Vatican yaionya Marekani

l Kuipiga Iraq kijeshi kutaua watoto na akina mama zaidi

l 'Huwezi kuupinga uovu kwa ovu jingine'

l   Maamuzi ya Umoja wa Mataifa yazingatie tunu ya uhai

 

VATICAN CITY

 

Askofu Mkuu Jean Louis Tauran, ambaye ni Katibu wa Uhusiano wa Vatican na Mataifa Ulimwenguni ameionya Marekani juu ya hali ya mambo ilivyo kimataifa hivi sasa hususan ni swala la kuishambulia kivita Iraq.

 Katika mahojiano yaliyofanywa ofisini kwake na gazeti moja la Italia liitwalo  “Avvenire” amesema msimamo wa Vatican kuhusu hali  ya Iraq ni “kuendelea na  mazungumzo daima na bila kuibagua nchi au serikali yoyote”. Alisisitiza kuwa muungwana hapingi uovu kwa kutumia uovu mwingine.

 Aliongeza kuwa “Iwapo jumuiya ya kimataifa, ikivuviwa na sheria za kimataifa pamoja na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ingefikiria kuwa matumizi ya nguvu ni njia nzuri, hili lingefanyiwa uamuzi kwa kufuata muundo wa Umoja wa Mataifa baada ya kupima vizuri matokeo ya njia hiyo kwa mamilioni ya Wairaq wasio na hatia, madhara kwa nchi jirani pamoja na utulivu wa dunia nzima.”

Uzoefu wa vita vilivyotokea huko Afughanistan hivi karibuni na hata huko Iraq katika miaka ya 90 umeonesha wazi kuwa waliopata madhara makubwa ya vifo, kukimbia na kukosa mahala pa kuishi ni raia wema, hasa akina mama na watoto badala ya walengwa wa vita wenyewe. “ Uamuzi wowote lazima upime madhara yatakayoupata umma mzima wa Wairaq wenyewe”.Alisisitiza

Kulingana na taarifa za shirika la Uingereza “Voice in the wildernes”(sauti ya nyikani) linalotoa misaada ya kibinadamu huko Iraq, linasema kuwa mamilioni ya watoto mpaka sasa wanaathirika na madhara yatokanayo na vita kama vile vilema vya mwili na akili, ugonjwa wa kwashakoo, kutokana na kukosa chakula. Ugonjwa huu huathiri kwa kiasi kikubwa kukua kwa mtoto na uwezo wa kutambua mambo na hivyo kupunguza nafasi ya kuwa mtu mwenye uwiano chanya.

Msemaji wa Shirika hilo Bwana Von Sponeck katika taarifa hiyo anasema vita na vikwazo vya Uchumi ilivyowekewa Iraq vimekuwa na madhara makubwa kwa watu wa kawaida wa Iraq sasa na kwa vizazi vingi vijavyo. Watoto wengi  hawana nafasi ya kupata elimu, maji safi, huduma za afya, na kukuwa wakiwa na utulivu. Aidha  watoto hao ndio wanaoonja adha ya uyatima kwa kukosa malezi ya wazazi wao kutokana na vifo huko vitani.

Akitoa mfano mmoja tu wa shambulizi la kujikinga lililofanywa na ndege za majeshi ya Marekani, katika mji wa Basra, tarehe  25 Januari 99,  shambulizi hilo liliuwa raia 17, kujeruhi watu mia moja, kuharibu nyumba za makazi ya watu 45 na kuharibu njia za usambazaji maji safi na taka katika mji huo hivyo kusababisha mfumuko wa magonjwa yaliyopelekea mlolongo wa vifo vingine zaidi.

Aidha maelfu ya akina mama ni wajane au wameachika kutokana na vita vya Iraq na Iran na baadaye vita vilivyoongozwa na Marekani katika miaka ya 90, kwani familia nyingi zimesambaratika kutokana na kulazimika kuwa wakimbizi. Hali hii inawapotezea Wairaq utamaduni na desturi zao hivyo kushindwa kuijenga upya Iraq.

