Ubakaji watoto wachanga ni aibu kwa Waafrika- Askofu Kyaruzi

lAsema asasi zinatumia uasherati kama mradi zikisingizia UKIMWI

lDola zinafumbia macho uhalifu na udhalilishaji utu

Na Mwandishi Wetu, Sumbawanga

LICHA ya kusema ulawiti na ubakaji dhidi ya watoto wachanga na mauaji ya utoaji mimba ni aibu kwa Waafrika, Askofu Damiani Kyaruzi amesema vyombo vya dola na asasi binafsi zimegeuza uasherati kuwa mradi kwa kisingizio cha kinga dhidi ya UKIMWI.

Mhashamu Kyaruzi ambaye ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, aliyasema hayo wakati akizungumza katika ibada ya mkesha wa Krismasi iliyofanyika kitaifa katika Kanisa Katoliki la Mamajusi Watatu lililopo jimboni humo katika mkoa wa Rukwa.

Katika Ibada hiyo, Mhashamu Kyaruzi alisema vitendo vya ubakaji na ulawiti vinavyofanywa dhidi ya watoto wachanga ni unyama uliokithiri na ni aibu kwa utamaduni wa Mwafrika.

"Uvunjaji wa Amri ya Sita (usizini) umefikia unyama zaidi ya unyama halisi; Ubakaji na ulawiti na hasa wa watoto wachanga ni udhalilishaji wa binadamu usiokuwa na mfano katika historia ya Mwafrika," alisema.

Aliilaumu tabia ya binadamu kuwahukumu wenzao hukumu ya kifo na akatolea mfano wa utoaji mimba ambao ni mauaji ya watoto ambao hawajazaliwa.

Alisema vitendo hivyo ni dhambi kwa kuwa havikubaliki katika mapenzi ya Mungu.

"Utoaji mimba umehalalishwa na mahali pengine pengi kampeni zinafanyika usiku na mchana ili utoaji mimba uhalalishwe. Tukumbuke kuwa kuua ni dhambi; usiue," alisema.

Katika ibada hiyo, Mhashamu Kyaruzi alisema kuwa, kutokana na kusambaratika kwa maadili na imani sahihi ya ki-Mungu, hata vyombo vya dola na asasi za kibinafsi (NGOs), sasa zinafumbia macho vitendo vya uhalifu na vinavyodhalilisha utu wa mwanadamu.

Alisema hivi sasa uasherati umegeuzwa kuwa mradi wa uchumi kwa baadhi ya vyombo kwani vinautumia kujipatia pesa kwa kisingizio cha kinga dhidi ya UKIMWI.

Alisema watu wamekuwa wakishauriwa kimakosa kufanya matendo ya zinaa kwa kutumia mipira (kondomu) kama njia ya kuwaepusha na maambukizi dhidi ya UKIMWI.

"Muepukane na uasherati na kila mmoja ajue kuuzuia na kuuweka mwili wake katika utakatifu na hekima na si katika hali ya tamaa mbaya," alisema.

Aliongeza, "UKIMWI ni ugonjwa unaoua; hauna kinga au tiba, ni janga la kitaifa na kimataifa, ni ugonjwa hatari unaotia mashaka mustakabali wa taifa letu kwani takwimu za vifo na wagonjwa wa UKIMWI na maambukizi mapya zinatisha.

UKIMWI ni adui dhidi ya mwanadamu na uhai wake; ni adui yetu sote na hivyo, lazima tuunganishe nguvu katika kumpiga vita."

Msiue kwa visingizio vya dini- Pengo

lPadre ashangaa habari za vita zilivyo na soko

Na Sebastian Mafwele

HALI ya baadhi ya watu kutumia dini kufanya uhalifu yakiwamo mauaji na vita imesababisha baadhi ya watu kuanza kupoteza imani na kutaka dini zifutwe kwa kuwa badala ya kuimarisha uhai, sasa zinakatisha, amesema Kardinari Pengo.

Mwadhama Pengo ambaye ni Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, aliyasema hayo wakati akiendesha ibada wakati wa Siku ya Mtakatifu Stephano, iliyofanyika katika parokia ya Msimbazi jimboni humo Jumatano iliyopita.

Alisema kuwa, kwa namna yoyote, hakuna mtu au kikundi cha watu kinachoruhusiwa kukatisha uhai wa mtu kwa kisingizio cha imani za kidini.

Kardinali Pengo alisema jamii yote haina budi kuuheshimu uhai wa mtu kwa kuwa mapenzi ya Mungu, yako katika uhai na uzima wa watu wake.

