Papa awahimiza Maaskofu; leeni hamu ya Utakatifu kwa mapadre na Waumini

CASTEL GANDOLFO, Italia

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amependekeza vipaumbele kwa maaskofu wote ili kupalilia hamu ya utakatifu miongoni mwa watu ulimwenguni pamoja na kusaidia mapadre, hasa pale wanapokumbana na matatizo.

Baba Mtakatifu alitoa wito huo alipokutana na maaskofu 120 kutoka nchi 33, waliokusanyika katika makazi yake ya Majira ya Kiangazi ya Castel Gandolfo.

Maaskofu hao walikuwa wakihudhuria mkutano wa siku 10 huko Roma ulioandaliwa ili kuwapa ushauri juu ya kutimiza majukumu yao mapya ya kichungaji.

Taarifa ilisema kuwa kikao cha kwanza cha namna hiyo kuandaliwa na Idara ya Maaskofu ya Vatican ulifanyika mwaka jana.

Baba Mtakatifu alisema kuwa katika jamii ya leo iliyoshehenezwa na kutojali dini na wakati mwingine kutawaliwa na uhasama, jukumu la kuwa askofu ni gumu sana.

“Kazi ya msingi ya  mchungaji ni kukuza hamu safi ya utakatifu katika waamini wote, utakatifu ambao wote tunaitiwa na ambamo jitihada zote za binadamu huishia,” Papa aliwaambia Maaskofu hao.

“Kipaumbele kingine kwenu ni kuwa makini kwa mapadre wenu, ambao ni washirika wenu wa karibu katika huduma yenu,” aliongeza. “Huduma ya kiroho kwa padre ni jukumu la msingi la kila Askofu wa jimbo.”

“Ishara aifanyayo Padre Siku ya  Upadrisho; kuweka mikono yake katika mikono ya askofu, kukiri mbele yake heshima ya kidugu na utii kwa mara ya kwanza inaweza kuonekana kama ishara katika maana moja tu. Ishara ambayo kwa kweli huwafungamanisha wote pamoja: padre na askofu,” alielezea Baba Mtakatifu.

Alisema, “Padre kijana huchagua  kujikabidhi kwa Askofu, na kwa upande wake askofu hujitoa mwenyewe kuwatunza wale walio mikononi mwake.”

“Kwa njia hii askofu huwa na wajibu wa kujua majaliwa ya wale ambao mikono yake huwakumbatia. Padre lazima aweze kuhisi, hasa katika nyakati za tufani,na upweke, kwamba mikono yake imeshikiliwa kikamilifu na Askofu,” alisema.

Aliongeza, “Kwa hiyo, ni lazima mjitoe kikamilifu kukuza miito ya kweli ya kipadre, kwa sala, ushuhuda wa maisha na uangalifu wa kichungaji.”

Hata hivyo, Baba Mtakatifu alikiri kwamba changamoto hii inahitaji majitoleo makubwa katika ulimwengu ambao ni tajiri wa njia za kiufundi, njia za vitu na faraja, lakini, unaoonekana maskini sana kimalengo, tunu na kanuni za maadili.

“Mtu wa leo ambaye amepoteza hali ya kujali tunu mara nyingi huchagua mambo yenye kikomo na kuhusiana na mambo fulani.  Katika mazingira haya ya kukosa imani na uhasama, utume wa Askofu si rahisi,” alisisitiza Papa.

Kuhusu uinjilishaji Baba Mtakatifu alisema, “Lazima tusisalimu amri kwa ukosefu wa matumaini na kuvunjika moyo, kwa sababu Roho huongoza Kanisa na hulipa kwa mpulizo wake moyo wa kujaribu kutafuta njia mpya za uinjilishaji ili kuweza kufikia sehemu ambazo bado kufikiwa na Injili.”

Alisema, “Ukweli wa Kikristo ni wa kuvutia na wenye kushawishi hasa kwa sababu unaweza kutia alama na mwelekeo kwamba uwepo wa binadamu, ukitangaza katika njia wazi kwamba Kristo ndiye Mwokozi wa watu.”

“Utangazaji huu unaendelea kuwa wazi leo kama ilivyokuwa mwanzoni mwa Ukristo, wakati upanukaji mkubwa wa kimisionari wa Injili ulipofanywa,” alisisitiza.

Maaskofu hao walifanyia mkutano wao katika Regina Apostolorum Pontifical Athenaeum, Kituo cha Chuo Kikuu kinachoongozwa na Wanalejio wa Roma. 

