Kanisa la Orthodoksi lalaumiwa kwa kukwamisha mazungumzo

VATICAN CITY

KIONGOZI Mkuu wa kitengo cha mazungumzo kati ya Kanisa Katoliki na dini nyingine (ekumene) cha Vatican, Mwadhama Walter Kardinali Kasper alisema Kanisa la Orthodoksi linastahili kulaumiwa kwa kukwamisha mazungumzo kati ya madhehebu hayo.

Aliyasema hayo hivi karibuni kuwa kwa sababu ya upinzani wake kwa shughuli za Kanisa Katoliki kwenye nchi hiyo yenye Wakristo wengi wa madhehebu ya Kiorthodoksi mazungumzo ambayo yaliishafikia hatua nzuri sasa yamesimama.

Alisema madai hayo zaidi ni ya kiitikadi na si ya kiteolojia ambayo mwishowe yanaweza kusababisha "uzushi wa kikanisa" kwa kuufungamanisha utume wa Kanisa na utambulisho wa kiutamaduni na kikabila.

"Kanisa la Orthodoksi la Urusi likiendelea kushikilia misimamo hii ya kiitikadi haliwezi tena kuanzisha mazungumzo na jamii ya sasa pamoja na Kanisa Katoliki yenye kujenga," alisema Kardinali huyo.

Kardinali Kasper alitoa maoni hayo yasiyo makali kutolewa na afisa wa Vatican juu ya mkwamo wa mazungumzo kati ya Kanisa la Orthodoksi la Urusi na Kanisa Katoliki, kwenye makala maalumu.

Makala haya yalichapishwa na gazeti la Ustaarabu wa Kikatoliki (La Civilta Catolica) gazeti lenye ushawishi mkubwa ambalo hutolewa na Shirika la Wajezuiti.

Licha ya upinzani wa Waorthodoksi dhidi ya kuongezeka kwa Wakatoliki kwenye nchi hiyo iliyokuwa ya Kikomunisti, mwezi uliopita Papa Yohane Paulo wa Pili alitangaza majimbo manne nchini Urusi.

Hatua hiyo ilitetewa na Vatican kama ni ya kawaida ya kiutawala, lakini ikashutumiwa na Kanisa la Othodoksi la Urusi kama ushahidi zaidi wa jinsi Kanisa Katoliki linavyoshawishi Waorthodoksi ili wajiunge nalo.

Hata hivyo Kardinali Kasper alisema kwamba wachungaji wa Kanisa Katoliki hawana lengo la kuwaleta waamini wa Kiorthodoksi kwenye Kanisa Katoliki, bali viongozi wa Kiorthodoksi ndiyo wamepanua maana ya ushawishi huo na hata kuhusisha juhudi za Kanisa Katoliki kuwahubiria wale wasioamini.

Alisema hili ni jambo ambalo Kanisa Katoliki haliwezi kamwe kukubaliana nalo kwani linapingana na utambulisho wake wa kimisionari na pia linaonyesha picha mbaya ya shughuli za kichungaji za Kanisa la Orthodoksi lenyewe.

"Kanisa la Orthodoksi linaona udhaifu wake wa kichungaji na kiuinjilishaji na kwa hiyo lina hofu na uwepo wa shughuli za Kanisa Katoliki zenye ufanisi katika medani ya kichungaji, ingawa ni wachache kinamba," alisema.

Alisema vipingamizi vya Kiorthodoksi kimsingi ni vya kiitikadi kwa maana kwamba vinalifungamanisha Kanisa hilo na utamaduni wa Kirusi jambo ambalo si kweli.

"Kanisa la Orthodoksi linatetea si tu mambo ya Kirusi ambayo hayapo tena bali pia uhusiano kati ya kanisa na watu au kanisa na utamaduni ambao tayari una matatizo kiteolojia," alisema.

Kardinali Kasper alitupilia mbali wazo la "eneo maalumu" kutenga Urusi kwa ajili ya Kanisa la Orthodoksi pekee na kusema kuwa kanisa lililoasisiwa na Kristo lilikuwa la kila mtu na mahali na kwamba halikuwa limegawanywa katika maeneo ya utawala.

Hata hiyo, alisema kuwa katika kuunda majimbo nchini Urusi Baba Mtakatifu alikuwa mwangalifu kuheshimu hisia za Waorthodoksi na kanuni ya kale ya "mji mmoja - askofu mmoja" kwa kuyaita majimbo hayo majina ya watakatifu badala ya majina ya miji yalipo.

Kardinali Kasper alirudia tena mwaliko wa Vatican kwa Kanisa la Orthodoksi la Urusi kutoa mifano halisi ya ushawishi wa Kikatoliki miongoni mwa Waorthodoksi jambo ambalo alisema halijawahi kufanyika.

Aidha kardinali huyo alikiri kwamba "baadhi ya Wakatoliki ni wakareketwa zaidi" lakini akasema jambo hilo ni la kawaida kwenye kila kanisa.

Alisisitiza kuwa Kanisa Katoliki lilikuwa halifanyi "Mkakati" "kujaribu kutumia udhaifu wa sasa wa makanisa ya Kiorhotodoksi na kuigeuza Urusi kuwa nchi ya Kikatoliki."

Hata hivyo alisema katika hatua ya mtu mmoja mmoja Mkristo wa kawaida wa Kanisa la Kiorthodoksi anaweza kuamua kujiunga na Kanisa Katoliki jambo ambalo ni mara chache kutokea na likitokea ni lazima liheshimiwe kwa sababu za uhuru wa kidini.

Alisema mwishoni uamuzi wa Kanisa la Orthodoksi la Urusi kusimamisha mazungumzo utaleta matokeo mazuri kinyume na yale yaliyotarajiwa na Waorthodoksi.

"Kwa kukatiza mazungumzo Kanisa la Orthodoksi la Urusi linajiharibu lenyewe pamoja na malengo yake kwa sababu linaimarisha itikadi kali badala ya zile za wastani."

"Lingefanya vema kuanzisha tena mazungumzo na Kanisa Katoliki badala ya kuyakatiza na kujiondoa kwenye mkwamo linamojikuta...ili kuchukua tena nafasi linayoistahili kwenye ulimwengu wa leo, hasa katika Ulaya inayoendelea kuungana," alisema.

Alisema kwamba Kanisa Katoliki lilikuwa tayari kushiriki na kukuza mazungumzo ya namna hii.