Papa aongeza matendo katika Rozari

l Atangaza Mwaka wa Rozari kwa ajili ya familia na Amani

l Sasa itakuwa na mafumbo 20

VATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, ameadhimisha mwaka wa 24 wa upapa wake kwa kutangaza mwaka wa Rozari, kuchapisha barua ya kitume kuhusu  sala ya Rozari ya Bikira Maria na kupendekeza ‘mafumbo ya nuru’ kuongezwa kwenye sala hiyo.

Papa alitia saini waraka huo na kuutoa katika moja ya mikutano yake ya kila juma mbele ya mahujaji 17, 000 waliokusanyika kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Mt. Petro, huko Vatican.

alitumia wasaa huo kusisitiza tena nia yake ya kuendelea kuwa Papa kadiri ya mapenzi ya Mungu ambapo alikabidhi mikononi mwa Maria ‘uhai wa Kanisa na ubinadamu unaojaribiwa.’

“Kwake nakabidhi maisha yangu ya baadaye. Naweka kila kitu mikononi mwake ili kwa upendo wa kimama, aendelee kuyapeleka kwa Mwanae”, aliongeza.

Katika barua hiyo ya kitume inayoitwa Rosarium Virginis Mariae (Rozari ya Bikira Maria), Papa anatoa Sala ya Maria kama ‘tafakari juu ya mafumbo ya maisha na kazi ya Kristo iwapo itasaliwa ‘kwa uchaji na si kwa midomo tu.

 “Kwa kurudia mwito wa Salamu Maria tunaweza kuakisi kikamilifu juu ya matukio muhimu ya Utume wa Mwana wa Mungu duniani ambao umeletwa kwetu na Injili pamoja na Mapokeo,” alieleza Papa.

Na kwa kuwa katika mafumbo 15 ambayo bado yanasaliwa hadi leo matukio makubwa ya maisha ya Kristo hadharani hayakutafakariwa, katika barua mpya ya kitume Papa anaongeza mafumbo matano anayoyaita ‘Mafumbo ya nuru’, yanajumuisha maisha ya hadharani ya Kristo tangu ubatizo wake katika mto Yordani yakihitimishwa na mateso yake.

 Katika Sehemu ya Pili ya Barua hiyo, Papa anatangaza ‘Mwaka wa Rozari’ kuanzia mwezi huu wa Oktoba2002,  hadi Oktoba 2003.

Baba Mtakatifu alielezea kuwa tangazo hilo la mwaka huu linaadhimisha matukio matatu muhimu ambayo ni mwanzo wa mwaka wa 25 wa Upapa wake, mwaka wa 120 wa Barua ya Baba Mtakatifu Leo wa Kumi na Tatu inayoitwa Supremi Apostolatus Officio, iliyoanzisha mfululizo wa nyaraka juu ya Rozari, na pia kufunga Mwaka Mtakatifu wa 2000.

Alisema katika historia ya Jubilei Kuu, desturi ilikuwa kwamba baada ya mwaka wa Jubilei uliotolewa kwa Kristo na kwa kazi ya ukombozi mwaka mmoja baada ya hapo, ulitangazwa ili kumuenzi Maria kama ishara ya kuomba msaada wake ili kuzaa matunda kwa njia ya neema zilizopokelewa katika Jubilei.

Kama ishara ya kuwaaga mahujaji alisema, “Mwaka wa Rozari Takatifu ambao tutauishi pamoja ni wazi utazaa matunda ya faida katika mioyo ya wote, utafanya upya na kuzidisha matendo ya neema za Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 na utakuwa chanzo cha amani ya dunia.”

Katika kuelezea uamuzi wake wa kuongeza mafumbo matano ya nuru katika rozari ya sasa, Papa alisema kuwa Rozari ya Bikira Maria ni kamaufupisho kamili(compedium) za Injili” uliolenga ‘kutafakari Sura ya Kristo’ kupitia macho ya Maria na kurudiarudia Sala ya Salamu Maria.

Mpaka sasa mafumbo 15 ya Rozari yaani ya Furaha, ya Uchungu na ya Utukufu yamekosa nyakati mahususi katika maisha ya Kristo hadharani, alieleza Baba Mtakatifu.

Kwa sababu hiyo, Papa anapendekeza kuingiza “mafumbo ya huduma ya Kristo ya hadharani kati ya Ubatizo wake na mateso yake.”

Alisema anamuacha huru mtu mmojammoja, au na jumuiya zao kuamua juu  ya hilo.