Marekani kuishambulia Iraq si haki- Kardinali Ratzinger

l Apendelea uamuzi utolewe na Umoja wa Mataifa

TRIESTE, Italia

 

MWADHAMA Kardinali Joseph Ratzinger haamini kwamba mashambulizi ya Marekani peke yake dhidi ya Iraq yangekuwa ya haki kimaadili katika hali ya sasa.

kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Idara ya Vatican ya Mafundisho ya Imani ambaye hata hivyo alikiri kutokuwa na maarifa ya kutosha katika masuala ya kisiasa, “Umoja wa Mataifa ndiyo asasi ambayo inapaswa kutoa uamuzi wa mwisho kuhusu Iraq.”

”Ni lazima kwamba jumuiya ya mataifa ifanye uamuzi, na si taifa tu lenye nguvu,” alisema kardinali huyo baada ya kupokea tuzo ya '2002 Trieste Liberal Award'. Maoni yake hayo yalichapishwa na gazeti la Italia la Avvenire.

"Ukweli wa kwamba Umoja wa Mataifa unatafuta njia ya kuepusha vita, ni wazo la busara kuna ushahidi wa kutosha kuwa uharibifu utakuwa mkubwa zaidi ya tunu zile zinazotegemewa kuhifadhiwa, kwa njia hiyo ya vita.” alisema kardinali huyo.

Alisema kuwa “Umoja wa Mataifa unaweza kushutumiwa” kutokana na hoja kadhaa, lakini pia akasema “ni chombo kilichoundwa baada ya vita ili kuratibu, pamoja na mambo mengine maadili ya siasa.”

Kardinali Ratzinger aliongeza kusema ”dhana ya ‘vita vya kujilinda’ haitokei wala kuonekana popote katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki.”

”Huwezi kusema tu kwamba katekisimu haihalalishi vita. Hata hivyo, ni kweli kwamba katekisimu imetengeneza mafundisho ambayo, kwa upande mmoja  hayatengi ukweli kuwa kuna tunu na watu ambavyo ni lazima vilindwe katika hali Fulani; kwa upande mwingine katekisimu inatoa mafundisho sahihi juu ya mipaka ya uwezekano huu.”

Kiongozi huyo  aliziomba dini tatu zinazotokana na Abraham kutoa Amri Kumi kama njia za kuwavunja moyo magaidi.

”Amri Kumi si mali binafsi ya Wakristo ama Wayahudi,” alisema Kardinali Ratzinger.

“Ni maelezo makuu ya sababu za maadili, ambayo yanapatikana pia katika busara ya tamaduni nyingine. Kurejea tena katika Amri Kumi inaweza kuwa muhimu ili kurejesha sababu hizo.”

Na huko Florence, Italia, Msaidizi wa Vatican katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva aliwashauri wale wanaopinga mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iraq kupendekeza suluhisho linalotekelezeka ili kulinda amani.

”Tunapendelea mazungumzo lakini pia kuheshimu sheria ya kimataifa,” alisema Askofu Mkuu Diarmuid Martin, msimamizi wa kudumu wa Vatican katika ofisi hizo za Umoja wa Mataifa, wakati akihutubia mkutano wa jumuiya na makundi 60 ya kanisa.

”Sheria inaruhusu utumiaji wa nguvu, lakini uamuzi wa kutumia nguvu unatolewa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pekee,” aliongeza.

Washiriki katika mkutano huo walitangaza ilani ambayo ilibeba maudhui “Amani: Hali ya Kanisa kwa ajili ya Maendeleo ya Dunia.”

Askofu Mkuu Martin alisisitiza kuwa “uwajibikaji ni muhimu sana sasa zaidi ya wakati wowote kabla.

Utumiaji nguvu daima na kila wakati ni njia inayoonyesha kushindwa.”

Kiongozi huyo pia alisema kuwa Umoja wa Mataifa “ni lazima usitumike kuendeleza maslahi ya upande mmoja. Kuuzuia Umoja wa Mataifa kutimiza jukumu lake kungeleteleza hatari kubwa kwa wote.”

Hata hivyo, Askofu Mkuu Martin hakupendelea utafutaji utulivu kwa gharama yoyote ile. “Katika nyakati hizi ngumu, wale wanaokataa matumizi ya nguvu ni lazima wawajibike kutoa maelezo juu ya njia ambayo inaweza kutumika ili kuepusha vita.”

Kwa namna ya pekee, aliwashauri Wakatoliki “kuchafua viatu vyao” katika kukabiliana na matatizo hayo kwa pamoja na katika kushawishi “serikali kuwekeza katika watu na kujitoa kikamilifu kwa chaguo pendelevu kwa ajili ya kila mtu maskini.”

Alisema kuwa katika vita dhidi ya ugaidi, ni lazima iwepo “heshima kwa sheria za nchi na watu kuishi pamoja.”

