Ujumbe wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili katika kuadhimisha Siku ya Amani Ulimwenguni

1 JANUARI 2002

1. Siku ya Amani Duniani mwaka huu inaadhimishwa huku wingu zito la matukio ya Septemba 11 iliyopita likiwa bado limetanda. Katika siku hiyo tukio la kutisha lilitendeka ambapo kwa saa chache maelfu ya watu wasio na hatia toka tamaduni na mataifa mbalimbali waliuawa. Tangu hapo watu ulimwenguni kote wamehisi hatari na hofu mpya juu ya maisha yajayo.

Ili kukabiliana na hali hii Kanisa linatoa ushuhuda kwa matumaini yake yaliyojikita kwenye imani kwamba uovu ,fumbo la udhalimu hauna kauli ya mwisho katika medani ya kibinadamu. Historia ya wokovu iliyosimuliwa katika Maandiko Matakatifu inaangaza historia nzima ya wokovu wa ulimwengu na kuonyesha kuwa matukio ya kibinadamu mara zote yanaongozwa na maongozi yenye huruma Mungu ambaye anajua jinsi ya kugusa hata wale wenye mioyo migumu na kuleta matunda hata kutoka pale panapoonekana kama udongo usio na rutuba.

Hayo ndiyo matumaini yanayolishikilia Kanisa mwanzoni mwa mwaka 2002, yaani kwa neema ya Mungu ulimwengu ambamo nguvu ya uovu inaonekana kwa mara nyingine kushinda utabatilishwa kuwa ulimwengu ambamo tamaa njema ya moyo wa kibinadamu itaushinda na ulimwengu wenye amani ya kweli utatawala.

Amani: Kazi ya haki na upendo

2. Matukio ya hivi karibuni, yakiwemo mauaji ya kutisha yaliyotajwa yananisukuma kurudi kwenye maudhui ambayo mara nyingi husumbua kilindi cha moyo wangu wakati ninapokumbuka matukio ya historia ambayo yamesheheneza maisha yangu hasa maisha yangu ya ujana.

Mateso makubwa ya makundi na mtu mmoja mmoja hata miongoni mwa marafiki zangu na wale tuliozoeana yaliyosababishwa na udiktekta wa Kinazi na Kikomunisti hayakuwa mbali na mawazo na sala zangu.

Mara nyingi nimesita na kutafakari juu ya swali hili tunarejeshaje utaratibu wa kimaadili na kijamii ulioharibiwa na matukio haya ya vurugu? Imani yangu iliyotafakariwa na inayothibitishwa tena na ufunuo wa kibiblia ni kwamba utaratibu ulioharibiwa hauwezi kurejeshwa isipokuwa kwa jibu linalojumuisha haki na msamaha. Nguzo za amani ya kweli ni haki mfumo ule wa upendo ambao ni msamaha.

3. Lakini katika hali ya sasa tunawezaje kuzungumzia haki na msamaha kama chanzo na sharti la amani? Tunaweza na ni lazima, haijalishi ni vigumu namna gani ugumu ambao mara nyingi hutokana na fikra kwamba haki na msamaha haviwezi kupatanishwa lakini msamaha ni kinyume cha hasira na kisasi na si kinyume cha haki. Kwa kweli amani ya kweli ni ‘kazi ya haki’ (Is 32:17).

Kama Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano ulivyosema amani ni ‘tunda la mpangilio sahihi wa mambo ambao Muumba ameuweka katika jamii ya binadamu ambao lazima ukamilishwe na kiu ya mwanadamu ya kuwa na utawala mkamilifu wa haki’ (Hati ya Kanisa na Ulimwengu/ Furaha na Matumaini, na 78). Kwa miaka zaidi ya 1500 Kanisa Katoliki limekuwa likirudia mafundisho ya Mt. Augustino wa Hippo juu ya hoja hii.

Anatukumbusha kuwa amani ambayo inaweza na ni lazima ijengwe katika ulimwengu huu ni amani ya mpangilio sahihi - "tranquillitas ordinis," mpangilio tulivu (Rej. Jiji la Mungu, 19, 13)

Kwa hiyo amani ya kweli ni tunda la haki, yaani, ile fadhila ya kimaadili na dhamana ya kisheria ambayo huhakikisha heshima kamili juu ya haki na wajibu, na mgawanyo wa haki wa faida na matatizo.