Akirejea mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11, mwaka huu yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) na katika Kituo Kikuu cha Biashara ya Kimataifa (WTC), Kardinali Pengo alisema,

"Kutokana na matukio ya Septemba 11, huko Marekani, baadhi ya watu duniani sasa wanafikiri kuwa imani za dini ndizo zinasababisha mauaji ya kutisha... Sasa wanaona hawana haja ya kuwa na Mungu kati yao kwa kuwa wanadhani bila kuishi na Mungu, watakuwa na maisha mazuri na matulivu. Hii yote ni kujidanganya tu," alisema.

Mwadhama Pengo alitahadharisha kuwa jamii haiwezi kuishi pasipo Mungu na kwamba hoja hiyo ni hatari kiroho na hata kimwili.

Kufuatia mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa Marekani Septemba 11, mwaka huu, nchi hiyo ilitangaza vita dhidi ya ugaidi duniani huku ikimsaka kwa udi na uvumba mtuhumiwa wa ugaidi huo, Osama Bin Laden.

Baadhi ya magaidi waliwadanganya baadhi ya Waislamu duniani na kuwafanya waamini kuwa vita dhidi ya ugaidi ni vita dhidi ya Uislamu.

Wakati huo huo: Padre Benedict Shayo wa Kanisa Katoliki Parokia ya Magomeni katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, amesema anashangaa kuona watu wanapenda kusikiliza na kusoma habari za vita hali inayoonesha kuwa watu wengi siku hizi wanapenda vita badala ya habari za amani.

Aliyasema hayo wakati akizungumza katika ibada ya maadhimisho ya Krismas iliyofanyika parokiani hapo.

"Kwa sasa ukisikiliza redio au kusoma magazeti, ni habari za vita ndizo zimejaa na wengi wanapenda kuzisikiliza na kuzisoma hizo. Yaani siku hizi habari za vita ndizo zinazouza magazeti.

Alisema hali hiyo inasababisha kuongezeka kwa uovu na inazidi kuchochea watu kufanya kosa la kutozingatia mafundisho yanayotolewa na dini.

Wanaojiua hupenda kufa wakati huo?

lIngawa uwezekano wa wanawake kujaribu kujiua ni mara nne ya ule wa wanaume, uwezekano wa wanaume kufaulu kujiua ni mara nne ya ule wa wanawake

Na Mwandihi Wetu

"KILA mtu anayejiua huwa na sababu zake mwenyewe: za kibinafsi, zisizojulikana, na zinazohangaisha," anasema Kay Redfield Jamison, mtaalamu wa magonjwa ya akili.

Muda mfupi kabla ya kujiua, mwandishi maarufu wa Japani aliyeishi katika miaka ya mapema katika karne ya 20, aliandika akisema "Kuishi ni kuteseka," Hata hivyo, alianza sentensi hiyo kwa maneno haya: "Kwa wazi, sitaki kufa, lakini...

Japokuwa watu wengio wanapenda na kuuthamini uhai uhai, visa vya kujiua vinaongezeka sana ulimwenguni pote.Hivi ni kwanini; kujiua husababishwa na mambo gani yasiyo dhahiri Je, Mtu mwenye tamaa hiyo mbaya aweza kusaidiwaje?Kwa msaada wa Gazeti la Amkeni! Toleo Oktoba 22, 2001"UHAI UNA THAMANI" tunaendelea kuwaletea sehemu ya makala juu ya tatizo hilo, wasomaji wetu ambao hawakubahatika kulipata gazeti hili

La, watu wengi wanapokabili hali hizo zenye mikazo hawajiui.

Basi, ni kwa nini watu fulani hufikiri kujiua ni suluhisho, na wengine hawafikiri hivyo?

Sababu za kujiua zilizo wazi

Kay Redfield Jamison, profesa wa magonjwa ya

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Visababishi visivyoonekana wazi

Kay Redfield Jamison, Profesa wa magonjwa ya

akili katika Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, asema hivi: "Uamuzi wa kujiua hutegemea hasa jinsi mtu anavyoelewa mambo."

Aongezea hivi:

"Akili za watu wengi, zinapokuwa timamu, hazioni kuwa jambo lolote lile linaweza kumfadhaisha mtu hata ajiue."

Eve K. Moscicki, wa Taasisi ya Kitaifa ya Marekani ya Masuala ya Akili, anasema kwamba visababishi vingine vingi vinavyoonekana wazi-hujumlika kuwaongoza watu kujiua.

Visababishi hivyo visivyoonekana wazi vyatia ndani magonjwa ya akili na magonjwa yanayosababishwa na uraibu, na maumbile ya chembe za urithi, na utendaji wa kemikali ubongoni. Tutachunguza baadhi ya visababishi hivyo.

