Make your own free website on Tripod.com

Wakatoliki, Walutheri kuungana?

VATICAN CITY

 

KANISA Katoliki linaendelea kufanya kazi kuelekea umoja kamili na Kanisa la Kilutheri, amesema Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili wakati akipokea ujumbe wa Kanisa la Kiluteri kutoka Norway.

Ujumbe huo uliwasilishwa katika Vatican siku ya sherehe ya Mtakatifu Olaf, Msimamizi wa Norway Mfalme huyo aliyekufa kishahidi ndiye aliyeleta Ukristo katika Norway mwaka 1015. Alipinduliwa na kuuawa mwaka 1028 na maadui wa kipagani.

“Tuna jukumu la kuendelea mbele zaidi katika njia ya mapatano,” alisema Baba Mtakatifu.

“Azimio la pamoja juu ya Mafundisho ya Kuhesabiwa Haki kati ya Shirikisho la Kanisa la Kilutheri na Kanisa Katoliki linasafisha njia kwa ushuhuda zaidi wa pamoja. Linatuleta katika hatua karibu na umoja kamili ambalo ni lengo la mazungumzo yetu.”

Azimio hilo lilisainiwa Augsburg, Ujerumani Oktoba 31 mwaka 1999.

Wakati wa Mkutano, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, alikumbuka ziara yake ya kitume katika Norway na nchi nyingine za Scandinavia mwaka 1989, na ibada ya kiekumene kwenye Kanisa Kuu la Nidaros katika Trondheim akiwa pamoja na Askofu Kristen Kyrre Bremer.

“Ilikuwa ni alama mpya na ya kina ya uhusiano wa kiekumene kati yetu ambao mwaka 1993, uliliwezesha Kanisa la Kiluteri kuruhusu jumuiya ya Kikatoliki kuadhimisha miaka 150 ya kuanzishwa tena kwa Kanisa Katoliki katika Norway ndani ya Kanisa la zamani sana,” alisema Baba Mtakatifu.

“Mungu atusaidie kutunza kilichopatikana mpaka sasa, na atupe nguvu katika jitihada zetu kuendeleza maendeleo kuelekea ushirikiano mpana zaidi,” alisema.

Wafransiskani wachangia kumaliza mgogoro wa Bethlehem

ROME, Italia

 

KITABU kipya juu ya mzingiro wa Kanisa kuu la Bethlehem kimepongeza na kusisitiza wajibu muhimu waliotimiza watawa wa Kifransiskani katika Nchi Takatifu ili kutanzua mgogoro huo.

Waandishi wa kitabu hicho: “balaa ya Kanisa la Kuzaliwa Bwana” ni mashahidi walioona kwa macho kila tukio katika mgogoro wa kanisa hilo na waliona wajibu uliotimizwa na Monasteri ya Wafransiskani ili kutanzua mzingiro huo.

Kitabu hicho kiliwasilishwa katika Roma na kuchapishwa na kampuni ya uchapishaji ya Ponte alle Grazie, kinasimulia siku 39 za balaa ya mgogoro kanisani, tangu Aprili 2 mpaka Mei 10, wakati majeshi ya Israel yalipolizingira eneo hilo ambamo Wapalestina karibu 200 walikuwa wamejichimbia.

Waandishi hao, Giuseppe Bonavolonta na Marc Innaro, waandishi wa habari wa Televisheni ya Taifa ya Italia (RAI) katika Mashariki ya Kati, wamechanganya ushuhuda wao na matukio ya kila siku yaliyoandikwa na Padre Ibrahim Faltas, Msimamizi wa Kanisa Kuu la Kuzaliwa Bwana.

“Nilikaa ndani ya kanisa kwa siku mbili za mwanzo za mgogoro na Giuseppe Bonavolonta alikuwa nje,” Innaro aliiambia Redio Vatican, Aprili 2, wakati waandishi walipokuwa wamenasa kwenye mapigano katika Mashariki ya Kati, walimpigia simu Padre Faltas.

“Tufungulie mlango Ibrahim, wanatujia, tumekwama, hatuwezi kurudi nyuma, Waisraeli wanatushambulia,” walimwambia Padre Ibrahim ambaye aliwajibu “Ndiyo njooni, lakini muwe makini kwa sababu wanashambulia hapa pia.”

“Tulidhani kuwa hiyo ndiyo ilikuwa sehemu salama zaidi,” alisema Innaro. “Saa chache baadaye, Wapalestina zaidi ya 200 wenye silaha walibisha hodi milangoni wakiwa na milipuko aina ya Kalashnikov waliingia na kutafuta hifadhi huko kuwakimbia wanajeshi wa Israeli walikuwa tayari wameukalia mji huo mzima.

“Kuanzia wakati huo na kuendelea tuliwaona Wafransiskani wa Nchi Takatifu wakijaribu kuingilia kati na kutanzua mgogoro, sura na kazi ya Mt. Fransisko akitembea kutoka sehemu moja hadi nyingine akiwa amebeba ujumbe wa utu, wa matumaini.”

