kusongwa na matatizo ya kuhitaji kujiliwaza afanye.

Kinasema, "Kama unahitaji kujiliwaza kuna mambo mengi unaweza kufanya kama vile: Kuvuta pumzi ndefu pole pole na kupumua polepole fanya hivi mara kadhaa. Fanya matembezi, kimbia mchakamchaka, ogelea, oga maji ya vuguvugu na fanya maongezi na mwenzako".Kuhusu uwezekano wa kuvuta kidogo, kwa kuonja na baadaye kuacha, kinaeleza kuwa kitendo cha kujaribu kuvuta kinaweza kukutawala, kama ilivyo kwa dawa za kulevya na pombe.

"Mara, ukianza, ni vigumu kuacha, na kama unataka kuacha, na utajutia na kuanza kuvuta. Hivyo usianze kuvua hata kidogo," kinasema.

Kinatoa vidokezo vya jinsi ya kushinda majaribu ya kuanza kuvuta. Kinasema, uwe na fikra zinazojitegemea, uelewe na udumu kwa lililo jema kwako, ujivunie kutokuwa mvutaji, usilaghaike kwa matangazo ya sigara na uyashinde majaribu ya kugusa sigara.

Kinatoa vidokezo vya jinsi ya kuyashinda majaribu ya kurudia kuvuta kuwa ni kufuata ushauri wa daktari, mshauri au mshauri nasaha wako.

Njia nyingine ni kutafuna bigijii au kula tunda au bisi kama unajiskia kutaka kuvuta, kunywa maji wakati wa kuamka asubuhi na wakati wa chakula na wakati wowote unapojisikia kuvuta.

Kinasisitiza, "Epuka vinywaji vyenye kuchochea uvutaji sigara kama vile kahawa na pombe. Jitenge na wavuta sigara".

Katika kipeperushi hicho, Blue Cross Society Tanzania, kimezitaja faida za kutokuwa mvutaji wa sigara kuwa ni pamoja na kutumia fedha zako kwa mambo mazuri ya kimaisha badala ya kuzipoteza kwenye tumbaku au sigara, kutotapata magonjwa yanayo sababishwa na uvutaji, kuwa na nafasi nzuri ya kujenga maisha thabiti, marefu na maisha yenye afya tele na hutaathiri afya na kusababisha usumbufu kwa wale wanaokuzunguka.

Kuhusu swali kuwa :Je unaweza kuacha kuvuta bila msaada?

Kinajibu, "Ndiyo, unaweza kufanya hivyo. Kimsingi baadhi ya wale ambao wanachagua kuacha kuvuta hufanya hivi bila msaada. Kinachohitajika ni uamuzi!

Mungu akusaidie!"

Ubunge, Uwaziri haupatikani kwa waganga- Kauli

Na Joseph Sabinus

KUTAFUTA uwaziri, ubunge, udiwani na chochote kwa imani za ushirikina, kumeelezwa kuchangia kukwama kwa maendeleo ya jamii kwa kumaliza pesa na kuzorotesha uwajibikaji.

Katibu Mtendaji wa Idara ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padre Raphael Kilumanga, aliyasema hayo mwishoni mwa juma katika semina ya siku moja kwa Wanaume Wakatoliki wa Parokia ya Mtoni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam juu ya jumuiya ndogondogo za kikristo.

Alisema jumuiya hizo zinao wajibu kuwaimarisha kiimani waaini wenzao wanaotumia muda na mali zao kwa imani hizo potofu.

Alisema kutokana na imani hizo kutawala, maendeleo ya jamii kiroho na kimwili yamekuwa yakizorota kutokana na ubinafsi unaoshamiri.

"Kuna watu wanakwenda kwa waganga ili kupata udiwani, ubunge eti hata wabunge wenane utasikia eti wanakwenda ili wawe mawaziri na huko wanapoteza pesa nyingi bure tu.

Matokeo yake, ubinafsi unaongezeka, kashfa za kidini na hata sasa kuheshimiana katika jamii kunakosekana," alisema.

