Papa atoboa siri ya Rozari

l Alipigwa risasi Siku ya Bikira Maria wa Fatima

l Aliitolea Tanzania kwa Bikira Maria

          

VATICAN CITY

 

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili,ametoboa siri ya yeye kuhimiza matumizi ya Sala ya Rozari Takatifu ya Bikira Maria.

Akizungumza kwa waamini wa waliokusanyika katika Viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro hivi karibuni, Baba Mtakatifu aliwahimiza Wakatoliki na watu wengine wanaosali Sala ya Rozari Takatifu, kuwa rozali inajumuisha njia bora za kukuza majitoleo ya kutafakari uso wa Kristo.

“Sababu muhimu ya kupendekeza tena kusali Rozari, ni ukweli kwamba inajumuisha njia bora za kukuza majitoleo ya kutafakari uso wa Kristo miongoni mwa waamini, jambo nililoliomba kufuatia Jubilei Kuu ya mwaka 2000,” alisema Baba Mtakatifu.

Akaongeza, “Bikira Maria ni mfano mkubwa wa tafakari ya Kikristo,” alieleza Papa akikumbuka maudhui ya barua yake ya kitume “Rosarium Virginis Mariae.”

“Tangu kuchukuliwa mimba kwa Kristo mpaka ufufuko na kupaa kwake mbinguni, Mama yake aliendelea kuelekeza moyo wake usio na doa kwa Mwanae wa Kimungu: tafakari ya ajabu, inayopenya mioyo, ya huzuni na yenye kung’ara,” alisisitiza.

“Ni katika mtazamo huu wa Ki-Maria, uliojaa imani na upendo, Mkristo na Jumuiya ya Kanisa, hufanya sala yao wakati wanaposali Rozari,” alisema Papa.

Alisema, hiyo ndiyo sababu ya yeye kupendekeza kuongezwa kwa Mafumbo ya Nuru katika Rozari, yanayohusu maisha na kazi za Yesu.

Katika KIONGOZI toleo lililopita, tuliripoti kuwa katika Maadhimisho ya Miaka 24 ya Upapa, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, alitangaza Mwaka wa Rozari na kupendekeza Mafumbo ya Nuru kuongezwa katika sala hiyo.

Historia ya maisha ya Papa Yohane Paulo wa Pili inaonyesha wazi Ibada kubwa aliyonayo yeye binafsi kwa Mama Bikira Maria. Tangu aliposimikwa kuwa Baba Mtakatifu ,aliutolea utume wake chini ya maombezi ya Bikira Maria,ndiyo maana hata nembo yake ina herufi’M’ ikimanisha ‘Matoleo maalumu kwa Bikira Maria’.

Katika  tukio lisilo la kawaida la jaribio la kumuua,lililofanyika Mei 13 mwaka 1981 na Mehmet Ali Agea (23) raia wa Uturuki,jaribio hilo lilifanyika katika sikukuu ya Bikira Maria wa Fatima ,na kuokoka kwake yeye alikuelezea ni kutokana na maombezi ya Bikira Maria.

Katika ziara zake katika nchi mbalimbali duniani,Papa amekuwa akisisitiza Ibada kwa Bikira Maria kwa kugawa zawadi ya rozali kwa kila anayekutana naye;na kumtaka asali Rozali.

Akiwa nchini Tanzania katika ziara yake ya Kichunguji mnamo Septemba 1990,Baba Mtakatifu mara tu baada ya kuwasili nchini alielekea katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu lililopo katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam,ambapo aliongoza sala ya Rozali kuiombea nchi hiyo  Amani na Utulivu.

Katika Barua ya Kitume inayoitwa Rosarium Virginis Mariae (Rozari ya Bikira Maria), Papa anatoa Sala ya Bikira Maria kama tafakari juu ya mafumbo ya maisha na kazi ya Kristo iwapo itasaliwa kwa uchaji na si kwa midomo tu.

