Make your own free website on Tripod.com

Hakuna maendeleo bila kuheshimu thamani ya mtu -  Vatican yasema

l Yataka tofauti za kiutamaduni ziheshimiwe

NEW YORK, Marekani

SERA za maendeleo ni lazima zijikite kwenye “utambuzi wa thamani ya binadamu” na kutambua “tofauti za kitamaduni,” ilisema Vatican katika Umoja wa Mataifa.

Wito huu ulitolewa na Askofu Mkuu Renato Martino, mwangalizi mkuu wa Vatican katika Umoja wa Mataifa, wakati wa mdahalo juu ya “Utamaduni na Maendeleo.”

Alisema kuwa mipango kwa ajili ya vita dhidi ya umaskini “lazima ijikite kwenye utambuzi wa thamani ya binadamu, utetezi wa haki za binadamu na uhuru wa msingi, na heshima kwa tofauti na upekee wa kiutamaduni.”

“Uelewa huu wa msingi unapelekea kuwepo kwa mshikamano wa kibinadamu ambao hukuza muungano wa kijamii na kukubali kwa kina urithi wa pamoja wa binadamu,” aliongeza askofu mkuu katika hotuba yake.

“Ni upendo wa Mungu peke yake unaoweza kuwafanya wake kwa waume wa kila taifa na utamaduni wawe kaka na dada, wanaweza kukiuka migawanyiko, tofauti za kiitikadi na kiuchumi, na ukiukaji wa vurugu ambao bado unawakandamiza wanadamu,” alisema mwakilishi huyo wa Vatican akinukuu ujumbe wa Papa Yohane Paulo wa Pili katika Siku ya Missioni Duniani.

“Hoja hiyo inasisitiza tamko lililotolewa na Vatican wakati wa Mkutano wa Kilele wa Maendeleo Endelevu,” aliendelea askofu mkuu “Ukweli kwamba dunia na rasilimali zake zote ni sehemu ya urithi wa pamoja kwa wanadamu wote ambao huumba maelewano yanayoendeleza kutegemeana, mkazo wa majukumu na kusisitiza umuhimu wa kanuni ya mshikamano wa dunia.”

“Ukweli huu unakuwa msingi wa maendeleo endelevu kwa kuongoza umuhimu wa kimaadili wa haki, ushirikiano wa kimataifa, amani, usalama na hamu ya kuboresha ustawi wa roho na mali wa vizazi vilivyopo na vijavyo,” aliendelea.

“Haya si mawazo mazuri au matashi mema ya baadaye tu. Na wala hayaonekani tu kama uwajibikaji wa kundi moja, asasi au wakala. Na wala mjadala hauwezi kujikita tu juu ya kulinda utamaduni kutoka zile kanuni ambazo zinaweza kuleta matokeo mazuri kwa maendeleo,” alisisitiza.

“Badala yake mjadala ni lazima ulenge katika utafutaji wa njia za kuruhusu utamaduni kusaidia maendeleo kama vile maendeleo yanavyopaswa kusaidia utamaduni,” alisema.

Askofu mkuu alitoa pendekezo hilo kuhusu mazingira mapya ya hali ya ulimwengu, akimnukuu Baba Mtakatifu alisema, “mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 mwaka jana na hali mbalimbali za ukosefu wa haki ulimwenguni kote, zinatukumbusha kwamba milenia iliyoanza inaleta changamoto kubwa.

Milenia hii inatoa wito wa majitoleo kwa upande wa mtu mmojammoja, watu na mataifa kulinda na kutetea haki na thamani ya kila mwanafamilia ya binadamu,” alisema.

Aliongeza “wakati huohuo, milenia inadai ujenzi wa utamaduni wa utandawazi wa mshikamano ambao utatoa maelezo zaidi si tu kwa maneno  juu ya uchumi bora au asasi za kisiasa ila zaidi mambo hayo inabidi yafanyike katika roho ya kuheshimiana na ushirikiano katika huduma ya maslahi ya pamoja.”

“Ujumbe wangu husikia tena na tena kwamba ulimwengu umebadilika sana,” alisema Askofu Mkuu Martino na kuongeza “Ni kweli umebadilika. Laikini wema wa msingi, thamani ya binadamu, ndoto na malengo huendelea kuwasukuma watu wa ulimwengu, hasa wale wanaotafuta maisha mema kwa ajili yao na vizazi vijavyo.”

