Mkuu wa Anglikana duniani kustaafu

l Vatikani yampongeza

LONDON, Uingereza

KIONGOZI wa Kanisa la Kianglikana duniani, Askofu Mkuu, Dk George Carey, wa Canterbury anatarajia kustaafu wadhifa huo mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makao Makuu ya Kanisa la Anglikana huko Canterbury, Uingereza hivi karibuni, Askofu Mkuu Carey (66), anastaafu miaka mitatu kabla ya muda wake kumalizika baada ya kushika wadhifa huo kwa miaka 11.

Hata hivyo, taarifa hiyo haikueleza kwa sababu gani askofu huyo anastaafu mapema kabla ya muda wake kumalizika.

Katika kipindi cha utawala wake kilichoelezwa kuwa kigumu kwa Kanisa hilo, limeshuhudia upadrisho wa wanawake kwa mara ya kwanza jambo ambalo lilisababisha mgawanyiko ndani ya kanisa hilo.

Mgawanyiko huo ulisababisha mbunge maarufu wa Chama cha Kihafidhina (Conservative) kuacha Kanisa hilo na kujiunga na Kanisa Katoliki.

Taarifa hiyo ilisema mgawanyiko huo ulidhibitiwa vizuri chini ya uongozi wa Askofu Mkuu Carey.

Hata hivyo, uongozi wa Askofu Carey ulishindwa kabisa kutatua tatizo la mahudhurio hafifu ya waamini kanisani.

Baada ya miaka 10 ya kuwa na mapadre wanawake bado baadhi ya waamini wanapinga mapadre hao, ambapo hadi sasa hakuna mwanamke askofu.

Miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa kurithi nafasi ya Carey ni pamoja na Askofu Mkuu wa Wales, Rowman Williams, Askofu wa London, Richard Charteris na Askofu wa Rochester, Dk. Michael Nazir-Ali, mwenye asili ya Pakistan ambaye anadaiwa kuwa na nafasi nzuri ya kuweza kuchaguliwa kuliongoza kanisa hilo duniani.

Wakati huo huo: Makao makuu ya Kanisa Katoliki duniani huko Vatikani yamemtumia salamu za pongezi Askofu Mkuu Carey, kwa juhudi zake za kuboresha uhusiano kati ya Kanisa la Anglikana na Kanisa Katoliki kwa kipindi alichokuwa madarakani.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Kipapa la Kukuza Umoja wa Kikristo ilisema "Tunajua ana ratiba ngumu kabla ya kustaafu, lakini tungependa kwa wakati huu kutoa shukrani zetu kubwa kwa baraka za miaka mingi ya uongozi wake kama askofu mkuu wa Canterbury," ilisema taarifa hiyo.

Askofu Mkuu George Carey, aliyeingia madarakani mwaka 1991, ni askofu wa 103 wa Canterbury kuongoza Waanglikana milioni 70, duniani.

Maaskofu wakutana na Vijana kujadili miito

INDIANAPOLIS, Marekani

ZAIDI ya Vijana Wakatoliki 250 na Maaskofu 47 nchini Marekani walifanya mazungumzo na kuombea miito wakati wa Mkutano wa Kitaifa wa Baraza la Vijana Wakatoliki.

Taarifa zilizokusanywa wakati wa mkutano zitapitiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani. Baadhi ya ofisi za kitaifa na kamati za majimbo zinazoshughulikia miito nchini kote zitasaidia kupanga na kutekeleza zoezi la kuamsha miito.

Mkutano huo ulikuwa ni mkubwa na wa aina yake katika historia ya Baraza la Vijana Wakatoliki nchini Marekani ambalo hukutana mara mbili kwa mwaka.

"Mkutano huu unakusaidia kuamua juu ya wito wako katika maisha," alisema mjumbe Marinello Saguin toka Parokia ya Mt. Fransisko wa Assizi huko Los Angeles na Mwanafunzi katika Shule ya Mt. Fransisko huko La Canada Flintridge, California.

"Mimi nafikiria upadre," alisema na kuongeza "kwa hiyo hii inanisaidia kufahamiana na watu wengine na kubadilishana nao uzoefu na kukua kiimani," aliliambia gazeti la The Criterion la Jimbo Kuu la Indianapolis.

Saguin ambaye mara nyingine huitwa "Nello" alisema amekuwa akijisikia wito wa upadre tangu alipokuwa darasa la nane.

"Watu waliniuliza iwapo niliwahi kufikiria kuwa padre kwa sababu nilikuwa natumikia misa Parokiani kwangu na watu walikuwa wakiniona nilivyo mcha Mungu wakati wa misa," alisema.

"Sala ni sehemu muhimu ya mfumo wa maamuzi yangu na pia kujiuliza maswali ya kunipa changamoto na kupata msaada toka kwa watu wengine. Mkutano huu ulijaa roho na uhai. Ulikuwa wa ajabu. Nilijifunza kutokana na simulizi za maaskofu juu ya maisha," alisema Saguin.

Askofu William L. Higi wa Lafayette, Indiana aliliambia gazeti la The Criterion "Niliguswa sana na undani wa maisha ya kiroho unaoelezwa na vijana hawa."

