Najisikia Kupwaya (6)

Kwa wasomaji wapya;

WAKO njiani kuelekea kituo cha polisi baada ya kukamatwa baani wakati wa usiku. Njiani, Fema alikuwa sambamba na Tausi huku akichanganyikiwa hususan, alipofikiria mambo yatakavyokuwa mbele ya safari. Ungana na Mtunzi Wetu TOM CHILALA, usikie Fema mwenyewe anasimulia nini.

Kila aina ya "kamba" niliyodhani nikiitumia kuwafunga askari hao itafanya kazi njema kama kamba ya chuma, ilionekana kufanya kazi dhaifu mithili ya kamba ya karatasi nailoni. Polisi hao hawakunisikia wala kuelewa ninasema nini, Ikabidi twende nikalale na kula bure.

Nikakumbuka tena maneno ya mama katika moja ya barua zake, "...kama ni kuoa, maliza masomo yako, tutakueleza namna ya kufanya na tutakuonesha mwanamke mzuri wa kuoa na namna ya kufanya.

Mwanangu, kumbuka maneno tulivyokuambia na baba yako kuwa huyo msichana unayemtaka, hafai kuingia katika ukoo na nyumba hii. Kuna mambo mengi makubwa juu yao acha."

Nikashindwa kuelewa kulikoni wazazi wangu wampinge namna hiyo hali wanajua kuwa mimi ni mvulana mwenye kustahili demokrasia ya mapenzi, sikujua Tausi ana dosari gani, sikujua na nilikuwa na hamu ya kujua sababu.

Hali hiyo, ilinifanya moto wa mapenzi yangu kwa Tausi, uzidi kuwaka mithili ya uliomwagiwa petroli. Wanasema asiyesikia la mkuu, huvunjika mguu, sasa sijui.

Nilianza kufikiria nilivyokuwa tegemeo na tumaini muhimu la familia yetu. Mtoto pekee wa kiume. Ndugu, jamaa na marafiki wote wenye mapenzi mema na ukoo wetu, walikuwa wakikesha; kila mtu kwa nafasi yake ili waniombee baraka na mafanikio tele maishani mwangu.

"Sasa bado mwezi mmoja na nusu ili tufanye mitihani yetu ya mwisho; hivi mambo yatakuwaje! Hapa si kupanda ubuyu nikitegemea kuvuna ngano?" Nilijisemea huku tukiwa njiani kuelekea shuleni baada ya kumaliza kifungo chetu siku hiyo.

Hivi unafikiri tungenusurika vipi kwenda gerezani wakati tuliposombwa kama wazembe na wazururaji wasio na utambulisho wowote. Sasa kama unakubali hilo unadhani ingekuwa muujiza gani tunusurike mbele ya hakimu yule?

Hata mimi nilishangaa mno maana tofauti na nilivyozoea kwa wengine, mwanafunzi yeyote aliyepatwa na matatizo yasiyohusu maamuzi mabaya ya shule, wanafunzi wenzake walimpa pole na kumsikitikia kwa muda mfupi tu; wakaenda zao kujisomea.

"Sasa, iweje leo niwe na umuhimu wa kujaza wanafunzi wengi namna hii mithili ya watu wanaomsubiri mgeni rasmi kwa ajili ya kuanza mkutano?" Fema nilijiuliza kimoyomoyo huku wanafunzi mbalimbali; wa kike na wa kiume wakizidi kuja kunitemelea bwenini.

Ilibidi nishituke maana hakuna aliyekuwa na uso ulioonesha shauku ya mimi kuja pale shuleni. Wengi waliniuliza imekuwaje nimeruhusiwa kurudi tena shuleni kuendelea na masomo.

Hawakuwa wakijua kuwa, maswali yao yalikuwa taarifa ngeni ambayo sikuwa ninaijua.

Hata hivyo, nikiwa sijawapa jibu walilotegemea wala mimi kujua kiundani maana ya maswali yao. Ghafla, Mwalimu wa Malezi na Nidhamu, anaingia pale bwenini kwetu. Akanichukua hadi ofisini kwa Mkuu wa Shule.

Sikujua habari za kurudi kwetu ziliwafikia vipi walimu hao hadi waitane na kutukutanisha ofisini kwa Mkuu wa Shule.

