Maumivu ya goti yazidi kumsumbua Baba Mtakatifu

l Ataka vijana wayajongee mateso ya Kristo

VATICAN CITY

BABA Mtakatifu Jumapili iliyopita aliungana na vijana kutoka Canada na Ulaya kwenye misa ya kuadhimisha Dominika ya matawi huko Vatican. hata hivyo hakuongoza misa hiyo kutokana na maumivu ya goti.

Baba Mtakatifu mwenye umri wa miaka 81 aliongoza sehemu ya kwanza ya liturujia akiwa amekaa kwenye kiti cha enzi altareni kwenye uwanja wa Mt. Petro jijini Roma.

Hata hivyo wakati wa ibada ya Ekaristi Takatifu alipiga magoti, na Kardinali Camillo Ruini, mjumbe wa Papa katika Roma, alichukua nafasi yake altareni.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kikatoliki (CNS), hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza katika miaka 23 ya uongozi wake kwamba alilazimika kukaa pembeni wakati wa misa ya Jumapili ya matawi

Vyanzo vingine vya habari vya kuaminika vilisema kuwa madaktari walijitahidi kumshawishi Baba Mtakatifu asiadhimishe misa kwa hofu kwamba hiyo ingesababisha maumivu zaidi yanayosababishwa na ugonjwa wa maungio.

Vyanzo hivyo, vilisema kuwa Papa alikubali akitumaini kwamba angepata nafuu hadi kufikia kipindi cha Juma Kuu.

Misa hiyo ya Jumapili ya Matawi ilikuwa ndiyo tukio kubwa kwa Vatican kuelekea maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni Toronto mwishoni mwa Julai.

Wajumbe 10 toka Canada waliungana na takriban wajumbe wengine 100 katika maandamano ya Jumapili ya Matawi kukumbuka kuingia kwa Yesu mjini Yerusalemu kwa shangwe wiki moja kabla ya kifo chake.

Tofauti na miaka iliyopita Papa hakushiriki kwenye maandamano ya matawi, badala yake alibariki matawi kadiri watu walivyokuwa wakipita.

Baba Mtakatifu alisikiliza kwa makini Injili iliyoimbwa kuelezea mateso ya Yesu Kristo, baadaye alitoa mahubiri yaliyojikita katika umuhimu wa msalaba kwa vijana wa Kikristo siku hizi.

Aliwashauri vijana ulimwenguni kote kumjongea Kristo na mateso yake wakitumia Injili kubadilisha jamii ya leo.

"Ninawahakikishia kwamba hamtavunjwa moyo. Hakuna mwingine, isipokuwa Kristo tu ndiye anaweza kuwapa ule upendo, amani na ule uhai wa milele mambo ambayo mioyo yenu inayatamani sana, " alisema.

Alisema kuwa alifarijiwa sana na ushiriki wa vijana katika liturujia, jambo ambalo alisema linaonyesha kuwa "hawauonei aibu msalaba." Kama wakazi wa Yerusalemu ya zamani, alisema kuwa watu siku hizi wameamua ama "kukaa na Kristo au kumkimbia au kubaki tu watazamaji wa kifo chake."

Alisema kuwa vijana wanaomfuata Kristo wamemchagua mwalimu mwenye busara na si "mfanyabiashara wa ndoto, si mwenye nguvu za ulimwengu huu na wala si mzungumzaji mwenye elimu na akili."

"Mnajua ni nani mumechagua kumfuata: Kristo mfufuka," alisema Baba Mtakatifu katika sauti ya juu kabisa.

Alisema kuwa mfano wa Kristo huwaonyesha watu jinsi ya kushuhudia ukweli na kupinga ulaghai na vitisho, kutoelewana na hofu, na hata ukatili pamoja na mateso yasiyo na huruma."

Wakanada waliohudhuria misa hiyo walikuwa ni wajumbe wa kamati ya mipango ya Siku ya Vijana Ulimwenguni ambao walifanya mazungumzo na maafisa wa Vatican kukamilisha mipango ya matukio muhimu huko Toronto Julai 23 hadi 28.

Debra Violette, aliyesoma somo la pili kwa lugha ya Kiingereza, anasimamia kituo cha mawasiliano ya simu kwenye makao makuu ya Siku ya Vijana Ulimwenguni mjini Toronto.

Aliliambia Shirika la Habari la Kikatoliki (CNS) kuwa kadiri maombi pamoja na simu zinavyozidi kumiminika "tunaweza kuhisi kukua kwa mwamko" kuelekea siku hiyo.

Maombezi katika misa hiyo yalitolewa kwa lugha saba kikiwemo Kipolandi, Kiarabu na Kiswahili. Maombi hayo yalitolewa kuombea utakatifu wa binafsi, kufanikiwa kwa uinjilishaji na kwa ajili ya upatanisho miongoni mwa Wakristo, Waislamu na Wayahudi katika nchi Takatifu.

Sebastien Lacroix, mratibu wa kituo cha hija ya msalaba cha Siku ya Vijana Ulimwenguni, alisoma ombi akiwaomba umoja wa Wakristo ili Kanisa liweze kutoa ushuhuda kwa ulimwengu.

Mwishoni mwa misa, Baba Mtakatifu aliwasalimu vijana wa Canada katika lugha za Kifaransa na Kiingereza na kuwaambia kwamba anatumaini mkutano wao nao wa kipindi cha majira ya kiangazi utaonyesha asili ya kanisa la kila mahali na wakati na kusaidia kueneza Injili.

"Endeleeni kumfuata Bwana kwa furaha na shauku. Yeye anayo maneno ya uhai wa milele. Anataka ninyi muwe nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia," alisema Baba Mtakatifu.