Lakini kwa sababu haki ya kibinadamu ni nyeti na isiyo kamilifu kutokana na mapungufu na ubinafsi wa watu na makundi ya watu, ni lazima ikamilishwe na msamaha ambao huponya na kujenga upya uhusiano wa kibinadamu uliyovurugwa kutoka kwenye misingi yake. Hii ni kweli katika hali kubwa na ndogo katika kiwango cha mtu mmoja au kwa upana na hata kwa mizania ya kimataifa. Msamaha haupingani kwa namna yoyote ile na haki, kana kwamba kusamehe kulikuwa na maana ya kusahau mabaya yaliyofanywa.

Msamaha ni ukamilifu wa haki ambao unaelekeza kwenye ule utulivu wa mpangilio ambao ni zaidi ya sana kuliko unyeti na usitishaji wa uhasama wa muda unaohusisha uponyaji wa ndani wa majeraha ambayo huumiza moyo wa binadamu. Haki na msamaha yote ni muhimu kwa uponyaji huo.

Ni pande mbili hizi za amani ambazo ningependa kuzizungumzia katika ujumbe huu. Siku ya Amani Ulimwenguni mwaka huu inatoa kwa binadamu wote na hasa wa viongozi wa mataifa fursa ya kufikiria juu ya matakwa ya haki na wito wa msamaha mbele ya matatizo ambayo yanaendelea kuukabili ulimwengu, bila kusahau kiwango kipya cha vurugu zilizoanzishwa na ugaidi wenye mpango.

Hali halisi kuhusu ugaidi

4.Ni hiyo amani iliyozaliwa na haki na msamaha ambayo leo inavamiwa na ugaidi wa kimataifa. Katika miaka ya karibuni, hasa baada ya kumalizika Vita Baridi, ugaidi umeendelea na kuwa mtandao tete wa kisiasa, kiuchumi na kiufundi ambao unavuka mipaka ya kitaifa na kufikia ulimwengu mzima. Makundi ya kigaidi yaliyojipanga vizuri yana rasilimali nyingi za kifedha na kwa hiyo hupanga mikakati mipana na tofauti, ili kuwaumiza watu wasio na hatia ambao hawahusiani na malengo yanayotafutwa na magaidi.

Wakati makundi ya kigaidi yanapotumia wafuasi wake kama silaha dhidi ya watu wasio na ulinzi na wasiotarajia mashambulizi wanaonyesha wazi matashi ya kifo ambayo huijaza mioyo yao. Ugaidi unatokana na chuki na unazalisha utengano, kutoaminiana na ufungaji. Vurugu zinaongezwa juu ya vurugu katika mlolongoo wa misiba ambao husababisha chuki vizazi baada ya vizazi kila mmoja kikirithi chuki ambayo ilivigawa vizazi vilivyotangulia.

Ugaidi umejengwa kwenye dharau dhidi ya maisha ya binadamu. Kwa sababu hii si tu kwamba ugaidi hutenda makosa yasiyovumiliwa lakini kwa sababu ugaidi hukimbilia vitisho na ukatili kama njia ya kisiasa na kijeshi ndiyo maana ugaidi wenyewe ni kweli kosa dhidi ya ubinadamu.

5. Kwa hiyo kuna haki ya kijilinda dhidi ya ugaidi, haki ambayo imekuwa siku zote na lazima itumiwe kwa kuheshimu mipaka ya kimaadili na kisheria katika kuchagua malengo na njia za kuyafikia. Mwenye hatia lazima atambuliwe kwa usahihi kwa kuwa uwajibikaji wa makosa yaliyofanywa na mtu daima ni wa mtu binafsi na hauwezi kupanuliwa na kufikia nchi nzima, makundi ya kikabila au dini ambayo magaidi wanaweza kuwa wanatoka.

Ushirika wa kimataifa katika kupambana na shughuli za kigaidi lazima pia uhusishe ahadi ya kijasiri kisiasa, kidiplomasia na kiuchumi ili kuwaondolea taabu wale walio katika hali ya ukandamizwaji na kuwekwa kando ambayo huwezesha mifumo ya magaidi kustawi. Uingizaji wa wale wanaofunzwa kuwa magaidi ni rahisi sana katika hali ambayo haki zinakandamizwa na ukosefu wa haki umevumiliwa kwa muda mrefu.