Mwakilishi wa Vatican UN atajwa

VATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili amemteua katibu mdogo wa Vatican wa uhusiano na mataifa, Mheshimiwa Monsinyori Celestino Migliore, kuwa mwakilishi wa Vatican katika Umoja wa Mataifa jijini New York.

Monsinyori Migliore anachukua nafasi ya Askofu Mkuu Renato Martino, ambaye ameteuliwa kuwa rais wa Shirika la Kipapa la Haki na Amani.

Uamuzi wa kumteua mtu kama huyo ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu la Vatican, maarufu kama Curia unaonyesha umuhimu ambao Baba Mtakatifu anauweka kwa mchango wa Vatican katika Umoja wa Mataifa liliripoti shirika la habari la ZENIT lenye makao yake mjini Roma.

Kazi ya Askofu Mkuu Martino imekuwa ni ya kimaamuzi katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa katika New York, na katika mikutano ya Umoja wa Mataifa.

Monsinyori Migliore, 50, atapewa daraja la uaskofu, kutokana na Papa kumpa heshima ya kuwa askofu mkuu, ilitangaza Vatican.

Mheshimiwa Monsinyori Celestino Migliore ambaye ni mzaliwa wa Cuneo, Italia, alipata daraja la Upadre hapo Juni 25, mwaka 1977. Baada ya kupata shahada katika sheria za kanisa, aliingia katika huduma ya kidiplomasia ya Vatican mwaka 1980, na amewahi kufanya kazi katika nchi za Angola, Marekani, Misri na Poland.

Katika mwaka 1992, Monsinyori Migliore aliteuliwa kuwa mwangalizi wa kudumu katika Baraza la Ulaya huko Strasbourg, Ufaransa, na katika mwaka 1995 alitajwa na Vatican kuwa katibu mdogo wa uhusiano wa mataifa katika ofisi ya Secretariati ya taifa la Vatican.

Kanisa haliwezi kuinyamazia Euthanasia – Papa

VATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili amesema kuwa Kanisa Katoliki halitanyamaza pale mataifa mbalimbali yatakapokuwa yakihalalisha mauaji ya watu hasa wagonjwa na wazee kwa kisingizio cha kuwaondolea maumivu (euthanasia).

 Papa alionya juu ya hatari za euthanasia, wakati alipokuwa akimpokea balozi mpya wa Ubegiji katika Vatican, nchi ambayo pamoja na Uswisi tayari zimehalalisha mauaji ya namna hiyo.

 Katika hotuba yake kwa mwanadiplomasia huyo wa Ubelgiji, Benoit Cardon De Lichtbuer, 60, Papa alisema “mtu ameumbwa na Mungu na kuitwa kushiriki katika maisha yake ya Kimungu, ndiyo maana Kanisa huheshimu na kulinda uhai.”

 “Ni kwa vipi Kanisa linaweza kunyamazisha shauku yake kubwa na majaribu mkabala na sheria zilizopitishwa hivi karibuni katika nchi mbalimbali ambazo zinahalalisha mauaji ya watu eti kuwapunguzia maumivu,” alihoji Baba Mtakatifu.

 “Katika jamii ambamo kinachojaliwa zaidi ni afya njema na faida, ni muhimu kuwaangalia kwa macho mengine watu dhaifu au wale walio karibu na mwisho wa uhai wao, hasa kwa kutumia na kuendeleza utunzaji wa faraja kwa wagonjwa wote ambao hali yao inahitaji kitu kama hicho,” alisema.

 Utunzaji huu “unawezesha kupunguza maumivu na kuwapa msaada kwa heshima wale wanaokaribia kufa,” alielezea Papa.

 “Utambuzi wa tabia takatifu na haki zisizopaswa kukiukwa za kila mtu ambazo wamepewa na Muumba, hiyo ndiyo ulinzi pekee dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu,” alisisitiza Baba Mtakatifu.

 Aliongeza kuwa “jamii ambayo itajiingiza katika hatari za kuvunja kanuni hizi itajiweka wazi kukabiliwa na hatari kubwa zaidi hasa kufanya haki za watu pamoja na tunu za msingi kutegemea tu makubaliano, ambayo hubadilika daima.”