“Na kwa kweli katika jina la ubinadamu Wafrasiskani walifaulu katika kile walichokusudia: kuokoa maisha ya binadamu kwa kujaribu kutoka nje kwenda kwa Waisraeli na Wapalestina,” waandishi hao walisema.

Kwa upande wake Mwandishi Giuseppe Bonavolonta aliongeza: “Kuna kitu fulani cha msingi katika ujumbe wa Kifransiskani. Kwani mapinduzi makubwa, matukio makubwa ya kifikra mara nyingi yamepelekea mifumuko ya kutovumiliana.

Ujumbe halisi ni ule wa mtu ambaye hufaulu kutembea kutoka kizuizi kwenda kingine, ambaye hufaulu kutimiza majukumu yake mwenyewe … kama mtu wa amani.”

Miezi sita baada ya mgogoro huo, hali inaendelea kuwa mbaya. “Watu bado wako na wasiwasi sana,” alisema Padre Ibrahim Faltas, Mlinzi wa Kanisa.

“Hakuna amri ya kutotoka nje usiku, Jeshi la Israeli haliko ndani ya mji, lakini watu hawawezi kwenda kazini. Kuna ukosefu wa kazi,” alisema.

“Mji umezuiwa hakuna watalii wala wahujaji na asilimia 80 ya watu wote wa Bethlehem hufanya kazi katika sekta ya utalii,” aliongeza Padre huyo.

“Hawawezi kwenda Israel kufanya kazi. Matumaini ni kwamba jumuiya ya kimataifa itafanya kila linalowezekana kutanzua mgogoro kati ya Waisraeli na Wapalestina.”

Naye Msemaji wa Monasteri ya Wafransiskani katika Nchi Takatifu Padre David Jaeger alisema katika mazingira ya namna hii, mzingiro wa kanisa kuu uliwakilisha ishara ya mateso ya ukanda mzima. Aliyasema hayo wakati wa kuwasilisha kitabu akiwa pamoja na Padre Giovanni Battistelli, mlinzi wa Nchi Takatifu.

Padre Jaeger alisema suala kuu la Bethlehem “kwa mara nyingine lilitoa haja ya haraka kwa jumuiya ya kimataifa kutoa ulinzi wa kisheria kwa eneo hili ambao tayari ulishafafanuliwa katika mwaka 1947 na Umoja wa Mataifa kama ‘corpus separatum’: dhamana maalumu ya kimataifa ya kisheria, inayotamaniwa sana na Umoja wa Mataifa pamoja na Kanisa, hasa kwa Sehemu Takatifu.

Padre Jaeger alipendekeza kuwa hili linaweza kutekelezwa kwa njia ya “mkataba wa pande mbili ambao utaheshimiwa na Waisraeli na Wapalestina, lakini pia na mataifa mengi ya Ulaya, Amerika na mengine ambayo yatasadia kuhakikisha utekelezaji wake.”

Askofu Mkuu Milingo sasa atumikia hadharani

l Asema alikuwa katika wakati mgumu, lakini alisali na kutunga nyimbo

VATICAN CITY

 

ASKOFU Mkuu Emmanuel Milingo wa Zambia amerejea rasmi katika maisha na huduma zake za hadharani katika mji mmoja mdogo karibu na Roma, taarifa ya Vatican imesema.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Shirika la Habari la ZENIT likinukuu Ofisi ya Habari ya Vatican iliwajulisha “waamini” kwamba Novemba 21 Askofu Mkuu huyo mstaafu wa Lusaka, aliongoza misa takatifu katika Abasia ya Casamari, jimboni Frosinone.

Misa hiyo ilikuwa ni tukio la kwanza hadharani kwa Askofu Mkuu huyo mpunga pepo, baada ya mwaka wa mafungo ya kiroho katika Argentina kufuatia “ndoa” yake ya Mei 2001 na Maria Sung.

Ndoa yao ilifungwa katika Ibada ya Shirikisho la Familia kwa ajili ya Amani na Umoja Duniani (Kanisa la Umoja), linaloongozwa na Mchungaji wa Kikorea Sun Myung Moon; ndoa ambayo hata, hivyo haikutambuliwa na Kanisa Katoliki.

Kuonekana kwake mara ya kwanza hadharani tangu kumaliza mafungo hayo ilikuwa katika Televisheni ya Taifa ya Italia (RAI), mwishoni mwa Septemba ambapo alisema kwamba, alikuwa ameteseka sana, lakini akasema kuwa jaribio hili sasa limempita.

“Niko mzima japokuwa nimepita katika nyakati ngumu. Nimeishi pia katika nyakati za furaha katika Argentina. Nilikuwa na muda wa kusali, kuandika, kutunga nyimbo na kutafakari,” aliongeza.

Abasia ya Casamari, mahali atakapofanyia mikutano yake ya hadhara iko karibu na mji wa Zagarolo, ambapo Askofu Mkuu huyo anaishi.

