Wanaohofia madaraka wanaua, kuficha mafaili - Padre

lAtaka wenye mimba wasinyanyaswe

Na Peter Dominic

BAADHI ya watu hususan wenye madaraka wanaishi kwa hofu na wako tayari kuua ama kuficha mafaili ili waendelee kutawala, amesema Padre Paul Njoka.

Padre Njoka ambaye ni Paroko Msaidizi wa Parokia ya Chang’ombe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-Salaam, aliyasema hayo wakati akihubiri katika ibada ya Jumapili iliyopita parokiani kwake.

Katika ibada hiyo iliyoongozwa na padre Deogratius Mutefunya kutoka katika jimbo la Peoria, Illinois nchini Marekani ,padre Njoka alisema kutokana na hofu ama uchu wa madaraka watu wengi wanaishi kwa hofu na wako tayari kuua ili waendelee kutawala katika madaraka yao.

Akiwafananisha watu hao na Mfalme Herode ambaye katika enzi zake,Padre Njoka alisema kutokana na hofu ya kunyang’anywa madaraka aliwafunga watu mbalimbali na kuwaua wengine wakiwamo mama na watoto wake.

"Inasikitisha kuwa mpaka sasa bado tupo Maherode wengi tunahofu kuzingira maisha yetu na kunyang’anywa madaraka.....tunaamua kuua au kuficha mafaili kama alivyofanya Herode. Herode alikuwa akishuku kuwa huyu anaweza kumpinga au kuchukua madaraka yake alimuua" alisema.

Alisema jamii ishirikiane vema katika mambo yote hata katika kukabidhi madaraka.

Aidha aliwaasa wanajamii wenye tabia ya kuwasakama wanawake (wasichana ) wanaopata mimba na kuzaa bila kumjua baba wa mtoto waache tabia hiyo na badala yake, wampongeze mama na kumpelekea mtoto zawadi.

"Tusiwasakame waliozaa bila kujua baba bali tumpe mama pongezi kwa kuwapelekea zawadi mtoto aliyezaliwa... tumpe mama pongezi kwa kuwa amevumilia na wala hakutoa mimba wala kumtupa mtoto jalalani" alisema.

Akikemea tabia ya utoaji mimba katika jamii padre Njoka alisema "Akinamama; kwanini mtoe mimba; madaktari wanaume na wanawake hao wote hawana tofauti na Herode ni Maherodi na Maherodia".

Wakati huo huo: waamini wa parokia hiyo ya Chang’ombe jimboni Dar-es-Salaam, Jumapili iliyopita walifanya ‘Harambee’ kuchangia ukarabati wa kanisa, nyumba ya mapadre na choo. Harambee hiyo iliongozwa na padre Deogratius Mutefunya.

Harambee hiyo ya jumapili iliyopita ni sehemu ya utaratibu wa waamini kujiletea maendeleo yao kwa mchango wa kila mwezi. Kiasi kilichopatikana hakikufahamika mara moja hadi KIONGOZI linaondoka parokiani hapo.

Katika harambee ya Desemba 2, 2001 shilingi 280,640/ zilipatikana.

Mchungaji KKKT: Kama wanaume nao wangebeba mimba...

l Mwinjilisti asema ujauzito ni kipindi kigumu kwa walioolewa

Na Elizabeth Stephen

WAKATI Mchungaji mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), amesema wanaume waache kuwatelekeza wajawazito badala yake wajiulize kama nao wangekuwa wanapata mimba wangefurahi kufanyiwa hivyo, Mwinjilisti wa KKKT amesema ujauzito ni kipindi kigumu kwa baadhi ya walioolewa kwa kuwa hutelekezwa.

Mchungaji Heri Mwakabonga wa Usharika wa Mabibo External jijini Dar es Salaam, alitoa kauli hiyo akiwaonya wanaume wenye tabia ya kuwatelekeza wanawake baada ya kuwapa mimba. Alikuwa akihubiri katika ibada liyofanyika kanisani kwake Jumapili iliyopita.

