Maaskofu Peru wapinga kuhalalishwa utoaji mimba

LIMA, Peru

 

JARIBIO la Bunge la Peru kufungua milango kwa utoaji mimba uliohalalishwa kisheria lilisababisha Maaskofu Wakatoliki kuandika barua iliyopuuza mashambulizi dhidi ya uhai wa watoto wasiozaliwa bado.

Juma lililopita baraza la maaskofu lilichapisha tamko lililoelekezwa kwa watunga sheria wa nchi hiyo, ambao juma moja kabla walikuwa wamepitisha kifungu ambacho kingerekebisha Katiba.

Waraka huo uliopitishwa na watunga sheria hao unatamka: “Adhabu ya kifo ni marufuku. Utoaji mimba umepigwa marufuku isipokuwa inaweza kuruhusiwa kisheria.”

Habari  zaidi zinasema ni sentensi hiyo ya mwisho iliyoamsha “malalamiko hayo makubwa” ya Maaskofu Wakatoliki.

“Kuhusishwa kwa uwezekano mbadala wa kisheria juu ya utoaji mimba katika Katiba, ni shambulizi dhidi ya uhai-haki ya kwanza ya msingi-kuwaachwa watoto wa Peru bila ulinzi wa kikatiba na kuwaweka wamama kukabili matokeo ya kushiriki katika mauaji ya watoto wao wenyewe,” lilisema tamko la maaskofu.

“Itakuwa ni mara ya kwanza kwamba inatamkwa eti utoaji mimba unaruhusiwa katika Katiba ya Latin Amerika,” waliongeza maaskofu hao.

“Suala la utoaji mimba si la kidini, kijamii au kisiasa pekee: ni tatizo la kibinadamu,” walisema na kuongeza “tunu ya uhai inapita mtazamo wa kiimani, kwa sababu ni suala la kibinadamu. Mtu mwenyewe yuko katika hatari kubwa sana.”

Barua ya maaskofu hao iliendelea kueleza sentensi ‘isipokuwa pale inaporuhusiwa kisheria,’ inafungua uwezekano kwamba siku zijazo uwezekano wa kwamba sheria inaruhusu utaongezeka na kuuacha utoaji mimba ukiwa umehalalishwa katika ngazi ya kikatiba.”

Maaskofu walionyesha kuchanganywa katika kifungu kilichopitishwa na wabunge “kwa upande mmoja, adhabu ya kifo ni marufuku … na kwa upande mwingine, uwezekano wa kisheria unawekwa wazi kwa kifo cha wasio na utetezi wa wasio na hatia.”

“Sisi,  maaskofu wa Peru, tunatoa wito kwa dola kuheshimu makubaliano ya kimataifa yaliyotiwa saini. Hii ndiyo sababu tunawakumbusha kwamba Mkataba wa Amerika juu ya Haki za Binadamu, au Mkataba wa San Jose de Costa Rica, ulioridhiwa na Peru, unasema: ‘Kila mtu ana haki ya kuwa na maisha ya heshima. Haki hii italindwa na sheria, kwa jumla, kuanzia wakati wa kutunga mimba. Hakuna atakayenyang’anywa uhai wake,” lilihitimishwa tamko la maaskofu.

Wanauamsho wa madhehebu mbalimbali wakutana Roma

ROME, Italia

 

VIONGOZI wa Uamsho kutoka madhehebu na jumuiya mbalimbali za Kikristo barani Ulaya, waliashimisha 30 ya Umoja wao wa Mashauriano (ECC) kwa kufanya mkutano uliozungumzia mahusiano baina yao. Lengo la umoja huo ni “kuvuvia, kushajiisha, kumotisha na kuwezesha uendelezaji wa uamsho wa Kanisa, Umoja wa Kikristo na uinjilishaji kote barani Ulaya.”

 Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na umoja huo ilisema kwamba baraza la umoja huo pamoja na wageni walitafakari tukio la Oktoba 9-13 juu ya jinsi wanavyoweza kuitikia wito wa Papa Yohane Paulo wa Pili “kutweka hadi kilindini.”

 Mwanateolojia wa Kikatoliki Padre Peter Hocken alipitia mikakati iliyopendekezwa, akisisitiza sehemu muungano na tofauti juu ya mada ya toba wa dhambi za miaka iliyopita.

 Mwanateolojia mwingine, Dan Juster, wa kundi la Masiha wa Kiyahudi, alijadili historia ya kundi la Masiha wa Kiyahudi na kuwashirikisha wajumbe maarifa mapya juu ya “Kuelekea Mtaguso wa Pili wa Jerusalem,” jitihada ya toba na upatanisho kati ya Wayahudi na Watu wa Mataifa ambao ni sehemu ya Ukristo.

 Katika mkutano wa Roma, Mchungaji mmoja wa Kanisa la Kipentekoste Peter Dippl wa Berlin, ambaye alikuwa ametumikia kama mwenyekiti mwenza wa ECC kwa miaka 12 alitangaza kustaafu wadhifa huo.

 Mchungaji huyo alirithiwa na mchungaji mwingine wa Kipentekoste Olaf Franke, pia wa Berlin, ambaye sasa ataungana na mwenyekiti mwenza wa Kikatoliki Kim Catherine-Marie Kollins, mwanachama wa Jumuiya ya Heri Nane.

Papa alaani shambulizi la Bali

VATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, amelaani shambulizi la kigaidi katika kisiwa cha Bali, Indonesia lililoacha watu 187 wakiwa wamekufa na zaidi ya 300 wakiwa wamejeruhiwa na kutuma salamu za rambirambi kwa ndugu wa wahanga.

