Baraza la Wawakilishi Marekani lapongezwa

WASHINGTON, D.C

 

Baraza la Maaskofu Katoliki wa Marekani limewapongeza wajumbe wa baraza la wawakilishi la nchi hiyo kwa kupitisha muswada ambao utaziwezesha hospitali au asasi za bima kukataa kufanya au kulipia utoaji mimba bila kuhatarisha misaada yao kutoka serikalini.

Baraza hilo lilipiga kura kupitisha muswada huo kwa kura 229 dhidi ya 189, hata hivyo muswada huo unakabiliana na kigingi kigumu zaidi katika Baraza la Seneti.

“Sheria ya namna hii inatakiwa haraka sana kwani inahakikisha tena kwamba hakuna mtoa huduma za afya yeyote atakayelazimishwa kushiriki utoaji mimba kinyume na utashi wake,” alisema Richard M. Doerflinger, naibu mkurugenzi wa Sekretarieti ya Shughuli za Kulinda Uhai ya Baraza la Maaskofu.

Naye Kardinali Anthony Bevilacqua, mwenyekiti wa Kamati ya Kulinda Uhai ya maaskofu, alikuwa amewaandikia habari wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi akiwashauri kupitisha muswada huo, unaofafanua mtazamo wa sheria dhidi ya ubaguzi ya mwaka 1996 iliyopitishwa na Baraza la Congress.

“Sheria ya sasa inalinda asasi za afya ikiwemo mipango ya kitabibu ya ukazi, kuachana na kulazimishwa na vyombo vya serikali kufanya utoaji mimba ama mafunzo juu ya utoaji mimba,”alisema Kardinali Bevilacqua.

“Muswada mpya unaweka wazi kwamba ulinzi huu unahusisha asasi zote za afya, zikiwemo hospitali na wanataaluma wengine wa afya wasio madaktari,” alisema na kuongeza “Pia ulinzi huu unahusisha asasi zinazoambiwa kwamba ni lazima zilipie utoaji mimba kinyume na utashi wao.”

Wakati huo huo, utawala wa Rais George W. Bush ulisema kuwa ungepanga fetuse s katika makundi kama watoto ambao hawajazaliwa hiyo ikiwa kama njia ya kupanua huduma ya prenatal kwa wanawake wenye kipato kidogo, liliripoti shirika la habari la Associated Press.

Mabadiliko hayo yanaruhusu majimbo ya kiserikali nchini Marekani kupanua bima za afya mpaka kuhusisha viinitete, kwa kuviorodhesha katika Mpango wa Kijimbo wa Bima ya Watoto, shirika hilo la habari lilisema.

Askofu Moscow  ataka Waorthodoksi wafafanue maneno

ROME, Italia

 

KATIKA kutafuta kuwa na mazungumzo baina ya Wakristo wa madhehebu mbalimbali katika Urusi, vifungu vinavyosababisha migawanyiko ni lazima vifafanuliwe.

Wito huo ulitolewa na mkuu wa Baraza la maaskofu Katoliki nchini humo Mhashamu Askofu Mkuu Tadeusz Kondrusiewicz.

 Askofu Mkuu Tadeusz Kondrusiewicz wa jimbo katoliki la Mama wa Mungu katika Moscow alielezea imani hii wakati akihudhuria mkutano mkuu wa Jumuiya ya Mabaraza ya Maaskofu wa Ulaya (CCEE), uliofanyika mjini Sarajevo, nchini Bosnia-Herzegovina.

 Kwa mujibu wa shirika la habari la SIR, Askofu Mkuu Kondrusiewicz alisisitiza kwamba Askofu mzaliwa wa Poland Jerzy Mazur na baadhi ya mapadre Wakatoliki walifukuzwa kutoka Urusi “bila sababu yoyote kabisa,” wakati “Dalai Lama, wachungaji wawili wa Kiprotestanti na viongozi wawili wa Kiislamu wamenyimwa viza za kuingilia nchini Urusi.”