Papa amtaka Sharon kukomesha mzingiro dhidi ya Arafat

l Aeleza mshikamano wake na ArafatVATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili ametoa wito kwa Waziri Mkuu wa Israel, Ariel Sharon kukomesha mzingiro kwenye makao makuu ya Kiongozi wa Wapalestina, Yasser Arafat katika Ramallah, akionya kuwa hatua hiyo inahatarisha jitihada za amani.

Msemaji wa Vatican, Dk. Joaquín Navarro-Valls aliripoti kuwa ujumbe huo ulitumwa kwa Waziri Mkuu wa Israel na katibu wa nchi wa Vatican, Kardinali Angeli Sodano, kwa niaba ya Papa na kusema kuwa papa pia alielezea mshikamano wake na Kiongozi wa Wapalestina.

“Kwa kuguswa na mashambulizi mabaya katika makao makuu ya Mamlaka ya Utawala wa Ndani wa Palestina, Papa anaomba ukomeshaji wa matendo ya namna hii, ambayo yanahatarisha jitihada za amani katika eneo hilo ambazo tayari zimelegea,” alisema Sodano kwa niaba ya Baba Mtakatifu.

Baba Mtakatifu pia alitaka “kurudiwa upya kwa haraka mazungumzo baina ya pande hizo mbili katika njia ya kuheshimiana na maelewano.”

Msemaji wa Vatican alisema kuwa Kardinali Sodano alituma ujumbe mwingine kwa Rais Arafat kuelezea “ukaribu wa Baba Mtakatifu na Wapalestina pamoja na uungaji mkono wa jitihada za amani.”

Kardinali Sodano alihakikisha katika ujumbe wake kuwa “Vatican itaendelea kutetea haki ya kila taifa kuishi katika amani ikiwa katika mipaka salama na katika hali ya kuheshimiana.”

Kwa miezi iliyopita Papa Yohane Paulo wa Pili aligusia hali ya Mashariki ya Kati katika mikutano yake mingi ya Jumatano na kabla ya kusali Sala ya Malaika wa Bwana siku za Jumapili. Akitoa wito wa kukomesha vurugu na kuanza upya mazungumzo.

Naye Askofu Mkuu Jean-Louis Tauran, katibu wa Vatican wa uhusiano na mataifa alirudia mara kadhaa kwamba kupatikana kwa amani katika Mashariki ya Kati kunahitaji kukubalika kwa haki ya Israel kuishi katika amani na hali ya Palestina kuwa Taifa huru.

Kuhusina na kulinda maeneo matakatifu na hasa Jerusalem, alisema kuwa Vatican haiombi mji huo uwekwe chini ya uangalizi wa kimataifa kama vyombo vingine vilivyowahi kuripoti.

Alisema kuwa kinyume chake Vatican inahitaji sheria zenye dhamana ya kimataifa ili maeneo matakatifu kwa Wayahudi, Waislamu na Wakristo yaheshimiwe.

Maelezo marefu ya msimamo wa Vatican juu ya suala hili yalitolewa na Askofu Mkuu Tauran katika Umoja wa Mataifa mwaka 1999 katika hotuba yake iliyokuwa na kichwa cha maneno “Vatican na Nchi Takatifu: Haki na Upendo.”

Jumanne iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa umepitisha azimio likiitaka Israel kukomesha mzingiro katika Ramallah, na kuondoka katika maeneo yaliyokaliwa kabla ya Septemba 2000.

Papa apongeza Njia ya Neokatekumenato, ataka ichunguzwe na Vatican

 

VATICAN CITY

 

Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili amepongeza hatua ya hivi karibuni ya kuidhinishwa kwa sheria za njia ya Neokatekumenato na kuwaomba viongozi wa kundi hilo kushirikiana na ujumbe wa Vatican ambao utachunguza mwenendo wake wa katekesi na liturujia.

Baba Mtakatifu aliyasema hayo wakati alipokutana na waanzilishi, makatekista na mapadre wa Neokatekumenato.

Alisema kuwa hatua ya Vatican ya kuidhinisha sheria hizo mwezi Juni, “inafungua hatua mpya katika Njia hiyo.”

Alisema kuwa sheria hizo ni msaada muhimu kwa maaskofu wa majimbo mahalia na hoja rejea za msingi kwa mchakato wa malezi wa kundi hilo kufanyika sawasawa na mafundisho pamoja na nidhamu ya Kanisa.

“Sasa ni juu ya ofisi husika za Vatican kuchunguza Maelekezo ya Katekesi ya Njia hiyo pamoja na mwenendo wa katekesi na liturujia,” aliongeza Baba Mtakatifu.