Katika ujumbe wake juu ya shambulizi hilo Baba Mtakatifu aliliita la “kikatili na kitendo cha vurugu kisichoongozwa.”

Ujumbe huo wa telegram uliotumwa kwa balozi wa Vatican jijini Jakarta, Katibu wa Vatican, Kardinali Angelo Sodano, alisema kuwa Papa “ameshutushwa sana na shambulizi hilo la kutisha.”

Ujumbe huo wa Papa ulisema kuwa “vitendo kama hivi vya kikatili haviwezi kuwa njia kuelekea jamii ya haki na iliyostaarabika, na ni lazima yalaaniwe na wote wanaojitahidi kujenga ulimwengu wenye amani juu ya heshima kwa thamani isiyokanika ya uhai wa kila binadamu.”

Waziri wa Ulinzi wa Indonesia, Matori Djalil Abdul alililaumu kundi la kigaidi la al-Qaida kuwa nyuma ya shambulizi la kisiwa cha utalii cha Bali.

Orodha ya kwanza ya waliokufa na waliojeruhiwa ilihusisha walau raia wa mataifa 16, wengi wao wakiwa Waustralia, ambapo 13 walidhibitishwa kuwa wamepoteza maisha na 110 wamejeruhiwa.

Naye Askofu Mkuu Francis Carroll, rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki wa Australia, alisema katika taarifa yake kuwa “Kwa niaba ya Kanisa Katoliki katika Australia, nawatumia salamu za pole wote wanaoomboleza au wanaosubiri habari zaidi, huruma yetu na uhakikisho wa sala zetu. Huduma za afya na ushauri nasaha za Kanisa zitakuwa tayari kupatikana kwa wale wote watakaohitaji hivyo.”

“Ninakaribisha Wakatoliki kuhudhuria katika makanisa ya maeneo yao na kushiriki katika sala, kuonyesha mshikamano wao na wahanga wa shambulizi hilo,” alisema Askofu huyo Mkuu wa Canberra na kuongeza “Ninapendekeza kwamba Jumapili ijayo iwe ni siku ya kitaifa ya sala na kumbukumbu.”

Aidha alisema “Hakuwezi kuwa na nafasi kwa ajili ya vurugu kwa jina la dini. Sasa hivi zaidi ya wakati mwingine wowote, wale wanaomwamini Mungu ni lazima wajenge madaraja ya amani. Wote wanaoamini kwamba ni watoto wa Mungu lazima wakiri kwamba wale wote wanaowazunguka ni kama dada na kaka katika familia moja ya kibinadamu. Australia inayo nafasi ya pekee kuuonyesha ulimwengu kuwa tamaduni na dini tofauti zinaweza kuishi pamoja kwa amani.”

Aliongeza “Kuna haki kutetea watu wasio na hatia dhidi ya ugaidi. Haki lazima itumike kwa kujali mipaka ya kimaadili na kisheria. Vurugu haziwezi kushughulikiwa kwa njia ya vurugu zaidi. Heshima, maelewano na mazungumzo ili kuandaa njia kwa ajili ya amani iliyojikita juu ya haki.”

Vyuo vikuu lazima vihifadhi utamaduni wa Kikristo - Papa

lAzungumzia changamoto za utandawazi

VATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu, Yohane Paulo wa Pili amesema vyuo vikuu na shule za Kikatoliki inabidi zikabiliane na changamoto za kulinda utamaduni na utambulisho wa Kikristo katika zama hizi za utandawazi.

 Papa aliyasema hayo alipokutana na maaskofu wa Chile wakati wa ziara yao huko Roma ifanyikao kila baada ya miaka mitano, 'ad limina'  alisema “katika nyakati za vitisho vikubwa vinavyoonekana hasa kwa nchi dhaifu kiuchumi, kiufundi na kiutamaduni.”

 Hata hivyo, “utandawazi bado unavyo vitu ambavyo vinaweza kutoa fursa ya kukuza utamaduni wa Kikristo,” alisema.

 Katika mazingira haya, Baba Mtakatifu alisema “jitihada za watu wa Chile kujiingiza katika jumuiya ya ulimwengu ni lazima waangalie ili wasipoteze utambulisho wao wa kiutamadumi.”

 Alisema kuwa ni lazima waepuke kupunguza kila kitu na kuwa “mabadilishano ya kiuchumi” na lazima watoe “kila mahali tunu bora kabisa za ‘alma patria,’ yao ambayo imeungana na mapokeo yao ya Kikatoliki.”

 “Hii itatajirisha  zaidi sana mazingira ya tamaduni nyingi kwa njia ya mitazamo ya kuheshimiana na kupalilia mazungumzo ambayo yanalenga kutafuta ukweli, baada ya kuachana na ubabaishaji na kuhusianisha mambo, ambayo huendeleza kutojali na kuharibu hali ya amani,” alisisitiza Baba Mtakatifu.

 “Shule pamoja na vyuo vikuu vya Kikatoliki, ambavyo, tumshukuru Mungu ni vingi sana nchini Chile, lazima vichangie kufikia hili,” alisema.

 “Nina hakika kwamba maaskofu wataendelea kuvipa vyuo hivi umuhimu mkubwa kwa sababu vimelengwa ili kuiongoza jamii ya Chile kufikia utume mzuri wa Injili ya Kristo.”