Alisema, ikitokea wanaume hao wakabeba mimba, itakuwa fundisho kwao kwani watakuwa wameona machungu anayo yapata mama mjamzito.

"Mabinti wengi sana wamekuwa wakibeba mimba zisizotarajiwa, matatizo wanayoyapata ni makubwa ikiwa ni pamoja na kutengwa na familia zao, ndugu, jamaa na marafiki. Kinachoshangaza, wahusika wanapopewa taarifa hizo wanakataa mizigo hiyo bila kujali machungu waliyonayo mabinti hao," alisema.

Mchungaji Mwakabonga aliongeza, "Tabia hiyo huenda ikaisha miaka ijayo wanaume nao watakapobeba mimba ili waone cha mtema kuni, watakuwa wamejifunza machungu anayopata mama mjamzito".

Amewashauri wazazi na walezi kutowanyanyasa mabinti zao pindi wanapopata mimba kabla ya wakati muafaka. Alisema limekuwa jambo la kawaida kwa wazazi kuwanyanyasa mabinti zao hadi wengine wanafikia hatua ya kuwatenga eti kwa madai kuwa binti amebeba mimba kabla ya ndoa.

Mchungaji huyo alisema kuwa, wapo wazazi wengine wanaodiriki hata kuwatenga watoto wao wa kiume kwa kisingizio kuwa wamewapa mimba mabinti za watu.

Alisema kinachotakiwa ni wazazi hao kuwaelimisha zaidi na kuwaonesha upendo ili wasirudie tena pasipo kinyongo. "Ni bora ukailea hiyo mimba, huwezi jua huenda huyo mtoto atakayezaliwa akaja kukusaidia baadaye," alisema.

Hata hivyo Mchungaji huyo alisema kuwa, hali hii inatokana na wahusika wa pande zote mbili kufanya tendo la ndoa nje ama kabla ya ndoa. Alisema kutokana na kitendo hiki cha wasichana kupata mimba kabla au nje ya ndoa, mabinti wengi wamekuwa wakivuruga malengo na taratibu katika maisha yao.

Naye Ndechongio Charles anaripoti kuwa: Mwinjilisti Nitisile Wickson wa KKKT, amesema kipindi cha ujauzito kwa akinamama walioolewa ni kigumu sana katika maisha kwa kuwa wengine hutelekezwa na waume zao.

Alikuwa akihubiri katika Usharika wa Keko Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mwinjilisti huyo alidai kuwa wanaume wengi si wavumilivu na akawahimiza kuiga mfano wa Yusufu aliyevumilia na kutunza usafi wa moyo uliomwezesha Bikira Maria kumzaa Yesu.

Wicksona ambaye ni mwinjilisti mwanafunzi katika Chuo cha Uinjilisti cha Maneromango, alisema kuwa hali ya kushindwa kuvumiliana imesababisha matatizo katika ndoa nyingi zikiwamo za kikristo ambapo nyingine huvunjika.

Alisema mwanandoa yeyote "anayetembea" nje ya ndoa yake, anakabiliwa na dhambi ya wizi dhidi ya mwenzie na ile ya uzinzi.

Aidha, katika ibada hiyo iliyoongozwa na Mchungaji Astorn Kibona ambaye pia ni Mkuu wa KKKT Jimbo la Temeke, Mwinjilisti huyo mwanafunzi alisema kuwa endapo jamii haitaepuka dhambo zote ukiwamo uchoyo ipo hatari ya Wakristo wengi kuikosa mbingu pindi Yesu atakaporudi.

"Mbele ya Mungu dhambi ni dhambi tu...Kama ni uchoyo hakuna uchoyo mkubwa wala mdogo na hata wizi ni hivyo hivyo tusijidanganye eti kuna wizi mdogo au mkubwa’ alisema.

Aidha, alisema wazee wa kanisa na wanakwaya na watumishi wengine wa kanisa wanao wajibu mkubwa wa kuwa ushuhuda na mfano bora wa Kristo ili wasiomjua Yesu wamjue kwa kupitia imani na matendo yao bora.

