Riwaya

Umeajiriwa na nani ?

Na Christopher Gamaina

"HAPANA; hali hii sio ya kawaida! Lazima nipate ufumbuzi wa masaibu haya, kulala njaa kila mara na hata kufikia kuazima nguo na kila leo nashinda nafanya kazi! Lazima kuna mtu ananichezea si bure."

Charo alisikika akilalamika peke yake huku amejikalia peke yake pale ofisini.

Aliiweka ile kalamu yake aina ya BIC juu ya meza kisha, akainamisha kichwa pale pale alipoketi akiwa amegubikwa mawazo. Muda si muda, alianza kudondosha chozi moja baada ya jingine.

Kadiri muda ulivyozidi kusonga mbele, ndivyo fahamu zilizidi kumtoka. Charo Rasheed hakuweza kuipokea sauti ya bosi wake iliyoita na kumtaka azipeleke barua kwa kuwa muda aliopewa kuziandika ulishagonga ukuta.

Ninajitahidi kutafuta lugha rahisi ya kueleza namna kijana huyu alivyokabiliwa na wakati mgumu pale ofisini lakini, nahisi na japo sina ushahidi, pengine Charo alikuwa ameadhirika kwa kipindi kirefu.

Bosi wake alizidi kuita na sasa ilikuwa mara ya tatu mfululizo. Bila mafanikio. Ndipo alipoamua kunyanyuka na kuufungua mlango wa ofisi yake hali bado akiwa mwenye hasira.

Alizivuta hatua mbili ndefu zilizomfikisha mlangoni pa ofisi ya sekretari wake.

Alisukuma mlango kwa kishindo cha nguvu lakini, hakuyaamini macho yake kwa kitendo alichokishuhudia katika ofisi ile ya Charo.

Achilia mbali zile barua alizokuwa amemwagiza sekretari huyo kuziandika ambazo nazo hazikuwa zimeandikwa, Charo alikuwa amejiachia sakafuni kwa mlalo wa kifudifudi huku machozi yakiendelea kumbubujika mithili ya maji ya bomba.

Huu ulikuwa kama muujiza mkubwa na wa awali kabisa kuonekana ofisini pale.

Akiwa pale kwenye sakafu ya ofisini kwake, Charo alionekana mithili ya mgonjwa aliyekuwa mahututi.

Huku amepigwa na butwaa, sekretari huyo akazua kitimbi kingine kilichoelekea kusababisha hasara kwa baadhi ya vifaa pale ofisini .

Charo alianza kujikokota na tumbo mithili ya nyoka huku akiitupa miguu hali iliyopelekea kuviangusha viti na mafaili ya ofisi.

"We Charo inuka tafadhali, hivi kulikoni!?" Bosi akauliza huku akijaribu kumnyanyua kwa kumshikilia Charo mikono.

Ni takribani miaka sita sasa tangu Charo afanye kazi ya ukarani katika ofisi ya Mkurugenzi wa Kampuni binafsi, inayoshughulika na utengenezaji pamoja na uuzaji fanicha mjini Tarime.

Ni mchapa kazi mzuri tu na bosi wake amekuwa akimwongezea mshahara mara kwa mara kutokana na bidii yake kazini.

Anaishi katika nyumba ya kupanga mjini hapo pamoja na mke wake aitwaye, Hilda. Walijaliwa kuwazaa watoto wawili wote wa kike.

Charo anayo ratiba aliyokwishaipanga kuifuata kila anaporejea kutoka kazini.

Kabla ya kuingia nyumbani kwake, huhakikisha anapita baani ili kujituliza kwa vinywaji kadha wa kadha. Pia, kijana huyu anayo tabia nyingine anayoipenda zaidi na zaidi, kuhakikisha kila siku anampata mwanamke wa kuisitiri haja yake ya kimwili hivi ndivyo anavyoshi.

Siyo kwamba ninamteta kwa kuwa hayupo, bali hata yeye ukimuuliza ni kwanini amekumbwa na shetani wa namna hiyo, hana jibu bali anakumbwa na kigugumizi cha ghafla kisichoisha hadi mtakapo badili mazungumzo.

Kisha, Charo huelekea nyumbani kwake na mara nyingi, huingia saa za usiku usiku.

Huwa amegida sana maji na anapofika tu, kitu cha kwanza hudai apewe chakula ambacho hakuacha pesa ya kukinunua na inapotokea kukikosa, ndipo zogo kubwa huzuka ndani dhidi ya mkewe.

Kama unapita njiani na kwa namna unavyomjua Charo kwa umbo na tabia ya nje, huwezi kuamini kuwa ndiye huyo anayofanya na kusikika akiyasema hayo.

