Wakatoliki Palestina wahofu machafuko  Arafat aking'olewa

BETHLEHEM, Ukingo wa Magharibi

 

BAADHI ya Wakristo wanahofu kuwa Waislamu wenye itikadi kali wanaweza kuchukua uongozi iwapo Rais wa Wapalestina Yasser Arafat ataondolewa madarakani.

”Nina hofu kwamba Waislamu wenye itikadi kali watachukua madaraka, kwa sababu hiyo ninataka Arafat abakie kuwa Kiongozi wetu,” alisema mwanafunzi mmoja Mkatoliki wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Bethlehem.

Naye Kiongozi wa wafanyabiashara ambaye pia ni Mkatoliki alisema kuwa Wakristo wengi katika eneo hilo wanakubaliana na mawazo ya mwanafunzi huyo.

Alisema kuwa wafuasi wa Arafat hawana ushawishi mkubwa miongoni mwa Wapalestina kama Waislamu wenye itikadi kali kama Kiongozi wa Hamas leader Sheikh Ahmed Yassin, ambaye “anaweza kuongoza mitaa.”

”Arafat amekuwa sehemu ya makundi ya watu wa kawaida, na Wakristo wanaogopa pale wanapoona makundi makubwa ya Kiislamu,” alisema.

Katika Bethlehem, mahali ambapo Wakristo japo ni wachache wana msingi mkubwa wa kiuchumi, na chama cha Arafat cha Fatah kina ushawishi mkubwa.

Alisema katika maeneo mengine kama Jericho, Waislamu wenye itikadi kali wana nguvu.

Majeshi ya Israel yalizingira makao makuu ya Arafat katika mji wa Ramallah kwenye Ukingo wa Magharibi kutokana na shambulizi la kujitoa muhanga lililofanywa na Wapalestina katika Tel Aviv, Israel, ambapo watu sita walipoteza maisha.

Katika uvamizi huo majeshi ya Israel yalivunja majengo kadhaa katika makao makuu hayo na kumwacha Arafat akiwa ndani pamoja na wafuasi wake wapatao 200.

Hapo Septemba 24, wanajeshi wa Israel wakiwa katika magari ya kivita pamoja na helikopta walishambulia ofisi za wanamgambo wa Hamas katika Ukanda wa Gaza kutafuta Wapalestina wanaojitoa mhanga, ambao hutumwa na kundi hilo.

Katika uvamizi huo watu sita walikufa wakiwemo raia watatu wa Palestina na wanamgambo sita wa Hamas.

Naye Meya wa  Bethlehem, Hanna Nasser, ambaye ni Mkatoliki, alisema kuwa Wapalestina na Waisraeli wanapaswa kujua kwamba kuondolewa kwa Arafat kutasababisha hali ya mambo kulegea sana.

"Palestina bila Arafat haifikiriki,” alisema Nasser na kuongeza “Sidhani kama hii itasaidia mwenendo wa amani au usalama na utengamavu wa hali ya mambo. Hakuna shaka hii italeta tu, ulegevu wa hali ya mambo.”

Pia alielezea mashaka yake juu ya hali ya sasa na kusema kwamba mambo yakiendelea hivi itakuwa vigumu kufanya uchaguzi wa Palestina mwezi Januari kama ilivyopangwa.

Hata hivyo, Bernard Sabella, profesa wa elimu jamii katika Chuo Kikuu cha Bethlehem alisema kuwa hofu ya baadhi ya wakazi wa Kikristo juu ya Waislamu wenye itikadi kali inaweza isiwe na msingi.

"Arafat amekuwa mwema hasa kwa uhusiano kati ya Waislamu na Wakristo, lakini nadhani pia kuwa kuna busara ya kutosha katika viongozi wa Kipalestina wa kisiasa, kijamii na kiuchumi katika jamii ya Palestina hata kati ya wale wenye msimamo mkali,” alisema Sabella.

Alisema Wakristo wanapaswa kuondokana na mawazo kwamba wao ni wachache na badala yake wajiingize katika siasa za Palestina na katika ajenda ya kijamii. Alisema wakati kuna Wakristo ambao tayari wamejihusisha katika mdahalo wa kisiasa kuna wengine wanajisikia kama walioachwa kando.

Katika Bethlehem hapo Septemba 23, Chama cha Fatah cha Arafat na Chama cha Kiislamu cha Kitaifa viliandaa maandamano ya pamoja mbele ya Kanisa la Nativity, huku wanafunzi wa chuo kikuu wakiimba nyimbo za kumuunga mkono Arafat.

