Ukosefu wa upendo, rehema, chanzo cha ugaidi - Pengo

l Asema haki si kwa njia ya jino kwa jino

l‘Akina mama kuweni chimbuko la upendo na amani’

Na Eric Samba

UKOSEFU wa upendo na rehema katika familia nyingi ndiyo chanzo cha maovu duniani ukiwemo ugaidi, amesema Kardinali Pengo

Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ambaye ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la dar es Salaam, aliyasema hayo wakati akihubiri katika Ibada maalum ya Kuaga Mwaka 2001 na kukaribisha mwaka 2002. Ibada hiyo ilifanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosef, jijini Dar es Salaam.

Alisema kutokana na ukosefu wa upendo wenye rehema (huruma) katika familia, jumuiya, jamii na mataifa, watoto wengi hukimbia familia zao na kuingia mitaani ambapo huonja ukatili wa ajabu.

Kutokana na hali hiyo, Mwadhama Pengo alisema watoto hao na watu wazima hujiona hawana cha kupoteza wala kutegemea hapa duniani na hivyo, kuwa tayari kufanaya chochote kujidhuru ama kuwadhuru wengine.

"Mtoto akikosa upendo nyumbani atatoka kwenda mitaani huko atajiingiza katika maovu na kutendewa ukatili. Hivyo, ataiona hali hiyo kuwa ni ya kawaida na hata kudhania kuwa hata kama angekuwa nyumbani, angetendewa hivyo," alisema.

Pia, alisema ili kuwa na amani duniani, lazima haki itendeke kwa kila mtu bila ubaguzi wa namna yoyote.

Alisema haki si ile ya kulipiza kisasi kwa kutumia sera ya "jino kwa jino" au "jicho kwa jicho" ambayo watu wengi huifikiria kimakosa kuwa ni muafaka katiaka kupatikana kwa haki.

"Tunafiki eti ikiwa mtu amemuua ndugu yangu, basi nina haki ya kulipiza kisasi, basi hiyo ndiyo haki, si kweli," alisisitiza.

Aliwataka wanawake kuwa chimbuko la upendo na haki katika familia, jamii na mataifa ili kurekebisha hali inayozidi kuwa mbaya.

"Tuwaombee akina mama ili wawe chanzo cha upendo na haki, kwani hali mbaya hutokea ndoa inapovunjika na mama kuondoka, watoto huamua kuondoka nyumbani," alisema Pengo.

Kauli ya Kardinali Pengo imekuja wakati ulimwengu umo mashakani kwa kusumbuliwa na tatizo la ugaidi na uskosefu wa amani, huku Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili akiwataka wanadini wote kuombea amani duniani.

Ndoa za jinsia moja ni aina ya uchunaji ngozi - Kanisa la Kristo

Na Josephs Sabinus

NDOA za watu wa jinsia moja na ubakaji zimeelezwa kuwa ni aina nyingine ya uchunaji ngozi za binadamu kwa kuwa vyote vinalenga kutoa kafara kwa miungu.

Wakizungumza kwa pamoja ofisini kwao jijini Dar es Salaam katikati ya juma, Mwinjilisti William Ngwira na Mwanakamati mmoja wa Kamati ya Uinjilisti, Joseph Maro; wote wa Kanisa la Kristo la Magomeni jijini Dar es Salaam, walisema vitendo hivyo ambavyo vimesikika zaidi katika kipindi cha mwaka uliopita, vina asili moja ya kuabudu dini zainazokiuka mapenzi ya Mungu wa kweli.

Wakizungumzia vitendo hivyo, Bw. Maro alisema, "Uchunaji ngozi za watu upo katika dini feki za watu ambapo watu hao hutumaini vitu fulani ili kufikia mafanikio badala ya kumtumaini Mungu.

Hao, wana miungu yao inayowatuma kufanya hivyo na uchunaji ngozi au ubakaji hautofautiani na kumuua mtoto wako au mzazi wako ili utajirike; hizi zote ni kafara tu, ni unyama."

Naye Mwinjilisti Ngwira alisema, "Mtu anayefikwa na tamaa ya kuchuna ngozi za binadamu mwenzake anakuwa na tamaa mbaya mno, ameangalia biashara zaidi na kutaka kutajirika bila kufanya kazi halali kama anavyoagiza Mungu.

