Make your own free website on Tripod.com

Najisikia Kupwaya (7)

Kwa wasomaji wapya;

WAKO njiani kuelekea kituo cha polisi baada ya kukamatwa baani wakati wa usiku. Njiani, Fema alikuwa sambamba na Tausi huku akichanganyikiwa hususan, alipofikiria mambo yatakavyokuwa mbele ya safari. Ungana na Mtunzi Wetu TOM CHILALA, usikie Fema mwenyewe anasimulia nini.

Mara ninasikia mlio wa viganja unaoshirikia mtu kuniiita. Ninapogeza macho, yanatua na kuganda juu ya mtoto wa watu, mjamzito, Tausi.

Tausi alikuwa kasimama mbele ya ile baa ijulikanayo kama EYATERA mjini hapo. Alikuwa kavalia sare ile ya watumishi wa baa. "Aaah! Hivi Tausi wangu amekuwa baa medi?!" Nikamaka na kubaki mdomo wazi.

Ingawa hadi sasa ninakiri kuwa nilifanya kosa la kumkubali shetani kwa jaribio kidogo lakini ninachokuambia, ni kile nilichokisema nikijipa nguvu. Sioni sababu ya kukuficha eti nijikoshe kwako.

"Pesa ni pesa. Hata kama umezipata kwa kumuuza mkeo, au mboga za majani. Zote ni pesa tu. Hata kama ni zile ulizozipata kwa umalaya au kwa kuuza Biblia, bado pesa ni pesa, mradi tu, zitakusaidia maana SHIDA HAINA ADABU."

Ndivyo nilivyojifariji kwa maneno baada ya kumuona eti TAUSI sasa ni baamedi; watu ambao katu maishani kwangu, sikupenda kuwa karibu nao lakini sasa, potelea mbali, si ni Tausi wangu bwana, nifanye nini; nimkane, haiwezekani labda yeye.

Yalikuwa sasa yamebakia takribani majuma mawili ili utimie muda tuliokusudia kutekeleza mipango yetu.

Hata hivyo, ukweli kuwa siku ya kifo cha nyani miti yote huteleza, ukajidhihilisha. Ninasema hivyo, maana hata mimi nilipigwa butwaa nilipoambiwa na Tausi mwenyewe kuwa, kazini kwao (katika baa), kumetokea upotevu wa pesa.

Sasa, wafanyakazi wote walikuwa wamefukuzwa na kunyimwa mishahara yao. Si hata wewe unajua baamedi wanavyonyanyswa utafikiri hata waajiri wao hawaoni umuhimu wa kuwa nao?

Sasa, tabu ikaongezeka maradufu. Madeni yakawa madeni. Kila kona yenye duka, tulikuwa tukidaiwa kwa ahadi ya kulipa mwisho wa mwezi. Sasa itakwaje!

Hata hivyo, akiba haiozi. Japo ni kidogo, lakini pesa ile kidogo tuliyokuwa tukibangaiza na kudunduliza, ikatumika kidogo kupunguza ukali. Tena tunashukuru kuwa, tulikuwa watu wazima tunaojua maana ya kuvumilia.

Kwa hali yote hiyo, kumbuka kuwa tumbo la Tausi linazdi kuongezeka ukubwa. Tukaamua kusafiri kiujanja ujanja huku tukiwakwepa waangalizi wa treni hadi tukamudu kufika kijiji tulichokitaka. Tena sikitaji ingawa ni maeneo ya kule nyumbani. Naogopa maana wale wazee wa pale wataanza kumtania baba na kumkumbusha hasira.

Nimkamtanguliza Tausi pale kijijini kwetu. Yeye akaenda nyumbani kwao na mimi nikaenda kupumzika kwa rafiki yangu Victor, kijiji jirani kabla ya kukifikia chetu. Njia hii ilikuwa na lengo la kuwapoteza boya wazazi wangu, ili wasijue kinachoendelea baina yangu na Tausi.

Baada ya kuridhika na muda wa mapumziko, nami sasa niliingia pale nyumbani huku nimejitwika mizigo yangu. "Habari za masomo?" Baba akaniuliza. Nami nikajibu, "Nzuri tu." " Vipi mitihani?" Baba akaendelea na maswali ambayo sio siri, yalikuwa yanazidi kunichanganya na kuniongezea kiwewe.

"Aaa! Yalikuwa ya hivyo hivyo tu; ya wastani." Nikajibu huku nikihofu kuwa huenda maswali hayo ni mitego ya baba na kwamba, huenda tayari ana taarifa zote juu ya kufukuzwa kwetu shule, kufungwa na sasa hata hiyo mimba ya Tausi anajua asili yake ni nini.

"Nilipata barua yako ya kutaka uchumba kwa huyu mtoto wa huyu Mzeee...Aaa. Nani huyuuu...Mzee Mwangulupe." Baba alianza mazungumzo hayo baada ya chakula cha jioni cha siku hiyo.

Kisha akaendelea, "Mwanangu, ukoo ule sio ukoo wa kuoa. Ni ukoo mbaya wenye mchezo wa usiku. Ukoo huo umeenea wachawi; hivi unaona ulivyo; nani ameendelea pale, watu wote wanaukimbia, wewe unataka kujipeleka pale! Hutaki ukoo wako ukue?"

" Narudia tena; kama kweli wewe ni mwanangu wa kuzaa, msijaribu kufanya uhusiano wowote na binti wa mji ule."

Msimamo wangu na wa baba, ikahitilafiana. Wakati yeye hataki kwa sababu anazozitaja, mimi naona kwa Tausi, nimefika. Kwanini nimsaliti na kumkana mtoto wa watu.