Alionya kuwa hakuna mtu yeyote anayepaswa kubweteka kuwa atauona ufalme wa mbinguni kwa kuwa yeye ni muimbaji mzee wa kanisa au mtumishi yeyote bali ataingia kutokana na imani na matendo yake bora.

Dawa ya maandamano si virungu- Wachungaji Moravian

l Mwingine ataka Yesu ashuhudiwe moyoni si mdomoni

l Wakili awashangaa Wamoravian wasiojua Katiba, ataka elimu iende sambamba na Neno la Mungu

Na Josephs Sabinus

WACHUNGAJI wa Kanisa la Moravian Tanzania, wamesema virungu na mabomu ya machozi si dawa ya maandamano na hivyo, Jeshi la Polisi litumie nguvu kuwadhibiti wanaofanya fujo sio kuzuia maandamano.

Wachungaji Tuntufye Mkumbwa wa Ushirika wa Temeke na Mchungaji Salatieli Mwakamyanda wa Ushirika wa Keko, wote katika Wilaya ya Mashariki Jimbo la Kusini, waliyasema hayo wakati wakizungumza na KIONGOZI kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa juma.

Walisema kuwa, Jeshi la Polisi halipaswi kutumia nguvu zake kuzuia maandamano ya amani kwa kuwa ni haki ya kikatiba ya wananchi na badala yake, ielekeze nguvu katika kuwadhibiti wanaobainika kufanya fujo.

Mchungaji Mkumbwa alisema, kama Serikali inataka kuepuka kabisa maandamano, ijenge na kuimarisha utamaduni wa kuwasikiliza wananchi wake, kujadiliana na kutimiza yanayohitajika kwa wakati muafaka.

"Kwanini wasiwasilikilize (Serikali na Polisi) ili wananchi wapate nafasi ya kutoa dukuduku zao. Kama mioyo yao imejaa dukuduku wafanye nini kama wamekosa pa kuulizia? Hata hivyo, kama wamekwisha sema maandamano ni ya amani, waachwe waandamane kwa taratibu zilizowekwa na zinazokubalika," alisema Mchungaji Mkumbwa.

Pamoja na kusisitiza kuwa jamii haina budi kuwa na utii kwa vyombo vilivyopo madarakani, Mchungaji Mkumbwa alisema Serikali haipaswi kila wakati kuogopa maandamano kwa kuwa mengine ni ya furaha au amani.

"Watu lazima wazitii Mamlaka zilizopo maana hiyo inaagizwa hata katika Maandiko Matakatifu. Unapoitii mamlaka halali, unamtii Mungu na pia, hata walio katika mamlaka, wawatii walio chini yao na hapo pia, watakuwa wanamtii Mungu," alisema.

Hata hivyo, aliwaasa wananchi kuepuka maandamano ya kuiga mkumbo kwa kuwa mara nyingi mtu anayefanya jambo kwa kuiga mkumbo, humaliza vibaya.

Naye Mchungaji Mwakamyanda wa Ushirika wa Keko, alishauri kuwa, endapo kikundi fulani kimetoa taarifa ya maandamano ya amani, ni vema Polisi wakawaruhusu na kufuatilia kwa karibu kuona kuwa maandamano hayo yanafanyika kwa amani kwani kuyazuia kwa kutumia virungu na mabomu ya machozi si dawa sahihi.

"Kama wametamka kuwa wanataka maandamano ya amani, polisi wawafuate waone hatima yao. Hakuna haja ya kuwazuia, polisi watangulie na ving’ora wengine wakiwa nyuma; wakifanya mambo yao wafanye tu, kama ni kusema, waseme ila anayefanya fujo, huyohuyo ndiye akamatwe na kushughulikiwa," alisema.

Alisema binafsi haoni sababu ya msingi kwa upande wa Tanzania Bara kuzuia maandamano yaliyoelezwa kuwa ya amani na kwamba, afadhali kama ingekuwa Zanzibar ambako kuna vitisho vya milipuko ya mabomu.