Hata ivyo, matatizo haya ya uchunaji ngozi, ubakaji na hata haya mambo ya UKIMWI, yanatokana na viongozi waliopo kuanzia ngazi ya familia kutowajibika vizuri katika jamii kimaadili na kiroho."

Wakizungumzia ndoa za jinsia moja pamoja na vitendo vya ubakaji, walisema vitendo hivyo havina budi kupigwa vita na wote wanaomfahamu na kumtumaini Mungu kwa kuwa vinakwenda kinyume na Maandiko Matakatifu.

"Hata katika Maandiko Matakatifu, Mungu aliwagiza wanadamu wazae na kuongezeka ili waijaze dunia, sasa vitendo vya kuingiliana kimwili kinyume na maumbile vinawezesha mtu kupata mtoto ili watu waongezeke?" alihoji Mwinjilisti Ngwira.

Alitaka jamii kuishi kwa mfano wa Yosefu mume wa Bikira Maria ambaye aliutunza usafi wa moyo.

"Viongozi wote wahimize kwa vitendo watu watii Amri na mapenzi ya Mungu sio matumizi ya kondomu. Watu waishi kwa usafi wa Moyo kama alivyoishi Yosefu," alisema.

Alisema unampomgawia mtu kondomu na kumhimiza awe na mpenzi mmoja ili kuepuka UKIMWI, una halalisha tendo la ndoa nje na kabla ya ndoa hali inayopingana na Mungu kwa kuwa hakuna sehemu katika Biblia iliyoandikwa kuwa kila mtu awe na mpenzi wake mwenyewe bali imeandikwa: Kila mtu awe na mke wake mwenyewe.

Naye Bw. Maro alisema, "Ndoa ya jinsia moja ni uchunaji ngozi mwingine. Sheria ya Mungu ni moja kuwa mwanamke aoane na mume, hakusema mwanamke aoane na mwanamke au mwanaume aoane na mwanamume.

Hata hivyo, Bw. Maro alisema jamii haina budi kumfahamu na kumtafuta Mungu wa kweli kwa kutumia Kanisa badala ya kujiangamiza kiroho kwa kutumia dini mbalimbali zisizo na maana.

Alizitaja dini zilizopo sasa kuwa ni zile zinazoabudu vitu vinavyoonekana, dini za mila na desturi, dini zilizoanzishwa na watu pamoja na dini zinazoutambua na kuukiri Ufalme wa Mungu (Kanisa) ambazo alisema ndizo zinastahili kuzingatiwa.

Kanisani si dampo la pesa mbovu-Mchungaji TAG

Na Jenifa Benedicto

MCHUNGAJI wa Kanisa la Tanzania Asemblies of God, Ilala, Titus Mukama amewataka waumini wa madhehebu hayo kumthamini Mungu na kumpa kilicho bora badala ya kutoa pesa ambazo zimechakaa kanisani hapo kama sadaka.

Mchungaji Mukama aliyasema hayo wakati wa ibada ya shukrani kwa kufika mwaka 2002 iliyofanyika katika ukumbi wa Vijana ,Amana jijini Dar Es Salaam.

Alisema kuwa watu wengi hufikiria kuwa kanisani ni mahali pa kupeleka pesa ambazo zimechakaa kitu ambacho alisema kuwa si kweli.

Alisema katika kukomesha tabia hiyo ambayo inaoneka kuwa kero ,kanisa lake litatoa bahasha kwa kila muumini kwa ajili ya sadaka na kila mmoja wakati wa matoleo atatakiwa kuandika jina lake juu ya bahasha hiyo.

"Ili kukomesha tabia hiyo, tutaanzisha mtindo wa watu ambao wanataka kumtolea Mungu sadaka ya shukrani kuandika majina yao juu ya bahasha"alisema Mchungaji Mukama.

Alisema kuwa mtindo huo wa bahasha utawawezesha viongozi wa kanisa kumtambua mtu ambaye ametoa pesa ambayo imechakaa na wao watamuita ili kumuonya.

Wakati huo huo : Mchungaji Mukama amewataka waumini hao kuwa wanyenyekevu mbele za Bwana hasa katika mwaka huu wa 2002.

Alisema kuwa kuanza mwaka kwa unyenyekevu ni vizuri na wao watabarikiwa katika kazi zao na hata maisha yao ya kila siku.