Basi, kutokana na hali hiyo ya kuwekewa kauzibe, nililazimika kuendesha urafiki wa kificho baina yangu na Tausi. Wakati huo, kila mmoja wetu alikuwa akifanya kila awezalo, kuona malengo yetu yanafanikiwa kufikia kilele cha matazamio.

Sio siri, kadiri siku zilivyokwenda, ndivyo penzi letu lilivyozidi kunoga. Hata hivyo, nilianza kushangaa na kujiuliza kuwa, iweje kadiri siku zinavyopita, ndivyo uchangamfu wa Tausi ulizidi kupungua kwangu. Sasa, Tausi alizidi kuonekana kupungua kiafya na kujawa na mawazo mengi.

Sio mimi peke yangu niliyesumbuliwa na hali hiyo ya Tausi, bali pia ndugu, jamaa na marafiki wote waliojua namna uhusiano wetu unavyoendeshwa kwa siri. Kila mmoja alikuwa na wasiwasi wa sirisiri moyoni mwake. Hata hivyo, wengine hawakufaulu kujizuia.

Hata baada ya kupewa majibu na Tausi ambayo ni dhahiri hawakuridhika nayo, wengine waliniendea na kuniuliza kulikoni tena.

Sikuwa na cha kusema badala ya kuwahakikishia kuwa sikujua kitu; nilikuwa kwenye usiku wa giza kama ilivyokuwa kwao.

Ni dhahiri kuwa, sikuwahi kumuuliza undani wa hali hiyo kwani nilijidhania kuwa ninajua sababu kumbe...(jaza jibu).

Watu walizidi kunichimbachimba. Nami, ehee; uzalendo ukanishinda. Nikasema hapa, huenda tayari wamejua wanalojua. Heri nami nichimbechimbe.

"Tausi! Tausi! Hivi hasa una lipi linalokusibu nawe unanitenga na kutokunishirikisha? Hivi unadhani kama ukipata tatizo, mshukiwa wa kwanza atakuwa nani?"

"Tausi! Ujue kuwa mimi sio mtoto mdogo, na wala si mgeni kwako. Ninakufahamu wazi; hiyo sio hali yako ya kawaida. Tafadhali mpenzi nieleze tatizo lako, nishirikishe kwa mazuri na mabaya," nikabembeleza zaidi.

Ghafla, tausi alianza kutiririsha machozi. Hali hiyo, ikanionesha kuwa huenda "nimechemsha’ katika mazungumzo na maswali yangu. " Yaani mimi, sijui heri nife tu," akasema huku machozi yakimtoka. Alikuwa kainamisha kichwa. Akasema, "najuta kupenda, najuta kuzaliwa".

Maneno hayo yakanifanya labda nijisikie kujiandaa "kurudisha kadi" yaani, kuvunja urafiki baina yangu na Tausi. Ilibidi nifikie hatua hiyo kwa kuwa sikujua kauli zake zilikuwa zinalenga kuhitimishwa na uamuzi gani.

Sio siri, kama kweli ingekuwa kuwa uamuzi wa Tausi ulielekea huko nilikodhani, ningekoma ubishi maana kwangu mimi, ndio kwanza nilikuwa nimekolea sawasawa.

"Tausi: inaonekana dunia zetu zimewahi mno kutengana. Kwa muda huu tu, hata busara za kawaida zinakataa. Yani Tausi leo hii unadiriki kunificha? Mbona dunia zetu zimewahi kurudishiana kadi mithili ya makahaba wa mjini na "matandiko ya kukodi?" nikatamka maneno ambayo sio siri, yalimwingia sawia akilini; yakamtoa nyoka shimoni.

"FEMA; imeniwia kazi ngumu kukueleza. Sio kwamba ni kwa kuwa sikupendi, bali ninatafuta namna nzuri ya kukufikishia ujumbe huu ambao pasi na shaka, unaweza kukusikitisha ama pengine hata kukuudhi," Tausi akatulia kidogo kumeza mate na kisha, akaendelea.

"...ama kweli dunia hii sijui ni nini na ni nani kayaleta haya. Uzushi umekuwa uzushi. Watu wamekuwa wazushi utafikiri wanaharishia midomoni. Inasikitisha sana uzushi eti siku hizi umekuwa kama fasheni. Ukiugua ukoma, wanazusha eti una UKIMWI. Usipotaka maisha ya anasa, wanasema wewe ni bahiri. Mkipendana na mkeo, wanasema umepewa dawa."

"...Ukiwa mzee sana, wanazusha eti wewe ni mchawi; mtu akifa kijijini, wanasema umemroga wewe. Ukiwa na pesa, wanasema wewe ni kibaka na mwizi sugu. Ama kweli, dunia inaumbua." Tausi akaanza tena kulia.

Nilizidi kutumia kila njia niwezayo kumshawishi ili aachane na mambo ya kike; mambo ya kulialia.

"Fema, zimepita siku nyingi mama akinionya na kunikanya juu ya mambo yale anayoambiwa na majirani. Mpenzi Fema, siwezi kukuficha mambo ambayo ninasikia yakisemwa huku nikijua bayana kuwa ni uzushi," Tausi akatulia kidogo kumeza mate.

" Eti ninyi wachawi; tena eti kwenu kuna asili ya magonjwa mabaya.

Watu wananikemea na kunisuta eti umenfanyia dawa za kwenu ndio maana wanazuia uhusiano wetu lakini mimi ninang’ng’ania tu; sisikii," akatulia na kuniangalia usoni ili kubaini umakini wangu.

"...la ajabu, wanasema kwamba baba yako ndiye mwenyekiti wa miliki yote ya wachawi katika eneo hili. Itaendela Toleo lijalo