 Alisema kuwa katika mazingira ya sasa ni lazima kufafanua na kufikia makubaliano juu ya kanuni za kiteolojia za misimamo mbalimbali kuhusiana na dhana kadhaa kama utume, ushawishi kwa waamini wa kanisa moja ili wajiunge na lingine na eneo halali kwa kanisa Fulani.

 “Sambamba na mtazamo huu, na kundi kiekumeni lenyewe lazima lipange katika roho ya upendo, ukweli na haki, likizingatia hali halisi ambamo inabidi lifatie kazi zake,” Askofu Mkuu Kondrusiewicz alisema.

 Alisema katika maoni yake, mtu hawezi kupuuza kuharibika kwa uhusiano kati ya Kanisa Katoliki na Patriaketi ya Moscow. Hali hii itaathiri kwa kiwango kikubwa uhusiano na Kanisa lote la Orthodoksi, “hasa ikizingatiwa kwamba katika Urusi ndiyo kuna Kanisa kubwa la Orthodoksi ulimwenguni kote.”

 “Zaidi ya hayo, ulimwengu wa leo unaangalia sana maendeleo ya uhusiano na Urusi, jambo ambalo linalotimiza wajibu muhimu katika siasa na uchumi,” alisema.

 Aidha alisema kuwa anaamini hivyo kwa sababu, “licha ya matatizo ya sasa katika uhusiano wetu na Kanisa la Orthodoksi, siku itafika wakati tutakapomtukuza Mungu pamoja na tutasaidia kujenga ustaarabu mpya wa upendo, uliojikita katika misingi ya Injili, kuheshimiana na usafi wa moyo.”

Utakatifu wa Mama Teresa wavuka hatua muhimu

l Makardinali na Maaskofu watambua 'tunu zake za kishujaa'

VATICAN CITY

 

Makardinali na maaskofu wa Idara inayoshughulikia Mambo ya Utakatifu wamekiri na kutambua “tunu za kishujaa” za Mama Teresa wa Calcutta katika maisha yake yote, kama hatua muhimu kuelekea kutangazwa kwake kuwa mtakatifu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Zenit lenye makao yake mjini Rome na linalojihusisha na habari za Kanisa Katoliki, habari hizo ziliripotiwa na Vatican .

Habari zaidi zilisema kuwa utambuzi huu umekuja siku moja baada ya kuwasilishwa kwa utafiti wenye kurasa 80,000 wa maisha ya Mama Teresa.

Habari zinasema kuwa makardinali na maaskofu hao wanatarajiwa kukutana tena ili kuutafakari muujiza unaodaiwa kusababishwa na maombezi ya Sista Agnes Gonxha Bojaxhiu (jina la ubatizo la Mama Teresa), ambapo mwanamke mmoja aliponywa uvimbe tumboni uliosababishwa na kansa.

Habari zisizothibishwa zilisema kuwa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili angeweza pia kuhudhuria mkutano huo na kutangaza mara moja utambuzi wa “tunu za kishujaa” za Mama Theresa na muujiza wake, vyanzo vya Vatican vilisema.

Mama Theresa aliyezaliwa katika Skopje, mji mkuu wa Macedonia mwaka 1910, mtawa huyo alikuwa maarufu ulimwenguni kote kutokana na huduma yake kwa maskini huko Calcutta, India.

Habari zaidi zilisema kuwa Mama Teresa anaweza kutangazwa mtakatifu mapema mwakani, hatua ambayo itavunja rekodi zote za miaka ya karibuni, kwa kuwa mchakato wa utakatifu wake ulianza rasmi hapo Julai 26, 1999, chini ya miaka miwili baada ya kifo chake.

Kwa kawaida michakato ya utakatifu ilipaswa kufunguliwa miaka mitano baada ya kifo chake, lakini Papa Yohane Paulo wa Pili alitoa ruhusa maalumu katika kesi hii.