Papa alieleza kwamba, anayaita mafumbo haya “Mafumbo ya Nuru” kwa sababu Kristo katika maisha yake ya hadharani alijionesha kama “Fumbo la Nuru:” “Wakati nikiwa bado ulimwenguni, mimi ndimi nuru ya ulimwengu’ (Yn. 9:5).”

Katika Kifungu cha 21 cha barua hiyo,Baba Mtakatifu anatilia mkazo Mafumbo ya Nuru yake matano ya maisha ya hadharani ya Yesu na kufafanua fumbo ambalo Mkristo hutafakari katika kila Kifungu cha matini yafuatayo: Ubatizo wa Yesu, Kujidhihirisha kwake katika Harusi ya Kana, Utangazaji wake wa Ufalme wa Mungu, pamoja na mwito wake kwa uongofu, Kugeuka kwake sura, na Kuweka Sakramenti ya Ekaristi kama kielelezo cha Fumbo la Pasaka.

“Ubatizo katika Yordani kwanza kabisa ni Fumbo  la Nuru,” alisema. “Hapa Kristo anaposhuka majini mtu asiye na hatia aliyefanyika ‘dhambi’ kwa ajili yetu (2Kor 5:21), mbingu zinafunguka na sauti ya Baba inamtangaza Kristo kama Mwana Mpendwa (Mt. 3:17) wakati Roho Mtakatifu anamshukia kumkabidhi utume ambao angeutiza.”

Fumbo jingine la nuru ni ishara ya kwanza iliyotolewa kule Kana (Yn. 2:1-12) wakati Kristo anapogeuza maji kuwa divai na kuwafungua wafuasi wake mioyo yao kupata imani kwa sababu ya ombi la Bikira Maria.

Fumbo jingine linahusu mahubiri ya Kristo wakati anapotangaza kuja kwa Ufalme wa Mungu na kutoa wito kwa watu ili waongoke (Rej. Mk 2: 13, Lk 7: 42-48) na anasamehe dhambi wote wanaomwendea Kristo kwa tumaini nyenyekevHuduma hiyo inaendelea  katika Sakramenti ya Upatanaisho ambayo ililikabidhi Kanisa.(Rej. Yh.20: 22-23).

Fumbo la nne ni “fumbo la nuru hasa” ambalo ni Kugeuka sura kwa Yesu tendo ambalo linatoa wito na mafundisho mengi na ya kufaa kwa Mkristo.

Fumbo la mwisho ni kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ambamo Kristo anatoa mwili na damu yake kama chakula katika maumbo ya mkate na divai na kushuhudia fumbo hilo ‘mpaka mwisho’ kwa sababu ya upendo wake kwa wanadamu ambao kwa ajili ya wokovu wao atajitoa kuwa sadaka (Yn 13:1).

Kwa mujibu wa barua hiyo, Papa anapendekeza kuwa mafumbo hayo ya Nuru yasaliwe siku ya Alhamisi ambapo mafumbo ya Furaha yatasaliwa siku za Jumatatu na Jumamosi, mafumbo ya Uchungu yatasaliwa Jumanne na Ijumaa na mafumbo ya Utukufu yatasaliwa siku ya Jumatano na Jumapili.

Maaskofu Ufaransa wapinga vita ya Iraq

PARIS, Ufaransa

 

KAMPENI  ya Marekani na mshirika wake mkuu Uingereza kutaka kuishambulia kijeshi Iraq imegonga kigingi kingine hivi karibuni baada ya Baraza la kudumu la Maaskofu Katoliki wa Ufaransa kusema hatua ya namna hiyo haiwezi kuhalalishwa katika hali ya sasa.

 Msimamo huo wa maaskofu dhidi ya kile ambacho kinapingwa na watu wengi duniani ulitolewa katika tamko lao lililotolewa juma lililopita.

 “Mazingira ya vurugu ambamo mashambulizi ya kijeshi katika sehemu mbalimbali za dunia hututumbukiza yanatuelekeza kurudia na kusisitiza tena kwamba heshima ya kila uhai wa binadamu ni sharti la amani ya kweli,” lilisema tamko hilo la baraza.

 Miongoni mwa wale waliotia saini tamko hilo ni pamoja na Askofu Mkuu Jean-Pierre Ricard wa Bordeaux, na rais wa baraza la maaskofu katoliki wa Ufaransa.

 Pia yumo Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Paris na mjumbe wa baraza hilo la kudumu, Mwadhama Jean-Marie Kardinali Lustiger. Tovuti ya Baraza la Maaskofu wa Ufaransa ni www.cef.fr.