Uchumi wa Iraq umeathirika sana baada ya kuwekewa vikwazo vya kiuchumi na jumuiya ya kimataifa kufuatia Iraq kuivamia Kuwait na kuikalia kimabavu. Tangu hapo raia wa Iraq walio wengi wamekuwa wakiishi katika hali ya kubahatisha maisha. Hao ndio waathirika wakubwa wa vita yoyote ile ikitokea kama inavyosisitizwa na Serikali ya Marekani licha ya kupingwa na dunia nzima.

Kuhusu mwaka mmoja baada ya mashambulizi ya kigaidi hapo septemba 11 mwaka jana, Askofu mkuu huyo alisema “tendo hilo la kikatili liliamsha watu wote kulaani ugaidi … na kuamsha viongozi katika jamii kuchunguza sababu za vitendo hivi vya vurugu visivyo vya kibinadamu.”

Aidha alisema kuwa “mkutano wa Assizi  uliofanyika Januari 24 pamoja na mkutano juu ya ‘Watu na Dini’ uliofanyika Palermo-Italia, imesisitiza kwamba dini haiwezi kuhalalisha ugaidi na kwamba waamini wote wanao wajibu wa pamoja wa kuondosha chuki.”

Kuhusu kupatikana kwa amani ya kudumu katika eneo zima la Mashariki ya Kati, alisema kwamba “kwanza kabisa wote waweke silaha chini na kuheshimu jitihada za kila mmoja, kila mmoja ajali sheria za kimataifa, maeneo yanayokaliwa yahamwe, sheria ya kimataifa itumike kulinda maeneo matakatifu kwa dini kuu tatu za Ukristo, Uyahudi na Uislamu.”

Alisema kuwa baada ya hayo kufanyika “jamii ya kimataifa iwepo zaidi katika eneo hilo ili kuwasaidia pande zote kufikia mwafaka.”

Alisema kuwa maneno ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kulaani ugaidi yamesaidia watu kuelewa kuwa teolojia ya ugaidi kamwe haiwezi kuwepo na kwamba makundi yenye itikadi kali yanayopata uvuvio kwenye Uislamu yasichanganywe na Waislamu safi.

Alisema kuwa viongozi wote wa dunia waliotembelea Vatican wamekubaliana na msimamo huo kwa sababu Vatican imeonya kuhusu kuchanganya mambo hayo mawili.

Kuhusu mabadiliko yaliyofanywa juu ya uhusiano kati ya Vatican na ulimwengu wa kiislamu , alisema “nadhani ni wazi kwa kila mtu kwamba kupinga ugaidi haimaanishi kupinga Uislamu … Papa na wasaidizi wake wamelisisitiza hili kwa mara kadhaa.”

Akichambua matokeo ya vita dhidi ya ugaidi katika mwaka huu wote alisema “kitu cha muhimu ni kwamba hakuna kiongozi yeyote wa kisiasa anayestahili cheo hicho au kiongozi wa dini anayeweza kuhalalisha ugaidi mahali popote ulimwengu … ni lazima tuadhibu wakosaji na kuhakikisha kwamba hawasababishi maafa zaidi.”

Hata hivyo alisema “ni lazima tuwe makini ili tusichanganye haki na kisasi na kuepuka kuwahusisha watu wote wa mahali fulani kuwajibishwa kwa ajili ya ukatili wa wale waliofanya mashambulizi.”

Makamu wa rais wa Marekani Bwana Dick Chenny katika hotuba yake kuadhimisha mwaka mmoja wa shambulio la kighaidi huko New York amezidi kusisitiza ulazima wa kuipiga Iraq kijeshi kwa kile anachokiita “ ili kuiweka dunia katika hali nzuri zaidi”.

Aliyepewa vipandikizi kuzuia mimba akumbwa na maafa

l  Ataota nywele hadi kwenye paji la uso

l Alizaa mtoto njiti, mlemavu; adai fidia ya Dola         Milioni 120

MISSISSIPI

 

MWANAMKE mmoja aliyewekewa vipandikizi ili kuzuia mimba, anaishitaki kampuni iliyompa vidhibiti mimba hivyo kwa kuwa vimemsababishia madhara na uwezekano wa kuzaa mtoto mlemavu, huku mwenyewe akikabiliwa na madhara mbalimbali yakiwamo uwezekano wa kuota nywele kwenye paji la uso na kutoka damu mfululizo.