Visababishi vikuu zaidi ni magonjwa yanayosababishwa na

uraibu na magonjwa ya akili, kama vile kushuka moyo, magonjwa ya hisia zinazo badilika-badilika, sizofrenia (kuchanganyikiwa kiakili), na kutumia vibaya vileo au dawa za kulevya.

Uchunguzi uliofanywa huko Ulaya na Marekani, unaonesha kwamba zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaojiua huugua magonjwa hayo.

Watafiti wa Sweden waligundua kwamba visa vya kujiua miongoni mwa wanaume wasiougua magonjwa hayo vilikuwa 8.3 kati ya wanaume 100,000, lakini miongoni mwa wale walioshuka moyo viliongezeka hadi visa 650 kati ya wanaume 100,000!

Na wataalamu wanasema kwamba hivyo ndivyo visababishi vya kujiua pia katika nchi za Mashariki.

Lakini, hata mambo yanayochochea watu kujiua yakijumlishwa pamoja na kushuka moyo, bado yawezekana kuepuka kujiua.

Profesa Jamison, ambaye wakati mmoja alijaribu kujiua, anasema hivi: "Watu huonekana kuwa wanaweza kustahimili au kuvumilia kushuka moyo maadamu wanatumai kwamba mambo yatakuwa afadhali.

"Hata hivyo, amegundua kwamba mtu asipoweza kustahimili mfadhaiko unaoongezeka hatua kwa hatua, uwezo wa mfumo wa akili wa kuzuia tamaa ya kujiua hupungua pole pole.

Analinganisha hali hiyo na jinsi breki za gari zinavyokwisha kwa sababu ya mkazo mwingi.

Ni muhimu kutambua mwelekeo huo kwani yawezekana kutibu mshtuko wa moyo.

Mtu anayehisi kuwa hajiwezi anaweza kurudia hali yake ya kawaida. Visababishi visivyoonekana wazi kushughulikiwa, watu wanaweza kutenda kwa njia tofauti wanapokumbwa na maumivu ya kihisia na mikazo ambayo mara nyingi huchochea watu kujiua.

Watu fulani hufikiri kwamba maumbile ya chembe za urithi ni kisababishi kisichoonekana wazi cha visa vingi vya kujiua.

Ni kweli kwamba chembe za urithi huchangia hisia za mtu kwa njia fulani, na uchunguzi umefunua kwamba familia nyingine huwa na visa vingi vya kujiua zaidi ya nyingine.

Lakini, "mwelekeo wa kujiua uliorithiwa haumaanishi kamwe kwamba mtu hawezi kuepuka kujiua," asema Jamison.

Utendaji wa kemikali ubongoni ni kisababishi kingine kisichoonekana wazi. Mabilioni ya chembe za neva huwasiliana ubongoni kupitia utendaji wa kemikali.

Kwenye ncha zilizotengana za nyuzi za neva kuna mapengo madogo yanayoitwa sinapsi.

Vitu fulani hupitisha habari kwenye sinapsi kupitia utendaji wa kemikali.

Huenda kiasi cha serotonin, kimojawapo cha vitu vinavyopitisha habari, huchangia uwezekano wa kibaiolojia wa mtu kujiua.

Kitabu Inside the Brain chaeleza hivi: "Kiasi kidogo cha serotonin chaweza kumnyang’anya mtu furaha maishani, kwa kupunguza tamaa yake ya kuishi na kuongeza uwezekano wa kushuka moyo na kujiua."

Hata hivyo, jambo la hakika ni kwamba hakuna mtu aliyepangiwa kujiua. Mamilioni ya watu hukabiliana na maumivu ya kihisia na mikazo. Wengine hujiua kutokana na jinsi ubongo na moyo unavyotenda wanapokabili mikazo.

Mbali na kushughulikia mambo yanayochochea watu kujiua, ni lazima visababishi visivyoonekana wazi vishughulikiwe pia.

Hivyo basi, ni jambo gani linalopasa kufanywa ili mtu awe na maoni yanayofaa yatakayomfanya afurahie tena kuishi?

Kujiua na upweke

Upweke ni mojawapo ya mambo yanayofanya watu washuke moyo na kujiua.

Jouko Lonnqvist ambaye aliongoza uchunguzi mmoja kuhusu visa vya kujiua nchini Finland, alisema hivi, "Watu wengi waliojiua walihisi upweke kila siku.

Walikuwa na wakati mwingi lakini hawakushirikiana sana na watu."

Kenshiro Ohara mtaalamu wa magonjwa ya akili kwenye shule ya tiba ya Chuo Kikuu cha Hamamatsu nchini Japan alitaarifu kwamba kujitenga kulisababisha ongezeko la hivi majuzi la idadi ya wanaume wa makamo waliojiua nchini humo.