Kabla ya kukutana na Kanisa la Umoja, Askofu Mkuu Milingo alikuwa  akiadhimisha misa za “uponyaji” zilizohudhuriwa na maelfu ya waamini. Kwa kuwa ibada hizi zilikuwa mara nyingi zenye msisimko zikiwa pia na “maelezo ya tena na tena” ya taratibu za upungaji pepo, maaskofu wa Italia walimpiga marufuku kutofanya misa katika majimbo yao.

Kutokana na hali hiyo, Askofu Milingo alilazimika kufanya shughuli zake katika mahoteli, hali hiyo ya kutengwa iliishia katika mgogoro ambao ulimfanya kutafuta kutambuliwa na Kanisa la Umoja.

Hata hivyo, mgogoro huo pia ulimpatia fursa ambazo mwanzo alizikosa, kama vile kukutana ana kwa ana na Baba Mtakatifu ambaye alimwomba kurejea kundini.

Tangazo la Vatican juu ya kurejea katika maisha ya hadhara  linasisitiza kukubaliwa kikamilifu tena kwa Askofu Mkuu huyo na Kanisa Katoliki, vyanzo vya Vatican vililiambia ZENIT.

Shahada ya Juu ya sheria za Kanisa sasa miaka mitatu

 

VATICAN CITY

 

MUDA wa Masomo kwa Shahada ya Juu katika Sheria za Kanisa (Canon Law) umeongezwa na kuwa miaka mitatu badala ya miaka miwili.

Habari kutoka Shirika la Habari la Vatican zinasema kuwa zoezi hilo litaanza katika mwaka  wa masomo wa 2003-2004 ambapo mitaala ya Shahada ya Juu maarufu kama licentiate itaongezwa kuwa  mihula sita katika mzunguko wa pili kati ya mizunguko mitatu ya masomo hadi kupata Shahada ya Udaktari.

Mitaala inayoagiza shahada hiyo kusomewa miaka miwili (mihula mitatu) iliyokuwa inatumika  hadi sasa ilianzishwa na Katiba ya Kitume ya mwaka, 1979 ijulikanayo kama “Sapientia Christiana,” iliyotangazwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili.

Agizo hilo kutoka Shirika la Habari la Vatican lililosainiwa na Mkuu wa Shirika hilo,Kardinali Zenon Grocholewski na Katibu wake,Askofu Mkuu Giuseppe Pittau, na kuidhinishwa na Baba Mtakatifu linasisitiza kuwa ili kusomea Shahada ya Juu ni lazima muhusika kuwa na Shahada ya Kwanza katika Sheria hizo za Kanisa.

Vile vile agizo hilo limetoa masharti kwa wote wanaotaka kuchukuwa Shahada ya Juu hiyo,ni lazima kujua lugha ya Kilatini.

Agizo hilo linaeleza kuwa mitaala iliyotangazwa mwaka 1979 si halali tena kwa ajili ya kufundisha na kuelewa masomo. Kanuni ya sasa ya sheria za kanisa ilichapishwa mwaka 1983, na kanuni ya Makanisa ya Mashariki ilichapishwa mwaka 1990.

Matini ya agizo hilo inasomeka hivi “baada ya kumaliza miaka miwili ya masomo ya 'licentiate', malezi ya kisheria kwa wanafunzi haikufikia kiwango cha maarifa ya Sheria za Kanisa yanayotakiwa sasa ili kutimiza majukumu ya kikanisa yanayodaiwa maadalizi mwafaka katika sheria za kanisa.”

Agizo hilo linazidi kueleza kuwa, wakati “masomo ya kiteolojia na kichungaji katika vitivo vya kitelojia yameboreshwa, muda na uangalifu mdogo vilitolewa kwa sheria za kanisa na lugha ya Kilatini katika Seminari Kuu.”

“Mabadiliko haya yanafanywa na Shirika la Elimu ya Kikatoliki, baada ya kupata ushauri kutoka vitivo na Vyuo vya Sheria za Kanisa” agizo hilo linabainisha.

Sheria za Kanisa zinahusisha taratibu za kimahakama au vifungu vya sheria vinavyotokana na mamlaka halali ya kanisa moja kwa moja au kwa njia ya mzunguko ili kuongoza maisha ya Kanisa. Maneno “Sheria za Kanisa” pia yanahusu sayansi inayotoa mafunzo ya jinsi sheria hizo zilivyotungwa.

Kwa mujibu wa taratibu, mapadre wanaoingia katika huduma ya kidiplomasia ya Vatican ni lazima wawe na shahada ya juu ya uzamili katika sheria za kanisa. Maaskofu na makamo maaskofu wengi wa majimbo pia wanazo shahada za juu za uzamili au hata za udaktari wa falsafa katika somo hili.

“Mageuzi haya ni ya muhimu sana kwa Kanisa, ikizingatiwa kwamba sheria za kanisa ni sehemu ya maisha yetu ya kidini; kwa hiyo haiwezi kutenganishwa na imani yetu,” alisema Askofu Mkuu Pittau katika agizo hilo na kuongeza “ni yule tu mwenye maarifa ya kutosha katika imani yetu anayeweza pia kuelewa utaratibu wa sheria hizi.”