Padre Kilumanga alisema kuwa, matokeo ya imani hizo potofu za ushirikina ni uwajibikaji mbovu na ongezeko la vitendo vya rushwa na uhalifu.

Aliikemea vitendo vya utoaji mimba na mauaji ya watoto wachanga kwani vinaonesha namna baadhi ya watu wasivyothamini uhai.

"Vitendo vya kutoa mimba na kuwaua watoto wachanga kisha kuwatupa kwenye mifuko ya rambo vinaonesha kuwa hawathamini uhai... Hata rushwa hutokana na moyo wa ubinafsi kwa watu. Ingawa Serikali inaipiga vita, lakini ni kama inapiga ngumi ukutani maana kibaya zaidi mpaka sasa sehemu nyingi huwezi kupata huduma bila kutoa rushwa," alisema.

Akisisitiza umuhimu wa jumuiya ndogo ndogo za kikristo, Padre Kilumanga alisema kuwa, Wakatoliki wanapaswa kujiunga katika jumuiya hizo na kushiriki kikamilifu bila kujali kuwa muumini ni mwanamke, mwanaume, kijana au mzee.

Alisema waamni katika jumuiya hizo washirikiane kujiletea mandeleo ya kiroho na kimwili.

Alisema katika jumuiya, Wakristo washirikishane kutafakari Neno la Mungu ili walifahamu vema kwani Wakristo wengi wana imani haba kwa kuwa hawalijui vema Neno la Mungu na kuliishi.

"Wanajumuiya washirikishane namna ya kukuza elimu ya imani. Si kwamba Wakatoliki hatuna imani, bali wengi wetu tuna imani haba.

Lengo katika jumuiya hizi liwe ni kukoleza na kuimarisha imani. Sisi Wakristo ni maskini wa elimu ya dini na dalili za hali hii ni utajiri wa matendo yetu yasiyo mema," alisema.

Aliyataja baadhi ya matendo hayo kuwa ni pamoja na watu kutodumu katika ndoa zao, udhaifu wa uelewano baina ya majirani, kutokuwa na amani na ukosefu wa ushirikiano miongoni mwa jamii. "Dalili hizi zinaonesha kuwa imani yetu ni duni na hivyo, tuna wajibu kuiimarisha zaidi."

Alisema jumuiya hizo zitumike kuhimiza sala, sakramenti, kutafakari Neno la Mungu na kuishi matendo mema.

Padre Kilumanga, aliongeza kuwa jumuiya hizo pia zinalo jukumu la kuhimiza jamii kuleta maendeleo na ujenzi wa taifa ikiwa ni pamoja na kushiriki chaguzi zote.

Aliwahimiza Wakatoliki kuongeza bidii katika kuitafakari Biblia kwa usahihi ili wasisumbuliwe na waamini wa madhehbu mengine ambao baadhi yao, huwarubuni kwa hoja potofu na hatimaye kuwateka.

Alisema, "Wakatoliki lazima wajue kuwa Biblia ndio mwongozo, msingi, dira; ni "Katiba mama" ya Kanisa. Usipojua Maandiko Matakatifu, huwezi kumjua Kristo.. Hivyo, ni muhimu tuyasome Maandiko Matakatifu, tuyatafakari na tuyaishi."

Aliongeza, "Katika jumuiya zetu tuwajue wenzetu wanaolegea kiroho na tuwasaidie... Jumuiya zisaidie kuwajua na kuwasaidia wenzetu wanaolegea kiroho. Pia, zitusaidie kutatua matatizo yetu ikiwamo migogoro ya wanandoa na kuwasaidie wanaohitaji msada wa huduma za afya na elimu lakini, hawana uwezo."

‘Wanaume tunzeni familia msimalize mishahara vilabuni’

Na Kevin Songambele, Mtwara

WANAUME wanaofanya kazi wameshauriwa kutofautisha muda wa kazi na sala ili kushiriki sehemu zote na pia, kuzijali familia zao badala ya kuzitelekeza na kumalizia mishahara yao vilabuni.