Hata hivyo ukweli uliowazi ni kwamba kujiua siyo suluhisho la matatizo yoyote yanayomsonga mtu.

Njia sahihi ni kulijua tatizo na kutafuta njia sahihi ya kulitatua. Yote hao yafanyike chini ya kivuli cha sala.

Kila linalotakiwa kufanyika lazima likubalike ndani ya mipango ya Mungu.

Je,Utamsaidiaje anayetaka kujiua?

Unapoona au mtu anapokuambia kuwa anataka kujiua, msikilize kwa makini huku ukimuachia nafasi ya kutosha ajieleze hisia zake.

Hata hivyo, katika visa vingi, mtu anayetaka kujiua hujitenga na kunyamaza. Ni muhimu wewe mwenyewe utambue kuwa ambua maumivu au hali ya kukosa tumaini inayomkumba ni halisi.

Jaribu kumtajia kwa upole mabadiliko fulani mahususi ambayo umeona katika tabia yake, huenda utamfanya akufunulie matatizo yake yote.

Onesha huruma unapomsikiliza. Ni muhimu kumkazia kwamba uhai wake ni wenye thamani kwako na kwa wengine.

Mjulishe ukimsisitiza namna kifo chake kitakavyokuumiza na kuwaumiza watu wengine pia katika jamii.

Msaidie atambue kuwa Mungu anamjali (1Petro 5: 7).

Hata hivyo, ikumbukwe kuwa wengi wanaofanikiwa kutimiza azima hizo mbaya za kujiua, kwa hatua za mwisho kabla ya kukata roho, hujutia sana uamuzi huo unaopingana na mpango wa maalumu wa Mungu katika kulinda uhai, ama wako mwenyewe , au wa mwenzio.

Hufikia hatua wakaanza kutapatapa wakitamani kupata msaada hata wa sisimizi ili waokolewe na hivyo wanusurike katika mauti hayo waliyojipalia wenyewe kwa makusudi.

Kujiua ni dhambi kama ilivyo dhambi ya kumuua mtu mwingine na haistahili kujaribiwa.

Hatutaki mahubiri ya kushambuliana- Mhubiri TAG

Na Benjamin Mwakibinga

MHUBIRI wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), amesema wahubiri nchini waache mahubiri ya kushambulia dini nyingine bali wahubiri Habari Njema za Wokovu kwa kuwa ndizo zinahitajika.

Mwinjilisti Stephen Mhayaya alisema hayo Jumapili iliyopita katika siku ya mwisho ya Mkutano Maalum wa Wiki ya Krismasi ulioandaliwa na Kanisa la TAG, Usharika wa Mabibo Sahara na kufanyika katika viwanja vya UFI - CLUB, Ubungo jijini Dar es Salaam.

Alisema wahubiri hawana budi kuwaeleza watu Habari Njema za Kristo ili wasiojua habari hizo za wokovu, wazifahamu.

Alisema hakuna maana kwa wahubiri kutumia muda wao na wa waamini katika kushambulia dini na madhehebu mengine kwani hali hiyo ni hatari.

Alisema wanaong’ang’ana kudai kuwa Yesu Kristo sio Mungu, waachwe lakini ieleweke kuwa wanajiangamiza wenyewe.

Aliwaonya baadhi ya wasomi wanaohoji juu ya kuwepo kwa Mungu na akasema hao hawana budi waache kupoteza muda wao. Alisema elimu wanayojivunia ina upeo mdogo wa kufahamu masuala ya kiroho.

Alisema kama mtu ni profesa, hawezi kujua mambo yote isipokuwa Mungu pekee.

Mwinjilisti Mhayaya alisema tangu zamani historia inaeleza kuwa ulimwengu umekuwa ukishuhudia mambo mabaya kwa mtu au taifa lililojaribu kuupinga Ukristo.

Alisema hata siku hizi jamii inashuhudia wapinzani wa Injili ya Kristo wakishindwa kutimiza malengo yao waliyokusudia katika jitihada zao za kuuzima Ukristo duniani.

Mwinjilisti huyo alisema kuwa Taifa litakalomkataa Mungu litaangamia kwa vile hekima na maarifa hutoka kwa Mungu na akawasisitiza Watanzania kutumia nafsi zao katika kumcha na kumtumikia Mungu.

Alisema Wakristo lazima wawe kielelezo cha matendo mema katika jamii na hawapaswi kuwa kituko cha kuudhalilisha Ukristo kwani ni fahari kwa Mungu kuona Wakristo na wanadamu wote kwa jumla.

Alisema ni aibu kusikia watu wenye majina ya Kikristo wakiwa vinara wa ulevi, uzinzi, ukahaba na hata unyambizi licha ya kuwa na majina mazuri ya watakatifu waliotangulia na akawaita watu hawa kuwa ni sawa na mbwa mwitu aliyevaa ngozi ya kondoo.