Wakati huo huo: Mtheolojia mmoja katika Chuo cha Kanisa la Moravian Tanzania kilichopo Mbeya (MOTHECO), Noel Mwakalinga, amesema kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulete mabadiliko ya watu katika maisha hususan kiroho.

Akihubiri katika Ibada ya Jumapili katika Ushirika wa Shule ya Uhuru (Kariakoo) jijini Dar es Salaam, alisema, "Kukiwa na nuru ya Kristo moyoni mwako, amani itapatikana lakini siyo kumshuhudia Kristo mdomoni pekee wakati moyoni hayupo," alisema.

Katika tukio jingine: Wakili wa Ushirika wa Temeke wa Kanisa la Moravian Tanzania, Bw. Gibson Kisamba, amesema jamii haina budi kuhakikisha kuwa Neno la Mungu linakwenda sambamba na elimu kwa kuwa bila elimu si rahsi kusoma wala kuyatafakari vema Maandiko Matakatifu.

Akihubiri katika ibada ya Jumapili iliyopita kanisani kwake, Bw. Gibson alisema Wakristo wachangie uendeshaji huduma za Kanisa ikiwa ni pamoja na elimu, afya na huduma za kiroho.

"Wakristo wawajibike na kujitolea kwa Kanisa. Ni bahati mbaya kuwa Wakristo wengine hawajui mambo hayo. Hata baadhi ya Wamoravian inasikitisha kuwa hawaijui wala hawajawahi kuishika Katiba ya Moravian," alisema.

Alihimiza kuwapo kwa heshima katika kupata na kutumia mali kwani zote zinatoka kwa Mungu.

Waministranti wahimizwa kuboresha usafi wa roho, kimwili

Na Benjamin Mwakibinga

WATOTO wanaofanya kazi za utumishi wakati wa ibada katika parokia za Kanisa Katoliki, wametakiwa kufanya huduma hizo huku wakiishi maisha safi kwa vile wanatumikia katika nyumba takatifu ya Mungu.

Ushauri huo ulitolewa hivi karibuni na Mama Mlezi wa Vijana Watumikiaji wa Misa katika Parokia ya Manzese, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Bibi Pudensia Ndwambo, wakati wa sherehe maalumu za kuwatia moyo vijana wa parokia hiyo. inayavijumuisha vigango vya Mabibo na Tandale.

Bibi Pudensia alisema watumishi wa misa hawana budi kujua kuwa waamini wanapowaona mbele ya Altare ya Bwana wakiwa na mapadre, wanawapa heshima kubwa katika Kristo na hivyo, ni wajibu wao kuitunza na kuiendeleza heshima hiyo ya kiroho.

Alisema kwa kawaida, jamii huwatazama watumishi hao kama alama ya matendo na tabia njema kwa watoto wengine ndani ya jamii, kimwili na kiroho.

Alisema mtoto anayetumikia anatakiwa kuwa mfano wa kufundishia watoto wengine katika kuishi vema maisha ya Ukristo.

Mlezi huyo wa Vijana alisema kuwa, kitendo cha mtumishi wa misa katika Kanisa kusikika akijihusisha na vitendo vichafu vya kimwili na kiroho, vinaliabisha na kulifedhehesha Kanisa.

Katika kuwatia moyo vijana hao takriban 100, Bibi Pudensia aliwaambia kuwa huduma wanayoitoa ni kwa Mungu na wala si tu kwa parokia na kwamba huduma yao inafanyika kuwa baraka kwa waamini.

Aidha, aliwataka watoto hao kuacha kuishia tu katika utumishi wa Kanisa na vyama vingine vya kitume parokiani, bali wajitoe hata kuamua kuwa mapadre.

"Ninyi ndio mapadre wa Kanisa la kesho kwa hiyo, mkitumika vizuri hapa ndipo mnajiandaa kuwa mapadre wazuri kesho," alisema Bi. Pudensia.