Baada ya kuhudhuria mkutano Askofu alisema "Nilifurahi kwa kushangaa na pia nilitiwa moyo sana" kuhusu hali ya baadaye ya miito ya kipadre na kitawa.

Kipindi kimojawapo cha mkutano kilizungumzia maisha ya Padre Mfransiskani Mychal Judge wa New York, aliyekufa wakati akitoa sakramenti ya mpako wa wagonjwa kwa mfanyakazi wa zimamoto ambaye aliumia vibaya wakati Kituo cha Biashara cha Kimataifa kilipoanguka baada ya kushambuliwa na magaidi hapo Septemba 11, mwaka jana.

"Ilikuwa ni mada inayogusa juu ya maisha ya mtu huyu aliyeitwa na Mungu kuwa Padre na aliyetoa maisha yake kuhudumia," alisema Askofu Higi.

"Kipindi hicho kilizungumzia mada ‘Nawezaje kutoa maisha yangu katika huduma, iwe mimi ni Padre, Mtawa au mtu wa ndoa?’" alisema Askofu Higi.

Mada juu ya Sikukuu ya Bikira Maria Kukingiwa Dhambi ya Asili iliangalia utashi wake na kusema ndiyo kwa Mungu. Mada nyingine zilihusu maisha ya Mwanaharakati wa kijamii, Dorothy Day, na utume wake alipokuwa na Shirika la Wafanyakazi la Kikatoliki huko New York.

Pia waliangalia maisha ya Edith Stein Sista mtawa wa shirika la Wakarmeli aliyeongoka toka dini ya Kiyahudi na ambaye alitangazwa mtakatifu mwaka 1998 na Papa Yohane Paulo wa Pili kwa jina la Theresa Benedicta wa Msalaba.

Mjumbe mwingine Megan Marriner, wa Parokia ya Mt. Benard na mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Jenks High School, Oklahoma, alisema kuwa aliamua kushiriki kwa sababu alijisikia Mungu alikuwa akimwita kujihusisha zaidi katika imani yake.

"Kwa kweli nilijisikia kama Mungu alikuwa akiniita kufanya jambo fulani, lakini sikujua ni nini," alisema Megan.

"Nilijaribu kusali rozari kila siku mwaka jana. Sidhani kama nataka kuwa mtawa, lakini kidogo nina hakika kwamba ninataka kuwa mhudumu mlei katika Kanisa," alisema.

Askofu Msaidizi Kenneth D. Steiner wa Portland, Oregon, alisema "Kweli, ilifurahisha kuona kiwango cha imani ya vijana na hamasa yao. Hawa kweli ni vijana wazuri na viongozi wema."

Aliongeza "Vijana wenye uvuvio. Inatia nguvu kwa maaskofu kufanya mazungumzo na vijana na kuadhimisha Ekaristi takatifu pamoja."

"Mkutano huu na baraza la vijana ni fursa kwa vijana kuwaonyesha maaskofu hamasa walio nayo vijana kwa ajili ya Kanisa," alisema Askofu Dennis M. Schnurr wa Duluth, Minnesota.

Matukio haya yanatukumbusha kwa mara nyingine tena kwamba vijana wako tayari kutoa vipaji na uwezo wao kwa ajili ya Kanisa hapa nchini" alisema.

Aliongeza, "Lazima tutafute njia zaidi kuwahusisha katika maisha ya kiparokia."

"Vijana kwenye mkutano kama huu kwa kweli wamehamasishwa kwa kuwa wapo vijana 24,000 hapa. Kukutana pamoja katika mkutano kama huu wa kitaifa wanapata nafasi ya kuimarishana kiimani, kupenda imani yao na nia yao ya kuleta mabadiliko ulimwenguni na katika Kanisa leo," alisema Askofu Schnurr.

Padre Pio kutangazwa Mtakatifu

VATICAN CITY

SHIRIKA la Kipapa linaloshughulikia mambo ya Utakatifu limepitisha uamuzi kumtangaza mtenda miujiza mashuhuri duniani mtawa wa Kiitaliano, Padre Pio, kuwa mtakatifu na tayari limetoa mapendekezo kwa Baba Mtakatifu.

Habari kutoka Vatikani zinasema kuwa Padre Pio aliyefariki mwaka 1968 akiwa na umri wa miaka 81; pia alikuwa na madonda matano kama ya Yesu Kristo.(Stigmata)

Pia Padre huyo alikuwa na uwezo wa kutenda miujiza mingi na hata kuonekana sehemu mbili kwa wakati mmoja.

Shirika hilo hupitisha uamuzi juu ya watu wanaopendekezwa kuwa watakatifu, baada ya miaka mingi ya uchunguzi juu ya maisha yao.

Baada ya hapo hutoa mapendekezo kwa Baba Mtakatifu ambaye hutoa uamuzi wa mwisho.

Endapo Baba Mtakatifu ataidhinisha mapendekezo ya shirika juu ya Padre Pio, jambo ambalo anatarajiwa kufanya, sherehe za utakatifu zitafanyika baadaye mwaka huu.

Padre Pio ni mtawa Mfransiskani Mkapuchini.