Papa apuuza upinzani wa Orthodoksi Urusi

l Atangaza majimbo manne

VATICAN CITY

LICHA ya upinzani toka Kanisa la Orthodoksi nchini Urusi, Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, ameyapandisha hadhi maeneo manne ya utawala ya Kanisa Katoliki nchini Urusi kuwa majimbo.

Uamuzi huo wa Baba Mtakatifu umeelezwa kuwa ni hatua kubwa kupigwa na Kanisa Katoliki katika kujijenga upya baada ya ukomunisti kusambaratika nchini Urusi zaidi ya miaka kumi iliyopita.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kikatoliki, (CNS), Vatican iliutetea uamuzi huo kama "hatua ya kawaida ya utawala" na kujibu shutuma za Kanisa la Orthodoksi kupitia taarifa isiyo na maneno makali.

Katika taarifa hiyo Vatican ilisema kwamba Kanisa Katoliki lina haki ya kuwahudumia waamini wake wote popote walipo, hata kwenye nchi zenye waamini wengi wa Kiorthodoksi.

"Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili hutaka kuitikia kikamilifu matakwa ya kichungaji ya wale ambao kwa uhuru wao wamelichagua Kanisa Katoliki na kutambua ndani yake ‘nyumba’ na ‘familia’ zao," ilisema taarifa hiyo.

Aidha Vatican iliyatupilia mbali mashtaka ya Waorthoksi walioiita hatua hiyo kama "uvamizi" wa sasa wa Kikatoliki katika Urusi kwa kusema kwamba muundo wa uongozi wa Kanisa Katoliki (hairakia) uliishajiimarisha nchini humo karne nyingi zilizopita.

"Hii hasa si kuingiza muundo mpya wa Kanisa katika maeneo hayo, bali ni kurejesha ule uliokuwepo kabla," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Hatua hiyo sasa itayafanya maeneo manne yaliyokuwa yakitawaliwa kwa mfumo wa usimamizi wa kitume kuwa majimbo matatu na jimbo kuu moja.

Jimbo Kuu la Moscow chini ya ulinzi wa Mama wa Mungu ambalo majimbo mengine yatalitegemea, linatokana na eneo la awali la usimamizi wa kitume lililokuwa likijulikana kama Urusi ya Ulaya Mashariki.

Jimbo kuu hilo litaongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu Tadeusz Kondrusiewicz, ambaye alikuwa msimamizi wake wa kitume tangu mwaka 1991.

Jimbo la Clement katika Saratov linatokana na eneo la awali la usimamizi wa kitume lililokuwa likijulikana kama Urusi ya Ulaya Kusini, litakaloongozwa na Mhashamu Askofu Clemens Pickel.

Huko Siberia Magharibi, jimbo la Kugeuka Sura, katika Novosibirsk, litaongozwa na Mhashamu Askofu Joseph Werth.

Nayo Siberia ya Mashariki imeunda jimbo la Mt. Joseph katika Irkutsk litakaloongozwa na Mhashamu Askofu Jerzy Mazur.

Mapema mwezi uliopita Mwakilishi wa Vatican nchini Askofu Mkuu Giorgio Zur, alielezea mpango wa kichungaji wa kiliunda upya Kanisa nchini humo wakati alipokutana na viongozi wa Kiorthodoksi.

Hata hivyo baadaye Kanisa la Orthodoksi katika taarifa yake lilisema "matendo yaliyopangwa na Vatican yalikuwa yanakiuka kanuni za sheria za Kanisa na miiko ya uhusiano kati ya Makanisa."

"Matendo ya namna hii yatafanya vikwazo vikubwa kwa maendeleo ya mazungumzo kati ya Kanisa Katoliki na la Orthodoksi," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Katika kujibu vipingamizi vya Waorthodoksi, Msemaji wa Vatican Askofu Joaquin Navaro-Valls alisisitiza hoja kadhaa ambazo ni:-

-Ni "kawaida" maeneo ya utawala wa kitume, ambayo kwa muda huwa na utawala na mwishowe kuwa jimbo.

-Wakatoliki katika Urusi wamerudia mara kadhaa kuomba maeneo hayo kupandishwa hadhi na kuwa majimbo.

-Vatican ilikuwa inawapa Wakatoliki katika Urusi kile tu ambacho waamini wa Kiorthodoksi hupata kama huduma ya kichungaji katika majimbo yao kwenye mataifa ya Magharibi.

Msemaji huyo wa Vatican alitoa mifano ya kuwepo kwa majimbo ya Kanisa la Orthodoksi huko Vienna, Austria, Brussels, Ubelgiji na Berlin.

-Serikali ya Urusi haikuwa na hatua hiyo kwa kuwa wanatambua makubaliano ya kimataifa juu ya uhuru wa kidini.

-Vatican inatumaini kwamba hatua hiyo itasaidia kufanikisha mazungumzo ya Kanisa la Orthodoksi nchini Urusi.

Msemaji huyo alisema kuwa Kanisa Katoliki kupitia Wakala wake wa Misaada kwa Makanisa yenye Shida, limetoa zaidi ya dola za Marekani milioni 17 kwa Kanisa la Orthodoksi nchini Urusi kwa miaka kumi iliyopita.

Taarifa nyingine ambatano isiyosainiwa iliyotolewa na Vatican, iliyatupilia mbali mashtaka ya Waorthodoksi kuwa hatua hiyo inalenga kushawishi waamini wake wajiunge na Kanisa Katoliki.

"Ongezeko la Wakatoliki nchini Urusi kwa kweli halitokani na Waorthodoksi kuacha kanisa lao na kujiunga na Kanisa Katoliki. Badala yake linatokana na mazingira ambayo kijadi yaliwafanya kuwa mbali na dini yoyote," ilisema taarifa hiyo.