Mwinjilisti huyo wa TAG, alisema Ukristo unabeba alama ya heshima katika jamii na aliwataka Wakristo kuwa macho juu ya masuala ya mitindo hususani ya mavazi kwa wanawake.

Aliongeza kuwa, suala la mavazi yanayolinda utu wa mtu na kuzingatia heshima ya ki- Mungu lisipotazamwa vizuri, litasababisha Ukristo kueleweka vibaya ndani ya jamii.

Wakati huo huo: Mwinjilisti Mhayaya amesema Wakristo wataendelea kuangamia na ugonjwa hatari wa UKIMWI endapo hawataishi kiaminifu na kukabidhi zaidi maisha yao kwa Yesu Kristo.

Aidha, alisema waamini waache kujifariji kuwa wao ni wanadamu hivyo ni wadhaifu bali watambue kuwa wana uzima wa Mungu ndani yao hivyo, wanapaswa kuvishinda vishawishi.

Baadhi ya wahubiri wa dini na madhehebu kadhaa badala ya kuhubiri Neno la Mungu kwa waamni wa dini zao, wamekuwa wakitumia muda mwingi kushambulia dini na madhehebu mengine.

Hali hiyo imekuwa ikilalamikiwa na waamini wao kwa kuwa inawakwaza na inapotosha Neno la Mungu na kujenga uhasama miongoni mwa jamii.

Dini ya kweli haichochei vurugu wala utengano bali inachochea umoja na upendo miongoni mwa jamii.

WASIOTUNZA MALI ZA KANISA NA WANAOKIUKA TARATIBU WAAMBIWA

Msilipake matope Kanisa

Na Neema Dawson

MAKAMU wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewataka wanajamii kuzitunza na kuzithamini mali za Kanisa badala ya kuzifuja na kulipaka matope Kanisa.

Aliyasema hayo wakati wa hafla ya kufunga mwaka 2001 na kuukaribisha mwaka mpya kwa wafanyakazi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania(TEC). Hafla hiyo ilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa TEC, Kurasini jijini Dar es Salaam.

Kardinali Pengo alisema wapo watu ambao huwa si waadilifu mara wanapoajiriwa kufanya kazi katika huduma mbalimbali zinazotolewa na Kanisa.

Alisema watu na watumishi wa namna hiyo, wanapaswa kuacha mtindo huo kwa kuwa wanalichafulia jina Kanisa.

"Kanisa Katoliki linajitahidi kuanzisha huduma nyingi muhimu kwa ajili ya kuwahudumia wananchi kimwili na kiroho. Huduma hizo za Kanisa hazitolewi kibiashara wala kwa lengo la faida," alisema.

Lakini imebainika wale wanaoajiliwa kufanya kazi katika huduma hizo wanakwenda kinyume kwa kufanya biashara kwa kuwatoza watu pesa nyingi isiyo halali na ambavyo haikupangwa lengo ikiwa ni kujinufaisha wao, kuwaumiza wananchi na kuliharibia jina Kanisa," alisema Mwadhama Pengo.

Alisema watu wengi wamekuwa wakilalamikia hali hiyo wakidai baadhi ya huduma za Kanisa zinatolewa kwa gharama kubwa kuliko asasi nyingi.

Alisema yeyote anayejihusisha na hali hiyo, hana budi kuiacha kwa kuwa inachafua jina la Kanisa.

"Utakuta wanalalamika kuwa gharama ya Panadol ni mara mbili zaidi ya ile ya kwenye maduka ya dawa, hali hiyo inasikitisha sana," alisema.

Hata hivyo alisema kuwa bado anaendelea kufanyia uchunguzi malalamiko hayo ambayo baadhi yake yamemfikia na pia amewataka Wakristo wote na wale wenye mapenzi mema, kutoa taarifa pindi wanapo baini hali ya ubadhirifu wa mali za Kanisa.

Katika hafla hiyo, wafanyakazi waliwaaaga wafanyakazi wenzao wawili akiwemo Mama Elizabeth Lufungilo ambaye alikuwa kitengo cha Radio Call ambaye amestaafu baada ya kufanya kazi TEC kwa muda wa miaka 17,na kumuaga Sista Stella Dativa

Sista Dativa ambaye ni wa Shirika la Moyo Safi wa Maria, Mgolole Morogoro alikuwa Idara Ya Mawasiliano katika Kitengo cha Vichokoo na Meneja Matangazo wa Gazeti la KIONGOZI. Sasa anarudi shirikani kwake.

Nafasi yake sasa inachukuliwa na Sista Constansia Mbenna ambaye pia ni wa shirika hilo.