Aliongeza kuwa, wakati umefika sasa kwa vijana wa Kitanzania kuitikia wito wa kumtumikia Mungu kwa njia ya Upadre badala ya kutegemea mapadre kutoka nje ya nchi.

Alisema vijana hao watakapopokea wito huo kikamilifu, watalisaidia Kanisa la Tanzania katika uinjilishaji ndani na nje ya nchi.

"Wenzetu sasa wanatushangaa sana sisi Waafrika kwa kutegemea sana mapadre wengi wa Kizungu kama vile sisi hatuna vijana wa kiume wanaoweza kuifanya kazi hiyo," alisema na kuhoji, "Muda uakapofika Mapadre hao wa Kizungu wakatakiwa kurudi kwao, nani atafanya huduma hiyo hapa kwetu?"

Awali, Paroko wa Parokia hiyo ya Manzese, Padre Manuel Gordejuela, aliwashukuru watoto hao kwa kusema kuwa kazi wanayoifanya ni Mungu pekee anayeweza kuwalipa.

Walemavu si watu maskini-SHIVAWATA

Na Neema Dawson

SHIRIKISHO la vyama vya Watu Wenye Ulemavu (SHIVAWATA) limesema kuwa walemavu siyo watu maskini ambao hawana uwezo wa kufanya kazi na upeo mdogo wa kuelewa kama baadhi ya jamii ya watu wanavyofikiri.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti Mstaafu wa shirikisho hilo Bw.Hosea Kalumuna wakati wa makabidhiano ya uongozi kati yake na uongozi mpya,makabidhiano yaliyofanyika katika Ofisi za Chama Cha Viziwi Tanzania (CHAVITA).

Bw.Kalumuna alisema kuwa walemavu wamekuwa wakitafsiriwa vibaya na kueleweka isivyo katika jamii lakini ukweli ni kwamba wao ni wafanyaji kazi wazuri na wako mstari wa mbele katika kujishughulisha na shughuli za ujenzi wa Taifa.

"Hakuna walemavu ambao ni tegemezi kwani wengi wanajishughulisha na shughulli mbalimbali"alisema Bw.Kalumuna.

Vile vile Mwenyekiti huyo Mstaafu wa SHIVAWATA ameutaka uongozi mpya chini ya Mwenyekiti wake Bw.Israel Kagaruki kudumisha umoja miongoni mwa walemavu wote na kuepuka migogoro , ubinafsi na majungu pamoja na kendesha shirikisho kwa maslahi ya walemavu wote.

Sambamba na hayo pia aliiomba serikali iwasaidie kwa kuwapatia walemavu ruzuku kama vyama vingine ili shirikisho hili liweze kujiendesha kwa kuanzisha miradi ambayo itatumika kwa kuwasaidia walemanvu ambao wako katika hali ngumu ya kimaisha.

Vile vile aliviomba vyama vya siasa vitambue uwezo wa watu wenye ulemavu na viwe na sera ambazo zinawatambua walemavu ambao nao ni miongoni mwa wapiga kura katika uchaguzi .

Viongozi waliochaguliwa kuongoza shirikisho hilo ni pamoja na Bw.Israel Kagaruki ambaye amechaguliwa kuwa Mwenyekiti, Makamu wake ni Bi. Eva Biswalo, Katibu Bw. Kaganzi Rutachwamagyo, Katibu Msaidizi Bw.Dickson Mreyange ambapo Mtunza hazina ni Bw. Abdallah Omary na Msaidizi wake akiwa ni Bi.Lupi Maswanya.

Tofautisheni Virus, UKIMWI - Askofu Kulola

Na Christopher Gamaina, Tarime

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Kimataifa la Evangelist Assemblies of God nchini(EAGT) ,Moses Kulola ameitaka jamii kotofautisha watu wenye Virus vya UKIMWI na wale unaougulia ugonjwa huo.