 “Mkabala na uwezekano wa operesheni ya kijeshi inayopigiwa upatu na Marekani dhidi ya Iraq, ni sehemu ya utume wetu kukumbusha kwamba kutanzua tofauti miongoni mwa mataifa, vita haiwezi kuchukuliwa kama njia miongoni mwa nyingine zinazoweza kuchaguliwa kufuatana na kufikiria maslahi au fursa,” maaskofu hao wa Ufaransa walieleza.

 “Kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa pamoja na maadili ya Kikatoliki, kuchagua matumizi ya silaha, hata kama hatua hiyo ina lengo linalopendelewa na kwa ajili ya maslahi ya pamoja, unahusisha uamuzi mkubwa vile kwamba huwezi kukimbilia njia ya vita isipokuwa katika hali isiyoepukika na pale tu endapo masharti magumu kadhaa yatakuwa yametimizwa, “ liliongeza tamko hilola maaskofu.

 “Kwa sasa, taarifa zilizopo haziwezi kuruhusu uhalalishaji wa kwamba masharti kama yalivyofupishwa katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki (Na. 2309) yametimizwa. Tunashiriki maoni ya namna hii na ya baraza la maaskofu ambayo wameyaeleza juu ya suala hili pamoja na mwangalizi wa Vatican katika Umoja wa Mataifa,” walisisitiza maaskofu hao.

 “Hivi utawala wa Iraq, pamoja na kwamba unalaaniwa kwa ukiakaji wake wa haki za watu katika Iraq na kwa sheria ya kimataifa, unahusisha kitisho cha haraka na cha mara moja, jambo ambalo linaweza kuwa kesi halali ya ulinzi? “ walihoji. Na kuongeza “iwapo utawala huo una kitisho cha kweli, haipasi njia zote kutumika kwanza badala ya kukimbilia njia za kijeshi kuuondoa?

 

“Matokeo ya ‘hatua hii ya bila kurudi nyuma’ ambayo ni hoja kuhusu kila vita, ni usumbufu kwa maoni ya umma,” waliendele kusema maaskofu hao.

 “Mkabiliano kati ya taifa la Kiarabu na Marekani utaimarisha hoja ya itikadi ya Uislamu wa siasa kali kuibua uhasama wa makundi yasiyolindwa na yasiyoharifiwa dhidi ya ‘Magharibi’ walisema.

 “Vita itapanua pengo ambalo tayari limechimbwa kati ya watu wetu na watu wa Ukanda wa Mashariki ya Kati, ambapo, zaidi ya hayo tunaweza kutaja kaka zetu wengi katika Kristo, pengo ambalo linasababisha hisia kali kwamba mataifa makubwa ‘hutumia vipimo viwili tofauti’ katika kutekeleza maazimio ya Umoja wa Mataifa,” walilalama Maaskofu hao wa Kifaransa.

 “Sasa hivi zaidi ya wakati mwingine wowote, haki ni msingi na sharti la amani,” lilihitimisha tamko hilo.

Waganda wawili, Wamisionari wanne watangazwa wenye heri

l Asema utakatifu ndiyo ushuhuda bora wa kutangaza Injili

 

VATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliadhimisha Jumapili ya Missioni Ulimwenguni kwa kuwatangaza wenyeheri vijana makatekista wawili kutoka Uganda pamoja na wamissionari wanne waliouawa kwa sababu ya imani yao.

 Katika ibada hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa la Mt. Petro papa aliwasifu wamisionari wake kwa waume kwa kujitoa bila ubinafsi ili kutangaza Injili.

 “Niko nanyi kila siku,” alisema Baba Mtakatifu. “Niko pamoja na wewe. Yesu analimbia kanisa lililoko safarini ulimwenguni. Niko pamoja nanyi, jumuiya ndogo za kikanisa katika nchi za misioni. Msiogope kujihusha katika mazungumzo na watu wote. Peleka ujumbe wa wokovu kwa kila mmoja. Muwe wajasiri!”

 baba Mtakatifu alisema kuwa huu ulikuwa ni ushuhuda ulioachwa na Daudi Okelo pamoja na Jildo Irwa, makatekista wa Uganda kaskazini ambao waliuawa kikatili kwa imani yao hapo Oktoba 18, mwaka 1918. Vyanzo vya kihistoria vinasema kuwa Daudi alikuwa na umri wa miaka 16 na Jildo miaka 12.

 Picha za vijana hao wa Kiganda zilitundikwa katika ya sehemu ya mbele ya Kanisa la Mt. Petro, mara baada ya Papa kutamka kanuni kuu ya uenye heri.