"Tutakutana tena Toronto kwenye Siku ya Vijana Ulimwenguni. Mungu awabariki wote," alisema.

Afisa wa Bush akiri kubadilishwa na Mama Theresa kimaisha

WASHINGTON DC, Marekani

MKURUGENZI mpya wa ofisi ya Rais wa Marekani, George W. Bush, anayeshughulikia Mambo ya Imani na Juhudi za Kijamii ofisi iliyoundwa na Bush baada ya kuwa Rais, Jim Towey, hataki kuzama katika kazi na kusahau ni kwanini amepewa nafasi ya kwanza.

Ndiyo maana kila siku huianza siku yake kwa kuhudhuria misa takatifu saa 12.30 asubuhi, kabla ya kuelekea ofisi yake akivuka mtaa mmoja kutoka Ikulu (White House).

Towey, ambaye ni Mkatoliki tangu kuzaliwa kwake alisema kuwa kuhudhuria Misa husaidia "kuweka mambo sawa."

Katika ofisi yake kuna vielelezo kadhaa vya imani yake ya kikatoliki. Kuna picha ya Mama Theresa ambayo iko karibu na ya Rais Bush, pamoja na picha ya Bibi Yetu wa Guadallupe inayoning’inia ukutani karibu na bendera ya Marekani.

Wakati alipoteuliwa kushika ofisi hiyo Februari Mosi mwaka huu kuchukua nafasi ya John DiIulio, vyombo vya habari vilimtaja kama mtu aliyewahi kuwa mshauri wa kisheria wa Mama Theresa kwa miaka 12 na pia mfanyakazi wa kujitolea kwa mwaka mmoja kwenye nyumba ya Mama Theresa ya kuhudumia watu wenye virusi vya ukimwi jijini Washington.

Katika hafla ya kukabidhiwa ofisi hiyo, Towey alimshukuru Mama Theresa kwa kumtambulisha katika "furaha hii itokanayo na kuwa rafiki wa wale wenye shida na wahitaji na kugundua heshima yao kubwa."

Akiongea na Shrika la Habari la Kikatoliki CNS) alimzungumzia Mama Thereza kama rafiki wa karibu, mwenye busara na wa kutegemewa. Alionyesha picha za Mama Theresa akiwa amemshika mmoja wa vijana wake wanne na wamisionari wa Upendo 40 wakiwa katika picha ya pamoja naye pamoja na mke wake siku ya ndoa yake.

Alisema kuwa alikutana na Mama Theresa miaka 20 iliyopita wakati akifanya kazi mjini Washington kama msajili kwenye ofisi ya Seneta Mark Hatfield, alipotembelea India kikazi na kuamua kuwa "ingekuwa vizuri" kukutana na Mama Teresa.

Mkutano huo ulimwezesha Towey kukutana na Sista Luke, aliyekuwa akiendesha nyumba ya wenye shida mjini Calcutta. Sista huyo alimpa nguo sabuni na mgonjwa wa ngozi na kumwomba amsafishe.

"Nilijivunia kusema nisingeweza kufanya hivyo" alisema Towey, lakini alikiri kwamba "hakuna hata kiungo changu kidogo sana kilichotaka kuwa pamoja na maskini."

Mkutano ule na uzoefu wa kujitolea katika nyumba za watawa hawa viliishia kubadilisha maisha yake, kuifanya upya imani yake kumwonyesha kwa mara ya kwanza kwamba "alikuwa na uwezo wa kupenda watu."

Kuwa na maskini, alisema, huvuvia kuwajibikia kwa njia moja au nyingine: "Aidha moyo wako unazidi kuwa baridi au kuwa na huruma. Huwezi kuwepo tu bila kuamua."

Alialimsifu Rais Bush kwa kusema kuwa amewahi kukutana na wanasiasa wengi sana ambao hujisikia vibaya kuwa karibu na maskini lakini yeye (Bush) si mmoja wao.

"hafanyi mambo hewani. Hajisikii amefanya zana bora mpaka amesaidia maskini," alisema Towey.

Alisema kuwa anajua Rais huipa umuhimu wa pekee ofisi yake "Sisi ni kaofisi kadogo kiuwezo," alisema, lakini akasema kuwa ana imani kwamba ofisi hiyo ni moja "kati ya zile ambazo Rais kila aamkapo huzifikiria."

Towey alisema vilevile kuna watu wanaodhani kuwa asasi za dini hazipaswi kupewa fedha za walipa kodi. Alisema kwamba "Hapa hakuna jipya" asasi za dini hupata fedha za umma ili ziwasaidie katika kuwahudumia maskini.

Aliwashauri watu wanaopinga shughuli za asasi za dini kujaribu kufikiria jamii isiyo na asasi hizo zinazotoa huduma zisizohesabika waone ilivyokosa matumaini na tunu bora za kibinadamu.

"Makundi hayahubiri juu ya dola za Marekani," alisema, akionyesha kwamba rais anaamini katika kutenganisha mambo ya kanisa na serikali.

Towey alisema wajibu mkubwa wa ofisi yake ni kuelimisha umma na hasa asasi za dini juu ya "mambo yaliyo chini ya sheria ya kutenga kanisa na serikali na yale yaliyo nje."

Kufanya kazi kubwa na katika mazingira ya kutoelewana ni sehemu kubwa ya kazi ya Towey, lakini anakuwa mwepesi kuonyesha "Sikukodiwa kuwa kiongozi wa kiroho, nipo kufuata sheria."

Anajua pia kwamba hana haja ya kuvaa imani yake kwenye mikono ya shati . "Imani inakuwa jambo la binafsi. Wakati ninapovaa beji ya ikulu na kwenda kazini."