Make your own free website on Tripod.com

Uhaba wa mapadre sio baraka - Papa

VATICAN CITY

BABA Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili amewataka Wakatoliki duniani kote kutokubali hoja kwamba uhaba wa miito ya upadre ni baraka kwa mlango wa nyuma ili kuwapa nafasi walei kujihusisha zaidi katika Kanisa.

Baba Mtakatifu aliyasema hayo hivi karibuni wakati alipokutana na mapadre wachungaji wa parokia za jimbo lake la Roma pamoja na wawakilishi wa makleri wanaoishi jijini humo.

"Wote tunajua ni kwa jinsi gani miito hii ni muhimu kwa maisha, ushuhuda na matendo ya kichungaji kwa ajili ya jumuiya zetu za Kanisa," alisema Baba Mtakatifu.

Alisema kupungua mfululizo kwa miito ya upadre na maisha ya kitawa ni "matokeo ya upungufu wa kiwango cha imani na umotomoto wa kiroho."

"Kwa hiyo, ni lazima tusiridhike na maelezo kwamba uhaba wa miito ya upadre utafidiwa na ukuaji wa utume wa walei au hata kidogo kudhani kwamba hilo limenuiwa na maongozi ya Mungu ili kupendelea ukuaji wa walei," alisema.

Alisema ni wazi kwamba huko Roma na sehemu nyingi ulimwenguni kuna vikwazo vingi vya kijamii dhidi ya kuchagua useja, upadre na maisha ya kitawa.

Watu wengi leo wanaona ugumu hata kufikiria kwamba wanaweza kufanya ahadi kwa maisha ambayo "huwazamisha kikamilifu na si kwa sehemu au kwa muda," alisema.

"Hata ni vigumu zaidi kwao kutambua kwamba wito wa namna hii si matokeo ya uchaguzi wao au kwa vipaji vyao," alisema Baba Mtakatifu.

Aliongeza "Wito huu unazaliwa kutoka kwa Mungu, kutokana na mpango wa upendo, ambao Mungu mwenyewe anao tangu milele yote kwa kila mtu binafsi."

Alisema kwa kuwa wito hutiririka kutoka kwa Mungu, haitoshi kwa jimbo kuwa na mpango mzuri wa kupata waombaji wanaotaka kuingia miito hiyo.

Aidha Baba Mtakatifu alisema, "ahadi ya kwanza na ya muhimu kufanya kwa ajili ya miito haiwezi kuwa kitu chochote zaidi ya sala."

"Kuombea miito siyo na haiwezi kuwa tunda la kuchoka, kana kwamba tumekwisha fanya kila kitu kinachowezekana na kupata matokeo hafifu, na kwa hiyo, hakuna lililobakia kufanywa isipokuwa kusali," alisema.

"Sala, kwa kweli, si kukasimu kitu fulani kwa Mungu kwamba atafanya kitu fulani kwa niaba yetu, badala yake ni kumtumainia Mungu, ‘kujiweka mikononi mwake ili atufanye wenye kumwamini na wawazi katika kufanya kazi za Mungu,’" Papa aliwaambia mapadre.

Papa pia aliwaambia mapadre hao kwamba mfano wao mwema ni muhimu ili kuwasaidia vijana kukubali wito ambao Mungu anaufikiria kwa ajili yao.

"Iwapo vijana wadogo na wakubwa watawaona mapadre wakijishughulisha na vitu vingi, wanaovurugikiwa kirahisi na kulalamika, wasiojali sala na majukumu ya kweli ya huduma yao, watawezaje kuvutiwa na maisha ya kipadre?" alihoji Baba Mtakatifu.

"Endapo wataguswa na hali ya sisi kuwa watumishi wa Kristo, ukarimu katika kulitumikia Kanisa, tulio tayari kubeba majukumu kwa ajili ya ukuaji kibinadamu na kiroho watu tuliokabidhiwa, watasukumwa kujiuliza iwapo labda hii ingekuwa ‘sehemu bora’ kwa ajili ya, chaguo bora kabisa kwa maisha yao ujana," alisema Baba Mtakatifu.

Aidha lisema seminari ya jimbo ni "mboni ya jicho la Askofu" kwa sababu kupitia seminari "Askofu huona hali ya baadaye ya Kanisa".

"Ninasema hivi kwa uzoefu niliyo nao wa kuwa Askofu kwa miaka mingi, kwanza huko Krakow, halafu hapa Roma: Krakow kwa miaka 20 na hapa Roma kwa miaka 24 sasa, " alisema.

Radio Vatican yashinda kesi

VATICAN CITY

MAHAKAMA moja mjini Roma imeitupilia mbali kesi dhidi ya maafisa watatu wa Radio Vatican, kwa kigezo kwamba redio hiyo haiko chini ya mamlaka ya serikali ya Italia.

Baadhi ya waendesha mashtaka wa Italia walikuwa wakiwatuhumu maafisa hao kuhatarisha maisha ya watu kwa kukiuka udhibiti wa mionzi inayotolewa na mitambo ya redio hiyo iliyojengwa karibu na makazi ya watu.

Katika hukumu yake, Jaji

Andrea Calabria, alisema kuwa Italia haina mamlaka yoyote juu ya maafisa hao, akirejea mkataba wa mwaka 1929 kati ya Mamlaka ya Vatican na Serikali ya Italia, mkataba ilioisimika Vatican kama taifa huru.

Miongoni mwa maafisa hao ni pamoja na Mwadhama Roberto Kardinali Tucci, aliyefanywa kardinali hivi karibuni na ambaye amesaidia kuandaa safari nyingi za ng’ambo za Baba Mtakatifu.

Wengine ni Padre Pasquale Borgomeo, Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho cha redio na Constantino Pacific ambaye ni mhandisi wa redio hiyo.

Taarifa ya Radio Vatican ilielezea kufurahishwa na matokeo ya kesi hiyo, lakini ikasisitiza kwamba ingeendelea kuchukua hatua mathubuti ili kuepusha madhara ya kiafya ambayo yanaweza kusababishwa na mitambo yake.

Mwaka jana Waziri wa Mazingira wa Italia wakati huo, Willer Bordon, alitishia kuikatia umeme Radio Vatican kama ingeshindwa kupunguza kiasi cha mionzi hiyo.

Alisema kiasi cha mionzi kilichokuwa kikitolewa na mitambo hiyo kilizidi kiwango kinachoruhusiwa kisheria nchini Italia zaidi ya mara tatu, hasa wakati wa matangazo ya jioni.

Hata hivyo uamuzi wa Waziri huyo ulipingwa na Waziri Mkuu wa wakati huo, Giuliano Amato.

Wakazi wa kitongoji cha Santa Maria di Galeria ilipo mitambo hiyo wamekuwa wakilalamikia mitambo hiyo kwamba imewasababisha watu kadhaa kuugua ugonjwa wa kansa ya damu.