"Tupo hapa kuonyesha uungaji wetu mkono kwa Arafat,” alisema Haneen Abu Sauda, 18,mwanafunzi wa biashara katika Chuo Kikuu cha  Bethlehem ambaye ni Mkatoliki.

"Yuko katika hali ngumu sasa hivi na tunataka kumwonyesha kwamba tuko naye. Siwezi kufikiria Palestina bila yeye. Sidhani kitakachotokea bila yeye. Sitaki kuona mauaji mengi zaidi,”alisema dada huyo.

Rafiki yake, Tamara Rishmawi, (18), wa Kanisa la Kiorthodoksi la Ugiriki ambaye pia ni mwanafunzi wa biashara katika Chuo Kikuu hicho, alisema kwamba ilikuwa muhimu kwa Wapalestina kuonyesha uungaji mkono wao kwa Arafat kwa sababu ya matendo mema aliyofanya kiongozi huyo kwa watu wake siku zilizopita.

Karismatiki walenga Uamsho wa Ulaya

CZESTOCHOWA, Poland

 

MKUTANO wa Karismatiki uliomalizika hivi karibuni ulilenga pamoja na mambo mengine kuchunguza “kile ambacho Roho Mtakatifu aliambia Kanisa la Ulaya.”

Mkutano wa Viongozi wa Karismatiki Katoliki wa Ulaya kwa ajili ya huduma za kimataifa ulikuwa na mada kuu: “Ulaya, Tweka Mpaka Klindini” uliishia kwenye sehemu ya hija huko Czestochowa.

Mkutano huo ulilenga na kujadili kile ambacho Mungu anajaribu kusema kadiri Ulaya inavyozidi kuendelea kuungana kisiasa na kiuchumi, na “kutambua mpango wa Mungu na mwito wa Ulaya kuanza upya tena,” taarifa hiyo ilisema.

Mkutano huo wa kimataifa ulifungwa kwa ibada ya misa takatifu iliyoongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu Stanislaw Nowak wa jimbo kuu la Czestochowa.

Washiriki wa mkutano huo walifanya hija huko Auschwitz mahali ilipo kambi alipofia Mt. Faustina Kowalska na ilipo sehemu ya hija kwa ajili ya Huruma ya Mungu katika Krakow, ambayo iliwekwa wakfu na Papa Yohane Paulo wa Pili mwezi Agosti alipotembelea nchi hiyo.

Habari zaidi juu ya Uamsho wa Karismatiki Katoliki Kimataifa zinapatikana kwenye tovuti (mtandao wa kompyuta) ambayo ni: www.iccrs.org.

Rozari ni silaha ya amani – Papa

VATICAN CITY

 

Siku ya Septemba 29 baba Mtakatifu alizungumzia Rozari kama Silaha ya Amani, ifuatayo ni hotuba yake aliyoitoa kabla ya kusali sala ya Malaika wa Bwana pamoja na waamini na mahujaji kwenye makazi yake ya majira ya kiangazi ya Castel Gandolfo.

 

 Wapendwa Kaka na Dada!

 

Tayari tuko kwenye mlango wa mwezi wa Oktoba, ambao huwa na Kumbukumbu ya kiliturujia ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu, mwezi huu unatusukuma kugundua tena mapokeo haya ya sala, ambayo ni rahisi lakini ya kina.

Rozari ni mwono wa kitaamuli wa sura ya Kristo, tunaweza kusema unaofanyika, kupitia macho ya Maria. Kwa hiyo, ni sala ambayo iko moyoni mwa Injili na iko katika amani kamili na wazo la Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vaticano na sana katika kueneda sambamba na yale niliyoonesha katika barua yangu ya kitume, “Novo Millennio Ineunte”: (Tuingie Milenia Mpya). Ni lazima kwamba Kanisa “litweke hadi Kilindini” mwa milenia mpya tukianzia na taamuli (tafakuri) kuhusu sura ya Kristo.

Kwa hiyo, ningependa kupendekeza kwa watu mmojammoja, familia na kwa Jumuiya Ndogondogo za Kikristo. Kulipa umuhimu ombi hili. Pia naandaa waraka ambao utawasaidia kugundua tena uzuri na undani wa sala hii.

Ningependa kukabidhi kwa mara nyingine tena njia kuu za amani kwa sala ya rozari. Tunakabiliwa na hali ya kimataifa iliyojaa mivutano, na sura za mapigano. Katika baadhi ya sehemu za ulimwengu, ambapo makabiliano ni ya nguvu sana – hapa ninafikiria hasa Nchi Takatifu ya Kristo – tunaweza kuona ubora wa njia hiyo ya Rozali. ingawa ni za muhimu juhudi za kisiasa zinafaa kidogo iwapo roho zinabakia katika hali mbaya na hakuna uwezekano wa kuonyesha nia ya moyo kuamsha tena njia ya mazungumzo.