Anayotamka ni matusi matupu.; tena matusi makubwa; na kwa sauti kubwa kubwa inayowafanya majirani zake washindwe kuzifaidi ndoto katikati ya usingizi wao. Wakati fulani, humshushia kipigo Hilda na kumfanya ashindwe hata kutembea siku iliyofuata.

Siku zote Charo ni mgumu na mkali sana kila anapoombwa pesa za matumizi na mkewe. Ni hodari na mwepesi wa kuwakatia maelfu ya shilingi wanawake wa nje na ndivyo ilivyo ada kuwa mhunzi hulia kwenye gae.

Hali hiyo imeifanya familia yake kwa jumla, idhoofike siku hata siku.

Kila anapoambiwa na mkewe kuacha tabia hiyo mbaya, huwa mkali kuliko pilipili na kugeuka mkali mithili ya nyati aliyepigwa busu la mkuki au mshale wenye sumu.

"Maisha tunayoishi kwa kadiri ninavyoyaona mume wangu, si mazuri. Hatuyamudu na tayari yamekwisha tushinda; bora tu, uachane na tabia ya kutojali familia yako.

" Hilda alilalamika siku moja na huku akijiandaa kuenda kliniki.

"Nimegundua unachotafuta. Unajua wanawake mkikaa bila kupigwa, sijui mnajisikiaje. Na kama ni hilo ndilo shida yako, mimi niko tayari! Nimeishakuambia hadi leo nina miezi mitano sijapokea mshahara.

Sasa hayo mawazo yako kwamba siijali familia kama; unaona hivyo, yafanye wewe maana nilishakuambia kuwa habari za watoto kununuliwa nguo, ni hadi hapo nitakapolipwa mshahara.

Nadhani huo usiwe wimbo na sitaki kusikia tena ukinipigia kelele kwa hilo!" Siku hiyo Charo akafoka. Na hiyo ndiyo ilikuwa ada kila alipoambiwa jambo la namna hiyo.

Pamoja na ukweli kwamba Charo hupata pesa nyingi kutokana na kazi yake ya ukarani, familia yake hufikia hatua ya kulala njaa baada ya kujikuta ametumia pesa zote katika anasa.

Kwa wasiomjua anavyotanua akiwa nje, wakati fulani, huwa wakijiuliza na kutafakari sana ni vipi pesa za mshahara wake hutumika na kuisha kwa muda mfupi kuliko ilivyo kawaida.

Kibaya zaidi, licha ya yeye kujua pesa za mshahara wake zinaingia na kutoka vipi kwake, Charo mwenyewe amediriki kusema ana mkosi na akajaribu kuzunguka kwa waganga wa miti shamba ili kufahamu sababu inayopelekea hali hiyo lakini wapi, hakufanikiwa.

Atafanikiwa vipi wakati hao anaowafuata wanamdanganya huku akiwaachia maelfu ya pesa ambazo zingetatua baadhi ya matatizo nyumbani eti sasa ndio wanaoziponda zinazobaki eti wamuondolee mkosi?

Kwa kadiri siku zilivyozidi kusonga mbele, ndivyo hali ilivyozidi kumuwia vigumu mithili ya jiwe. Kila alipopata pesa, alizitumia kwa ulevi na kuwabadilisha wanawake ambao walimchuna kisawa sawa mithili ya nguo.

Kilichozidi kumsumbua siku baada ya siku, ni pale anapokoswa raha na kujihisi mwenye huzuni, anapo maliza na kila alichodhani anacho.

Lakini, mara nyingi alikuwa akijikisoa na hata kujuta akiahidi kutorudia mara mambo yatakapoenda vizuri.

Hizo zilikuwa ni njozi za mchana kwa kijana Charo. Ninasema hivyo kwani aliyasahau yote na kukimbilia kwenye majumba ya starehe pamoja na wale aliowaita watoto wabichi mara tu, alipozitia mfukoni.

Ilikuwa kawaida ya Charo kuanza kujilaumu. Ndipo anaposikika sasa akisema, "Oh! sasa nimegundua ninainyanyasa familia yangu.

Sasa nitahakikisha ninaihudumia vizuri mara nitakapopokea mshahara.

Mara anasikika, Oh! Nimegundua ninaweza kuyahatarisha maisha yangu na hata mke wangu endapo nitaendelea na tabia hii ya kuwabadili wanawake machangudoa. Tena licha ya kosa hilo, eti sikumbuki walau jaribio la kubahatisha usalama kwa kutumia kinga yoyote ile. Naapa sirudii tena tabia hii mbaya!

Hali hiyo ilizidi kuiyumbisha akili ya Charo kwa kipindi kirefu.

Alisikika mara kwa mara akijihoji mbele ya watu wakati hana pesa akisema kuwa ni vipi amekuwa dhaifu kuidhibiti na kuiacha kabisa.