Akitumia Maandiko Matakatifu toka katika kitabu cha Mika 6:8.

Mchungaji huyo alisema;Mungu humwangalia mtu anayetenda haki na anayeenenda kwa unyenyekevu pamoja na anayependa rehema.

"Kumpendeza Mungu ni kutenda haki, kutetemeka mbele zake kusamehe watu waliowakosea pamoja na kuishi maisha ya Utakatifu"aliasa.

Alisema kufikia mwaka huu ni wema wa Mungu kwani watu wamefariki dunia na wengine ni wagonjwa.

Aliongeza kusema kuwa mwaka uliopita kila mtu alipitishwa katika mapito yake, bali Mungu amewashindia ili waweze kumtolea Bwana sadaka iliyo hai na ya kumbariki.

MAPAMBANO YA UKIMWI MWAKA 2002:

KKKT laitaka Serikali ifunge viwanda vya bia, baa

l Lasema heri uchumi uanguke watu wasife ovyo

l Chonde chonde wenye UKIMWI muwe na huruma

Na Josephs Sabinus

KANISA la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT Jimbo la Temeke limesema ili kupambana na UKIMWI serikali ipige marufuku utengenezaji na uuzaji wa pombe kwani sasa pombe imekuwa sumu inayoua watu na pia, amewataka wenye UKIMWI kuwa na huruma ili wasiambukize wengine.

Mkuu wa KKKT Jimbo la Temeke mchungaji Astorn Kibona aliyasema hayo wakati akizungumza na KIONGOZI ofisini kwake katikati ya juma jijini Dar es salaam.

KIONGOZI lilitaka kujua mawazo yake ili kupambana na janga la UKIMWI katika kipindi cha mwaka 2002.

Alisema bado UKIMWI ni tishio licha ya juhudi za serikali na dini mbalimbali kwa kuwa uzalishaji, uuzaji na unywaji wa pombe unachangia watu kupuuza kanuni za kuepuka UKIMWI.

Kibona ambaye pia ni Mchungaji wa Usharika wa Keko wa kanisa hilo alisema serikali haipaswi kuendelea kuzalisha na kuuza pombe huku ikijua kuwa pombe hiyo inachangia vifo vya wananchi wake.

Gazeti hili lilipotaka kujua kama hali hiyo haitaathiri pato la taifa na kuangusha uchumi wa nchi kwa jumla mchungaji Kibona alisema kuwa hali ya kuendelea kuzalisha pombe ikijulikana kuwa pombe hiyo inachangia vifo na maafa kwa watu ni kutahimini pesa kuliko uhai wa wananchi.

"Kipo bora, kuangamiza uhai wa watu ili kuongeza pato la taifa au kuokoa uhai wa watu kutengeneza pombe na kuiuza kwa watu huku ikijulikana wazi kuwa inasababisha maambukizi ya UKIMWI ni sawa na kutengeneza sumu na kuwauzia wananchi" alisema

aliongeza, "Njia za kuongeza pato la taifa ni nyingi. Matunda yanaoza mashambani kwa wakulima inabidi viwanda viongozwe na hata kusogezwa vijijini ili matunda yanayozalishwa yatengenezwe juisi hata watoto wadogo wanywe.

Inashangaza sana viwanda vya bia na stoo za bia zinafanya kazi usiku na mchana kuliko hata viwanda vya nguo juisi na vitu vingine.

Hii yote ni kwa kuwa siku hizi watu wanajali faida. Hivi faida inayoangamiza uhai wa watu ni faida gani hiyo? Serikali kama iko serious (makini) na vita dhidi ya UKIMWI, ipige marufuku baa zote pamoja na tabia ya kutumia sherehe kwa ajili ya mikesha mbalimbali".

Alifafanua kuwa, mikesha katika sherehe nyingi huambatana na ngoma mbalimbali na ulevi hali ambazo alisema huchochea maambukizi ya UKIMWI kutokana na vitendo vya zinaa.

Alisema jamii itumie mikesha ya sikukuu za kidini kwa sala katika nyumba za ibada na nyumbani badala ya kufikiri kuwa sherehe ni lazima kukesha katika kumbi za starehe.

