Wakatoliki, Waprotestanti, Waorthodox watakiwa kuwa mfano

BABA Mtakatifu Yohane Paul wa Pili, amewataka vijana wapatao 70,000 wa madhehebu ya Kikatoliki Waprotestanti na Waorthodox, kuwa mstari wa mbele katika kuomba na kudumisha amani duniani.

Baba Mtakatifu alitoa wito huo katika ujumbe wake alioutuma kwa vijana hao walipokusanyika huko Budepest kwa ajili ya kuomba amani na kujenga umoja utakaowasaidia kumtambua vema Yesu Kristo.

Aliwataka kuzidisha maombi yao ili amani ya kweli ipatikane na kudumu duniani hasa katika kipindi hiki ambacho dunia ipo katika machafuko ya vita.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la ZENIT vijana hao walikutana Desemba 28, Mwaka Jana wakiwa pamoja na Padre Rodger na Askofu Mkuu wa Jimbo la Budepest.

Habari zinasema vijana hao walirejea makwao Januari Mosi, mwaka huu baada ya kukaa pamoja kwa siku tano wakiomba amani na kujenga umoja.

Padre Rodger aliwahimiza vijana hao kuzingatia imani na maombi kwani ndiyo pekee yanayoweza kubadili moyo wa mtu.

Alisema ni muhimu kufanya hivuo kwa kuwa mtu anapoomba kwa bidii na upendo, ataingia katika amani na mambo atakayofanya yatasimamiwa na Mungu.

Baba Mtakatifu ataka Mwaka 2002 uwe wa haki

ROMA, Italia

BABA Mtakatifu Yohane Paul wa Pili, ametoa wito kwa jamii kuutumia Mwaka wa 2002 katika kupigania haki na kupambana na uovu.

Aliyasema hayo katika misa iliyoafanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Roma mwanzoni mwa mwaka.

Baba Mtakatifu alihimiza kuombea amani duniani ili haki ipatikane kwa kuwa bila haki hakuna amani.

Aliwaambia mahujaji zaidi ya 1000 waliohudhuria misa hiyo kwa kuwa sasa dunia inashuhudia vitendo vinavyotishia haki na kuongeza utengano wa kijamii na kimataifa.

Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwanajamii kukomesha vitendo vyote vinavyopotosha haki duniani na kuongeza utengano.