"Hatukuwa na namna ya kuwasaidia kwani tulipopata taarifa zenu kiusahihi, mlikuwa mmekwisha hukumiwa na mmetumikia kifungo cha siku nne.... Hata hivyo, kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za shule, uongozi wa shule unasikitika kukuambia kuwa, umeshindwa kukusaidia zaidi kwa kuwa kwa kawaida, mwanafunzi aliyefungwa au kukaa nje ya shule bila taarifa maalumu na ruhusa ya shule, anakuwa amejifukuza shule mwenyewe.

Hivyo, shule inasikitika kukuambia kuwa, tunapozungumza sasa, wewe si mwanajumuiya wa shule hii.

Hii haikuwa njia yako ya maisha. Hata hivyo, usikate tamaa.

Unaweza kujaribu sehemu nyingine na mambo yakaenda vizuri zaidi kuliko hapa. La msingi tu, usiogope wala kukata tamaa katika maisha," akamaliza Mkuu wa Shule kutuambia kila mmoja alivyoitwa kwa zamu yake.

Nilipotoka nje ya ofisi, nilimkuta Tausi akiwa ameinamisha kichwa chake na kukiegemeza mtini. Machozi yalikuwa yakimtoka asijue afanye nini na wapi pawe kimbilio lake.

Ama kweli asiyesikia la mkuu, huvunjika guu. Nilianza kukumbuka mambo mengi.

"Nitaingiaje nyumbani kwetu Fema, nitasemaje maskini mbona baba ataniua! Fema ni wewe uliyesababisha sasa unaona? Hivi raha tulizokuwa tunaponda zilikuwa zinatuelekeza huku! Ndizo zinanigeuka na kunirudi namna hii, si heri nife tu. Ema sio siri NAJISIKIA KUPWAYA hapa duniani.

Fikiria Fema tumefukuzwa shule, hali yangu unaiona si muda mrefu tu, nitakuwa mjamzito asiyejiweza; hivi Fema mimi nitafanyaje; si afadhali...".

"Hee! Hivi Tausi ana maana gani. Ina maana anataka ajiue! Hivi akifa na hiyo mimba nitamzika wapi?!" Nikamaka kimoyomoyo.

Hizo, zilizkuwa sekunde chache tu, tangu nizinduke toka usingizi ule ambao katu sikuufurahia. Usingizi ambao kila lepe lake, lilinionesha ndoto za anga nyekundu iliyojaa damu, majinamizi na vitu vya kutisha ikiwamo dunia kujigeuzageuza. Ndivyo vilivyotawala usingizi wote. Ama kweli kuzimia ni nusu kabisa ya kifo.

Nikakumbuka namna tulivyorudi kwa pamoja mimi na Tausi hadi kwa Mkuu wa Shule kwenda kubembeleza ili atusaidie walau kwa huruma na busara zake za kawaida na za kibinadamu, lakini kauli ile ya msimamo kuwa, "UAMUZI HUU NI WA KISHERIA NA WALA HAUBADILISHWI," ikanipa tena usingizi ule mbaya.

Sijui ni baada ya siku ngapi lakini, nilifumbua macho na kujikuta peke yangu katika kitanda kimoja wapo ndani ya wadi ya wagonjwa wenye matatizo ya akili katika hospitali ya wilaya.

Hata hivyo, baada ya majuma matatu, nikaruhusiwa kutoka. Mambo yakaanza kuonekana dhahiri yalivyo magumu; namna ugumu wa maisha ulivyokuwa bado unajiandaa kunisonga zaidi.

"Nitakula wapi? Nitalala wapi? Tausi yuko wapi na mimba yangu?" yote hayo najiuliza pasi kutarajia njiani; tena kwa sauti ninayodhani kuwa ni ya kunitosha mimi mwenyewe kusikia kumbe, ni tangazo lisilo rasmi. Watu walikuwa wakinitazama kwa mshangao wa namna yake.

Sasa nilikuwa ni nusu ya mwendawazimu anayekatiza zake; akienda aendako na wala sijatambui. Ubao ulikuwa umenibana ipasavyo. Ninakatiza na kukatiza mitaa ili mradi tu, muda uende; giza liingie nitafute mtaro nitakaolala ili kesho nitafute akili mpya.

Itaendelea Toleo lijalo