Aidha, Mkuu huyo wa Jimbo alitoa wito kwa wenye ugonjwa wa UKIMWI kuguswa na dhamiri ya Kimungu ili wasiwaambukize wengine kwa makusudi kwa kuwa kitendo hicho ni dhambi ya mauaji.

Siri katika ndoa ni sumu kali- Kanisa Katoliki

l Monsinyori ataka barua za siri katika ndoa zichanwe

Na Pd. Raphael Kilumanga

KANISA Katoliki limeielezea tabia ya usiri miongoni mwa wanandoa kama chanzo hatari cha kusambaratika kwa ndoa.

Hayo yalisema Jumamosi iliyopita na Katibu Mtendaji wa Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Monsinyori Julian Kangalawe wakati akizungumza katika ibada ya ndoa baina ya Bw. Ildefonce Lilanga na Bi. Esther Mathew, iliyofanyika katika Kanisa la TEC.

Alisema katika maisha ya ndoa, hakuna kitu chochote ambacho mwanandoa mmoja anapaswa kukifanya kuwa siri yake pekee na hivyo, kumficha mwenzie kwa kuwa wote ni kitu kimoja.

Monsinyori Kangalawe alisema kuwa, tabia ya wanandoa kufichana baadhi ya mambo muhimu ni hatari kwao wenyewe na katika ndoa yao ambayo ni mpango na upendo wa Mungu.

"Tabia ya kuwa na siri katika ndoa ni hatari na inaweza kuharibu na kusambaratisha ndoa yenu...Barua zote za siri chaneni tena zichanwe na mwenzako wa ndoa baada ya kumuonesha. Siri ya mke amjulishe mume na siri ya mume amjulishe mke," alisema Monsinyori Kangalawe.

Alisisitiza kuwa marafiki wote wa mmoja wa wanandoa wanapaswa kujulikana kwa wanandoa wote na kuwa marafiki wa familia kwa kuwa marafiki wa siri ni rahisi kuchakaza ndoa.

"Marafiki wa siri wanaweza kuchakaza ndoa kwa sababu ndoa ni upendo wa Mungu," alisema.

Alisema kwa kuwa ndoa ipo ili kuendeleza upendo wa Mungu kwa wanadamu, kila mwanandoa hana budi kujiona kama zawadi ya mmoja kwa mwingine.

"Mume awe zawadi kwa mke na mke awe zawadi kwa mume katika maisha yote ," alisema.

Akifafanua zaidi maana ya upendo wa watu wa ndoa, Monsinyori Kangalawe, alisema upendo huo hauna budi kutafuta faida ya mtu mwingine yaani, ni upendo ambao Wayunani wanauita, AGAPE.

Alisema, "Agape ni upendo unaomtafutia mwingine faida... Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtuma Mwanawe wa Pekee ili mwanadamu apate faida; yaani ukombozi; na kwa kuwa Mungu ni upendo, alipenda upendo huu uendelee ndipo akamuumba mwanadamu kwa mfano wake na kumtaka aendeleze upendo huo."

Aliwasisitiza wanandoa hao kuifanya familia yao kuwa makao ya Baba, Mwana na Roho Mtakatifu kwa kudumisha upendo baina yao najamii nzima.

Wanaodai Yesu si Mungu wanafanya marudio-Paroko

Na Peter Dominic

KIONGOZI mmoja wa Kanisa Katoliki nchini, amesema kuwa propaganda zinazoenezwa juu ya kupotosha ukweli kuwa Yesu si Mungu,hazilikasirishi Kanisa kwa vile si mara ya kwanza kuwepo kwa kauli kama hizo.

Akihubiri katika Ibada Takatifu ya mkesha wa Mwaka Mpya, kiongozi huyo Paroko wa Parokia ya Mtoni katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padre Edward Devis alisema miaka 2000 iliyopita , baada ya Kristo, alizaliwa mtu mwingine akawafundisha watu kuwa Yesu si Mungu, hivyo hao watu wanaosema tena Yesu si Mungu,hawana budi kufahamu kuwa hiyo ni marudio.

Mwaka jana kijana mmoja kutoka Morogoro, alibeba bango kupinga ukweli kuwa Yesu si Mungu kwa lengo la kuwakasirisha Wakristo, lakini hakufaulu kulikasirisha Kanisa kwa vile, si mara ya kwanza kuwepo kwa mtu kama huyo.