Bado inabidi itamkwe wazi kwamba ukosefu wa haki unaoendelea ulimwenguni hauwezi kamwe kutumika kama kisingizio kuhalalisha ugaidi; na lazima iwekwe wazi kwamba wahanga wa uvunjifu wa taratibu ambazo ugaidi unataka kuzifikia unahusisha mamilioni ya wake kwa waume ambao wako katika nafasi dhaifu kustahimili kuvunjika kwa mshikamano wa kimataifa - yaani, watu wa mataifa yanayoendelea ambao tayari wanaishi kwenye ukingo mdogo wa maisha na ambao wangeathiriwa zaidi na vurugu za kiuchumi na kisiasa ulimwenguni. Madai ya magaidi kwamba wanafanya wanayofanya kwa niaba ya maskini ni uongo wa wazi.

Usiue kwa jina la Mungu

6. Wale wanaoua kwa matendo ya kigaidi kwa kweli hukatisha tamaa ubinadamu, maisha na wakati ujao. Katika mtazamo wao, kila kitu ni cha kuchukiwa na kuharibiwa. Magaidi wanasema kuwa ukweliwanaouamini au mateso ambayo wameyapata ni makubwa mno kiasi kwamba eti wana haki hata ya kuangamiza maisha ya watu wasio na hatia. Mara nyingi, ugaidi ni matokeo ya kushabikia itikadi kali zinazotokana na imani kwamba mtazamo wa mtu fulani kuhusu ukweli lazima uaminiwe na mwingine yeyote hata kwa kulazimishwa.

Hata pale ukweli unapofikiwa unakuwa ni kwa kiasi fulani na si kwa ukamilifu, na hauwezi kulazimishwa kwa mtu yeyote. Heshima kwa dhamiri ya mtu ambamo sura ya Mungu inaakisiwa (Rej. Mwa 1:26-27), inamaanisha kuwa tunaweza tu kupendekeza ukweli kwa wengine ambao ni juu yao kuupokea. Kujaribu kulazimisha watu wengine kupokea ukweli huo kwa njia za vurugu ni kosa kubwa dhidi ya heshima ya binadamu na mwishowe kosa dhidi ya Mungu, ambaye binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wake. Kwa sababu hii, kile ambacho kinaitwa imani kali ni mtazamo ambao kabisa unapingana na imani katika Mungu. Ugaidi haunyonyi tu watu, bali unamnyonya hata Mungu: na kuishia kumfanya kama sanamu ambayo inatumiwa na mtu kwa malengo yake binafsi.

7. Hivyo, hakuna kiongozi wa dini anayeweza kutetea ugaidi, au hata kuuhubiri. Ni kufuru mtu kujitangaza kuwa ni gaidi katika jina la Mungu na kufanya vurugu kwa wengine katika jina lake. Vurugu za kigaidi ni kupinga imani katika Mungu, Muumbaji wa mwanadamu anayemjali mwanadamu huyo na kumpenda. Ni vile vile kinyume na imani katika Bwana Yesu Kristo, aliyewafundisha wafuasi wake kusali: "Utusamehe deni zetu kama nasi tunavyowasamehe wadeni wetu" (Mt 6:12). Kwa kufuata mafundisho na mfano wa Yesu, Wakristo wanaamini kuwa kuonyesha huruma ni kuuishi ukweli wa maisha yetu: tunaweza na lazima tuwe na huruma kwa sababu tumeonyeshwa huruma hiyo na Mungu amabaye ni upendo (Rej. 1Yn 4:7-12). Mungu ambaye huingia katika historia kutukomboa, na kwa matendo makuu ya Ijumaa Kuu ambayo huandaa ushindi wa Jumapili ya Pasaka, ni Mungu wa Huruma na Msamaha (Rej. Zab. 103: 3-4, 10-13). Yesu aliwaambia wale waliomuuliza kwa nini alikuwa akila na wadhambi: "Nendeni mjifunze maana ya maneno haya, ‘Napenda rehema na si sadaka’. Maana nalikuja kuwaita si watu wema bali wenye dhambi," (Mt. 9: 13). Wafuasi wa Kristo waliobatizwa katika Kifo na Ufufuko wake vinavyokomboa, lazima wawe wanawake na wanaume wenye huruma na msamaha.