Wapenda maendeleo tusaidieni- Paroko wa Kyela

Na Pd. Raphael Kilumanga, Mbeya

PAROKO wa Parokia ya Mtakatifu Mathias Mulumba, Kyela katika Jimbo Katoliki la Mbeya, amewapongeza waamini wake kwa kujitolea kutumia nguvu zao kujenga kanisa na akatoa wito kwa wenye mapenzi mema kuwaunga mkono kwa hali na mali kukamilisha ujenzi huo.

Paroko huyo Padre Paul Mwanyalila, alitoa pongezi na wito huo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi parokiani kwake juma lililopita.

Alisema moyo waliouonesha waamini wa parokia hiyo katika kujiletea maendeleo, hauna budi kuigwa na jamii nzima kwani mtu anayeonesha bidii mwenyewe ni rahisi kusaidiwa pale nguvu zake zinapoishia.

Alisema waamini hao wamechangia nguvukazi na mali zao kwa ujenzi wa kanisa ambalo kwa mujibu wa tathmini za mwaka 1996, linagharimu jumla ya shilingi milioni 146/= za Kitanzania.

"Gharama hiyo ilikuwa kwa kipindi hicho na ni wazi kwamba sasa zimepanda," alisema.

Alitoa wito kwa Serikali, makanisa, mashirika na asasi za kidini na za kibinafsi; pamoja na watu wote wenye mapenzi mema na hasa wazawa wa Kyela popote walipo, kuchangia kwa hali na mali ili kufanikisha ujenzi huo.

Parokia ya Mtakatifu Mathias Mulumba, Kyela, ina waamini takribani 6000 na vigango zaidi ya14. Ilianzishwa mwaka 1968.

Ujenzi huo utakapokamilika, kanisa hilo litamudu kuhudumia waamni 1200.

Serikali, asasi na wafadhili mbalimbali wamekuwa wakisisitiza jamii kuchangia kwa juhudi katika kujletea maendeleo na huku wakisema wako tayari kuwasaidia pale ambapo juhudi za kujiletea maendeleo zimekwama badala ya kutaka watu kutaka kusaidiwa kila kitu.

Hivi sasa ujenzi huo uko kaika hatua za kukamilisha msingi na kunyanyua ukuta.

Kwa yeyote mwenye mapenzi mema aliyeguswa na ombi hili, na kupenda kuunga mkono juhudi za waamini hao, atume mchango au msaada wake kwa: Paroko,

Parokia ya Kyela,

S.L.P. 170.

KYELA.

Ulimwengu sasa hofu tupu- Askofu Kilaini

Na Peter Dominic

ULIMWENGU wa sasa umejaa wasiwasi kwa sababu watu wengine wanafurahia kuona wengine wakiteketea, amesema Askofu Method Kilaini.

Mhashamu Kilaini ambye ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, aliyasema hayo wakai akihubiri katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini dar es Salaam katika ibada ya Krismasi.

Alisema kutokana na kuporomoka kwa imani na maadili, hivi sasa baadhi ya watu hawathamini maisha yao na ya wenzao kiasi kwamba wako tayari kuyaangamiza wakati wowote.

"Kuna watu siku hizi ambao wako tayari kufa ili kuteketeza wengine. Tuombe kwa sala na sisi wenyewe tufanye mazingira mazuri ya kuleta amani duniani," alisema.

Askofu Kilaini alisema il kupunguza mawazo ya uovu katika jamii, kila mmoja anapaswa kuwa na ishara ya familia takatifu ndani ya nyumba yake ili pindi aionapo, mawazo hayo yamtoke na kuyavuta yale yenye maadili ya ki Mungu.

"Ukiwa na picha ya Yesu ukutani au rozari, huwezi kuitazama halafu ukatukana au kufikiria mambo mabaya kwa kuwa Yesu anakuwa ni kiini cha maisha yako," alisema.

Asasi zahimizwa kushawishi watu kupima UKIMWI

Na Neema Dawson

ASASI mbalimbali za kibinafsi zinazojihusisha na mapambano dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI, zimehimizwakuongeza bidii katika kuwashawishi watu wajitokeze kupimwa ili wajijue kama wameathirika na UKIMWI.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Kazi , Maendeleo ya Vijana na Michezo, Bw. Steven Kisui, wakati akifunga semina ya Umoja wa Mzizi wa Kuunganisha Vijana nchini (TAYOBO ). Semina hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni ambapo vijana wapatao 40.

Alisema kuwa baadhi ya mashirika yamekuwa yakiuchukulia ugonjwa wa UKIMWI kama mradi wa kupatia fedha kwa maslahi yao binafsi badala ya kuisaidia jamii nzima, kwa mafundisho sahihi ya kujikinga na ugonjwa huo.