Padre Devis alisema kuwa,wengi wanaosema Mungu hayupo, hawana budi kutambua kuwa Mungu anawacheka tu anaposikia wanasema hivyo.

Hata hivyo Padre Devis alisema imani ya watu hapa duniani ni tofauti hivyo Kanisa Katoliki linaheshimu imani ya watu wengine.

"Tunawahurumia wale ambao hawajapata Habari Njema ya Yesu, Mwana wa Mungu ambaye ndiye Mkombozi," aliongeza.

Mnamo mwaka jana, kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Hamis Rajabu Dibagula, alibeba bango na kukatiza katika mitaa akipinga imani ya wakristo kuamini kuwa Yesu ni Mungu, hali ambayo ilipelekea kukamatwa kwake na kufunguliwa mashitaka ya uchochezi na kuhatarisha amani ya nchi.

Hukumu iliyotolewa na vyombo vya sheria huko Morogoro baada ya kumtia hatiani, ilisababisha waumini wa dini ya kiislamu Mkoa wa Dar es salaam na maeneo mengine nchini kuandamana hali ambayo ilielekea kuhatarisha amani ya nchi.

Hata hivyo adhabu ya kifungo cha miaka miwili kwa Dibagula, ilitenguliwa na Mahakama Kuu nchini.

Paroko huyo alisema kuwa siku hiyo ya mkesha wa mwaka mpya ni siku kuu ya Mama wa Mungu na inasisitiza Umungu wa Mtoto Yesu.

"Hatuwezi kusahau kuwa Mungu alifika kwetu kupitia kwake Bikira Maria," alisema na kuongeza, "Tuanze mwaka kwa kutumia sala ya Maria."

TEC wahimiza shukrani kwa Mungu

Na Pd. Raphael Kilumanga

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), licha ya kuwahimiza waamini kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuuanza vema mwaka 2002, limewahimiza pia kuuona Mkutano wa AMECEA-2002 kuwa ni wenye thamani kwa Watanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutakiana heri ya mwaka mpya na kumuaga mmoja wa masista wa TEC, Januari 1, mwaka huu, Kurasini jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TEC, Padre Pius Rutechura, alisema jamii haina budi kumshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuishi hadi sasa na kupata mafanikio mbalimbali.

Alisema licha ya kuwa na matatizo ya hapa na pale, hawana budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwasaidia kuyavuka hadi kufikia hapo walipo sasa.

Alisema kila mmoja ana wajibu wa kumshukuru kwa mafanikio aliyoyapata, kwani yanatokana na mapenzi ya Mungu.

Aidha, licha ya kuwashukuru waamini kwa kuonesha moyo na juhudi zaidi katika maandalizi ya Mkutano Mkuu wa AMECEA unaotarajiwa kufanyika nchini, Padre Rutechura aliwataka kuzidisha thamani ya ziada kwa mkutano huo badala ya kuuona kama kitu cha kawaida.

"Naomba watu hasa Wakatoliki nchini na wote wenye mapenzi mema kuongeza thamani ya ziada ili kuukamilisha na kuufanikisha mkutano huu," alisema.

AMECEA ni Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Nchi za Mashariki Mwa Afrika.

Mkutano wa AMECEA mwaka huu unatarajiwa kufanyika Kurasini jijini Dar es Salaam, Julai 14 hadi 28 na tayari maaskofu toka nchi wananchama wanazidi kuthibitisha ushiriki wao.

Kila Mkatoliki, Mkristo, Mtanzania na yeyote mwenye mapenzi mema, anawajibu wa kuchangia kwa hali na mali kufanikiwa kwa mkutano huo kwa kuwa ni heshima kubwa kwa Watanzania wote.

Wakati huo huo: Katibu Mkuu huyo wa TEC, amemshukuru Sista Jovitha Mwenda CICM, kwa kulitumikia kwa moyo wa ufanisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, akiwa katika Kitengo cha Jikoni.

Padre Rutechura amemwelezea Sista Jovitha kuwa mtumishi bora, mchangamfu na muigizaji mzuri licha ya hali yake ya ukimya.

Naye Meneja wa Kituo cha Mafunzo na Mikutano cha TEC, Sista Flora Chuma, katika hafla hiyo ya kupongezana na kumuaga, amesema Sista Jovitha alikuwa mchapakazi kwa kuwa katika kitengo chake, aliendesha shughuli zote kwa ufaisi.

