Make your own free website on Tripod.com

Wanasayansi wapinga utengenezaji watu

WASHINGTON DC, Marekani

JOPO la Wanasayansi maarufu nchini Marekani limepinga mfumo wa kutengeneza viinitete vya binadamu kwa njia ya maabara, ambavyo baadaye vitakuzwa na kuwa watu.

Wanasayansi hao walifikia uamuzi huo baada ya kukutana na kutafakari mfumo huo ambao baadhi ya wanasayansi wenzao wanapenda kuutekeleza kinyume na matakawa ya watu wengi duniani.

Walisema mfumo huo utasababisha matatizo mengi kwani vitoto vya wanyama waliotengenezwa kwa njia hiyo huwa na mapungufu mbalimbali ikiwa ni pamoja na ulemavu.

Wanasayansi hao pia walisema wanyama wengi waliotengenezwa kwa kutumia mfumo huo huwa dhaifu na baadaye kufariki kutokana na kushambuliwa na magonjwa mbalimali.

Aidha walisema wale wanyama wachache wanaomudu kuishi kwa muda huandamwa na matatizo mbalimabli ya kiafya.

Walisema kwa upande wao wanaunga mkono tu mfumo huo endapo una lengo la kutumia viinitete vya binadamu kwa nia ya kufanya utafiti kwa ajili ya tiba na si kutengeneza binadamu.

Hatua hiyo ya jopo la wanasayansi maarufu wa Marekani imekuja wakati Bunge la Seneti nchini Marekani linajiandaa kujadili suala hilo ambalo tayari limeishapingwa na Baraza la Wawakilishi. Baraza la Wawakilishi pia limepinga utafiti kwa ajili ya tiba.

Rais wa Marekani, George W. Bush, anapinga vikali mfumo huo unashabikiwa na baadhi ya wanasayansi wakiongozwa na mwanasayansi Mwitaliano Dk. Severino, kwa madai kwamba unakiuka maadili ya kidini na kibinadamu.

Mfumo huo unaungwa mkono na baadhi ya watu ambao wanadhani utafiti huo utazalisha watu watakaoweza kufanya kazi nyingi kwa muda mfupi na kuleta tiba kwa baadhi ya magonjwa sugu.

Kanisa Katoliki likiongozwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili limekuwa mpinzani mkuu wa utengenezaji binadamu kwenye maabara kwa lengo lolote lile kwa sababu hatua hiyo inakiuka maadili na kufuru dhidi ya Mwenyezi Mungu.

Papa ataka Kwaresima ilete mabadiliko kwa Wakristo

VATICAN CITY,

BABA Mtakatifu, Yohane Paulo wa Pili, amewataka Wakristo kutumia kipindi cha Mfungo Mtakatifu wa Kwaresima kufanya mabadiliko katika maisha yao kwa kuacha dhambi na kumrudia Mungu.

Akiongea na mahujaji waliofurika viwanja vya Basilika ya Mtakatifu Petro huko Vatican siku ya Jumatano ya Majivu, Baba Mtakatifu aliwataka Wakristo kusikiliza maneno ya Yesu "Tubuni na kuiamini Injili."

"Katika siku hii ya ‘Jumatano ya Majivu’ tunaanza maandalizi ya Pasaka. Tunakumbuka kwamba tu wadhambi tunaohitaji uongofu. Lakini jitihada zetu hazitoshi. Lazima tutegemee neema ya Mungu," alisema.

Aliongeza, "Kwa njia ya Kwaresima tunatafakari fumbo hili la upendo wa ajabu, yaani neema ya Ukombozi isiyo na mwisho."

Alisema kuwa Mungu aliwaumba wanadamu kwa upendo na kuwakusudia kwa upendo ili washiriki katika maisha yake na huomba kutoka kwao mwitikio huru na wa huruma.

"Hii ndiyo maana ya kuwasaidia wahitaji na kufanya matendo ya huruma wakati wa Kwaresima. Ni mapaji yetu kwa Mungu tukiitikia mapaji anayotujalia sisi," alisema Baba Mtakatifu.

Aidha, alisema mapaji kama haya kwa sasa yanahitajika zaidi ya wakati mwingine wowote katika ulimwengu uliotingwa na kufikiria faida tu.

Alimwomba Bikira Maria Mama wa Mungu na Mama wa Kanisa kuwaongoza watu wote kipindi cha Kwaresima ili waweze kuifikia salama Pasaka ya utukufu wa Mwanaye.