Make your own free website on Tripod.com

Kumbe hata Mama Theresa alihisi kuachwa na Mungu!

l Pia aliwahi kufikiri 'labda Mungu hayupo'

VATICAN CITY

PAMOJA na kuishi maisha yaliyowagusa watu wengi duniani na hata kufikia hatua ya kumwita ‘mtakatifu anayeishi’, Mama Thereza wa Calcutta naye pia alikumbana na mashaka, kuachwa, kutopendwa na Mungu na hata kufikiri kwamba Mungu hayupo.

Padre wa Shirika la Wamisionari wa Upendo lenye mapadre na watawa wa kike na kiume lililoanzishwa na Mama Theresa, Brian Kolodiejchuk, ameeleza kushtushwa kwake na magumu ambayo mtawa huyo alikumbana nayo, kadiri anavyozidi kupata barua za Mama Theresa kwa viongozi wake wa kiroho.

Padre huyo ambaye ndiye anayeshughulikia maandalizi ya Mama Theresa kutangazwa mtakatifu, alisema kuwa sasa hashangai kuona jinsi ilivyomchukua muda mrefu mtawa huyo kufungua nyumba ya wenye shida, wagomjwa na wasio na makazi.

Alisema kitu cha kushangaza zaidi ni jinsi alivyofanya mambo makubwa na ya ajabu, pamoja na kwamba kwa miaka mingi alionja na kuhisi kwamba Mungu alikuwa amemwacha.

Alisema barua za Mama Theresa kwa viongozi wake wa kiroho kwa miaka mingi zimejaa marejeo ya "giza la ndani" kujisikia kutopendwa na Mungu na hata kushawishika kuwa na mashaka kama kweli Mungu yupo.

Kwa mujibu wa padre Brian, kuanzia miaka ya 1959-60 mtawa huyo aliwahi kuandika katika shajara ya kiroho kuwa, "Katika roho yangu, nahisi maumivu ya ajabu ya kupoteza, ya Mungu kutonipenda, ya Mungu kutokuwa Mungu, ya Mungu kutokuwepo kabisa."

Alisema kuwa katika barua nyingine aliandika kwamba alitaka kumpenda Mungu, "kwa kiwango ambacho hajawahi kupendwa" lakini bado alihisi upendo wake ulikuwa haujibiwi.

"Katika mazingira ya maisha ya Mama Theresa, mawazo si kitu cha kusikia tu, lakini ni ishara za utakatifu," alisema Padre Brian katika mahojiano na Shirika la Habari la Kikatoliki (CNS) mwishoni mwa Februari.

"Mama Theresa aliamini kwamba Mungu yupo na kwamba alikuwa na mpango maalumu na maisha yake pamoja na kwamba hakuhisi uwepo wake," aliongeza.

"Kila mmoja anapenda kushirikishana, na kuzungumzia mambo, kutiwa moyo na wengine," alisema na kuongeza "lakini Mama Theresa pamoja na kuumia kwa ndani, aliendelea kutabasamu, aliendelea kuwa mwenye furaha."

Aidha alisema kuwa katika barua ya mwaka 1961 kwa Wamisionari wa Upendo aliandika, "Bila kuteseka kazi yetu ingekuwa sawa na kazi nyingine yoyote ya kijamii. Mateso yote ya watu maskini lazima yakombolewe na ni lazima sisi tuyashiriki."

Padre Brian, 45, Mkanada alipadrishwa akiwa ni miongoni mwa mapadre wa kwanza wa Shirika la Wamisionari wa Upendo.

Inasemakana kuwa baadhi ya wanachama wa Shirika la Mama Theresa walikuwa wakimsikia akiita Septemba 10, 1946 kama "Siku ya Uvuvio," ambapo katika siku hiyo akiwa ndani ya garimoshi huko India aling’amua wito wa kuishi na kufanya kazi na maskini.

Mama Theresa aliuelezea wito huo kama "amri, wajibu, na jambo la hakika kabisa" kwamba ilikuwa lazima kwake kuacha Shirika la Masista wa Loreto na kwenda katika mabanda ya Calcutta kujitoa kikamilifu kuwasaidia maskini.

"Tulifikri kwamba kwa njia fulani, ambayo hakuieleza, aling’amua wito wa Yesu," alisema Padre Brian.