Katika kuelezea uamuzi wake wa kuongeza mafumbo matano ya nuru katika Rozari ya sasa, Papa alisema kuwa, Rozari ya Bikira Maria ni kama ufupisho kamili wa Injili uliolenga kutafakari sura ya Kristo kupitia macho ya Maria na kurudiarudia Sala ya Salamu Maria.

Alisema hadi sasa mafumbo 15 ya Rozari yaani, ya Furaha, Uchungu na Utukufu, yamekosa nyakati mahususi katika maisha ya Kristo hadharani.

Kwa sababu hiyo, Baba Mtakatifu alipendekeza kuingiza Mafumbo ya Huduma ya Kristo ya hadharani kati ya Ubatizo wake na mateso yake.

Katika Kifungu cha 21 cha barua hiyo, Papa anatilia mkazo juu ya Mafumbo ya Nuru  ya maisha ya hadharani ya Yesu na kufafanua fumbo ambalo Mkristo hutafakari katika kifungu cha matini.

Anayataja matini hayo kuwa ni Ubatizo wa Yesu, Kujidhihirisha kwake katika Harusi ya Kana, Utangazaji wake wa Ufalme wa Mungu, Mwito wake kwa uongofu, kugeuka kwake sura na kuweka Sakramenti ya Ekaristi kama kielelezo cha Fumbo la Pasaka.

Akizungumza hivi karibuni, Baba Mtakatifu alisema, “Kama kila sala ya dhati, Rozari haituondoi kutoka uhalisia wa mambo, ila hutusaidia kuiishi sala hiyo tukiwa tumeunganika na Kristo kwa ndani, huku tukitoa ushuhuda  kwa upendo.”

Papa Yohane Paulo wa Pili, pia aliwakumbusha waamini, kama alivyofanya katika barua yake ya kitume, kwamba amani na familia ni malengo mawili ya msingi ya kusali Rozari.

Kwa namna ya pekee, Papa alitoa wito wa kuwaombea watu wa Urusi ambao katika siku hizi za hivi karibuni, wamekuwa katika mateso makali wakati wa mgogoro wa utekaji nyara katika jumba la maigizo jijini Moscow.

Mgogoro huo uliisha Jumamosi ya Novemba 26, mwaka huu, baada ya makomandoo wa Jeshi la Urusi kuwaokoa mateka ambapo watekaji nyara wote 50 waliuawa pamoja na mateka 117.

“Wakati tunawaombea wahanga wa kisa hicho cha maumivu, tumwombe Bikira Mtakatifu ili matukio kama haya yasiweze kurudiwa,” alisema Papa.

Vatican yaisaidia Uganda kupiga vita UKIMWI

l Yatenga fedha, yazindua mpango wa elimu na kinga

VATICAN CITY

 

VATICAN imechangia kuimarisha vita dhidi ya UKIMWI nchini Uganda kwa kutoa kiasi cha euro 500,000 pamoja na juhudi nyingine.

Habari hizo zilichapishwa katika tamko la Shirika la Vatican la “Cor Unum,” asasi ya Vatican inayoongozwa na Askofu Mkuu Paul Cordes, ambayo ina dhamana ya kukuza na kuratibu huduma za hisani katika Kanisa duniani.

Habari zaidi zinasema Askofu Mkuu Cordes, alifanya ziara nchini Uganda hivi karibuni kuangalia pamoja na mambo mengine, mipango ya kupiga vita UKIMWI.

Mchango huo wa Vatican ulifanywa kwa ombi la Papa Yohane Paulo wa Pili alilotoa  mwezi Februari mwaka jana, kuunga mkono kazi za asasi za Kikatoliki, zisizo za serikali na za Wamisionari wa Upendo.

Wakati wa ziara ya Uganda, Askofu Mkuu Cordes, alitoa umuhimu wa pekee kwa hali ya watoto.