Kwa mujibu wa habari zilizochapishwa katika Jarida la ‘Population Research Institute’, toleo la Juni 18, mwaka huu, mhanga huyo wa vipandikizi anazishitaki Kampuni za kutengeneza dawa za Wyeth Pharmacenticals, OBGYN, zilizompa vidhibiti mimba hivyo hatari na kumweleza kuwa madhara aliyoyapata hayakutokana na vipandikizi alivyowekewa.

Habari zinasema baadhi ya wahanga katika kesi hiyo, wanaowakilishwa na Mawakili James D. Bell na Johnny Davis, wanadai kesi hiyo iamuliwe na jopo la majaji na pia, walipwe fidia ya Dola za Kimarekani 120.

Mwaka 1999, Wyeth ililipa Dola Milioni 54 kwa wahanga 36,000 wa vipandikizi.

Kesi  hii inaonesha kuwa kutokana na madhara bayana yaliyosababishwa na vipandikizi alivyowekewa mwanamke huyo mwaka 1993, amedhurika na ataendelea kudhurika ikiwa ni pamoja na kupata maumivu ya kichwa na kuongezeka uzito  kwa kiasi kikubwa.

Madhara mengine yanayomkabili mwanamke huyo, ni kuota nywele hadi katika paji la uso, kifua na tumboni, kutoka damu mfululizo, kutoona vizuri, uharibifu wa moyo na homa za mara kwa mara.

Aidha,  habari hizo zinasema, vipandikizi hivyo vimemsababishia ulemavu na madhara mengine ya kiakili na kimwili.

Pamoja na hayo, habari zinasema vipandikizi hivyo vimemsababishia mama huyo mateso makubwa, kutumia gharama kubwa za matibabu, kupoteza uwezo wa kuishi maisha yenye furaha, kutofanya kazi kwa ufanisi na kupungua umri wa kuishi.

Aidha,  amepoteza nafasi yake ya mapato na uwezo wa kufanya kazi ya kumwingizia kipato.

Washitakiwa hao Wyeth na Yazoo City Medical Clinic, wanadaiwa kufahamu kuwa vipandikizi vinasababisha madhara kwa watumiaji, lakini hazikueleza ukweli kuwa vinadhuru mwili na kuathiri vibaya chembechembe hai za mwenendo wa damu ya wanawake wanaovitumia na kusababisha sumu.

Kwa mujibu wa Jarida hilo, washitakiwa Wyeth wanadaiwa kuwa, kwa makusudi kabisa, walishindwa kueleza waziwazi na kutoa taarifa sahihi kwa jamii juu ya hatari zinazoweza kuletwa na matumizi ya vipandikizi.

 Habari zaidi zilisema Wyeth walishindwa kuwaeleza mawakala wao hali na mazingira ya wazi kuwa matumizi za vipandikizi yanaleta hatari ya kunenepa sana, maumivu ya kichwa yanayoambatana na homa za vipindi na kuzaa watoto walemavu.

“Mashitaka yanaeleza kuwa mwanamke huyo alimwendea mganga aliyemweka vipandikizi hivyo katika kliniki ya Yazoo lakini aliambiwa kuwa  matatizo yanayompata hayatokani na vipandikizi hivyo,” lilisema Jarida hilo.

Katika kipindi chote cha kuficha kwa makusudi hatari za vipandikizi, Wyeth iliendelea kuchuma faida kubwa kutokana na mauzo ya dawa hiyo.

Kesi inayataja mashitaka saba yakiwemo ya kutenda kosa kwa makusudi, udanganyifu wa taarifa, kusababisha madhara, kukataa kutoa fidia baada ya madhara kutokea, kukiuka kanuni zinazolinda wateja, uzembe, kupuuzia na kumshawishi mteja kutumia dawa bila kuwa na ufahamu wa kutosha.

Hata hivyo, bado vipandikizi vipo kwenye orodha ya Bodi ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) licha ya kampeni za Shirika la “Population Research Institute” kutaka dawa hiyo isitishwe na kuondolewa katika soko.

Vipandikizi bado vinatengenezwa Ulaya kwa ajili ya kusambaza katika nchi maskini (zinazoendelea). Dawa hiyo inatengenezwa na Leiras International Findland.

Kumekuwa na malalamiko toka kwa watumiaji mbalimbali wa vizuia mimba kama njia ya kupanga uzazi kwa madai kuwa, wazalishaji na wauzaji hawaelezi ukweli juu ya madhara ya vizuia mimba hivyo vikiwamo vipandikizi.