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Padre Silvanus Kessy, OSB, wakati akitoa mafundisho ya kiroho kwa wafanyakazi wa Abassia ya Ndanda. Mafundisho hayo yalifanyika Zakeo Ndanda.

Alisema, baadhi ya wanaume ambao ni wafanyakazi wamekuwa wakifanya makosa kupuuzia kwenda kanisani na kushiriki katika Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristo kwa visingizio vya kazi.

Kiongozi huyo wa kiroho aliilaumu tabia ya baadhi ya wanaume kutozijali na kuzihudumia ipasavyo na badala yake kujishirikisha na ulevi.

Alisema wanaume wakiwa wazazi, wazitunze familia zao na kuwajibika ipasavyo kimalezi.

"Inashangaza kuona wanaume wengi wanazitelekeza familia zao kwa kujali anasa.

Mtu anapokea mshahara wa mwisho wa mwezi. Badala ya kurudi nyumbani na kupanga bajeti, anakwenda kilabuni. Je, mnafikiri mtakuwa na maendeleo kwa hali hiyo?" alihoji.

Aidha, Padre Kessy alisema, jamii hususan Wakatoliki, haina budi kuifanya kazi kuwa ni changamoto ya kumshukuru na kumtumikia Mungu zaidi.

Alisema lazima wanaume watambue kuwa kupata kwao kazi ni zawadi waliyotunukiwa na Mungu hivyo, ni wajibu wao kumshukuru kwa imani, maneno na matendo sahihi.

"Mfanyakazi anatakiwa kusali zaidi kumshukuru Mungu kwa kumpa zawadi hiyo. Nadhani mnajua kuna watu wengi wenye elimu ya juu na ufundi wa aina mbalimbali, lakini hawana kazi. Hivyo, nawaombeni ndugu zangu tumshukuru Mungu kwa zawadi aliyowapatia.

YUDEF yataka wanafunzi vyuo vya ufundi kuwa wabunifu

Na Anthony Ngonyani

MTENDAJI Mkuu wa Shirika la Kuendeleza Vijana nchini (YUDEF), Sista Sandra Stich, amewataka wanafunzi wa vyuo vya ufundi nchini, kuwa wabunifu huku wakizingatia kuwa ubunifu ndio msingi wa kazi yao.

Sista Sandra alitoa kauli hiyo mwishoni mwa juma wakati akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Alisema moja ya matatizo makubwa yanayowakabili wanafunzi wa vyuo vya ufundi nchini ni ukosefu wa moyo wa kujituma miongoni mwao, na uzembe katika kubuni mitindo.

Alisema hali inawasababisha wanavyuo hao kuiga mitindo kutoka nje ya nchi.

"Ili fundi akamilike, anatakiwa kuwa mbunifu wa mitindo ya aina mbalimbali na kuacha kuiga mitindo kutoka nchi za nje kama Ulaya," alisema Sista Sandra.

Alisema hali hiyo ni aibu kwa mafundi kwani inaonesha kuwa hawana nia ya kujifunza kwa kubuni mitindo yao wenyewe bali wanategemea kuiga.

Sista Sandra alisema kuwa, ili kuondokana na tatizo hilo ni muhimu jamii ikawaandaa vijana kwa kuwajengea utamaduni wa kuwa wabunifu ili wawe mafundi bora wa baadaye.

Aliwataka vijana kuacha tabia ya kukata tamaa ya kujifunza kwa muda mrefu kwa kuweka mbele tamaa ya fedha.

"Baadhi ya matatizo yanayowakabili vijana ni kuwa hawataki kujifunza kwa muda mrefu na badala yake, wanatanguliza tamaa ya pesa," alisema.

