Make your own free website on Tripod.com

Riwaya

Najisikia Kupwaya (5)

Kwa wasomaji wapya: Tausi ametumia kila njia kumshawishi na kumlainisha Fema hadi Fema ameamua kumfichulia siri iliyo moyoni mwake. Hata hivyo wakiwa shuleni wamechanganya masomo na mapenzi, siku moja wanatoka nje ya shule kwa ajili ya starehe zao. Siku uendayo uchi, ndiyo unayokumbana na mkweo. Kulikoni, fuatilia kwa makini kisa hiki cha kusisimua.

"Yaani siku zote hizo leo ndipo umepata wazo hilo la kuoana; mbona umechelewa?" Tausi akatulia.

"Si kwamba sikupendi na kwamba ninakupotezea muda na kukuharibia maisha, wazo ninalo tangu siku nyingi sana isipokuwa, nimelisema leo kwani tatizo liko wapi, mambo mazuri hayahitaji haraka," nikamlainisha.

Tausi naye akasema yake, "Mimi nilishaamua tangu zamani tu; iwe isiwe, ni hadi kifo ndipo tutatengana," Tukatazamana kila mtu kwa jicho la kuibia na tulipofumaniana, tukatishiana tabasamu za kutosha.

Kengele ya saa ya ukutani katika baa ile tuliyokuwa ililia. Nilinyanyua macho yangu na kuyatupa ilipotokea sauti ya kengele hiyo. Nikashuhudia kuwa tayari ulikuwa ni usiku wa kutosha na ninaomba radhi kwa heshima yangu, nisiutaje muda huo.

Baa hiyo ambayo pia ni nyumba ya wageni, sasa ilikuwa imezingirwa na askari polisi kadhaa waliokuwa katika msako kufuatia vitendo vya ubakaji na ukabaji vilivyofanyika eneo la jirani jioni hiyo.

Kwa mara nyingine, nilitamani dunia ipasuke ili nijifiche ndani yake.

Lakini, itawezekana vipi wakati jeuri ya kuipasua dunia sinayo na hata jambo hilo ni kitendawaili kisicho na jibu sahihi?

Kila njia niliyotaka kutumia ili kuepuka adha hiyo iliyokuwa mbele yetu, ilionekana kupwaya na kuwa mbaya kuliko nyingine. Sina shaka kuwa hata wewe unajua wazi kuwa siku uendayo uchi, ndiyo unayokutana na mkweo.

Hali hiyo ya kujikuta katika mazingira tata namna hiyo, ilinifanya mpaka sasa nikiri kuwa, nilikuwa NAJISIKIA KUPWAYA.

Kwanini hali hiyo isinikute wakati nilichanganyikiwa nisijue la kufanya? Nasema hivyo kwani licha ya kusaidia kumuokoa mwenzangu Tausi, mimi mwemyewe sikujua ningejitambulisha na kujiokoa vipi toka katika fagio hilo la chuma ambalo lilikuwa linaelekea kutuzoa kama takataka zisizofaa hata kwa mbolea au kulishia mifugo?

Kilikuwa kipindi kigumu kwetu kwani tulishindwa namna ya kujitambulisha na pia, hatukuwa na vitambulisho vyovyote. Unajua kwanini tuliamua kuviacha shuleni vitambulisho hivyo? Hivi unadhani tutembee navyo halafu likitokea "zali" halafu kikadondoka; utakuwa mgeni wa nani? Sasa tulikuwa kumbe tumeruka maji...

Tofauti na ilivyokuwa katika mawazo yangu, siku hiyo ilikuwa ni siku maalumu kwa ajili ya maonesho mbalimbalimbali ya disko. Kumbe, ni hali hiyo iliyosababisha watu wengi wengi kuingia ukumbini pale.

Hata hivyo, muda kamili wa kuanza mambo yenyewe, ulikuwa haujatimia. Sasa, nina kila sababu ya kumlaumu hata Tausi kwa kuwa kumbe yeye alijua dhahiri mambo yote ambayo huwa yanafanyika pale ukumbini katika siku kama hiyo. Nasema hivyo nikizingatia kuwa kumbe ndiyo maana, aling’ang’ania tuwe pale kwa mapumziko yetu ya siku hiyo.

Siku ya namna hiyo katika ukumbi huo, nimekuwa nikisikia kwa watu tu. Ni siku ambayo kuna kuwa na watu wengi, wa namna nyingi. Pia, kuna kuwa na mambo mengi mno.

Ndivyo ilivyokuwa hata siku hiyo yenyewe. Ingawa mambo yalikuwa hayajawaka moto, lakini hali ya unywaji, ulaji, miondoko, vilibainisha wazi kuwa, walikuwapo watu wengi.

Ni kweli maana siku hiyo kumbe walikuwapo waliowaacha wake zao wajawazito, wakasingizia kuwa wametumwa nje ya mkoa kikazi kumbe..., walikuwapo pia wasichana na wanawake waliotoroka wagonjwa wao waliolazwa hospitalini, wapo wanawake wengine ambao ni siku hiyo tu, walitoka kulia machozi ya uchungu na upweke baada ya kuonana na waume zao walio kifungoni.

Wapo pia wasichana waliokilaumu kitendo cha Mungu kuwazawadia watoto katika maisha yao. Hao, waliwafungia watoto wao wachanga katika vyumba vya nyumba zao. Kila mmoja alikwenda akiwa katika jozi.

Hata hivyo, hawakukosa wale wanaokwenda "ku-heng’i (kuning’ania) bila uangalizi wa mtu; si mvulana, si msichana. Ili mradi tu, kila mmoja alikwenda kwa hali ambayo anakusudia bila kujua kuwa, akipanda ulezi, atavuna ulezi na akapanda UKIMWI, atavuna UKIMWI.