Hali hii ya kutokusema ukweli, imewafanya watumiaji wengi kuathirika kiafya na kisaikolojia.

Nini kilimsibu Askofu Mkuu Milingo hadi akafunga 'ndoa'?

ROME, Italia

 

ALIYEKUWA Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Lusaka nchini Zambia Mhashamu Askofu Emmanuel Milingo amesema kwamba  alikuwa mhanga wa njama za madhehebu ya Sun Myung Moon yaliyoandaa ndoa yake na mwanamke wa Kikorea, Maria Sung.

“Kwa njia yoyote sikuwa mimi niliyemtafuta Mchungaji Moon. Walikuwa ni wafuasi wake waliofanya hivyo,” anasema Askofu huyo katika kitabu cha historia ya maisha yake  ambacho kitachapishwa na 'Edizioni Paolini'.

Askofu mkuu huyo anasema kwamba alikuwa ni mhanga wa ushawishi. “Baadaye nilitambua kuwa nilikuwa nimeangukia mtegoni,” anaandika Askofu Mkuu huyo.

Aidha Askofu Milingo anathibitisha ripoti zilizozagaa mwezi Mei 2001 kufuatia “ndoa” yake iliyoandaliwa na Shirikisho la Familia kwa ajili ya Amani na Umoja wa Ulimwengu kuwa, walikuwa na nia ya kuonyesha uwepo wao Barani Afrika kwa kuanzisha Kanisa Katoliki jingine sambamba na hili.

Ili kuhakikisha kwamba mafunuo yaliyomo kitabuni yanaaminiwa, ameambatanisha barua yenye sahihi yake. 'Ni mahojiano ambayo ningependa kuyatoa ili yatie nuru kwenye ukweli bila kuacha eneo lolote la kutiliwa mashaka,” alisema.

Kitabu hicho chenye kichwa cha maneno “Kuopolewa kutoka kwenye Matope” kitachapishwa siku zijazo Italia, ambapo gazeti la Avvenire tayari limechapisha .

Askofu Mkuu Milingo mwenye umri wa miaka 72  alifunga ndoa na Maria Sung mwenye miaka 43 katika ibada ya halaiki iliyoongozwa na Mchungaji Moon jijini New York.

Madhehebu ya Moon yanasemekana kuwa yaliandaa ndoa hiyo na kuitangaza sana kwenye vyombo vya habari ili kuwavuta Wakatoliki wengi.

Katika mahojiano aliyoyafanya kutokea kwenye makazi yake huko Argentina katika nyumba ya 'Fokolare Movement', Askofu Mkuu Milingo alisema kuwa mkutano wake wa kwanza na Mchungaji Moon ulifanyika kwa matumaini ya kuanzisha uhusiano kati ya madhehebu yake na Kanisa Katoliki.

Alisema kuwa ndiyo wakati huo ile hali yake ya kuchanganyikiwa ilifikia kilele, kutokana na hali ya kutengwa aliyoionja ndani ya Kanisa Katoliki.

Askofu Mkuu Milingo alihamishwa kutoka Jimbo Kuu la Lusaka kwenda Vatican, ambapo aliteuliwa kuwa mshauri wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wahamiaji na Wasafiri, kufuatia hali ya kutoeleweka kwa utume wa uponyaji aliokuwa akiufanya nchini Zambia.

Alisema kuwa wafuasi wa Moon walishurutisha ‘ndoa’ yake na akakubali. Alisema kuwa hata hivyo, hana hakika iwapo alipewa dawa fulani au la.

Katika kuonyesha kwamba uamuzi wa kufunga ‘ndoa’ haukuwa wake alisema kuwa “Bado hakuelewa kwa nini alifanya uamuzi huo.”

Hata hivyo, hakuzungumzia kabisa kuhusiana na siku 72 alizoishi na Maria Sung, ila alisema tu kuwa wakati fulani alimwomba Mungu afe.

Alisema kuwa marafiki zake wawili wa Kiitaliano walimsaidia sana kuachana na madhehebu ya Moon. Baadaye alienda Castel Gandolfo kukutana na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.