Tohara kwa wanawake yazidi kushamiri

l Musoma hufanyika hadharani, Mbulu kwa kificho

Na Dalphina Rubyema

LICHA ya Kanisa Katoliki na Serikali kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu juu ya madhara ya tohara kwa wanawake, vitendo hivyo vimekuwa vikiendelea siku hadi siku kwa baadhi ya maeneo ambapo jimboni Musoma hufanyika hadharani na jimboni Mbulu hufanyika kwa kificho, imefahamika.

Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti na wajumbe kutoka katika majimbo ya kanisa katoliki ya Musoma na Mbulu wakati wakizungumza na gazeti hili mwishoni mwa juma jijini Dar es Salaam.

Wajumbe hao ni miongoni mwa washiriki wa Mkutano wa Mwaka wa Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki (CARITAS- Tanzania), uliofanyia katika Kituo cha Mafunzo na Mikutano cha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kilichopo Kurasini.

Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Maendeleo jimboni Musoma, Padre Julius Ogalla, alisema mapadre wa Jimbo la Musoma katika ibada za kila siku wamekuwa wakihubiri juu ya athari za tohara kwa wanawake lakini, bado hazijakoma.

Alizitaja baadhi ya athari hizo kuwa ni pamoja na hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa hatari wa UKIMWI kutokana na njia zinazotumika kufanya tohara hizo kutokuwa usalama.

"Tumekuwa tukihubiri kuwa ingawa wasichana wanao tahiriwa huwa na nyembe zao wenyewe, bado wapo hatarini kupata UKIMWI. Kwa sababu ngariba akimaliza kumkeketa msichana mmoja, anamwendea mwingine kabla hata hajanawa mikono. Sasa vidole vinakuwa vimejaa damu iliyochuruzika kutoka kwa yule wa kwanza," alisema Padre Ogalla.

Aliwataka wote wanaoshiriki vitendo hivyo, kutambua kuwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na Maandiko Matakatifu ya Mungu kwani katika Biblia Takatifu hakuna hata sehemu moja iliyoandikwa kwamba mwanamke afanyiwe tohara.

"Katika Kitabu cha Mwanzo sura ya 17: 10-14, Biblia inasema: ...Kila mwamume wa kwenu atatahiriwa... mwanaume asiyetahiriwa atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu..." alisema Padre Ogalla.

Aliongeza kuwa, hakuna sehemu yoyote katika Biblia iliyoandikwa kuwa watoto wa kike watahiriwe.

Hata hivyo, alikiri kuwa katika Jimbo la Musoma vitendo vya tohara kwa wanawake vilipungua kwa kipindi cha mwaka 2000, lakini vikaongezeka tena mwaka jana kutokana na kilichodaiwa kuwa wasichana ambao hawakutahiriwa mwaka juzi, hawakupata wachumba.

"Unajua makabila ya Musoma hususan Wakurya wanathamini sana tohara kwa wanawake. Mwaka 2000 hawakutahiriwa wasicha wengi lakini mwaka jana wengi sana walitahiriwa tena hadharani kwa madai kwamba wale ambao hawakutahiriwa mwaka juzi walikosa wachumba," alisema.

Hata hivyo, Padre Ogalla alikiri kuwa zamani mila za tohara kwa wanawake kwa kiasi fulani, zilikuwa na faida kwa sababu zilichangia kuwazuia wasichana kushiriki tendo la ndoa kabla ya ndoa.

Alisema kwa sasa mila hizo zimepitwa na wakati kutokana na kuwep kwa UKIMWI na pia, wasichana wanaofanyiwa tohara, hakuna anayekutwa akiwa bikira.

Alipendekeza Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), viongozi wa dini na viongozi wa mila na desturi kuungana pamoja na kukemea vitendo hivyo.

Naye mshiriki wa mkutano huo kutoka Jimbo la Mbulu ambaye hakutaka jina litajwe gazetini, alisema vitendo hivyo bado vinaendelea jimboni humo isipokuwa tofauti na Jimbo la Musoma, Mbulu hufanyika kwa siri.