Sista Jovitha alianza kulitumikia TEC tangu Mei 11, 2000 hadi anapoondoka Januari 5, mwaka huu.

Alishika nafasi ya Sista Florancia Mkwizu ambaye kwa sasa yupo katika Shule ya Sekondari ya Regina Mundi, jimboni Mahenge.

Mchungaji atamani uwezo wa kutengua ndoa za Kikristo

Na Getrude Madembwe

"Kama kungekuwa na sheria za kufungua ndoa za Kikristo, ndoa nyingine ningezifungua maana zinatia hata huruma, watu wanagombana hata hawapati suluhisho," amesema Mchungaji Moses wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Usharika wa Kawe.

Maarifa ambaye ni Mchungaji Kiongozi wa usharika huo uliopo katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani, aliyasema hayo wakati akizungumza katika Ibada ya Mwaka Mpya iliyofanyika kanisani hapo juu ya namna vijana wanavyotakiwa kuwa karibu na kuzingatia mambo yanayompendeza Mungu badala ya kukazania ya kidunia.

Aliwaambia vijana ambao hawajaoa na wale ambao hawajaolewa kuhudhuria vipindi na semina mbalimbali zinazotoa mafundisho juu ya ndoa na namna ya kupata mchumba bora ili baadaye wasijilaumu endapo hawatafanya uchaguzi mzuri wa wachumba.

"Mkipata wachumba bomu shauri yenu na kwa taarifa yenu ndoa za Kikristo hazitenguliwi bila sababu maalumu. Hamtaki kuhudhuria vipindi vya vijana au mafundisho ya dini sababu eti mpo bize," alisema.

Alisema kuwa ndoa nyingi zina mikwaruzo na hii inatokana na watu wanaoamua kuoana kutojuana kiundani maana ya ndoa na kwamba wengi wa wanandoa hao, ni wale wanaokutana mitaani na kuamua kuoana bila ya kuchunguzana.

Alisema, "Ndoa nyingine zinatia hata huruma, watu wanagombana hata hawapati suluhisho. Sasa unajiuliza: Hawa watu walichunguzana vya kutosha na kupendana kwa upendo wa dhati au walikuwa wakidanganyana tu?"

Aliongeza, "Tunachokifanya kwa watu hawa ni kuwapa usuluhisho na wala siyo kuwaambia eti tunaifungua ndoa hiyo, hatuwezi kufanya hivyo sababu nyinyi wenyewe mlisema kuwa mtatunzana kwa taabu na raha tena kwa sauti sasa iweje tuwaachanishe!"

Aidha, aliwashauri wazazi kuwalea watoto wao katika misingi ambayo ni ya kumpendeza Mungu na wala sio kuwaacha wajiongoze wenyewe.

Alisema kama wao (wazazi ) wasingelelewa katika misingi iliyokuwa bora na imara, kusingekuwepo na Wazee wa Kanisa na kamwe Kanisa lisingekuwa na watu wengi wa umri mkubwa.

Aliwataka vijana wa Usharika huo kujiunga katika vikundi ili kuweza kumtambua mchumba ambaye anafaa na yupi ambaye ni mdanganyifu.

"Vijana wengi hawataki kujiunga na umoja wa vijana wakidhani kuwa wataimba kwaya na wala hakuna mambo mengine wanayofundishwa, kumbe kuna mafundisho mengi wanayofundishwa."

Akihubiri katika ibada hiyo, Mchungaji Maarifa aliwataka wamini wake kumshukuru Mungu kwa kuwafikisha Mwaka huu wa 2002.

"Siyo kwamba nyinyi ni wema sana au mumemhonga Mungu na wale waliokufa ni waovu au hawakutoa hongo bali ni kwa mapenzi yake mpo hai, anawataka muendelee kumtumikia kwa wema na uaminifu," alisisitiza.

Aliwahimiza kuuanza mwaka huu kwa kutanguliza Yesu kwa kila jambo ambalo wanataka kulifanya.

Mhubiri agawa ‘namba za simu’ kanisani

l Atoa pia namba za fax na E-mail

l Atahadharisha mbinu za utapeli

Na Mwandishi Wetu

MHUBIRI mmoja wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), amegawa namba za simu kanisani ili ziwasaidie waamini kwa mawasiliano na Mungu.