Alisema asasi nyingine zimekuwa zikizingatia kwa vijana mijini bila kujua idadi ya waathiri na maeneo yote yanayopaswa kufikiwa elimu dhidi ya UKIMWI.

Baadhi ya washiriki wa semina hiyo walikubali kupimwa ugonjwa huo hatari wa UKIMWI na miongoni mwa waliopima, mmoja aligundulika kuwa ameathirika na ugonjwa huo.

Mkurugenzi huyo alisema kuwa, hali hiyo ni mfano bora wa kuingwa kwa na asasi nyingine za kibinafsi zinazojihusisha na mapambano dhidi ya UKIMWI.

Askofu wa AIC ataka jamii kuishi Kimungu

Na Margareth Charles

ASKOFU Charles Salalah wa Kanisa la Africa Inland Church Tanzania, amewaasa waamini wa madhehebu mbalimbali ya Kikristo kuishi katika maadili yaliyojengwa kwa misingi ya Neno la Mungu.

Alitoa wito huo katika ibada ya pamoja iliyoandaliwa na Umoja wa Makanisa ya Kikristo na kufanyika katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Maxmillian Kolbe, Mwenge jijini Dar es Salaam.

Ibada hiyo ya pamoja ya Umoja wa Makanisa ilifanyika wakati wa Sikukuu ya Krismas, Jumanne iliyopita.

Alisema inashangaza mno kwani licha ya kujua kuwa mambo kadhaa hayampendezi Mungu na wao wenyewe, bado baadhi ya watu wamekuwa wakifanya mambo hayo kwa makusudi.

Askofu Salalah alisema hali hii inatokana na ukweli kuwa baadhi ya watu wanamjua Mungu lakini hawamuheshimu wala kumshukuru.

"Lile tusilolipenda ndilo tulitendalo na lile tulipendalo hatulitendi; kwa hiyo watu wanamjua Mungu lakini hawamshukuru," alisema.

Aidha, alisema athari ya dhambi imewaingiza wanadamu katika ibada potofu na maadili potofu na hata kwenye tatizo la kujenga jamii ya watu iliyoporomoka kimaadili.

Alisema kusudi la kuzaliwa Yesu Kristo ni kumpatanisha mwanadamu na Mungu, lakini kutokana na dhambi, mwanadamu amekuwa akitafuta maisha yake kwa kuzindikwa, kuvalishwa hirizi na kukataa kufuata maadili ambayo Mungu ameyaweka.

Hata hivyo alisema mwanadamu hapaswi kuenenda kinyume na maadili ya Mungu kwani kwa kufanya hivyo ni kuenenda kinyume na mapenzi ya Mungu.

Alisema kuwa, mwanadamu anaweza kuenenda sawasawa na mapenzi ya Mungu endapo kila mmoja wetu ataishi kwa kufuata maadili yaliyojengwa katika misingi ya Neno la Mungu.

Vijana wahimizana kupambana na UKIMWI

Na Eric Samba

VIJANA nchini wamepeana changamoto na kuhimizana kuzingatia mabadiliko ya tabia ili kupambana na gonjwa hatari la UKIMWI ambalo ni tishio katika jamii.

Vijana hao wametoa changamoto hiyo Jumamosi iliyopita kupitia michezo mbali mbali waliyoicheza katika tamasha la vijana lililoandaliwa na Chama cha Vijana Hai (Youth Alive Club) Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kufanyika katika Kituo cha Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Katika tamasha hilo lililokuwa na kaulimbiu KUKUA NI KUBADILIKA, MABADILIKO YA TABIA YANAWEZEKANA.

Vijana hao walitoa jumbe mahsusi za kuwataka vijana wenzao kote nchini kuinuka na kukabiliana na adui anayetishia maisha yao.

"Waliotangulia kufa kwa UKIMWI hao hawapo tena, lililobakia ni sisi kuhamasisha," ilisema sehemu ya ujumbe uliotolewa na vijana wa kikundi cha Fourth World Movement.

Mgeni rasmi katika tamasha hilo alikuwa Balozi Isaya Chialo ambaye ni Msimamizi wa Chama cha Vijana Hai katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam.

Balozi huyo aliwataka vijana hao kuwa mabalozi wazuri kwa vijana wengine ambao hawajapata ujumbe muhimu juu ya mabadiliko ya tabia ili kupambana na UKIMWI.

"Ninyi mliohudhuria tamasha hili na kupata ujumbe mzuri wa mabadiliko ya tabia lazima mwende na kuwa walimu kwa wenzenu huko nje ili nao wajue njia za kubadili tabia na waweze kuepuka hatari ya UKIMWI," alisema Chialo.