Tunataka mapadre bora sio 'bora padre'-Askofu

Na Frt. Charles Kuandika, Songea

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Iringa, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa, amewataka vijana wa wito Upadre kote nchini, kuzingatia masomo na malezi yatolewayo katika seminari mbalimbali ili wawe mapadre bora wa kesho na siyo "bora mapadre"

Mhshamu Ngalalekumtwa aliyasema hayo hivi karibuni katika Seminari Kuu ya Peharamiho, Songea, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kufuatia ziara ya kichungaji inayofanywa na maaskofu watatu wa Kanda ya Kusini.

Alisema lengo la Kanisa Katoliki siyo kuwa na mapadre wengi bila kujali ubora wao bali Kanisa linalenga kuwatafuta mapadre bora watakaoifanya vema kazi ya Mungu.

"Lengo la Mama Kanisa siyo tu kupata mapadre wengi bali wawe wengi na bora ili waweze kufanya kazi vema katika shamba la Bwana," alisema Mhashamu Ngalalekumtwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Seminari Kuu ya Peramiho.

Akifafanua zaidi Askofu Ngalalekumtwa alisema kuwa, yeye pamoja na Askofu Mkuu Nobert Mtega wa Jimbo Kuu la Songea, na Askofu Bruno Ngonyani wa Jimbo la Lindi, walifanya ziara hiyo ya siku tano tangu Machi 6, Mwaka huu ili kuwatia shime mashemasi na mafrateri katika safari yao ya Wito wa Upadre.

Akiwakaribisha Maaskofu hao na kuwashukuru kwa niaba ya Seminari Kuu ya Peramiho, Gambera wa Seminari Kuu hiyo, Padre Titus Amigu, aliwataka wanajumuiya hiyo kushirikiana kwa dhati na maaskofu hao ili ziara hiyo ifikie malengo yaliyokusudiwa.

Alisema ni muhimu kufanya hivyo kwa kuwa ziara hiyo ni changamoto na bahati ya pekee kukaa pamoja na maaskofu kwa siku zote hizo.

Habari zaidi zinasema, kwa kipindi cha ziara ya maaskofu hao seminarini hapo, maaskofu hao wanashiriki shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiunga na shughuli za darasani wakisikiliza masomo na kujibu maswali ya walimu, kushiriki michezo mbalimbali, kazi za mikono na ibada.

TUKIO LA UGAIDI NCHINI MAREKANI

Watanzania watakiwa kupata fundisho

l CARITAS yatakiwa kufuta msamiati wa neno ‘huruma’

Na Dalphina Rubyema

TUKIO la kigaidi lililo fanyika nchini Marekani Septemba mwaka jana ,limetakiwa kuwa fundisho kwa Watanzania kuishi kwa kutegemea uchumi wake badala ya misaada kutoka nje.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),Padre Pius Rutechura wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Shirika la Misaada la CARITAS-Tanzania.

Mkutano huo ulimalizika mwishoni mwa juma kwenye ukumbi wa Baraza hilo.

Padre Rutechura alisema kuwa kitendo hicho cha kigaidi ambacho kilipelekea kulipuliwa kwa Jengo la Biashara la Kimataifa nchini Marekani, kilisababisha kuyumba kwa dunia nzima ambapo pamoja na mambo mengine,maelfu ya watu wamebaki bila ajira,kufilisika kwa mabenki, kushuka kwa uchumi na kupungua kwa misaada kwa mataifa maskini ikiwemo Tanzania.

Kufuatia hali hiyo,Katibu Mkuu huyo wa TEC, ametoa changamoto kwa washiriki wa mkutano huo ambao ni Waratibu wa CARITAS na Vitengo vyake kutoka Majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini, kutafuta mbinu zitakazo wezesha shirika hilo kuwa CARITAS isiyo tegemea zaidi wafadhili.

"Msamiati wa ‘HURUMA’ hauna tena nafasi. Kinachotakiwa sasa ni kuwahamasisha watu. Hamasa na kubadilishana taarifa lazima viwe miongoni mwa msamiati wa CARITAS," alisema.