Mhubiri huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Uinjilisti wa Usharika wa Keko katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Bw. Happygod Y. Mkonyi, aliyasema hayo wakati akihubiri katika Usharika wake wakati wa Ibada ya Kuanza Mwaka Mpya wa 2002, Januari Mosi.

Alisisitiza kuuanza Mwaka 2002 kwa kumweka mbele Yesu Kristo katika maisha. Mhubiri huyo alisema kuwa ili kupata mawasilianao na Mungu, ni vema watu wakatumia simu aliyoitaja kuwa ni namba 333.

Alifafanua kuwa namba hiyo inawakilisha Maandiko Matakatifu kutoka katika Kitabu cha Yeremia 33: 3 (Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua).

Alisema namba ya telegramu ili kuwasiliana na Mungu ni Luka 18:13, (...bali alijipigapiga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi).

Alisema namba ya fax ni Isaya 65:24 ( Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia).

Namba ya Vodacom ni Mathayo 14:30(Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe).

E-Mail, ni Luka 24:45 (Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa Maandiko).

Wakati huo huo: Katika Ibada hiyo ya Mwaka Mpya, Mhubiri huyo aliwahimiza wazazi kuwa makini dhidi ya mbinu mpya zinazotumiwa na matapeli ili kuwaibia na kuwafanyia vitendo vya kinyama wasichana.

Alisema wazazi wawahimize watoto na wao wenyewe wawaepuke watu asiowajua wanaotaka kujenga nao mazoea ya haraka bila sababu ya msingi.

Alisema siku hizi umezuka mtindo wa matapeli kuwafuata wasichana na kuwaulizia jambo huku wakiwafanyia mbinu za kushirikina ambazo huwafanya wasichana hao kupoteza fahamu.

Aliongeza kuwa, matapeli hao wanapofanikiwa kupoteza fahamu za vijana hao hususan wasichana, huwachukua hadi sehemu wanazozijua wenyewe ambako huwafanyia vitendo vya ubakaji.

Aliendelea kusema kuwa, wengi wa matapeli hao ni walioathirika na UKIMWI na sasa wanaamua kuueneza kwa njia hizo za kikatili.

Aliongeza kuwa mapataeli hao wanapompumbaza mtu baada ya kumfanyia vitendo vya ushirikina, huambatana hadi nyumbani ambapo mhanga huanza kuchukua vitu nyumbani na kuwapa bila yeye kujijua ikiwa ni pamoja na pesa.

Alisema wizi wa mwingine hufanywa baada ya matapeli hao kuwadunga sindano za kulevya abiria wanaosafiri nyakati za usiku katika mabasi na kuwaibia mali zao.

Alisema wazazi wawahimize vijana wao kuwa makini na watu wa namna hiyo.

"Mtu anajidai ana shida anataka kuulizia; kwanini asiulizie watu wazima au askari na badala yake anakimbilia kuulizia wasichana," alisema.

IGWUTA yaitaka serikali ifuatilie mradi wa umeme wa Stiegiler

l Yaambiwa kuruhusu matumizi ya umeme wa diseli ni uharibifu wa fedha

Na Dalphina Rubyema

KATIKA kupunguza matumizi yasiyo ya lazima,serikali imeshauriwa kufuatilia na kufufua mradi wa nishati ya umeme uliobuniwa na Mhandisi kutoka nchini Ujerumani Bw.Stiegiler miaka 108 iliyopita, badala ya kuagiza wataalamu kutoka nje kwa ajili ya kufunga mitambo inayotumia umeme wa dizeli.

Ushauri huo umetolewa katikati ya juma na Katibu Mkuu wa Umoja wa Wafanyakazi wa Viwandani na Wafanyakazi wengine nchini (IGWUTA),Bw.Shaweji Marenda wakati akizungumza na gazeti hili nje ya ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO).

Bw.Marenda alisema kuwa kutokana na ukweli kwamba Tanzania ni nchi masikini, litakuwa ni jambo la kushangaza na kusikitisha endapo serikali itakubali kuwaleta wataalamu hao ambao watalipwa mshahara wa shilingi milioni 20 kwa Mwezi wakati kuna uwezekano mkubwa wa kupata nishati hapa hapa nchini.