“Mkutano wetu ulikuwa mzuri,” anasema Askofu Mkuu, “hakunituhumu kwa jambo lolote. Aliniambia tu kwa imani: "katika jina la Kristo, rudi katika Kanisa Katoliki.”

Kufuatia dakika 20 alizokutana na Baba Mtakatifu, anasema: “nilijisikia nyumbani tena. Na wakati huo nilitambua makosa yangu.”

Baada ya hapo anasema alizungumza na Askofu Mkuu Tarcisio Bertone, Katibu wa Shirika la Mafundisho ya Imani, na maofisa wengine muhimu juu ya suala hilo.

Aliendelea kusema kuwa baada ya hapo alimtembelea tena Baba Mtakatifu baada ya kumweleza Maria Sung kuhusu nia ya kuachana naye na kurudi kwenye wito wake, na kwenda kwenye mafungo ya kiroho kwenye viunga vya jiji la Roma na baadaye Argentina.

Alisema, “niliokolewa kwenye ukingo wa shimo la maangamizi.” Aidha anasema kuwa sasa amegundua kuwa watu wengi walitoa sala na sadaka zao wakimwomba Mungu ili aweze kurudi kanisani. hakujua kama kaka na dada zake ulimwenguni kote walimpenda kiasi hiki.

Vatican yamteua Kardinali Pengo kuwa mjumbe Shirika la  Kipapa

VATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili amemteua Askofu Mkuu wa jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuwa mjumbe wa Shirika la Kipapa la Mafundisho ya Imani linaloongozwa na Mwadhama Joseph Kardinali Ratzinger.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari ya Vatican kupitia tovuti website ya taifa la Vatican, ilisema pamoja na Pengo wengine walioteuliwa ni makardinali, Claudio Hummes Askofu Mkuu wa Sao Paulo Brazil, Crescensio Seppe Mkuu wa Shirika la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Mario Francesco Pampedda, Mkuu wa Mahakama ya Kipapa.

Baba Mtakatifu pia aliwateua maaskofu Henryk Muszynski wa Gniezno, Poland Askofu Mkuu Jean-Pirre Ricard wa Bordeaux, Ufaransa. Na  Askofu Salvatore Fisichella, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Laterano, kuwa wajumbe wa shirika hilo.

Taarifa hiyo ilisema kuwa wajumbe hao watakuwa wanawashauri wale wanaoliongoza shirika hilo na kukutana katika mkutano mkuu kila baada ya miaka miwili.

Shirika hilo lilianzishwa mwaka 1542 na Baba

Mtakatifu Paulo wa Tatu likiwa na katiba iliyojulikana kama “Licet ab initio,” ambapo mwanzoni lilikuwa likijulikana kama Baraza Takatifu la Uchunguzi kwa kuwa kazi yake ilikuwa ni kulilinda Kanisa dhidi ya uzushi. Ndilo shirika kongwe kati ya mashirika tisa yaliyoko chini ya Baraza Kuu la Kanisa au Roman Curia.

Kwa mujibu wa katiba ya kitume ya Baba Mtakatifu “Pastor Bonus” ya mwaka 1988 “wajibu hasa wa Shirika la Mafundisho ya Imani ni kuendeleza na kulinda mafundisho juu ya imani na maadili ya ulimwengu wa Kikatoliki: kwa sababu hii kila kitu ambacho kinagusa masuala hayo yanaangukia ndani ya madaraka ya shirika hilo.”

Padre mwingine afukuzwa Urusi

MKURUGENZI wa Ofisi ya Habari ya Vatican, Dk. Joaquin Navarro-Valls, alitangaza kuwa padre mwingine wa Kanisa Katoliki amefukuzwa kutoka nchini Urusi.

 Alisema kuwa “hili ni tendo baya kabisa kwamba sasa kuna mazungumzo juu ya utesaji wa kweli.”

 Aidha alisema kwamba mpaka sasa Vatican haijapata maelezo yoyote rasmi juu ya sababu zilizopelekea kufukuzwa huko.  Kumekuwa na wimbi la kuwaondolea hati za kuwawezesha kuishi nchini humo viongozi wa Kanisa Katoliki. Nchi ya Urusi ina waumini wengi wa madhehebu ya Kiorthodoksi. Vatican itajaribu kulitatua tatizo hili kwa njia ya kidiplomasia.”