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza Machi 6-8,uliandaliwa na CARITAS-Tanzania Makao Makuu ambapo pamoja na mambo mengine,washiriki walitoa taarifa za utendaji katika majinbo yao.

‘Watumishi wa Mungu elezeni wazi umungu wa Yesu’

Na Martin Amlima, Songea

MAPADRE na watumishi wote wa Mungu wamehimizwa kueleza bayana juu ya ukweli wa umungu wa Yesu bila kuogopa ikiwa ni pamoja na kukemea vikali uhalifu.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Gombera wa Seminari kuu ya Peharamiho Padre Titus Amigu, wakati akizungumza na waseminaristi na mashemasi wa Seminari Kuu hiyo.

Alisema Mhubiri wa Neno la Mungu hapaswi kuogopa lolote kwani yeye ni mjumbe kwa binadamu wote bila kujali cheo cha mtu.

Padre Amigu alisema mapadre wakiwa watumishi wa Mungu wahubiri Neno la Mungu kwa uwazi na usahihi mintarafu mapenzi ya Mungu na ukweli juu ya Umungu wa Yesu ili waishi kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Aliwaambia mashemasi na waseminaristi hao kuwa wakiwa mapadre watarajiwa wawakilishe na kuwaelimisha kwa usahihi na ujasiri waamini wao ili waijue vema na kuiishi imani yao.

"Wakristo wengi hawafahamu mambo mengi yanayohusu imani yao. Hii ni kwa sababu hawajaelezwa wala kuelimishwa ipasavyo’ alisema.

Alisema Mhubiri wa Neno la Mungu ni nabii na hivyo hana budi kuwa tayari kuufia ukweli uliopo katika imani kwani hutoka kwa Mungu.

Mchungaji wa KKKT awataka wanawake kuacha kwenda kwa waganga

l Asema dawa ya yote ni Mungu

Na Meryna Chillonji

WANAWAKE wa Kikristo nchini wametakiwa kuacha tabia ya kukimbilia kwa waganga wa kienyeji kutafuta suluhisho la matatizo yao na badala yake, wayapeleke matatizo yao mbele ya Mungu.

Mhubiri mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) katika usharika wa Kipawa, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Bi. Rose Kaneno, aliyasema hayo wakati wa ibada ya kuadhimisha siku ya kuombea wanawake duniani iliyofanyika hivi karibuni kanisani hapo.

Mhubiri huyo aliwashauri wanawake wote kutojishungulisha na waganga wa kienyeji na imani za ushirikina kwa namna yoyote na badala yake, wazidi kudumu katika imani yao na maombi huku wakitambua kuwa mwanadamu pasipo maombi, mambo yake hayawezi kumnyookea.

"Mungu anao uwezo zaidi ya mtu yeyote kwa sababu yeye ndiye muumba wa yote hivyo basi wanawake wenzangu msikubali kuwa watumwa wa shetani kwa sababu ya kuhangaika," alisema.

Aliongeza, "Inashangaza kuona mama na akili zake anahangaika kwenda kwa waganga eti kutafuta mtoto! Msihangaike, Roho Mtakatifu ndiye anayefanya kazi na hakuna mwingine. Kwa hiyo, msidanganyike na mambo ya kupita".

Pia, alitoa wito kwa akina mama hao kukazania kuomba kwani wasipofanya hivyo, mambo yote yataharibika.

"Mwanamke mpumbavu huvunja nyumba kwa mikono yake, lakini mwanamke mwelevu huijenga nyumba yake. Kwa hiyo, wanawake tusipokuwa imara, tunaweza kuiharibu jamii yetu sisi wenyewe," alisema.