Askofu Kolola alitoa kauli hiyo Jumapili iliyopita alipokuwa akihubiri katika Mkutano Mkubwa wa Injili uliofanyika katika uwanja wa kanisa hilo lililopo mtaa wa Ronsoti mjini hapa.

Akitofautisha watu hao,Askofu huyo alisema kuwa watu wenye Virus nya UKIMWI inawezekana wakawa wanene na wenye afya nzuri daima tofauti na wagonjwa wa UKIMWI (AIDS) ambao hukonda na kupungua uzito kwa haraka pamoja na kuugua homa zisizo koma.

Alisema watu hawapaswi kudanganyika kwa kutazama tu kwa kuwachukulia watu wanene wote kuwa wako salama kwa kuwa wenye Virus huendelea kunenepeana hadi miaka kumi na ishirini kabla ya kuugua UKIMWI kulingana na chakula wanachotumia.

Aidha Askofu huyo wa EAGT alilaumu tabia ya baadhi ya watu katika jamii hususan vijana wanaoagizwa na viongozi wao wa kiroho kwenda kupimwa UKIMWI kabla ya kufungishwa ndoa lakini wanapofika mahospitalini huwahonga madaktari wahusika ili wawaandikie kuwa wako salama.

Aliwataka watu kuacha vitendo vya uzinzi na ulevi ambavyo ni kichocheo kikubwa cha maambukizi ya ugonjwa hatari wa UKIMWI licha ya kumaliza nguvu kazi lakini pia unaathiri watu kimwili na kiroho.

Wakati huo huo: Askofu Kalola amewaonya vijana wenye uroho wa ngono wanaorubunika kwa umbile zuri la mtu na hivyo kukubali kufunga ndoa za mitaani kwa kuwa kufanya hivyo mbali na kumkosea Mungu vile vile wana hatarisha na kujiharibia maisha yao ya baadaye.

Wananchi watakiwa kuwarithisha watoto makanisa ya kisasa

Na Anthony Ngonyani.

MWINJILISTI Wertony Liwachi Mtokambali amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa makanisa ili wawaachie watoto wao urithi wa makanisa ya kisasa lengo likuwa ni kuimarisha imani za watoto hao.

Mtokambali aliyasema hayo mwanzoni mwa wiki hii wakati alipokuwa akihubiri katika Kanisa la Anglikana la Watakatifu Wote Dinari ya Temeke jijini Dar es Salaam.

Alisema ni wajibu wa wazazi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa makanisa na sio jukumu la wafadhili na wanachi wachache wenye fedha kufanya kazi hiyo peke yao.

Alisema wananchi wengi wamejiwekea utaratibu wa kuwaachia urithi watoto wao vitu vya kifahari ikiwa ni pamoja na magari na nyumba na wanasahau kuwaachia makanisa yaliyo bora.

Vile vile Mwinjilisti Liwachi Mtokambali ambaye alitoa mahubiri yake wakati wa Misa ya Sikuu ya Ufunuo wa Yesu Kristo, aliendesha harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa hilo.

Katika harambee hiyo jumla ya shilingi 32,000 zilipatikana.

Kubalini Yesu awatamie kama kuku anavyotamia mayai-Padre

Na Getrude Madembwe

WAAMINI wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo nchini,wametakiwa kukubali kutamiwa na Yesu kama kuku anavyo yatamia mayai yake.

Ushauri huo umetolewa na Padre Wilfred Kwayo wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu alipokuwa akihubiri katika ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Parokia ya Kawe Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Akifafanua zaidi juu ya kauli yake hiyo,Padre Kwayo alisema kuwa wale watakao kubali kutamiwa na Yesu, matunda yake watayaona baada ya muda mfupi na wale watakao kataa watakuwa wameharibika kama mayai viza ambayo yalikata kutamiwa na kuku.

Padre Kwayo alifafanua zaidi kauli yake kwa kutoa hadithi ifuatayo:-

"Kulikuwa na mayai kumi ambayo yalikuwa yametagwa na kuku, ilifikia kipindi yale mayai yalitaka kujua hatima yake ndipo siku moja mayai hayo yaliamua kumuuliza kuku kuwa wataendelea kukaa katika hali hiyo mpaka lini?".