Akifafanua zaidi kuhusu mradi huo unaojulikana kama Stiegiler Gorge Power and Flood Control Development,Bw.Marenda alisema kuwa tayari utafiti huo umekwisha kamilika na taarifa ilikwisha kabidhiwa kwa serikali.

Alisema Mradi huo ambao ulikamilishwa Agosti mwaka 1980 na Shirika la Chakula duniani (FAO) baada ya Stiegiler kuuawa na tembo,mwaka 1907,una uwezo wa kutoa Megawati 2001 kwa kipindi cha miaka 21 bila kikomo

Alisema serikali iliangalie kwa makini suala hili la kuendeleza mradi huo ambao upo katika maporomoko ya mto Rufiji .

Aliwaomba wataalamu mbalimbali waishauri serikali na chama tawala kukubali kutumia umeme huo.

"Sisi hatupingi Ubinafsishaji kwa sababu suala hili kwetu ni uhai ila tunachoshauri ni kwamba serikali ijiangalie kwanza umasikini ulionao,kuruhusu utumiaji wa umeme wa dizeli ina maana Tanzania inakuwa mtumiaji mkuu wa dizeli"alisema Bw.Marenda.

Aliongeza kusema "kwa kweli inasikitisha sana,kwanza hao watalaamu wenyewe watakaa kwa muda wa miaka miwili tu baada ya hapo wataondoka na sisi tulipouliza itakuwaje,tulipata jibu kuwa watakuwa wanaagiza wataalamu kwa awamu,sasa sijui kila siku Tanzania itakuwa ni ya kuagiza wataalamu kutoka nje ya nchi?"Alihoji.

Mwinjilisti wa AICT ataka Sheria ya Roho itawale

Na Getrude Madembwe

MWINJILISTI Deus Ngwashemi wa African Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Pwani amewataka waumini wa Kanisa hilo watumie sheria ya rohoni katika maisha yao ya kila siku.

Mwinjilisti Ngwashemi aliyasema hayo alipokuwa akihubiri katika Ibada ya Jumapili iliyofanyika katika Kanisani la Magomeni jijini Dar Es Salaam.

Alisema inashangaza kumuona Mkristo anajiongoza mwenyewe au kutumia sheria za nchi zilizopo bila ya kutumia sheria iliyopo rohoni mwake.

"Siyo kwamba nasema kuwa muache kufuata sheria zilizopo, ila ninachomaanisha hapa ni kuitumia ile sheria ambayo tunayo katika mioyo yetu, sheria ambayo imetawaliwa na huruma," alisema .

Aliongeza, "Kama mkitumia sheria hiyo ya rohoni, haki itatendeka na hata yale yasiyompendeza Mungu yatapungua kama siyo kuisha kabisa.

Aidha, aliwahimiza waamini hao kukumbuka siku ambayo walizopata mwanga wa kuanza kumtambua na kumtumikia Mungu kama wanavyokumbuka siku nyingine muhimu za kumbukmbu zikiwamo zile za kuzaliwa.

"Watu wengi hapa ukiwauliza walipata wokovu siku gani hawakumbuki lakini siku za kuzaliwa kila mtu anajua. Sasa kwa nini msiwe na tabia ya kufanya hata sherehe ndogo tu kwa ajili ya kukumbuka siku ambayo ulipata wokovu?’’ alihoji Mwinjilisti huyo.

Pia aliwataka waamini hao kuwa na upendo wa dhati na kuachana kabisa na upendo wa kinafiki.

Alisema kuwa katika dini kunaweza kuwa na unafiki, lakini kuwa katika upendo na uhusiano bora na Mungu, kamwe hakuna uhusiano na unafiki.

Alisema kuwa tabia ya watu ya kuhama hama ili kumtafuta Mungu haitawasaidia chochote kwa kuwa, uhusiano mzuri na Mungu siyo dini.

Alitoa mfano wa nchi ya India ambapo kuna miungu wapatao milioni 350 na bado itaongezeka hivyo wasipomwamini Mungu aliye hai, watakuwa ni watu wa kutangatanga tu bila kumpata Mungu wa kweli.

"Tunachotakiwa ni kujitengenezea mazingira mazuri ya kwenda mbinguni ili Yesu atakaporudi mara ya pili atukute tupo tayari kwenda naye katika makao mapya," alisema.