Hitaji la msamaha

8. Lakini msamaha hasa una maana gani? Na kwa nini tunapaswa kusamehe? Tafakuri juu ya msamaha haiwezi kukwepa maswali haya. Nikirudi katika yale niliyoyaandika katika ujumbe wangu wa Siku ya Amani Ulimwenguni mwaka 1997 (Toa Msamaha na Upokee Amani"),ningependa kurudia tena kwamba msamaha unakaa katika mioyo ya watu kabla haujawa ukweli halisi wa kijamii. Ni kwa kiasi kile tu maadili na utamaduni wa msamaha vinapotawala ndiyo tunaweza kutumainia "siasa" za msamaha zinayoeleza katika mienendo na sheria za jamii ili kupitia kwa hizo ijikite katika tabia za binadamu.

Msamaha ni zaidi ya yote uchaguzi wa binadamu na uamuzi wa moyo kwenda kinyume na hulka ya asili ya kulipa ovu kwa ovu. Kipimo cha uamuzi namna hiyo ni upendo wa Mungu unaotuvuta kwake pamoja na kuwa na dhambi. Uamuzi huo una mfano wake kamili katika msamaha wa Kristo ambaye msalabani aliomba, "Baba, wasamehe, kwani hawajui watendalo" (Lk 23:34).

Kwa maana hiyo msamaha una chanzo na kigezo cha Kimungu. Hii haimaanishi kwamba umuhimu wake hauwezi kueleweka katika mwanga wa fikra za kibinadamu, na hasa ile hali ambayo watu hung’amua kwanza pale wanapotenda uovu. Wanaonja udhaifu wa kibinadamu, na wanataka wengine wawachukulie vizuri pamoja na makosa yao. Kwanini tusiwatendee wengine vile tunavyotaka watutendee sisi? Binadamu wote wanayo matumaini ya kuweza kuanza upya, na si kubakia daima wamefungiwa katika makosa na hatia zao.

Wote wanapenda kuinua macho na kutazama wakati ujao na kugundua uwezekano mpya wa tumaini na udhatiti.

9. Msamaha kama tendo la kibinadamu, ni juu ya jitihada zote za binafsi, lakini watu mmoja mmoja kiasili wanaishi katika jamii, wamewekwa katika mfumo wa mawasiliano ambapo kwa kupitia mahusiano baina yao hujieleza katika namna nzuri na mbaya.

Vile vile, jamii pia inahitaji sana msamaha. Familia, makundi ya watu katika jamii mabalimbali kimataifa, na jumuiya ya kimataifa yenyewe; zote zinahitaji msamaha ili kufanya upya mshikamano ambao umeharibika, ili kuvuka mipaka ya kulaumiana na kushinda kishawishi cha kubaguana bila kupata nafasi ya kujitetea.

Uwezo wa kusamehe umelala katika msingi wa dhana juu ya jamii ya siku zijazo iliyojengeka katika na haki na mshikamano.

Kinyume chake, kushindwa kusamehe hasa pale kunapochangia kuendeleza migogoro, ni gharama sana katika maendeleo ya watu. Rasilimali muhimu ambazo zingetumika kuleta maendeleo ya watu, haki na amani hutumika kwa ajili ya silaha. Fikiria mateso wanayopata watu kwa kushindwa kupatana! Amani ni muhimu kwa maendaleo.

Lakini amani ya kweli inawezekana tu kupitia msamaha

Msamaha njia kuu

10. Msamaha si pendekezo ambalo linaweza kueleweka mara moja au kukubalika kwa urahisi. Kwa njia nyingi ni ujumbe kinza au wa fumbo. Kwa kweli msamaha kuhusisha kile kinachoonekana kama hasara ya muda mfupi ili kupata faida ya muda mrefu.

Vurugu ni kinyume chake kabisa; kuhiari kama zifanyavyo kupata faida y a muda mfupi kuhusisha hasara ya kweli na ya daima.