Musoma, Tabora kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 ya Imani

l Musoma wazungusha Msalaba wa Jubilei Kuu, sanamu ya Bikira Maria vingangoni

Pd. Eduard Ntunde, Tabora na Mwandishi Wetu, Dar

WAKATI Parokia Katoliki ya Musoma, imezindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 mwaka huu kwa kuzungusha Msalaba wa Jubilei Kuu ya Mwaka Mtakatifu 2000 na sanamu ya Bikira Maria, katika vigango vyake, Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, limetoa wito kwa waamini wake kulichangia kwa hali na mali ili kufanikisha Maadhimisho ya Miaka 50 ya uinjilishaji katika Parokia ya Urambo yatakayofanyika Agosti 15, mwaka huu.

Mkurugenzi wa Mipango na Maendeleo wa Jimbo Katoliki la Musoma, Padre Julius Ogalla, ameliambia KIONGOZI mwishoni mwa juma jijini Dar es Salaam, kuwa maadhimisho hayo yalizinduliwa Februari 25, mwaka huu.

Alisema miongoni mwa shughuli muhimu zinazotekelezwa ni pamoja na kuwaandaa na kuwajenga waamini kiroho na kimwili.

"Pia, tutashughulikia ujenzi wa pango jipya la Bikira Maria na kuweka vigae kwenye sakafu ya kanisa zima," alisema.

Aidha, taarifa za kijimbo zilizopatikana mjini Tabora hivi karibuni, zimesema kuwa Jubilei hiyo katika Parokia ya Urambo ni miongoni mwa Jubilei zinazoadhimishwa katika parokia tatu jimboni humo.

Habari zimezitaja parokia nyingine zilizo mbioni kuadhimisha jubilei kuwa ni Ndono inayoadhimisha miaka 75 na Parokia ya Tabora Mjini ambayo inaadhimisha miaka 100.

Katika kufanikisha Jubilei hiyo, taarifa imesema watumishi wa Mungu na wanataaluma mbalimbali katika kanisa, wanaendelea kutoa mafundisho mbalimbali kwa washiriki na vikundi mbalimbali.

Imeongeza kuwa mafundisho hayo ni moja ya njia zinazotumika jimboni humo kuwahamasisha waamini kujiletea maendeleo yao wenyewe kiroho na kimwili.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Wana-Urambo, waamini wote wa Jimbo Kuu la Tabora na wote wenye mapenzi mema popote walipo, wanaombwa kuchangia kwa hali na mali kufanikisha maadhimisho hayo kwani yanalenga kuinufaisha jamii nzima.

Jubilei ya kumshukuru Mungu katika Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, ilizinduliwa rasmi Julai 15, mwaka jana na Askofu Mkuu Mhashamu Mario. A. Mgulunde wa Jimbo Kuu la Tabora.

Wahubiri watakiwa kufanya maandalizi kabla ya kuhubiri

Na Richard Timothy, RCJ,

WAHUBIRI wa madhehebu mbalimbali ya kidini nchini, wametakiwa kuwa makini na kujiandaa ipasavyo pindi wanapoenda kuhubiri Neno la Mungu.

Hayo yamesemwa na Msaidizi Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Kinondoni katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Lewis Hiza wakati alipokuwa akichangia mada katika kikao maalumu cha watumishi wa Jimbo hilo.

Katika kikao hicho kilichofanyika kwenye Usharika wa Mbezi Beach hivi karibuni, Mchungaji Hiza alisema kuwa, hivi sasa Wakristo na wasio Wakristo wanaielewa vilivyo Biblia hivyo, wahubiri hawana budi kuwa mahiri zaidi katika kutoa Neno la Mungu.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuepusha upotoshaji wa Maandiko Matakatifu.

Aliwataka wahubiri hao, hususan, wachungaji na wainjilishaji kufuta fikra kuwa baadhi ya Wakristo ni mbumbumbu wa Neno la Mungu.

"Wakristo wa leo wanasoma sana Biblia na kushiriki vipindi mbalimbali vya Neno la Mungu katika sehemu mbalimbali ikiwa ni pamoja na uinjilisti wa nyumba kwa nyumba...," alisema.

Wasabato waambiwa: Utakatifu ni wakati wote, siyo Jumamosi tu

Na Innocent Ndwewe,

WAAMINI wa Kanisa la Sabato wametakiwa kuwa Watakatifu wakati wote badala ya kujenga utamaduni wa kuwa watakatifu katika siku za sabato (Jumamosi) pekee.