"Kuku aliyaambia mayai hayo kuwa kama yanataka kubadilika ni lazima kwanza ayatamie kwa muda wa siku 21 ili yabadilike.Mayai matano yalikubali na mengine matano yalikataa".

"Yaliyokubali baada ya siku 21 yalibadilika na mengine matano yaliyokataa yalioza na kuwa mayai viza".

Kutokana na hadithi yake hiyo,Padre Kwayo aliwataka Wakristo wasikubali kuwa yale mayai matano yaliyokataa kutamiwa kwani wakifanya hivyo watakuwa wameoza na hawatafaa mbele za Bwana".

Aidha Padre Kwayo amewataka wanawake kuacha kutumia vidonge vya Uzazi wa Mpango vinavyojulikana kama safe plan, kwa vile vinaenda kinyume na matakwa ya Mungu.

Padre Kwayo ambaye pia ni Mlezi wa nyumba ya vijana wanaojiunga na Shirika hilo lilipo katika Jimbo Katoliki la Moshi aliwataka wanawake wanaotumia vidonge hivyo kuacha tabia hiyo mara moja na badala yake waige mfano wa Bikiara Maria.

"Kama Bikira Maria angetumia vidonge hivyo isingekuwa rahisi kwake yeye kupata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu"alisema.

Aliongeza kwamba wanaotumia vidonge hivyo huwa wanaharibu utaratibu mzima wa kupata mimba.

"Wanawake wanapotumia vidonge hivyo huharibu kabisa utaratibu wa upataji mimba .Sasa kama Bikira Maria angekuwa anatumia vidonge isingekuwa rahisi kwake yeye kuwa mjamzito sababu sehemu ya kuhifadhi mtoto pangekuwa pameharibiwa na vidonge hivyo" alisema Padre Kwayo.

KKKT Dar wataka vijana Mbeya kuacha mataputapu

l Vijana Keko warejea, Mchungaji awapongeza

Na Josephs Sabinus

VIJANA mkoani Mbeya wameshauriwa kuepuka ulevi wa aina zote ukiwamo wa pombe za kienyeji na badala yake waelekeze nguvu zao katika kumtumikia Mungu kama ilivyokuwa kwa wazee.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Keko Dayosisi ya Mashariki na Pwani Bw. Edwin Kimaro.

Alikuwa akizungumza na KIONGOZI mintarafu safari ya vijana hao waliyoifanya mkoani Mbeya.

Katika mazungumzo hayo ya Jumapili iliyopita mhusika huyo ambaye pia ni Katibu wa umoja huo Bw. Elineema Masawe Kimaro alisema kuwa katika ziara yao katika mkoa huo wamebaini kuwa mwitikio wa wazee katika kumtumikia Mungu ni mkubwa kuliko mwitiko wa vijana.

Alisema mwitiko wa vijana kati ya miaka 12-20 katika utumishi wa Mungu ni duni kwa kuwa wengi wao wameelekeza nguvu zao katika ulevi.

Alisema vijana wote hawana budi kutumia kipindi kilichopo sasa kuachana na vitendo visivyo na manufaa kwao na badala yake watumie muda uliopo na mali waliyonayo kuandaa maisha yao baadaye duniani na mbinguni.

Kwa pamoja Bw. Kimaro na Elineema walisema kuwa katika ziara yao walitembelea sharika ya Kandete, Tukuyu, Ipinda na Mihanji katika Dayosisi ya Konde ya KKKT. wakiwa Mahanji walitembelea vijiji vya Mahenge na Sebe.

Kwa mujibu wa viongozi hao wa vijana wa KKKT wa Keko jijini Dar wakiwa ziarani vijana hao walitoa huduma ya uinjilishaji kwa njia ya nyimbo, maigizo,mikutano ya Injili (mahubiri) na vipindi vya maombi.