 “Wanatolewa kwa jumuiya nzima ya Kikristo kama mfano wa utakatifu na fadhila, na kama vielelezo na waombezi kwa makatekista ulimwenguni kote, na hasa wale walio katika sehemu zile ambapo makatekista bado wanateseka kwa sababu ya imani yao, na wakati mwingine kukabiliwa na kutengwa kijamii na hata hatari kubwa,” alisema papa katika mahubiri yake.

 Aidha Baba Mtakatifu aliuelezea mfano wa makatekista hao kama unaoweza kuvuvia maisha ya “wanaume na wanawake wengi – katika Uganda, katika Afrika, na mahali popote – kujibu kwa ukarimu wito wa kuwa katekista, kwa kuleta maarifa juu ya Kristo kwa wengine na kuimarisha imani ya jumuiya zile ambazo ni hivi karibuni tu zimepokea Injili ya wokovu.”

 Wakati wa misa ya kuwatangaza wenyeheri makatekista hao, nyimbo za utamaduni wa Kiafrika ziliimbwa na ujumbe mkubwa wa kutoka Uganda uliohudhuria misa hiyo ukiongozwa na Makamu wa Rais wa Uganda, Dk. Speciosa Wandira Kazibwe, ambapo Waafrika wengi walivalia nguo zao za kijadi.

 Wakati wa misa hiyo pia kulikuwa na nyimbo katika lugha ya ki-Tamil, ili kumkumbuka mwingine wa waliotangazwa kuwa wenyeheri, Mary wa Mateso.

 Mwenyeheri huyo aliyezaliwa(1839-1904) katika Ufaransa  Hélčne Marie de Chappotin de Neuville , alianzisha Shirika la kitawa la Wamisionari wa Maria katika India, mwaka 1874. Leo shirika hilo lina watawa 8,000 katika nchi 77.

 Pia katika misa hiyo Baba Mtakatifu alimtangaza kuwa mwenyeheri Mwitaliano Liduina Maneguzzi (1901-1941), mhubiri wa Injili katika Ethiopia, ambaye alikuwa mtawa wa kwanza katika Shirika la Masista wa Mt. Francis de Sales. Kazi yake ya umisionari ilifupishwa katika umri wa miaka 40 kwa ugonjwa wa kansa.

 Mmoja wa wale waliohudhuria misa hiyo, Mwitaliano Giacomo Colombo, 52, alikuwa miongoni mwa wale waliohudhuria sherehe za uenyeheri. Colombo aliponywa katika mwaka 1976 kutokana na majeruhi ya ajali mbaya ya gari baada ya familia yake kumwombea apone kupitia maombezi ya Liduina.

 Watumishi wa Mungu wengine wawili waliotangazwa kuwa wenyeheri ni Waitaliano Andrea Giacinto Longhin (1863-1936) aliyekuwa mtawa wa Kikapuchin na kwa miaka 32 kama Askofu wa Treviso, ambapo alikuwa mfano kwa kuishi umaskini na kwa unyenyekevu. Alikuwa akijulikana kama “askofu wa kanisa.”

 Mwingine ni Mwitaliano Marcantonio Durando (1801-1880), padre wa Shirika la Kitume ambaye pia alikuwa mwanzilishi wa Shirika la Masista wa Nazarene. Kama Mt. Vincent wa Paulo, “alijua namna ya kutambua katika ubinadamu wa Kristo kielelezo kikubwa cha upendo wa Mungu kwa kila mtu,” alisema Baba Mtakatifu.

 Kutangazwa wenyeheri kwa Wakristo hawa sita “kunatukumbusha kuwa huduma ya kwanza ambayo tunapaswa kutoa kwa utume ni utafutaji wa kweli na endelevu wa utakatifu,” alisisitiza Baba Mtakatifu. “Hatuwezi kutoa ushuhuda kwa Injili kikamilifu kama hatuiishi kwanza kiaminifu.”

 Mwishoni mwa sherehe hizo, kabla ya kusali sala ya Malaika wa Bwana, Papa aliwasifu “wamisionari wake kwa waume – mapadre, watawa wa kike na kiume, pamoja na walei – waliotumia nguvu zao katika utumishi wa mstari wa mbele kwa Kristo, na kwa nyakati nyingine hata kutoa ushuhuda kwa damu yao.”

 Kwa mujibu wa Shirika la Vatican la Uinjilishaji wa Watu, mwaka jana tu wamisionari Wakatoliki 33 waliuawa katika Asia, Afrika na Amerika ya Kusini wakati wakihubiri Injili.

 Habari zaidi kutoka Vatican zinasema kuwa, hadi sasa Baba Mtakatifu yohane Paulo wa Pili ametangaza wenyeheri 1,303 katika miaka 24 ya upapa wake.