Msamaha unaweza kuonekana kama udhaifu lakini unahitaji nguvu za kiroho na ujasiri wa kimaadili, katika kuutoa na katika kuukubali unaweza kuonekana kwa njia fulani kama kutupunguza lakini kwa kweli unatuongoza katika utu mkamilifu na uliotajirika kwa utukufu wa Muumba.

Utume wangu kwa huduma ya Injili unaniwajibisha na wakati huo huo kunitia nguvu kusisitiza juu ya umuhimu wa msamaha. Ninafanya hivyo tena leo nikitumaini kuamsha fikra makini na pevu juu ya mada hii nikitazamia kuamka tena kwa roho ya ubinadamu mioyoni mwa watu na katika uhusiano kati ya watu ulimwenguni.

11. Tukitafakari juu ya masamaha, akili zetu hugeuka kuelekea hali ya misuguano ambayo bila kikomo huendeleza zaidi undani wenye kuleta mgawanyiko na kile kinachoonekana kama mlolongo usioepukika wa mikasa ya kibinafsi na ya jumla.

Ninazungumzia hasa yale yanayotokea katika Nchi Takatifu ile sehemu iliyobarikiwa, ya mkutano wa Mungu na binadamu, mahali ambapo Yesu, Mfalme wa Amani, aliishi, alikufa na kufufuka kutoka wafu.

Hali ya sasa ya kimataifa iliyovurugika inasukuma miito zaidi kutanzua mgogoro katika ya waarabu na Waisraeli ambao umekuwa ukiendelea kwa ziadi ya miaka hamsini katika awamu tofauti za mivutano mikubwa na midogo.

Kimbilio la kujihusisha na matendo ya kigaidi na vita, linaloendelea na ambalo huongeza hali kuwa mbaya na kupunguza matumaini kwa pande zote, lazima mwishowe litoe njia kwa suluhisho muafaka. Haki na matakwa ya kila upande yanaweza kuchukuliwa kwa uzito, ulali na katika njia sawa iwapo na lini kuna utashi kuacha haki na upatanisho vitawale. Kwa mara nyingine tena nawashauri ndugu zangu wapendwa wanaoishi katika Nchi Takatifu kushughulikia zama mpya ya kuheshimiana na mapatano yenye kujenga.

Maelewano na ushirikiano baina ya dini

12. Katika juhudi zote hizi viongozi wa dini wana wajibu mkubwa.

Madhehebu mbalimbali ya Kikristo pamoja na dini kubwa za ulimwengu zinahitaji kufanya kazi pamoja ili kuondoa sababu za kijamii na kiutamaduni zinazosababisha ugaidi. Wanaweza kufanya hivi kwa kufundisha ukubwa na heshima ya nafsi ya binadamu na kwa kuhubiri maana wazi ya umoja wa familia ya kibinadamu.

Hili ni eneo maalumu la mazungumzo ya kiekumene na baina ya dini mbalimbali na ushirikiano, hii ni huduma muhimu ambayo dini yaweza kutoa kwa amani ya ulimwengu.

Kwa maana ya pekee, ninaamini kuwa viongozi wa dini za Kiyahudi Kikristo na Kiislamu lazima sasa wawe mstari wa mbele kulaani ugaidi waziwazi na kuwanyima magaidi kila aina ya uhalali uwe wa kidini au kimaadili.

13. Katika kushuhudia ukweli kwa namna ya kawaida kwamba kuawa watu wasio na hatia kwa makusudi ni kosa kubwa wakati wote, mahali popote na bila ubaguzi. viongozi wa dini ulimwenguni watasaidia kuunda maoni ya umma yanayokubalika kimaadili ambayo ni muhimu katika kujenga jamii ya kiraia ya kimataifa yenye uwezo wa kutafuta mpangilio tulivu katika haki na uhuru.

Katika kushughulikia ahadi za namna hii, viongozi dini mbalimbali hawaezi kufanya kingine isipokuwa kutafuta njia ya msamaha, ambayo kufungua njia kuelekea uelewano baina ya watu, kuheshimiana na kuaminiana. Msaada ambao dini zinaweza kutoa ili kuleta amani na kupinga ugaidi unahusisha kikamilifu kuhubiri kwake msamaha kwa wale wanaosamehe na kwa kutafuta masamaha wanajua kwamba kuna ukweli mkuu na kwamba kwa kukubali ukweli huo dini zinaweza kwenda juu zaidi ya peo zao zenyewe za kawaida.