Nao Mwenyekiti wa chama hicho, Bi. Veronica Komba na Mratibu wake, Bi. Mary Mwakaliku, waliliambia KIONGOZI kwa pamoja kuwa chama cha Vijana Hai huandaa na kuendesha semina za siku saba ambazo huwawezesha vijana kujifahamu, kuwa na malengo na kuchukua hatua.

Walisema kuwa endapo vijana watajiingiza katika masuala ya mapenzi mapema basi itakuwa vigumu kufikia malengo yao.

Tamasha hilo liliwashirikisha vijana toka vikundi mbali mbali kikiwemo Youth Alive yenyewe, Child in The Sun, Fourth World Movement, Karisimatiki na Ardhi Sekondari.

Hadi sasa Chama cha Vijana Hai kimekwisha endesha semina za mabadiliko ya tabia katika mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Morogoro, Mbeya, Kilimanjaro, Tanga, Unguja na Pemba.

Tamasha hilo pia lilihudhuriwa na Mlezi wa Chama cha Vijana Hai, Padre Georges Marie Loire, viongozi wa vikundi vilivyoshiriki na baadhi ya wazazi.

 

 

Maharusi wapewa dawa ya kuishi salama

Na Pd. Raphael Kilumanga

MENEJA wa Kituo cha Mafunzo na Mikutano na Kaimu Katibu wa Idara ya Liturujia katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), wamewapa mbinu maharusi ili wazitumie kama dawa ya kuwawezesha kuishi vema maishani mwao.

Walikuwa wakizungumza katika sherehe za kuwaaga na kuwatakia maisha mema ya ndoa wafanyakazi wa TEC, Ildefonce Lllanga na Esther Mathew wanaofunga ndoa Jumamosi hii.

Meneja huyo Sista Flora Chuma nakatibu huyo, Monsinyori Julian Kangalawe, walisema uaminifu na upendo baina ya wanandoa wenyewe na ndugu zao, ndio msingi mkubwa wa kuimarisha ndoa yao.

"Bila kuwa na uaminifu na upendo, nyumba yenu itaathirika na hata kuvunjika na hali hiyo; itaathiri vibaya maisha ya watoto wenu," alisema Sista Flora.

Meneja huyo wa Senta ya TEC, aliwashauri kuepuka aina na kiwango chochote cha ubaguzi wa ndugu wa pande zote mbili, kwa mume na kwa mke.

"Achaneni na ubaguzi wa ndugu zenu, haina maana mke kupendelea ndugu zake pekee akawachukia ndugu wa mume; ndugu wa mume wakija eti ananuna au mume akiona ndugu wa mke ananuna; hiyo ni hatari katika maisha ya ndoa," alisema.

Naye Monsinyori Kangalawe, alisema ili kudumisha upendo baina ya pande zote mbili, wana ndoa hawana budi kujenga utamaduni wa kujengana.

"Kama mwanaume una zawadi na unataka kuipeleka kwa ndugu zako, mpe mkeo aipeleke na kama ni mwanamke una zawadi unataka kuipeleka kwenu, mpe mumeo aipeleke.

Lazima mke amjenge mume kwa ndugu zake na muzme amjenge mke kwa ndugu zake. Kwa kufanya hivyo mtaimarisha uhusiano baina yenu na ndugu zenu," alisema Monsinyori Kangalawe.

Monsinyori Kangalawe aliwahimiza wanandoa hao watarajiwa kuvumiliana na kupendana katika maisha yao yote.

"Uaminifu na upendo uwe ni zawadi ya kila mmoja kwa mwingine. Mpokeane kama zawadi ya kila mmoja kwa mwingine na zawadi hiyo ichukuliwe kama ilivyo," alisisitiza Monsinyori Kangalawe.

Mmoja wa ndugu waliokuwapo katika sherehe hizo zilizofanyikaTEC Alhamisi iliyopita ambaye jina lake halikupatikana mara moja, alisema, "Mwanangu uhakikishe hauweki madoa kwenye ndoa yako lilivyo hili shati langu maana ndoa ya madoadoa haipendezi maishani," alisema huku akionesha shati lake lenye madoadoa.

Licha ya kuwasisitiza kuwa wacha Mungu zaidi katika maisha yao, waliwaasa kuwatumia wasimamizi wao, Bw. Peter Maduki na Bibi Oliva Kinabo kama hatua ya mwanzo ya kutatua matatizo yao.

Ibada ya Ndoa baina ya Bw. Ildefonce na Bi. Esther, inafanyika Jumamosi hii katika kanisa la TEC na kufuatiwa na tafrija katika ukumbi wa EQUATOR GRILL, Temeke.