Walishiriki matamasha ya kuchangia ununuzi wa vyombo vya kwaya ambapo katika usharika wa Kandete zilipatikana shilingi 170,000 na Mahanji zilipatikana shilingi 112,000 zikiwa ni pesa taslimu na ahadi.

Wakitoa taarifa ya kurejea kwao kwa waumini Jumapili iliyopita Mkuu wa Jimbo la Temeke na ambaye pia ni mchungaji wa usharika huo Astorn Kibona aliwapongeza kwa kushiriki uinjilishaji kwa watu. Alisema moyo huo hauna budi kuigwa na watu wengine.

Siku chache kabla ya sikukuu ya Krismasi vijana 28 walifanya ziara ya kichungaji katika jimbo la Konde la KKKT mkoani Mbeya.

Walioshiriki ziara hiyo ni pamoja na Mwinjilisti Emmanuel Duge Mzee wa Kanisa Mama Kalokola mwalimu wa Kwaya John Myavilwa na Bw Stanley Kilasi.

Wengine ni Elineema Masawe, Edwin Kimaro, Jane John, Stanly Kilasi, Dafroza James, Erick Kwijage na Onesmo Mwasumbi.

Wengine waliokuwa katika ziara hiyo ni Twelu Jumande, Grace Sijanga, Steven Kilasi, Elizabeth Charles,Modestus Kikwete, Godfrey Ezekiel, Lusline Mwanza, Joyce Samwel na Dickson Mwamasage.

Wengine ni Okisima Kamulali, Lydia Manisya, Lusekelo Mulenga, Nevile Meema, Brison Mboka, Suzana James, Paulina Gondwe, Pendael Lameck, Benjamin Mdoe, Remmy Dizombe na Gabriel Zacharia.

Moshi kupata mashemasi sita

l Masista wanane waadhimisha Jubilei

Na Mwandishi Wetu, Moshi

WASEMINARISTI sita wa Jimbo Katoliki la Moshi, wanatarajia kupata daraja ya ushemasi kati ya Januari 25 na Januari 29 mwaka huu.

Taarifa kutoka ndani ya Jimbo hilo zinasema kuwa Mashemasi hao watarajiwa,watapata daraja hiyo kutoka katika Seminari Kuu ya Segerea iliyopo katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam,Semiari Kuu ya Kipalapala jimboni Tabora na Parokia ya Njiro,Jimbo Kuu la Arusha.

Taarifa hiyo ya kijimbo imesema kati ya Waseminaristi hao wawili ni wa jimbo,wawili wa Maisha ya Kitume ya Kazi za Roho Mtakatifu na wawili ni wa Shirika la Mateso (Passionists).

Taarifa hiyo imewataja mashemasi hao watarajiwa kuwa ni Reginald Sipendi,Landelin Makiluli (Jimbo Moshi),Prascus Massawe na Josefati Kiwori (Passionist). Wengine ni Antipas Tarimo na Innocent Samson Mkwe wote wa Maisha ya Kitume ya Kazi za Roho Mtakatifu (ALCP/OSS).

Taarifa hiyo imewatakia Mashemasi hao watarajiwa ,neema na baraka tele za Mungu pamoja na kuwatakia matayarisho mema kwa Dalaja ya Upadre.

Wakati huo huo: Masista wanane wa Jamii ya Kazi za Kitume ya Roho Mtakatifu jimboni humo,wameadhimisha Jubilei ya miaka 25 ya Uwakfu. Sherehe za maadhimisho hayo zilifanyika hivi karibuni katika Makao Makuu ya Shirika hilo yaliyopo eneo la Rauya jimboni humo.

Taarifa ya kijimbo imewataja wajubileri hao kuwa ni Sista Akwilina Orotha,Sista Anastasia Swai,Sista Crispina Lyimo na Sista Clara Zachariah. Wengine ni Sista Flora Mrosso,Sista Philomena Ngalo,Sista Restuta Mamremi na Sista Theresia Urassa.