“Katika Uganda, asilimia 50 ya watoto wamepoteza walau mzazi mmoja kwa sababu ya UKIMWI. Wengi wa watoto hao wanakabiliwa na hatari ya kuishia mitaani” na kujihusisha katika uhalifu, lilisema Shirika la 'Cor Unum'.

“Cor Unum” ilisema kwamba imeanzisha vipaumbele kadhaa katika Uganda, ambavyo ni pamoja na kuwapa yatima familia, kuendeleza elimu kwa njia ya kujenga na kusaidia shule na kutoa elimu ya afya ya kinga dhidi ya UKIMWI.

Vipaumbele vingine ni kutoa mafunzo ya kitaaluma, hasa kwa wavulana wanaoondoka katika mahabusu za vituo vya watoto wadogo na kuanzisha nyumba kwa ajili ya watoto wanaougua UKIMWI, itakayoendeshwa na Wamisionari wa Upendo.

“Mradi huu uko kwenye mazingira ya kupiga vita UKIMWI unaoendeshwa katika ngazi ya taifa,” na kuheshimu “mipaka ya Benki ya Dunia na Shrika la Fedha Duniani (IMF),” tamko hilo lilisema.

Uganda imekuwa nchi ya maabara katika kupambana na UKIMWI. Ni moja ya nchi chache ambamo kiwango cha maambukizo ya VVU( Virusi vya UKIMWI) yamepungua kutoka asilimia 9.51 hadi 8.30,” iliripoti Cor Unum.

“Hata hivyo, matokeo haya si lazima yasifikiriwe kama hatua ya mwisho bali kama mwanzo wa maslahi na miradi mipya,” ilielezea Shirika hilo.

Oktoba 25, Askofu Mkuu Cordes alitembelea Cowa, kituo cha mafunzo ya kitaaluma katika jiji la Kampala kwa ajili ya wavulana ambao huko nyuma walikuwa katika vituo vya mahabusu za watoto.

Siku iliyofuata, Askofu Mkuu alipokewa na Wamisionari wa Upendo ili kuzindua nyumba ya watoto 60  wanaougua UKIMWI.

Habari zinasema kuw,a baada ya hapo alitembelea nyumba ya watoto yatima ya Nsambya na shule ya Cowa kwa ajili ya mafunzo ya kitaaluma ya wasichana yatima ambao wazazi wao walikufa kwa UKIMWI.

Siku ya Oktoba 27, Askofu Mkuu Cordes alihudhuria sherehe katika Jimbo Kuu Katoliki la Kampala.

Siku iliyofuata alitembelea Gulu, kaskazini mwa Uganda, ambapo Kanisa linafanya kazi kwa ajili ya kuleta amani katika eneo hilo jirani na Sudan ambalo limekuwa vitani kwa miaka 15.

Oktoba 29, Askofu Mkuu alikutana na Baraza la Maaskofu Katoliki wa Uganda pamoja na shirika la Caritas-Uganda.

Oktoba 30, rais huyo wa “Cor Unum” alitembelea sehemu ya hija ya mashahidi wa Uganda ya Namugongo.

Jumapili ya Oktoba 20, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliwatangaza wenyeheri vijana wawili wa Uganda — Daudi Okelo na Jildo Irwa – makatekista waliouawa Oktoba 18, mwaka 1918.

Biblia ya Kijapan yakamilika

TOKYO, Japan

 

KITUO cha Mafunzo ya Bilblia cha Wafransiskani cha Tokyo, nchini Japan kimechapisha toleo la ‘Kitabu cha Yeremiah’ katika Biblia kwa lugha ya Kijapan hatua ambayo inakamilisha tafsiri ya Biblia iliyofanyika katika awamu 37.

Kituo hicho cha mafunzo kijulikanacho kama, Furanshisukp-kai-Seisho, kinachoongozwa na Padre Odaka Takeshi, kimekamilisha kazi iliyoanzishwa mwaka 1956 na mkurugenzi aliyepita, Padre Bernardino Schneider, OFM, ambaye katika umri wa miaka 84, bado anajihusisha katika mradi huo.