Lakini, ni nani anaweza kutuingizia hisia za namna hiyo kama si Mungu pekee? Ni muhimu  sana sala hiyo sasa, zaidi ya wakati wowote. Kwamba sala kwa ajili ya amani zinainuliwa kwake ulimwenguni kote. Hasa katika mtazamo huu, rozari inajionesha yenyewe kama sala ya kufaa. Inajenga amani pia kwa sababu, wakati inaomba neema za Mungu, inapanda pia kwa yule anayeisali, mbegu ya wema, ambapo kutokana na mbegu hiyo matunda ya haki na mshikamano katika maisha ya kibinafsi na kijamii yanaweza kutarajiwa.

Ninafikiria mataifa, lakini pia familia: ni amani kiasi gani ingehakikishwa katika uhusiano wa kifamilia, iwapo rozari takatifu ingesaliwa na familia!

[Baba Mtakatifu aliwasalimu mahujaji katika lugha saba za Kifaranza, Kiingereza, Kijerumani, Kihispania, Kireno, Kipolandi na Kiitaliano. Katika Kiingereza alisema:]

"Ninawasalimu sana mahujaji na wageni wote wanaozungumza Kiingereza, na ninawakaribisha kuufanya mwezi wa Oktoba wakati maalumu wa uangalifu wa pekee katika kusali rozari, sala kuu ya maombezi kwa Maria. Juu yenu na familia zenu, ninaomba iwepo furaha na amani ya Bwana".

[Mwishoni kwa Kiitaliano, Papa alisema:]

Sala ambayo tunakaribia kuisali, inaanza kwa kukumbuka tangazo la Malaika Mkuu Gabriel kwa Bikira Maria. Kwa kweli, leo ni sherehe ya malaika wakuu Mikael, Gabriel na Raphael: Ninaomba wahudumu hawa wakuu wa Mungu watusaidie kupelekeana daima upendo mkarimu kwa mapenzi yake.

Itakuwa vigumu kuhalalisha shambulizi dhidi ya Iraq - Kardinali McCarrick

WASHINGTON, D.C., Marekani

 

AKISISISTIZA tena msimamo wa wa Baraza la Maaskofu Katoliki wa Marekani, Askofu Mkuu wa Washington, Kardinali Theodore McCarrick aliwashauri watunga sheria kuepuka vita na Iraq isipokuwa uhai wa Marekani kama umo katika hatari ya mara moja.

“Sasa hivi tungesema vita ya kujilinda iwapo hali fulani ingeruhusu,” alisema Askofu huyo Mkuu wa Washington wakati akiongea na radio ya WTOP, kwa mujibu wa gazeti la Catholic Standard.

“Unapoiangalia Iraq, ninahisi iwapo Rais angekuwa na habari za aina hiyo kwamba tupo katika hatari ya kweli mara moja, kutoka Iraq hapo tungeweza kuwa na kesi,” alisema kardinali.

“Sidhani kama maaskofu wanahisi kesi ya namna hiyo imeishafanywa,” aliongeza “Ndiyo maana tunasema tafadhali nenda taratibu, tafadhali jaribu kuona kwa hakika jinsi hali ilivyo kabla ya kufanya jambo fulani ambalo tungesema lisingekuwa la maadili.”

Askofu huyo mkuu alikuwa katika kipindi maalumu cha “Muulize Kardinali” ambapo maswali mengi yalijikita juu ya Iraq, kashfa za ngono kwa maklero, utafiti juu ya seli shina za viinitete na uhaba wa mapadre.

Kardinali huyo alisema kuwa hata katika vita ya kujilinda, nchi husika inapaswa kufuata sheria za ulinganifu wa njia zitakazotumika na kuepuka madhara kwa raia wema.

Aliongeza kuwa shambulizi la kwanza dhidi ya Iraq litakuwa vigumu sana kulihalalisha, bila kuwepo ushahidi wa wazi juu ya kuwepo kwa silaha za kibayolojia nchini humo.

“Nadhani kile maaskofu wanachotumaini ni kwamba kadiri Rais na Bunge la Congress wanavyozungumzia jambo hili, tunaweza kuwa na fursa ya kupima tunu za kimaadili, kitu ambacho watakifikiria pia,” alisema Kardinali McCarrick.

 

 

It is prepared by Miss. Christina Nyambo. Authorised and run by Rev. Fr. Revocatus Makonge, Exec. Sec. of the Communications Department of TEC.

 

Please visit the TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE WEB SITE