"Mwanangu huko masomoni uliko, zingatia masomo maana ndiyo yamekupeleka. Ukiwa huko masomoni, achana na wala usihangaike kuyatafuta mambo ya dunia maana hayo, huwa ni yale yasiyo na haraka. Na pia, hayaitwi; huja yenyewe,"

Ghafla nikakumbuka barua ya mwisho ya mama iliyokuwa na sehemu yenye maneno hayo yalinigusa huku tumetangulizwa mbele na kufungwa mashati yetu wawili wawili tukitangulizwa kwenda kituo cha polisi.

Hii ilikuwa baada ya kukosa utambulisho wa kueleweka kama walivyokuwa kwa

baadhi ya wateja wenzetu katika baada na ukumbi ule.

Kila aina ya kamba niliyodhani nikiitumia kuwafunga askari hao itafanya kazi njema kama kamba ya chuma, ilionekana kufanya kazi dhaifu mithili ya kamba ya karatasi. Ikabidi twende.

Sehemu nyingine ya barua ya mama niliyoikumbuka wakati kwa mara ya kwanza sasa, ninakwena kula na kulala bure katika kituo cha polisi, ni ile iliyokuwa na maneno haya;

"...kama ni kuoa, maliza masomo yako, tutakueleza namna ya kufanya na tutakuonesha mwanamke mzuri wa kuoa na namna ya kufanya. Mwanangu, kumbuka maneno tulivyokuambia na baba yako kuwa huyo msichana unayemtaka, hafai kuingia katika ukoo na nyumba hii. Kuna mambo mengi makubwa juu yao acha.

Wimbo Niupendao

Hakuna Aliye Sawa na Mungu

Na Neema Dawson

BAADHI ya wanajamii, wamekuwa wakijipa vyeo na mamlaka makubwa hapa duniani. Lakini, Maandiko Matakatifu (Biblia), yameeleza bayana kuwa, hakuna mtu yeyote juu ya mbingu na hata duniani, aliye sawa na Mungu na anayeweza kujilinganisha naye.

Wimbo wa "Hakuna Aliye Sawa na Mungu", ulioimbwa na Kwaya ya Bikira Maria wa Konsolata, Parokia ya Kawe katika Jimbo Kuu Katoliki la Dar-Es-Salaam, unasisitiza ukweli huo.

Wimbo huo ambao ni utunzi wa Mwalimu Edwine Bazil Lukanda, ni moja kati ya nyimbo zilizorekodiwa mwaka 2000 kwenye albamu yao ya tatu yenye jina, HAKUNA ALIYESAWA NA MUNGU.

Katibu wa Kwaya hiyo, Bw. Frank Bususi Ngilangwa, amesema katika mazungumzo yake na KIONGOZI jijini Dar-Es-salaam, kuwa, nia ya kutungwa wimbo huo, ni kufikisha ujumbe kwa waamini na wote wenye mapenzi mema juu ya kuufahamu utukufu wa Mungu.

Pia, kuwafanya wanadamu wautambue uweza wa pekee wa Mungu na kutambua kuwa, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Bw. Ngilangwa alisisitiza, "...na vitu vyote vilivyopo hapa duniani hutolewa na Mungu si hivyo tu, bali hata kuwaasa wanajamii wote kutojipatia utukufu badala yake, utukufu wote wamuachie Mwenyezi Mungu aliyetupa uhai tulionao."

Wimbo huo ulitungwa mwaka 2000, ili kumuenzi Somo wa Parokia hiyo ambaye ni Mtakatifu Michael, ili waamini wanapoadhimisha Sikukuu ya Somo wao, waelewe ugumu alioupata Malaika Michael katika kutetea utukufu wa Mungu na kwamba, hakuna mwingine aliye sawa na Mungu.

Albamu hiyo ni ya tatu kurekodiwa baada ya rekodi ya kwanza iliyorekodiwa mwaka 1997 isemayo Kristo Pasaka Yetu na Waacheni Waje Kwangu iliyorekodiwa mwaka 1999.

Albamu ya Hakuna Aliye sawa na Mungu, ilirekodiwa katika studio ya Mawingi iliyopo katika Jengo la Umoja wa Vijana, jijini Dar-Es-Salaam.

Kwa mujibu wa Bw. Frank, kwaya hiyo inao waimbaji wapatao 28. Mlezi wake ni Sista Veronika, Mwenyekiti ni George M. Masanja, na Msaidizi wake ni Kalisti Joseph.

Katibu msaidizi ni Christopher Mluge, Mweka Hazina ni Wilhem Mushi na Mwalimu Mkuu wa Kwaya ni Godfrey Mpile.

Msaidizi wa Mwalimu Mkuu wa Kwaya ni Philibet Bundu.

Baadhi ya matatizo yanayoikabili kwaya hiyo ni pamoja na ukosefu wa miradi ya kuiwezesha kutunisha mfuko wake.

Wimbo wenyewe ndio huu

KIITIKIO: Ni nani kweli ni nani aliye sawa na Mungu, Ni nani kweli ni nani aliye sawa na Mungux2.

1. Yeye asaidiana na Malaika wa kule mbinguni, Rafaeli, Gabrieni na Malaika wengine mbinguni.

KIITIKIO: Ni nani kweli ni nani aliye sawa na Mungu, Ni nani kweli ni nani aliye sawa na Mungux2.

2. Michael maana yake ni nani aliyesawa na Mungu yeye ndiye aliye mkuu wa malaika walio mbinguni.

KIITIKIO: Ni nani kweli ni nani aliye sawa na Mungu, Ni nani kweli ni nani aliye sawa na Mungux2.

3. Mtakatifu Rafael pia ni Malaika Mkuu maana kubwa ya jina Rafaeli ndiye dawa ya Mungu.