Wazo la kutoa tafsiri hiyo liliibuka mwaka 1952, wakati Japan ikiwa bado inafanya ukarabati kutokana na madhara ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Mwaka huo Padre Schneider, mzaliwa wa Cincinnati, Ohio, aliwasili katika Tokyo kama mmisionari.

Inasemekana kuwa wakati huo toleo pekee lililokuwepo katika lugha ya Kijapan lilikuwa ni la Biblia ya Kilatini la Vulgate. Lilikuwa ni katika lugha ya Kijapan ya zamani ambayo vijana wa sasa wa Kijapan hawawezi kuiongea.

Tafsiri hiyo iliyoanzishwa na Padre Schneider iko katika Kijapan cha kuongea na imezingatia makala za hivi karibuni zinazokosoa tafsiri iliyotangulia. hata hivyo imehifadhi Biblia ya Vulgate katika lugha ya Kilatini.

Padre Takeshi alitangaza kuwa ndani ya miaka mitano ijayo kituo hicho kinatumaini kuchapisha tafsiri ya Biblia kamili katika kitabu kimoja.

Inasemekana kuwa toleo la mwisho la Biblia katika kitabu kimoja lilichapishwa katika miaka ya 1980 na Chama cha Biblia cha Japan katika mradi ambamo wanafunzi Wakatoliki na Waprotestanti walishiriki.

BAADA YA KUMALIZIKA UTEKAJI NYARA KATIKA URUSI

Viongozi wa dini wataka amani

l Papa na Askofu Mkuu waomba sala

MOSCOW, Urusi

 

VIONGOZI wa Kanisa Katoliki katika Urusi na Roma wametoa wito wa amani baada ya kumalizika mzingiro wa jumba la michezo ya kuigiza lililokuwa limejaa mateka na watekaji nyara, hatua iliyoacha mateka zaidi ya 100 na watekaji wote 50 wakiwa wamekufa .

 Akihutubia makundi ya watu waliokuwa wamekusanyika katika Vatican, Papa Yohane Paulo wa Pili alisema: “Tuombe leo, kwa namna ya pekee, maombezi ya Bikira Maria anayependwa sana na watu wa Urusi, ambao katika siku hizi za mwisho wameteseka sana.”

 “Wakati tunasali na kuomba kwa ajili ya wahanga wa mkasa wa hivi karibuni na wa kuhuzunisha, tuombe kwa Bikira Maria mtakatifu ili matukio kama haya yasirudiwe tena,” aliongeza Papa.

 Msemaji wa Vatican Dk. Joaquín Navarro-Valls, alisema kuwa wakati wa kitendo cha utekaji nyara katika Moscow kilichofanywa na waasi wa Chechnya, Papa Yohane Paulo wa Pili alikuwa akipata habari za mara kwa mara juu ya jambo hilo kutoka kwa Monsinyori Celestino Migliore, katibu mdogo wa Vatican mwenye dhamana ya mahusiano na mataifa.

 Wakati wa mzingiro wa jumba la michezo ya kuigiza jijini Moscow, Monsinyori Migliore alikuwa katika Urusi katika ujumbe wa kidiplomasia.

 Mganga Mkuu katika Moscow, Dk. Andrei Seltsovsky alisema leo kuwa, wote isipokuwa mateka 117 walipoteza maisha wakati wa operesheni ya uokoaji wa mateka siku ya Jumamosi, watu hao walikufa kutokana na matokeo ya gesi iliyotumika kuwadhoofisha watekaji nyara, Shirika la Habari la Associated Press liliripoti, likinukuu Shirika la Habari la Urusi Interfax.

 Aidha Dk. Seltsovky aliliambia Interfax kwamba watu zaidi ya 300 walikuwa bado wamelazwa hospitalini, wakiwemo watu 150 ambao walikuwa katika wodi za wagonjwa mahututi.