Aliongeza "Lakini sasa kutokana na kusoma barua zake kwa viongozi wake wa kiroho, ni wazi alionja kile ambacho wanateolojia hukiita kama ‘maelezo ya ndani ya kufikirika’ kwa hakika alisikia sauti kichwani mwake ikimwambia nini cha kufanya na iliendelea kwa miezi kadhaa."

Aliendelea kusema kuwa "Wito ulikuwa wa moja kwa moja kiasi kwamba alijua lilikuwa jambo sahihi licha ya kukumbana na giza hili kubwa kwa miaka mingi, labda mpaka miaka ya 1970."

Alisema wakati fulani Askofu Mkuu Mstaafu wa Calcutta alitaka kumshirikisha barua za Mama Theresa mwanzilishi mmoja ambaye alikuwa akipigana kuanzisha shirika la kitawa.

Hata hivyo alisema "Mama Theresa alimsihi asifanye hivyo na kumwomba kuwa barua zake ziharibiwe."

Alisema kwamba Mama Theresa alimwambia Askofu Mkuu kuwa "Watu wakijua juu ya mwanzo wa huduma zangu watanifikiria zaidi mimi, na kumfikiria kidogo Yesu."

Alipoulizwa iwapo hashtuki kuona kama anasaliti matakwa ya Mama Theresa kwa kutangaza habari hizo hadharani, Padre Brian alijibu, "Nadhani mtazamo wake ni tofauti sasa."

Baadhi ya barua na kumbukumbu zake za matukio ya kila siku zilichapishwa mwaka jana katika "Jarida la Tafakuri za Kiteolojia" linalotolewa na Shule ya Teolojia ya Vidyajoti katika New Delhi, India inayoendeshwa na Shirika la Wayezuiti.

"Uchunguzi juu ya imani yake katika maisha si kujishughulisha tu ili mradi," alisema Padre Brian na kuongeza "Kutangazwa mwenyeheri na mtakatifu ni kutambua si tu kazi(huduma) ya mtu katika maisha jambo ambalo ni wazi kwa Mama Theresa, bali ni kutambua utakatifu."

Aidha Padre Brian alisema kuwa baadhi ya watu wanaweza kuwa wameshangazwa au hata kushtushwa na mapambano ya kiroho ya Mama Theresa.

Hata hivyo, alielezea matumaini yake kuwa hiyo itawasaidia wengi kufikia "utambuzi wa ndani na mkamilifu wa utakatifu, ambao Mama Theresa aliuishi kwa njia ya kawaida na ya ajabu: alikichukua kwa tabasamu kile Yesu alichompatia na kubaki mwaminifu hata katika mambo madogo sana."

Alisema kuwa hisia za kwamba Mungu yuko mbali sana au hata kwamba hayupo ni mang’amuzi ya kawaida ya kiroho.

"Labda hatutakuwa na kiwango sawa cha manga’amuzi ya namna hiyo, lakini mengi ya yale aliyofanya yalikuwa ya kawaida, lakini yalifikia kutokuwa ya kawaida wakati yote yalipowekwa pamoja," alisema.

Mama Theresa mwanzilishi wa Shirika la Wamisionari wa Upendo lenye mapadre, na watawa wa kike na kiume na aliyejulikana na wengi enzi za uhai wake kama mtakatifu anayeishi, alifarikia Septemba, 1997.

Mwaka 1999 Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alitengua utaratibu wa kusubiri miaka mitano kabla ya kuanza harakati za kutangaza mwenyeheri na kuagiza uchunguzi uanze kuhusu maisha na kazi za Mama Theresa.

Pamoja na kwamba Padre Brian anafanya kazi hiyo ya maandalizi tangu saa 2. 00 asubuhi mpaka saa 1:00 usiku, alisema kwamba anaamini itachukua "miezi kadha" kabla ya Vatican kutambua kwamba Mama Theresa kwa ushujaa aliishi fadhila za Kikristo na kumtangaza kuwa mtumishi wa Mungu.

Alisema kazi pia inaendelea kuandaa ripoti kuhusu muujiza mkubwa ambao unahitajika kwa kutangazwa mwenyeheri, ambao ulitokea mwaka 1998 ambapo mwanamke wa kihindi alipona uvimbe wa ajabu uliokuwa tumboni mwake.

"Watu wananiambia fanya haraka," alisema

na kuongeza "Lakini mlolongo rasmi huchukua muda. Mlolongo huo umetengenezwa ili kujua akili ya watu wa Mungu na uhakikisho wa muujiza ni uthibitisho wa Mungu juu ya hilo."