"Watu hawa baada ya kukutana na Kanisa Katoliki waliomba kubatizwa na kujiunga nalo. Hilo pekee linatosha kukanusha mashtaka eti ya kushawishi Waorthodoksi ili wajiunge na Kanisa Katoliki, mastaka ambayo mara nyingi yanaundwa kwa njia zisizo wazi, ambayo kwa hakika yanasababishwa na kutojua ukweli wenyewe," ilisema taarifa ya Vatican.

Ilisema namba ndogo ya jumuiya za kikatoliki katika Urusi hazina kusudi na hazina mwelekeo wa "kuvuruga utambulisho wa kiutamaduni wa nchi ambayo kimapokeo inatambuliwa kama nchi ya Kiorthodoksi."

Aidha taarifa ya Vatican ilitoa pitio la kihistoria kuhusu uwepo wa Kanisa Katoliki katika Urusi ili kuweka wazi urejeaji mpya wa muundo wa uongozi wa Kanisa (hairakia) ambao hauwezi kuchukuliwa kama njia ya uvamizi au mwingiliano.

Ilielezea takwimu za zaidi ya Wakatoliki 112, 000 mwaka 1858 katika jimbo kuu la Mohilev, na parokia zaidi ya 30 nchini kote na hadi miaka ya 1920 Wakatoliki walifikia 1.6 milioni katika majimbo manne na parokia 580.

"Ongezeko kubwa la Wakatoliki katika Urusi au katika majimbo ya Kisovieti kwenye karne ya 20, lilitokana na uhamiaji wa lazima kwa watu kutoka Polandi, Ujerumani na wengine kutoka nchini humo," ilielezea Vatican.

Mwaka 1991 baada ya Sovieti kusambaratika Vatican ilianzisha maeneo mawili ya usimamizi wa kitume kushughulikia upangaji mpya wa kichungaji, moja katika Urusi ya Ulaya na moja katika Siberia.

Mwaka 1999 kila moja ya maeneo haya ya utawala iligawanywa katika maeneo mawili ya usimamizi wa kitume.

Vatican inakadiria Wakatoliki nchini Urusi kuwa 1.4 milioni, takribani Wakatoliki milioni moja wapo Siberia ya Magharibi ambapo katika maeneo ya Urusi karibu na Ulaya wanakadiriwa kuwepo Wakatoliki 300, 000. Hiyo ni kwa mujibu wa takwimu za kanisa.

Vatican yatoa ratiba ya Ijumaa Kuu, Pasaka

VATICAN CITY

MAKAO Makuu ya Kanisa Katoliki duniani huko Vatican yametoa ratiba atakayofuata Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kuhudhuria maadhimisho makubwa ya kiliturujia kuanzia siku ya Ijumaa Kuu hadi Pasaka yenyewe.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Baraza la Kipapa linaloshughulikia Mawasiliano ya Jamii, ratiba hiyo inaonyesha kuwa, Baba Mtakatifu anatarajia kuongoza Njia ya msalaba siku ya Ijumaa Kuu itakayofanyika Coliseum, jijini Roma kuanzia saa 2 hadi saa 3:40 usiku

Ratiba hiyo inaonyesha kuwa siku ya Jumapili ya Pasaka yenyewe Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili ataongoza misa takatifu ya Pasaka itakayofanyika viwanja vya Mt. Petro jijini Roma kuanzia saa 2. 25 hadi 3. 55 asubuhi.

Mara baada ya misa takatifu hiyo kuanzia saa 3. 55 hadi 4. 55, Baba Mtakatifu atatoa ujumbe na baraka ya Pasaka "Urbi et Orbi" (Kwa Mji na kwa Ulimwengu) shughuli itakayofanyika pia katika viwanja vya Mt. Petro.

Taarifa hiyo ilisema kuwa matangazo ya ibada hizo kwa njia ya televisheni kwa ajili ya ulimwengu mzima yatatolewa na Televisheni ya Italia (RAI) kwa kushirikiana na Kituo cha Televisheni cha Vatican yakiratibiwa na Baraza la Kipapa linaloshughulikia Mawasiliano ya Jamii.

Aidha matangazo hayo kwa eneo la Ulaya yatapatikana kupitia Umoja wa Utangazaji wa Ulaya (Eurovision) na katika eneo la Amerika ya Kusini kupitia asasi ya televisheni katika eneo hilo (OTI) ambapo watangazaji wengine katika maeneo hayo wametakiwa kuwasiliana na asasi husika.

Taarifa hiyo ilieleza pia kuwa matangazo mengine yatapatikana kupitia mtandao wa kawaida wa setilaiti ambapo wale watakaotaka kupokea matangazo ya picha na sauti kwa kutumia teknolojia ya Intelsat na matangazo ya televisheni wametakiwa kuwasiliana na wataoji wa huduma za simu.

Pia taarifa hiyo ilieleza kuwa huduma ya kuunganishwa katika setilaiti inatolewa bure kwa nchi zote nje ya eneo la Ulaya.

Kwa upande wa nchi zinazoendelea za ulimwengu wa tatu zenye matatizo maalumu, kwa kupitia mapendekezo ya Mwakilishi wa Papa katika nchi hizo Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii litalipia gharama za kuunganishwa lakini si zile za matangazo ya ndani.

Taarifa hiyo imeongeza kueleza kuwa matangazo yote hayo yatakuwa yakiambatana na maelezo maalumu yatakayotolewa kwa lugha za Kiingereza, Kifaransa, Kireno, Kihispania na Kiukraina.

Kwa upande wa maelezo kwa lugha ya Kiitaliano televisheni ya Italia itatoa huduma hiyo. Hata hivyo, huduma hiyo itafuatia na maombi maalumu.