Ushauri huo umetolewa hivi karibuni na Mchungaji mmoja wa Kanisa hilo, Joshua Malongo wakati wa Mkutano wa Injili ulioandaliwa na Kanisa hilo na kufanyika katika viwanja vya Mwananyamala jijini Dar es Salaam. Bado mkutano huo unaendelea.

Mchungaji Malongo, kutoka Kanisa la Sabato Temeke, alisema kuwa utakatifu wa kweli ni hali ya kufanya matendo mema wakati wote na mahali popote.

"Mtu unapaswa kuwa mtakatifu mahali popote, iwe kazini, shuleni, kwenye familia na mahali popote kwani Mungu yupo mahali popote," alisema.

Alisema, "Watu wengine wanajifanya watakatifu siku ya Jumamosi (Sabato), lakini siku hiyo ikisha pita tu, wanabadilika na kuendelea kufanya matendo ya uovu".

Mkutano huo ulianza Februari 24, mwaka huu na utamalizika Machi 16 mwaka huu. Wahubiri mbalimbali wa Kanisa hilo wamekuwa wakihubiri Neno la Mungu.

MFEC yawakopesha wananchi mifugo ya mamilioni

Na christopher Gamaina,Tarime

KITUO cha Maendeleo ya Kilimo cha Mogabiri (MFEC) wilayani hapa,kimewakopesha wananchi mifugo mbalimbali wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 28,imefahamika.

Kwa mujibu wa Meneja wa Kituo hicho, Bw.Godluck Kimara, mifugo hiyo ni pamoja na ng’ombe 88 wa maziwa wenye thamani ya shilingi milioni 26.4, mbuzi 20 wa maziwa wenye thamani ya shilingi milioni 1.4 na mbuzi wa nyama wenye thamani ya shilingi 220,000.

Meneja huyo ambaye alitoa maelezo hayo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi ofisini kwake mwishoni mwa juma, alisema kuwa utaratibu wa kukopesha mifugo hao ulifanyika kati ya Machi na Desemba mwaka jana lengo likiwa ni kuwainua wananchi kiuchumi.

Alisema kuwa, wananchi waliokopeshwa ni wale walio kwenye vikundi vya maendeleo, wakulima wadogo wadogo, wenye mashamba na malisho ya kutosha na waliokwisha shiriki mafunzo ya ufugaji bora ambayo hutolewa bure kituoni hapo.

Alisema kuwa kila mwananchi aliyekopeshwa ng’ombe mmoja alipewa sharti la kurejesha ndama jike wawili na aliyepewa mbuzi mmoja wa maziwa ama wa nyama, alitakiwa kurudisha mbuzi watatu.

"Baada ya kuturudishia sisi kilicho chetu, mifugo yote inayosalia, itakuwa ni mali ya mkopeshwaji,"alisema Bw. Kimaro.

Kuhusu kilimo cha mazao mbalimbali zikiwemo mbogamboga, Kimaro amesema kuwa, MFEC huwahamasisha wananchi kwa kutumia sinema na video kwa njia ya mikutano na kuwapeleka kujionea namna wenzao wanavyo shughulika.

Meneja huyo alisema kuwa MFEC inatarajia kukopesha wananchi jumla ya ng’ombe 30 wa maziwa na mbuzi 30 wa maziwa wote wenye thamani ya shilingi milioni 9.4 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Aidha, alisema kituo hicho kinatarajia kuongeza vijijini vya kuendeshea shughuli zake kutoka 24 vilivyopo kwa sasa hadi vijijini 30 ifikapo Desemba mwaka huu.

Aliongeza kuwa kituo hicho ambacho kipo chini ya Kanisa la Anglikana, pia kinatarajia kuanzisha mradi wa ufugaji wa nyuki kwa njia ya kisasa na ufugaji wa samaki wenye mabawa.