Make your own free website on Tripod.com

Riwaya

Najisikia Kupwaya (3)

Kwa wasomaji wapya: Tausi ametumia kila njia kumshawishi na kumlainisha Fema hadi Fema ameamua kumfichulia siri iliyo moyoni mwake. Hata hivyo wakiwa shuleni wamechanganya masomo na mapenzi, siku moja wanatoka nje ya shule kwa ajili ya starehe zao. Siku uendayo uchi, ndiyo unayokumbana na mkweo. Kulikoni, fuatilia kwa makini kisa hiki cha kusisimua.

Na Tom Chilala

"Lakini ujue kuwa una wajibu wa kunionesha mwingine kama wewe ambaye sasa nitamueleza nililotaka kukueleza wewe."

"Hivi Tausi ana tatizo?" Nilijiuliza kimoyomoyo na kuendelea kuwaza, "Kumbe ndiyo maana anakonda! Naye anazidi kufeli masomo kama mimi, mbona "picha inazidi kuungua" sasa kama ni hivyo? Au anaumwa; mbona kasheshe sasa," nikajisemea huku nikimtazama kwa chati.

Alikuwa akichanganya konyagi na soda yake aina ya sprite.

Ghafla, nikakumbuka kosa. Nikajiona "un fit" mbele ya watu wote waliokuwa mle baani.

Nilikumbuka kuwa, miongoni mwa wateja wale wote, ni mimi na Tausi tuliokuwa wanafunzi; tena wanaosubiri kufanya mtihani wao wa mwisho hasa ukizingatia kuwa, katika mitihani ya kuvuka Kidato cha Pili, Tausi alifeli na hivyo sasa, tulikuwa darasa moja.

Nilijiona kuumbuka nafsini kwani ni dhahiri kabisa kuwa wenzetu muda huo waliutumia kujisomea na kutatua matatizo mbalimbali ya kitaaluma lakini sisi...

Ama kweli sikio la kufa, halisikii dawa.

Nilitupilia mbali wazo hilo na kuendelea na mazungumzo yetu. "Mpenzi Tau," Tausi akarudisha kinywaji chake mezani, akameza fundo lililokuwa mdomoni na kuniangalia usoni ishara ya kunisikiliza kwa makini.

"Imeniwia vigumu kukueleza. Sio kwamba ni kwa kuwa sikupendi, la hasha, bali ninatafuta njia nzuri ya kukufikishia ujumbe huu mzito na wa kusisimua. Nasema hivyo maana sijui wewe utaupokea vipi." Nikamgeukia na kumtazama usoni.

Tausi aliangalia chini huku akiwa na hamu ya kusikiliza hilo kombora linalo kuja. Nadhani alijua kuwa mambo si shwari; lolote laweza kutokea maana siku hizi...Akatikisa kichwa ishara ya kunitaka niendelee.

"Tau, siwezi kukuficha kitu; tumetoka mbali. Nikikuficha wewe, nitamwambia nani? Mimi bado nakuamini na kukuthamini sana ingawa sijui wewe mwenzangu kwa kuwa umenitangulia mjini, labda tayari kiimani umekwisha nitupa mithili ya jongoo na mti wake," nikatulia kumeza mate.

Safari hii pia nikamtazama kwa chati ili kubaini umakini wake katika mazungumzo haya.

Alikuwa ikiitikia kwa kichwa ishara wazi kwamba ninachelewa kukisema hicho, nilichotaka kukisema. Nikaendelea,"Tau, sio siri siridhiki kukuona ukiwa rafiki yangu tu, bila sote kuwa na lengo la kuishi pamoja kama mke na mume; siyo siri na katu siridhiki kabisa na ...".

Tausi alivuta pumzi na kuishusha kwa pamoja. Nikatulia kidogo na kuendelea, "... baada ya kumaliza masomo, mimi nimenuia kabisa katika hili; au wewe unaonaje maana nisijekuwa nina..." Sijui kama kweli au vipi sijui lakini tulia kwanza.

"Fema, hakika leo ndiyo nimeamini kuwa hakuna cha kunipenda ila tu, unanichezea akili na kunipotezea muda," akasema Tausi nami nikadakiza, " Kwanini unasema hivyo?"

"Yaani siku zote hizo leo ndipo umepata wazo hilo la kuoana; mbona umechelewa?" Tausi akatulia.

Itaendelea