 Watekaji nyara 50, ambao walitajwa kama magaidi wakiwemo wanawake 18, pia walikufa wakati wa operesheni ya uokoaji iliyofanywa na makomandoo wa Urusi.

 Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Moscow,  Mhashamu Thaddeus Kondrusiewicz, na rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki wa Urusi, alitoa waraka akielezea “faraja na huzuni, sala na matumaini” ya Wakatoliki wa Urusi baada ya kumalizika kwa mgogoro huo.

 “Leo, katika parokia zote nchini Urusi, sala zinainuliwa kwa Bwana Mungu mwenye huruma sana kwa ajili ya kuzipa roho za marehemu waliokufa mapumziko ya amani, faraja kwa jamaa zao na marafiki, kupona haraka kwa majeruhi, kwa nguvu ya kiroho kwa wale walionusurika katika tendo hilo baya la kihalifu pamoja na kurejeshwa kwa amani na maelewano katika Urusi,” ulisema ujumbe huo uliotolewa na ofisi ya habari ya maaskofu.

 Katika tamko hilo pia Askofu anawaomba raia wa Urusi “kudhibiti hisia zao badala ya kulipiza kisasi kwa ajili ya maumivu ya kuondokewa na kaka pamoja na dada zetu wasio na hatia, na wenye historia na imani tofauti.”

 Askofu Mkuu Kondrusiewicz, alishauri raia wote, hasa mamlaka za kiserikali, “kufanya kila kinachowezekana ili kusitisha kuendelea kuharibika kwa hali ya mvutano katika jamii kwenye nyanja za kisiasa, mazungumzo baina ya dini mbalimbali na katika ngazi za kikabila.”

 “Tunamwomba Mungu mmoja wa pekee na Mwumbaji ili atupe busara na matumaini, tunamwomba ailinde nchi yetu dhidi ya matukio ya kutisha ya aina hiyo, na atuweke katika njia ya kuelekea amani na ustawi,” ulimalizia ujumbe huo wa maaskofu.

Kuweni watakatifu, waaminifu kwa Roma, Papa awaambia  Waseminari, Mapadre

VATICAN CITY

 

WAKATI wa mkutano na mapadre pamoja na waseminari wa Chuo cha Kipapa cha German-Hungaria, Papa Yohane Paulo wa Pili alisisitiza haja ya utakatifu na uaminifu kwa Roma.

Mkutano huo ulisaidia Chuo hicho katika kuadhimisha mwaka wa 450 tangu kuanzishwa kwake.

Chuo hicho ambacho pia kinajulikana kama “Germanicum,” kilianzishwa kutokana na juhudi za Mt. Ignatius wa Loyola, aliyemwomba Papa Julius wa Tatu kufungua kituo huko Roma kwa ajili ya kuwapatia mafunzo mapadre wa kesho waliokuwa wakitoka Dola ya Roma.

Katika mkutano wake na wanafunzi hao, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili aliwatia moyo “kujifunza ‘romanitas njema.’”

“Upendo wa kina na uaminifu kwa Mrithi wa Mt. Petro, pamoja na utii wa ndani na wa nje kwa mafundisho na nidhamu ya Kanisa, vitawawezesha kushiriki katika uamsho muhimu wa uhai wa makanisa ya nchi zenu mlizozaliwa,” alisema Papa.

Hivi sasa wengi wa waseminari na mapadre wa chuo cha Germanicum ni Wajerumani, ingawa baadhi yao walitoka Hungaria na mahali pengine.

Kabla ya kuwaaga wanafunzi hao, Baba Mtakatifu alielezea matumaini yake akisema “muwe mapadre watakatifu.”

“Ifanyeni misa takatifu kuwa kituo cha kiroho kwa siku nzima na kusali sana,” alisema na kuongeza “Chukueni rozari mikononi mwenu ili kutafakari uso wa Kristo pamoja na Bikira Maria.”