Kuombea Amani

14. Kwa sababu hii sala kwa ajili ya kuombea amani si wazo la baadaye la kazi ya kutafuta. Ni katika asili hasa ya ujenzi wa amani ya mpangilio (taratibu), haki na uhuru. Kuombea amani ni kufungua mioyo ya binadamu ili nguvu ya Mungu yenye kufanya mambo yote upya iweze kuingia. Kwa nguvu ya neema yake iletayo uhai Mungu aweza kuumba (kutengeneza) milango ya amani mahali ambapo vikwazo na vizuizi vilikuwa vinaonekana. Anaweza kufanya mshikamano wa familia ya kibinadamu uwe imara na mkubwa pamoja na historia ya mgawanyiko na migogoro isiyoisha. Kuombea amani ni kuombea haki, kuombea utaratibu sahihi wa uhusiano ndani ya na miongoni mwa mataifa na watu.

Ni kuombea uhuru, hasa uhuru wa kidini ambao ni haki ya msingi ya binadamu na ya kiraia kwa kila mtu. Kuombea amani ni kutafuta msamaha wa Mungu na kuomba ujasiri wa kusamehe wale ambao wametukosea.

Kwa sababu zote hizi nimewaalika wawakilishi wa dini zote duniani kuja Assizi, mji wa Mt.Fransisko, tarehe 24 Januari 2002, kuombea amani. Kwa kufanya hivyo, tutaonyesha kuwa imani safi ya dini ni chemichemi isiyokauka ya kuheshimiana na utulivu miongoni mwa watu. Kwa kweli ni pingamizi dhidi ya vurugu na migogoro katika wakati huu wa kukata tamaa. Kwa kiwango kikubwa familia ya binadamu inahitaji kukumbushwa kuhusu sababu zetu zisizoshindwa za kuwa na matumaini. Kwa hakika, ni matumaini haya mbayo tunakusudia kuyatangaza kule Assizi kuomba Mungu mwenye nguvu katika maneno mazuri ya Mt. Fransisko mwenyewe - "kumfanya kila mmoja wetu awe chombo cha amani yake."

15. Hakuna amani bila haki, hakuna haki bila msamaha: hili ndilo katika ujumbe huu ninalotaka kusema kwa waamini na wasioamin vile vile kwa wanawake na wanaume wote wenye mapenzi mema ambao wanahusika na majaliwa mema ya familia ya binadamu kwa nyakati zijazo.

Hakuna amani bila haki, hakuna haki bila msahama hili ndilo ninalotaka kuwaambia wale wote wenye kuwajibika na majaliwa ya baadaye ya jamii ya binadamu ili waongozwe katika maamuzi mazito na magumu kwa mwanga wa kweli wa binadamu siku zote, wakiwa na mtazamo wa mambo mema kwa manufaa ya wote.

Hakuna amani bila haki, hakuna haki bila msahama: sitachoka kurudia onyo hili kwa wale ambao kwa sababu moja ama nyingine wanaendeleza hisia za chuki, hamu ya kulipiza kisasi au matashi ya kuharibu (uharibifu).

Katika siku hii ya Amani ulimwenguni naomba sala kuu iinuke kutoka mioyoni mwa waamini wote kwa ajili ya wahanga wa ugaidi kwa ajili ya familia zao ambazo zimekumbwa sana na msiba, kwa ajili ya watu wote ambao wanaendelea kuumizwa na kusumbuliwa na ugaidi pamoja na vita.

Ninamomba mwanga wa sala yetu usambae hata kwa wale ambao wanamkosea sana Mungu na watu kwa matendo haya yasiyo na huruma, ili wajiangalie katika mioyo yao, waone uovu wa yale wanayoyafanya, waache makusudio ya vurugu na watafute msamaha katika nyakati hizi zilizovurugika. Ninaomba familia nzima ya binadamu itafute amani ya kweli na yenye kudumu inayozalishwa kwa ndoa kati ya haki na huruma.

Kutoka Vatikano, 8 Desemba, 2001